Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!

Icon

Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia

Mlango wa Kumi na Mbili: Waafrika, Waarabu, na Ukombozi wa Afrika

Tukimpinga yoyote yule aliyekuwa akifanya kazi kwa maslahi ya Ufaransa au Uingereza. Mpaka hii leo niko dhidi yao. —Ahmed Ben Bella

Mzee Aboud “Mmasai”

Algeria ni kitu chepesi kufahamika. Nilikwenda Algeria kabla ya mapinduzi na ipo picha nilopiga mie na Ben Bella na watu wengine. Tulikwenda mwishomwisho wa mwezi wa Novemba [mwaka 1963]. Mimi, Twala, Ali Mwinyi Tambwe, yupo kijana mmoja akiitwa Khatibu.

Tuliondokea Dar es Salaam kwa ndege. Tumepitia Addis Ababa, Ethiopia, Jordan. Msafara wenyewe ulikuwa mzungukomzunguko. Hatukwenda moja kwa moja. Safari sisi tulipakiwa kama mizigo. Alotowa fikra ya kwenda Algeria kwa kweli alikuwa Oscar [Kambona]. Manake unajuwa, kitu kimoja nataka…Hanga alikuwa hawezi kufanya kitu chochote bila ya kumshauri Oscar. Alikuwa rafki yake sana. Waliishi Ulaya pamoja nasikia. Walikuwa wako karibu sana sana…Kutoka Jordan tukaja Sudan, halafu ndo tukenda Algeria. Ilikuwa ni safari ya kubabaisha. Sie tumekaa Algeria sku tatu. Hatukukaa Algiers. Tulikaa kwenye kijiji kimoja karibu ya kilima. Pale ndo tuliwekwa sie na Ben Bella alikuja kule na mara nyingi akija laasiri. Tulikuwa na mtarjumani wao.

Kulikuwa na jambo moja la viongozi wa Kiaafrika. Walikuwa wanataka kufanya Umoja wa Afrika kama alivokuwa anataka Kwame Nkrumah. Mapinduzi ya Zanzibar yalikuwa yameshafikiriwa Zanzibar, sasa watu wa Zanzibar wakitaka silaha za kuwasaidia. Ndo kitu kilichowapeleka na lengo kubwa ni sisi tumepata kura nyingi lakini tumenyimwa.1 Kuna mapendeleo baina ya Waarabu na British Resident, serikali. Iliwapendeleya hawa. Hiyo ndo sababu tulozungumzia kule kwa Ben Bella ili atusaidie kupata silaha. Kakubali baada ya maneno mengi. Halafu tukaondoka sisi hatukupata kitu. Nasikia wakenda watu wengine mimi siwajuwi. Nadhani hata Oscar [Kambona] alikwenda.

Huku kwetu sie aliondoka Saleh [Saadalla], ndo alikuwa Mwenyekiti wetu kwenda kwa Ben Bella. Hapa Zanzibar aliondoka, Saadalla, na mie, na Twala, na Khatibu, basi. Tambwe tulikwenda naye. Si alitumwa na Oscar. Tulikuwa na mtu mmoja mwengine lakini simjui nani. Alikuwa mtu wa bara, alikuwa katika ofisi ya Mambo ya Nje lakini simjui uzuri mtu huyo. Mimi nilijuwana naye katika hiyohiyo safari. Nadhani tulikuwa tunafika watu wanane. Tukaekwa katika nyumba ya nje kilimani kule.

Aloanza mazungumzo ilikuwa ni Saleh. Na ilitakiwa aanze yeye kwa sababu yeye ndio Mwenyekiti wa lile tendo lenyewe. Na ndo mwenyewe katika nchi, wale wengine ni katika msaada wa kutufikisha sisi pale, hawajuwi kitu. Na Saleh neno lake aloanza mazungumzo…Ben Bella alikuwa na watu wake pale. Sijui walikuwa wangapi. Nasikitika, ile picha ngelikuwa nayo hapa. Nilipiga na Waarabu fulani walikuwa wamevaa vilemba. Ben Bella alikuwa amevaa nguzo za kijeshi. Wale waliovaa vilemba kwenye ile picha tulopiga Algeria walikuwa ni watu wa kule kule. Sio sie. Tena ni watu wakubwa kwa sababu wale ndo walokuwa wanatufundisha mambo yote. Na ndo alokuja nao yeye [Ben Bella] siku ya awwal. Hawa watu watatu vigogo hivi vinaonekana. Sasa Saleh alisema hivi: sisi hatukushindwa katika uchaguzi.

Uchaguzi sisi hatukushindwa. Tuna viti vingi kuliko ZNP. Sisi tuna kura nyingi kuliko kura za ZNP na ZPPP. Lakini kwa mujibu wa majimbo yalivokatwa, ndio wakaweza ZNP kupata viti viwili va kuweza kufanya muungano na ZPPP ili wapate kufuzu kuunda serikali. Na juu ya hivo, tulikwishawazidi ZNP kwa viti viwili, viti viwili au kimoja kama hivi. Lakini muungano wa ZNP na ZPPP ndio uliofanya ZNP kupata madaraka ya serikali na ndio kumuwacha Shamte mwenye viti vitatu kuchukuwa madaraka ya Uwaziri Mkuu. Haya ni maneno ambayo Saleh Saadalla Akida… [Kama nilivoelezea kabla] sisi tulikwenda kumuona Nyerere mwezi mmoja kabla ya mapinduzi, kakataa kutuona. Kakataa kabisa. Nyerere alizizuwia [silaha] khasa zisende Zanzibar.2

Hawa watu walikuwa na ugomvi, baina ya Kawawa na Oscar. Hata kwenye mikutano ya hadhara wanavutana. Kwa sababu kila mtu anamsema mwenzake kwa Nyerere. Nyerere akijitizama mwenyewe. Silaha zetu kachukuwa yeye Nyerere. Zilikuwa zetu na zilituwa Dar es Salaam kwa usalama, lakini ndo tumekosa usalama. Alokwenda kwiba ni mtu mkubwa sana—Oscar [Kambona].3 Silaha nyengine zilikuwa ni mzigo maalumu pamoja na bastola. Alituletea Oscar. Miwani zilitengenezwa Ujerumani. Manake zile bastola tulizoletewa mimi ilikuwa mara ya mwanzo kuziona. Zilikuwa kubwa, nzuri, ndogo, zina magazine [kitasa cha risasi]. Mimi sikuiona mizigo. Imezuwiliwa ndani ya meli Dar es Salaam. Hapa kilikuja kijizigo kidogo. Kina Bren gun mbili tatu. Shot gun zipo. Machine gun ipo, hand pistols zilikuwemo. Zile zilipitia Pemba kutoka Tanga. Kutoka Pemba zikashuka Forodhani, kwenye mchanga pale, saa nne ya asubuhi. Asikari wako tele pale. Na huku ni benki ya Standard Bank of South Africa.

Pale kwenye Forodha Mchanga ndo iliposhuka. Manake ingeshuka uchochoroni ingekamatwa. Nilikwenda na Khalid Sefu Al-Mauly. Alikuwa hajuwi kabisa kuhusu aina ya mzigo. Yeye alikuwa anafanya kazi ndani ya meli. Tukenda, nkachukuwa masanduku yangu. Ananiambia “nini”, nikamwambia “bia hizi.” Bia, brandi, manake imepangwa uzuri sana. Pombe hii, wacha tunakwenda pata chochote. Imepangwa kwenye sanduku kama hardboard laini lilikuwa na kanda za chuma. Yalikuwa masanduku matatu. Nilikuwa nalo hapa nyumbani, lilikaa likigaragara. Moja nilikuwa nalo mie. Lina kamba zile za chuma za kufungia mizigo hivi katika masanduku. Ya mistari ya rangi ilopiga hivi [kama krosi].4 Lilikuwepo hapa chumba hiki, hata nikivumbikia ndizi. Ngarawa ndo ilobeba hayo masanduku. Kuna ngarawa zinaweza kubeba hata mbuzi sita.

Tulipakia ndani ya motokari ya Ali Saidi. Tumetoka pale Forodha Mchanga, tumepita Beitlajaibu, tumeingia njia ya Wizara ya Kilimo mlangoni pale, kichochoro kile kidogo, tukapita moja kwa moja Kituo cha Polisi cha Darajani, tukaja zetu mpaka kwangu tukateremsha sanduku moja kwangu. Tukenda nalo mpaka Kwa Hani. Kwanza tumepita Gongoni kwa Saleh na tumeipita polisi ya Kisimamajongoo, mwangoni. Tukenda tukasimama kwa Saleh, hatujapakuwa. Tumeongea tu. Tukenda zetu Kwa Hani. Kwa Hani tukateremsha kwa Mohamed Omar “Masharubu”. Moja tukateremsha kwa Khamis Beni. Waladhaaliin. Yale ndo yalotumika Ziwani. Ni kidogo tu. Moja, mawili. Vijibastolabastola vile vilikuwepo mkononi. Alaaa. Si dhahir bwana, utakwenda bila ya kile. Nyingi sana hazijatumika. Zilotumika labda zitakuwa nne au tano kama hivi. Hazifiki. Ilikuwa haina haja. Halafu zote zilikwenda Ubago wakati Warusi wako hapa. Na Warusi ndo wakatengeneza lile handaki la kuweka [silaha]. Hakuna mtu aloleta silaha kabla ya mapinduzi isipokuwa Algeria tu peke yake.

Zile zilotoka baina ya Kenya na Tanga sijui zilipita njia gani lakini zilifika Unguja. Sikuhusika nazo. Zilitokea Kenya zile. Manake Kenya kuna mahala unavuka, mimi sikujui, sijapata kwenda. Kule Mombasa kuja Tanganyika iko sehemu ina bahari unavuka, lakini ukivuka ile ukija katika Tanganyika unaweza kuja kwa miguu huku, mpaka juu, na ukenda kwa ngarawa unaweza kuvuka ukaja tokea Pemba, na wanokimbia Pemba ndimo wanakomofikia humo. Mara nyingi utasikia wamefikia humo. Sasa hizi zilifika, zimekwenda Ubago, lakini naamini zimepitia Pemba, halafu Pemba tena, baada ya mapinduzi zimebebwa polepole. Zilipitia Pemba, Mkoani, kule zimekaa, manake ndo mahala penye ngome ya Afro-Shirazi.

Ile operation ilikuwa bara. Silaha zile ziloibiwa zile katika meli kwa amri ya huyu Mnyasa, Oscar Kambona. Na akapewa askari wale wawili, ndo waloteremsha na wakashindika. Mmoja Kepteni nani huyu, mtu wa Kigoma, na mmoja wa Tanga. Hawakuleta wenyewe. Hizi ilikuwa boti ya nanhii…ya wavuvi…manake misafara yote ilikuwa inafanywa na baba yake Fuko. Bagamoyo, Mlingotini, ndo kwake, na hapa Gongoni, Unguja. Jirani ya Saleh Saadallah. Kwasababu ndugu yake yeye babake Fuko ndo mkewe Ibrahim Saadalla, biti Huseni. Operations zile aliwachiwa babake Fuko pamoja na mtoto wake anaitwa Huseni. Manake Abdulaziz Twala alikuwa na mchango mkubwa katika mambo haya ya kuwasili kwa vitu kama silaha. Unajuwa mambo mengi unasahau. Siku nyingi. Yeye alikuwa ni wa tatu katika uongozi wa mapinduzi. Baada ya Hanga, Saleh, Twala.

Mimi habari nyingi za watu wa mbalimbali sizijuwi. Kulikuwa na vikundi tafauti katika Chama cha Afro-Shirazi, lakini sio Umma Party. Mie nlozungumza wote, visa vyote va memba wa Afro-Shirazi. Lakini viongozi wa Afro-Shirazi wa akhir ya juu, kina Karume, hawahusiki. Wamekuja kufanywa tu kuwa viongozi wa mapinduzi baadae. Kwa sababu watu wengi walokuwa kwenye shughuli za mapinduzi walikuwa hawamuamini Karume.

Mimi mapanga najuwa watu wote walikuwa nayo. Lakini mishare na mikuki, hayo mambo labda ya Youth League walikuwa nayo. Sisi hatujapanga kishenzi, tume organize vitu kisayansi kabisa. Ukitaka kuingia mahala lazim jeshi la polisi liwe na wewe. Ndo maana wakanitenga kina Karume kuwaambia watu, watumishi wa serikali wasiseme na mimi ati. Na asikari hasa! Hana haki ya kusema na mie. Wakaeneza picha zangu mote humu. Jabir Uki na Khamis Fadhil wanaweza kuzikumbuka tarehe. Mimi sizikumbuki. Ukweli, nilikuwa mtu wa hatari sana, na mpaka leo. Si nimekuonesha barua ya usalama ilioniondolea kizuwizi alioitia saini George Salim.

 

Rais Mstaafu Ahmed Ben Bella

Ni kweli [Nyerere] alikuja kututembelea na alionana na mimi na alifurahi kuniona. Nilimjuwa Nyerere wakati wa ukombozi wa kisilaha dhidi ya ukoloni uliokuwa ukiishi ndani ya nchi zetu. Hivi vilikuwa ni vita va ukombozi. Katika mabara ya Asia, Amerika ya Kusini na Afrika. Kilikuwa ni kipindi cha kihistoria. Historia inatengenezwa kwa mujibu wa vipindi, awamu. Kipindi tunachokizungumzia kilikuwa kipindi cha ukombozi wa kutumia silaha. Ukoloni ulikuwa umekwisha na tulitaka kuunda Umoja wa Afrika kupitia [Organisation of African Unity] OAU. Mimi nilikuwa mmoja wa waasisi wa OAU. Wakati huo Nyerere alikuwa akiiwakilisha Tanganyika na akiitwa “Mwalimu.” Ndani ya OAU kuna baadhi walikuwa dhidi ya Waarabu. Kwa mfano, kulikuwa na maudhui ya kuchaguwa lugha. Kiingereza na Kifaransa lakini waliikataa lugha ya Kiarabu. Gamal Abdel Nasser alikuwa na mimi na alikasirika sana.

Kulikuwa na tatizo la Zanzibar. Waarabu walikuwa wameifanya Zanzibar koloni lao. Nyerere alikuwa na fikra hizo (na sisi pia) au tusingelimpokea. Ukweli mimi ni Mwarabu ndugu yangu. Wakati huo mimi nilikuwa ni Raisi na nilikuwa na thaqafa [taarifa]. Nilikuwa najuwa kuwa kulikuwa na matatizo na ndugu zetu weusi wa Kiafrika. Kulikuweko ubaguzi na Uislamu ni dhidi ya ubaguzi. Na Uislamu dhidi ya Ukristo pia si mzuri. Nyerere aliniambia “una mahusiano mazuri na [Gamal Abdel] Nasser na msimamo wake juu ya Zanzibar si mzuri.” Nyerere aliniambia “sikiliza, Nasser aniunge mkono…” na akaniomba nizungumze na Nasser abadilishe msimamo wake na asiwaunge mkono wabaguzi wa rangi Zanzibar ambao ni dhidi ya uzalendo wa Kiarabu na Uislamu, na nini Waarabu wanafanya dhidi ya ndugu zetu wa Kiafrika. Ni haramu katika dini ya Kiislamu. Hakuna ubora isipokuwa kwenye kumcha Mungu. Nyerere mwenyewe aliniomba hilo. Nasser alikuwa yuko pamoja na kikundi [ZNP] ambacho kilikuwa dhidi ya Nyerere.5

Na ndani ya OAU kulikuwa na vikundivikundi ambavyo vilikuwa havina mahusiano mazuri na Waarabu. Ukweli, Nyerere hakuwa mmoja wao. Yeye na Nkrumah wa Ghana, Modibo Ketia wa Mali na Sekou Toure wa Guinea. Hawa ndio walikuwa mijitu mikubwa ya Afrika. Nyerere akaniomba, baada ya ziara yake, nimuombe Nasser aizuwie sauti ya Masri ya Waarabu kuwaunga mkono Waarabu wa Zanzibar na tukaanza [kazi na] Djoudi. Namjuwa na yuhai. Anazungumza Kiingereza kizuri sana lakini sionani naye mara kwa mara. Kulikuwa na mirengo yenye kupingana ndani ya OAU na nilifaulu pamoja na Nasser kuwakinaisha wengine wenye fikra kama zetu kuianzisha Kamati ya Ukombozi wa Afrika. Na Djoudi alihusika na mafunzo ya kijeshi. Alikuwa muwakilishi wetu na mimi ndiye niliemchaguwa. Alikuwa ni Kanali katika chama cha ukombozi cha FLN na alikuwepo nchini kwenu. Alikuwa ndo dhamana wa Kamati ya Ukombozi wa Afrika.6 Viongozi wote wa ukombozi wa Afrika walikuwa hapa Algeria na mimi. Tukiwapa chakula na silaha.

Siwezi kukumbuka vizuri lakini ndugu zetu walituomba silaha na meli ya Ibn Khaldun ilikuwa kwa ajili ya kubeba silaha. Kiukweli, tulikuwa pamoja na Nyerere. Hatukushajiisha ukombozi ndani ya Zanzibar. Tulimuunga mkono [Nyerere] na kazi yake na nilimtetea kilillahi. Nyerere ni Mkristo lakini tukimuhishimu. Sikiliza ndugu yangu. Kitu chochote ambacho Waafrika walikubaliana nacho sisi tulikiunga mkono. Mrengo wowote ule ambao ukiungwa mkono na nchi za Magharibi tulikuwa dhidi yake. Yoyote yule ambaye alikuwa akifanya kazi kwa maslahi ya Ufaransa, au Uingereza, sisi tulikuwa tuko dhidi yake. Mpaka hii leo nitakuwa dhidi yake. Wamemchukuwa ndugu yetu mweusi kutoka Afrika wamempeleka Marekani kufanya kazi katika mashamba ya pamba. Huu ndio ustaarabu wa nchi za Magharibi. Mimi si mbaguzi lakini ni dhidi ya ukoloni. Sisi tuliona ni jambo takatifu kuwaunga mkono Waafrika ambao walikuwa wakifanya kazi ya kuzigomboa nchi zao. Akinijia Muafrika, au Mhindi Mwekundu [wa Marekani], na anataka kuigombowa nchi yake, kwangu mimi huo ni wajibu uliotakasika. Na hatuwaungi mkono kwa maneno matupu. Tunawaunga mkono kwa silaha. Tunawaunga mkono kwa pesa. Kwa kuwatengenezea nyaraka na pasipoti. Mpaka hii leo.

Fidel Castro na Che Guevara walikuwa wanafahamu kuhusu Zanzibar lakini kijuujuu. Si kwa undani. Walikuwa hawaruhusiwi kufanya jambo lolote.7

Che Guevera alikuwa mtu asie na majigambo na alikuwa mtu wa Magharibi! Nini nchi za Magharibi zimeifanyia Afrika ni kitu kisichoweza kukubalika. Ni dhambi. Nilitowa silaha, na leo na kesho nitafanya hivohivo.

Tulimuunga mkono Nyerere [pale alipopinduliwa] ili aweze kujirudishia nguvu za utawala. Ndani ya mwaka mmoja yalifanyika mapinduzi ya kijeshi isihirini na mbili baada ya yetu Algeria. Nchi za Magharibi ndio chanzo. Viongozi wetu, mpaka hii leo, wana vitu viwili tu. Bendera na wimbo wa taifa. Hatuna ilimu yenye kutuunganishia mambo. Tuna ilimu ya vipandevipande. Tuna OAU au AU ambayo haifanyi kitu. Haitangulizi kitu, wala haibadilishi kitu. Hata ndani ya OAU Nkrumah alikuwa ana nguvu kuliko Nyerere. Katika kazi khasa ya ukombozi dhidi ya nchi za Magharibi Nkrumah alikuwa ana nguvu zaidi kuliko Nyerere.8 Tuliwaunga mkono wale ambao waliokuwa dhidi ya maadui zetu—nchi za Magharibi. Jana na leo.

Ndugu yangu, sikubali kuwa Nyerere alikuwa ni haini. Hii siwezi kukubali. Alikuwa dhaifu. Namfahamu vizuri. Nilionana naye, nikazungumza naye na akaja kwetu na tulikuwa pamoja ndani ya OAU tukipigana myereka na wale ambao walikuwa si dhidi ya ukoloni. Na mpaka leo OAU/AU inaumwa gonjwa hili. Tulikuwa nchi kumi na mbili, pamoja na Nyerere, ambazo ziliusimamia ukombozi wa Afrika. Djoudi tulikuwa naye katika jeshi la ukombozi na alizisimamia nchi tisa za Kamati ya Ukombozi wa Afrika, na akizungumza Kifaransa na Kiingereza kizuri alichojifundisha Yujbara, moja katika miji ya Algeria.

Kamati ya Ukombozi wa Afrika ilikubaliana kwa pamoja au bila ya pamoja kuunga mkono kila harakati za ukombozi za Afrika. Ni lazima wajuwe kila kitu kiliopo kuhusu ukombozi. Tulikuwa pamoja dhidi ya wengine. Nkrumah, Modibo Keita, Sekou Toure, Nasser na mimi mwenyewe. Wengi walikuwa wako dhidi yetu. Kwa ukweli Nyerere alikuwa pamoja na sisi.

Haile Sellasie hakusema kitu chochote dhidi ya njia tuliokuwa tunakwenda juu yake. Lakini kwa ukweli nilikuwa sina raha na siasa zake za Ethiopia. Sikuwa na raha kama nilivokuwa na raha na misimamo ya Sekou Toure na Nkrumah. Hao wawili walikuwa dhidi ya ukoloni.

 

Balozi Noureddin Djoudi na Kamati ya Ukombozi ya OAU

Nilizungumza na Rais [Ben Bella] jana. Kama unavojuwa anaamini sana mashirikiano baina ya Waafrika na Waarabu. Unajuwa kuna mengi sana ya kusema ambayo hayajapata kuzungumzwa si kwa njia za rasmi au zisizo rasmi. Wakati ule [wa mapinduzi ya Zanzibar] Maisraili walikuwa wana ndege zao pale, na kile walichokiita kuwa ni programu ya mafunzo. Nilizungumza na Kambona na Nyerere na tukaweza kuwatowa [Maisraili] na pia walikuwa na mpango wa kijeshi Uganda. Kwa hiyo kuna mahusiano baina ya kuwepo wao Afrika Mashariki na mambo mengi yaliotokea. Kwa hakika, mapinduzi yalipotokea Zanzibar, niliwasiliana na Abdurahman Babu na Nyerere. Nikasema kuwa kama mna mahusiano mazuri na Rais Ben Bella basi sidhani kama atakuwa na furaha na yanayotokea. Munaweza kufanya ukombozi lakini si mauwaji ya halaiki. Na kuwepo kwa Okello ni jambo lisilofahamika. Hakuhusika kabisa na Zanzibar. Unajuwa hata watu kama Abdurahman Babu walipumbazwa na tukio la mapinduzi. Nakusudia hawakuwa na mahusiano ya moja kwa moja nayo.

Si rahisi kuelezea na maelezo yake kidogo ni marefu. Kuna masuala mengi, na maelezo mengi ambayo hayawezi kufahamishwa kiurahisi na unajuwa mahusiano baina ya viongozi wa Zanzibar hayakuwa mazuri.

Habari ya [meli] MV Ibn Khaldun hiyo ni hadithi nyingine kwa sababu Ibn Khaldun ilipeleka msaada Tanganyika na tulikuwa na baadhi ya silaha kwa ajili ya FRELIMO, Msumbiji, lakini baada ya kushindwa kwa maasi ya kijeshi Tanganyika ya mwezi wa Januari [1964] niligunduwa kuwa walipaingilia [Waingereza] mahala tulipozificha silaha na pakategwa mtego wa bomu. Ungelitokea mripuko mkubwa ambao ungeiangukia Algeria lakini tuliutambuwa na mapema. Na hapo pia yapo mengi ya kusemwa. Baadhi ya silaha zilipotea, nyengine ziliharibiwa. Kilikuwa ni kipindi muhimu kwa sababu FRELIMO ilikuwa inaandaa ukombozi wake.

Hata suala la utumwa ni lazima liulizwe kwa njia ya maana ya utumwa. Nakusudia, kuna utumwa wa kuwekwa nyumbani. Na kuna kuwakamata na kuwauza watumwa na kuwapeleka Marekani ya kaskazini na ya kusini na kwengineko. Sasa wamejaribu kuficha nini Wazungu wamefanya, kama ni Waingereza, Wafaransa, au Wareno, na kuzitupa lawama juu ya migongo ya Waarabu wakati kihistoria Waarabu hawajaingia ndani ya bara la Afrika kukamata watumwa.9 Watumwa walisalimishwa kwa Waarabu ya imma kutoka kwa Wareno au mara nyingine kutoka kwa machifu wa Kiafrika wenyewe. Na zaidi, kuna sharia ndani ya Qur’an inayowalazimisha Waarabu/Waislamu wanapomiliki watumwa. Mtumwa anatakiwa ale chakula kilekile anachokula bwana wake, anatakiwa achukuliwe kama ni memba wa familia, na zaidi ya yote, watu wanasahau kuwa kitendo cha kwanza dhidi ya utumwa katika Uislamu ni pale Mtume Muhammad (Salaa na salamu za Allah zimshukie) alipomnunua mtumwa wake na akampa uhuru hapohapo. Kwa hakika Uislamu ulikuwa ni wa mwanzo kupinga utumwa na maamuzi ya Wazungu ya kupinga utumwa yalikuja mwisho wa karne ya kumi na tisa, na mwanzo wa karne ya ishirini. Nilipokuwepo Angola niliona na Wanaangola watakwambia, kuwa walipokuwa wanachukuliwa watumwa kupelekwa Brazil, Kanisa liliibariki biashara ya utumwa kwa kusema kuwa imehalalishwa kidini kwa sababu mtu mweusi alikuwa hana roho! Haya ni mambo ambayo yanafaa kuonyeshwa tena hadharani.

Nafikiri pia Waarabu wamefanya makosa mingi kwa kutokwenda Afrika na kujionea wenyewe hali halisi ya mambo yalivyo kwa kutumia angalau pesa zao kidogo. Siku za harakati za ukombozi, nani alisimama na Waafrika? Walikuwa ni Waarabu peke yao! Afrika kulikuwa na watu kama Mobutu ambaye aliiunga mkono siasa ya kibaguzi ya Afrika ya Kusini. Ni lazima tuyafahamu vizuri yaliopita nyuma kwanza.

Kwenda Somalia Kuisaidia Zanzibar—Balozi Mbarak Khalfan

Jina langu Mbarak Khalfan Al Sabahi, nimezaliwa Zanzibar siku kama leo, na nimesomeshwa Zanzibar katika skuli za serikali mpaka standard 8, baada ya standard 8, nikafanyiwa varangevarange na Wazungu ikabidi kugombana ugomvi mkubwa ukafika mpaka Jumuiya ya Wazee. Muhimu nikasoma kidogo miezi sita katika Muslim Academy, Al Maahad Al Islami, baadae ilipofika mwezi wa June mwaka 1956 nikaondoka Zanzibar kuelekea Masri kwenda kusoma. Na tangu miaka hiyo tena nlosoma Masri…ilipotokea mapinduzi ikabidi tena kuondoka Masri. Kwanza tulitiwa jela. Nimetiwa jela kwa sababu nilikuwa President wa Zanzibar Youth and Students Union ambayo ilikuwa ikiwakilisha All Zanzibar Students Union.

Ilikuwa mwezi wa June 1965 vilevile baada ya kumaliza mtihani siku ile ile wamekuja maaskari kanzu wakanambia tuna haja na wewe mara moja. Sababu yao ni kuwa Karume kataka nirudishwe. Kulikuwa na mzozano mkubwa. Walitakiwa watoto kwanza, wale walokuja 1958 wote, wadogowadogo wale, wote warejeshwe sasa kila wakija kuwachukuwa hawaonekani. Walikuwa hawawapati. Sasa Hija Saleh akasema huyu ndo yuko nyuma ya mambo yote.

Kulikuwa na vijana wengi kwa hakika na kila mmoja alikuwa ana mchango wake lakini yule bwana akashikilia kuwa mimi ndo nilokuwa ukubwa nimeukamata mie kwa hio ni lazim mie wa ilhali wakati ule mie, tulikuwa sisi tumeshawaachia wengine kuiongoza Zanzibar Youth Union na sisi tulikuwa tuko nje. Mimi, Maalim Ahmed Humud, Mohammed Abdalla Gharib, Nassor Mohammed Nassor, vijana wengi…Maryam bin Breik, vijana wengine tulokuwa katika kamati. Tumekata shauri kwamba tuwaachie watu wa nje tu. Basi, wakaniweka ndani mwezi na kitu, mimi na Mohammed Abdalla Mohammed Gharibu Al-Oufy. Vijana hawakunyamaza alhamdulilllahi. Walipiga mbio huku na huku wakapeleka ma telegrams katika students unions zote za dunia ikawa telegrams zinakwenda kwa Gamal Abdel Nasser, na bakhti nzuri kulikuwa na mkutano wa Arab League. Tena kule wakatokea wale ma-leaders [viongozi] wa Arab League, King Hussein, Abdel Salaam Aarif, hawa wamesema kwamba OK, usiwarudishe hawa, sisi tutawachukuwa. Bakhti nzuri yule Abdel Salaam Aarif kamleta tena Waziri Mkuu wake kutaka twende Baghdad. Tukatolewa pale, tukapelekwa Baghdad.10

Wallahi kwa wakati ule tunavojuwa sisi kwamba wote walikuwa wana sympathize [wanatuonea huruma] kwa sababu yale mapinduzi yalivotolewa, lile tangazo lake, kwamba Waarabu wamewakandamiza Waafrika wamepinduliwa.

Ilivotoka duniani. Sasa Cairo wao hawakutaka kufahamisha, au sio hawakutaka, manake, sikusikia mimi kitu chochote kinachofahamisha kwamba hii kinyume na hivo, na ilhali hakuna katika Dola ya Kiarabu yoyote inayoijuwa Zanzibar na kifaah [mapambano] ya Zanzibar, zaidi kuliko Masri hakuna. Nakupa mfano tu. Ilifika hadi Karume katika mkutano wa kisiasa, uhuru wetu sisi hautotoka Cairo wala Accra. Kwa sababu kulikuwa na mahusiano mazuri na ZNP (Zanzibar Nationalist Party) na nchi zote nyingine za Kiarabu, na za Kiafrika zinazopigania uhuru. Na Afro-Shirazi hawakuwa nayo hiyo. Na Cairo ndo ilokuwa inasaidia nchi nyingine zote wakati ule kupata uhuru wao. Sasa sisi ilikuwa Wamasri au serikali ya Masri ilikuwa alal akal [angalau] iwafahamishe watu wengine hii serikali ya Zanzibar si serikali ya Waarabu, ni serikali ya wananchi wa Zanzibar na wananchi wa Zanzibar wako hivi hivi hivi.

Mimi nahisi kwanza, kuna mfano wa Kiarabu, ngombe akishaanguka visu vinakuwa vingi. Kwanza upande mmoja ZNP ilikuwa haipo tena. Wamehakikisha kwamba wameshaondoka, hawa jamaa wameshaidhibiti hali kisawasawa, mawaziri wametiwa ndani, Mfalme kaondoshwa, na hakuna ispokuwa hawa [ASP] kushirikiana nao. Najua kwamba Iraq walikuwa wanafahamu kwa sababu wale vijana wetu, wanafunzi waliokuwa wanasoma Iraq waliwafahamisha vizuuri na bakhti nzuri waliifahamu kwa sababu tangu hapo wao wanao mchango katika watu wao, Waarabu wa Kiiraqi walokuwako Zanzibar. Walikuwa wanafuatilia vizuri sana. Kwa hivo naona Iraq waliwahi hata kutaka kuleta jeshi lakini hapakuwa na mawasiliano. Wale National Guards wenyewe walijitolea as volunteers valantia.

Unajuwa wakati ule magaazeti yote ya Magharibi na ya Mashariki yalikuwa yakiunga mkono mapinduzi. Manake wale Makomred walikuwa wakiungwa mkono na nchi za Mashariki, na hawa wengine huku [ASP], wamekuwa wakiungwa mkono na Wazungu. Na magazeti ya Kiarabu ya wakati ule yalikuwa mara nyingi yananakili kila kitu. Maana yake, chochote ulichokuwa unakisoma wakati ule katika habari za Kiarabu zilikuwa zikinakiliwa kutoka kwenye magazeti yaliotoka Ulaya, makala za zamani sana. Nasser yeye alikuwa anayo idhaa lakini magazeti wana copy kutoka Associated Press (AP), lao walikuwa nalo moja ambalo halifanyi chochote.

Hakukuwa na mkataba wa kijeshi lakini kulikuwa, mimi sikuhudhuria katika mikutano yao ya siri, lakini nilikuwa nikiona wanaletwa vijana wa Kizanzibari kuchukuwa mafunzo kwenye mambo ya kijeshi. Na vilevile kulikuwa, na baada ya uhuru, kulikuwa na mipango imefanywa, kuja vijana kutoka Zanzibar kusoma fani za kijeshi za kila aina. Moja katika hizo ni jeshi la anga, navy, majeshi ya ardhi, na mimi mmoja katika hao nlikuwa nishapasi kwenda zangu Chuo Kikuu nikaambiwa la, wewe bwana serikali ya Zanzibar imekuteua kuwa wewe ndo utokuwa kiongozi wa jeshi la anga la Zanzibar kwa hio wewe jina lako namba one, tulizana kwanza, usende popote, ngojea mpaka itakapokuja listi kaamil, kopi ya list imeshaletwa, mpaka itakapokuwa tayari utaungana na wenzio, wewe utakwenda Jeshi la Anga. Kwa hivo Mohammed Faiq hakusema kweli au kakupa nusu habari. Na kabla Waengereza kukataa kuwapa himaya Wazanzibari ilikuwa huku chini kwa chini ZNP ilikuwa inao muelekeo namna huo.

Mambo kama hayo alikuwa [anayo] mwenyewe Sheikh Ali Muhsin. Yeye mwenyewe binafsi. Maana yake ndo alokuwa akija sana huku [Masri]. Na mambo mengine ya ZNP yalikuwa hayapitishwi penye ofisi yake Cairo kwa sababu ilikuja kujulikana kwamba baadhi ya vijana wepya wepya pale, wanakuja pale kufanya ujasusi na kuwapelekea habari. Kumbe wanajia yao. Tuliwahi kuwakamata watoto wawili watatu. Waliwahi kukamatwa namna hiyo na wengine wahai mpaka leo.

Lakini katika gurupu lilokuja mwaka 1958 kumekuja watoto wa scholarship tu. Na group moja watu wazee wenyewe na pesa zao wamewaleta watoto wao wamefuatana nao watizamwe wakae katika nyumba wanaotizamwa Wazanzibari lakini masomo yao wazee wao watalipa wenyewe.

Alikuwepo Ibrahim Omar, Masoud Makua, Usi Khamis ambaye yuhai mpaka leo, Ibrahim Omar nasikia tu yupo yuhai, mbali kuna Daulat Khamisi, mtoto wa Maalim Khamis Mandoa, hao wote si Waarabu hao, na wengineo na wengineo chungu nzima. Hakuna Mwarabu na imefanywa kusudi kwa sababu huyu Ahmed Rashad alisema “unaona hizo [nafasi za kwende kusoma], basi utaona watakuja watoto wa Kiarabu watupu!”

Alisema kabla yake. Na baadae alivowaona kina Yusuf Bahurmuz na nani na kina Thani wale watoto wa Kikumbaro akasema “sikukwambia unaona hao!” Akaambiwa hawa bwana wamekuja kwa pesa zao. Hiyo argument [hoja] inakuwa baina ya Ahmed Rashad na Seleman Malik. Seleman Malik ndo alokuwa rais wa maktab (ofisi) ya Zanzibar pale Cairo. Sasa ndo anatueleza, “huyu yakhe mtu hatari sana huyu!”

Nilijuwa kuhusu mapinduzi through BBC ya Kizungu na ya Kiarabu. Asubuhi na mapema. Kwamba kuna ghasia za mapinduzi Zanzibar na serikali imeshapinduliwa na hakuna upinzani Zanzibar nzima ispokuwa Malindi na Mfalme anatarajiwa kuondoka wakati wowote Zanzibar. Basi tena ndo tukaitana sisi, wale viongozi wakubwa wa umoja wa wanafunzi wa Kizanzibari. Baada ya hapo ndo tukaitana sote mkutano tukakata shauri twende kwa Sheikh Ahmed Lemky.

Nnaoweza kuwakumbuka ni Maalim Ahmed Humud Al-Maamiri, Mungu amrahamu, na Mohammed Abdalla Mohammed Gharib, Nassor Mohammed Nassor Al-Hadhrami, Mohammed Ali Muhsin, Mariam bin Breik, Salha Al-Mugheiri, Maalim Harith bin Khelef, ambaye sasa ndio Mufti wa Zanzibar, Masoud Rashid Al-Gheithi, Ahmed Sleman al-Gheithi. Tukakutana sote, tukakata shauri kwamba sote tukakutane na Balozi wa Zanzibar, Masri, Ahmed Lemky. Balozi alikuwa bado hata hana nyumba yuko katika hoteli. Tukenda hoteli, tukakutana.

Bwana Ali Khamisi [Jaribu] alokuwa Naibu Balozi na baadae Spika [wa pili] wa Baraza la Wakilishi (BLW) alikuwepo.11 Basi tukazungumza pale tukasema sasa tuyatizame nini la kufanya. Halafu usiku yeye [Ahmed Lemky] akatuchaguwa mimi na Maalim Ahmed Humud, na baadhi ya vijana, Muhammed Gharib, kwamba nyie njoni tukutaneni siri. Pale ndo tukapanga tena kwamba tujaribu kukutana na Mfalme, Sayyid Jamshid, na jamaa kuwa na mawasiliano na ndani. Jamshid alikuwa ndani ya meli, inakwenda ikirudi. Tena pale tukatafuta kila njia.12

Asirande tu ndani ya meli, wende Pemba aiuzulu ile serikali yake na afanye serikali ya Kipindi cha Hatari (Emergency Government) kwa mujibu wa nguvu za kikatiba alizokuwa nazo. Na kwa sababu Pemba ni 100% majority ni wafuasi wa ZNP na ZPPP kwa hivo, wafanye hivo. Tukatoka na mie nimepelekwa Mogadishu. Alopelekwa Mombasa ni Muhammed Abdalla Muhammed Gharibu. Tukenda.

Ikiwa Mfalme kafika Somalia niiombe serikali ya Somalia aje zake pale nionane naye mie nimpe fikra ile. Na alokwenda Mombasa Muhammed Gharibu anajuwana na watu chungu nzima kule jamaa zake wapo, wamfanyie mpango ende akaonane naye amwambie sisi tumetumwa na Ahmed Lemky na tunashauri hivi hivi hivi hivi. Somalia mimi nilikuwa na rafiki zangu wengi sana wamo katika jeshi. Tulikuwa nao skuli ya sekondari nimesoma nao Helwan [Masri]. Kwa hivo ilikuwa rahisi kwangu mimi kuwa na mawasiliano nao.

Nimetoka Cairo halafu Aden mpaka Mogadishu. Nilikwenda kwa ndege. Nimefika Mogadishu siku ileile nimeanza mawasiliano na nikawapata siku ya pili au siku ya tatu yake. Wamefurahi sana. Nakumbuka wao wakaniambia sisi tumeshasikia, sisi tuna wakubwa zetu, wakati wowote tunaweza kuja kukuchukua ukaonane na General Siad Barre. Basi wakanijia asubuhi siku hiyo wakaniambia haya yallah! Kavae upesi upesi twende zetu. Nilikuwa nakunywa chai wakaniambia wacha twende zetu. Wakanitia pale ndani ya gari moja kwa moja mpaka makao makuu ya jeshi. Nikawekwa ukumbini pale nikaitwa nikamkuta. Anasema Kiswahili kama mimi na wewe. Siad Barre. Akanambia yote unotaka kusema nshajuwa lakini ilobakia sasa hivi wewe unambie wewe tu. Akasema sisi kwa moyo wetu watu wa Somalia na hakuna wanayofahamu haya zaidi kuliko sisi. Kwa hivyo sisi tayari kwa lolote nambie nini nyinyi mnataka tu. Nikamwambia tunataka mutusaidie turudishe nchi. Kwa kifupi hivo. Vipi? Twende tukapinduwe! Mnao watu? Nikamwambia wapo vijana na ndani tuna watu wetu vilevile. Akasema basi, kwanza, mimi sitoweza rasmi kufanza hivo. Ikiwa tutafanya tutafanya kifichoficho na wapo vijana telee hapa askari wanasema Kiswahili kama mimi au zaidi kuliko mie. Tutakupeni hao. Hatupeleki mtu ambaye hajui Kiswahili lakini usafiri kutoka hapa kwenda Zanzibar hatuwezi kutowa sisi kwa vile Serikali haina njia nyingine. Lakini juu ya hivo ntakupa fikra toka wewe hapa nenda zako mpaka Kismayu.

Kismayu watu wote wanasema Kiswahili na kuna watu wana alaka nzuri na Sultan na wanampenda Sultan wenu kama sisi, na kaonane nao. Nani huyu bwana? Unamjuwa Seif Rizeiki? Baba yake! [Akanambia] akini usije ukataja kuwa una alaka na mie kwa mtu yoyote ispokuwa huyu bwana. Peke yake. Mwambie kuwa mimi nimekutuma. Mueleze hiyo kadhia yenyewe asijuwe mtu yoyote mwengine. Nikamwambia hakuna tatizo. Nikatoka mie nikenda. Sasa katika kuulizauliza kumbe mimi nafatwa na watu wa usalama wa Kisomali. Na bahati mbaya siku ile zilikuja ndege za Kikenya kupiga mipakani mwa Somalia. Sasa nyuso ngeni pale ni mimi nilioingia. Usiku akaja Seif huyu akanchukua akanipeleleka kwa Babake tukafuturu palepale Kismayu. Baada ya kufuturu akakaa pembeni, haya sasa nambie. Umejia nini? Nikamuelezea ile yoote kadhia tangu mwanzo mpaka mwisho. Akanambia kwanza nionyeshe kitambulisho chako. Nikamuonyesha. Nilikuwa na barua mimi kutoka kwa Ahmed Lemky akiwa ni Balozi wa Zanzibar yenye kusema: “Huyu ni mjumbe wangu mimi kwa yoyote atakayehusika na naomba apewe msaada wowote.” Basi akanambia sisi tayari na tunaijuwa Unguja na Pemba yake vizuuri na wapi pakushuka tunajuwa. Mimi nna watu wangu wanaweza kukushusheni kama mnataka Pemba, mnataka Unguja, popote pale. Na mimi nnazo jahazi kiasi 10 au 12 kanambia. Na zote ntakupeni. Nendeni mkafanye mipango mkiwa tayari nipeni habari tu. Basi, nikarudi mie , siku ya pili asubuhi, nataka kwenda kupanda gari kurejea Mogadishu, nikakamatwa!

Akanikamata yule askari kanzu, akanambia wewe jasusi. Nikatiwa ndani pale, ghasia moja kwa moja, nkamwambia mimi namtaka mkubwa wenu. Basi akaja mkubwa pale akanambia hapana, hakuna mmoja ataweza kukusikiliza hapa, atakayeweza kukutowa wewe, labda muhaafidh [Mkuu wa Mkoa] mwenyewe wa Mogadishu. Nikamwambia nnaomba basi kupelekwa. Yule ofisa aliniona mtu maakul kidogo akanipeleka mpaka kwa muhaafidh. Nikamwambia muhaafidh skiliza, mie nimekuja hapa kuzuru jamaa imetokea bakhti mbaya, basi akanambia basi sasa hivi toka nenda zako. Nikamwambia hakuna basi sasa hivi au gari. Akanifanyia nikapanda lori la polisi. Kunipeleka pale, mpaka Barawa, Barawa nipande gari mpaka Mogadishu. Nikarudi pale nkamwambia Siad Barre huyu mtu hivi hivi hivi. Akanambia sasa nendeni mkatayarishe, silaha tutakupeni sisi. Mufanye tektiki zenu mkiwa tayari nambieni.

Sasa Sheikh Ahmed Lemky, kanipa code barua kwa maneno mengine kumbe unakusudia mengine. Kanambia hii ndo ya kutumilia. Akanambia ukitaka kuwasiliana na mimi barua zako zipeleke Ubalozi wa Masri pale Mogadishu. Kumbe yakhe yule Balozi barua zangu zote alikuwa hakuzipeleka. Ama balozi au kule zilokokwenda hazikumfika Sheikh Ahmed. Alivonambia Sheikh Ahmed. Yeye kakaa ananlaumu mimi katika mkutano kwamba huyu bwana tumempeleka kule ameshapata watoto wanawake wa Kisomali kule wameshamrusha roho, hatuulizi kheri wala shari. Nimekaa mwezi mzima mimi. Ramadhani nzima nimemaliza kule. Nangojea jawabu. Kila nkenda kwa nanhi anasema hakuna jawabu, hakuna hivi, hakuna hivi. Mwisho nikaamua niondoke. Nikamwambia mie naondoka nakwenda Masri. Nikenda Masri.

Kwenda Masri, jamaa wakanambia wewe yakhe namna gani? Haikufika hata barua moja? Hata barua moja haikufika! Haiwezi kuwa. Basi twendeni sasa hivi. Ilikuwa usiku. Nikatoka palepale usiku nakwenda nikamkuta Ahmed Lemky na mkewe, na mtoto wa dada yake, wanatoka wanakwenda sinema. Nikamwambia Ahmed kwa hiasni yako bwana, mara moja. Akasema aa! Njoo kesho asubuhi maana yake nitawavunjia, unawajuwa wanawake. Njoo kesho asubuhi. Ukinambia sasa hivi na ukinambia asubuhi sawasawa. Kwa hiyo njoo asubuhi. Basi, mimi jamaa huku wakanambia, yakhe huyu bwana sie yule wa mwanzo, hakuna zile hamasa, na anasema umekwenda huko na sasa hivi sidhani kama ataukubali ushauri wako.

Mimi nikasisitiza lazima nikutane nae. Basi nkakutana naye nkamueleza yoote yale yamefika wapi, akanambia, lakini Mbarak hukutwambia chochote! Nkamwambia mie nimeleta, akasema, wapi bwana we! Unajuwa akaanza kufanya maskharamaskhara pale. Kunistihizai yaani. Mie nikasema maneno alonambia kina Maalim Ahmed kweli. Akasema basi si lazima sasa hivii. Huu si wakati munasib. Tena basi tukaishia pale, huu si wakati munasib, na bora tuanze tena, haidhuru japo ikichukuwa miaka khamsini. Katika maneno yalonivunja moyo ya Ahmed Lemky ni hiyo. Inahitajia mipango mipya…hakuwa na zile hamasa za mwanzo na kwa hivo mie, Maalim Ahmed akasema, haya, tufanye harakati ya ukombozi wa Zanzibar. Namwambia, kwanini hatuwi na contact [mawasiliano] na Ahmed Seif Kharusi na Sultan? Siku hizo bado hawajagombana bado. Basi tukafanya contact sisi na Ahmed Seif. Na tukawaita walewale vijana wale, wenye msimamo mkali wale, nkafahamisha sasa hivi ndo kama hivi, sisi hatuna mawasiliano na ndani, itabidi tufanye mawasiliano na ndani, nchi ziko tayari za kutusaidia. Kwa ukweli vijana wa Eritrea yakhe walikuja, wale wa harakati za ukombozi wa Eritrea, walikuja, wale tangu siku za marehemu Seleman Malik, alikuwa ni rafiki wa karibu wa Idris Kalaidos, amekufa maskini, mmoja katika viongozi wakubwa wa ukombozi wa Eritrea. Wao walikuwa tayari. Wanasema uhuru wa Zanzibar ni uhuru wa Eritrea vilevile, kama walivosema Wasomali.

Kwa hivo tukaanza tena upya. Tulipokuja kukutana tukasema lazima tuwe na kiongozi wetu hapa, mimi na wewe na nanhi, hapana anotujuwa sisi. Ndani ya Zanzibar wala duniani. Kwa hivo tutafute mtu wa kutuwakilisha, ama Mfalme, au Ahmed Lemky, au Ahmed Seif Kharusi tukakata shauri pale tumwendee Ahmed Lemky, tumwambie yeye atuongoze.13 Wakati huo ameshahama katika hoteli yuko kwenye fleti chini Midan Tahrir. Tukamwendea bwana. Tukamwambia yote hayo. Hayaa. Maalim katunga kijitabu kidogo kizuri kinachoelezea ile nukta tuliozungumza na wewe sasa hivi, ya kufahamisha, nini ZNP, na kuwa ZNP-Hizbu, si chama cha siasa. Ni harakati ya umma. Kwa hivo tukafanya hiyo, tukampelekea Sheikh Ahmed, kafurahi sana Sheikh Ahmed Kharusi, akakichapisha yeye, halafu baadae kitabu kilekile Ahmed Lemky kakifasiri akatia jina lake yeye kwamba yeye ndo mwandishi wa kile kitabu. Kakitafsiri kwa Kiarabu lakini. Kile cha kizungu cha Maalim Ahmed hakutia jina lake lakini kiliandikwa vizuri sana.

 

UAE Yawapokea Wazanzibari—Sheikh Mohammed Abdulmuttalib (Mutta)

Kwa hakika mimi mwanzo nilielewa hili suala la kuletwa silaha Dar es Salaam. Nililifahamu kama lilivokuwa likisemwa kwamba Ben Bella ameleta silaha kusaidia harakati za ukombozi pale Dar es Salaam, kwa sababu kilikuwa kituo cha harakati za ukombozi wa Afrika. Kwa vile kulikuwa na makao makuu ya harakati za ukombozi zilikuwa zikisimamiwa na Nyerere na Kambona, ambao wote wamefariki hao. Mimi nafahamu kwamba ile meli, MV Ibn Khaldun, ilifika Dar es Salaam tarehe 6 Januari 1964. Nilifahamu hivo. Linonifanya kufahamu zaidi ni maneno ya Ben Bella mwenyewe kutoka kwenye mdomo wake. Ilifika meli ya Algeria MV Ibn Khaldun imebeba silaha, ikasemekana kwamba ni mchango wa Ben Bella katika harakati za ukombozi. Sasa nakuja kuelewa Ben Bella zile silaha kazileta kwa lengo la uvamizi wa Zanzibar unotusikitisha ulotokea 1964.

Katika vitabu fulani fulani. Na miongoni ni kitabu nilichokisoma Al Hakika Al Zinjibar—Ukweli wa Zanzibar alikiandika marehemu Ahmed Lemky. Nikazidi kufahamu kumbe silaha lengo lake lilikuwa kusaidia harakati za ukombozi. Nyerere kazitumia, ambapo katika kitabu cha Bwana Ahmed Lemky amesema, silaha hizo zilipakiwa katika mashua ya shirika la uvuvi lilokuwa mwenyewe Myahudi maarufu akiitwa Frans Misha [Misha Finsilber]. Zikavushwa, ndo zilotumika katika mauwaji na uvamizi ulofanyika Zanzibar. Na hizo silaha kumbe zilikuwa Ben Bella kwa kukubali mwenyewe katika mahojiano ya magazeti baada ya kutoka jela, kumbe mwenyewe kasema kwamba kazileta kwa lengo la kumsaidia Nyerere katika kuondosha, kupinduwa, kumuondosha Sultan, anamwita Sultan Jair, yaani Sultan dhalim wa Zanzibar.

Ben Bella mahojiano hayo aliyafanya alipokuja hapa Emirates. Sasa kutoka jela, Sheikh Sultan, hakimu wa Sharjah, alimualika. Kamualika aje hapa kutembea kama ni mmoja wa viongozi wa Afrika, maarufu duniani, na maarufu kwa sote. Na sisi Wazanzibari nataka kusema, katika wakati wa mapinduzi ya watu mashahidi milioni ya Algeria, kumpinga mkoloni wa Kifaransa, katika nchi za Kiafrika, sisi, Zanzibar, ndo tulokuwa katika nafasi ya mbele katika kuunga mkono kadhia hiyo, kumuunga mkono Ben Bella na wenzake katika kugomboa nchi yao.14 Tulifanya maandamano, tukamlaani mkoloni wa Kifaransa, ndio nguvu tuliokuwa nazo wakati huo wa ukoloni Zanzibar. Tungelikuwa na uwezo zaidi tungelifanya. Imani yetu ilikuwa kubwa, na kadhalika napenda kurudi nyuma. Katika wakati ilipokuwa imehujumiwa Masri, 1956, Wazanzibari ni sisi tulokuwa katika watu wa mwanzo kufanya maandamano, na vikafungwa vitambaa veusi na kuonyesha msimamo wetu kuiunga mkono Masri, kwa mujibu wa mambo nilioyasoma katika taarikh/historia ya Zanzibar. Inasemekana pia marehemu Suleiman Badar, marehemu Muhsin Badar, na wengineo, walijitolea kwenda kupigana kuitetea Masri. Kinyume na tulivofanya sisi, yeye Ben Bella anatafakhari kwamba anakuja kuleta silaha, kusaidia kuuliwa watu kama sisi tulosimama na yeye.

Aliulizwa katika magaezeti suala hili la silaha. Akajibu akasema “naam nimefanya.” Alihojiwa na majarida kama skukosea, hili Al Khaleej lilioko hapa au kabla halikubadilishwa jina likiitwa Aazimiya Al Arabiyya, nafikiri mimi. Lakini muhimu alihojiwa. Akaulizwa suala hili khassa, akajibu, naam, nimefanya. Kwa nini? “Nimemsaidia Msoshalisti mwenzangu Nyerere.” Hivi ndo alivojibu. Akaambiwa, unajuwa kama waliouliwa ni watu na wengi ni Waislamu? Akasema “haijanikhusu, mimi nilikuwa namuondosha Sultan Al Jairu,” yaani, Sultani alokuwa dhalimu. Yeye Ben Bella kasema. Zikafanywa mbinu za kutaka sisi tuonane na yeye, yeye mwenyewe akakwepa, akakataa. Wakati ule wanasiasa wa zamani wa Kizanzibari walikuwa wapo hapa. Alikuwepo Dr. Ahmed Idarus Baalawi, alikuwepo Bwana Amani Thani. Sina hakika kama marehemu Sheikh Ali Muhsin alikuwa ameshatoka jela au bado kwa sababu nimesahau kidogo. Almuhimu, alikwepa manake na mimi niliambiwa nende, almuradi alikwepa, alikataa kuonana na sisi. Ilikua twende Sharjah, Emirates, ilikuwa nchi ya mwanzo iliomualika, Sheikh Sultan, alimuhishimu lakini kwa hakika halafu alimvunja moyo kila mtu. Kisha akenda zake Kuwait akaulizwa suala hilohilo akajibu vilvile katika jarida la Al Mujtamaa Al Balaagh la Kuwait, mhariri wake Abdurrahman Wilaayati. Jarida maarufu hilo. Jawabu alojibu huku [Emirates] akajibu kule [Kuwait] vilevile.

Zaidi alosema wazi ni Ahmed Khalifa Suwedi alokuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa United Arab Emirates (UAE). Katika kuzungumza naye jambo hili sku hiyo, alikuweko marehemu Hammuda bin Ali, Assistant Minister of State for UAE, alikuweko na Khilaf Said Al-Dhahiri, mkubwa wa uhamiaji wa UAE yotee. Siku hiyo tulikwenda kuzungumza matatizo ya Wazanzibari kuhusu sisi ukaazi wetu, hilo ndilo lengo tulioliendea. Tulionana nao hapo Sharjah. Ahmed Khalifa akasema, kwa hakika yalipotokea mambo ya Zanzibar nilikuwa mwanafunzi Cairo, ambaye sasa Ahmed Khalifa Suwedi ndo mumathil khaassa, mjumbe khassa wa Rais wa UAE, Sheikh Khalifa bin Zayed Al-Nahyan. Na ambaye kabla huyu huyu alikuwa ana wadhifa huo kwa Sheikh Zayed bin Sultan. Mmoja katika mtu shupavu, na alikuwa ni mtu mmakinifu, na ana sifa nyingi nzuri Ahmed Khalifa Suwedi.

Sisi tulikuwa tukililia suala la ukaazi wetu kwa vile tulikwenda pale kwa kuwa sisi watu wa Zanzibar, Jumuiya ya Kizanzibari. Sasa katika kuzungumza alisema kuwa, mimi nilikuwa mwanafunzi wakti ule. Abdel Nasser ndo alotupoteza katika kadhia hii, alitupoteza katika hii kadhia. Katueleza vengine kumbe tumekuja kuona mambo vengine, sivo vile tulivokuwa tumeelezwa na Wamasri. Hii ni kauli kaisema mbele yangu mie na Bwana Amani Thani yupo. Hii ilikuwa katika mazungumzo. Hakukuwa na mazungumzo kuhusu politics [siasa] za Zanzibar au haikuwa kuzungumza juu ya mpango wowote juu ya Zanzibar. Wakimbizi wa Zanzibar walioko UAE, nini khatima yao juu ya suala la uraia? Kwa sababu yeye ndo alikuwa ni mtu mwenye khatamu nyingi na mkubwa wa uhamiaji, alikuwepo na pia Waziri wa Mambo ya Ndani alikuwapo, marehemu Hammuda bin Ali. Katika mazungumzo, baada ya kumuuliza na kumueleza, na kama kususuika kwa msimamo wao, akasema, sisi msitulaumu, mimi nilikuwa mwanafunzi, tulikuwa hatujuwi, na akendelea kusema, sisi wengi mawazo yetu tulikuwa tukiiangalia Masri. Haya ndo maneno alokuwa amezungumza Ahmed Khalifa Suwedi. Sasa tukirudi nyuma huku sijui kama umeisoma ile ripoti ya shirika la kijasusi la Kimarekani CIA inayotoka kila baada ya miaka fulani. Na mimi naongeza vile kusema pia nimesoma, wavamizi wa kuivamia Zanzibar, wewe mwenyewe umeona. Na nafikiri umesoma kitabu alichokiandika mwenyewe John Okello Revolution in Zanzibar, kwa kuwa wao jumla walovamia, sote hatukuwa Wazanzibari.15

Nakumbuka kama skukosea, hotuba yake ilonukuliwa katika majarida [magazeti] ya Kenya yote, alipokuwa anarudi Korea, Moi Raisi wa Kenya. Palipokuwa na mgogoro baina ya yeye na Kanali Udongo, kwa vile Kanali Udongo yeye kabila yake ni Mjaluo. Aliporudi Moi Korea, kama sijakosea, 1992 au 1993, alimwambia, nyinyi ndugu zangu akina Kanali Udongo, mnapenda kujiingiza katika mambo, kila kitu mnajiingiza. Nyinyi mmejiingiza mambo ya South Sudan, nyinyi mmejiingiza mambo ya Uganda kumuweka Museveni, nyinyi mmehusika na njama za lile jaribio la kutaka kupindua Kenya, kisha akamwambia, na nyinyi ndo mlotumiliwa katika kuipinduwa Serikali ya Zanzibar! Haya maneno kayasema Daniel Arap Moi. Hakusema Mutta au mtu mwengine. Mchango wa nje ndio ulioleta kuja kuiondosha serikali yetu ya Zanzibar. Imezinduliwa kihalali tarehe 10 Disemba 1963. Dola ya Zanzibar. Haya yote nanukuu kauli mbalimbali.

Na alokuja akasema zaidi tulipokaa nae ni Oscar Kambona. Kambona kaeleza yoote, mipango yote ilofanyika. Kakubali yeye mwenyewe mbele yangu. Kakubali mbele ya Sheikh Ali Muhsin. Kakubali mbele ya Amani Thani. Kakubali mbele ya jumla ya watu. Hatukukusudia sisi tudhukuru majina ya watu woote. Tunataka ule ushahidi tu. Waloipinduwa nchi ni wageni. Kwamba na mimi pia, Kambona, naskitika sana nilikuwa na mchango wangu. Lakini sisi ndo tulopanga yale mambo, pamoja na Nyerere, na walokuja kuvamia nchi yenu ni watu wengine. Haya ndo maneno alosema hayati Oscar Kambona. Na nafikiri inafahamika kasema mara nyingi, kasema wazi na katika kuzungumza na watu.

Yote ukiangalia utaona inaskitisha, si fikra tulizokuwa nazo. Tulikuwa tukiona imetokea mapinduzi, kumbe kumetokea uvamizi. Khasa kwa vile sisi wengine tulikuwa wadogo, kama unavojuwa. Tumeona yale mambo, kwa hakika tumeona watu, lakini tulikuwa sisi kwa wakti ule ah! mbona huyu anasema Kiswahili chake cha kibara. Mbona hatumjui. Anatoka nchi gani huyu? Watu wageniwageni tumeona. Hata wengine wametuulia wazee wetu. Alokuja akamuuwa baba yangu mimi, kama unavojuwa, ni Kaujore ambaye kwamba si Mzanzibari. Alikwenda wazi kuwauwa watu watano msikitini buree! Mambo haya yanaonekana kwa ushahidi wa CIA, kwa kitabu cha John Okello, kwa ushahidi wa President Daniel Arap Moi. Ushahidi anosema mwenyewe Ben Bella na Kambona. Hawa ndo watu muhimu sana walotoa ushahidi kuonyesha kwamba yalotokea Zanzibar wao wametoa michango na zote zilikuwa kwa nguvu za kigeni. Mwenye hoja yoyote ataweza kuzielezea anavotaka yeye mwenyewe, azizungumze kama anaweza kuzungumza kinyume cha hivo.

Raisi Boumedienne katika utawala, unajuwa utawala wake ulikuwa kipindi halafu yake akafariki. Lakini kuhusu suala letu sisi, tulimuona Balozi wa Algeria kwa masikitiko makubwa, na nikamulezea vipi Zanzibar msimamo wetu na wao, na khatima waliotufanyia wao Algeria, na hii ndo hali yetu unatuona hii. Anaitwa, familia yao namkumbuka, Al Masoudi au Al Masoud, nafikiri karibu kafariki huyu bwana. Balozi wa mwanzo wa Algeria UAE. Ipo katika munasaba fulani fulani ilitokea katika pirikapirika inatokea siku ya kusheherekea kupata uhuru, mara itatokea kwenda kuwaamkia Mashekehe katika munaasabat fulani fulani, huwa tunazungumza nae sisi akavutika na mazungumzo, akasema, njooni tuzungumze ofisini. Tukenda tukazungumza ofisini kwake tukamuelezea yote. Akakaa kimya sku hiyo akatwita. Akatwambia skilizeni, haya tunazungumza baina ya sisi na nyie, yametokea hayo yametuskitisha sana na Boumedienne anayajuwa na ni jambo linalomtia uchungu juu ya msimamo kwenda kututia sisi katika taarikh, historia, chafu kama hiyo. Haya maneno namnukuu Balozi wa Algeria alotwambia maneno kutoka kwa Boumedienne. Msimamo alofanya sisi tunaujuwa na hata akatumia Boumedienne kama ni moja katika sababu ya kujiingiza mambo huyu Ben Bella yalokuwa hastahiki, ndio moja katika sababu sisi tumempindua. Kwa hiyo Boumedienne alilielewa sana suala la Zanzibar.

Boumedienne alikuwa ana hamu na suala la Zanzibar na alipata kuwajuwa watu mbalimbali wanaouhisika na suala la Zanzibar. Tukamwambia, mmoja anohusika bwana, na alotwambia sisi maneno ya ushahidi huo ni hayati Oscar Kambona. Huyo ndo atakupeni yeye maneno zaidi kafanya nini Ben Bella. Kambona akatakiwa aitwe, tukawapa njia wakamwita Kambona wakaonana naye. Akenda Kambona akaona nao wanohusika. Na katika jambo ambalo huyu Balozi akiskitika, akisema huyu Boutaflika anamtetea sana huyu Nyerere kwa sababu huyu ni katika watu alokuwa pamoja na Ben Bella. Ni jambo ambalo sisi tukiona unyonge. Hatufurahiki na msimamo wake huyu Boutaflika. Kambona walikutana na Boumedienne tena wakenda kivyao wenyewe.

Mimi nimekuja hapa Dubai 1966. Nimeondoka Zanzibar baada ya matokeo ya kuskitisha yalotokea na kadhalika matokeo ya kuuliwa babangu miezi minane baada ya kutokea matokeo ya kuskitisha ya 1964. Nimekuja kwa kuondoka kama ni mkimbizi. Kwa sababu baada ya kutokea mambo yale, ya kuuliwa mzee wetu sisi, Mwenye Enzi Mungu amrahamu, miezi minane au saba baada ya mapinduzi, uvamizi, mimi nliondoka nikenda zangu bara. Nikenda zangu bara kwa sababu mimi mama zangu watu wa bara. Mamangu mimi mama zake, wazee wake ni watu wa bara, Kilosa, Usagara. Ndo nikenda kwa wajomba zangu nikakaa nao watu wa kule, halafu yake, ikanibidi mimi lazma niondoke nikatafute mustakbal, Zanzibar ilikuwa hapakaliki sku zile. Nikaja zangu Zanzibar, nimefika Zanzibar sikukaa, muda mchache mara siku hiyo saa nane ya usiku, ilikuwa nimekaa barazani kwetu nyumbani, nafikiri kama tunavokaa majumbani pale barazani tunazungumza tunapiga masoga, nakumbuka kama nilikuwa na kijana mmoja, sahiba yetu jirani akiitwa Ali Nassor Falahi, nafikiri unamjuwa yuko Maskati, ndugu yake Muhammed Nassor Falahi and Ahmed Nassor Falahi. Tumekaa tunazungumza pale, mara akatokea mtu mimi nilikuwa sikumjuwa kavaa nguo za kiraia nikamjuwa kakake pale, nikamjuwa anaitwa Sergeant Kongo (CID) mimi mwanafunzi 1966 nna miaka kama kumi na tano kumi na sita. Kaja pale akankuta nimekaa, nilikuwa na kijichuma mkononi, akaja akanikamata na wenzake wawili, Sergeant Kongo, maarufu alikuwa. Akaingia ndani nyumbani kwetu na kunisachi mimi mwilini huku akinichochachocha kwa bastola na ilhali yeye alikuwa kalewa! Nini? Kwamba wamekuja kunkamata mimi wamesikia mtoto wa miaka kumi na tano nataka kulipa kisasi cha babangu. Ndo kosa langu na hata kama nilikuwa nataka kufanya kweli. Ndo nnakuja habari ya Dubai nakuelezea hapo yangu mwenyewe.

Nikaja nkachukuliwa pale nikapelekwa Malindi Police Station, nikakamatwa nikaambiwa huyu bwana tumemkamata, yaani mimi mtoto wa miaka kumi na tano, kumi na sita, tumemkuta kakaa barazani, tena tumepata ripoti kwamba anataka kulipa kisasi cha babake, manake babangu mie kauliwa na Muhammed Abdalla Kaujore, memba wa Baraza la Mapinduzi, ambaye anatoka bara. Hii haikuwa ghasia huyu ni memba wa Baraza la Mapinduzi, ni mtu wa serikali, ni kama Waziri. Kaja kufanya kitendo hicho. Hakikufanywa na watu wahuni tu. Mimi nikistaajabu yale mambo, manake yale mambo yenyewe sielewi. Tangu hapo sijifahamu katika hali ya mambo yalotokea Zanzibar yale, halafu kuuliwa babangu.

Manake hatujijuwi tumetawanyika. Halafu tena kinatokea kitu kama kile. Naona jambo kubwa saana. Hatari kubwa hii! Watakuja kuniua maana yake kazi yao ilikuwa kuuwa tu. Sasa pale baada ya kukamatwa, wakawa wanaandikaandika wale polisi wakawa wanazungumza, wanasema “Kama huyu, huyu mtoto mdogo, kuna ushahidi gani?” Wenyewe kwa wenyewe. Wakasema tufanyeni hatutaki balaa. Tutamngoja bwana mkubwa asubuhi, yaani siku zile usiku wa manane ni usiku mkubwa Zanzibar. Nkakaa pale nkawekwa kituo cha Malindi mpaka asubuhi, kesha nkapelekwa, kuna mahkama. Ilikuwa mahkama hiyo ilikuwa primary court ikiitwa. Ilikuwa korti yenyewe waliiweka pale ilipokuwa ofisi ya Bwana Soud Ahmed Busaidi. Pale ilikuwa imewekwa mahali ilikuwa imefanywa kama mahkama hivi. Basi asubuhi mimi napelekwa kwenda kushtakiwa kwamba nataka kulipa kisasi cha babangu alouliwa buree! Watu watano na mtoto mdogo waliuliwa msikitini Zanzibar. Katika hao na watu wawili walijeruhiwa. Siku nlopelekwa mimi nikamkuta na marehemu Maalim Juma Himidi wa Darajani School. Tulikuwa pamoja na wengine siwakumbuki. Na alikuwa jaji wakti ule yule jamaa akiitwa Haji, sijui nani, ni mtu wa Kizanzibari, mamake alikuwa Hizbu mmoja mkubwa, lakini huyu alikuwa Afro-Shirazi mkubwa. Akaitwa Maalim Juma Himidi, alianza kabla yangu mimi au baada yangu mimi, almuhimu mimi nikaitwa. Yule bwana Haji akaulizana na wenzake. Ndo mambo gani vipi hivi? Alishangaa yeye kuona mambo yale. “Toka nenda zako nyumbani. Mbio!” Na mimi nyumbani ndo palepale. Nkazidi kuingiliwa na vitisho. Nkaona bora niondoke haraka.

Sasa mimi ndo nnasafiri kutoka Zanzibar. Mimi nikaondoka Zanzibar baada ya matokeo yale, nikasafiri nafikiri tarehe naikumbuka. Nimeondoka Zanzibar katika tarehe 19 Julai 1966 kwa meli ya Karfuyes. Tulikuwa majmua ya watu. Kundi letu sisi alikuwako Sheikhuna, bila ya shaka unamjuwa, alikuweko Muhammed Seif Barwani, Ahmed Ishti, Said Seif Riyami ambaye yeye ni mmoja katika wakuu wa Polisi Oman, unamjuwa wewe mwenyewe, ndugu yake Abii Seif. Khalfan Hilali. Yaani jamaa wengi sana waliingia ndani ya meli hiyo. Wengine Zanzibar, wengine wakapandia Mombasa iliposimama.

Ilikuwa kitu maarufu wakti ule watu kufahamu maudhui yetu. Wakawa wanatuonea huruma. Wengine hujificha chini ya pango chini. Kuna wengine kama unavojuwa taabu walioipata. Waliingia kwenye mavi ya ngombe. Wengine wakafa njiani. Tuliingia kwa njia ya bandarini. Tuliogopa zaidi tusije tukakamatwa na askari wale wa Karume pale. Wale waliokuwa katika meli wakituonea huruma kusema kweli. Kuna wengine waliingia walikata tiket mpaka Mombasa. Sisi nafikiri tulikuwa hatupungui ishirini. Muhimu chombo kikenda na muhimu tumefika Dubai. Mwezi huo huo wa Julai 1966 tulifika Dubai. Tukafika Dubai. Kufika bandari. Kwa hakika si bandarini. Kulikuwa hakuna bandari wakti ule 1966. Tumefika tumesimama mbali sana hata Dubai hatukuoni manake Dubai bado ilikuwa hakuna maendeleo ya leo. Mbali sana hata hatukuoni. Tukakaa zaidi ya saa moja. Mara ikaja boti. Kwa mbali tunaiona inakuja hiyo, hiyo, hiyo, hiyo. Katika boti akateremka mtu Mwarabu, nimekuja kumjua baadae, tumejuwana, akiitwa Rashid Matrushi, mmoja katika maofisa wa Idara, nafikiri ilikuwa ya bandari au idara ya paspoti. Akapanda ndani ya meli na maaskari walikuwepo pale wa Kidubai. Akasema Wazanzibari wasimame upande mmoja. Tukasimama. Akasema hawa kwa amri ya Sheikh Rashid na bila ya kikwazo chochote wateremke nchini. Huo ulikuwa ni ujumbe kaleta mwenyewe marehemu Sheikh Rashid bin Said Al-Maktoum, Mungu amrehemu na amuweke pahala pema.

Sie tukateremka rasmi. Tukashuka nchini kila mmoja tena akatafuta njia yake. Dubai muhimu nilipofika mimi nimekuta jamaa wameshasimama, wameshaunda jumuiya ya kusaidiana. Nimeyakuta tayari kabisa. Ishaundwa Association. Na hapa nna barua ambayo kwamba alipelekewa Sheikh Rashid ya tarehe 13 July 1964 ilotiwa saini na Bwana Ali Masoud Thani ndo aloanzisha jumuiya wakati ule ndo aloandika barua. Mwanawe yule alokuwa Cairo, Masoud Ali Masoud Thani. Marehemu babake ndo alotia saini barua hii akampelekea Sheikh Rashid, baada ya kumuamkia kumwambia nakuletea hii barua kwa niaba ya Wazanzibari walokimbia baada ya kile kinachoitwa mapinduzi ya kibaguzi. Tunakuja kwako kutaka himaya na kutaka msaada. Nia yetu ni kuasisi sisi jumuiya ya khairiya chini ya uangalizi wako ili kusaidia wale watoto walobaki kule watakapokuja huku. Hatuwezi sisi hii jumuiya kuiunda bila ya kutaka muwafaka wako. Na napenda kukujuulisha tunataka utupe muwafaka wako ili tuweze kuiasisi jumuiya hii ya khairiya. Na kadhalika anamwambia katika barua hiyo, British Resident [Balozi wa Kiingereza], anajuwa hayo na yeye hana kizuizi chochote kuundwa jumuiya hii. Tunaomba utupe rukhsa ili jumuiya hii iwe inasema kwa niaba ya Wazanzibari wote. Hii ndo barua. Sheikh Rashid barua hii hii akaandika “La mania ladayna.” Sina pingamizi kuunda Jumuiya ya Wazanzibari.

Jumuiya hii iliundwa. Ilikuwa na Katiba yake na vipengele va Katiba viko vingi lakini katika lengo kuu ilikuwa ni kuwapokea katika makaazi mepya Wazanzibari hapa katika nchi walotuchangilia hapa Dubai. Na katika mwaka 1965 alikuja Mtukufu Mfalme wetu Sayyid Jamshid bin Abdullah, pamoja na marehemu Bwana Ahmed Seif Kharusi. Kaja Mfalme wetu kuja kumshukuru Sheikh Rashid kwa mapokezi ya kuwapokea wakimbizi wa Kizanzibari. Katika kumshukuru, pia kumuomba, na kumtafadhilisha, awe raia zake ni kama amana, yeye awatabir kama ni raia zake. Awachukulie kama ni raia zake. Sheikh Rashid Mungu amrehemu, alilipokea suala hili kwa furaha kubwa sana na akakubali kama sisi ni amana kwake. Na ndo mpaka leo hii ndo sisi tumekaa hapa. Sasa Mwenye Enzi Mungu, Sayyid Jamshid, Mungu ampe umri mrefu Mfalme wetu nasema tena, na namshukuru na namuombea dua daima Sheikh Rashid Al-Maktoum, na wanawe watukufu, ambao hatuna fadhila za kuwalipa. Baada ya sisi kuwa tumetoka kwetu, tumenyanyaswa nchi yetu wenyewe! Tumefukuzwa, tumenajisiwa, tumenyanganywa kila kitu. Kwetuu! Tumekuja kwa watu wageni wasotujuwa wametupokea, alhamdulillah Mungu awajazi kheri.

Baada ya hapo mimi niko hapa nikendazangu kusoma Qatar, na 1966 mwaka huo huo nkenda zangu kusoma Kuwait na Kuwait wakitoa scholarships [nafasi za kusoma] khasa kuwasaidia wakimbizi wa Kizanzibari. Alofanya jambo hili, alolisimamisha Mungu amrehemu na amlaze mahali pema, ambaye hatuna fadhila za kumlipa, Bwana Ahmed Lemky. Yeye ndo alokuwa balozi wetu wa kwanza kuteuliwa baada ya kupata uhuru wetu Zanzibar, wa halali, tarehe 10 Disemba 1963. Alikuwa Balozi huko Masri. Na kama unavojuwa, Zanzibar ilipopata uhuru ilijiunga na Umoja wa Mataifa kuwa ni Dola kamili na tulikuwa na ofisi kama unavujuwa, na vilevile na Cairo, na ilikuwa Zanzibar inaendelea kufungua ubalozi Indonesia ambako aliyekuwa Rais Ali Hassan Mwinyi ndie angelikuwa Balozi wetu Jakarta, lakini bahati mbaya Dola ya Zanzibar ikaanguka.

Na kadhalika vilevile Qatar ilitowa scholarships kwa njia ya huyu huyu Bwana Ahmed Lemky. Baadae nikashika mimi nafasi ile kuhusu scholarships za Qatar. Na Bahrain, Arabian Gulf University ilichukuwa watoto wetu wa Kizanzibari, mbali kutoka Zanzibar Association. Na kadhalika hatuitoi kwenye shukurani serikali na watu wa Iraq ya wakati ule. Walitusaidia sana. Tulikuwa na wanafunzi mimi nafikri wanafika mia tatu! Kuwaonea huruma kwa kibinaadamu watoto wetu wakasomeshwa. Tunashukuru sanaa! Tunazishukuru pia nchi mbalimbali zilizosimama na sisi. Saudia Arabia pia ilitusaidia kwa upande wa kibinaadamu vilevile.

Sasa kuna kitu muhimu sana baada ya hiyo Association yetu kuundwa Dubai. Jumuiya hii ilitambulikana na United Nations High Commission for Refugees (UNHCR) ambayo ilisimama na sisi na kutusaidia sana! Hata ndio msingi wa kusimamishwa majengo ya Kizanzibari ya hapa Rashidiya, Dubai. Iliasisiwa khasa fikra hii, kweli walitoa Zanzibar Association, lakini ilikuwa UNHCR, alikuwepo muwakilishi Bwana Gubia, aki deal [akiwasiliana] na sisi. Yeye nafikiri ndo alokuwa mjumbe wa UNHRC, nafikiri katika Mashariki ya Kati, kwa wakimbizi wa Kifalastini na sisi Wazanzibari nafikiri. Na Bwana Gubia kwa upande wake United Nations ikawa tukapata scholarships sisi watu wetu wakasoma Libnani, Lebanon. Njia ya huyu UNHCR. Baada ya Gubia wakaja watu wengine tena wanohusika, tukaendelea nao. Na kadhalika vilevile mimi vile msimamo wangu walivoniona jamaa wa kuwasaidia wenzangu na kujuwana na watu kidogokidogo wakapendelea mimi niingie katika Jumuiya ya Kizanzibari. Nilikuwa mgumu sana, sikukubali kuingia kwa sababu ni kitu kipya kwangu mimi. Kuna kazi ngumu. Basi mwisho wakamtumilia marehemu ndugu yangu Hashim ambaye yeye ndo alonchukuwa mimi toka udogoni kuja hapa. Kama babangu alikuwa. Akanilazimisha mie nikaingia Kamati ya Jumuiya kama ni memba. Ndo nlivoanza. Haukufika muda mkubwa nikachaguliwa Raisi wa Jumuiya ya Kizanzibari na nikazidi kufunguwa mawasiliano sehemu mbalimbali. Tulilazimika kwa vile Wazanzibari walikuwa wametawanyika kwenye nchi zote za jirani ya Dubai. Bila ya shaka msimamo wa viongozi wengine wa UAE, Mfalme wa Sharjah, Mfalme wa Ummu Qulwein, kote, tunashukuru. Abu Dhabi. Kote tunashukuru.

Hii Zanzibar Association baada ya kuingia mimi tukazidi kutafuta sehemu za kuweza kusaidia watu wetu, na katika Al Aalam Al-Islami, ulimwengu wa Kiislamu. Tumejaribu zaidi sisi kutafuta njia katika jumuiya za kibinaadamu na nyingine zilikuwa zina nguvu za kututetea na kutusemea. Sisi tukawa tunafanya kazi na Zanzibar Organisation ambayo ilikuwa ni organization ya kisiasa. Sisi kwa upande wa kibinaadamu tumeshirikiana nao khususan wale watu wetu walokuwa wakionewa bure na hawajulikani kama ni hai au maiti. Tukawa vilevile tuna deal na Amnesty International, shirika maarufu la kupigania haki za binaadamu duniani na kuwa tunashirikiana na Human Rights Association Organisation.

Na kadhalika vilevile Zanzibar Association ilitambuliwa rasmi na World Muslim League ya Saudi Arabia. Kudhulumiwa watu wetu wa Zanzibar bure, walikuwa wakifungwa na dhulma zilozokuwa zikipitikana, kama zile ndoa za nguvu, za kuuliwa watu kiholela, au kunajisiwa watu kwa nguvu. Haya yote yalipita na yalifanywa na watu wenye nyadhifa zao. Ni mambo ya kuskitisha. Walishirikiana wote pamoja na Nyerere vilevile. Na Nyerere angeliweza yeye kumwambia Karume alipolizuwia gazeti la Uhuru Zanzibar, haya maneno sasa namnukuu Oscar Kambona, narudi nyuma samahani…Kambona anasema Othman Sharifu alipokuwa Ubalozi wa Tanzania Washington, D.C. na Hanga alikuwa kama Balozi kule Guinea. Karume kawataka hawa na lengo lake lilikuwa anataka kuwauwa kwa sababu Karume walikuwa maadui zake hawa walokuwa wale Afro-Shirazi wazalendo. Mimi nikamuuliza Kambona, kwani Afro-Shirazi wazalendo ni nini? Namuuliza Kambona katika mazungumzo., anatuzungumzia sisi. Anasema Afro-Shirazi wazalendo ni wale walokuwa Wazanzibari wenyeji. Anasema, samahani leo nakwambia hivi. Anamuogopa Othman Sharifu, anamuogopa Hanga, wale walokuwa wasomi. Ndo maana alitangulia kuwamaliza kina Twala, Saleh Saadalla Akida, Mdungi Usi.

Hawa walikuwa tishio kwake na khususan kuwa wamesoma na wana msimamo. Alipowaita akina Hanga ilikuwa ni katika mpango wa kutaka kuwauwa. Hanga alivoitwa, anasema Kambona, alimwendea Ahmed Sekou Toure, akamwambia naitwa na mimi nachelea nikiitwa ntakwenda kukamatwa niuwawe wakati mimi ni Balozi. Akasema, hakukasir Sekou Toure, almuradi akampigia simu Nyerere na akaandika barua, kuwa huyu anakuja, chukuwa dhamana kama kuna wasiwasi wowote wa kuuliwa na kama anakosa ahukumiwe kwenye vyombo va kisheria. Nyerere akamjibu kwa barua, kuwa dhamana mimi, basi aje Hanga na sitompeleka Zanzibar. Hatouwawa. Kadhalika Othman Sharifu.

Wao wakaja zao, Kambona akapata habari. Anasema yeye alikuwa hayupo, alikuwa Mwanza au sijui wapi, lakini tena Othman Sharifu keshavishwa nguo za jela na kanyolewa kipara na ndege ishaletwa kutoka Zanzibar. Anasema, nkatoka nkenda kwa Nyeyere. Nkamwambia, Mwalimu, kama unataka kumkamata huyu, kwanza ujuwe huyu ni Balozi, aachishwe wadhifa huyu kwanza. Akamjibu kwamba mimi siwezi, Karume kamtaka. Akamwambia Karume kamtaka huyu na Hanga lakini wewe si ulimuahidi Sekou Toure hutawapeleka Zanzibar? Akamwambia, lakini Mwalimu, Karume ulipoandika makala na haikumpendeza alisema Karume kuwa yeye atavunja Muungano ikiwa utataka gazeti la Uhuru litaingia Zanzibar, itakuwa gazeti bora kuliko roho ya mtu? Kambona anasema haikuwa lolote isipokuwa aliwapeleka Zanzibar.

Hiyo ndio hali ilivokuwa. Sasa mimi nimezungumza kirefu kwa bahati mbaya lakini kuna mambo na nimerukia hili, lakini Zanzibar Association ilikuwa ikiendelea. Iikuwa ikifanya kazi zake za kibinaadamu. Ilikuwa ikisimamia watu kupata scholarships kwenda kusoma. Ilikuwa na haiba na heshma yake sehemu za Gulf. Pakitokea popote matatizo ya Wazanzibari ilikuwa mie nakwenda kwa vile mie nilikuwa Raisi wa Jumuiya, naonana na authorities [wakubwa], wanatusaidia wakubwa wa nchi, wafalme. Kote huko, Saudi Arabia mpaka Bahrain.

Kwa mfano kadhia moja inanikumbusha msimamo wa Bahrain. Nasrin unamjuwa katika wale walioolewa kwa nguvu. Baada ya kuwachiwa, bila ya shaka baada ya pressure [shinikizo] kubwa alofanyiwa Nyerere. Wakafunguliwa, wakatoroshwa. Nasrin maskini alikuwa hajui afanye nini. Kaja zake Dubai, hana visa, hawamjui airport, mimi nilikuwa nimesafiri, ikabidi ende Bahrain. Bahrain marehemu Bwana Salim Slim, Mungu amrehemu, akawaelezea kuhusu mtoto wa kike kuwa hana visa tumteremshe hapa, ikaelezewa kadhia yake. Watawala wa Bahrain kwa ubinaadamu wa Al Khalifa, Mungu amuhifadhi, walisimama wakamsaidia mtoto. Mimi nilipofika nikasikia. Kupata habari yake nikachukuwa nyaraka zote na magazeti na kila kitu nkenda kwa Sheikh Rashid Mungu amrehemu. Nikamwambia Sheikh Rashid nimekuja kwa kadhia hii. Akanambia nenda kwa Sheikh Muhammed bin Rashid ambaye ni Ruler wa leo wa Dubai. Sheikh Muhammed akasema nipitie usiku. Nikampitia usiku nikamuelezea, hakukassir, hapohapo akatoa amri akifika ateremke kwa amri yake. Jinsi walivokuwa na huruma watu hawa. Huko kwetu viongozi wetu wanatuuwa, wanatunyanyasa, hawa wametuonea huruma jamani. Nasrin unajuwa, mtoto wa miaka kumi na tatu, kaozeshwa kwa nguvu kwa bunduki! Haya, akaletwa Nasrin, nikapelekwa mimi mpaka kwenye mlango wa ndege kwa amri ya Sheikh, nikamteremsha akapata fursa kukaa nchini. Hii ni kadhia moja tu katika kadhia nyingi za kibinaadamu ambazo Association ilikuwa ikipigania kuwapigania watu wetu katika nchi hii.

Hapa kwa hakika hadithi ya Zanzibar Association ni hadithi ndefu sana kama unavojuwa. Hadithi ndefu sana. Kuna mengi yamefanyika katika Association ya kibinaadamu, na misimamo mingi ya kiungwana imesimama, inajulikana. Association ilikuwa ni kitu muhimu sana kwa Wazanzibari, la ingelikuwa hakuna Association Wazanzibari wangelikuwa wamesambaratika. Mimi naeleza Zanzibar Association ilikuweko, bila ya shaka ilikuwa ni kitu, sijui wanakiona vipi Watanzania, walikuwa wakifasiri Serikali kama ni tishio kwao ilhali sisi mambo yetu yote yalikuwa ni ya kibinaadamu tu. Ilikuwa wanaona kuwa ni aibu kwamba kuna Association ilotambuliwa na United Nations High Commission for Refugees. Jambo hili lilikuwa likiwauma saana! Wakiona ni matusi kwa Dola yao. Kama ni aibu kufedheheshwa, kutoka aibu zao mambo waliotufanyia. Dhulma waliotufanyia wakti ule.

 

Zanzibar Association kwa hakika sasa haiko tena. Kutokuweko kwake hakuna alaka na kuweko kwa Tanzania Association. Ni vitu viwili mbalimbali nnataka kukueleza ufahamu. Baada ya kufa kwa Jumuiya ya Kizanzibari ikafunguliwa hiyo Jumuiya ya Watanzania, ukafunguliwa sasa na ubalozi Abu Dhabi. Ilifunguliwa Tanzania Association si kwa kuwa kuja kuichukuwa Zanzibar Association.

Zanzibar Association ilikuwa imeshakufa. Ishauliwa! Tanzania Association inakuja kwa mujibu wa Katiba ya Nchi na Katiba yao. Juzi Tanzania Association wamefanya futari, wametualika sote, bahati mbaya mimi sikupata gari lakini nilialikwa. Kenya Friendship Association tunaalikwa tunakwenda.

Mpaka sasa hivi hakuna mgogoro khassa. Imefika wakati hakuna mgogoro kwa sababu upande wa pili [Zanzibar] hakuna tena. Zanzibar Association haiko tena lakini nataka kukwambia kitu kimoja. Sisi tulipokuwa na Association, tulikuwa sisi hapana haja ya kufanya ugomvi kwa sababu tukiwachukuwa ndugu zetu, kutoka Tanzania, madam ndugu zetu kutoka Dar es Salaam au kutoka Kenya ilikuwa sisi tukiwasaidia na wanajuwa wenyewe. Tulikuwa na memba sisi wa aina hiyo tena wengi na si wa kutoka Zanzibar tu. Na katika Katiba ya Association Coastal Strip [Mwambao] imo lakini sisi tukazidi kuomba zaidi tukakubaliwa tukawatia hao wenzetu kutoka Dar es Salaam na nini na nini. Si sisi kwa sisi? Sisi ndugu ati. Sote sisi ni ndugu. Kisiasa kitu kingine, wendawazimu wa kisiasa na wazimu wao, walokuwa na akili wataendesha vizuri. Ikiwa wendawazimu wataendesha mambo kiwazimu. Sisi yapo mahusiano. Saudia imeshafungua Ubalozi Dar es Salaam, na Tanzania imefunguwa Ubalozi Saudia. UAE ina Ubalozi Dar es Salaam, Dar es Salaam ina ubalozi huku [Abu Dhabi] vilevile kama unavojuwa.

Msimamo wa Omani kama unavojuwa masala ya Wazanzibari kwa jumla, sasa mimi nam quote Mfalme Mtukufu wa Oman, Sultan Qaboos bin Said. Alipoanza kuja katika utawala na khatamu za utawala, alifanyiwa mahojiano, kama sijakosea lile jarida zamani likiitwa Al Hawadith, alifanyiwa mahojiano ilikuwa makala jarida lote Qaboos tu anaelezea. Lote! Nakumbuka kile kifungu alichoulizwa nini maoni yako juu ya kadhia ya Wazanzibari na kadhia ya Zanzibar? Nakumbuka hivii. Sultan akajibu kwamba hii ni kadhia ya kibinaadamu, si jukumu linalotukhusu sisi Oman, bali linakhusu ulimwengu mzima na nchi za Kiarabu zote. Hii ndo jawabu alojibu Sultan Qaboos bin Said.

Sayyid Khalifa bin Haroub akizungumzia katika miaka ya 1920 au 30 kuhusu ndoto yake ya kutaka kuona nchi za East Africa zinaungana kama United States of America. Kama kawaida yake Sayyid Khalifa, ulikuwa utawala wake, sio kama wanavosingizia watu, sisi ndo tulikuwa wa mwanzo tulosema juu ya masuala ya muungano. Wala isimpitikie mtu kama labda sisi Wazanzibari tunaupinga muungano. La hakuna anayekataa Muungano. Nani anakataa Muungano? Lakini mambo yende kwa kidesturi, kuheshimiana, si kukandamizana na kunyanyasana. La. Na haya mambo ya kufanya East African Community, mchango wa watu wa mwanzo toka wakati wa vuguvugu la ukombozi walisimama kina marehemu Sheikh Ali Muhsin na wengineo, walikuwa akina Tom Mboya. Wazanzibari ndo walokuwa katika mstari wa mwanzo. Hakuna mtu alopinga. Kinachopingwa ni unyanyasaji. Kama kwamba sisi tumekutekeni! Kutufanyia kejeli. Ndo jambo lisilotakiwa. Sisi si tanguwapo tumeungana? Si mimi nimekwambia mamangu Msagara? Na wangapi na wangapi walikuwa wengine wazee wao Wanyamwezi, Wazaramu, tumechanganya damu sote. Na hili suala la kutia fitna, sijui utumwa, sijui kitu gani. Hili suala bwana limefanywa na kabila moja tu? Walikuwa Waafrika wakiuzana. Iwe kosa wamefanya watu walokuwa Waislamu tu? Ndo iwe kosa. Uchafu wote walofanya wengine walokuwa si Waislamu wamechukuliwa wametupwa na kusahaulia na wamekumbukwa Waislamu tu. Makabila yanajulikana ya kibara, wa kabila fulani walikuwa watumwa wao fulani, na kabila fulani walikuwa watumwa wao fulani. Yote yanajulikana hayo. Waafrika kwa Waafrika.

Mie ntakuelezea kisa. Nilipokwenda zangu bara mimi huo mwaka 1966, nilipofika mimi nkawaona wazee wangu, mjomba wangu Habibu nikamuona, nkawaona bibi zangu kina Biti Kinyamare, Biti Farahani, wazee wetu wengine kina Mjomba Kibwana, na hao wengine tulikhusiana nao kina Mwinyi Kondo, na nani, kwenye ukoo wa mama yetu. Kina Khamisi Mrisho. Sasa siku hiyo nkaambiwa nitapelekwa kwenda kumsalimia bibi yetu. Anakuwa upande wa babake bibi yetu Biti Kinyamare na Biti Hogore katika daraja ya wazee. Nikatoka mimi nikapelekwa siku hiyo. Biti Hogore siku hizo alikuwa ana uwezo. Biti Hogore alikuwa mtu mzima nilipomkuta wakti ule. Ameshafika 70 na kitu. Nikenda zangu, kumsalimia. Nyumba yake ina uwa mkubwa. Kakaa kwenye kiti, kashika bakora, na mapete ya dhahabu kwenye vidole, na kajifunika kanga. “Karibu mjukuu wangu.” Nikenda kumbusu mkono, nikamsalimia. Nilikwenda mimi na mjomba wangu Habibu, na Bibi Kitimare, ndugu wa mama yangu marehemu. Hapa nataka kukueleza kitu. Akatokea bibi mmoja sikumbuki kama nimekosea jina, kama akiitwa Biti Nyama. Huyo bibi mkubwa kuliko Biti Hogore. Huyo bibi mimi nasema alikuwa thamanini na kitu. Anakuja pale. Mimi nainuka kwenda kumsalimia yule Bibi, Biti Nyama. Tabia yetu Wazanzibari, tunamsalimia mtu yoyote. Hakuna ubaguzi. Nikazuwiliwa “kaa kitako!” Nikashtuka. Nikakaa kitako mie. Yule bibi akaulizwa, “unamjuwa huyu?” Akatizama, “huyu kama sura za Biti Muhamedi naona.” Nikaulizwa, “unamjuwa huyu bibi?” Nikasema “bibi ni bibi.” “Huyu ni mtumwa wenu!” Msagara, hawa ni Wasagara. Waafrika kwao Kilosa. Wasagara na Waruguru ni bin ami lazima ujuwe.

Mimi bwana nkwambie nilishtuka kwa sababu kule Zanzibar nasikia utumwa lakini hatujauona utumwa wanaousema. Huyo mwenye kuusema hajauona. Utumwa, sijui nini, Waarabu! Sasa mimi nnasema, bibi zangu mimi, hawa si Waafrika? Mbona yule mtumwa wao? Nikamuuliza mjomba wangu Habibu. Kwani bibi zetu Waarabu? Akanambia hata. Waafrika, Wasagara. Ndo nkaanza kufahamu sasa. Wana watumwa hawa Wasagara Waafrika nao huku Nyerere akituambia “Waarabu!” Karume akituambia “Waarabu!” Kumbe watumwa wako Waafrika kwa Waafrika, sisi wenyewe upande wa mama yangu Wasagara, mimi bibi zangu Wasagara. Bibi zetu wenyewe ndo hao Waafrika. Hadithi yangu mwenyewe.

Tunasikia mvutano uliokuweko huko kwetu sasa hivi juu ya suala la Zanzibar, na jambo ninaloliomba wakae chini wazungumze. Fujo haitoleta kheri. Wakae chini wazungumze, wahafamiane namna watakavotekeleza. Haiwezekani kwani ni kweli Zanzibar ilikuwa ni Dola. Ilipata uhuru tarehe 10 Disemba 1963. Ilikuwa memba katika Umoja wa Mataifa. Ni jambo ambalo haikutangaza Umoja wa Mataifa wala haikuandikwa barua itolewe na mpaka leo haikutolewa. Yamefanywa mambo kiholela tu. Walivoingia Muungano, kila mtu anaulezea, mimi nasema si wa halali. Almuhimu ni kwamba huu si wakati wa kuendeleza migogoro. Huu ni wakti wa kusikilizana. Tusitafute mambo ikawa kama Ruwanda, ikawa nchi yetu kama Iraqi, ikawa nchi yetu kama Afghanistani, kama Somalia, tukawapa fursa madola. Leo madola yamekaa yanangojea tu wapi pakwenda kushika watakwenda kushika. Tukianza kugombana wataanza kuingia hawa. Tizama leo Pakistani inavoingia katika matatizo kwa kutofahamiana. Itakuja kuwa kama Iraqi na Afghanistan. Bahati mbaya. Au kama Somalia. Ni jambo la kuskitisha. Waangalie watu watizame mbele. Mahatma Gandhi kasema kama macho yetu yako mbele hayako nyuma, tutizame mbele.

Nchi isitiwe katika fujo labda iwe hapana budi na kwa nini iwe hapana budi wakati watu wana akili zao. Hayo yalopita tunajuwa, ni madola makubwa. Tutasamehe lakini hatutosahau. Bila ya shaka yaliotufika wewe unayajuwa unakumbuka yanaumiza sana. Mtu umekaa anakuja kumchukuwa binti yako, anakwenda mtu fulani amchukuwe akamnajis tu. Ilikuwa hamna usalama katika nchi. Unaweza ukakaa ukaambiwa nyumba toka kaitamani Saidi Washoto, kaitamani nani. Haya mambo yalifanyika kwetu sisi. Nani asojuwa? Kuna watu waliouliwa wazee wao wakaona machoni mwao. Haya mambo jamani ni mambo mingine. Hawa wanazungumza vitu vengine. Haya mambo yanaumiza. Au kama mimi aliuliwa babangu buree! Kaambiwa Karume akasema “mwendawazimu yule” ndo ilokuwa jawabu yake. Mwendawazimu yule Kaujore. Haya. Nyerere wala hakushituka! Nyerere hakushituka wala hakujali! Anasema siku Kambona alokwenda kumwambia Nyerere habari ya kuuliwa watu msikitini, akamwambia “unaona mambo haya?” Maana Kambona akijaribu baadae akiyaona yale makosa. Akasema nimemwendea Nyerere, hakunambia “ndio” hakunambia “sio.” Kanitizama tu hivi akageuza uso. Hakunambia “sio” wala “ndio.” Kimya! “Asukuut alamatu ridhaa.” Kunyamaza ni dalili ya kukubali jambo. Anasema Kambona, Nyerere hakunambia “fyoko!” Hii ndo hali. Utaona mambo mengine haya watu wameyafanya kama mali yao. Hii nchi (Zanzibar) kama mali yao. Walobaki wote si mali yao.

Ndo haya masala yanayozungumzwa juu ya Zanzibar na Tanganyika. Maana mimi sizungumzii masala ya kijamii. Masala ya kijamii sisi hatuwezi kukosana sisi watu wa Zanzibar na watu wa bara. Ni ndugu kama ninavofahamu mie. Lakini anaelezea Kambona anasema, wakati ilipokuwa kunazungumzwa juu ya jina, jinsi wengine walivokuwa wana hamu ya kulifuta hili jina la Zanzibar, walipozungumza kutafuta jina la muungano wa Zanzibar na Tangayika upewe jina gani? Yakatoka majina matatu: Tanzibar, Tangabar, nimelisahau la mwisho. Muhimu, Nyerere katoka na jina jipya. Akasema “Tanzania.”16 Jamaa wakasataajabu, hii “Tanzania” ina alaka gani? Nyerere akasema nataka “Tanzania” kwa sababu hili jina la “Azania” ndilo jina la Bahari ya Hindi mpaka Afrika ya Kusini ikiitwa hivooo! Huyu Nyerere anasema. Sasa ndo kuna “Azania Street” kule bara Tanganyika, na kama unakumbuka Afrika ya Kusini ikiitwa “Azania.” Harakati za mwanzo za Afrika ya Kusini zikiitwa harakati za “Azania.” Anaelezea Mahmud Ismail katika kitabu cha taarikh ya Tanzania, kitabu kinaitwa Tanzania, Tanganyika na Zanzibar, ni majina mawili yameunganishwa. “Tan” ni Tanganyika, na “Zania” ni “Azania.” Azania ulikuwa ni utawala miaka elfu kabla hajaziliwa Yesu, ulikuwa ufalme wa kipagani, inajulikana. Kulikuwa mwanzo na “Osanik” halafu ikaja “Azania” Empire. Kote huku, inaingia mpaka Indian Ocean, mwanzo ikiitwa “Osanik” kasha ikaja kuitwa “Azania.” Kama alivosema Nyerere, Afrika ya Kusini kulikuwa na pahali pakiitwa “Azania” ni kweli. “Tanzania” haina uhusiano wowote na Tanganyika na Zanzibar! Ni Tanganyika na Azania! Tukiambiwa siku zote, unaona majina mawili, Tanganyika na Zanzibar! Imekhusu nini “Azania?” Zanzibar wapi? Kitendawili hicho kakifichuwa Oscar Kambona.

Kambona ni kiungo muhimu kwa matokeo ya Zanzibar. Bila ya kiasi. Kwanza, yeye alikiri rasmi kwetu sisi, mbele ya Sheikh Ali Muhsin, mbele ya Bwana Amani Thani, na mimi nlikuweko. Alikiri rasmi kama zile njama zilifanywa kule (Tanganyika). Hilo alikiri rasmi. Na alikiri rasmi kwamba ulikuwa uvamizi na kama hivo unavosikia wewe. Hilo kakiri rasmi.

Pia alitaja vitu vingine ambavo nilivihakikisha kutoka kwa watu wengine. Jambo moja ni kuna nyimbo kubwa inayoimbwa Tanzania juu ya ujamaa, yaani “African socialism.” Sasa Kambona alituelezea ambavo sivyo tulivodhania. Baada ya ukombozi katika Afrika chini ya Jangwa la Sahara kulikuwa na wasiwasi wa nchi kuja kuifuata njia ya Ukoministi zile siku za Vita Baridi (Cold War). Vitu kama usoshalisti na ideology kama hizo zilikuwa zikiwatia khofu sana Wazungu. Kwa hivo kitu cha kuwatowa watu kutoka kwenye “usoshalisti wa kisayansi” na Marxism, ndipo walipokaa, anasema Kambona, Mmarekani ilifika hadi kumpa onyo Nyerere la saa 24. Wamarekani pia walimwambia Mngereza kuwa huyu mtu wenu huyu tunampa masaa 24 kama hamtochukuwa action yoyote kuhusu kusambaa kwa ukoministi na usoshalisti, sisi tutamuondosha katika utawala. Haya maneno Kambona kasema.

Kesha kasema, Waengereza, wakamtumainisha, wakampa matumaini Mmarekani kwamba usijali “Nyerere is our post-office in Africa.” [Nyerere ni sanduku letu la barua Afrika]. Sasa nini wakafanya Waingereza? Wakakaa wakafikirii, sasa sikiliza hapa ndo muhimu. Wakaitunga wao hii ideology ya “African socialism” wakakaa chini na Nyerere. Wakampa mwanamke anaitwa Joan Wickens, akawa analipwa mshahara kukaa na Nyerere. Joan Wickens ni British Jew, ni memba, anatuelezea Kambona, katika British House of Commons, akachaguliwa rasmi na kulipwa mshahara na serikali ya Kiingereza, kumfahamisha Nyerere hiyo walomtegenezea wao Waengereza “African socialism” ambao ndio huo ujamaa.17 Kwanini? Kwa sababu kuwa divert attention Waafrika wasiifate socialism ya ki Marxism-Leninism. Ujamaa, kwa alivosema Kambona ulitengenezwa na Waingereza na ulipangwa na Waingereza. Nyerere alikuwa kama ni chombo, anatuelezea Kambona, kuweko kwake pale, ile Sekretariat ya Kamati ya OAU ya Ukombozi wa Afrika, Nyerere awe ni kama chungio. Wanaomtaka nchi za Magharibi, yeye Nyerere ndo ampeleke mbele. Asotakikana, amkwamize, huku akijivika pazia la kisoshalisti.

Huyu [Robert] Mugabe wakati ule, alituambia Kambona, kwamba alichaguliwa na Waingereza kuliko Joshua Nkomo, kwa sababu zao wenyewe, mafalio yao wenyewe. Waingereza hawakumtaka Nkomo. Halafu katika baadhi ya maneno aliyotueleza Kambona, na hizi ni fursa mbali mbali. Wakati mmoja Nyerere aliwaita hawa wenye vyama va kupigania uhuru chini ya Jangwa la Sahara. Anakusudia watu kama Joshua Nkomo, watu kama Samora Machel, kina Kapwepwe, na nani. Anasema Kambona, siku moja Nyerere aliwaita hao viongozi na katika jumla ya maneno alowaambia, nakutahadharisheni sana na Waafrika weupe walokuweko Kaskazini ya Afrika. Hawa ni hatari zaidi kuliko Waafrika weupe walioko kusini ya Afrika. Katika kusema maneno yale, katika mtu aliyetatizana na Nyerere, ambaye tangu wapo walikuwa hawapatani vizuri, aliyetatizana naye sana na kujibizana naye ni Nkomo. Akajibizana naye sana Nkomo juu ya masala haya.

Kabla ya ukombozi wa Zimbabwe kwa siku chache, nilikwenda kutembelea Libya, palikuwa na mkutano wa kama sherehe ya vijana wa Kiarabu. Mimi nikapata bahati Balozi hapa katika watu aliowaalika hapa Imarat (Dubai) na mimi nikapata kupachikwa nkenda. Kule Libya hoteli (Funduk Al Shaati) nlokaa nlikaa na huyu Nkomo. Tukakaa tukazungumza nkampa salamu za Sheikh Ali Muhsin akaniuliza vipi hali yake, akaskitika sana mambo alofanyiwa Sheikh Ali na Nyerere, mtu barabara na nini. Katika kukaa siku mbili tatu mimi nikamuuliza na nikam quote [nikamnukuu] Kambona hasa. Nikamwambia Kambona kasema kadhaa, kadhaa, kadhaa. Nini fikra yako? Akanijibu Nkomo mwenyewe kuniambia, hayo ni kweli na huyu Nyerere ana mambo ya ubaguzi wa kidini na kikabila. Vipi itakuwa leo atatufarikisha sisi na Waafrika weupe wa kaskazini? Hawa walitusaidia katika ukombozi wetu. Huyu Nkomo alinambia.

Sasa, baada ya kugomboka Zimbabwe, kulikuwa na maonyesho fulani, nikenda mimi nikafuatana na watu wa Imarati (Emirates), katika niliofuatana nao Issa Al Ghureri, na watu wawili wengine. Sote watu wane kutoka huku. Tulifuatana tukenda. Kulikuwa na kama chakula cha usiku kidogo hivi alifanya Mugabe kwa wageni walokuja kutoka nje. Nkamuona Nkomo nkamfatia, tukasalimiana, tukakumbatiana na ghasia, tukakaa tukazungumza. Tukayarudia tena mazungumzo yale na huku Zimbabwe imeshagomboka. Akazidi kuyahakikisha yale maneno kuhusu Nyerere na akanitajia mengi zaidi juu ya ubaguzi wa mtu huyu. Sasa mimi nimepata kwa Kambona, nimepata kwa Nkomo.

Na kuna maneno ambayo aliwahi kutuambia huyuhuyu Kambona kwamba yule Mondlane wa FRELIMO wa mwanzo, alituelezea kisa chake. Mimi nilikuwa nkijuwa kuwa Mondlane alipokea parcel [kifurushi] Dar es Salaam kutoka kwa Wareno na alipoifunguwa ilimripukia akafa kwa sababu Wareno ndo alokuwa akipigana nao yeye. Kambona ananieleza na kuniambia, sikiliza Mutta, wewe huyajuwi haya mambo. Haya mambo usitake kutafuta mambo. Haya mambo alifanya Nyerere kwa kutumwa. Aliyefanya ni yeye huyu. Kafanya kwa njia maalumu kwa sababu Mondlane alikuwa hajapendeza kwa bwana zake Nyerere. Na kweli alikuwa na msimamo tafauti na kwa hakika nilipata habari zaidi kutokana na wenyewe watu wa Msumbiji. Basi sisi Wazanzibari tunasingiziwa uwongo mwingi bila ya kiasi na Nyerere na watu wake. Wametusingizia uwongo mwingi hasa sisi Wazanzibari.

Hata ikafika hadi Kambona akatueleza siku moja na alisema maneno makubwa sana. Alisema nataka nikuelezeni. Mnakumbuka kile kisa cha Katanga? Mimi wakati ule nilikuwa mdogo. Anasema Kambona, kulikuwa na mkutano, ambao Nyerere alikuwako kwenye mkutano huo. Wakakubailiana Nyerere, Gamal Abdel Nasser, Bourguiba, nk. Walikubaliana kwamba hawa jamaa wapatiwe silaha wasije wakazidiwa kwenye ukombozi wa Kongo. Silaha zikitoka nchi za kisoshalist na zinapita Tanganyika kwa kuwasaidia wale wenye kupigana. Sasa kwa ajili mapigano makali Kongo wakati ule, katika harakati za Lumumba kama unakumbuka, kulikuwa na vita vikali sehemu ya Katanga. Wale wakombozi walipigana washafika sasa kufaulu lakini katikati hapa ilikuja misaada kutoka madola ikabidi sasa wakombozi wanahitaji misaada kwa haraka.18

Anasema Kambona, kwa vile mimi ni Katibu Mkuu wa Kamati ya Ukombozi wa Afrika ya OAU, na wakati Nyerere ni mkubwa wangu, nikapeleka salamu kwenye zile nchi ambazo zina kawaida ya kusaidia. Hawakurudi nyuma. Egypt Air ikaja imebeba shehena kamili ya silaha kusaidia ili wakombozi wasishindwe kule wanopigana Kongo watu wa Lumumba.19 Nimekaa kule mimi, niko Mwanza, anasema Kambona nangoja silaha zije. Mara huku amenijia Regional Commissioner anantafuta. Nini? Akanambia unaitwa Dar es Salaam. Nikapewa simu nizungumze na mtu alokuwa responsible [dhamana] pale Dar es Salaam alikuwa mkubwa wa polisi au kitu kama hivi. Nikenda Dar es Salaam, anasema Kambona. Kufika Dar es Salaam nikamuuliza kwanini umefanya hivi? Akasema nilipata amri mie. Nani? Mwalimu kanipa amri hiyo. Anasema, nikatoka mimi nikamwendea Mwalimu. Mwalimu namna gani kule watu wanauwawa bwana? Wameelemewa, wanangojea silaha kwa haraka na zimeletwa kwa emergency. Anasema Mwalimu akasema, mimi sizipeleki silaha kule. Kwanini? Wale ni Wakominist. Anasema katika kujibizana pale Nyerere akamwambia kwani mimi kanijia balozi wa Kimarekani kaja hapa analia. Anasema unawasaidia Makominist wewe? Mimi siwezi kuwasaidia Makominist. Anasema Kambona, kwisha ndo ukaona ule ukombozi ukabinywa ndo ikapelekea mchango mkubwa alioufanya Nyerere kurahisisha kuuwawa Patrice Lumumba ambaye baadae akajifanya yeye ni kama mmoja aliyeskitika sana kumsemea Patrice Lumumba. Haya maneno kanielezea Oscar Kambona kwa mdomo wake. Mimi haya nilikuwa sikuyasikia. Nikiona mie kinyume cha huyu Nyerere mimi sikufichi, kama unavojuwa wewe. Huyu bwana, upande mwengine kumbe akitumika kwa faida nyingine. Tukiona hivi, tukiona vile, haya ndio mambo ambayo yalitendeka.

Na nakumbuka kijana mmoja katika watu walokuwa muhimu katika struggle [harakati] ya FRELIMO. Katika jumla ya mazungumzo ananambia, wakati Zanzibar ilipopinduliwa, sote tulitiwa sumu kuhusu mapinduzi ya Zanzibar. Mapinduzi ya Afrika, Waarabu wachache, na ghasia. Anasema huyu kijana, mimi nikifuatana sana na Mzee Mondlane kabla hajauwawa. Kwenye mkutano wa Zanzibar sote tukenda. Karume anatowa hotuba. Mondlane alisikitishwa sana na ile hotuba. Anasema kama naweza kufanya ningeliondoka. Anasema katika hotuba yake Karume, nakwambieni, na nyinyi mnaokaa na Wazungu, nyie wengine, hata nyinyi watu wa Mozambique nyinyi, msikae mkanywa chai nao hawa mashombe walochanganya na Wareno hawa. Pia wao wachinjwe tu kama sisi tulivochinja Zanzibar. Huyu ndo mkombozi anasema maneno kama haya, alisema Eduardo Mondlane. Nikamuuliza yule kijana kwanini wewe ulishtushwa na haya maneno? Akanambia sikiliza bwana. Sisi Mozambique tuko wenye asili mbalimbali. Wengine ni weupee lakini wazee wetu ni Waafrika. Na kwani Wareno wote walikuwa wabaya? Akawataja wakubwa waliokuwa weupe ndani ya FRELIMO. Kama fulani, tukamuuwe yule. Kama fulani tukamuuwe yule. Basi anasema Mondlane alikasirika sana hata akamtoa maana mchonga meno Nyerere kwa kumsikia Karume kusema maneno kama yale.

Kambona akisema wazi kuwa yeye mwenyewe alishiriki katika kuivamia Zanzibar. Anakubali yeye. Anasema kwanza Nyerere alikuwa hataki kusikia neno “Uislamu.” Pili, anasema, ile Nyerere kutaifisha haya majumba na vidukaviduka Tanzania nzima unajuwa maana yake nini? Yeye sasa anatuuliza sisi Kambona. Nikamwambia kwa ajili ya huo Ujamaa wake alionao. Akasema hapana! Kwa sababu wakati ule Dar es Salaam, not less [si chini ya] 80–85% wa wamiliki walikuwa ni Waislamu Waswahili. Kwa sababu mazingira ya Dar es Salaam yalikuwa ya Kiisilamu na unajuwa Tanzania ni nchi ya Kiisilamu. Sasa Nyerere kuupiga vita Uislamu na kuipiga vita East African Muslim Welfare Society (EAMWS) akazitaifisha mali za Waislamu ili wasiweze kutowa mchango kwa harakati za kimaendeleo za Waislamu. Halafu Kambona akasema, kwa mfano wale waliokuwa si Waislamu, kwa mfano mzee wangu mimi mwenyewe mtu mzima, John Rupia [Nyerere] aliitaifisha mali yake lakini alimrudishia baada yake. Lakini wale walokuwa Waislamu Nyerere hakuwarejeshea kwa sababu ni Waislamu. Mpaka wakfu na misikiti na kila kitu kikataifishwa. Mwisho tukashtuka sisi. Tukaona eh! Kila kitu cha Waislamu kimechukuliwa! Nyerere alitaka kuwalemaza Waislamu.

Na Nyerere na Kambona hawakusikilizana kwa sababu alikuwa hataki mtu yoyote awe juu yake. Ndo ukaona hata vijanavijana waliosoma huwavunja moyo. Wewe nini wewe, si umesomea mambo ya umeme? Ngoja ngoja! Atapiga simu Nyerere, fulani mchukuweni ende akalemazwe huko. Utaona mtu kama Kawawa ndo kamuweka karibu na chini yake. Kwanza hakusoma. Pili, ni mtu heewallah bwana! Wale walosoma aliwaweka halafu akawanyanyapaa akawaweka mbali hukooo. Wengine akawaondowa akawapeleka Mabalozi. Kambona alisema hajakubaliana na Nyerere kuhusu Ujamaa kwa sababu akijuwa kuwa ni mambo ya uwongo. Mimi, anasema Kambona, sijakubaliana kuwachukuwa watu kwenda kuwatupa katika vijiji maporini wakenda kuliwa na simba. Vijiji vinachukuwa miaka mingapi kuvitengeneza? Mambo aliyokuwa akifanya Karume anavotaka pia Kambona alikuwa akipingapinga. Nyerere akimuona Kambona kuwa alikuwa ana tamaa ya kutawala lakini Kambona akisema kama alikuwa ana tamaa asingelimuokoa Nyerere pale alipopinduliwa tarehe 20 Januari 1964 wakati jeshi la Tanganyika lilipoasi. Nani asojuwa kuwa jeshi lilimtaka Kambona aishike nchi? Akenda kumtafuta Nyerere mafichoni yakaletwa majeshi ya Kiingereza kumrudisha Nyerere madarakani.

Alikuwa akisema, mimi hamu yangu nitoke nikishafaulu nikalivunje lile sanamu la Karume, nikishalivunja, basi tena nakuwachieni wenyewe mwende upande gani. Na baina ya sisi Tanganyika na nyinyi Zanzibar itakuwa ni shauri la kulirekibisha suala la muungano ikiwa Wazanzibari na Watanganyika wanataka au hawataki. Alikusudia mambo yende kwa mafahamiano na si kwa mabavu.

Jambo muhimu ambalo Kambona alituhadithia ni kwamba wakati alivokuwa Nyerere bado yuko katika utawala mchango mkubwa katowa juu ya haya mambo yanayotokea mauwaji yalofanyika Ruwanda na Burundi. Tukamuuliza kwanini? Akasema kulikuwa na kambi, kama sikukosea, ikiitwa “sabasaba” kule Tabora au Dodoma. Anasema kwenye kambi hii walikuwa wakifunzwa Wahutu ili wende wakawapige Watutsi. Nyerere akiwafunza Wahutu wende wakawauwe Watutsi kwenye hiyo kambi ya “sabasaba” huko Tanzania, anasema Kambona.

Na utakuja kuona baada ya matokeo yaliotokea ya mauwaji Watutsi walisema mchango mkubwa kautowa Nyerere katika mauwaji ya wenyewe kwa wenyewe hapa. Kwa hiyo alipochaguliwa Nyerere kama ni mpatanishaji Watutsi walikataa. Huyu ndo sababu kubwa ya mauwaji yaliotokea kwetu. Mimi nikayakumbuka maneno ya Kambona kumbe hawa walikuwa wana kambi ya Wahutu wakipewa mafunzo wawauwe Watutsi. Mpaka mwisho [Benjamin] Mkapa akipata tabu kuamiliana na hawa Watutsi kwa sababu wale bado wanaona hawa Watanzania wanawasaidia tu hawa Wahutu. Nyerere akiwapa training [mafunzo] na mimi nafikiri hakuna tatizo katika Afrika Nyerere hakuwa na mkono wake. Utakumbuka Biafra. Hakuna tatizo mtu huyu hakuna mkono wake. Mpaka makanisa East Timor akaingia na akakorofisha karafuu za Zanzibar zisinunuliwe na Indonesia. Na alisema kama ataweza kukichukuwa kisiwa cha Zanzibar mpaka katikati ya Bahari ya Hindi akakizamisha basi nitafanya kwa sababu kisiwa hichi kina “foreign influence” [ushawishi kutoka nje] nao ni Uwarabu, nao ni Uislamu.

Na neno “Mwarabu” nini maana yake nataka kukwambia hapa anapokusudia mtu kama Nyerere. Maneno aliyoyasema mwana historia maarufu Basil Davidson anasema alokuwa Muisilamu ni Mwarabu hata akiwa na kabila gani kwa sababu Afrika linatakiwa liwe bara la Wakristo. Niliwahi kumwambia Dokta Salmin [Amour] maneno haya zamani alipokuwa President wa Zanzibar.

Anaposema Mwarabu hakusudii Mwarabu damu, anakusudia Mwarabu dini! Ndo pale Nyerere aliposema Waafrika weupe wa Kusini hawana hatari kubwa kwetu sisi kama Waafrika weupe wa Kaskasini ya Afrika kwa sababu wale ni Waisilamu. Kina Masri, kina Sudan, kina Tunisia, wale ndo Waarabu! Sio wao tu bali hata Wanyamwezi waliokuwa Waislamu kwa nadharia yao hawa kina Nyerere yule ni Mwarabu. Madam ni Muislamu, Msagara, Mzigua, Mruguru, Mzaramu, madhal ni Muislamu ndio ile “Mwaarabuu!” anamkusudia Muislamu. Kwa hivo Mwarabu hapigwi vita, Muislamu ndo anopigwa vita. Ndo ukaona vile vinyago mpaka leo kaviwacha kila siku ya ukumbusho Mwarabu anapigwa mapanga na mashoka, maana yake ndo wanampiga Muislamu. Hio ndo nadharia yao waliokuwa nayo wao wenyewe. Nambie tatizo gani katika Afrika ambalo haumo mkono wa Nyerere? Lipi? Hakuna tatizo ambalo hayumo. Kila pahala penye ugomvi, kila pahala penye vita kachochea. Kaingilia Uganda. Si kwa sababu yoyote. Kwa sababu nini? Idi Amin ni Mwarabu kwa sababu ni Muislamu. Yamefanywa maovu mangapi mbona hakuingilia. Mimi baba yangu kauliwa msikitini na Baraza la Mapinduzi wakati yeye anaweza kumfunga, mbona kawafunga wengine akawaachia wengine? Lakini si kwa maslahi yake. Haya ni mambo ya chuki wakati sisi Waislamu wa Afrika ya Mashariki hatuna mambo ya chuki za kidini. Bila ya shaka kuna mengi zaidi watu hawajuwi na watakayoyasoma watafunguwa macho. Walikuwa hawayajuwi. Maana haya ni maalumati tunayanukuu. Watu bila ya shaka wataerevuka. Anapofahamu mtu “Kwani sawa wenye kujuwa na wasiojuwa?” Na kama mtu umemtia ujingani ukaweza ukamfanya hivo basi jinga likierevuka mwerevu yuko mashakani.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: