Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!

Icon

Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia

Mlango wa Kumi: Makomred na “Mungu wa Waafrika”

Walikuwa ni wasoshalisti wa mrengo wa kushoto, ndio, lakini kikundi kidogo na kibanzi cha kikundi kidogo. Wangeliweza kutomaza sera za mrengo wa kushoto lakini isingelisababisha Vita Baridi. Kilichofanya wajiambatanishe na Mashariki ni kule kukataa kwa nchi za Magharibi kuitambuwa Zanzibar. —Julius K. Nyerere

 

Mzee Ramadhani

Kwanza nilimkabili huyu Khamisi Darwish. Nilimwendea nikenda muuliza. Bwana wewe, nataka nkuulize. Hawa Komred kweli nambari moja kunako mapinduzi? Akanambia, bwana Komred si nambari moja. Nikamuuliza kwa nini wasiwe namba moja? Mbona kuna uvumi kuwa hawa ndo nambari moja? Akasema “si kweli.” Ingelikuwa namba moja hii siri ingelivuja, ingekuwa si siri tena hiyo. Isingekuwa siri tena. Mbona hili suala limeshakuwa linavuma kuwa hawa ni nambari moja? Akanambia “sikiliza e bwana wee. Mimi suala nnalokwambia, hawa ni kirukia.” Kirukia? Eeeh. Kirukia vipi? Akasema, ehee! Hawa bwana suala la Jumamosi hawalijuwi. Hawa wanalijuwa suala la Jumapili, watu wameshachukuwa hatamu. Na wao walikuwa na utaratibu wao. Siri yao wenyewe. Sisi hatujuwi, wala kikundi cha Mfalme hakijuwi. Wao walikuwa na siri yao. Na Ali Muhsin na yeye alikuwa na siri yake kwa upande wa Mfalme. Makundi matatu haya yalikuwa hayaelewani.

Komred angelikuwa yuko shinani, hii serikali sasa hivi ingelikuwa ya Abrahmani Babu. Komred si mpumbavu. Na unawajuwa kama Makomred ni wasomi, kuliko huku tuliko sie? Sisi tulikuwa mabumbumbu, tumetumia kichwa mchungu, lakini wenzetu walikuwa wakitumia elimu. Komred kirukia. Jumaapili Komred ukimtaja. Sio shina. Hamna. Kamuulize Natepe atakwambia kuhusu jamaa hawa. Ma Afro-Shirazi magogo, wengine walio hai wanajuwa.

Suala letu sie, hili bwana, ni akina Mdungi, akina Hanga, pamoja na akina Twala. Kikundi chao nakumbuka kilikuwa ni watu watano. Mwanzo. Walikaa pamoja, walijadili, hata Mzee Karume, yeye alikuwa hajuwi kwamba watu wanazungumza nini. Mzee Karume kaja kujuwa dakika ya mwisho, kuambiwa, bwana we, sasa inabidi wewe ingia botini, nenda zako nyuma ya Chumbe au Dar es Salaam. Kuna nini? Akaambiwa, aa! Wewe tulizana. Sasa leo ukisema kuwa hawa Komred ni namba moja, si kweli. Kirukia.

Bahati nzuri kwa siku ya pili yake, nikamkuta Natepe sasa. Nikasema, ehe! Bwana we, hebu njoo. Kuja pale nkamuuliza. Bwana we, kidogo nna utata. Mimi naona kidogo kama limenitia uchungu. “Haya, uchungu wako nini? Komred wawe nambari moja, sisi tuwe namba mbili?” Akasema “ah! Wewe umechanganyikiwa? Darweshi, hebu ugoro wako unao?” “Nnao.” Mpe kwanza anuse huyu. Nikanusa ugoro. Akanambia, “sasa akili zako zimeshachangamka.” Sasa nnachokueleza, kama utasahau, au umesahau, wao ikiwa leo kama ni namba moja, hivi unafikiria hii serikali ingelikuwa mikononi mwetu? Kwa sababu ingekuwa wao bado sasa hivi ingekuwa wao ni President wa nchi hii. Babu ndo angelikuwa President wa nchi hii. Chupuchupu yetu sisi ingelikuwa si vile kuwa kuwazuwia wale walitaka kutupinduwa sisi. Na uelewe kwamba kwanza walikuwa na mtu, kamandoo wa hali ya juu anaejuwa vita. Sisi hatujuwi. Sisi tulikwenda kule kimabavu tukalivamia tu lile boma. Na yalikuwa kutokana na position [nafasi] tulikuwa naye Kisasi na yeye ni mkuu katika kituo cha polisi. Kila akiulizwa “hata, hapafanyiki kitu chochote. Hata, hapafanyiki kitu chochote.”

 

Wanawake wa Mapinduzi

Sasa, hii ukisema kuwa wao ndo namba moja, inatoka wapi namba moja hiyo? Na nani aliyekubaliana na masuala haya? Mimi ninachokueleza ukweli hasa ukitaka kujuwa ukweli, hii siri, ni kubwa mno. Na angelikuwa yule Bi Kazija yuhai basi ningelikwambia nyumba hiyo yeye alikuwa kama ni mkunga wa Wamanyema, yaani watu sasa wakiingia kule, wanazungumza…Bi Kazija alikuwa Michenzani hapa. Huyo ungelikwenda ukamuuliza, angelikwambia “mwanangu kaa kitako. Mwanzo, hawa kina Hanga, kina nani, walikuwa wanakutana humu mwangu wanazungumza.”

Mimi mwisho nikalishwa kiapo, bibi alinilisha kiapo khasa, tukijakusikia umedumba, hili limevuja, tutajuwa wewe. Yamezugumzwa huko, yamepangwa, hata yalipokuja kutoka mikononi mwao, yakatufika sie, wakaingizwa kina Mfaranyaki, hata wakaingia kina Okello, hili jungu huku limeshamaliza kazi yake. Watu walikuwa wanavaa kanzu kwa sababu yule bibi alikuwa mtu wa tiba tiba, kama mganga. Wakenda kule, watu watasema “si mganga wao Wamanyema huyu?” Mtu anakwenda nampenda mwanamke huyu nipatie dawa, mtu anakuwa hashtukiwi, na mtaa wenyewe wa Ngambo. Kila mmoja ni kivyakevyake tu. Zamani mitaa yenyewe ilikuwa ni ya kuokoteaokotea tu. Sasa, Natepe akanambia, sahau kitu kama hicho kunambia kuwa hawa ni namba moja. Si kweli. Nakula kiapo mahala popote.

Mzee Khamis Darweshi katika kutueleza, bwana, Michenzani kulikua na bibi mmoja pale wa Kimanyema. Huyu bibi tulikuwa tunakutana pale watu fulani. Mchango wake yule mama alikuwa anatupa busara tunampa busara. Lakini siri zetu yule mama alikuwa anazielewa vizuri. Tulikuwa tunazingatia mambo yetu ya mapinduzi. Yule bibi alikuwa anatowa mchango wa hali na mali katika utendaji wa masuala haya. Khasa, lengo wao walimuweka kama security [usalama] wao, kwa sababu ni aliyekuwa majumba makubwa haya alikuwa kwa yule aliyekuwa akijengesha maskuli ya serikali, Humud Said Kharusi. Alikuwa nao karibu kwa sababu nini, yeye kule kafanya kazi muda mrefu sana na wale, sasa jamii ile anaifahamu vizuri sana, na wakati wowote yeye anaweza kwenda kuzungumza nao, akataka chochote anachotaka. Wale wakijuwa huyu ni mzee wetu kwa sababu kwanza huyu mfano kama katulea. Akiuza uji. Sio kilikuwa kikao cha kila siku. Wanaweza wakaa wiki hawajukatana. Lakini kikao hicho Musa Maisara, au Yusuf Himidi, wao wanaambiwa majumbani. Manake waliwachaguwa wale wabarawabara. Wanakwenda pale kama mazungumzo ya kitani, sasa watu walikuwa hawana wasiwasi nao. Kumbe bwana moto wa kumbi unakwenda.

Hapa pia palikuwa na mwanamke mmoja wa Kirundi, na wote wawili hawa wameshafariki wako mbele za haki na mumewe, Shauri Moyo, ndiko kulikokuwa na nyumba yao. Msituni. Huko kulikuwa na vikao tafautitafauti kila wakati. Na huyu mwanamke huyu katowa mchango mkubwa katika mapinduzi kuliko Bikazija wa Michenzani. Kwa sababu huyu alikuwa anajuwa nini kinatendeka. Alikuwa anajuwa nini kitatendeka na nini kinatendeka. Halafu utakuja kukuta kwamba masilaha mengi anayaficha huyu mwanamke.

Masilaha ambayo kama mapanga yalinunuliwa hapa, na zengine nakumbuka, kama pinde, mishare, zile walikuwa wakitengeneza Wamakonde sehemu za sirisiri tu. Mumewe tukimwita Mohamed “Mrundi.” Alitowa mchango mkubwa na alishiriki Mtoni. Alikuwa na masharubu makubwa sana. Yeye alikuwa ni msimamazi wa publiki. Mkewe alikuwa na hali kubwa sana, tena alikuwa ni mtu alietumikia mambo haya kwa hali na mali, juu ya unyonge wake. Mimi nilikuja kusikitika niliposikia yule bibi na mumewe wamefia Welezo, kwenda kutupwa kama mbwa. Wamekufa hata yule jongoo anathamani. Wamefia Welezo. Mimi roho iliniuma sana. Kwa kukosa kutazamwa. Sisi tu ndo tulokuwa tunakwenda “vipi, vipi…” lakini mtu kama huyo ushujaa alioufanya ni wajibu ashughulikiwe.

Watatu alikuwepo Kidongo Chekundu hapo. Ameshafariki pia huyo. Alikuwa Myasa huyu. Lakini katika wote hao watatu hawaingii katika huyu wa Kirundi. Kwa sababu wa Kirundi alikuwa yeye anageuka kama kiroboto. Akikwambia “baba pita ndani, toka mlango wa nyuma, nenda kiunga cha mua hicho, kakate mua” wewe unakwenda kule unasema unakwenda kukata mua, unamkuta mtu kule anakwambia, ukitokeza tu pale, anajuwa huyu ndiye wetu huyu. Na mambo mengi kuhusu habari ya hii serikali ya kimapinduzi alikuwa anayajuwa vizuri sana. Hili suala la Manamba akilijuwa, viongozi gani gani walivokuwa wakikutana, alikuwa anajuwa, suala zote zote.

Hanga alikuwa akijuwana naye sana. Kwa sababu yeye Hanga alikuwa anakwenda kuzungumza na baba yake yule mtoto mwanamke. Akizungumza naye bukheri. Mwisho huyu babake Hanga alikuwa akimwambia yule mtoto mwanamke wewe ungelikuwa mwanamme bwana ungelikuwa kiongozi shujaa mkubwa sana wewe. Lakini lake liko hapa. Hazungumzi kwa baba yake Hanga. Lakini Hanga anamwambia. Mpaka ilibidi ujuwe kitu mpaka kufika Hanga kumuamini yule mama na kumpa maelezo ya hawa Manamba ujuwe kwamba ni mtu siri kubwa sana. Hanga anatoka saa sita za usiku, saa saba za usiku, saa nane za usiku, anakwenda Shauri Moyo anamchukuwa yule bibi anakwenda naye kwake kule kuzungumza na wakubwa wengine. Kutaka kujuwa yale yake yanayotokea upande ule. Wakishamaliza anapelekwa nyumbani yule mtoto mwanamke. Kwa sababu kwa Hanga hawezi kwenda mtoto mwanamme kule. Ndo maana ukaja ukisikia, Hanga anacheza bao hapo Mwembe Shauri, mpaka akina Sefu [Bakari] wakaja kusema “waziri mzima anakwenda kucheza bao na raia bwana, halafu anatoka kwa miguu anapita akitembea.” Watu wakamwambia “kwani si kachaguliwa na watu yule?” Sasa Sefu neno hilo ndo likamkera zaidi, “Mbona huyu ana mapenzi na watu kupita kiasi?” Na hii, pesa, Hanga alikuwa ana mwaga tu. Na alikuwa mcheshi sana. Na ni mtu mkarimu. Sasa Sefu ile ikimchukia.

Natepe kahudhuria mara mbili tu kikao cha Bi Kazija, tena mwisho, sio shinani. Shina limeshamaliza, sasa makombo yakuitwa tufanye nini, tunaitwa mmojammoja. Kaitwa Sefu Bakari kwanza, kaitwa yeye Natepe, halafu akaja akaitwa Darweshi, mwishomwisho, akaja kuitwa Kisasi, kwa sababu Kisasi yeye ni mkubwa wa polisi. Bwana hapa pana ushauri. Utatusaidia vipi wewe? Polisi ndo wewe, sasa sisi tunatafuta hii nchi. Sasa wewe utatusaidia nini? Jawabu ya Kisasi, anasema, siri itazuwilika? Mimi naweza kukinga lakini jee, nyinyi wenyewe mtazuwia. Tutazuwia. Mtazuwia? Tutazuwia. Sawa. Yule sentry wa kule ni Afro-Shirazi. Kapanguwapanguwa, kawaweka wale Afro-Shirazi. Siku ile ya Jumamosi. Sefu Bakari nafsi yake hakuingia. Na Natepe pia hakuingia. Akaingia Yusuf Himidi, Mfaranyaki, Washoto, Kaujore, Okello.

 

Shina Lapinduliwa

Jiko lilipanga mipango yake yakakamilika. Likakabidhi mipango ile. Kwa dakika za mwisho. Baada ya kuwa mipango imeshapangika, watu wameshaingia, wameshachukuwa, wamekuja kumkabidhi Mzee Karume. Sasa utakuja kukuta Mzee Karume jiko lile kaja kulijuwa mwisho. Uwaziri Mkuu akachukuwa Hanga. Kumbe mambo haya yalivokuwa chimbuko liko kwa huku?

Utakumbuka kulikuwa na vijana wa Kizaramo walikuwa wakivaa suruali kipande wakiitwa “Tupendane.” Ile iliwahi kumtia hatiani Mzee Karume. Aliwahi kushtakiwa Mzee Karume na akakanusha pale Victoria Gardens kwenye Baraza la Kutunga Sheria. Akasema wale Tupendane ni watu wahuni. Akanusurika hapo lakini walimkamia vibaya sana Hizbu kwa suala la Tupendane. Kutokana na suala lile ikaonekana kwamba masuala haya Mzee Karume asiambiwe. Akija kuambiwa huyu bwana atakuja sema “aa mimi sifanyi.” Watu walichoka. Kila wakipiga kura watu wananyanganywa. Kila ikipigwa kura, kushinda, watu wanachukuwa. Akaambiwa Mzee Karume. Hatufanikiwi, sasa hivi wewe una mpango gani? “Twendeni hivohivo, kuna siku Mungu atatupa.” Wakaona, huyu keshaogopa. Yalee ya Tupendane.

Majungu ya Sefu [Bakari] kwa Hanga. Babu yeye alikuwa kama ni mchochezi tu hivi. Sasa na huyu Sefu alikuwa akili duni. Babu akaona sasa mimi nitafanya vipi hawa niwaparaganye? Akaona hapa sasa nipitishe chokochoko hii. Lakini wa kumtumilia huyu Sefu. Sefu anamwambia Mzee Karume, hawa bwana wanataka kukupinduwa. Akina Hanga na akina Othman Sharifu. Mzee Karume aliwahi kukataa. Asema “hata!” Akamwambia “ehee!” Bwana kama huyajuwi mimi ndo naeyajuwa. Sasa kwa mapenzi aliyokuwa akimpenda Sefu, Mzee Karume, sote tulikuwa tunasangaa. Huyu kampenda kiasi gani, hata inafika budi leo kwamba huyu uwongo umekuwa wenzake anawauza tu, anawauza tu? Kujipendekeza kwa Mzee Karume na kumwambia maneno ya unafikiunafiki na Mzee Karume hata alipokuja kushtuka, na wakati huku watu wameshakufa. Baada ya akina Saidi Idi Bavuai kumpa ule kweli kuwa maneno anokwambia huyu ni ya uwongo. Utapoteza viongozi wangapi wewe? Baadae Babu alitaka akiondoka Mzee Karume cheo akamate Sefu Bakari. Babu anamdanganya. Kwa sababu sifikirii kama kweli Mzee Karume cheo akamate Sefu iwe kikae muda wa wiki moja Babu hajachukuwa. Si kweli. Angemzidi maarifa. Lazma.

Abdurahmani Babu lilikuwa Koministi la kupepea. Sio mchezo bwana. Kwanza, moja, lilikuwa somi. Msomi mzuri kwelikweli bwana. Sasa utakuta leo mtu kama Sefu kurubuniwa na Babu ni kitu rahisi. Babu masuala ya Manamba aliyajuwa kwa mshtukio tena. Nakumbuka safari moja aliwahi kusema “hi! Afro-Shirazi wana uchawi yakhe. Mpaka wamefika kuwashirikisha Wamakonde? Kwamba leo mpaka Wamakonde wamekubali kuingia kunako mapinduzi? Ama hawa Afro-Shirazi wachawi hawa.” Akina Ali Sultani hao walikuwa wanazungumza “jamani, na nyie Wamakonde nanyi mnakuja kuipinduwa nchi?” Kubakia masihara tu “mjomba, mjomba!”

Kukaa kwa siku tatu yule bwana halafu akapewa Umakamo wa Raisi, jungu la Sefu Bakari. Alimuendea Mzee Karume akamwambia, huyu Waziri Mkuu. Unajuwa Waziri Mkuu ndo serikali? Ukimpa Uwaziri Mkuu huyu na huyu msomi, kuliko wewe, muda tu serikali hii atakuja iweka miguu juu matokeo yake atakuja kuwa Raisi huyu. Wewe umeipata pataje hata ukaja kuniambia hivo?

“Kiundani, kikundi kikubwa hiki, mpaka akina Othman Sharifu wamo, katika kikundi hiki cha Hanga.” Akamwambia hawa wana vikao va siri. Cabinet [baraza] ya akina Sefu, Natepe, Hamid Ameir wa Donge, wakakutana na wakasema mtu akenda akaulizwa masuala haya na Mzee Karume sie tutayaunga mkono. Wasomi wale, sisi hatuna tulichokisoma, tunaambiwa tu ni Baraza la Mapinduzi. Lakini hawa wasomi hawa, huyu bwana huyu, atatuweka miguu juu? Sasa Mzee Karume kila anomuita anampa hadithi zilezile. Twala alisema kama tunataka kupinduwa serikali, tunataka kumpa nani? Wale walipoona Hanga amewachaguwa wasomi kuendesha nchi wale waliona vibaya. Pale ndipo alipoambiwa Mzee Karume, badilisha system haraka sana, muweke makamo wako, usimuweke Waziri Mkuu. Akaja akabadilishwa Hanga akafanywa Makamo wa Raisi.

Okello kitu kilichokuwa kikimchukia, kwamba Wamanga, Mzee Thabit Kombo akenda Raha Leo, hakuna adhabu wanayoipata. Anawahifadhi. Ilimkera zaidi, Mmanga wa hapa Koani. Kateketeza watu yule Mmanga, halafu leo kakamatwa yule Mmanga. Baada ya kukamatwa kaletwa Raha Leo, hakuadhibiwa. Sasa Okello ndo akasema “Mmanga yule kauwa watu, Mzee Thabit leo kamtia kwenye chumba cha peke yake? Na hakuna adhabu yoyote.” Kila sisi tukitaka atolewe mle ndani Mzee Thabit anasema “tulieni, tulieni, huko ndani adhabu yake anaipata!” Sasa bwana huyu tumekataa nini anafanya nini. Itabidi mpaka serikali tuipinduwe. Ipinduliwe tena hii! Lakini hapo, walewale askari wake wakaja kusema “huko tunakotaka kwende siko.” Wanamwambia Okello. Kikao kilekile sasa kilibidi kizungumze katika kikao na akina Mfaranyaki.

Masuala haya yakamfika Sefu, Sefu yakamfika Mzee Karume. “Mpelekeni Pemba!” Hapo utakuja kukuta, askari wake Okello hawakuwa na imani hiyo. Wakimfikiria, leo huyu Mganda, ametoka Uganda huyu, Mzee Thabit ametoka Makunduchi, sasa, kwa nini leo hawa viongozi wadhalilishwe? Okello alituita ati hapa Miti Ulaya. Ndo walewale askari walitoka wakasema mbona kunataka kuingia umwagaji wa damu wa kipumbavu? Sisi tumesema kama Karume ndio President wa nchi hii, ndo jabari wa nchi hii, na yeye huyu anataka kumuua Mzee Thabit Kombo, huyu Karume atanusurika vipi? Ndo hapo jamaa, kina Sefu, ikabidi sasa Okello apelekwe Pemba. Wewe sasa nenda kwa Wapemba ukawafanyie kazi. Kwa sababu huko nako kuna kina Mkame Ndume. Wanawaka! Kawashughulikie! Kenda Pemba, kawashughulikia kweli. Baada ya kumaliza kuwashughulikia kule, kurudi sasa, anarudi, jamani mimi nnarudi. Panda ndege uje zako. Kuja hapa moja kwa moja, uwanja wa ndege. “Bwana hii ndege ulopanda hii utaipanda hiihii.” Baada ya hapo huku usisogee tena.

Kikundi hichi cha Hanga, wote wasomi. Sasa utakuja kukuta hiki kigengi hichi [cha] Hanga, kilimchafuwa roho Mzee Karume, kuona kwamba, huyu katika hili jiko hili hakushiriki! Sisi tuloshiriki, sisi kwanini tubakwe bakwe hivi tuwekwe ovyoovyo. Na hili jambo letu? Hili jiko letu sie. Sasa Karume alipokuja kuligundua hili jiko linataka kwenda hivyo ndo pale aliposema “wapelekeni Kama.” Likapelekwa Kama. Hukohuko Kama ndo walokopigwa marisasi na kuzikwa huko handaki moja.

Liko handaki bwana tena lilichimbwa na jeshi. Huyu alokuwa anakaa Gongoni hapa, Saadalla, kwanini akapiga kelele hapo juu Kiinua Miguu, tena usiku “jamani e, nakwenda kuuliwa wee!” Alitolewa usiku hapo akapelekwa moja kwa moja Kama. Hilo ndo lilosababisha wale jamaa kupoteza maisha yao. Ingelikuwa hakuuliwa Zanzibar ingekwenda kisomi na nakumbuka huenda hata huu muungano pengine usingekuwepo.

Mwalimu aliunga mkono, lakini sasa kutokana na Ukoministi wengine waliousoma, madam Mchina hapa aliingia, basi vitu vote hapa vingekwenda kwa Mchina, kwa hivyo linda hii nchi! Lakini hapo tena walipofeli, ikabidi sasa vile walivokuwa wakitaka…kwa sababu Kassim Hanga alikuwa ni Mzaramu yule. Sasa utakuja kuta, jiko lingekuwa lihai, basi Thabit Kombo na Karume wangekwama. Kabisa! Wangelikwenda mfumo wa Afro-Shirazi. Kusingelikuwa na Muungano. Wangelitafuta himaya kutoka nchi za Kisoshalisti kwa ajili ya ulinzi ingelikuwa hii nchi inataka kupinduliwa na Waarabu.

Mfalme alipotoka hapa kwenda Uiengereza, mkimbizi, kwanini natawaliwa kwenye kizimbani na nyinyi mpo? George Mooring alimjibu: wewe [Ali Muhsin] na Karume muwe kitu hiki: kimoja. Msiwabaguwe. Hawa wengi kuliko nyie. Wewe ukakataa. Kukataa kwako vita vya Juni nikakwambia, kidogo tu nusra serikali yako iaunguke. Nikaleta jeshi kutoka Kenya. Hatima yake wewe si uliniondosha mimi Zanzibar? Ondoka, nenda zako. Kuondoka kwangu mimi nikafika Kenya nikamkuta balozi mwenzangu. Kitu nilichomwambia. Zanzibar mimi naondoka lakini nchi haipo mbali itapinduliwa. Sijaondoka nikaja kusikia imeshapinduliwa. Sasa leo wewe [Sheikh Ali Muhsin] unakuja kuzungumza masuala kama hayo, tukusaidie nini? Sasa hapo ndo inabidi sisi tukuhifadhi tu sisi hapa. Lakini tena Ali Muhsin yeye ikabidi akaruka na chokochoko. Waingereza ikabidi kule wakamfanyia matatizo, wakaona sasa huyu Ali Muhsin itabidi ende akaishi Dubai au Maskati. Kwa sababu hajatulia. Ilionekana wazi wale wangelifanya chini juu kuipinduwa hii. Kwa sababu mfano mmoja ntakupa. Mmarekani alipoambiwa aondowe mnara wake wa Tunguu, basi ziliwahi kuja hapa manwari mbili kwa uchungu na hasira. Lakini Mrusi alisema hapo ndipo patakuwa maziko yetu, na Mchina akasema tutazikana hapo, tutakitumbuwa maji kisiwa hicho.

Lenye nguvu zaidi bwana wewe, huu upande wasio soma huu, ndo wenye wengi, na huyu, huyu Karume huyu, ndo walomtaka wenyewe. Ndo walokuwa wanamtaka wenyewe! Wana Afro-Shirazi wote. Sasa waliosoma kila wanalolizungumza wanabanisha tu wenyewe kwa wenyewe tu huko. Halivuji hilo! Hilo hata mimi ukiniuliza ntakwambia, “Wallahi Laadhim,” undani hasa silijuwi. Kwa sababu ilikuwa siri yao wenyewe kabambe. Wameliweza hili jiko la mwanzo hili, e vipi hili jiko la pili? Kwa sababu haya yalikuwa wasomi kwa wasomi, hawakuthubutu kulileta uraini.

Na wengi walokuwa wakimsapoti Mzee Karume walikuwa hawakusoma. Upande wa huku juu, wasomi wao ndio kweli, walikuwa wengi lakini walikuwa haba. Sasa wakasema hiyo hangaika yote alotuhangaikia, huyu kwanini aondoke, wakae hawa? Haiwezekani! Haya wanasema upande wa uraiani sasa. Huyu ndo alotuhangaikia. Na Sefu sasa, alikuwa upande wa huku, na watu walokuwa hawakusoma, na yeye kwa sababu hakusoma. Katika wana mapinduzi wengi walokuwa wamesoma labda Kisasi peke yake. Ndo aliyekuwa katoka kwao Moshi na cheo chake kaja hapa. Yeye ndiye aliyekuwa kasoma. Lakini waliobakia wote hao, usidanganyike, akina Mfaranyaki hao, akina Kaujore, mbumbunda, akina Saidi Washoto, mbumbunda! Wengi wengi, akina Hamid Ameri hao Kurani. Sasa utakuja kukuta wengi walikuwa hawana elimu.

Huku nyuma lilikuwa lao hili, moja. Akina Hanga na Mzee Karume. Kwa sababu Afro-Shirazi ndio iliowasukuma wale masomo ya nje. Imewapeleka. Kisomo. Sasa hawakuweza kuja kukanusha ghafla tu wakati yule ndo alowapeleka kule. Hanga, nenda nje. Mdungi, nenda nje. Twala, nenda nje. Wote walipelekwa na Afro-Shirazi kwenda kusoma ili tukija kupata utawala hapa tusije tukayumba. Walisoma, walipasi, wamerudi. Sasa kuja kurudi matokeo yake, kukamata serikali, Othman Sharifu alipelekwa Marekani. Hukohuko na yeye alifanya majungu yake.

Wasomi walitaka lile shina lisiwe halikusoma. Lile shina liwe na mtu kasoma. Sio mtu kama Mzee Karume. Majungu ya utawala sasa. Msomi na asiosoma pana tafauti hapo. Sasa hapo wakaona Karume akitowa command [amri] yake ndo moja kwa moja. “Tunakwenda nao tu lakini mbona mambo yanakwenda pindukapinduka hivi?” “Hakusoma huyo! Tumchukulie hivohivo.” “Tumchukulie vipi?” Sasa tutamchukuliaje hivo? Lazima pafanywe mabadiliko hapa. Sasa pakaingia kidudu sasa, kikawa kinachokowa. Kikachokowa, kikachokowa, kikachokowa. Sefu yeye ina maana anarudi upande wa Mzee Karume.1 Kwa kwamba ikiwa hutowahishimu wenye elimu matatizo. Jamii inakuwa haiwezi kwenda mbele. Na wenye elimu wakiwadharau walokuwa hawajasoma, sasa wataiendeleza vipi jamii? Mzee Karume ndo pale alipotowa elimu bure. Elimu bure, hakuna malipo. Akafunguwa maskuli. Ikawa watoto wanakwenda kusoma. Unajuwa, usifikirie kwamba hawa wasomi, jamii isiosoma, raia, wao ndio wakiwachukia. Hata. Wangeliwaelimisha, wasiwangeliwachukia. Ila tu hii ngazi ya mwanzo. Hii ngazi ya mwanzo itakaa hapa kwa muda gani na kishasema madam mimi nimekaa katika kiti hiki hakuna labda kusema mpaka mbono huyu, mpaka afe. Wewe unajuwa atakufa lini? Una taarifa zake unajuwa siku gani atakufa? Aa! Sasa? Lakufanywa lazima upatikane utaratibu wa mageuzi. Hatamu tukamate sie. Wale jamaa ndo walipojiponza hapo. Ingelikuwa hawakupanga njama hiyo wangelikuweko mpaka sasa.

Baada ya Mzee Karume, tabaka ile ingelikuwa imeendelea. Mpaka Othman Sharifu na yeye angelikamata hatamu. Walifanya pupa. Uroho wa madaraka. Walifanya uroho. Uroho ndo uliosababisha kuwaponza. Unaona sasa. Sefu na yeye, majungu yake yote alioyafanya, matokeo yake, kufa Mzee Karume, na yeye aliangukia kilio “utawala wangu huu!” Sasa tutakuonaje weye? Unalilia utawala wako. “Utawala wako vipi? Hebu tufahamishe” aliulizwa.

Kuja Aboud Jumbe akalitawanya lile Baraza la Mapinduzi. Jumbe alimwambia Mzee Thabit “mimi Baraza nalitawanya hili.” Midomomidomo haya nje. Sefu akampeleka mikoani huko. Suala hili lilipangwa na Mwalimu kule. Mlete mkuu wa mkoa. Fulani? Mlete mkuu wa wilaya huku.

Lengo lake [Sefu] lilikuwa hata Jumbe atakapokufa atapata utawala. Nafasi ile alikuwa anaitaka hasa. Kila alipokuwa anawaendea akina Natepe, Natepe akisema “mmh, usitafute balaa. Cheo si unacho, si unakwenda unapotaka. Uhuru si unao bwana. Madaraka hayo unalindwa na askari. Mengine yako peke yako hayo.” Wasingelimuunga mkono.

 

Zanzibar Mtihani—Mzee Joseph Bhalo

Mzee Joseph Bhalo ni mmoja kati ya viongozi wakubwa wa Kimakonde ambao walishiriki katika mapinduzi ya Zanzibar ya 1964. Wakati mashirikiano baina ya askari wa polisi na kikundi cha akina Mzee Aboud Mmasai hayajulikani, Mzee Joseph alimiminiwa sifa ya kuwa yeye ndiye aliyeivunja ghala ya silaha ya Ziwani.

Wapinduzi nnaowakumbuka ni Joseph Nchelenga, alikuwepo Chefu Mawile, Joni (John) Kawajire, Tajiri Fundi, hao ndio watu nnaowakumbuka. Na hapo yuko Koani alikuwepo Kakarange. Yule Mzaramu. Hao ndio watu nnaowakumbuka. Viongozi walikuwa John Okello, Muhammed Kaujore. Hao viongozi walikuwepo. Hao ndo walioshika sukani pamoja na sie watu kumi. Sasa Karume alikuwa hajuwi kama nilivokueleza. Ukisikia kama Karume alikuwa anajuwa, uongo. Atakupoteza bure. Unasikia bwana. Utapata uongo. Karume hakujuwa! Tumefanya sisi. Hakuambiwa kwa sababu yeye ni mkubwa, ni kiongozi, kiongozi wa nchi. Ukenda kumwambia itakuwa “lo! usifanye hivo. Usifanye! Usithubutu kufanya kama hivo.”

Tulikuwa na wasiwasi naye atamkatazeni. Bora tusiseme tumuache hivohivo. Alikwenda kuchukuliwa. Akapelekwa Raha Leo. Pale ndo akakabidhiwa yeye [Karume] serikali. Sasa wewe kazi yako. Manamba hakuna. Karume hakuna.

Mmakonde kuwa ni mwanamapinduzi mpaka leo hajulikani! Hajulikani kabisaa! Hayumoo! Nchi amaeshaichukuwa mwenyewe [Mzanzibari] ndo mwanamapinduzi. Yule hayumoo! Hayumoo kabisa! Mwenyewe ndo mwanamapinduzi. Uwongo mwingi na yeye [Mzanzibari] hajuwi. Ameshapata sasa hivi, anasema uongo, uongo, uongo. Yeye yuko ofisini sasa. Sasa yeye hajuwi alofanya kazi hii. Hajuwi ni nani. Binaadamu tulivyo, tulivyo. Leo ukimwambia mwanamapinduzi Mmakonde alishiriki atakwambia “muongo huyo! Muongo huyo!” Hakushiriki chochote. Niulize mimi, yule hajuwi chochote! Unaona kazi sasa hiyo. Hajajulikana mpaka leo. Wanawatupia Wamakonde uongo mtupu. Mmakonde gani alokaa kwenye kiti? Hiyo ni chuki. Hiyo ni fitna isiokuwa na maana yoyote. Mambo yamepita basi. Mambo ya kifitina.

Siku ya mapinduzi hasa ndo siku ya kumuogopa mtu. Si leo. Hayo yanayozungumwa leo yanazungumzwa kwa shibe. Sisi soote tumeuwa! Unajuwa, sote tumeuwa. Si fulani ndo alouwa. Hapana. Wote tumeuwa kwa sababu sote tulikuwa wanamapinduzi. Kwenda kwenye mapinduzi tulikwenda kwa pamoja, tukafanya kazi kwa pamoja, kwa kugombowa nchi yetu, bas!

Wale walokuwa wamekalia mapinduzi, kuweka mapinduzi, kumbe sivyo! Walofanya mapinduzi wengine, anavosema yeye vingine. Mapinduzi, mapinduzi, mapinduzi, siku ileile iliopatikana serikali, siku ileile, wakati huohuo, yakawa yamekwisha! Sasa yale ya uundaji serikali, yale ni mapambo yale. Haya yalofanyika nje ndo mapinduzi. Itakapoandikwa [historia ya mapinduzi] uongo utajulikana hapohapo. Ukweli utajulikana hapohapo. Walofanya mapinduzi khasa pesa hawajapata. Wanatumia wale walokuwa hawakufanya kazi yoyote hapa. Wao ndo wenye kula matunda yale. Wale walofanya mapinduzi hakuna hata shilingi moja walopata. Upo lakini? Wale mpaka leo hata shilingi moja hawajapata. Hata kuhisabia kuwa mwanamapinduzi. Hakuna! Hakuna! Tokea ile siku ya vita imekwisha, bas! Hili neno nakwambia. Ukiwa utaandika [kitabu], itakuwa “eee! Kumbe imekwenda hivi. Huyu bwana ameandika vipi? Mbona mapinduzi namna kadhaa kadhaa kadhaa.” Itazuwa mjadala kwa watu. Eeeh!

Mimi nakwambiaje? Unataka khasa historia ya mapinduzi? Hiyo mnayodanganywa mnoipata ofisini mtu ameshapata kazi amekuwa mwanamapinduzi. Watu wanadanganywa. Hapa, mapinduzi halisi walikuwa watu wachache. Watu wachache hao wa kutoka bara. Si watu wa hapa. Watu wa hapa walifichwa. Kwa sababu ya kuwa walifichwa. Sijui namna gani. Mwenyewe Karume, msiwaambie watu wa hapa mkiwaambia watu wa hapa watahalibu. Mwenyewe Karume anasema.2 Sasa kweli imefanyika, Wandekereko, Wanyamwezi, Wamakonde, wakafanya kazi hiyo. Tulikwenda wakaanza kuwasambaza watu, msiwaambie watu. Siri! Watu wahapa. Mwenyewe Karume. Suala hili ni hatari ya nchi. Wasiambiwe watu wa hapa.

Hapa tulipo tuwaambiwe watu wa bara. Tuwaambie watu wa bara watupu! John Okello anasema. Wandengereko, Wanyamwezi na Wamakonde na Warundi, Waruguru. Ilikuwa na siri hiyo. Kenya (Ndagaa) alikuwa askari Unguja, Yangeyange, Mruguru (Koani) alikuwa askari Dar es salaam, Okello wamemfata Bhalo. Tunataka mtu anaojuwa bunduki.

Mmakonde alopelekwa Nairobi kutibiwa. Alikuwepo Sidimba, wengi walikuweko Wamakonde lakini hata mmoja hakutiwa katika baraza au serikalini. Mfaranyaki alitiwa kwa jeuri yake mwenyewe. Si kwa kumchaguwa wao. Huyu atatoboa siri bora tumtie. Bavuai alikuwa anaaminiwa kwa ushiriki wa ulevi na uvutaji bangi. Huyu angeweza kutuongoza. Akawasahau wale walomtia kwenye mapinduzi.

Kule anatutizama yeye kwa moyo wake wa kutupenda sie. Manake Karume alikuwa peke yake. Si mtu wa bara! Karume mtu wa bara ati. Watu wa hapa walikuwa hawamuungi mkono yule.

[Sasa] tuongoze sisi wenyewe [Wazanzibari] si wageni. Washafanya kazi imekwisha. Mtu aloshiriki hawamfuati. Wakikubali kama sisi tumeshiriki tutaonekana wakubwa. Tutaonekana watu. Madam sisi tumefanya kazi imepatikana serikali, basi. Ndizi ile anaweza kuidai mtu akisema kama ardhi yake. Sisi tunatizama tu. Wanaleta maneno ya juujuu ya uwongouwongo. Hawajuwi chochote. Chochote hawajuwi.

Wale hawakubali. Kwasababu yenyewe: siri hii wamepata wapi watu hawa? Manake washenzi hawa wameipata wapi? Tunaitwa washenzi sie. Tukiwaeleza ukweli watatuita washenzi. Hawakubali. Wanakubali uwongo. Kuniweka mimi mbele Mwanansumbiji hawataki. Kumfata Mwanansumbiji hawataki. Kitu hicho hawataki kabisaa! Lakini mambo kama haya sisi tumewachia. Tumepeleka barua yetu kwa Raisi na majina. Maraisi wote walokuja hapa. Hawakujibu. Karume angelikuweko saa hizi angelinisikiliza lakini alikuwa peke yake.

Majina tumepeleka kule. Mpaka leo, kimyaa! Kesho anatoka Uraisi yule. Si basi. Imeshakwisha! Tutamwendea mwengine. Bure! Bas! Hapa alioshiriki, Raisi [Ali] Hassan Mwinyi. Basi huyo haijambo kidogo. Ilikuwa haijambo kidogo lakini na yeye akaambiwa usiwape kichwa hao. Ikesha! Nasie, tumechoka hasa kwenda [Ikulu] kila wakati. Tukafanye nini? Tumewaachia. Tunawatizama macho. Alikuweko Dadi, mtu wa hapa, kwao Mkokotoni. Alikuwa anashiriki yote. Lakini akisema yeye peke yake! Haifai kitu! Mwisho wamemwambia “wewe unatetea watu kuliko wewe mwenyewe? Watu kwao bara? Kwanini?” Ndo wanavosema. Hayaa!

Wataona aibu kubwa! Kutoa siri yetu kutangazwa wataona aibu kubwa. Hatujapata mtu wa kulifanya suala kama hilo. Na mambo yatakwenda.

Muda ni mrefu lakini inaweza kupasuliwa. Kumbe watu wamefichwa. Walofanya kitendo hichi kumbe hawakufanikiwa. Itakuwa aibu kwao. Kubwa! Mpaka leo serikali yetu hii ina dhambi ilofanya. Wamefanya tendo, halafu wameficha, halafu anaonekana yeye ni mtu. Siyo. Dhambi ya kuficha. Ndo mambo mengine hayaongoki. Uongozi hauongoki. Mambo hayendi. Alofanya kitendo wewe umemficha. Alokuwa hajafanya kitendo amekuwa mtu. Si dhambi hiyo?

Suala kama hilo tungelimpata mtu akalitowa nje. Wasishtuke kwanini na wao wanasema uwongo? Wasishtuke kwanini? Kumbe wamegunduwa wapi? Sasa mimi ntakuwa vipi? Mimi muongo! Hana uso. Uongo! Sasa kimyakimya mambo yenu tudanganyane hapahapa. Si nje. Nje watu wanajuwa ukweli wa mambo. Tudanganyane hapahapa Unguja. Mnavofanya Unguja si halali. Watu walofanya hawakupewa kitu. Sisi tutaendelea hivihivi tutakataa. Basi Mungu yuko.

Ukitaka ukweli wa mambo ya mapinduzi watu wa hapa hawajuwi kitu. Watu wanojuwa watu wa njee! Watu wa nje wale wametupwa kwa sababu si pao hapa. Wako watu wanasema petu hapa! Basi hao ndo wanoharibu wanosema “petu hapa!”

Serikali ya pili [ya Tanganyika] inasema ukweli wakati mwengine. Mna dhambi. Mmekosa radhi nyie. Uongo ndo mnootegemea. Si halali. Limegundulikana, aibu itakuwepo. Halali gani itakuwa kwao wao? Itabidi waweke uhalali mpya. Wengine watakuwa nje. Haitokuwa salama. Mwanya mkubwa utakuwa kwa wanaodai serikali. Upinzani utakuwa umepata mwanya mkubwa! Kumbe wanatudanganya, uongo. Si halali. Sisi hatufanyi hivo. Unaona kazi hio?

Zanzibar itapata faida gani kwa mwanya huo? Serikali itajuwa mbele baadae kipi cha kufanya. Hawa watafanya mbele hawa. Si mepesi. Makubwa! Mwizi umejificha, ukakamatwa, atakuona weye mbaya! Mwizi atakuona weye mbaya! Yeye anataka afiche siri yake mpaka afe. Ndo anavofikiria yeye afanye. Ukimgunduwa atakuona wewe mbaya. Serikali itakuona wewe mbaya! Miaka 45 haiondoki siri kama hii? Si halali.

Kwa watu waliosaidia tungekuwa tunadanganywadanganywa. Leo hudanganywi chochote. Unatupwa kama…Sisi tulofanya kile [kitendo cha mapinduzi] tunaombewa mabaya. Tulofanya kitendo roho iuliwe halafu leo mtu anakuficha na anakuona wewe si kitu. Si ubaya huo? Halali hiyo?

Nakupa Nchumbiji. Siri ya Nchumbiji watu wanatizama mbele. Hapa hawaoni mbele. Uongo mwiingii! Mambo mabaya ya kiserikali hakuna. Yamekatika. Tuondoshe uchafu huu kwanza kwa kungudulikana kitu hicho [mapinduzi]. Watajijuwa. Lazma watajijuwa. Kwenye serikali kuu itakuwa ubaya, wataamuwa wao. Tumefanya hivi, tumefanya hivi…Si uzuri, si halali. Tufanye kitu, watu watawale, wawe radhi. Itakuwa hivo. Tukipigana wewe na mie atokee mtu atuamue. Ikitoka nje itaamuliwa. Serikali hii inavuma mapinduzi lakini sivo! Serikali inajuwa. Suala hili linajulikana wazi. Walofanya wengine walokaa watu wengine. Serikali inajuwa. Aibu. Tufanye kitu sasa. Itaamuliwa wakati huo. Lazima! Madam liko nje litafanyiwa kazi. Pana aibu gani tena. Tutaweza kwenda mbele.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: