Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!

Icon

Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia

Mlango wa Ishirini: Mapinduzi Ndani na Nje

Kwa hivyo, kuanzisha vita vya uonevu vya kuishambuliya nchi nyingine si jarima la kimataifa tu, bali ni upeo wa jarima la kimataifa ambalo linatafautiyana na jarima nyinginezo za vita kwa vile katika vita vya uonevu hutendwa jumla ya matendo maovu yote ya jarima. —Robert H. Jackson, Muendesha mashtaka wa Kimarekani katika kesi za Nuremberg

Profesa Ali A. Mazrui ametowa mifano miwili mikubwa ya mapatano duniani. Mfano wa kwanza ni mapatano baina ya Waingereza na Wamarekani ambao waliwahi kuwa maadui wa muda mrefu na hivi sasa ni marafiki wakubwa duniani. Mfano wake wa pili ni mapatano baina ya Japan na Marekani baada ya kuwa maadui na hivi sasa kuwa marafiki wakubwa duniani.

Profesa Mazrui ameandika:

Kusameheyana baina ya Waarabu na Waafrika huenda kukawa baina ya mfumo wa Kimarekani-Kiingereza (wa mwendo mdogo lakini imara) na wa Kimarekani-Kijapani (wa haraka lakini wa kijuujuu)…Mapatano baina ya Waarabu na Waafrika yanakusanya si kumbukumbu za mapinduzi ya Zanzibar peke yake, bali kimsingi zaidi, kumbukumbu za kuhusika kwa Waarabu na biashara ya utumwa Afrika.1

Tumeshaona kuwa ni mara nyingi sana suala la mapinduzi ya Zanzibar limekuwa likihusishwa na “utumwa wa Waarabu.” Chimbuko la itikadi hii limetokana na kutojulikana kwa chimbuko halisi la mapinduzi yenyewe. Tatizo kubwa lilikuwa ni kuyatizama mapinduzi ya Zanzibar kuwa ilibidi yatokee kwa sababu ya unaosemekana kuwa ulikuwa ni utawala wa kimabavu wa Wazanzibari wenye asili ya Kiarabu. Mavamizi ya Zanzibar hayakuwa ni kitu ambacho lazima ilibidi kitokee. Ulikuwa ni mpango maalumu wa nchi moja kuivamiya ya pili na kuificha siri nzito ambayo umekijenga kimya kilichoikosesha usingizi Zanzibar kwa muda wa miaka arubaini na sita.

Kwa miaka zaidi ya khamsini Wazanzibari wamekuwa wakiendeshwa na upotoshaji wa kihistoria ambao umechangiya kwa njia kubwa katika mapambano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyowaondoleya utulivu wa kujipa maendeleo na neema kubwa zaidi wanazostahiki kuwa nazo. Vitabu vingi kuhusu historia ya Zanzibar havikuandikwa na Wazanzibari na vimejaa fitina za upotoshaji zenye kuwagawa Wazanzibari katika misingi ya Uafrika na Uwarabu na khasa kushadidiya uovu wa Waarabu bila ya kudaiwa ushahidi wa tuhuma zao.

Haitoshi kuitambuwa hakika ya yale yaliyoisibu Zanzibar katika mapinduzi na muungano na Tanganyika bila ya Wazanzibari wenyewe kukiri kuwa mifarakano yao wenyewe kwa wenyewe ndiyo iliyowapa wengine mwanya wa kuwaingiliya na kuwaondoleya masikilizano na neema za kuungana. Kurekebishika kwa mapinduzi na muungano kutatokana na mapinduzi ya kifikra na muungano wa Wazanzibari ndani ya Zanzibar kwanza. Hakuna nchi, au kiongozi, au taasisi ambazo zitaweza kuwapatanisha Wazanzibari kabla ya wenyewe kulivuwa jumba la buibui liloendeleya kuwapotosha na kuwanyima njiya ya kutokeya. Watu wenye kupatana ni wale wenye nia ya kupatana na wakawalazimisha viongozi wao kwenda na uwamuzi wao. Penye jahazi lenye kuzama watu huwa hawamtafuti nahodha mweusi au nahodha mweupe na ubaguzi huchukuwa likizo la moja kwa moja.

Kwa mujibu wa matokeyo ya utafiti huu, Zanzibar haina budi kwanza kuamuwa kujikombowa kutokana na mzimu wa kihistoria uloziiba nyoyo na akili za Wazanzibari na za Watanganyika kwanza na kuendeleya kuiandika na kuisomesha historia ambayo haikupotoshwa na kuitiya jamii nzima ndani ya upofu. Mtoto wa tembo anapolelewa kutokeya mdogo huwa anafungwa myororo wa mguu kunako chuma basi hata anapolifikiya tambo la kuwa tembo mkubwa bado huendelea kuamini kuwa hana nguvu za kuuvunja myororo wa chuma ambacho hakina nguvu za kumzuwiya ikiwa ataamuwa kuukata. Ukombozi wa Wazanzibari wa kwanza ni ukombozi wa nguvu za akili ambazo zinafikiri nje ya gofu/sanduku la kihistoria.

La pili ambalo haliwezi kupatikana bila ya ukombozi wa kifikra ni uchapaji kazi kwa kuwasomesha watu wake na uongozi mpya wa mustakbal wenye kuwatiya tamaa kubwa ya kimaisha kizazi kipya, na kuchachamaa kujirejesheya utambulisho wake badala ya kupoteza nguvu kwenye makosa ya wanasiasa waliyopita na siasa za kulaumiyana na kutoaminiyana.

Tabia ya kumgojeya kiongozi mmoja kuja kuikowa jamii ni tabia yenye kuwapa viongozi wachache mwanya wa kuitumiliya jamii kuendeleza maslahi yao ya kisiasa na ya kibinafsi. Jamii inapoamuwa kumuwachiya kila kitu kiongozi mmoja peke yake huwa imeamuwa kuwa nchi ikifaulu husifiwa kiongozi na inaposhindwa kufaulu pia hulaumiwa kiongozi. Jukumu la kijamii hubakishwa katika kutiya kura kila baada ya kipindi maalumu na kupumzika mpaka baada ya kipindi chengine kuwadiya.

Kwa upande mwengine wa dunia, Europe iliyopondwapondwa kwa vita, na Japan iliyoangamizwa ziliamuwa kujirudishiya tena uhai. Japan haikupoteza wakati kuilaumu Marekani kwa kuipiga mabomu na Ujerumani iliamua kuungana na maadui zake baada ya kujengwa upya kwa Mpango wa Marshall. Hivi karibuni Ujerumani imeamua kujenga mapatano na nchi ambayo ilikuwa ikiiandama kuivuruga ambayo ni Urusi. Nchi ambazo zilikuwa maadui zimeamuwa kwa utulivu na kwa akili kufuata maslahi yao. Jee, Zanzibar na Tanganyika zinahitajiya Mpango wa Afrabia kama Europe ilipojengwa upya kwa Mpango wa Marshall?

Kuna maslahi gani baada ya kuufahamu uhalisia wa mapinduzi, kuendeleya kuyakumbatia yaliyopita badala ya kuyafukuziya na kuyatiya mkononi ya mustakbal? Wazanzibari watatizama nyuma ambako kamwe hawatoweza kurudi au wataelekeya mbele kunakowakabili? Tanganyika haina haja kuendeleya kujitisha au kutishwa na umoja wa Wazanzibari bali iyakaribishe mabadiliko Zanzibar kwa faida za pande mbili. Tanganyika na Zanzibar zilizo huru zina nafasi kubwa zaidi ya kulijenga Shirikisho la Afrika Mashariki na Kati na kujinyankuliya nguvu za kiuchumi na za kisiasa bila ya kujitafutiya uhalali wa kuunganganiya muungano wenye kutawaliwa na Tanganyika.

Lakini Mwalimu Nyerere akisisitiza kila alipopata fursa baada ya kufariki duniya Mzee Karume kwa kusema kuwa kiongozi huyo wa Zanzibar alikuwa ana hamasa kubwa juu ya Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar. Kwa mujibu wa Profesa Issa Shivji na kwa kurudiya:

Hakuna kitu kilicho mbali na ukweli kama hicho. Kama kuna kitu kimoja ambacho Wazanzibari wanamuadhimisha Karume nacho, mbali ya utawala wake wenye kutumiya nguvu, ni Uzanzibari wa Karume na ukaidi wake usiotetereka kukataa kumezwa ndani ya Muungano utakaoipotezeya Zanzibar uhuru na haki yake ya kujitawala. Smith, ambaye alikuwa ana nafasi ya kuonana na Nyerere anapotaka na maofisa wengine alipokuwa akifanya utafiti wake, kwa mfano, alisema kuwa ilikuwa tishio la Nyerere kuwaondowa askari wa Kitanganyika visiwani ndiko kulomfanya Karume mwisho kuukubali Muungano. Lakini alikuwa anayumba mpaka dakika ya mwisho. ‘Hata alitishiya kutohudhuriya sherehe zilizofanywa Dar es Salaam pale hati za Muungano zilipokuwa tayari kubadilishana…’ Kama tulivokwisha kuona, Karume aliitawala Zanzibar bila ya kuzijali hati za Muungano wakati Nyerere aliendeleya kuitumiya sheria kuzidi kuimeza Zanzibar ndani ya Muungano.2

Mapinduzi ya tarehe 7 Aprili 1972

Mzee Abeid Amani Karume aliingiwa na wasiwasi mkubwa kutoka kwa akina Abdalla Kassim Hanga na wenzake. Kama Hanga aliweza kuyapanga Mapinduzi kwa msaada mkubwa kutoka Tanganyika na kuipinduwa serikali ya Zanzibar bila ya kumshirikisha basi na yeye pia anaweza kupinduliwa.

Kulikuwa na mvutano mkubwa baina ya Mzee Karume na Mwalimu Nyerere baina ya mwisho wa mwaka 1971 na mwanzoni mwa mwaka 1972. Kwa mujibu wa vyanzo vyenye kuaminika Mzee Aboud Jumbe aliandika barua na kuipeleka Bara yenye lengo la kutaka mambo kadhaa yarejeshewe serikali ya Zanzibar. Kuna mengi kabla ya hapo ambayo Bara iliikataliya Zanzibar na khasa yale yaliyoonekana kuyaingiliya madaraka ya Zanzibar.

Chanzo kinasema kuwa Mzee Karume akisema kuwa Nyerere “keshatuowa sote sasa na anajifanya kama mume ndani ya nyumba.” Karume na wenzake walikuwa washamgunduwa nini Nyerere anafanya ndani ya jamii na akiwafanyiya wao nini. Mwanzo na kwenye huo mkutano muhimu baina ya Baraza la Mapinduzi na Baraza la Mawaziri wa Bara Nyerere aliwafurusha wajumbe wa Zanzibar kama watoto wadogo na ikabidi zitafutwe mbinu nyingine za kupambana naye.

Hapo ndipo baina ya mwisho wa mwaka 1971 na mwanzoni mwa mwaka 1972 Mzee Karume aliondoka Zanzibar pamoja na memba wa Baraza la Mapinduzi kwenda kuonana na Nyerere pamoja na Baraza lake la Mawaziri. Mzee Karume alikwenda Dar es Salaam akiwa na ile barua iliyoandikwa na kutiwa saini na Mzee Aboud Jumbe kwa sifa yake kama ni Waziri wa Nchi kuhusu Mambo ya Muungano. Walipofika kwenye kikao Mwalimu Nyerere aliliuliza BLM: “Haya yaliyomo ndani ya hii barua ndiyo mnayoyataka?” Mzee Karume alimjibu kwa kumwambiya “waulize wanaume”. Walipoulizwa wote walijibu “ndiyo” mara tatu. Nyerere alikasirika sana na akaomba makaratasi yote yaliyokuwapo pale yakusanywe na akasema “wakati wake bado haujafika!” Mzee Karume akamjibu: “kaa nayo hayo makaratasi na wakati utakapofika utatwita!” Mzee Karume akainuka, akavunja kikao, akarudi kwake Zanzibar.

Mzee Karume alikwenda Dar es Salaam na ujumbe mzito wenye mambo mane ambayo yalikuwa na niya ya kuirudishiya Zanzibar sifa zake kama ni nchi. Barua iliyotiwa saini na Mzee Jumbe ilitaka Zanzibar iwe na polisi wake wenyewe, igawane na Tanganyika asilimia 50-50 ya nafasi zote za Balozi za Tanzania duniani, uwepo uraia wa Zanzibar, na Zanzibar iwe na sarafu yake wenyewe.

Maalim Seif Sharif Hamad amesajiliwa kwenye kitabu kuhusu maisha yake akisema kuwa “Karume pia alikuwa anapanga awe na sarafu yake mwenyewe tafauti na ya bara. Maandalizi yalikuwa yamefika mbali na yalikuwa yakifanyika kwa siri kubwa. Kulikuwapo na Kaunsela katika Kamisheni ya Juu ya Tanzania ya London kwa jina la Omar Zahran ambaye alikuwa ni mtu wa kutoka Zanzibar na ndiye aliyepewa kazi maalumu ya kutengeneza sarafu mpya. Kwa hiyo ni jambo ambalo linajulikana kuwa viongozi hao wawili walikuwa hawasikilizani na Karume alikuwa akitiliwa shaka kuwa alikuwa akijiandaa kuuvunja muungano —ndipo nadharia ya Nyerere kuwatumiliya Makomred wa Umma kumuuwa Karume.”3

Mwalimu Nyerere alipinga Mzee Aboud Jumbe asiwe Rais wa Zanzibar baada ya kuuliwa Mzee Abeid Amani Karume lakini jawabu ya viongozi wa Zanzibar ilikuwa “sisi tushamtangaza.” Baada ya tarehe 7 Aprili 1972 Mzee Jumbe akaanza kuyapitiya yote yale yaliyokuwa yakiibana Zanzibar na akaamuwa kwenda kinyume na wenzake wote na kuitathmini upya na hadharani kesi ya uhaini ambayo baadhi ya vikao vyake vilikuwa vikisikilizwa hadharani jambo ambalo kwa wakati ule lilikuwa ni la nadra ulimwenguni. Mzee Jumbe alifahamu kuwa kesi ile ilikuwa na utata mkubwa katika masuala ya uadilifu na mwisho wake akawasamehe wote waliyokuwa wametuhumiwa.

Baada ya kesi hiyo ambayo ilikuwa maarufu sana Zanzibar ndipo Mzee Aboud Jumbe alipoamuwa kutafuta njiya ya kuilinda Zanzibar kwa kuifunguwa milango ya kidemokrasiya na kuanzishwa kwa Baraza la Wawakilishi. Alitambuwa kuwa hakukuwa na niya safi baina ya viongozi wa Zanzibar na wa Tanzania Bara. Wakati viongozi wa Zanzibar walikuwa wanataka kuuimarisha udugu na ujirani mwema kumbe wenzao wa Tanganyika walikuwa wana lao la kuitawala Zanzibar na kuwa lengo hilo bado limo ndani ya nyoyo zao. Na kwa kuwa viongozi wa bara walitambuwa kuwa viongozi wa Zanzibar walikuwa wanataka kuirejesheya Zanzibar sifa zake kama ni nchi, viongozi wa bara maisha wakiwarudisha kwenye Katiba ile ambayo iliwapa ukubwa wa utawala juu ya Zanzibar.

Ikumbukwe kwamba baada ya kuuliwa Mzee Abeid Amani Karume na yaliyotokeya hakukuingiya tena katika jeshi, polisi au usalama Zanzibar, Muhindi, Mwarabu au Mgazija.

Mapinduzi Dhidi ya Mzee Aboud Jumbe

Mzee Aboud Jumbe ameiweka sawa rekodi ya historiya ya kujiuzulu kwake khasa kwa wale wenye kusema au kuandika kuwa aliamuwa kuzikoroga hisia za uzalendo Zanzibar baada ya kuukosa Uraisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kipindi cha uongozi wa Mwalimu Nyerere. Piya ameweka sawa kuwa aliamuwa kujiuzulu kwa khiyari yake nafasi zote alizokuwa akizishikiliya. Kumbukumbu za mkutano maalum wa Halmashauri Kuu ya Taifa uliofanyika Dodoma tarehe 24–30, Januari, 1984 umenukuu:

Endapo mkutano utaamini au hata kuwa na mashaka kwamba yeye au Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wanahusika na tuhuma hizi, mkutano umpe hisani ya kumruhusu avue wadhifa aliopewa. Kwa kuzingatia maneno haya, mkutano haukuwa na mashaka yeyote kwamba mambo haya yalitendeka mbele yake na chini ya uongozi wake, hivyo Mkutano ulimpa Makamu hisani hiyo. Naye Makamu Ndugu Aboud Jumbe akaipokea hiyo hisani na kwa moyo mkunjufu alisimama na kuiambia Halmashauri Kuu ya Taifa kwamba anajiuzulu katika nafasi zake zote za uongozi. Kikao kilikubali kauli hii bila ya kutokea wa kuipinga. Makamu alihitimisha hotuba yake kwa kusisitiza kuwa sababu ya msingi ya ombi lake imesimama juu ya msingi wa kuaminika; ikiwa haaminiwi, basi hana haki ya kuendelea kwenye siasa au kuutumikia umma.4

Mzee Jumbe alitaka kurudi Zanzibar moja kwa moja kwa ndege yake lakini rubani wake aliamuwa kuumwa siku ile.5 Maelezo ya Katibu Mkuu Mzee Rashidi Kawawa yalielezeya juu ya “hali mbaya ya vurugu ya kisiasa nchini” na Mwenyekiti [Mwalimu Nyerere] alitowa “ufafanuzi kuhusu maadui wa maendeleo ya Zanzibar” ambao adui wa kwanza aliyemtaja alikuwa ni:

a)    Hizbu—Hawa ni wapinzani wa siku nyingi wa Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano. Wanaona Muungano unawapunguzia uwezo wa kufanya fujo Visiwani. Hawa wanajulikana tangu zamani. Lakini siku hizi hawana nguvu. Na upinzani wao hauhitaji kuzungumzwa na kikao maalum cha Halmashauri Kuu ya Taifa.6

b)     

Si hivyo tu, Mwenyekiti alisisitiza kuwa: “Kosa la uhaini wa kuvunja nchi ni kubwa na ni tofauti kabisa na uhaini wa aina nyingine. Kuvunja nchi maana yake ni kuanzisha vita vya wenyewe kwa wenyewe. Afadhali kosa la kuiondowa Serikali kuliko hili la kuvunja nchi.”7

Kama ni kosa basi ni kosa la jinai la kimataifa kwa Dola ya Tanganyika chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere kuivamiya na kuimeza dola ya Zanzibar na si kwa Mzee Aboud Jumbe ambaye hata hajahusika na mapinduzi ya Zanzibar awe dhambi yake ni kusema kuwa Tanzania kuna Serikali Tatu, na kuomba ijadiliwe upya hati ya Muungano, na “kuhusu maandalizi ya kesi ya SMZ dhidi ya serikali ya Muungano” ambayo Mwenyekiti “alitoa hadharani mpango mkubwa na wa siri sana wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuishtaki Serikali ya Muungano katika Mahakama ya Katiba kwa madhumuni ya kuleta mzozo wa kisheria na hatimaye kuvunja Muungano.”8

Chanzo kinaelezeya kuwa tarehe 20 Disemba 1983 Mzee Aboud Jumbe alimuandikiya barua (yenye saini yake) Mwalimu Nyerere kumuelezeya masikitiko yake juu ya kudhoofishwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na hatuwa za kuchukuliwa za kuirejesheya Zanzibar hishma yake. Pia alielezeya Mzee Jumbe kuhusu suala la muungano na khasa kuhusu Mkataba wa Muungano ambao ulikuwa uundiwe Kamati ya pamoja kabla haukupitishwa na kuwa kitendo hicho hakikufanyika na Mkataba wa Muungano ukachukuliwa kuwa ni Mkataba wa kudumu kinyume na makubaliyano. Pia alitaka paundwe Baraza la Rais na Korti ya Rufaa juu ya mambo yanayohusiyana na muungano.

Alielezeya pia katika mambo ambayo yasingepasa kuwemo ndani ya muungano ni Polisi, Uhamiaji, Mikopo ya Biashara na mashirikiano na nchi za nje, aina tafauti za Kodi, Bandari, Mabenki, Mafuta na Gesi, nk. Mzee Jumbe aliongeza kuwa yuko tayari kuonana na Mwenyekiti wa CCM na kuyafahamisha zaidi maudhui ya barua yake ikiwa kutakuwa na haja ya kufanya hivyo. Tarehe 22 Disemba 1983 Mzee Jumbe alipokeya majibu ya barua yenye saini ya Mwalimu ikielezeya kuwa ni vizuri hayo masuala yakajadiliwa ndani ya Zanzibar (Baraza la Wakilishi) kabla ya kulifikisha kunako Halmashauri Kuu ya CCM.

Matokeo yake Mzee Jumbe ‘akakatwa kichwa’ na anaishi mpaka leo wakati matokeo ya Mzee Karume yalimsafirisha kutoka dunia hii kuelekeya ya pili.

 

Mapinduzi Dhidi ya Dokta Salmin Amour na OIC

Dokta Salmin Amour atakumbukwa milele kwa msimamo wake juu ya kujaribu kuiingiza Zanzibar ndani ya taasisi ya Kiisilamu ya OIC na kutokubali kuburuzwa na hayati Mwalimu Nyerere. Aliona mbele mtego wa kuingizwa kwenye Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hakupata kuwa na tamaa ya kuishika nafasi hiyo kwa kufahamu kuwa haikuwa na maslahi kwa Zanzibar. Tatizo la uongozi wake ni alilotaka kulifanya katika kuikwamuwa Zanzibar kutoka makucha ya Tanganyika halikupata kuungwa mkono na muamko wa Wazanzibari waliyo wengi.

Dkt. Salmin alijaribu “Kuondoa kikomo cha vipindi viwili vya miaka mitano mitano kwa mtu yeyote ambaye ni Rais wa Zanzibar.” Mwalimu Nyerere hakujiwekea muda wakati wa uraisi wake ili apate muda wa kuyakamilisha malengo yake lakini alipoamua kungatuka aliweka vikwazo vya muda kwa maraisi waliofuatilia wa Zanzibar na Tanganyika.9

Kamati Kuu ya CCM ilimkataliya Rais Mstaafu Dk. Salmin Amour na Rais yoyote yule atakayekuja baadaye Zanzibar kwa kusema: “…inapendekeza na kuishauri Halmashauri Kuu ya Taifa, kwamba suala la kujadili ukomo wa vipindi viwili vya Urais wa Zanzibar liahirishiwe hadi wakati mwengine muafaka baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu 2000.”10

Mapinduzi Dhidi ya Maalim Seif Sharif Hamad

Mzee Aboud Jumbe aliomba kustaafu tarehe 28 Januari 1984 baada ya kupinduliwa kwa mapinduzi baridi. Katika uchaguzi wa uteuzi wa “Mgombea pekee katika Uchaguzi wa Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar” uliofanyika tarehe 14 Agosti 1985, mapinduzi mengine yalikuwa yanamsubiri Maalim Seif Sharif Hamad na wenzake. Idadi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu waliopiga kura walikuwa 163. Seif Sharif Hamad alipata kura 78 na Idris Abdul Wakil alipata kura 85 na hakukuwa na kura zilizoharibika. Mzee Idris alipata kura 7 zaidi kuliko Maalim Seif. Amir Jamal, aliyekuwa Waziri wa Fedha bara, alilalamika baada ya mkutano, “Hii nchi inakwenda wapi? Tumemuacha huyu kijana [Maalim Seif] mwenye nguvu, na tumemchagua huyu mzee.”11

Mwalimu Nyerere aliwataka viongozi wote akiwemo Maalim Seif wamuunge mkono na wamsaidiye Mzee Idris Abdul Wakil kuwa Rais wa Zanzibar ingawa kwenye kampeni za CCM Pemba alikuwa anapingwa waziwazi. Kwa mujibu wa Maalim Seif, Nyerere aliamuwa kwenda Pemba na kila alipokuwa analitaja jina la Mzee Idris alikuwa anazomewa na kila alipokuwa analitaja jina la Maalim Seif alikuwa anapigiwa vifijo.12 Alisema Mwalimu kuwa “anafahamu shauku ya Wapemba kuwa Idris ni Raisi wa nne wa Zanzibar ambaye hatoki Pemba” kwa hiyo “naahidi kuwa mara ijayo nitayachukuwa maoni yenu na nitayafanyiya kazi.” Siku ya pili, anaendelea kuelezeya Maalim Seif, Mwalimu Nyerere alihutubiya Unguja na waziwazi alitumiya siasa za wagawe uwatawale. Alisema “Watizameni hawa Wapemba. Wanamtaka Raisi wao wenyewe, na ikiwa na nyinyi mtamtaka Raisi wenu wenyewe, basi vipi tutaiendesha nchi hii?” Aliwaaambiya “Idris ni mtu wenu, ikiwa Wapemba wanampenda au hawampendi, wamuunge mkono.”13

Maalim Seif anamsifu Mzee Idris kuwa alikuwa ni “mtu asiyejiona, mkweli, na mtu wa dini…Alikuwa anaipenda Zanzibar na alikuwa akiwachukiya wanasiasa mafisadi lakini alikuwa hana uamuzi mkubwa wa uongozi…Kabla hajafariki alimtuma rafiki yake mkubwa, marehemu Mzee Ali Muhammed aje anione. Alisema alikuwa na ujumbe kutoka kwa Sheikh Idris wa kuniomba msamaha kwa mambo yalionifika…nikamwambia mwambie nimemsamehe kwa lolote lile alilonifanyia duniani na akhera.”14

Tarehe 11–13 Mei 1988 kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kilifanya mkutano wa tatu Dodoma na Halmashauri ilipokeya na kujadili taarifa ya ziara ya Katibu Mkuu wa Chama, Mzee Rashid Mfaume Kawawa uliyofanyika mwezi Aprili 1988 “kukagua uhai wa chama.” Katika jumla ya sababu ya kutoridhishwa na hali ya kisiasa Unguja na hasa Mikoa ya Kaskazini na Kusini zilikuwa hujuma dhidi ya Chama, Chama kuingiliwa na Maadui, na Kampeni Dhidi ya waasisi wa Chama. “Wazee wa Mikoa ya Pemba walimwarifu Katibu Mkuu kwamba Pemba Chama hakipo, ipo Serikali tu.”

Kampeni dhidi ya waasisi wa Chama “imekuwa ikiambatana na kebehi ya mapinduzi ya mwaka 1964, mapinduzi ambayo yaliungoa utawala dhalimu wa sultani, na kurejesha uhuru na heshima ya Wazanzibar.”

Halmashauri Kuu ya Taifa

iliwaona watuhumiwa wafuatao ni wasaliti wa Chama, hivyo kwa kauli moja iliamua kuwafukuza kutoka katika Chama Cha Mapinduzi.

1. Ndugu Seif Shariff Hamad

2. Ndugu Suleiman Seif Hamad

3. Ndugu Hamad Rashid Mohamed

4. Ndugu Soud Yussuf Mgeni

5. Ndugu Khatib Hassan Khatib

6. Ndugu Shaaban Khamis Mloo

7. Ndugu Ali Haji Pandu

…Tume ya Udhibiti na Nidhamu ifanye kazi ya kuwadhibiti Juma Ngwali, Masoud Omar, Maulidi Makame, Juma Othman Juma, Makame Ussi Machano, na Asha Bakari…

Vile vile Kikao kilisisitiza kuwa wanachama washirikishwe kupitia vikao vyao matawini kuwafichua wale wote waliohusika katika kuvuruga hali ya utulivu wa kisiasa Zanzibar.15

Mapinduzi Umoja wa Mataifa (UN)

Tanganyika ilipoupata uhuru wake tarehe 9 Disemba 1961 na ilipotaka kujiunga na Umoja wa Mataifa, Mwalimu Nyerere kwa sifa yake kama ni Waziri Mkuu alipeleka ombi kwa Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo, Bwana U Thant, na alipeleka barua tarehe 9 Disemba 1962 ya kukubali uwanachama na masharti yake kwa mujibu wa Katiba ya jumuiya hiyo. Zanzibar piya ilifanya hivyohivyo. Waziri Mkuu, Bwana Muhammed Shamte, alimpelekeya barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ya kuomba uwanachama na kumhakikishiya kuwa Zanzibar imeyakubali masharti ya uwanachama wa jumuiya.

Zanzibar ilipoupata uhuru wake tarehe 10 Disemba 1963, miaka mitatu baada ya uhuru wa Tanganyika, Waziri Mkuu wake, Sheikh Muhammed Shamte, alipeleka barua ya ombi la kutaka kujiunga na Umoja wa Mataifa na Zanzibar ilipokubaliwa uwanachama Bwana Shamte alimpelekeya barua Katibu Mkuu kukubali kuyatimiza masharti ya Katiba ya Umoja wa Mataifa (Angaliya kiambatanisho B).16

Tarehe hiyohiyo ya 10 Disemba 1963, Sultan wa Kikatiba wa Zanzibar, Sayyid Jamshid bin Abdulla bin Khalifa alimpelekeya barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kumjuulisha kuwa Waziri Mkuu Sheikh Muhammed Shamte Hamadi na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Biashara, Sheikh Ali Muhsin, wataiwakilisha Zanzibar katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakati ombi la uwanachama wa Zanzibar litakapowasilishwa (Angaliya kiambatanisho C).17 Zanzibar ikawa mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa tarehe 16 Disemba 1963 na Dola ya Zanzibar ikapinduliwa tarehe 12 Januari 1964.

Tarehe 27 Aprili 1964 Umoja wa Mataifa ulipata taarifa kutoka vyombo vya habari kuwa Tanganyika na Zanzibar ambazo kabla zilikuwa ni memba tafauti wa umoja huo kuwa zimekuwa ni Nchi moja yenye uwakilishi wa nchi za nje mmoja. Bwana C.A. Stavropoulos, Katibu Mkuu wa Ushauri wa Sheria wa Umoja wa Mataifa, alimuandikiya barua Katibu Mkuu U Thant, kupitiya kwa Bwana Jose Rolz-Bennett (Deputy Chef de Cabinet), kuwa Umoja wa Mataifa bado haijaarifiwa rasmi kuhusu kuundwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Barua imeanza kwa kusema:

Kukosekana kwa waraka [wa makubaliyano ya muungano] ni vigumu kuamuwa kwamba Dola mbili za Tanganyika na Zanzibar zimeungana kuunda Dola mpya kabisa, au Zanzibar imejiunga na Tanganyika (ambayo ni kubwa sana kwa eneo na kwa idadi ya watu), na huku Tanganyika ikiendeleya kuwepo chini ya jina jipya na eneo na idadi ya watu kubwa zaidi. Kuna mifumo tafauti ndani ya sheria ya kimataifa, na mifano ya mifumo tafauti ipo katika uwanachama na uendeshaji wa Umoja wa Mataifa.18

Barua inaendeleya kufahamisha kuwa muungano wa Misri na Syria wa kuunda Nchi moja ya Umoja wa Jamhuri ya Kiarabu [UAR] ulifanyika mwaka 1958. Serikali ya UAR ilimuarifu rasmi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kumuomba awaarifu rasmi wanachama wa umoja huo na mashirika yake. Tarehe 24 Februari 1958 Ujumbe wa Kudumu wa Misri wa Umoja wa Mataifa uliuarifu kwa barua Umoja huo kuwa:

Maoni ya wananchi wa Misri na Syria yaliyokusanywa tarehe 21 Februari 1958 yameonyesha wazi khiyari ya watu wa Misri na Syria kuziunganisha nchi zao mbili na kuunda Nchi moja, na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Umoja wa Jamhuri ya Kiarabu ana hishima ya kumuarifu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuundwa kwa Umoja wa Jamhuri ya Kiarabu, na Cairo mji mkuu wake, na kuchaguliwa kwenye kura hiyohiyo ya maoni, kuwa Rais Gamal Abdel Nasser atakuwa ni Rais wa Jamhuri mpya.19

C. A. Stavropoulos hakuwa na hakika Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ilikuwa na sura gani na alimuarifu U Thant kuwa “iko wazi kuwa Katibu Mkuu atakuwa ana mamlaka ya kubainisha hali na kutokana na msingi huo afanye mipango ya kuwaweka wawakilishi wa Jamhuri ya Muungano badala ya wale wa Tanganyika na Zanzibar na kuchukuwa hatuwa nyingine kuhusu kubadilisha jina, bendera, nk.”18 Badala ya kuwasiliyana na serikali mpya ya nchi ya Zanzibar ambayo ilikuwa na uwanachama wa Umoja wa Mataifa, Stavropoulos aliomba mawasiliano na muwakilishi wa Tanganyika tu na kuwa “aarifiwe kuhusu umuhimu wa kupata tamko kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa Katibu Mkuu kwa ajili ya kusambazwa kwa mashirika husika juu ya kuundwa kwa Jamhuri, na kuzileta sifa za uwakilishi mmoja wa Jamhuri.”20

Mei 6 1964 Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje kutoka Dar es Salaam ilimpelekeya barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kumuarifu kuwa

Mkataba wa Muungano baina ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar umetiwa saini tarehe 22 Aprili 1964 na kuwa Mkataba huo ulipitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi la Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, na Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zimeungana na kuwa Nchi moja tarehe 26 Aprili 1964, chini ya jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na chini ya Uraisi wa Mwalimu Julius K. Nyerere. Kopi ya Mkataba wa Muungano imeambatanishwa na barua hii.21

Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambalo lilipelekwa Umoja wa Mataifa kutoka Dar es Salaam kwenye barua ambayo haina nembo, wala jina la mhusika aliyetiya saini, halikukaa zaidi ya miezi sita (Angaliya viambatanisho mwisho wa kitabu).22 Tarehe 2 Novemba 1964 barua kutoka Ujumbe wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, uliyopo New York, na yenye mhuri wa Tanganyika, na ambayo haina jina au saini ya mtu yoyote, ilimuarifu Katibu Mkuu kuwa “Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kuanziya sasa, itajulikana kuwa ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” (Angaliya viambatanisho D, E, F, G, H, I).

Barua muhimu ya kuuarifu Umoja wa Mataifa kuhusu kuundwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na miezi sita baada ya hapo kubadilishwa jina na kuitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilikosa jina la mtu na cheo chake na saini kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Dar es Salaam. Barua ya ujumbe mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikuwa na jina na saini ya Oscar S. Kambona, Waziri wa Mambo ya Nje. Barua haikusema ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulikuwa na watu 16. Kati ya hao watatu (3) walitoka Zanzibar:

1. Mheshimiwa Abdulrahman Babu, Waziri wa Biashara na Mashirika.

2. Mheshimiwa Othman Sharif, Balozi wa Tanzania Marekani.

3. Bwana Adam Mwakanjuki, Ofisa wa Mambo ya Nchi za Nje.

Wajumbe kumi na tatu (13) waliyotoka Tanganyika ni:

1. Mheshimiwa Oscar S. Kambona, Waziri wa Mambo ya Nje, na Mwenyekiti wa Ujumbe.

2. Bwana John Malecela, Mjumbe wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa.

3. Bwana E.E. Seaton, Mkurugenzi wa Utafiti, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje.

4. Bwana G.S.Magombe, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje.

5. Bwana Benjamin Mkapa, Naibu Katibu, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje.

6. Bwana A. B. C. Danieli, Konsela, Ujumbe wa Kudumu wa Tanzania, Umoja wa Mataifa.

7. Bwana W. Ramsay, Ofisa wa Utafiti, Ujumbe wa Kudumu wa Tanzania, Umoja wa Mataifa.

8. Bwana D. Phombeah, Ubalozi wa Tanzania, London (Mshauri).

9. Bibi Martha Bulengo, Naibu Seketeri, Wizara ya Maendeleo ya Jamii na Utamaduni wa Taifa (Mshauri).

10. Bwana P. C. Bakilana, Mwanasheria Mkuu, Wizara ya Uadilifu (Mshauri).

11. Bibi E. Malecela (Mshauri).23

Mbali ya kuzidiwa kwa idadi, waheshimiwa waliochaguliwa kuiwakilisha Zanzibar ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakukuwa na hata mmoja ambaye alikuwa ana mamlaka ya kuzungumza kwa niaba ya Zanzibar. Babu alikuwa si tena Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje. Othman Sharif hakuwa karibu au akipatana na uongozi wa Mzee Karume uliyokuwemo ndani ya Zanzibar. Adam Mwakanjuki alikuwa mpinduzi lakini alikuwa ni ofisa baina ya waheshimiwa wawili kutoka Zanzibar ambao kisheria hawakuwa wakiwakilisha mamlaka ya nchi ya Zanzibar ambayo ilikuwa imeshafutwa kwenye barua kutoka Wizara ya Nje ya Dar es Salaam kwenda Umoja wa Mataifa.

Nyuma kidogo, tarehe 14 Mei 1964 C. A. Stavropoulos alimuandikiya tena barua Jose Rolz-Bennett juu ya maudhui ya kuusajili Mkataba wa Muungano baina ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kwa mujibu wa kifungu 102 cha Katiba ya Umoja wa Mataifa. Alimuarifu kuwa “Kifungu hichohicho kinatowa maelezo kuwa mikataba ambayo haikusajiliwa haiwezi kutajwa mbele ya shirika lolote lile la Umoja wa Mataifa.”24 Stavropoulos akapendekeza kwa Rolz-Bennett apeleke barua ya simu kwa muwakilishi wao aliyekuwepo Dar es Salaam ili aufikishe ujumbe ufuatao Serikalini:

Kwa hisani yako iarifu Serikali kuhusu maelezo yaliyomo kwenye kifungu 102 cha Katiba ambacho kinawataka memba wa Umoja wa Mataifa waisajili kwa haraka mikataba ambayo wameifunga, na sharti hili linatumika kwa Mkataba wa Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar. Taratibu za kukipa nguvu kifungu 102 cha Katiba kinahitajiya Serikali inayosajili kuipa Seketeriet kopi moja ya Mkataba ambayo imeshuhudiwa kuwa ni ya kweli na kopi kamili ambayo itakuwa na maelezo ya kutoridhika yatakayofanywa na pande husika, na kopi mbili zaidi za Mkataba, na kauli kuhusu tarehe na mpango wa kuanza uwanachama.25

La msingi ni kwa vile Zanzibar na Tanganyika zilikuwa nchi mbili ambazo zilikuwa ni wanachama wa Umoja wa Mataifa suala la uwanachama wa Nchi moja haukupelekwa kujadiliwa kwenye Kamati ya Usalama ya Umoja huo. Kulikuwa na taarifa tu kutoka kwa Katibu Mkuu kwenda Baraza Kuu kuutambuwa uwanachama mpya wa nchi mbili kuwa moja kwa mujibu wa barua iliyotoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Dar es Salaam ya tarehe 6 May, 1964.26

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliridhika na barua hiyo na ule ushauri aliopewa na C.C. Stavropoulos wa kutaka Mkataba wa Muungano usajiliwe kwa mujibu wa kifungu 102 cha Katiba ya Umoja wa Mataifa ukawachwa kwa sababu zisojulikana. Hapa tena inawezekana kuwa wasiwasi usiokuwa na msingi aliyowatiya Nyerere Wamarekani kuhusu Vita Baridi na kuingiya Ukoministi ulitowa tija ya kumsaidiya Mwalimu akae na uwanachama wa Nchi moja ndani ya Umoja wa Mataifa bila ya kuulizwa au kuhojiwa zaidi.

Ukweli unabakiya kuwa Mkataba wa Muungano baina ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar haukuwahi kusajiliwa katika Seketeriet ya Umoja wa Mataifa. Kwa mujibu wa Andrei Kolomoets wa Ofisi ya Mambo ya Kisheria ua Umoja wa Mataifa “Kama ulisajiliwa basi kungelikuwepo rekodi katika Data Base na shahada ya usajili ingelikuwepo. Nimecheki, haipo.”27  

Zanzibar, Ezekieli, na Jangwa la Mifupa Mikavu

Wazanzibari na Watanganyika wamechotwa akili na wapishi wachache sana waliyoamuwa kujificha nyuma ya paziya la mapinduzi na la muungano kwa miaka arubaini na sita. Mwalimu Nyerere alisema kuwa “nyumba ya Tanzania imetikisika” ingawa hakuweza kutupa sababu halisi za mtikisiko huo ingawa alitaka mjadala wake uendelee. Kuendeleya kulaumiyana hakutoleta faida yoyote ila kulizidisha joto la malumbano lisilotowa mwangaza. Mapinduzi yamejitandiya nyumba ya buibui na yameweka bawaba zenye kutu kwenye mlango wa Muungano. “Na hakika nyumba dhaifu mno kuliko zote ni jumba la buibui, laiti kuwa wanajua.”28

Kabla ya kufariki kwake, hayati Mwalimu Nyerere alikwishatowa ishara ya kuanguka kwa jumba la buibui kwa sababu, kama mjenzi mahiri, alikuwa akiufahamu upya, uimara, na hatima wa nyumba aliyoijenga. Utabiri wa kuanguka kwa jumba la buibui utatimiya pale patakapopatikana uongozi ambao umeamuwa kuendeleya kuyafumba macho na kukataa kuziyona nyufa za misingi ya Mapinduzi na Muungano. Watawala wasiotaka kuziyona nyufa za misingi ni mfano wa ile mifupa mikavu iliyokata tamaa na kushindwa kuamini kuwa itaweza kuitomeya na kuinusuru nyumba na maendeleo ya wananchi wao.

Kwa kumaliziya, Nabii Ezekieli aliombwa atowe habari nzuri juu ya mifupa iliyojaa kunako bonde. Pakatokeya kishindo kikubwa “na mifupa ikasogeleana, mfupa kwa mfupa mwenziwe…lakini haikuwamo pumzi ndani yake.” Mifupa iliweza kuzungumzishana lakini ilishindwa kuungana. Ndivyo jamii mbili za Kizanzibari, ile yenye mizizi mirefu, na ile yenye mizizi mifupi Zanzibar, kukatishwa tamaa na mirengo yenye kuwafarikisha na kushindwa kuishi pamoja na kuijenga Zanzibar. Mifupa yao imekauka na imetawanyika na haiko pamoja ndani ya kiwiliwili cha Zanzibar.

Aliposhindwa Nabii Ezekieli kuisemesha mifupa ndipo alipoambiwa: “Tabiri utabirie upepo, mwanadamu, ukauambie upepo, Bwana Mungu anasema hivi: njoo kutoka pande za upepo nne. E pumzi ukawapuzie [puliziye] hawa waliouawa, wapate kuishi. Basi nikatabiri kama alivoniamuru, pumzi ikawaingia, wakaishi wakasimama kwa miguu yao, jeshi kubwa mno.”29

Viongozi wa Zanzibari wameisemesha mifupa ya Kizanzibari na inaitikiya na inahudhuria mikutano na vikao lakini haikuamuwa kusimama kuiteteya na kuidai haki ya Zanzibar kwa sauti moja kwa sababu uongozi bado ulikuwa haujaamuwa. Umma huamka wakati wa uchaguzi na kurudi kunako bonde la mifupa uchaguzi unapomalizika.

Kitabu hichi huenda kikawa ni upepo wa kuiondowa khofu ili Wazanzibari na Watanganyika kwanza waweze kuukubali ukweli na baadaye kukaa na kuzugumza kama ni watu walio sawa na wenye kuishi ndani ya wakati mmoja na kuamuwa namna ya kuitengeneza upya misingi ya Mapinduzi na Muungano. Upepo huu utategemea kuwepo kwa mazingira matatu muhimu:

1. Ushirikiyano wa makundi makubwa wenye kuongozwa na Uzanzibari, na wenye kuongozwa na ilimu iliyokomboka, vyombo vya habari vyenye kufuata maadili na uchunguzi wa kina, na raia wenye ukakamavu katika kila jimbo, mtaa, na viyambo.

2. Kutowachiya kuyafahamu makisiyo ya ukweli wa historiya kuninginiya juu ya maslahi ya vyama vya siasa vinavyopingana juu ya utaifa na dola ya Zanzibar, ikiwa tawala au vya upinzani, ambavyo bado vina viongozi na wafuasi wengi ambao wamo ndani ya jumba la buibui la mapinduzi na muungano.

3. Kuuilimisha umma kuhusu mapinduzi mapya ya kifikra na kuupiga fundo mtutu wa bunduki wenye kuilinda dhambi ya Tanganyika ya kuivamiya nchi ya Zanzibar, ni njia pekee ya kuzuwiya kuendeleya kuitesa Zanzibar na kuirejesheya kiti chake katika Umoja wa Mataifa.

 

Oscar Kambona na Afrabia

Katika mwanasiasa muhimu sana wa Tanganyika na Tanzania muhimu sana ambaye hakubahatika kuandika au kuandikiwa kumbukumbu juu ya maisha yake ni hayati Oscar S. Kambona na khasa juu ya undani wa ugomvi na mivutano baina yake, Mwalimu Nyerere na Mzee Rashidi Kawawa. Hadithi ya Kambona na uhusiyano wake na mapinduzi na muungano wa Zanzibar ni ndefu kuliko ilivyogusiwa ndani ya kitabu hichi na sidhani kama kuna mtu mbali ya hayati Mwalimu Nyerere ambaye angelikuwa ana uwezo wa kuiyandika kwa tafasili zake. Kabla ya kufariki duniya Oscar alikuwa ni mtu aliyevunjika kabisa na hayati Mwalimu Nyerere alipozipata habari za kifo chake kutoka Balozi wa Tanzania London, kauli yake ya kwanza ilikuwa “Oh, poor fellow!” Watu waliogopa hata kwenda mazikoni kwake alipozikwa Dar es Salaam kwa kumuogopa Mwalimu.

Kambona alikuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa TANU na baada ya uhuru wa Tanganyika aliwahi kuzishika Wizara za Ulinzi, Mambo ya Nchi za Nje, Ilimu na Mambo ya Ndani. Mwaka 1967 alikosana na Mwalimu Nyerere na alikimbiya na kwenda zake uhamishoni London alikoishi miaka 25. Kwa mujibu wa mdogo wake, Andrew Kambona, Oscar alirudi Tanzania wakati wa kuanzishwa vyama vingi akiwa katika hali mbaya ya kinafsi na kiuchumi.30 Alianzisha chama cha kisiasa The Tanzania Democratic Alliance Party (TDAP).

Katika barua ya tarehe 15 Oktoba, 1993, Oscar Kambona alimuandikiya barua kiongozi mmoja wa nchi za Kiarabu za Ghuba ambayo kwa mujibu wa Andrew Kambona haikumfikiya. Aliandika Oscar: “Moja katika hamu yetu ni kuujenga upya uhusiano maalumu uliyokuwepo baina ya nchi zetu kutoka zama za kale na tunachukuwa fursa hii kuelezeya shauku yetu kuwa baada ya kuunda Serikali ijayo tungelipendeleya utupe hishma ya kuwa wa mwanzo wa kuipa nchi yetu Ziara ya Kitaifa….Na mwisho tutapenda kukuhakikishiya niya yetu ya kuuimarisha uhusiano maalumu na wa kihistoria baina ya nchi zetu mbili ambao tunautizamiya kuwa nje ya itibari za kisiasa.”31

Hayo ni maneno ndani ya barua iliyotiwa saini na Oscar S. Kambona baada ya kuyasimamiya mapinduzi yaliyokuwa na lengo la kukimaliza kiti cha ubeberu mkongwe Afrika Mashariki na Kati. Barua haina dalili ya kujuta kwa yaliyotokeya kunako mapinduzi lakini ni ishara tosha kuwa hata kinara cha utekelezaji wa mapinduzi ya Zanzibar kilifika mahala na kuziyona faida za uhusiano mkongwe baina ya Waafrika na Waarabu—Afrabia.

Hiyo ndiyo kazi ambayo inangojewa kufanywa na uongozi ambao unaona ipo haja ya kuusitisha mtikisiko aliyouzungumziya Mwalimu Nyerere usiendelee pale aliposema:

Tunachotaka ni kwamba nyufa hizo zieleweke na tukubaliane kwamba kazi yetu ni kuziziba na tupate uongozi unaoelewa hivo. Kwamba kazi ni kuziba nyufa tulizoziona katika taifa letu. Kazi si kuendelea kulitikisa taifa hili. Litabomoka. Halitabaki.32

Pambazuko jipya la kheri limejichomoza katika siku za karibuni Zanzibar. Tumeshuhudia viongozi wa kambi mbili za siasa, CCM na CUF, wakiweka kando tafauti zao za itikadi na wakiwaongoza Wazanzibari kwenye umoja na utengamano. Kinachowaunganisha ni kuzisimamiya kidete haki za Zanzibar. Hizi ni dalili njema zinazopaswa kupongezwa na kila mwenye kuitakiya kheri Zanzibar. Viongozi wakuu wa vyama viwili vya siasa Zanzibar, Mheshimiwa Rais Dkt. Amani Abeid Karume wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Maalim Seif Sharif Hamad wa Chama Cha Wananchi (CUF) wamejitokeza kuwaunganisha Wazanzibari kuulinda utambulisho wao na kuzihami rasilimali zao.

Kati ya wawili hawa, mwenye kustahiki pongezi za aina ya pekee ni Mheshimiwa Rais Amani Abeid Karume kwa sababu yeye ndiye mwenye dhamana ya uongozi. Asingetowa nafasi ya kujengeka umoja huu, jitihada za wengine zisingefuwa dafu. Katika kipindi cha takriban miaka miwili sasa, ameonyesha ushujaa wa hali ya juu kwa kuongoza Serikali ambayo imeweka rekodi ya kutoogopa katika kupiganiya maslahi ya Zanzibar, tena kwa uwazi na kwa hoja.

Hapana shaka yoyote historia itamuandika vyema katika hili na bado ana nafasi ya pekee ya kuwaongoza Wazanzibari siyo tu kufunguwa ukurasa mpya bali kuandika kitabu kipya kabisa katika mahusiyano yao yatakayotowa nafasi ya ujenzi wa mustakbali mwema kwao na kwa vizazi vyao. Katika hili, Rais Karume ana nafasi pekee kwani yeye na familia yake ni mfano mwema wa mjengeko wa jamii ya Kizanzibari uliyotokana na mchanganyiko wa damu wa aina yake, mchanganyiko wa Afrabia.

Wazanzibari wote wamepitiwa na dunia vichwani na miguuni mwao kwa yaliyotendeka huko nyuma na wakati umefika kwa Rais Karume kuwaonyesha na kuwaachiya Wazanzibari njia za kutokeya, za nje na za ndani, ili Zanzibar ijirudishiye utulivu na maendeleo ya kudumu. Maalim Seif naye anapaswa kuendeleza mkabala mpya wa kisiasa aliyojitambulisha nao katika miaka ya karibuni ili pamoja na Rais Karume wakumbukwe kwa kuitendeya kheri Zanzibar. Historia iko upande wao.

Nguzo Saba za Hikma na Mapinduzi ya Afrabia

Kwenye kitabu chenye kuchemsha bongo kiitwacho The New Asian Hemisphere: The Irressistible Shift of Global Power to the East Profesa Kishore Mahbubani amezitaja “nguzo saba za hikma za Magharibi” zilizochangiya kulirudishiya bara la Asia hadhi na mchango wake duniani: Soko Huriya, Sayansi na Teknolojiya, Ustahiki (meritocracy), Kutoongozwa na Mirengo ya Kiaidiolojiya (pragmatism), Thakafa ya Amani, Utawala wa Sheria, na Ilimu.33 Zanzibar imepita ndani ya nusu karne ambayo ingeliweza kupiga hatuwa kubwa zaidi ingelikuwa imepata nafasi ya kuziiga nguzo saba za hikma kutoka Magharibi:

1. Kutoongozwa na Mirengo ya Kiaidiolojiya: Mapinduzi ya Zanzibar na muungano yaliongozwa na mrengo wa kisiasa wa Pan-Africanism ambao umewafitinisha Waafrika na Waarabu. Mrengo wa Pan-Africanism umeshindwa kuwailimisha Wazanzibari au Watanganyika kuhusu historia ya mchango wa Tanganyika katika mapinduzi ya Zanzibar na muungano wake na Tanganyika. Kutokana na historia ndefu ya mchanganyiko mkubwa wa Kiafrika na wa Kiarabu, Zanzibar inahitajiya kuongozwa na mrengo wa kisiasa wa Afrabia ambao unautukuza uhusiyano mkongwe baina ya Waafrika na Waarabu badala ya kuudhoofisha na ndiyo msingi uliyoijenga Organisation of African Unity (OAU) na hivi sasa African Union (AU).

2. Thakafa ya Amani: Mavamizi ya Zanzibar kutoka Tanganyika yaliofanywa na makhasimu wa Mzee Karume na mauwaji ya halaiki na vitisho vilivyofuatiliya baada ya Mapinduzi, kumewafanya Wazanzibari waliyopita wasiaminiyane wenyewe kwa wenyewe na wasiwaamini ndugu na jirani zao wa Tanganyika. Hishima ya maisha ya binaadamu ilivurugwa kwa kiasi kikubwa na haki za binaadamu zilidharauliwa sana huko nyuma. Hadithi za kubuni za “utumwa wa Waarabu” zimesababisha kukosekana kuuhishimu mchanganyiko maalumu wa kikabila na wa kiasili wa Kizanzibari na ukaongeza chuki na kutoelewana baina ya vyama vya kisiasa. Zanzibar ya leo imepiga hatuwa kubwa sana kwa kutoruhusu usambazaji wa habari zisizo na uthibitisho au zenye kuongeza mifarakano ndani ya jamii ya Kizanzibari.

3. Utawala wa Sheria: Ulitoweka kwa muda mrefu kwa sababu roho ya kupinduwana iliendeleya kwa kipindi kirefu na ikawa vigumu kurudi kunako utulivu na amani kwa sababu vyombo vya sheria vilikosa misingi ya kuwajibika. Hali ilianza kurudi katika kipindi cha utawala wa Mzee Aboud Jumbe na khasa pale alipolianzisha Baraza la Wawakilishi la Zanzibar. Hali ya kisheriya ya hivi sasa Zanzibar ni yenye kutowa matumaini makubwa na mustakbal mzuri. Kizazi cha leo cha Zanzibar hakina kumbukumbu ya mapinduzi ya Zanzibar na kwa hiyo kina uwezo mkubwa zaidi wa kusonga mbele kuliko kile kilichokuwa karibu na mapinduzi.

4. Ustahiki: Fikra ya Uafrika kuutawala Ushirazi, Uwarabu, Uhindi, nk, ni athari za mrengo wa kisiasa wa Pan-Africanism katika mazingira ya Zanzibar ya mchanganyiko wa watu. Kuuliwa kwa marehemu Mzee Abeid Amani Karume kulisababisha makabila fulani yasikuwemo ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama wa nchi au kutopewa nafasi za kuendeleya na masomo. Msingi wa baadhi ya Wazanzibari kuonekana kuwa ni wa daraja la pili au umuhimu wao kuwemo zaidi kwenye biashara na si utawala pia unatokana na mrengo wa kisiasa uliyokuwa ukishadidiya nani ana haki zaidi Zanzibar, mgeni au mwenyeji na tafisiri ya ugeni au uwenyeji ulitegemeya kigezo cha kuwa na asili ya kutoka bara la Afrika au bara la Asia. Zanzibar ya leo inaelekeya kuwashirikisha Wazanzibari wa kila kabila na asili katika maamuzi muhimu ya mustakbal wake.

5. Ilimu: Wazanzibari wengi sana wenye ilimu na ujuzi wa kimataifa wameweza kutowa mchango mkubwa sana kwenye nchi zilizowakaribisha na tayari Wazanzibari wamejiandaa na kujielekeza kuuvuna utajiri huo kwa maslaha ya Zanzibar. Kukiwezesha kizazi kipya na taasisi za kijamii, walimu na wanafaunzi kuufahamu ukweli wa mapinduzi ya Zanzibar na muungano wake kutawajengeya Wazanzibari ari na utambulisho mpya ndani na nje ya nchi yao. Zanzibar inaweza kuwaandaa wanafunzi wake na kuwaombeya misaada ya nafasi nyingi za kusoma kwenye vyuo vikuu vyenye kuhishimika vya nchi za Magharibi. Wakati hali ya kiuchumi ya Zanzibar inakuwa wanafunzi wengi au wote watakaopatiwa nafasi za kwenda kusoma masomo ya juu nchi za Magharibi wataweza kurudi kuitumikiya Zanzibar.

6. Sayansi na Teknolojiya: Hili limekuwa gumu kupiga hatuwa kwa sababu ya utajiri wa Zanzibar ambao ni watu wake wenye ilimu na ujuzi kuwepo nje ya Zanzibar na kukosekana mbinu za kuwavutiya kurudi ikiwa moja kwa moja, kuazimwa na kulipwa na nchi husika kuja kuisaidiya Zanzibar, au kwa kujitoleya.

7. Soko Huriya: Linategemeya jamii ambayo imewekeza kwa hali ya juu kwenye sekta ya ilimu kutoka chekecheya mpaka chuo kikuu na kuitumiya ilimu kwenye sekta za sayansi na teknolojiya katika miradi ya kiuchumi ambayo itawainuwa Wazanzibari walio wengi kutoka hali duni za kiilimu na kiuchumi na kuwaweka kunako tabaka lenye nguvu za kiuchumi na lenye kulinda amani. Miradi ya kiuchumi ya Zanzibar itaweza kutekelezeka kwa ufanisi mkubwa iwapo itaendeshwa na Wazanzibari wenye kila aina ya ujuzi na ilimu na katika sekta ambazo Zanzibar itaweza kujiimarisha kutokana na sifa zake za kiilimu, kiuchumi, na za kihsitoria.

Eqbal Ahmad alikuwa na fikra ya kufunguwa Pakistani Chuo Kikuu cha Ibn Khaldun ambacho kilikuwa kiwe na minhaji ya masomo yenye mfungamano baina ya masomo ya kisasa ya kidunia na tamaduni za turathi za zamani. Hoja ya Ahmad ilikuwa

hatutoweza kupigana na misimamo mikali ya kidini mpaka tutakapoweza kulizalisha tabaka lenye masomo ya kileo la wapenda maendeleo ambao pia wana ilimu ya turathi zilizopita na wenye kuweza kuchaguwa yale yaliyo mazuri.34

Zanzibar inaweza kufikiriya mifumo tafauti ya Chuo cha Afrabia ikiwa kwa njiya ya mitandao au teknolojiya mpya za mawasiliyano, au kwa kuudurusu mfumo wa Chuo Kikuu cha Umoja wa Mataifa, au kwa kuuchanganya mfumo wa kwanza na wa pili, au kuzipeleka mbele programu za Afrabia katika vyuo vikuu vya kawaida.35

Lengo ni kuwaleta pamoja wanafunzi na wasomi wa Kiafrika na wa Kiarabu na kukiandaa kizazi kipya ambacho kitapatiwa nafasi za kusoma za makusudi kunako vyuo vyenye hadhi duniani. Lengo la mwisho si kuukuza Uafrika au Uwarabu au kukwama ndani ya uzalendo wa Afrabia. Hapo itakuwa tumeipanda ngazi halafu tumetumbikiya ndani ya pango jingine na jumba jipya la buibui.

Siku zote, lengo liwe kuondowa umasikini unaoletwa na ujinga na upotoshaji wa binaadamu kwa ujumla. Na ujinga na upotoshaji unaletwa na fitina zenye kuichafuwa na kuiiba akili ya binaadamu kujitegemea mwenyewe na kumuomba Muumba wake ampe na amuongezee ilimu ili atoke kunako giza aelekee kunako zuka la ukweli na ukombozi. Mapinduzi ya kuziondowa fitina ni mapinduzi yatakayoleta thakafa na utamaduni wa amani Zanzibar na Afrika Mashariki yake.

Hili litawezekana ikiwa litaongozwa kwa kuvifufuwa vituo vikongwe na kuvijenga vituo vipya vya ilimu vya Waafrika na vya Waarabu, vya Waislam na vya Wakristo. Kucha za chuki na fitina hazitamuwacha binaadamu peke yake kama hajapigana kujenga mfungamano baina ya binaadamu wenye kuongozwa na mwangaza wa dini na ilimu za kidunia zisoweka mipaka, mirengo, au madhehebu.

Utekelezaji wa nguzo saba za hikma kutoka ustaarabu wa Magharibi ambazo ni chachu ya muinuko wa bara la Asia unahitajiya kufungamana na turathi za dini ya Kiislam na mijadala ya amani na dini nyenginezo ili msukumo wa maendeleo ya kiilimu na kiuchumi uweze kusimama juu ya mafundisho ya kidini yenye kuzingatiya mahitajiyo ya kidunia, na kitengo cha akhlaki cha shirika la Umoja wa Mataifa la UNESCO.36 Zanzibar iliyopitiya misukosuko mikubwa mikubwa katika historiya yake ya karibuni ina nafasi kubwa ya kutowa mfano wa uongozi kwa nchi jirani na za mbali.

Kwa hakika katika ufunuo wa uvamizi wa Zanzibar wa tarehe 12 Januari 1964 limo zingatiyo kwa wenye kiu ya kuipatiya Zanzibar njiya mpya na muelekeyo mpya wa mustakbal wake. Ndoto ya Mwalimu Nyerere ya kuitupa Zanzibar katikati ya kisima cha Bahari ya Hindi imekuwa ni neema kwa Yusuf wa Zanzibar. Mapatano ya Wazanzibari ndani na nje ya Zanzibar ni jambo ambalo haliwezi kuzuwilika endapo wataliweka kando suala la uzawa kutoka mabara ya Afrika na Asia au visiwa vya Unguja na Pemba.

Mchango wa wazee wa mapinduzi ni changamoto nzito kwa uongozi na viongozi wa Tanganyika usiojali kujipa madaraka na ukubwa kwa kuitawala Zanzibar. Mapinduzi ya Afrabia ni mapinduzi ya kukataa kubaguliwa kwa misingi ya kutoka bara la Afrika au la Asia, Pemba au Unguja na ndiyo msingi pekee wa mashirikiyano ambao utaweza kuijenga Zanzibar ikawa almasi ndani ya taji la Afrabia.

Wenye kuyachezeya mapinduzi yenye kuwaunganisha na kukataa kubaguliwa kwa mujibu wa mabara ya Afrika au Asia na badala yake kuenziwa kwa mujibu wa mchango na utu na uraia wao wanazichezeya nguvu za uwakilishi wa umma ambazo hawana nguvu za kuzizuwiya. Hakuna tamaa kuwa maelezo yaliyomo ndani ya kitabu hichi yatayabadilisha mawazo ya wale waliojazwa na kujaa chuki dhidi ya Zanzibar au wale ambao hawako tayari kusamehe hata kama wako tayari kusahau. Max Planck alisema: “ukweli mpya wa kisayansi haushindi kwa kuwaridhisha wapinzani na kuwafanya wauone mwangaza, bali kwa sababu mwishowe wapinzani wake hujifiya, na kizazi kipya huinukiya na uzowefu wa ukweli mpya.”37

Na kizazi kipya chenye uwezo mkubwa wa kiilimu na upungufu wa ubinafsi kinahitajiya kuuonyesha umma faida zitakazoweza kupatikana kwa kuifuata njia mpya na mustakbal ambao hakuna atakayewajengeya isipokuwa wao wenyewe. Ikiwa mfumo wa njiya mpya ni wa kushinda katika mapinduzi mapya ya Zanzibar “idadi na nguvu ya hoja zenye kukinaisha na zitazouunga mkono mfumo huo utaongezeka.”38 Hoja moja ya kitabu kama hichi siyo itakayoweza kuleta mapinduzi mapya ya kifikra Zanzibar au kuukaribisha mustakbal mpya wa Waafrika na Waarabu. Mapinduzi yatakayoongozwa na walimu, wanasharia, wafanyabiashara, viongozi wa kidini, na mabingwa wa fani mbalimbali, ndiyo yatakayoweza kuleta mabadiliko yenye kuongozwa na hisia ya jamii moja ya Uzanzibari ambayo ina nguvu zaidi kuliko Uunguja, Upemba, Uafrika, Uwarabu, Ushirazi, Ukaskazini, Umakunduchi, na si mapinduzi ya mtu au kikundi cha watu au ya chama kimoja cha siasa.

Baada ya kupatikana mapinduzi yatakayowaunganisha Wazanzibari badala ya kuwagawa ndipo hatuwa ya pili ya kuendeleya kuujenga na kuulinda umoja na uhuru wa Zanzibar kwa kuziinua hali ngumu za kiuchumi za Wazanzibari wa makundi yote yenye utiifu kwa Zanzibar itakapofuatiliya. Na kufaulu kwa hatuwa ya pili hapana budi kuzitumiya ilimu za Wazanzibari waliyoko ndani na nje ili kuijenga nchi ya Zanzibar—almasi ya Afrika na ya dunia ndani ya taji la uhusiano mkongwe wa Waafrika na Waarabu.

Fikra ya Afrabia imesimama juu ya ukweli na ushahidi wa uhusiano mkongwe baina ya Waafrika na Waarabu ambao umeunganishwa na dini na thakafa ya Kiislamu. Afrabia inaondowa haja ya kuindeleza dhambi ya kuukaba uhuru wa Zanzibar na umoja wa Afrika. Ina uwezo wa kujenga mazingira mapya ya mustakbal wa Waislam Waafrika na Waislam wa Asia kwa kuutumiya umahiri wenye kujenga amani na neema kwa Waislam na kwa Wakristo. Afrabia itaweza kuwa mradi wenye kufaulu iwapo itaziunganisha nguvu za kifedha za Waarabu, rasilimali za watu na maliasili ya Afrika, na kuzitekeleza nguzo saba za hikma kutoka ustaarabu wa Magharibi. Zanzibar ina kila sifa za kujiandaa na kuweza kuutekeleza mkusanyiko wa fedha, rasilimali, na maadili na kuwa mfano wa kujivuniya wa Afrika Mashariki na nchi za Kiarabu.

Lakini hayo hayatokuja iwapo kuchezewa na kuchafuliwa kwa historia ya Zanzibar kutaendeleya kulifanya suala la muungano wenye kuyalinda mapinduzi ya Tanganyika ndiyo suala lenye kuwagawa Wazanzibari zaidi kuliko mapinduzi yenyewe yenye mkono mkubwa wa Tanganyika. Miafaka mitatu ilifeli kutokana na Wazanzibari kutoaminiyana wenyewe kwa wenyewe na kutokana na waasisi na warithi wa Tanganyika ambayo ilikuwa mshiriki mkuu wa mapinduzi na muungano wenye kuyalinda mapinduzi kuwa mpatanishaji mkuu.

Katika historia ya miaka 50 iliyopita hakuna aliyekuwa na uwezo wa kuwapatanisha Wazanzibari isipokuwa Wazanzibari wenye niya na vitendo vya kuaminiyana na kupendana. Mwenye Enzi Mungu amesema kuwa “Hatabadilisha hali ya watu mpaka wao wenyewe wabadilishe yaliomo ndani ya nafsi zao.”39 Na wa kubadilika si Waafrika tu bali na Waarabu wa bara la Afrika na la Asia pia wanatakiwa kuibadilisha mitizamo yao juu ya mapinduzi ya Zanzibar kutokana na upotoshaji uliyowakumba na wao piya. Waarabu wa Afrika na Waarabu wa Asia watakuwa na mchango mkubwa iwapo watavichanganya vitu viwili kwa faida yao ya leo na ya baadaye.

Jambo la kwanza ni mchango wa kiuwanachama wa Waarabu wa Afrika katika Jumuiya ya Afrika (Africa Union) na mchango wa kifedha kutoka Waarabu wa Asia katika kuigharimiya miradi itakayokuwa na faida kubwa na za muda mrefu kwa Waarabu na kwa Waafrika.40 Afrika ni bara lenye neema kuliko mabara yote duniani na linaweza kujileteya maendeleo makubwa sana bila ya kutegemeya siasa ya ombaomba na kuingiliwa kuendesha mambo yake kwa kulifuata zumari la kisiasa linalopigwa kutoka nje ya Afrika.

Jambo la pili ni kulichangamsha Gwaride la Zama Hizi (March to Modernity) ambalo msomi kutoka kisiwa cha Singapore, Profesa Kishore Mahbubani, amefahamisha kwa kuandika: “Hakuna njiya yoyote ile ya Gwaride la Zama Hizi litaweza kulifagiya Bara la Asia bila ya kuwaathiri Waasia bilioni moja ambao ni Waislam (Waislam milioni mbili tu ndiwo wenye kuishi Afrika Kaskazini na Ulaya).”41

Mahbubani hakuuweka mkazo wa Gwaride la Zama Hizi lenye chimbuko lake kutoka nchi za Magharibi kupitiya Japan, Korea ya Kusini, Singapore, Malaysia, India, Uchina, na Indonesia, kwa kulifananisha na majumba marefu yaliyojengwa Dubai peke yake. Anaendeleya Mahbubani na maneno haya:

Hadithi kubwa zaidi ni gwaride la zama hizi ni la ndani ya nafsi. Viongozi wakuu wenye kuiongoza Dubai ni viongozi wa kileo na waliyobobeya kama wengine wowote wale wa miji ya kimataifa. Lengo lao ni kuifanya Dubai na miji mengine ya Ghuba kuwa ni ya kileo. Ikiwa Dubai itafaulu, basi inaweza ikatowa mwangaza mpya wa tamaa katika ulimwengu wa Kiislam. Inaweza nchi za Magharibi wakayaunga mkono maendeleo ya namna hiyo—na wanaweza wasiyaunge mkono!42

Chuo Kikuu cha Yale cha Marekani kinatiliya mkazo na kuringiya mahusiyano yake na Uchina ambayo yanarudi nyuma mwaka 1854 alipokhitimu Yung Wing kutoka chuo hicho.43 Wakati wa utawala wa Sayyid Said bin Sultan, Zanzibar na Oman ziliandaa safari ya meli ya Sultana iliyopakiya mizigo ya zawadi kutoka Maskati na kuongeza mengine zaidi kutoka Zanzibar na kuwasili New York Alkhamisi tarehe 30 Aprili 1840.44

Wachina waliijuwa Afrika Mashariki na sehemu nyenginezo kutoka Waomani. Mwaka 1050 A.D. Sheikh Abdullah Al-Omani aliuingiya mdomo wa mto Pearl na akatupa nanga Whampoa na akaendeleya mpaka akafika Guangzhou. Anauliza Bingwa, Profesa E. Harper Johnson:

Nini ingelikuwa khatima ya Oman na mataifa mengine yaliyowekwa chini ya utawala wa Kireno na nchi nyengine zenye nguvu za Magharibi kama Uchina ingeliungana na Oman na nchi nyengine za Afrika na Mashariki ya Kati kwa lengo la kuitawala Ulaya? Hichi ni kitendawili kilichofunikwa ndani ya siri kwa vizazi vitakavyokuja baadaye kukiteguwa.45

Kizazi cha leo kutoka Zanzibar, Tanganyika, nchi nane zinazopakana na Tanzania, nchi za Magharibi na za Kiarabu, kina nafasi kubwa ya kuiongoza njiya iliyopitwa na safari ya meli ya Sultana ya Marekani au ya kabla yake ya Sheikh Abdulla Al-Omani ya Uchina, kulizinduwa Gwaride jipya la ilimu na la kiuchumi la Zama Hizi. Njia nzuri na yenye tija la muda mrefu ni kuwachaguwa na kuwaanda vijana wa Kiafrika na wa Kiarabu watakaoweza kupata nafasi za kusoma kwenye ngazi zote za vyuo vikuu vyenye sifa Ulaya na Marekani. Hawa ndiwo vijana watakaoweza kuzivunja kuta baina ya Waislam na Wakristo na baina ya Waafrika na Waarabu alizozizungumziya Rais Barack Obama wa Marekani na Profesa Ali A. Mazrui.

Kuta ndefu zenye kuwagawa Waafrika na Waarabu, Waislam na Wakristo, zinapaswa kuvunjwa kwa kuanzisha mfumo wa ilimu utakaowafundisha wanafunzi tamaduni za Kikristo zenye kutowa ilimu nzuri kuhusu Uislam kama zile za akina Johann Wolfgang von Goethe wa Ujerumani, Ralph Waldo Emerson wa Marekani, na Alexander Pushkin wa Urusi, nk.46 Pia wanafunzi wataweza kusoma kuhusu daraja kubwa anayopewa Yesu Kristo (Issa mtoto wa Bibi Maryam) katika Qur’an na historia ya mchango wa kiilimu katika Ustaarabu wa Kikristo wa nchi za Magharibi.Uhuru utakaoweza kuletwa na ilimu ya juu hauna budi uanze kuzipanda ngazi kutokeya ilimu ya chekecheya, ya chuoni, ya msingi, na ya sekondari. Ni mapinduzii ya ilimu peke yake yenye uwezo wa kumkombowa Muafrika na Mwarabu, Muislam na Mkristo, na kuwatowa kunako kwenye giza la upotoshaji na khadaa la mapinduzi ya Zanzibar na sababu zake.

Ufunguo wa historia iliyofichwa huenda pia ikautikisa msingi wa iliyokuwa Tanganyika, marafiki na majirani zake, na kwa karibu zaidi waasisi wakongwe wa vyama vya kisiasa wenye kuujuwa ukweli uliyofichwa ambao umeendeleya kuwanufaisha wao na warithi wao. Kizazi kipya, na wengi kati ya wazee, kimegubikwa na guo la khadaa na upotoshaji wa historia ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo kufunguliwa kwake huenda kukatowa mwangaza utakaoimurika njia mpya ya Shirikisho.

 

Maudhui na Mazingatio

Mpaka hapa tulipofika, na kutoka na simulizi za wazee za kabla yake, inadhihirika kwamba Wazanzibari kwa ujumla walipandiya tu kwa kujigamba kama walikuwemo katika mapinduzi wakati hawakuwemo ndani ya jiko la mapinduzi au ndani ya usiku wa mapinduzi. Hata Mzee Karume alishirikishwa kwa sababu alikuwa ni kiongozi mwenye kuungwa mkono na wafuasi wengi wa ASP lakini si kama alikuwa Jemedari wa mapinduzi ya Zanzibar kama inavyotangaziwa. Na wengine kutoka pande zote za ASP na Makomred ingawaje baadhi yao walishirikishwa kijuujuu tu bila kuujuwa undani wa matayarisho ya mapinduzi yenyewe. Na khasa wale wenye asili ya Kizanzibari yenye kwenda nyuma kwa daraja nyingi ndiyo kabisa waliwekwa kando.

Kwa ufupi, Mapinduzi ya Zanzibar yalifanywa na wageni kwa lengo la kuwadhibiti wenyeji (Wazanzibari) pamoja na nchi yao. Hii inauthibitisha ule msemo wa Nyerere “Hayo ndio maumbile ya uhuru; lazima upiganiwe na ulindwe na wenye hamu nao. Uhuru wenye kupiganiwa na watu wa nje unakwenda kwa watu wa nje.” Kutokana na maelezo yote yaliyopita ionekanavyo humu kitabuni, ingefaa viongozi wa aina zote na wasomi wa kitabu wakajiuliza masuala matatu yafuatayo ili kusawazisha hali ya mambo kutokana na khadaa zilizotendeka ili papatikane kuaminiyana tena baina ya Wazanzibari na baina ya Wazanzibari na Watanganyika kwa maslahi ya nchi na vizazi vijavyo.

1. Siasa ya Pan-Africanism yenye kusema kuwa Zanzibar ni ya Waafrika wenye asili ya kutoka bara la Afrika peke yake na si ya Wazanzibari kutoka mabara mengine ni siasa ya kibaguzi na kikaburu yenye kuongozwa na kikundi cha viongozi wachache waasisi na wafuasi wao.

2. Wakati umefika kwa Tanganyika na dunia kuukubali ukweli kuwa Zanzibar ni ya Wazanzibari wote na si mali asili ya Tanganyika na kutambuwa kuwa Umoja wa Afrika hautoweza kufikiwa ikiwa Muungano pekee barani Afrika baina ya Tanganyika na Zanzibar hautopata suluhisho la kudumu.

3. Licha ya mahitajio ya kuufahamu ukweli wa “Mapinduzi”, Wazanzibari walionyanganywa nchi yao na waliodhulumiwa kwa hali, mali au mali asili, au kifo, watakuwa na madai gani ya kikanuni za kimataifa dhidi ya kikundi cha watu wachache na ushawishi wao mkubwa ndani ya taasisi wanazozimiliki na kuziongoza?

Mabadiliko ya mfumo uliozoweleka kwa muda mrefu kunaweza kusambaza khofu kongwe ya kuiona Zanzibar ikiinuka. Tutarajiye sana upinzani mkali kutoka Tanganyika na khasa kutoka kwa jumuiya zisizo za Kiserikali (NGOs) ambazo zimekuwa mstari wa mbele kueneza propaganda chafu dhidi ya Wazanzibari na Waarabu—Waislamu kwa jumla. Kwa mujibu wa mwandishi Mohammed Ghassany “Watafanya kila hila na kila mbinu. Watatupa tabu sana na njia pekee ni kuuilimisha umma na wale ambao wameshatiwa sumu dhidi ya Waarabu na biashara ya utumwa peke yao.”47

Wajanja na wenye kukhadaa wanapenda sana kutumiya mbinu za kuhamakisha, kutiya hisiya ya kudhulumu, kuonyesha hatari kubwa itakayowakabili wasiyotaka kuwafuata, na hujivalisha guo la utukufu, ili kuulinda ujanja na khofu zao. Kwa vile ni binaadamu wenye khofu ya kuogopa kujulikana huanza kuwatiya khofu na kuwaondoleya hoja wale wenye kutaka kuwadhibiti na kuwatawala kimawazo na kimabavu. Wanaposhindwa kupata muradi wao hujaribu kujifanya wamehamaki na wamekereka. Wakishindwa hubabaika na wakawa hawana raha na kuanza kutishiya. Wanapoona tayari kushindwa huanza kukata tamaa na kuingiwa na dhiki ya moyo. Saikolojiya yao inafuata mwenendo na vituo maalumu.48

 

Faida za Mapinduzi ya Afrabia

Nchi ya Oman inajenga bandari ambayo ni ya tatu kwa ukubwa duniani na inaweza ikaingiya ubia na bandari mpya yenye sifa ya kimataifa ya Zanzibar au bandari mpya za Tanganyika. Watalii wanaotembeleya Oman au UAE, au sehemu nyengine za Asia wanaweza kuendeleya na safari zao na kuzizuru mbuga za wanyama za Tanganyika, Kenya, nk.

Katika faida nyenginezo, hakuna watu wengi wenye kusema lugha ya Kiswahili nje ya Tanzania kama nchi ya Oman na hakuna watu wengi wenye asili ya Kiomani nje ya Oman kama Afrika Mashariki. Wananchi wa Oman kwa upande wao wanaweza kuleta mabadiliko kwa kutoogopa kuutumiya Uswahili au Uafrika wao. Vipindi va televisheni vya Kiomani juu ya Afrika Mashariki vimeleta muamko mkubwa kwa Waomani ambao wakiisikiya tu Afrika Mashariki. Waomani wengi wa Oman ya leo huenda wakawa wameyasikiya mapinduzi ya Zanzibar au wamezisoma habari zake lakini hawakuyashuhudiya mapinduzi au athari zake. Kwa hiyo uwezekano mkubwa wa kuyaondowa machungu na khasara upo.

Ndani ya muda mfupi Zanzibar na Tanganyika pamoja na Msumbiji na Oman, na UAE, au Qatar, zinaweza zikapiga hatuwa kubwa kwa kutumiya rasilmali kidogo za kifedha. Fikiriya utajiri wa mahusiyano ya kihistoria, kithakafa, na kilugha baina ya sehemu mbili hizi za duniya. Fikiriya Zanzibar na Tanganyika zisinunuwe kutoka nchi nyingine yoyote ile duniani nini Oman na UAE zinaweza kuuza, na Oman na UAE zisinunuwe kutoka nchi yoyote nyengine nini Zanzibar na Tanganyika zinaweza kuuza. Fikiriya mashindano ya mpira wa miguu yenye kujenga urafiki na udugu baina ya vijana waliyo chini ya umri wa miaka 15 baina ya pande mbili za uhusiyano mkongwe wa Afrabia.

Zanzibar na Tanganyika zinaweza kununuwa mafuta ya petroli, kubadilishana utaalamu na Oman na UAE kuendeleza viwanda vyake vya petroli na gesi. Oman au UAE zinaweza zikafunguwa vituo vya petroli Zanzibar na Tanganyika kwa kushirikiyana na wafanyabiashara wenzao. Zanzibar na Tanganyika zinaweza zikamiliki pamoja na Oman au UAE meli na ndege kubwa za kubebeya mizigo ambazo zinaweza kufika mpaka Kongo. Oman na/au UAE inaweza ikazinunuwa karafuu za Zanzibar na kuzisafirisha ndani ya vyombo vya bahari vinavomilikiwa na Wazanzibari na Waomani.

Inasemekena marehemu Abdulrahman Babu alikuwa na miradi mitatu ambayo alivinjari kuiweka sawa lakini Nyerere aliikataa. Mradi wa kwanza ulikuwa ni mradi wa kiwanda cha mafuta ya chikichi (palm oil) alichotaka kukianzisha Kigoma ambapo Majapani walikuwa waugeuze ukanda wote wa eneo lenye kulizunguka Ziwa Tanganyika kuwa ni la chikichi na viwanda vya mafuta. Wajapani wangelijenga njiya za mabomba mpaka Dar es Salaam kwa ajili ya kuyasafirisha mafuta. Mradi wa pili wa Babu ulikuwa ni kujenga miji midogomidogo ambayo ndiyo ingelikuwa ni vituo vya kibiashara khususan kutoka vijijini ambapo WaCuba walikwishatuma hata watu wao kwa matayarisho ya uchoraji na usanifu wake. Mradi mwengine na wa tatu ulikuwa Rufiji Basin Development wa kilimo na khasa cha mpunga. Alikwisha kagua nyumba ya kununuwa ambayo ndiyo ilikuwa ikiendeleya kujengwa, lengo lake likiwa ni kufunguwa ofisi (NGO) ya masuala ya kijamii lakini akafariki dunia mwaka 1996.

Ni vigumu kuweza kutoka kwenye mapinduzi ya kuumaliza mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar kuelekeya kunako mapinduzi ya kiuchumi wakati jina la “Serikali ya Mapinduzi” haliashirii utulivu na usalama wa nchi au rasilmali za wawekezaji khasa kwa uchumi ambao hautegemei sana sekta ya utalii. Dunia nzima hakuna nchi yenye kuitwa “Serikali ya Mapinduzi.” Wasiwasi wa mwandishi huyu ni kuwa wenye kufaidika khasa na jina hilo ni wale waliyohusika na mapinduzi ya Zanzibar kwa sababu kisaikolojiya Zanzibar maisha inakuwemo kunako hali ya kupinduwana na kuwapoteza waekezaji makini. Zanzibar kabla na baada ya uvamizi wa Tanganyika ilikuwa na jina ambalo ndilo jina la nchi kama ilivyokuwa ikijulikana Umoja wa Mataifa.

Advertisements

One Response

  1. NOELL says:

    MIMI NAITWA NOELL NIPO MAGOMENI NAOMBA MNITUMIE HISTORY YA MWALIMU NYERERE ENZI ZA UKOLONI MPAKA UHURU. NAPENDA SANA.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: