Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!

Icon

Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia

Mlango wa Ishirini na Moja: Nyumba ya Afrabia

…Lakini huenda mkachukia kitu nacho ni kheri kwenu. Na huenda mkapenda kitu nacho ni shari kwenu. Na Mwenyezi Mungu anajua na nyinyi hamjui. —Qur’ani 2:216

Tanzania haiwezi kwenda na wakati na Tanganyika isiende na wakati huo huo pia. —Julius K. Nyerere

Hakuna asiyefahamu kuwa Wazanzibari ni watu waliochanganya damu sana na wanatoka kwenye makabila yenye asili tafauti ima kwa uzawa au kwa ndoa, kabla na baada ya mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964. Ni bahati mbaya kwamba kuchanganya damu kwao huko hakukuwasaidiya pale walipoingiliwa na kuchanganywa na siasa za kuupinga ukoloni na kudai uhuru wao, na matokeo yake wakaathiriwa na fitina na chuki za kikabila zilizojengwa na kushamiri khasa ndani ya kipindi cha ukoloni kutoka madola makubwa ya Magharibi.

Waafrika na Waarabu, wakiungwa mkono na Wazanzibari wa makabila mengine wakiwemo Washirazi ambao ndiyo waliyo wengi Zanzibar, wote, walitawaliwa na mirengo ya kizalendo iliyoshadidiya kwa siri au kwa dhahiri misingi ya kikabila ambayo iliwagawa badala ya kuwaunganisha. Hata Uislam, dini ya takriban asilimia 99% ya Wazanzibari, ambao hautambuwi mipaka ya uzawa wala ya ukabila haukuweza kuwasaidiya Waislamu waliotawaliwa na kuzongwa kifikra na siasa chafu ya wakoloni ya “Wagawe Uwatawale”.

Lakini ukichunguza kwa undani utakuta ni wachache tu kati ya watu wa koo zilizochanganya damu Zanzibar waliyomo katika vurugu za hapa na pale katika siasa mambo leo. Ukipeleleza utawakuta wengi wanaoendeleza malumbano ya siasa za chuki na khasama hawana mchanganyiko huu wa damu na wa ndoa baina ya watu wenye asili za Kiafrika na Kiarabu.

Tukifanya uchunguzi mdogo tu wa familia moja moja utakuta Zanzibar ya jana si ya leo. Kukhasimiyana na kuuwana Wazanzibari wenyewe kwa wenyewe wakati kila mmoja takriban amemhusu mwengine au ameowana naye ni jambo lisiloelezeka kirahisi bila ya kuufahamu upotoshaji wa ukweli wa mapinduzi ya Zanzibar. Mlolongo ni mrefu na hautokwisha tukiuendeleza ndani ya kitabu hichi na itabidi kikosee kwa kutowataja wengine ambao watahisi nimewadharau au sikuwajali uzawa wao kabla na baada ya mapinduzi. Mfano mmoja ninaoutowa utosheleze kuthibitisha hoja ninayoijenga.

Saeed Al Battashy amezaliwa karibuni na ana umri mdogo wa miaka minne leo na ni mzaliwa wa Uingereza sehemu za East London. Mtoto mdogo huyu pia ni Banyani na kizazi chake wameishi na kutumika kwenye kasri ya Sultan wa Zanzibar kabla ya mapinduzi.1 Wengi katika ukoo wa kifalme wa Zanzibar wana asili za Kiomani, Kitumbatu, Kiganda, Kinyasa, Kingazija, Kiethiopia, Kimsumbiji na makabila mengi mengineyo ya Kiafrika kutoka bara ambayo ni vigumu kuyajuwa. Babu yake Saeed Al Battashy amewahi kuwa Rais wa Zanzibar kwa miaka mingi baada ya mapinduzi. Kati ya mengi, mjukuu huyu ana babu aliyewahi kushtakiwa kwa kosa la kumuuwa marehemu Rais Abeid Amani Karume mwaka 1972 na akahukumiwa kifo. Kama ilivyo kwa Saeed Al Battashy aliyeko Uingereza hivi leo, ndivyo walivyo babu zake wote hawa, Mungu awarehemu waliokufa na awape umri mrefu walio hai. Hivi karibuni tu babu yake mmoja alizinduwa kitabu Zanzibar kuhusu maisha yake na siasa za Zanzibar kiitwacho Ukabila, Mapinduzi, na Harakati za Kupiganiya Haki za Binaadamu Zanzibar: Kumbukumbu za Maisha ya Ali Sultan Issa na Seif Sharif Hamad.

Watoto wa khaloo yake (mama mdogo) Saeed Al Battashy ni wajukuu wa Rais Karume kutoka mmoja kati ya watoto wa marehemu Rais Abeid Amani Karume. Mzee Karume alishazaa watoto wawili wa kiume ambao wana damu za mchanganyiko kabla ya tarehe 12 Januari, 1964. Nimemchagua kijana huyu Saeed Al Battashy kama ni kigezo cha mahusiyano ya Afrabia yalivyo kwa nchi ndogo kieneo na masikini kiuchumi lakini kubwa kisiasa na tajiri kwa historia na uzawa wa raia zake.

Leo hii watoto, wala si wajukuu, wa marehemu Brigedia Yusuf Himid, mwanamapinduzi aliyetajwa sana ndani ya kitabu hichi ni Waafrabia na ni wajukuu wa marehemu Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani, kupitiya muasisi wa siasa ya uzalendo wa Kizanzibari, marehemu Bwana Mohamed Salim “Jinja” ambaye alisoma Chuo Kikuu cha Oxford (1944–48). Watoto wa marehemu Mzee Yusuf Himid wana damu za ki-Al-Busaidi na wametokana na ukoo wa Awlad Hemed bin Said ambao ndiyo wafalme wa karne na karne na watawala wa eneo lote kuanziya pwani ya Somalia kushuka chini kwenye ukanda wa Pwani wa Afrika Mashariki.

Rais wa hivi sasa wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Amani Abeid Karume ana damu ya Kihindi kabla hata ya Mapinduzi ya 1964 na watoto wake wote aliyozaa wana damu ya Kisomali na Kiarabu tena wakiwa katika mizizi ya utawala tokea enzi na enzi za nchi ya Zanzibar. Hii ndiyo Afrabia. Ni wajukuu wa mwanzilishi wa vuguvugu la siasa za kizalendo za kujigombowa kutokana na fedheha ya kutawaliwa na kudai uhuru, na msomi wa kusifika na mwandishi wa kutajika, marehemu Sheikh Mohamed Salim Al-Barwani (maarufu “Jinja”). Hawa ndio watoto wa Rais Amani Abeid Karume.

Mmoja wa Manaibu Waziri katika Serikali ya sasa Zanzibar anafuata madhehebu ya Kiismailiya yanayoongozwa na Aga Khan. Daktari mmoja maarufu nchini Oman ana mtoto wa kuzaa na marehemu Mzee Abeid Amani Karume na kati ya ndugu zake kwa baba, mmoja ameolewa na aliyepata kuwa mgombea nafasi ya makamo wa Rais kupitiya chama cha upinzani cha CUF ambaye ana asili ya Kishirazi (Kiirani).

Kabla mapinduzi ya 1964 kufanyika Rais Aboud Jumbe Mwinyi watoto wake aliwazaa na bibi wa kabila ya Al-Kindy ambaye mwaka huu amefariki akiwa na umri wa miaka 103. Watoto wake wakubwa kabla mapinduzi ya 1964 wote wana babu mzaa mama akiwa ni Sheikh Abdullah Al-Kindy.

Bibi Moza bint Khalfan Al-Barwani, bibi yake aliyekuwa kiongozi wa Zanzibar Nationalist Party (ZNP au “Hizbu”, neno la Kiarabu ambalo maana yake kwa Kiswahili ni “Chama”), marehemu Sheikh Ali Muhsin, amekhusiana na Wamakonde. Babu wa Kimakonde wa babu yake Sheikh Ali Muhsin wa upande wa kwa mama, Sheikh Nassor bin Issa Al-Barwani, ambaye ni Chifu Mwanya wa Wamakonde ndiye aliyeitowa ardhi ya mji wa Mgao Mwanya ambayo ndiyo iliyouasisi mji wa Lindi.2 Tukichunguza tutakuta ni watu wachache sana waliyoko Zanzibar ambao hawana mtiririko wa aina hii kati ya watawala, wanasiasa na hata raia wa leo au kabla ya mapinduzi.

Itakubidi uchambuwe koo nyingi na historia za mtiririko wake, utafute nani hawakukhusiyana toka ntoke na watu wa asili za makabila tafauti iwe kwa uzawa au ndoa. Na hili si la baada ya mapinduzi bali ni la kutokeya karne na karne, dahari na miaka. Koo hizi ukizifuatiliya utazikuta damu zilizojikita khasa ni za Kiarabu na za Kiafrika na haya hayakuanziya hivi karibuni bali ni muendelezo wa maingiliyano ya jamii mbali mbali karne kwa karne.

Hakuna buku kubwa kama buku lililoandikwa na viini vya uzazi vya DNA ambavyo vimo ndani ya kila kiwiliwili cha binaadamu. Mimi ni Muafrabia wa uzawa, ndowa, thakafa na imani. Baba yangu mzazi, marehemu Bwana Mohammed Abdalla Mohamed Ghassany (maarufu “Bingwa”) amezaliwa na baba mwenye kabila ya Kiarabu ya Al Ghassani na mama yake ni Bibi Sarah bint Ahmed bin Muhammed Al Barwani Awlad Hijji ambaye alizaliwa Kongo, Kisangani. Bibi yake marehemu baba yangu mzaa baba, Bibi Zuhura bint Mfaume, ni Mwera wa Lindi, kusini ya Tanzania. Bibi yake baba yangu mzaa baba ni Bibi Mwajuwaye bint Tambwe Waminakule, kutoka kabila la Kimanyema la Wabwuywe. Marehemu mama yangu, Bibi Asya bint Abdalla Al-Jahdhami na bibi yangu mzaa mama ni Bibi Neyu bint Hemed bin Muhammed bin Hemed bin Said Al-Busaidi (Awlad Hemed).

Matokeo ya vipimo va DNA vinathibitisha kuwa upande wangu wa baba unatokana na Haplogroup J1e (+L147). Kundi hili linarudi nyuma miaka 10,000 kwenye historia ya viini vya Y-chromosome na asili ya kundi hili inatokana na sehemu ambayo leo inajulikana kuwa ni Iraq au ile sehemu baina ya mito miwili ya Tigris na Euphrates.

Kabla ya hapo kundi la M267 liliondokeya kaskazini ya Afrika Mashariki kiasi ya miaka 60,000 nyuma. Kundi la J1 M267 ni kundi liloanzisha mapinduzi ya kilimo katika kipindi kinachojulikana kwa jina la “Neolithic.” Kuna waliyoelekeya Afrika ya Kaskazini, na wapo waliyoelekeya Arabuni na Ethiopia. Wengine wakaelekeya sehemu ya Bahari ya Mediterranean na walomalizikiya Europe wengi wao ni Mayahudi wa Ashkenaz. Kutokana na matokeyo ya utafiti wa mtDNA, kundi la upande wa marehemu mama yangu, Haplogroup L3, liliondoka Afrika inapata miaka 80,000 elfu nyuma kuliko kundi la marehemu baba yangu.

Haya yote yanathibitisha kitu kimoja nacho ni kama tunavyofahamishwa na dini zote kuwa binaadamu wote asili zao ni moja na wote wanatokana na Adam na Hawa na asili ya binaadamu wote ni Afrika. Ametuambiya Bwana Mtume Muhammad (SAW) kuwa hakuna aliye bora baina ya Mwarabu na Muajemi. Ametufundisha Nabii Issa (Sala na salamu za Mwenye Enzi Mungu zimteremkiye), kuwa wafanyie watu yale ambayo wewe utapenda wakufanyie.

Zanzibar ni mfano mzuri wa kuzitambuwa, kuziheshimu na kuzisherehekeya asili za binaadamu wote na zuka la mustakbali wake litaletwa na watu wa kawaida waliyotoka nje ya pango la upotoshaji na kupitiya wao kupatikana uongozi unaotokana na mchanganyiko wa uzawa ambao una nguvu zaidi kuliko zile za Kiafrika au za Kiarabu—nguvu za umoja, nguvu za Afrabia.

Mfano mzuri wakati wa Mapinduzi ni ule wa urafiki na ubinaadamu baina ya Mmakonde Bwana Yohana (Sadiki) Ntanga na Bwana Abdallah Majid Al-Siyabi, Mzanzibari mwenye asili ya Kiarabu kutoka Nizwa, Oman. Watu hawa wawili waliishi kwa urafiki na mafahamiyano mazuri kabla ya mapinduzi na wakati wa mapinduzi Bwana Yohana alimchukuwa na kwenda kumficha rafiki yake Bwana Abdalla ambaye alikuwa akitafutwa na wanamapinduzi. Inasemekana kuwa wakati wa siasa za chuki baadhi wafuasi wa ZNP waliwazuwiliya wafuasi wa ASP kulima au kuteka maji kwenye visima vyao, lakini Bwana Abdalla hakufanya hivyo na alimuachiya Bwana Yohana kufanya shughuli zake kama kawaida.

Ulipofika wakati wa Mapinduzi Bwana Yohana akamchukuwa Bwana Abdalla na kwenda kumficha uwandani sehemu za Tunguu. Bwana Abdalla alikuwa ameficha fedha zake mahala fulani na akamuelekeza Bwana Yohana wapi zilipo mpaka hali ilipotuliya. Alipoondoka kwenda Oman, Bwana Abdalla alimkabidhi Bwana Yohana kwa maandishi na mbele ya viongozi wa serikali vikataa vya shamba la minazi pamoja na nyumba mpaka atakaporudi mwenyewe kutoka Oman. Mwaka 1999 Sheha kwa ushirikiyano na Polisi wa Fuoni na Katibu wa Wilaya ya Kati walitaka kumnyanganya Bwana Ntanga hivyo vikataa na nyumba.

Kwa kifupi, marafiki wawili hawa walisimama pamoja na Bwana Abdalla akampelekeya mualiko Bwana Yohana ende Oman akatembee lakini safari hiyo haikujaaliwa kuwa.3

Kwa upande mwengine, utakuta pia kuna familia zenye majina nusu ya Kikristo na Kiislamu na hili kwa Zanzibar halishangazi hata kidogo. Hivi leo ukenda sehemu za Kisauni kuelekeya barabara mpya ya Fumba pana sehemu inaitwa “Msikiti na Kanisa” na tayari limeshakuwa jina la mtaa huo. Sababu yake ni msikiti uliyopo ukuta kwa ukuta na kanisa na mote humo mnasaliwa wala waumini hawagombani. Ni pa kutolewa mfano lakini hukutii vyombo vya habari vya Zanzibar kulikuza hili kwani kwa Zanzibar ni jambo la kawaida tu. Ndivyo historia ilivyoijenga Zanzibar na ndivyo ilivyo hadi leo. Na mfano mwengine wa kale ni ile minara miwili, wa kanisa na wa msikiti iliyopo Mkunazini katika kisiwa cha Unguja.

Kujenga mshikamano madhubuti baina ya Waislamu wa Afrika Mashariki na Kati utategemeya kuwakusanya na kuzinyanyuwa hali za Waislam kiilimu, kiuchumi na kijamii katika kupiganiya haki zao sawasawa na raia wengine katika nchi hizo. Ni muhimu pia kwa Waislam kuwa na mahusiano mazuri na waumini wa dini nyingine na kuondowa chanzo kikubwa cha fitina na uadui ambacho ni suala la utumwa lililojengwa juu ya misingi ya ujinga bila ya uthibitisho wenye kulindwa na ushahidi madhubuti. Kosa kubwa la Zanzibar ilipokuwa inadai uhuru wake na wakati inadai haki zake kama ni nchi ni kulipuuza suala la utumwa ambalo ndilo lililowafitinisha na linalotumiwa kama ni kisingiziyo kikubwa cha kubomolewa Dola ya Zanzibar na kuogopwa kurejea tena.

Mtizamo uliyojikombowa kutokana na upotoshaji wa suala la utumwa wa Afrika Mashariki una uwezo wa kuwaondoleya ukhasama Waislam na Wakristo. Nchi za Kikristo na za Kiisilamu zina nafasi ya kufanya ukarimu wa kuwaleteya Waafrika Wakristo na Waislam maendeleo yatayojengeka juu ya msingi wa kuhishimiana na wa kutafuta maslahi ya pamoja. Kuwatakiya maendeleo waumini wa dini fulani na kuwazuwiliya waumini wa dini nyengine maendeleo si dalili ya kumtakiya mwenziyo mema unayojitakiya mwenyewe.

Ukombozi wa Zanzibar haumo kwenye kujenga hamaki dhidi ya mazingira ya khadaa, njama na hila, bali umo ndani ya umoja unaosimama baada ya kulivuwa guo la buibui lililolifunika pango la upotoshaji wa historia. Tuondoe mabuibui tuukumbatiye umoja. Jambo muhimu na la kwanza kuliko yote ni kuusimamisha msamaha ndani ya jamii ya Kizanzibari kupitiya ukweli na pengine hata kusoma dua nchi nzima kuiombeya Zanzibar na Tanganyika maghfira na mazingira ya haraka ya mustakbal mwema.

Msamaha kupitiya ukweli haina maana ya kufukuwa majeraha ya historia. Maafa yaliyoikumba Zanzibar si ya kubuni bali ni mambo ambayo yametokeya na yameshuhudiwa. Utumwa ulifanyika Zanzibar, Tanganyika, na kote Afrika Mashariki na Kati, na hakuna haja ya kujiroweka ndani ya uwongo wa hadithi za kubuni za utumwa na kuwa uokovu wa Yesu Kristo ndiwo uliyomkomboa mwana wa Afrika kutoka uovu wa utumwa wa “wageni” wakikusudiwa Waarabu na Waislam. Waliyoipinduwa Zanzibar hawakuwa vijukuu wala virembwe vya watumwa na hakuna ushahidi wowote ule kuwa wapinduzi na wapinduliwa walikuwa na uhusiano wowote ule na utumwa uliofanyika Zanzibar. Ukweli ni kuwa nyuma ya propaganda hakuna kuwachukiya Waarabu au kuwapenda Waafrika bali kuna maslaha ya kisiasa na ya kiuchumi yenye mtizamo na upeo wenye kuona mbali sana.

Kwa hiyo si lengo la kitabu hichi kutonesha vidonda na kufukuwa majeraha ya historia. Wala si lengo lake kuamsha hisia za chuki na khasama kati ya watenda na watendewa. Maana tukiichunguza kwa makini historia ya Zanzibar, sote ni watenda na watendewa kwa nyakati tafauti. Tulipoacha kuukubali na kuusherehekeya mchanganyiko wa kipekee unaounda jamii yetu, sote tulikosa. Huu si wakati wa kutazama nyuma. Tuangaze mbele kwenye mustakbal unaotuunganisha tena na kwa pamoja tusimamiye maslahi ya nchi tuipendayo—Zanzibar na Tanganyika. Tukiwa na mtazamo wa aina hiyo, tutangunduwa kuwa hakuna haja ya kukataana na kutaka kutimuwana, tutagunduwa kuwa pamoja na udogo wake kieneo, Zanzibar ina nafasi ya kutosha kutuingiza sote. Kama ilivyokuwa hakuna haja ya watawala wa Watanganyika kuwa na khofu juu ya Zanzibar na Wazanzibari hawana haja ya kuhuzunika kwa yaliowafika. Zanzibar ina kila sababu ya kuziteteya haki zake ndani ya muungano bila ya Tanganyika kuhamaki na kuwaona Wazanzibari kuwa ni watu matata.

Zanzibar inahitajiya mtizamo na mfumo mpya kabisa wa mahusiano yake na Tanganyika lakini usiwe mfumo uliojengwa na uadui au khofu ya Zanzibar kuuvunja Muungano unaotawaliwa na Tanganyika. Wakati umefika wa kuanza kuzijenga fikra mpya Zanzibar na Tanganyika. Kwa mfano, pafanyike mabadiliko ya Katiba ili Urais wa Muungano uwe kwa mzunguko kikatiba baina ya nchi shiriki za Tanganyika na Zanzibar badala ya kufuata utaratibu usiyokuwa na dhamana au unaotegemeya dhana ya “wengi wape.” Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Muungano anaweza akawa Kikatiba anatoka Zanzibar. Jeshi linaweza likawa ni la Muungano lakini ulinzi wa ndani wa Zanzibar ukawa ni wa Wazanzibari. Zanzibar inaweza ikajiunga na Taasisi za Kimataifa ambazo zitakuwa na maslahi makubwa ya kiuchumi kwa Zanzibar na Tanganyika, na kadhalika.

Juhudi maalumu zinaweza zikachukuliwa kuvifuta vitabu vyenye kuendeleza chuki na fitina baina ya Wazanzibari, baina ya Wazanzibari na Watanganyika, na baina ya Waislamu na Wakristo, kwa kutunga vitabu na vipindi vya redio na televisheni ambavyo vitaielekeza jamii kunako ukweli na msamaha. Dola ya Zanzibar inaweza ikaanzisha mfuko maalumu utakaochangiwa na jamii ya kimataifa na utakaokuwa na lengo la kuzipoza nyoyo za Wazanzibari waliofikwa na maafa tafauti. Zanzibar ni lulu ndani ya taji la Afrabia juu ya kichwa cha bara tajiri kuliko yote na la mwangaza—Afrika.

Ametahadharisha Bwana Muyaka bin Haji Al-Ghassani pale aliposema:

Kimya kina mshindo mkuu, ndivyo wambavyo wavyele

Kimya chataka k’umbuu, viunoni mtatile

Kimya msikidharau, nami sikidharawile

Kimya kina mambo mbele, tahadharini na kimya

Kimya ni kinga kizushi, kuzukiya walewale

Kimya kitazua moshi, mato musiyafumbule

Kimya kina mshawishi, kwa daima na milele

Kimya kina mambo mbele, tahadharini na kimya

Kimya vuani maozi, vuani mato muole

Kimya kitangusha mwazi, mwendako msijikule

Kimya chatunda p’umzi, kiumbizi kiumbile

Kimya kina mambo mbele, tahadharini na kimya

Na amesema mpigania haki za watu weusi Marekani, Dk. Martin Luther King Jr.: “Si mabavu ya wachache yenye kunitisha mimi, bali ukimya wa walio wengi.”

Ewe Mola Wetu! Tuingize kunako mlango wa ukweli wenye kuiwekeya Zanzibar na Tanganyika hishima duniani na tutowe kunako pango la upotoshaji wa historia kupitiya mlango wa ukweli na hishima. Tupandishe ngazi itakayotuzidishiya ilimu na kutuondoleya umasikini wa ujinga na ujinga wa umasikini na tupe uwezo wa kuzitambuwa dhamira za maisha yetu duniani zitakazokuridhisha Wewe na utupe furaha za kuzikamilisha. Wewe Ndiye Mwenye Kutulinda na Wewe Ndiye Mwenye Majeshi Yasiyoshindwa!

Mungu Ibariki:

Zanzibar Mpya

Tanzania Mpya

Afrabia Mpya

AMIN

Advertisements

2 Responses

 1. Ahsante kwa ujumbe wako, ambao umenifanya nitokwe na machozi. Sio kwasababu umenitonesha kidonda ,laa hasha. Nimekua na chuki juu ya chama tawala ccm na viongozi wake na hata kuwachukia Watanganyika na baadhi ya wa unguja walioisaliti Taifa la Zanzibar.

  Baada ya kusoma kidogo tu ujumbe wako huu nimefunguka macho,imani na kuosheka moyo wangu, na kuyasahau yaliopita kama unavo tusisitiza. Bila ya kuendeleza chuki hizi za Utanganyika na U CCM, lilobakia ni kudumisha Umoja wetu na amani ambayo tokea mwanzo ndio jambo nililokua naliomba kwa kila sala.

  What can i say, …..litreture ???? its you have given our old swahili peon & litreture . Ujumbe wako wa misemo hii inanikumbusha Marehemu( Mpuu wagu,yaani bibi wa mama yangu …kule Pemba in 1972, alipokua akikaa na ukili wake ) . Alikua mara nyingi akitumia maneno haya ya kiswahili cha ndani kabisa.

  Ni vigumu vijana walo kuyafahamu unani wake. Lakini mimi nayaelewa wazi na yana uzit na ma-ana nyeti ndani yake.Sina budi ila kusambaza ujmbe huu kwa ndugu na jamaa in Zanzibar.

  Nitaendelea kumaliza ku-usoma ujumbe huu na ku-save kwenye USB. ASW akuzidishi kheri na baraka ili tuunganishe zanzibar yetu na vizazi vijavyo. Mola ibariki Zanzibar na watu wake Amen.

 2. YUSUPH KIJOLE says:

  Nimesoma habari hii ukweli mie asili yangu ni bara lakini ulichoandika hapa nimekuelewa vizuri, ukweli tunatakiwa tushikamane na endapo kuna mapungufu basi tufuate taratibu kurekebisha bila jazba.Mimi ni muislam naamini ndugu yangu ni muislam yoyote ulimwenguni sioni sababu ya kumchukia mtu kwa sababu za kilimwengu wengi wetu tuna ndugu zanzibar na Bara hivyo kuwachukia wenzetu itakuwa si vizuri.Chamsingi ni sisi wenyewe kuchangua viongozi ambao wataendeleza maslahi ya Zanzibar na Tanzania kwa jumla bila kutubangua.Mola akujaalie afya njema na maisha marefu.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: