Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!

Icon

Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia

Mlango wa Kumi na Moja: Katibu wa Midani ya Mapinduzi

Kila mzee mtu mzima anayekufa Afrika ni sawa na maktaba nzima kuwaka moto. —Amadou Hampate Ba

Mzee Ahmed Othman Aboud, maarufu Mzee Aboud “Mmasai” kutokana na marehemu mama yake mzazi alitokana na kabila la Kimasai. Mzee Aboud alijiunga na Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) tarehe 1 July 1956. Pia alikuwa memba wa The Tanganyika Local Government Workers Union, Tanganyika African Traders Union, na National Union of Tanganyika Worker’s (NUTA). Mzee Aboud alikuwa Katibu wa Midani ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 na katika siku zake za mwisho alikuwa ni memba wa Chama cha Wananchi (CUF). Katika picha ya “Wanamapinduzi wa Zanzibar II” kwenye kitabu cha Anthony Clayton The Zanzibar Revolution and Its Aftermath,” Mzee Aboud yuko baina ya Abdalla Kassim Hanga na Abeid Karume na kwa vile mwandishi alishindwa kumtabuwa akamuandika kuwa ni “unknown”—“yaani hajulikani”. Kwenye picha hiyo Mzee Aboud anaonekana ameushika mkono wake wa kulia.

 

Mzee Aboud “Mmasai”

Tuanze pale baada ya uchaguzi wa Julai 1963, watu walivokuwa kama wamepata kiharusi. Nilivokuta mimi. Mimi binafsi nilikuwa mtumishi wa serikali bara, katika Baraza la Mji, Dar es Salaam katika 1950s. Ikaundwa TANU katika 1957. Mimi nilikuwa mwanachama wa TANU. Baada ya harakati za kisiasa zilokuwepo kule Tanganyika na zilokuwepo hapa Zanzibar 31 Disemba 1959 nikaacha kazi kule Dar es Salaam nikaja Unguja 1960 Januari mimi nipo Unguja.

Nimekaa nikaangalia hali ya mambo nikajiunga na Afro-Shirazi Mei 27, 1960 na tawi langu lilikuwa Mwembetanga. Baada ya shughuli za kisiasa 1961 zikatokea fujo Unguja. Ilipotokea riot ya Unguja kwa hakika mimi nilikuwa siijui.

Nilikuwa wakala katika kituo cha polisi cha Mwera, ilokuwa skuli ya Mwera na hili ni jimbo la Fuoni. Mgombea wa Afro-Shirazi alikuwa Aboud Jumbe, mgombea wa Hizbu alikuwa Maalim Hilali. Baada ya uchaguzi kufungwa, saa imekwisha, kituo kufungwa tukapata habari kuna ugomvi, fujo. Hapo tukaja sisi kuchukuliwa na gari ya polisi, ikiwa chini ya usimamizi wa Major Bott, tukapelekwa Fuoni kwenye kituo cha kuhisabia kura. Mimi nikiwa wakala katika kituo cha kupigia kura cha Mwera, halafu nikawa wakala wa kuhisabu kura katika kituo cha Fuoni.

Baada ya uchaguzi kwisha, mahesabu yale ya uchaguzi kumalizika, ikawa ni usiku, tukapakiwa ndani ya gari ileile, chini ya Major Bott, mpaka Kijangwani ilipokuwa ni ofisi ya Afro-Shirazi kwa mambo ya uchaguzi. Tukatuliwa pale, akaripoti Bott kwa ofisi ile kwa watu wa jimbo la Fuoni wa Afro-Shirazi ndo hawa na watu wa Hizbu sijui kenda nao wapi, lakini sote tulipakiwa kwenye gari moja chini ya ulinzi wa polisi kwa usalama wetu. Tukaongoza, mimi nikaja zangu nyumbani nikaletwa na polisi vilevile mpaka kwangu, basi umekwisha uchaguzi ule na ghasia zile, watu wakatiwa ndani, wakafungwa, wengine wakahukumiwa miaka mingimingi, na kundi la watu likakamatwa likajaa jela tele, wakapelekwa kisiwani wengine. Kwa bahati nzuri au mbaya, lakini kwa maisha ya kisiasa kila mtu alokuwa kidogo ana muamko wa kisiasa anaweza kuona kuwa ilikuwa bahati nzuri kukamatwa kwangu nikatiwa jela.

Nikakaa rumande, nikashtakiwa mahakamani kiasi ya miezi sita kama hivi, siwezi kusema miezi sita kamili. Sikuweka rikodi hiyo. Niliposhtakiwa, nilishtakiwa na mtu mmoja nilikuwa simjui ndo siku hiyo nilimjuwa, watu wawili, mimi nilikuwa mshtakiwa nambari moja, yule mwenzangu ni mshtakiwa nambari mbili. Na mashtaka yetu kwamba tumechochea, nimechochea, na nimeongoza fujo, tangu wakati wa asubuhi, kuanzia saa nne ya asubuhi mpaka saa kumi na mbili jioni.

Sasa tuzungumze hiyo kesi. Sote tulikuwa na shahada za memba wa kuhisabu kura au wa kituo cha kupigia kura, ASP na Hizbu. Na kwa bahati nzuri kituo cha kupigia kura chetu ofisa wake alikuwa Maalim Ali Said Al Kharusi na mgombea alikuwa Maalim Hilali kwa ZNP. Walikuwepo polisi kulinda usalama na polisi alokuwepo pale alikuwa Inspekta Aboud Saidi na moja wa Konstebul alokuwepo nnaemkumbuka alikuwa namba PC 47. Hii namba mpaka ntakufa naikumbuka. Kwa sababu hawa wote, wagombea wa ZNP na maofisa wa polisi walikuwa ni mashahidi wangu ndani ya korti kwamba mimi sijakuwemo katika fujo za Juni na wengine polisi akiwa mmoja ni Aboud Saidi, huyu ndo alokuwa na dhamana ya eneo lile wakati ule. Na huyu askari nilokuwa naye ubavuni PC 47, na Major Bott aliyekuja kutuchukuwa, naye nilimtia katika ushahidi huo. Ijapokuwa wote niliowatia hawakuitwa mbele ya mahkama, mahkama ilitosheka kama mimi sijakuwa ndani ya fujo, nitolewe, sina makosa. Mashahidi walikubali baada ya kutowa zile saini zao nje, kama Maalim Ali Said Al Kharusi yeye alikuwa ndo ofisa msimamizi na zote saini zake, na Maalim Hilal alikubali. Hawajakataa kama hawanijuwi, wananijuwa kutokea utoto wangu, nilipokuwa mie niko skuli lakini habari ya uchaguzi walikuwa hawajuwi mpaka nilipotowa zile hati ambazo zina saini zao. Na ile kesi ilishikwa na mwanasharia Talati, ndo aloishika ile kesi yangu.

Ikawa mimi sina kesi ya kujibu, nikawachiwa huru. Hakimu aliniambia, alinieleza ndani ya mahkama kwamba unaweza kuwashtaki hawa polisi kwamba wamekudhulumu kwa kukuweka ndani lakini kwa bahati nzuri au mbaya kushtaki kunataka pesa, kwanza, kwa sababu unataka uwende ukanunuwe hukumu halafu ina taratibu nyengine kubwa na yote inataka pesa na mimi sina pesa. Mimi nikiishi mkono kwa mdomo. Sasa nitafanyaje. Tukaacha. Nilipomaliza tumekaa tukizungumza habari ya fujo watu kwa jumla, memba wote wa Afro-Shirazi walikuwa wamevunjika moyo na tayari kufanya ugomvi wowote kama walivoanziwa, lakini matokeo yake yalikuwa si mazuri, yalikuwa mabaya kwa sababu wale watu wanoishi mashamba pande zote mbili, upande wa Afro-Shirazi na upande wa Hizbu, lakini kuna baadhi ya watu walikuwa si Hizbu wala si Afro-Shirazi lakini waliathirika katika ghasia zile kwa maumizi, wengine watu wenye mashamba yao ambao ni memba wa ZNP waliwakatiakatia migomba wakawafukuza ndani ya mashamba, matokeo yakawa si mazuri, uhusiano wa kijamii ukawa mbaya. Na jamaa waliokuwa Hizbu ambao wanakaa kule wanyonge wameishiwa wameumizwa, wamepigwa, wengi wamekufa. Haijulikani nani kafanya, na saa ngapi imetokeya, haijulikani, ni vurugu.

Fujo siwezi kuzielezea lakini ukweli wa mambo uchaguzi ulikuwa na mambo ya kupenyezana watu ambao walikuwa na haki ya jimbo lile au na wengine hawana haki ya jimbo lile. Hizo ndo sababu mpaka leo watu wanagombana hapa Unguja. Imeshakuwa sugu hiyo. Inavyosemekana, ni kituo cha Gulioni kiloanza fujo ikaambukizwa na Darajani. Kituo cha kule kilianza fujo kwa sababu ya watu kutoka Funguni kuja Gulioni kupiga kura, ni karibu pale wanavuka tu. Sasa na kwa mujibu wa wakati ule watu wa Malindi walikuwa wakiogopwa kwa sababu walikuwa wana umoja, akipigwa mmoja wamepigwa wote. Hivo ndo ilikuwa watu wanawaogopa. Inavosemekana. Mimi si shahidi wa jambo hilo. Inavosemekana. Sasa ndo ikaendelea ghasia Darajani mpaka…Darajani ndo ilikuwa kubwa, kubwa sana ndo ilikuwa Darajani. Basi pale tukawa tunakaa tunafanya uchaguzi kwa kujiamini, tunajiona akilini mwetu kwamba sisi ni wababe! (Vicheko). Hata ulipofanywa uchaguzi wa mwisho, na hapa katikati ilikuwa serikali ya mpito, mpaka tulipokuja kwenye uchaguzi wa mwisho [Julai 1963], ZNP ikapata serikali baada ya kufanywa kuunganisha viti na ZPPP. Mimi binafsi nilikuwa wakala wa kuhisabu kura, mimi na Diria, tulikuwa wawili, mimi na Mheshimiwa Ahmed Diria, Victoria Garden, ndio uchaguzi ulikohesabiwa. Tukashindwa. Wa jimbo hili la Darajani tukashindwa kwa voti mia mbili na mgombea wetu alikuwa Thabit Kombo, na mgombea wa ZNP alikuwa Ibun Saleh. Basi tukashindwa tukarudi. Mimi nilisikitika sana. Nilipotoka kule sikutoka nje kwangu kabisa.

Nililala nyumbani nikatapika matapishi mabaya mpaka damu. Uchungu. Kwa nini tumekosa na kulikuwa hakuna sababu ya kukosa. Na tukajuwa sababu zengine za kukosea, baadae lakini. Haya, siku ile mimi nimekaa kitako, sikutoka, siku ya pili nkenda Gongoni. Hiyo hapa inaanza sasa maudhui.

 

Uchaguzi au Risasi?

Kujuwa chanzo cha mapinduzi, ina maana kila mtu anajuwa chanzo chake yeye kujuwa mapinduzi. Sasa kwa mfano wangu mie. Mimi nimejuwa mapinduzi kutokana na Saleh Saadalla, ndo alonambia “sasa tufanye mapinduzi.”1 Kwa kweli zile fikra yeye alizozitowa yeye kuhusu mapinduzi zimetokana na uchaguzi kwa mujibu ninavozielewa mimi. Uchaguzi ule kwamba tushashindwa lakini tuloshindwa tuna idadi kubwa ya voti kuliko waloshinda. Lakini waloshinda wana majimbo mengi zaidi kuliko sie wenye idadi kubwa. Sasa hapa hizi ndo fikra za Saleh ziloingia kwangu na mimi nkakubali tufanye.

Haijawa uchaguzi wa kura kwa mtu mmoja. Uchaguzi ulokuweko ni wa viti. Mtu mmoja, voti moja, ndo ilivokuwa, lakini ushindi hauhisabiwi kwa mujibu wa idadi ya kura. Ukihisabiwa kwa idadi ya ushindi wa viti, majimbo, ndo aloshinda. Sasa ukija kuangalia idadi kubwa ya viti ilikuwa baina ya vyama viwili, mchanganyiko wa viti va chama cha Hizbu, mchanganyiko wa viti va ZPPP ilipoungana pamoja, vikawa ni vingi kuliko viti vya Afro-Shirazi.

Kiti cha Mlandege wamechukuwa Hizbu. Tulipitwa kwa kura mia mbili ziada. Na zilikuwa hizi kura zilopita hapa, ni wapiga kura wa Kihindi, ambao hawakuipigia Afro-Shirazi. Waliipigia Hizbu. Ni wao walikuwa idadi yao mia nne. Wengi wao ni Wahindi wa jamatini. Sasa ukiangalia, ukichambua, kwa nini wakatupita kwa kura mia mbili? Tulikuwa sisi tumewapita Hizbu kwa kura mia mbili kabla kufanya hesabu za Wahindi ambao walikuwa ni kura mia nne. Kwa sababu walikuwa Wahindi wale kutoka Mlandege njia panda, Darajani, mpaka Mlandege, kituo cha polisi. Ilikuwa mtaa ule ni Wahindi watupu. Usione leo kuna maduka ya jamaa. Kulikuwa hakuna duka la mtu mweusi, hata moja…Kwa maoni ya kila mtu, uchaguzi mkuu wa Julai 1963 ulikuwa wa haki. 100%. Haijawa ugomvi, haijawa vita, haijawa kupandikiza watu. Haijakuweko.

Tulikataa kwamba hatutaki. Kuna njia mbili, kuna karatasi na kuna risasi. Sasa unaweza kuchaguwa moja wapo katika hizo. Uchaguzi ulikuwa wa haki. Mia juu ya mia. Kwa fikira zangu. Kila mtu anaweza kusema anavotaka. Hata akisema kuwa Mngereza kahusika kugawa majimbo, alikuwa ndiye muendeshaji wa nchi hii. Kwa hivyo ni lazim atakuwa yeye amehusika na kugawa majimbo na kusimamia uchaguzi. Lazima tufike kunako ukweli.

Tusijidanganye nafsi zetu. Ninavofahamu mimi, mapinduzi yalikuwa ni kwa ajili ya kufata uchaguzi namna mbili, kura au risasi, hakuna jingine. Lakini kwa kudai kulikuwa na ghilba, ni uwongo. Si kweli. Uchaguzi wa Juni uloleta fujo, tulipiga kura, kura ilikwenda safi kabisa. Fujo tu ndo ilitokea mjini. Tukahisabu kura akashindwa Maalim Hilal na Aboud Jumbe. Kihalali kabisa, wakapeana mikono, wakakubaliana. Ule ulikuwa uchaguzi wa kwanza ambao ungelikuwa pia ni wa mwisho. Kwa ajili ya fujo, na kwa ajili ya usawa wa viti, ambavyo ndo kitu kikubwa, ikafanywa serikali ya muungano, au ya mshikizo, ikiitwa “interim government.”

Mapinduzi yamekuja kutokana na fujo za Juni. Kwa sababu viongozi maalumu wakaona kwamba sie hawa Hizbu hawatuwezi, wamepata kama majaribio. Watu wote wakisema “hawatuwezi, sie tunaweza kupigana nao”. Sasa tulipoingia katika fikra za mapinduzi tulikuwa na moyo kwamba watu wote watatuunga mkono. Hii ni fikra ya msingi nnoweza mimi kuielewa kwa kutokana na Saleh Saadalla.

Tatizo la Waarabu na Waunguja halijakuwepo. Hii nakwambia kitu kweli. Hata utakuja kukuta Waarabu wengi wameuliwa mashamba, ukipeleleza, walouwa si Waunguja, lakini walokuja Unguja. Kama jamaa Wamakonde, wameuwa Waarabu wengi sana. Hii nyumba ingekuwa kuukuu ningekuonyesha risasi ya Mmakonde mmoja. Sie tumekaa barazani kapiga risasi pale. Walikuwa watu watatu wamefatana, halafu wakenda kumuuwa kijana mmoja anaitwa Mzee, kwenye kijumba cha simu. Wakamkuta. Kuna sababu gani? Wakaingia ndani kwake wakaiba. Si kuiba, kuchukuwa.

Watu wa Kiunguja bwana ukitaka kumfurahisha mwite “Mwarabu”, “Mwarabu wangu hebu njoo nkwambie.” Ukitaka kumfurahisha, kumridhisha khasa. Ni upuuzi. Mambo yametengenezwa baada ya mapinduzi kuleta msuguwano katika nchi.

Kuhusu Wamakonde sijuwi. Hilo jambo siwezi kukueleza kwa sababu sijakaa mie kuona wanavokuja, na kuja kwao na nini. Lakini hapa ile kuambiwa kuwa kuna chuki baina ya Waarabu na watu wa Unguja, uwongo.

Kwa sababu hawa ndo wanotawala. Kumbuka Baraza la Mapinduzi lote ni watu wa Kitanganyika. Utasema nini?

Mie siwezi kuelewa jambo hilo, lakini mimi ninavyoelewa, Muunguja, Mzanzibari, anaishi shamba, mjini, unakwenda kumridhisha unamwita “e Mwarabu wangu njoo nkwambie bwana.” Tizama bwana, hii baada ya mapinduzi kwisha kila kitu kinasemwa. Kuna hadithi nyingi. Si za kweli, si chochote. Karume akisema [kuhusu utumwa] kwenye mikutano mara nyingi. Ni huyo tu. Hajatokea kiongozi mwengine kusimama akasema maneno kama hayo.

Hayana ushahidi wa chochote. Manake alisema yale makaburi pale wamezikwa Waafrika watumwa sijui walofanya nini. Na yale makaburi ya wagonjwa wa ndui pale. Na yakapata majina mpaka leo, Kisiwa Ndui. Lakini ndo anasema, mtu hajibiwi. Wewe utashangaa kwani. Viongozi wengi wa Afro-Shirazi ni wabara, kina Mtoro Rehani Kingo, kina nani. Unatarajia nini kutoka kwao?

Wanolaumiwa ni viongozi. Na anolaumu ni mwanachama wa uongozi ule. Yule ndo anolaumu. Nimejaribu kuwalaumu waache mambo hayo. Manake hili suala ni zito, lakini kweli limesemwa. Na amesema Karume “wakimbieni wenye ilimu”.

“Na hawa Waarabu walitufanya watumwa.” Na ni kweli, watumwa walikuwepo duniani. Si Waarabu tu walofanya. Mambo mengi sana. Wapo watumwa wa Kihindi hapa. Au hujui?

Hilo ni jambo litakufa wenyewe. Unajuwa kitu kitakachouwa? Ni lazima ipatikane serikali ya kidemokrasia, kwa kura, halafu iwepo biashara huru, biashara zikipatikana, biashara nzuri, na hakuna khofu. Leo khofu tele. Kwa kuifikiri tu hivi. Zanzibar ingekuwa nzuri. Na jambo ambalo lingekuwa gumu, jambo moja lingekuwa gumu, ni ubaguzi. Ubaguzi ungelikuwapo. Ambayo sasa ni kubwa zaidi kuliko tunavofikiri ingelikuweko. Lazima ingelikuwepo. Kwa sababu kutokea hapo ulikuwapo ukabila. Hii ndo kitu kikubwa kinachojulikana.

Huu sio ubaguzi. Huu ni udikteta wa moja kwa moja. Udikteta wa moja kwa moja. Iwe serikali yenye kuchaguliwa na watu, ambayo imepigiwa kura kama ilopigiwa kura hiyo ya historia [ZNP) na iwachiwe iendelee, ili upatikane utulivu. Manake sasa raia hana haki. Anakuja askari kukukamata tu saa yoyote, huna makosa, akakutia ndani. Wewe huna kosa. Lakini keshaamini yeye akukamate akutie ndani. Au kakaa Raisi, kakaa kwake huko anafikiri, fulani mtieni ndani. Huendi mahakamani, huhukumiwi, hujui umekosa nini.

Kwani risasi matokeo yake ni Zanzibar tu? Imeanza Uingereza. Lakini haijawa hivyo. Haijafika hadi hii. Hivo leo daraja hii tulonayo leo, wakati huu, saa hii, tunaweza kutoa pumzi, lakini kabla ya hivi, tulikuwa hata kuongea hatuwezi (vicheko).

Chombo cha Afrabia kitafanya kazi. Lakini hawa watu mafisadi huku, wote. Bara na hapa Zanzibar. Watu wamejaa ufisadi. Tena kila akiwa ana cheo kikubwa, anakuwa fisadi zaidi. Ingelikuwa hawa wafanyakazi kweli wanataka maendeleo, mambo yasingeliharibika hivi ya uchumi. Watafanya lakini hawatofanya. Afrabia itakufa njiani. Kabisaa. Chini ya mfumo wa serikali hii, itakufa. Na yasajili maneno yangu, ukumbuke jina langu. Vingapi vimekufa vilivoanzishwa vizuri? Vingapi? Sasa mimi ndo nakuwa ndo dhamana wa biashara ile. Mimi namuweka ndugu yangu, rafki yangu, jamaa yangu, ambaye tunasikilizana. Yeye ndo atakaa pale kufanya vile. Yule ndo atakuwa wakala wa kuiba vitu vetu sie. Kwa hivyo itakuwa biashara inakwenda bila ya faida. Inakwenda kwa khasara. Waarabu kule hawakubali.

Ufumbuzi, tubadilishe serikali tu basi. Tupate serikali nyengine ya wapiga kura, tupige kura, tupate serikali mpya. Ile serikali mpya kwa miaka miwili, mitatu ya mwanzo, itaweza kujiamini. Haya hawa hawafanyi kitu. Hawatofanya maisha. Donda ndugu mara mbili hawa watu! Chronic, double chronic. Hawendi. Wamejaa ufisadi.

Jamii inabadalika kwa sababu ya ubinafsi. Kitu kilicholeta hii ni utawala. Watu walokuwa kwenye utawala, hawako tayari kuutowa utawala kuwapa wengine kwa njia ya kura. Hawako tayari.

Sio mie, ni binaadamu, yoyote, anapofanya kitu kikawa sivyo huona kwanini nimefanya. Hujuta. Na sio leo tu. Kutokea zamani. Watu wakijuta kwa mambo yao. Nimejuta eh! Kwa nini nisijute na hakuna kilicho chema kilichofanyika katika taifa? (anacheka). Kwa nini tusijute. Huna uwezo wa kuzuwia lisifanyike.

Yale mazingira yaliokuwepo ndo yalochaguwa mawaziri. Jana nilimfikiri kijana moja, yuko Kwa Hani, akivuta kiko hivi, akifanya kazi melini. Najuwa meli aliacha zamani. Alikuwa ana mchango mkubwa katika mapinduzi. Anawajuwa watu wengi, na alikuwemo kwenye kundi letu.

Karume alikuwa ana ushawishi mkubwa juu ya memba wa Afro-Shirazi. Na ungemkosa ndani ingekuwa fujo nyengine. Sasa kuzuwia fujo ile ndo akafanywa Raisi bila ya madaraka ya utekelezaji, kama Mfalme wa Kikatiba. Ndo Hanga akawa Waziri Mkuu. Kuondowa fujo. Hiyo kitu wazi kila mtu anajuwa. Kuja hawa kuja kumbadili kumfanya yeye [Karume] mtekelezaji, aaah!

 

Jiko la Mwanzo la Mapinduzi

Baada ya kushindwa uchaguzi wa Julai 1963 nilikwenda Gongoni, nikakutana na Mheshimiwa Saleh Saadalla, kwa matembezi. Sahib akaniuliza, “sasa tutafanya nini?” Nkamwambia “mimi sijui la kufanya, hapa sasa hivi imefika mahala la kufanya mimi sijui.” “Lakini wewe uko tayari?” Nikamwambia “lolote litakalokuwa limekubalika kufanyika mimi niko tayari nalo.” Akanambia “unajuwa hakuna jambo la kufanya isipokuwa mapinduzi?” Nikamwambia “niko tayari mimi kufanya mapinduzi. Niko tayari saana.” Akanambia, kamwite Hanga. Nkenda Kikwajuni, Hanga akikaa Kikwajuni maanake. Nikenda nkamwita, nikamwambia bwana, “Maalim Saleh anakwita bwana, sasa hivi wende.” “Sasa hivi, eh?” Nikamwambia “eh.” Akaingia ndani, nilimkuta amevaa nguo ya kulalia, maana hana anapokwenda. Na akaingia ndani, akavaa suruali na shati, viatu, tukaandamana. Tulipokwenda Gongoni tukamkuta Saleh kakaa anafikiri nini la kufanya au nini la kusema. Tumeingia ndani mpaka tumefika pale ukumbini kwake, hana khabari, yupo amezama kwenye fikra. Tukamwita, Hanga akamshika kichwa “unasinzia?” “Nafikiri namna ya njia ya kuyaingilia, mkabala wa mwanzo.”

Tunajuwana. Tuko watu wa chama kimoja. Umefahamu. Shughuli zetu za pamoja, za kisiasa. Wakati fulani niliwahi mimi kuwa memba, mfanya kazi wa jimbo la Saleh Saadalla, nikimsaidia kama seketeri wake binafsi wakati mimi nilikuwa seketeri wa Aboud Jumbe. Tunaendeana. Sote ni memba wa chama cha ASP. Basi. Sio jambo jengine ziada. Wale viongozi na sie wafuasi. Tunapata pakuzungumza. Sijui umenielewa?

Sasa Saleh akamueleza Hanga, Bwana Abdalla Kassim Hanga, akamuelezea kwamba hivi hivi…kwamba nimefikiri tufanye mpango wa mapinduzi. Hanga akasema “sawasawa”. “Wewe nenda kamwite Twala”, ili mimi. Nikenda nkamwita Twala, Miembeni katika ofisi ya chama cha wafanyakazi. Sasa sikumbuki alikuwa kwenye chama kipi cha wafanyakazi kwa sababu vyama vilikuwa mbalimbali. Nikamwita akaja, akaambiwa, akasema “hakuna njia nyengine, nina hakika.” “Njia ilioko tukubali kutawaliwa iwe imekwisha kesi au tuamue.” Ilivokubalika, tukasema sasa bwana, haya mapinduzi si rahisi, kumuendea mtu kumwambia “tupinduwe.” Hawatokuwa tayari ikiwa kwa kuwaambia jambo lolote, lakini kwanza tutafute watu maarufu katika vitaa vitaa vetu vidogo ambao wana msimamo madhubuti tunaowajua.

Ikawa imefikiriwa hivyo. Hanga akasema, hakuna, kwanza tujuwe kama tuna watu madhubuti tunoweza kuwapata katika jeshi la polisi. Nkasema, Twala akasema, polisi wako wengi, hao wakubwa wakubwa wako upande wa huku, Kwa Hani. Ikiwa tutapata watu wa Kwa Hani yoyote mwenye ushawishi na askari yoyote tutaanza kuzungumza habari hizi. Pale nikachukuwa mie dhamana, nikamwambia mie nnaye Hamisi “Beni”, nnaye Mohammed, na wengine, tutakwenda zungumza huko. Na yuko kijana mmoja Rajab, wa bara huyu, kwao bara, Rajab nani yule? Nimemsahau, sasa ndo namkumbuka, namuona hasa. Nikenda nkazungumza na Hamis “Beni” kama ni mtu wa kwanza kabisa. Hamis “Beni” akanambia “sawa”. Hamis “Beni” alikuwa pwani kule “boat man”, baharia, alikuwa na akina Karume pamoja. Nkamwambia twende kwa Mohammed Omar, tukamuendea Mohammed Omar, Mohammed Omar kumzungumza, akiitwa maarufu Mohammed Omar “Masharubu”. Akaniambia “sikiliza bwana, mimi nauza ulevi hapa, na hapa wanakuja kulewa askari hawa, sasa tukae hapa tungoje mpaka mchana, jioni, usiondoke, tutapika chakula, tutakula hapa hapa.” Ina maana yeye kakubali mapinduzi. Akaja Sajent Ngusa. Akampampa ulevi. Kabla ya kunywa, akamwambia, mimi sikupi ulevi kwanza. Sikiliza habari zangu hizi. Akamueleza. Akamwambia, sie tuko tayari zamani watu, lakini hatujuwi tuungane na nani, tunakuogopeni watu wa Unguja. Tukaja tukaongea naye pale pamoja, akaniambia “sasa bwana wewe wapate watu wawili. Ukiwapata watu wawili hawa wakakubaliana na wewe, basi tumeshafaulu.” Namwambia “nani?” Akanambia “mmoja anaitwa Simba Ismail, Sergeant Simba Ismail. Huyu Simba Ismail ana ushawishi na nusu ya asikari wa Ziwani, kwa sababu ni Sergeant anopendeza kwa asikari.” Nikamwambia “nitampataje. Mimi hata kumjuwa kwa sura simjui.” Rahisi. Mimi kesho, wewe njoo, mimi ntakuja hapa mapema, mimi kesho sina kazi kabisaa, nitakuja.

Asubuhi mie ndo nimeshakunywa chai nikapita Gongoni nikampa taarifa Saleh tulipofika, Saleh akaniambia “vizuri sana.” Nikamwambia “mimi nakwenda.” Nkenda mimi zangu kwa Mohammed. Kufika nilimkuta Ngusa na Simba tayari. Akanambia Ngusa, “huyu ndio Simba Ismail, nilokwambia.” Tukaongeaongea, akanambia “e bwana kuna mambo mawili, mimi tayari kubahatisha lakini si tayari kumuona Sergeant Saleh kumwambia maneno haya, lakini nimefikiri kuna mmoja ana ushawishi mkubwa Mtoni ntakwenda kumwambia.” Namwambia “sasa huyu ntampataje mie?” Akanambia mimi nikimpata ntamleta kwako tu saa yoyote. Ntakwenda mimi lakini Saleh, huyu Saleh ndo mwenye kikosi cha ulinzi. Kuna sehemu kazi yake ulinzi tu, wanakuwa katika mapalace huku, pale quarter guard, wanakuwa wao, manake wao ndo wanachukuwa ulinzi wa nchi nzima. Mtu wa Kilwa huyu kwao. Nikamwambia “ntampataje” akanambia sijui lakini huyu anasali msikiti wa Ijumaa wa Malindi kila siku, hakosi. Sasa mie ntakwenda kule ntakuonyesha tu “yulee” siku ya Ijumaa. Nkamwambia “nipeleke.” Na kwake anakaa Kikwajuni. “Ah! nende Kikwajuni, nende msikitini?” Nkasema “twende, ntakwenda mskitini.” Nikenda msikitini nkamuona Saleh nkamwamkia nkesha, nkamwambia “Saleh, mimi sikufichi bwana, sina siri ya jambo hili, nataka unifahamu. Unakujuwa kwangu?” Akanambia “sikujuwi. Kwani kuna nini?” Ndo nakwambia nlivyo mimi. Tunafanya mipango, na tuna kikosi chetu tayari kikubwa, lakini nimeona lazim nije nikuone wewe kwa sababu wewe ndo dhamana wa kikosi cha ulinzi cha Zanzibar! Na juu yako ni maofisa wengine. Umefahamu? Tunataka kupinduwa Unguja, unasemaje? Akanambia “Ah, hiyo rahisi. Tunaweza kufanya, ngoja siku ya zamu yangu, mimi ntakapokuwa mlangoni, siku ile ndo mfanye. Lakini itachukuwa kipande hapa itapindukia mwezi huu wote wa Disemba huu utakwisha huu, mie sijachukuwa, mie ntachukuwa katika Januari, katikati ya mwezi. Lakini ntakwambia rosta.” Nkamwambia “sawa.” Kuja, nika ripoti, nikamwambia “bado Juma Maneno sasa.”

Tukaja tukampata Juma Maneno. Saleh akaja kunipa ripoti hapa nyumbani. Juma Maneno kaja kwangu na Simba Ismail. Juma Maneno wa Mtoni, Saleh wa Ziwani. Hawa ndo walikuwa wale wakiitwa Police Mobile Force [PMF]. Sasa huyu Juma Maneno alipokuja hapa, tukaongea akanambia “mimi nimekubali, lakini jambo moja. Tukaonane na huyo alokuwa juu yako wewe.” Nikamwambia “rahisi, twenzetu.” Nikavaa suruali hapa tukenda Gongoni nikampambanisha na Saleh. Ilikuwa Hanga kwa hali yoyote hatoonyeshwa na mtu. Walipokwenda wakaongea wakapatana wakapeana mkono tukapika chakula tukala pamoja sku moja.

Sasa tunamtaka Kisasi. Mimi nkenda nyumbani kwake. Nkamwambia, e bwana Kisasi mie nimekuja unifunge au unikubalie. “Nini?” Namwambia, sie bwana tunataka kufanya mapinduzi tena kikosi kikubwa hata ukinifunga tutakuuwa. Nataka ufahamu kiasi hicho. Mimi niko jela lakini wewe utauliwa. “Nini?” Namwambia “sisi tunataka mapinduzi.” Akanambia, lakini mimi wewe peke yako bwana sikubaliani na wewe, lazim nimpate alohusika khasa mkuu. Nikamleta kwa Saleh. Kisasi akakataa kabisa mpaka akakutana na Hanga. Hanga alipokutana naye, tuifupishe hadithi…wakazungumza, akakataa kuongea mjini hapa wakenda kuongea Kitope. Kitope, kwenye nyumba ya Mwarabu fulani. Ah! Huyu Mwarabu nimemsahau jina lake, lakini siku yoyote, ngekuwa mzima mie ningekwishakwambia hata kesho ngekupeleka, maana yake yupo Kitope hapo kwake kwenye msikiti na, ule mti unonuka mavi, mdoriani. Mdoriani mkubwa, msikitini, iko nyumba pale pembeni, kubwa, ina saruji mbele ya kuanikia karafuu, mbata, nini. Tukenda tukakaa pale, tukapikiwa chakula tukala na wanawe na yeye.

Kitope ni ngome ya Afro-Shirazi, na ni karibu, kuliko kwenda Bambi. Ilipokwisha kubalika, ikawa sasa Hamis “Beni”, Mohammed “Masharabu” wao ndo kazi yao kukusanya watu wa kufanya mambo yale, kutafuta watu kwa kuingia Ziwani. Wao ndo walokuwa mas’uli wa kutafuta watu wa kuingia ndani ya boma Ziwani. Sie huku tumebaki na uongozi wa juu.

Mtoni aliwachiwa Juma Maneno, lakini hakufanya kazi nzuri. Ilibidi sie tulokuwa Ziwani twende tukasaidie.Tukenda Dar es Salaam, mie na Saleh Saadalla. Madhumuni tumuone Mwalimu Nyerere kumpa habari hizi. Kwa hivyo tukenda muona Waziri Mkuu Mheshimiwa Rashid Kawawa. Tukaongeaongea naye kutaka nafasi hizo akazungumza na Mwalimu tukashindwa kumpata. Kakataa kuonana na sie, kwa sababu anazozijuwa mwenyewe. Tukarudi mikono mitupu. Umenipata lakini. Tuliporudi mikono mitupu tukaripoti kwa mwenyekiti wa mapinduzi, Abdalla Kassim Hanga. Tulipokwisha ripoti kwake akakaa kwa muda tukafanya safari nyingine. Mimi, Hanga, Saleh, Twala. Tukenda kumuona Oscar [Kambona]. Oscar alituunga mkono mara moja. Lakini akasema mimi ni Waziri tu, lazima nipate rukhsa ya juu kwa jambo hili, lakini niwachieni mie.

Pale, palikuwa, sijui, na yule, ndo Balozi, au ndo nani, wa Algeria, nadhani Balozi, maana yake kulikuwa na bendera pale. Tukenda kwake, tukaongeaongea kidogo, tukampigia simu moja kwa moja, akapiga Oscar, direct na Ben Bella, akaongea Hanga. Ben Bella akatuunga mkono na akatuletea silaha kamili, ndani ya meli. Meli imezuwiliwa na serikali ya Tanganyika, bandarini Dar es Salaam. Hatuna la kufanya. Wakati ule, tuliporudi huku, mimi na Twala tulikwenda Bweleo kwa Mzee Mwinchum kuona namna gani tukiweza kupata silaha tutaziweka. Ikawa, tukaingia baina ya Bweleo na Dimani na kuelekea pwani. Kuna mapango makubwamakubwa ya majabali. Tukenda tukalitazama pamoja watu watatu, tukakubali lile, kwamba hili na hili litafaa. Mzee Mwinchum alokuwa Mwenyekiti wa Afro-Shirazi, Bweleo. Hapo, tukarudi mjini tukaripoti. Siku ya tatu au yane, tukenda na Saleh, na Mwenyekiti tukenda naye, akatazamaa, tukakubaliana napo, kwa sababu ni pazuri, tena pako ndani ya ghuba. Ile ya kutokea kwa BiKhole, na huku Bweleo, na Fumba. Si lipo ghuba limepita. Ilikuwa pale ni mahala pazuri sana kwa sababu za usalama wa kimapinduzi.

Kulikuwa na silaha kidogo kwa Oscar Kambona, hizi silaha zetu za jeshi hizi. Akatupa mukhtasari, tulikuwa mie na Twala. Tukabeba zile silaha, Msasani tumezichukuwa, kwake ndani manake karibu ya pwani. Na tulikuta zimeshafikishwa pale. Na alokuwa akibeba kutusaidia kutia alikuwa Kitwana Kondo. Huyu ndo alokuwa mlinzi wa Oscar, ambaye mpaka alifanywa akawa Meya [wa Dar es Salaam]. Yule ndo alotusaidia kubeba. Akazifikisha pwani pale ufukweni. Akazilinda, sie tulipofika, tulikuwa tunatokea Bagamoyo, kwa ngarawa. Tulitokea Bagamoyo kwa ngarawa na mshipi wa kurambaza ule. Tumekuja nao huku tunaonekana, pale tukakutana na boti moja ya Tanganyika police. Pana kama kichunguu hivi ukiingia hivi, kama jabali lile, visiwavisiwa vidogovidogo. Lakini walitupuuza tu. Waliona hawa wavuvi. Tumevaa matambara yale. Na chombo chetu ulikuwa upepo mzuri, mpaka tulipofika pale tukatia zile. Kuja zetu sasa. Tulikuwa na mashine ya kubandika ile. Tukabandika mashine. Tukapiga spidi kubwa. Sasa tushapita kisiwa hiki cha Chumbe, tuko ndani ya Zanzibar. Sasa tunataka kukisi kuingia ndani ya ghuba ya Fumba, na boti ya polisi inakuja, Zanzibar police. Alikuwa yule Banyani ndani, wako katika patroli, akiitwa Samra, Simri [Misra] sijuwi, tunamuona yeye, alikuwa Mshangama Masharubu, na nadhani Mohamed Ali Bahari. Lakini walikuwa watu wazuri, wengi. Wananyayuwa lile dude lile, lenye kupaza sauti. “Punguza spidi, simameni!” Twala akawaambia “Hatusimami, wala spidi hatupunguzi, na chochote mtakachofanya na sie tutafanya.” Twala ali kreki. Anamwambia Mzee Huseni “kaza moto, pandisha na tanga pale.” Twala akasema “unajuwa, tukifanya maskhara watatukamata, hii boti yao kubwa.” Akatoa ki bren gun cha pata hivi, kile wanaita nini? Sten gun. Ndio Sten gun. Hapana. Liko jina lake dogodogo. Wanatumia sana askari, kama bunduki. Akaitoa ile akaijaza. Akawaambia “hivi ndo tulivyo, njooni!” Hawakuja.

Mambo hayo yalikuwa wiki moja, au wiki mbili kabla ya mapinduzi. Hata wiki moja bado, mbili hazijafika. Badala ya kuingia Fumba tukaingia Bweleo. Kwa sababu Bweleo ndo tulikuwa na mipango yetu. Lakini Bweleo kulikuwa ni 100% usalama juu yetu. Sasa tulipofika tu, tukamkuta, nani yule pwani pale ufukweni…tukamwambia “kamwite Mwinchumu chairman haraka kabisa mwambie tupo hapa.” “Na aje na vijana.” Usiku bwana, alfajiri kubwa. Wamekuja watu sijui, zaidi ya kumi. “Unasemaje Mzee.” “Vitu hivi, chairman.” Tukavituwa tukawa salama. Sasa tatizo lilioko polisi sasa. Sisi hatujasafiri navyo. Tumeviwacha palepale, kwa chairman Mwinchumu wa Bweleo. Asubuhi tulipoingia ndani ya mutukari, tunafika kituo cha polisi cha Kiembesamaki, wanasachiwa watu. “Ewe bwana, tokeni tusachi gari.” “Kuna nini?” Ananambia “jana kulikuwa na vishindo huku.” Sachi. Yuko askari mmoja “umelala Fumba leo” nikamwambia “kesho ntalala Makunduchi,” kwao Makunduchi (vicheko). Tukasachiwa pale. Na tumekwenda gari mbalimbali mie na Twala. Zile gari za abiria. Silaha hizi tulizokuja nazo sie, tulizozichukuwa kwa Oscar ni silaha khasa. Nipe, nkupe.

Hatukuzitumia. Hatujatumia silaha ya risasi sie. Ila ikiwa kujihami. Tulikuwa nazo zile na tulizigawa kwa fulani, kwa fulani, kwa fulani. Lakini zote zilirudishwa. Basi, tukarudi, tukawa tunangoja. Sasa ile [silaha za Algeria kupitia Dar es Salaam] inakuwa imekawiya, tukaenda Tanga, mimi na Saleh, kutafuta njia ya pili. Wakati ule Tanga, Area Commissioner [Mkuu wa Mkoa] alikuwa Ali Mwinyi Tambwe. Tukaongeaongea kule, tukakutana na Jimmy Ringo, katika…ilikuwa sherehe fulani ya chama, usiku katika michezo ile. Tukakutana na Jimmy Ringo. “Nini Jimmy?” anasema “nakuja tu.” Nikamwambia “kuja tupu huwezi. Umekuja na vitu vingine lakini haizuru.” Sie tukatoka, hatujafanikiwa Tanga. Tukarudi, tukaripoti. Tukawaambia, basi tuwache, tungoje, wakati unawadia. Sasa ikija Januari, Disemba inamalizika. Tukaamua tuingie. Sasa tumuone Saleh kwanza na Ngusa. Tukarudi tukamuona Saleh tukamwambia jitihada nyengine hatuna, jitihada yetu ya kutaka kuingia tu. Akasema “sawa,” siku yoyote mtakayokuja mie ntakupeni nafasi. Nkamuona Ngusa, Ngusa akanambia “sasa sie tunataka kujuwa nini cha kufanya?” Asikari wakija wakivamia bunduki si watatuuwa tu. Sisi hatuna kitu. Akasema, tuzitowe bunduki zote zilio ndani quarter guard, bolt, spring, na magazine, tuziweke mbalimbali, vitu hivi, hata asikari akija kuchukuwa bunduki, haina kitu chochote ndani. Bolt iko mbali, magazine iko mbali, bunduki yenyewe liko mbali. Na risasi ziko mbali.

Sasa hiki chumba cha risasi kiko sawasawa na pipe juu kule ile ya upepo, atatakiwa mtu apande madhubuti, ikiwa mambo yamezidi atie moto tu. Nikamwambia “sawa.” Tukafanya utaratibu ukesha. D-Day [siku ya siku] ilipofika, ilikuwa Jumamosi kuamkia Jumapili, Januari 11 usiku, ni Jumaamosi kuamkia Jumaapili. Tumeingia sie Ziwani. Mimi nimekwenda Ziwani. Mimi nimepanda juu ya quarter guard, mimi nimekosewa risasi na Major Bott, Ziwani. Sergeant Saleh kuona kikosi kile kiloingia simo mimi, akazuwia pale. Ndo tumekwenda kwa mujibu wa muongozo wake. Kwamba sku ile yeye alikuwa pale. Ndo ikawa rahisi ati. Lakini alizuwia, alizuwia kwanza, hakuniona mie, na zile alama tulopeana. Kwa bahati nzuri kutaka kupiga kengele ile, alipigwa begani hapa. Kupigwa begani Major Bott kaja kule juu tena. Kuona mtu akapiga risasi Major Bott. Risasi ya kwanza kulia ilikuwa yake yeye na nnadhani huyu alikuwa ni Major Bott kwa sababu alikuwa anaonekana wazi katika usiku ule.

Lakini ukweli wa mambo ilikuwa inangojwa zamu ya Sergeant Saleh atakapokuwa kamanda wa silaha Ziwani. Ile kusema leo na kesho alikuwa Twala. Twala mwenyewe aliwahi kuitwa polisi, alihojiwa na Nassor “Mlawwaz.” Akimuhoji Twala kwa jambo hilo. Halafu akampeleka akenda kwa Kamishina mwenyewe. Akaachiwa. Akisema, na watu wakizungumza hoteli, barazani, nikawa na mimi nazungumza hivyohivyo. Ile ilikuwa kwa makusudi. Sio kitu kilotengenezwa uwongouwongo. Na ilitumiwa Twala kwa sababu ya Chama cha Wafanyakazi. Na ndo akaitwa. Lakini haijakawiya. Alipomaliza yale mazungumzo alipoondoka, siku mbili tatu, Saleh akawa yuko kazini na ikawa siku nzuri Jumamosi, watu wakaingia. Na ule usiku wote walikuwa wako hadhiri. Hata Raha Leo siku walodhania kuwa itakuwa khasa, walipeleka jeshi kubwa pale radio. Siku ilokuwa iwe hawakupeleka. Mtu tuloweza kumsaidia ilikuwa Babu tu kwa sababu ilikuwa afungwe. Tulimsafirisha kwa amri ya Saleh Saadalla. Hata Hanga alimlaumu Saleh. “Kwanini umemsafirisha huyu?” Hanga na Babu ilikuwa ni mdomo tu, lakini kisiasa walikuwa mbalimbali. Hawafahamiani kabisa! 100%.

Kuhusu uhusiano wangu na jeshi la Kiingereza, tumeondoka hapa 1942, watu sabini na tano, kutoka skuli, watu wawili kutoka jeshi la polisi. Huyu alotoka polisi alikuwa ni Khelef Said Rashid Al-Mauly. Na mwengine alikuwa ni Jacob Malambeka, Msukuma. Tukawa sote watu sabini na saba. Sabini na tano sote kutoka skuli. Tumefika Nairobi, katika kambi ya Karen Camp, tukawa depot pale, Karen. Katika “signal.” Ndipo tulipozinduka. Tunaingia tukakuta imeandikwa kwenye bango kubwa “ingia kujifunza wende kufa.” Sasa ile kufa imeandikwa double “a”, “kufaa.” Inamaana kama “kufaa.” Uende ukafae. Lakini haijulikani nini maana yake. Basi tukarejea depot pale, kama asikari kuruti. Tulipomaliza depot, tukenda kituo cha ufundi palepale kutufunza mambo mbalimbali. Kuna walokuwa wanajifunza dispatch radio, kuna walokuwa wanafunzwa wires, to lay down telephones, kuna tulokuwa tunafunzwa wireless and line operators. Wireless na line tukifunzwa namna ya kutandika wires, na Morse Code, na matengenezo madogomadogo ya wire sets. Sets zetu na sounders tukitumia.

Kilichotendeka kwa kuondoka kwangu asubuhi ile siku ya Jumamosi tarehe 11 Januari, 1964 mpaka kuamkia Jumapili, baada ya kuamka asubuhi, kitu cha kwanza baada ya kumaliza mambo yangu na kutoka, nilikwenda kwa Saleh. Nilipokwenda kumuona Mheshimiwa Saleh Saadalla Akida, tukaongea habari hizi kwamba sasa ilobaki ni kupita kituo, na katika kituo muhimu khasa tukajuwa watu wako vipi. Sehemu zote mbili. Basi, kituo chetu muhimu cha kwanza, kwa ajili ya Ziwani ni Kwa Hani. Kwa yule Khamis “Benii”! Tukenda tukaongea, Mohamed “Masharubu” akenda Ziwani ndani, quarters, kumuona Sergeant Ngusa. Tukajuwana mipango ya pale ilivokuwa. Akamuona Sergeant Waziri, tukenda sote, sehemu zote mbili, sehemu ya juu kule ilokuwa skuli ya Aga Khani, kule, kulikuwa karibu na magari. Tukenda tukaona zile waya zilivokuwa zishakatwa kama tulivyoagiza. Zile zimekatwa Jumamosi, alfajiri ya kuamkia Jumamosi. Ijumaa mosi zimeshakatwa. Na ilivokuwa upande ule hakuna mtindo wa polisi kupita kule, mara kwa mara, wanatarajia kwamba yale magari yako depot, yako pale parking yard [panapowekwa magari] yake, wale sentry wa pale ndo wanokuwa muhimu kwa ile pale, na wakati ule alikuwa jamaa mmoja akiitwa Feruzi, siku ile, na ndo alokuwa yeye dhamana. Huyu ni Sergeant wa madereva. Sasa, tukakuta mambo yale pale yapo tayari, na tukaja huku upande wa Mwembe Matarumbeta, pana gate pale, ya sentry. Ili ku cheki police quarters, ndo pale mlango wao wa kuingilia pale. Anakaa asikari pale, akifunguwa mlango kwa magari, kwa nini, watu wanapita. Kuona kama zile bawabu za mlango zimetolewa. Si vinakuwa vyuma kama va geti zile, za kupandisha na kuteremsha. Basi tulihakikisha ile moja imetoka ile bolt yake yote, kwa hivo huwezi kufunga, unakwenda tu bila ya kizuwizi. Sasa ile imetolewa usiku wa kuamkia Jumamosi, kama ulivotolewa waya kule, usiku wa kuamkia Jumamosi. Sasa sehemu mbili ziko wazi. Kuna mtu mmoja ambaye ndo alokuwa mkuu wa kikosi kile kule Kwa Hani, akiitwa Farhani. Farhani nani huyu? Nimemsahau babake. Lakini ana jina la Kimanyemamanyema hivi. Watu wa Kimanyemamanyema.

Nikamkuta. Akasema, “watu wote hata kazini hawakwenda leo. Watu wamekaa standby [tayari]. Wanokwenda pwani hawajenda, wanokwenda wapi hawakwenda. Wote wako tayari.” Hawa ndo wanopita kwenye geti, chini ya quarters. Nilikwambia kulikuwa na vile visilaha viwili vitatu, hawa ndo walokuwa navo, kwa kujihami ikiwa wametoka watu kule. Manake hawa ndo wanopita quarters. Tukarudi, mimi nikaripoti kwa Saleh. Nikenda kwa Twala nikaonana naye. Twala akanambia “Saleh na brother Hanga lazim waondoke leo.” He! Namwambia “sasa wataondoka na nini?” Ananiambia “wataondoka na chombo chochote.” Na nani atasafiri nao? Ikabidi Mohamed Omar “Masharubu” afatane na msafara ule. Manake ni lazim ende mtu tunomuamini, tunakuwa hatuna wasiwasi naye. Litakalotokea si atakayekwenda mbio. Lakini atakuwa na wao pamoja. Nikarudi tena Kwa Hani. Nikamtafuta Mohamed. Nikaambiwa kenda shamba, Mwera, jirani na kina Amar Salum. Yeye alikuwa ana mawasiliano na wazee wake. Ikanibidi nichukuwe gari ya Ali Saidi. Tukenda. Tukamkuta Mohamed. Nikamwambia Mohamed “utakwenda na Hanga na Saleh.” Akanambia “sawa twendezetu basi.” Tukaja akajitengeneza, saa moja ya usiku, baina ya saa moja na saa mbili ya usiku wa Jumamosi Hanga na Saleh wakaingia ndani ya ngarawa wakaondoka.

Saleh alikuwa hataki kuondoka. Nikamwambia “ikiwa hutaki kuondoka utakuwa umeasi.” Kwa hivyo sisi tunataka uondoke. Kwa sababu ikiwa kutakuwa na makosa yoyote ya kuelekea kushindwa au kukamatwa au kulipiza kisasi, watakapokuja kukulipiza wewe kisasi utatuvunja sote nguvu zetu. Kwa hivyo watu washakubali wende. Akaja Simba Ismail, akasema “lazim ende. Akiwa hataki tutampakia kwa nguvu.” Akakubali, akalainika. Kama saa tatu ya usiku, mbili, tatu, akaondoka. Wakati mimi nakwenda kuhakikisha kusafiri, memba wa Umma Party, hawana hata habari. Wako hapo barazani. Hapohapo nimepita mimi, wako pale wamekaa kitako.

Mimi nlikwenda mchukuwa Hanga usiku ule wa mapinduzi, mapema kidogo. Nlikwenda mie na Mohamed Omar Masharubu. Kikwajuni, kwa Ali Ngwengwe. Sasa alipokuwa anatoka Hanga akamuaga mjomba wake, mwangoni pale, akamkumbatia. Akambusu. Na mjomba akambusu Hanga. Wakabusiana. Akamwambia “mjomba Mgu akipenda tutakutana, lakini usitaharruk kwa utakayoyasikia yatakayotokea leo usiku. Mwenye Enzi Mungu akipenda tutafuzu.” Na hapo ndo mkewe Hanga, yule Bimkubwa Saidi wa Maghee, yuko ndani. Basi sijui sku zile keshamuoa au bado, Allahu Yaalam Wa Rasulu. Anakuja mwangoni kumuaga. Tukamchukuwa tukaja naye Kizingo, upande huu kuna makaburi na mikadi, pale ndipo tulipompeleka akaingia ndani ya ngarawa. Ngarawa ya nani, ya baba yake Fuko.2

Napita mimi, Imam wetu wa Msikiti ananambia “usiku huu unatoka unakwenda wapi?” Nikamwambia natoka nakwenda kumuamkia bwana mkubwa [baba yangu]. Mie lazim nende usiku, kwake, lazim, halafu ndo nakuja lala. Nikakutana na Mzee Mbaba, alokuwa Inspekta wa polisi, na baadhi ya wanawake, kakaa katikati na kundi la wanawake. “Wapi unakwenda usiku huu?” Nikamwambia “nakwenda nyumbani kwa babangu mie. Ndo kweli nilikuwa nakwenda kumuaga.” Huu ndo ulokuwa ukweli wa mambo. Niliporudi tena kutokea huko kama saa nne unusu ya usiku. Sasa mimi niliporudi hapa saa nne usiku nilikutana hapa nyumbani na Simba Ismail, tuko barazani, Juma Maneno, Ngusa yupo hapa barazani, Saleh hayupo. Saleh yuko kazini. “Je vipi?” Nkamwambia “kila mtu position [nafasi] yake sasa hivi ende akakae. Hakuna mchezo sasa. Wakati ukifika, hakuna kungojana, time ikifika, saa sita kasoro dakika tano, tunaingia bomani.” Isizidi. “Barabara, barabara.” “Barabara, barabara.” Kwaheri.

Wakatoka wakenda zao. Saa sita kasoro dakika kumi na tano, mimi nimeshaingia ndani ya yard [eneo]. Peke yangu. Nimepita hapa chini Mwembe Matarumbeta. Kwa sababu mimi nataka kupanda juu kule, ya quarter guard.

Kuna kidude kile cha kuunguzia nyumba yote iunguwe. Sasa nilipoingia mie pale nakwenda zanguu mpaka kwenye muembe mkubwa Bomani ulokuwa nyuma kule, wakichezea paredi askari. Pale mchana pana kivuli kizuurii! Pale na quarter guard ile pale. Sasa ilibidi nitambae kwa tumbo. Sasa kwa upande huu, wa magharibi, kuna taa nyingi, ndo mbele. Kule ndo kuna mahala pazuri pa kupanda. Huku hakuna lakini, nkaona sasa ntarudisha mafunzo yangu ya kijeshi. Pale ndo nkapanda kwenye bomba la maji lile.

Mimi ndo mtu wa mwanzo kuingia Bomani [Ziwani]. Wa mwanzo kabisa. Mpaka dakika kumi, dakika tano nzima nimekaa kwenye nanhii, kwenye sakafu ya juu. Natazama harakati. Ndo kukatokea kidogo kutofahamiana. Kwasababu Sergeant Waziri alikuwa anantarajia ataniona mie, halafu awache wazi gate [lango]. Sasa hakuniona, kataka kuzuwia. Kutaka kuzuwia, Bott akaona kule juu. Major Bott. Sasa Major Bott alipoona, kilichomjuulisha ni ile sauti yangu juu kumwambia Sergeant Waziri “wacha!” Bott akaanza kupiga risasi kule.

Na ukenda Bomani, nadhani, mpaka leo utakuta alama ya risasi alokosea Bott akapiga kwenye hii kona hapa ya jengo, mimi nkaaunga chini, au sivo angenipiga risasi ya mbavu. Sasa kuondoka mie kuanguka kwangu pale nikafika miguu yangu juu ya magunia ya mchanga yalokuwa yamewekwa pale. Kichwa kikafika kwenye saruji, kwenye lami, ile njia imetiwa lami, ndo nkaanza kupata na ugonjwa wa macho kudhihirika. Hapo ndipo mapambano yalianza. Alipigwa begani Sergeant Saleh kwa kuangusha ile firimbi ya alert. Watu wakavunja mlango, gari kule zilikwishatiwa funguo, na yule Sergeant Feruzi alokuwa dhamana pale, ilikuwa imeshatengenea. Wale walipoingia walivamia magari tu. Wale waloingiliwa kule. Wale walikuwa ni madereva. Walipoingilia kule kwenye waya ule walifikia kwenye gari. Zile gari ndo zilikuja moja ikapakia bunduki zote zilokuwa pale zikapelekwa Kijangwani.

Ni kiasi ya watu ishirini tu wa Ziwani. Na hawa ni kundi lilotoka Kwa Hani. Mtoni ilikuwa ni mchangayiko. Juzi tulikutana na kijana mmoja akiitwa Hamid Ameri ambaye ndo nlokwenda kumshawishi akubali. Yeye ndo alokuwa dhamana wa Mtoni, chini ya Youth League. Na kina Ramadhani Haji. Wengine siwajuwi. Lakini kina Haji Mlenge, ambaye alikuwa dereva wa Waziri Mkuu Hanga, halafu akawa dereva wa Makamo wa Raisi huyohuyo baada ya mabadiliko…

Sie tumekwenda, mimi nimekwenda kule [Mtoni], mambo yashawaka moto. Kufika kwangu Ramadhani [Haji] akapigwa risasi ya tumbo ile, pamoja na kikundi nlokuwa nacho. Kikundi nlokuwa nacho mimi ni wanachama wa ASP walokuwa kutokana na Kitope. Tukaingia kwa daafa moja, kwa nguvu kabisa. Na sie tuna silaha za kawaida kama za wale. Pale wakasalimu amri. Kwa nguvu hii ilotoka huku [Ziwani]. Mtoni walikuwa hawajamaliza. Wanazonganazongana tu. Wale wana silaha za bunduki, hawa hawana.

Watu walitoka Kwa Hani, Kitope kidogo, halafu kwa alivokuwa Hamid [Ameir] yule ni mtu wa Donge walikuwepo, watu wa Donge walikuwepo wakaungana naye. Na Youth League, ndo akina Sefu Bakari walikuwa na hadhi, na [Abdalla Saidi] Natepe.

Mimi sikuwaona kina Sefu Bakari na Natepe, lakini wanajuwa mambo. Kama Natepe, ndo alokuwa anakuja kwa mashauri mara kwa mara kwa Saleh [Saadalla]. Alikuwa kila wakati ndo anakuja kuuliza. Lakini wao walikuwa na kisehemu chao, cha Youth League, mimi siwezi kukieleza, sijui. Manake walipewa dhamana, kwa sababu itakuwa haijaelekea kutaka kumuongoza mtu ambaye ni Raisi au ni Katibu Mkuu. Manake yule Sefu alikuwa ni mkubwa wa Youth League.3 Natepe alikuwa ni Katibu Mkuu wa Youth League. Sasa wale wawili walikuwa wanakuja kufanya mashauri kwa Saleh Saadalla.

Hilo jambo lilikuwa ni mafahamiano ya kwanza. Ilikuwa hatutaki kuchanganya mapinduzi na chama.4 Ni vitu tafauti. Hata wao Youth League waliripotiwa wale na akina Karume, Youth League walikuwa wanataka kufanya mapinduzi. Karume alisema “wahuni hawa wanataka kufanya nanhi.” Karume alikuwa akipinga kabisa. Ati amejikinga, anataka ale yeye tu, kuku mzuri na mbuzi.

Wanaweza Youth League kutengeneza listi yao ya watu wale walokuwa kwenye matawi, kwa sababu wanajuwa hizo habari zote. Na upande huu ambao tulookuwa waasis wa mapinduzi, nchi hii, yetu, nafasi yetu haikuwa ya kawaida, maanake mara kuingia, chuki ya huyu anamchukia huyu, kama nilivokwambia mie kwanza, Raisi wa dola anawachukia raia na memba wa chama. Wewe fikiri pataandikika kitu. Wale wakipendeza kwa Raisi. Kwa hivo itakuwa listi kamili wamejaa watu wa bara watupu au wengi wao.

Listi ya waasisi, mbali ya sisi viongozi, ntakwambia ni Hanga, Saleh, Twala, Khamis Beni, Mohamed Masharubu, Ngusa, Juma Maneno, Ismaili, Saleh, bas! Hawa nawakumbuka uzuri. Hata akija Munkar wa Nakiri ntajibu suala hilo. Sina tabu nalo.

Khamis Beni khasa alikuwa ni raia wa kawaida, kazi yake boatman, alikuwa akisikilizana na Karume sana, lakini kaanza kuudhiana naye sana wakati wa maandalizi ya mapinduzi. Manake alikuwa hataki anamuona mtu anashughulika asijue anashughulikia nini. Lazma ajuwe, kama Mngu. Kwa sababu alikuwa…Mzee Karume alikuwa ni mtu mzuri, lakini alikuwa ni dikteta wa daraja la kwanza. Hataki kukosolewa. Hata ukimkosowa, akiliona ni zuri atakujalifanya mwenyewe baadae. Lakini kwa wakati ule wewe umeliongoza halitaki. Madam halikutoka kwake. Amekuwa kama Musollini wa Italy.

Ile ingekuwa tumekishauri chama yasingefanyika mapinduzi. Hili jambo kabisa nakupa. Ilikuwa wale watu hatuwaamini. Tulikuwa hatuna fikra nyengine ziada. Siwezi kukudanganya. Lakini wale watu walikuwa si waaminifu. Wote walikuwa ni watu wazima, wazee, hawako tayari kupangana na chochote cha nguvunguvu.

Ewe bwana wee ukumbuke miaka mingapi leo, arubaini, nilikuwa na umri gani hapo? Leo unambie mapinduzi leo, ntakubali? Sote tuloshiriki kupanga, na nini, ukiwatazama wazee wa Afro-Shirazi, wanaweza kutuzaa sote. Huna utakayemwambia akakubaliana na wewe.

[Kwa upande wa Tanganyika] Kitwana Kondo alikuwa mlinzi wa Oscar Kambona. Hata tulipokwenda sie kuonana na Oscar, huyu tunaye. Tukenda Msasani kwake kule Oscar pwani majabalini huyu tunaye usiku. Sie tunaongea yeye kakaa kule. Huyu kaja Unguja, kama kesho kutwa tutaingia Ziwani. Kaja kafikia nyumbani kwa Saleh Saadalla Akida, Gongoni. Na kaja na ujumbe kutoka kwa Oscar kwa Saadalla. Ujumbe ule ulimwambia Abdalla Hanga, green light, go ahead, [endelea na mapinduzi] na siku ya mwanzo mtakapotangaza serikali yenu mie ntaleta askari kukulinda wewe. Sasa sijui alikuwa na maana gani kusema ntaleta askari nikulinde. Sasa siku ya pili, ya tatu, akaleta jeshi, jeshi aloleta ni askari wa FFU [Field Force Unit] wakiongozwa na Captain Baruti kutoka Kigoma na Inspekta Zonga kwao Tanga. Mie ndo nkenda pokea jeshi lile. Na tukawapeleka Mtoni. Hiyo ndio zawadi ya Kitwana Kondo. Pundugu alikuja, baada ya mambo kutulia, akawa polisi kama ni Naibu Kamishna kwa kuongoza kikosi cha polisi.

Tulifikiria ingekuwa mapinduzi hayajafaulu tungelifanya nini na ndio maana tukawaondowa watu wawili wale [Hanga na Saadalla]. Najuwa wale kwa kuamini kwamba wale watafanya kila njia kupata msaada wa sisi hapa wa kupigana. Sisi siku ile tuloingia ndani ya mapinduzi tuliandika barua kwa President Nyerere, President Kenyata, na President Milton Obote. Tukazitia posta. “Tunataka kuondoa ukoloni wa mwisho.” Hatukusema tunataka kuondoa Waarabu. Tumesema tunataka kuondoa “last colonialism”. Ukoloni wa mwanzo wa Kiingereza uliulinda ukoloni wa Zanzibar wa Kiarabu. Kwa hivyo hii ya kwanza [ya Muingereza] tushaondoa, na hii [ya Mwarabu] tunaondoa. Tunataka mtutambuwe kwa haraka.

Tuliiandika siku moja kabla. Hanga, Twala na Saadalla, na mimi, lakini mwandishi dhamana ni Twala. Timu yetu ya watu wane. Tumeandika wazi. Sie tunaingia Bomani na barua zinakwenda huku. Zimetiwa posta Dar es Salaam. Barua inasema: usiku tunachukuwa khatuwa hii, tunataka mtutambuwe. Na ndio sababu ilivoondoka meli hapa ya Unguja ilipompakia Mfalme na watu wake ikenda Kenya, ikakataliwa kupewa mafuta, ikakataliwa kukaa, wakakataliwa kushuka. Basi sijui kama wamepewa vyakula na vyenginevyo.5 Chini ya ushawishi wa Kiingereza, British High Commission [Balozi], na serikali ya Tanganyika, wakakubali wale kushuka [Dar es Salaam], na British High Commission ikawapokea kama ni wakimbizi, na ikawasafirisha Uingereza kwa usalama wao. Si ndo mara tu baada ya mapinduzi akaja hapa Waziri wa mwanzo wa Mambo ya Nchi za Nje wa Kenya, tukanywa naye chai Ikulu. Jina lake linaanza na K [Mbiyu Kionange] mwembamba mwembamba hivi. Ndo alokuja hapa akaonana na Raisi na akafanyiwa party, na ndo siku alosema Karume kumwambia Jamali Ramadhani Nasibu, “hii ni nzuri kinywani lakini ikishaingia tumboni inakuwa kama farasi alokuwa hana khatamu, anakwenda mbio anakimbilia polisi tu. Basi usinywe.” Uganda hawajatujibu kheri au shari. Walikuwa kimya. Basi sijui tena baadae. Mambo ya kiserikali yanaishia kwenye cabinet ambayo mimi siyajuwi. Nyerere kaleta kikosi kile cha polisi. Barua amesaini kiongozi wa mapinduzi, Abdalla Kassim Hanga. Na yeye Hanga ndo alofanya ordha na watu wapewe medal [nishani], ya walopigana, na akampa Raisi Nyerere, kabla ya kuuliwa, kabla ya hata kufukuzwa. Basi sijui ndo hiyo ilomsababisha kufukuzwa, sijui.

Tunavoamini sisi Ali Muhsin, shabaha yake yote ni kumuondowa Mfalme na kuifanya jamhuri nchi hii. Tunavoamini sisi. Pengine kweli, pengine si kweli. Kwa sababu sote tunaamini Ali Muhsin alikuwa hataki Ufalme. Sisi tunajuwa Mngereza anajuwa yote. Matokeo yake alileta manwari mbili zikasimama hapa. Moja Chumbe, moja Prison Island. Hata kama zile details [maelezo] walikuwa hawajazijuwa walijuwa mapinduzi yatatokea.6

Mimi binafsi, dadangu alikuwa ni mmoja katika viongozi wa wanawake katika ZNP. Siku ile ya mapinduzi Ali Muhsin alikuja mchana hapa na mimi nilikwenda kule kwa shangazi langu. Nkenda, nikakutana na dada, Ali Mushin kaja akanikuta mimi nyumbani. Tukaongeaongea maskharamaskhara, nikamwambia, “Sheikh Ali mimi naona kama mwisho wenu uko karibu bwana. Hamuwezi kuendesha hii serikali.” Akanambia “Mimi najuwa nyie magozi mnataka kupinduwa Unguja zamani gani.” Walikuwa wanajuwa. Dharau. Na dharau yao kubwa ni ilikuwa juu ya silaha.7

Wanaona hawa hawana hata bunduki, watapinduwa wapi. Na sie tuna jeshi kubwa huku. Hajui kwamba hili la huku lishakufa kama fimbo ya Nabii Sulemani. Kumbe imeshaliwa na mchwa imeshaanguka yote. Jeshi lilokuwa madhubuti ni Mtoni na limewahi kuzuwiliwa kabla hatukuingia mpaka likamalizika. Na lile lilikuwa jeshi kubwa, lile ndo special service, SS, wakiita Mobile Police Force.

Mapinduzi, first shot round about [risasi ya mwanzo ilifyetuliwa] saa 1:30, 1: 45 alfajiri/asubuhi. Wale kuingia ndani, wale waliokuwa na Youth, wamepita kule, gari zilikwisha tiwa funguo, gari hizi za serikali, sasa wale madereva walokwisha tengenezwa kule walikuja kuvamia gari tu. Sasa zile gari ndo zilichukuliwa kubebea silaha, hizi za quarter guard huku, kwanza kupeleka Kijangwani. Halafu watu wametia wakipigapiga. Zikilia ovyo usiku zile. Hazina shabaha yoyote. Sasa hapa ndipo control [udhibiti] ya mapinduzi imepotea. Kwa sababu ilikuwa ni fujo tu, kila mtu akifika anapewa bunduki anapiga, akipewa bunduki anavunja nyumba ya mtu. Huo ndio mwanzo wa mapinduzi ya Unguja [Zanzibar] na ikamalizikia hapo. Sasa hapo kuna tatizo kubwa lilikuwa Mtoni. Wale waloingia Mtoni, kikosi cha polisi cha Mtoni kilipigana mpaka sisi huku [kutoka Ziwani] ikabidi tutoke twende kule. Sasa imeleta matatizo kwamba kituo cha Malindi kimesahauliwa. Kituo cha polisi cha Malindi kilivamiwa na maofisa wakubwa wa polisi kwa kuzuwia gati na upande ule wa kule wa palace [jumba la Mfalme]. Na huku ilikuwa lazim twende kwa sababu tukiwacha ile itakuwa na nguvu, na wale wana silaha nyingi kule. Tukabidi twende kule. Tukaacha kidogo huku. Kule walikufa watu wawili, wa kikwetu, lakini pia kuna askari wane watano walipoteza maisha yao vilevile na mmoja alodhurika zaidi na yuhai ni Ramadhani Haji. Alipigwa risasi na mlinzi lakini ilikuwa haikwendwa uzuri tumboni. Badili ya kuingia imepita. Kwa hivyo imemuunguza huku, matumbo yametoka, na alikuwa upande wangu, kwa hivyo alivokuwa karibu yangu lile shati langu mimi ndo nlovaa, ndo nlotowa nkamfunga mie, matumbo yalikuwa yashakuwa yako nje, akatiwa ndani ya gari na yuko kijana mmoja ambaye ni katika nduguze vilevile huyo. Huyo Ramadhani ni katika mmoja alotokea Youth League.

Ziwani hakujakuwa na kazi, na ilianguka kwa urahisi, mara moja. Hakujakuwa na tatizo. Ilozuwiwa ilikuwa ndo hiyo [Mtoni] tu nlokwambia. Mtoni kulikuwa na mapigano. Sio madogo, makubwa kidogo. Kwa sababu baadhi yao wengine [wanamapinduzi] kule hawana ujuzi wa bunduki. Halafu, kulikuwa hakuna mipango mizuri. Sasa lakini sisi tulivokwenda tulikwenda kimabavu. Maanake ilikuwa hakuna njia nyengine. Tulikuwa na jamaa mmoja…akasema “jamani? Twendeni tu. Tuingie moja kwa moja pale quarter guard. Tukishaingia quarter guard, basi.” Hapa ndipo walipokufa watu wawili. Lakini tumeingia quarter guard. Tulipoingia quarter guard, likapigwa tarumbeta, tarumbeta lile lilipigwa quarter guard na ofisi kuu. Yule alopiga tarumbeta, alipigwa, amekufa yule. Sasa wale wanakuja kukusanyika kwa nguvu upande ule, sie tushachukuwa kila kitu. Iliwabidi wasalim amri. Wengi walisalim amri wakachukuliwa wakapelekwa, huku…gerezani. Wengine walikimbia. Polisi ya Ziwani, Mobile Police, walikuwa vijana wenye damu safi ya Kizanzibari. Haijakuwa nanii…chakachaka, hapana. Kwa hivo hata zile risasi zilokwenda za kuchaguwana kidogo. Ilikuwa ni damu ya Kizanzibari safi. Na ndo wengi wametolewa tolewa, nini, ah!

Magereza haikuendewa. Magereza ilikwenda funguliwa tu na mob [watu]. Halafu kwa sauti ilotolewa katika redio, mahabusu wote watolewe huru, wakafunguliwa wale. Mtoni ndo kulikuwa na mapambano mazito. Na Malindi Police Station. Malindi ilikuwa chini ka Kamishna wa Polisi [Sullivan]. Palikuwa pazito mpaka akatoka Mfalme, akenda akapanda na watu wake ndani ya meli, ndo akatoka Kamishna na maofisa wake kwenda kule.

Kuivamia Malindi hii ilipangwa Raha Leo wazi. Manake Malindi vikosi vyake vimetengenezwa va mkamatio hapa Raha Leo. Makundi tu ya Afro-Shirazi yalokuja, wewe utakuwa dhamana wa kundi hili, wewe utakuwa dhamana wa kundi hili, wewe utakuwa dhamana wa kundi hili. Baada ya vita va Malindi hata Raha Leo sikwenda tena. Baada ya kurudi kumaliza nikakaa nyumbani. Baada ya kurudi kule siku ya pili au ya tatu nkakutana na Ali Muhsin, Raha Leo. Anapanda ngazi, mie nateremka ngazi. Nilimwambia mie Ali Muhsin “umefanya makosa” Ngazini, ngazini. Manake kaja kujisalimisha mwenyewe, hajakamatwa. Kajileta mwenyewe. Halafu sikumuona tena Ali Muhsin mpaka nkaja nkamuona niko Magomeni mwezi wa Ramadhani ashafunguliwa, Dar es Salaam, msikitini tena. Yeye na Abudu, na alifikia Magomeni kwa jamaa yake fulani. Tukaongea pale. Akawa “mimi nakwenda Lindi kwa jamaa zangu.” Nkamwambia, “Ali Muhsin, mimi si mtoto. Mie najuwa unakwenda zako Arabuni na unapitia Tanga, tena sio mpakani.” “Ah! Tusiongee tena.” Nikamwambia “basi. Mie hayajanihusu. Nayajuwa. Mie tangu uko jela naijuwa njia utakayopita.”

Mapinduzi tulivotaka ifanyike sivo ilivofanyika, lakini ingefanyika tulivotaka ingekuwa…tena wakati ule ilikuwa mob [kundi la watu] limeshaingia, fujo. Na ndipo alipokufa rafki yangu, Mapolo. Huyu alitoka Kitope. Huyu kafa Malindi. Yeye akiendesha gari ile, ya polisi tulochukuwa kule, akapakia watu, wakapita njia ya Hollis Road. Njia ileile tulosema isipitwe. Watu wateremkie Funguni, waje hapa kituo cha petroli, ndo inaitwaje? Auto Sale. Watokee pale, na wengine wapitie kwa Safriji, wapite Kokoni, watokee uwanjani Malindi kwa pembeni. Wengine wende mlangoni Malindi kuingia gatini. Hawakufanya vile. Wamekwenda mob mbele, wote wamekwenda Hollis Road, wale wako juu wanakupigeni wanakuoneni. Sasa Mapolo anafunguwa mlango, wale waliomo watoke, yeye kala chuma, kafa pale pale. Nimeskitika sana. Rafiki yangu mpenzi Mapolo. Myamwezi huyu wa Kitope. Mimi nilopoambiwa kuwa amekufa, nililia. Nimesema wangekufa wote wale afadhali (vicheko).

Wale walikimbilia kwa kumzuwia Jamshid asipatikane. Sasa Malindi ilikuwa iwe hivi. Kaskazini ni kutoka Hollis Road kuja Malindi polisi. Hii ndo Kaskazini, isitumiwe. Watu wapite Funguni, waje Malindi, Jongeani, wakiwache Kituo cha Polisi cha Malindi, wapite katika kijia kile cha Bwawani, kwa leo, watokee Auto Sale, chini ya kituo cha polisi. Pale pana mikingo ya lile dude la barafu, ya Auto Sale, na kuna vituo va petroli. Si rahisi kupiga risasi pale. Na wengine wapite Darajani kwa Sapriji, watokee Kokoni, wapite Dega, watokee Malindi, ubavuni.

Hizi ndo zilokuwa zangu mimi. Yale maagizo yote ya pale yalikuwa yangu. Hii nikimpa Ahmed Gharibu na kundi lake kubwa, ya Malindi, ya kupita Kokoni. Walikuwa wengi kwa sababu baada ya Ahmed kupitia njia ile kavuka, unaona hapa Makao Makuu ya Hizbu ilipokuwa [Darajani], akapita pale, kama Mbuyuni anakwenda, na pale palikuwa rough-rough hivi, mpaka karibu ya Kituo cha Polisi cha Malindi. Huku kaona kuzunguka. Ndo nkamwambia “Maalim namna gani?

Umefanya makosa. Tungewakamata wote wale, manake wasingeliweza kutoroka.” Hakufuata amri. Na ndo hata wale waloingia Malindi kule akauliwa Mapolo. Walichukuwa njia ya katikati wakaacha kuchukuwa njia ya Malindi, Funguni. Ahmed Gharibu tulimwambia apite hapa Darajani police station, apite, pale kona ile inaitwaje. Dega, umefahamu, apinde kulia, anakwenda kama kwa yule Muhindi alokuwa akiuza vifuu yule, akiuza vifuu na maganda ya machungwa. Pana uchochoro wa maghala, palikuwa na maghala hivi. Njia nyembamba hivi. Mkono wa kushoto unakwenda kwa Sayyid Omar bin Smeit huku, mkono wa kulia unakwenda zako Kituo cha Polisi cha Malindi. Hapa katikati ndo kwa Omar Zahrani. Sasa ile ndo njia nyembamba ile ndo tulotaka apite ya ghala, ili atokee kwenye kile kikuta chembamba cha Malindi police station. Wakiingia mle wanavamia counter kwa mgongoni.

Ile ya kupita Malindi, ilikuwa chini ya Mapolo. Kupitia Funguni, waje zao hapa. Kuna instruction [maelekezo] ambayo mimi binafsi naliongoza kikundi. Kupita Darajani police station, tukatambaa na line ileile ya njia ile, kwenye benki ile, moja kwa moja, mpaka kwenye garage ya motokari na petrol station, ambayo ndo pale polisi, hili hapa ndo jengo, hii njia unakwenda zako Malindi, Kokoni. Pale ndo zikaanza action, kuja kuandamana na nyumba zile zoote, mpaka hapa Baraza la Mji, halafu tukatokea duka la petrol station na zikiuzwa motokari. Hapa na pale. Tukitumia cover ya zile ngoeko za nyumba. Mapolo alikosea au hakufuata mipango. Wakapita Hollis Road moja kwa moja, katikati. Kwa bahati mbaya, Mapolo kufika kwenye [leo pana] traffic light, akapigwa risasi, akafa. Na pale yeye ndo alokuwa the first man to enjoy the bullet [mtu wa mwanzo kula risasi]. Wakati ule anapigwa, mimi namuona. Nalitokwa na machozi, lakini siku lose control. Nashukuru. Kwa hivyo tulikuwa na watu sita. Wawili walikuwa na machine gun, zile [kutoka Algeria] tukazipiga kwa pamoja. Wakati Ahmed Gharibu, kwa kutokea Dega, akawa anapiga yeye juu, walikokuwa wale. Kwao Ahmed Gharibu alipata risasi ya mguu. Ilikuwa kwa makosa kwenye kisigino. Kiatu (anacheka) kiliruka. Ilikuwa very nice joke [lilikuwa ni jambo la kuchekesha]. Na si rahisi kuamini. Lakini risasi ilipiga kwenye kisigino.

Nilikuwa nimepanda juu. Sasa utapigaje? Sasa ungekaa chini pale wanakupiga na wewe huwaoni. Lile jengo lile, petrol station, ubavuni mwake, kuna jengo jengine, kuna ngazi, mpaka leo ziko pale. Pale ndipo unapopandia juu balcony. Juu wakikaa Wahindi, Bohora, walokuwa na biashara ile.

Wasifadhaike kwa nini? Ilikuwa gari moja Simca, ndani mle, alikuwa mtoto…“kuna wezi wanataka kuiba gari chini”, anawaambia wazee wake. Kwa Kihindi mpaka Kiswahili. Yeye kila akisema wale wazee wale wanamvuta. Mie nilikuwa sina hamu hiyo [ya kuiba gari], wala sie hatujawa na hamu hiyo. Pale ndo zilipoanguka risasi. Nadhani polisi ilipiga risasi ndani mle lakini sijui kama iliuwa au haikuuwa, sina hakika. Walipiga.

Kilikuwa ni kipindi kifupi. Kama dakika arubaini na tano au kama saa moja. Manake wale mpaka wamehakikisha Jamshid ameshaingia ndani ya meli.

Mimi ndo nloongoza, na Mohamed Khatibu. Hawezi kunambia mtu jambo jengine. Na akisema atasema tu anavotaka. Mimi sipendi kuongea habari hizi. Na juu walikuwa chungu nzima na walikuwa wana risasi nyingi. Hatujapata fursa ya kukiuka kile kikuta kile, zilikuwa risasi zinakuja kama mvua pale. Yuko kijana mmoja, Khatibu Mohamed, maskini amekufa, huyu alikwenda kwa tumbo, na upande huu wa pili ambao Ahmed anakuja kwa tumbo, kwa sababu hawa wote walipata mafunzo ya kijeshi. Wote walikuwa asikari kabla. Ahmed Gharibu, na huyo Khatibu. Ahmed Gharibu alikuwa katika East Africa Education Corp, alikuwa mwalimu jeshini na aliondoka na cheo cha Sergeant-Major. Ami yake alikuwa mwalimu wa chuoni wa nyumba ile ya palace [nyumba ya mfalme]. Kazaliwa humo, kazaliwa palace, kakuwa palace, wote na wazee wake huko.8

Na Mapolo alikuwa polisi wakati ule. Sasa wanataka kuingia kwenye kile kikuta kile. Si umeona kikuta kile kimekuja nyuma hivi kifupi? Lakini kilikuwa kinatoka risasi ka mvua, hapiti mtu pale. Sasa pale ndipo zilipotumika Bren Gun (anacheka) kutoka Algeria, pale zimetumika Bren Gun, ndo hizo anozosema yule Kamishna Sullivan, hakuitambuwa sound [sauti ya bunduki] aliyoisikiya.9 Zilikuwa sita, huku na huku. Zimetumika, zilikuwa za polisi vilevile pale. Sasa upande ule mmoja, wa pili, ambao wangekuwa wamekwenda Mapolo, kuwazi. Ndio mlango mkuu wa kituo cha polisi. Kule ndo walokopita kina Sullivan na wenzake wote, na yule Banyani [Misra], nimeshawasahau kwenda kumtowa Jamshid. Sasa wale wote wakenda mwangoni kuingia gatini. Walipotoka pale sie tunafukuzia gatini. Sasa gatini ilikuwa pata nikushike. Hakuna kiongozi. Zilikuwa zinakwenda risasi kutoka Cine Afrique.

Si ile alama ile ya round about, na gate ile, kwa kumzuwia Jamshid. Asitoke. Lakini kapita. Kwa sababu wale walioipanga mipango walikuwa ni maofisa wenye ujuzi. Kumbe hiki kishindo chote huku kilikuwa wao wameshamtowa na watu wake wote.

Amur Dugheshi hata mapinduzi yuko? Baada ya mapinduzi ndo wamekuja wao. Musa Maisara ndo nlomuweka mie polisi. Manake yuko mtoto, huyu anoitwa Maulidi Mshangama, ndugu yake Maulidi Mshangama, Othmani. Yule alikuwa amekamatwa, sijui kwa kosa la trafik au nini. Akaekwa ndani sku moja kabla ya mapinduzi. Alikuwa Malindi kule. Mie ndo nlokwenda wafungulia.

Ahmed Gharibu alikuwa Sergeant huyu katika jeshi. Alikuwa mwalimu na memba wa Action Group ya Afro-Shirazi. Sikiliza. Makao makuu ya mapinduzi ni Saleh Saadalla. Sasa kuna vikosi vilotoka mle na vinaripoti kwake. Sasa vingine wewe huvijuwi. Lakini tulikuwa na alama ya kitambaa tulifunga hapa siku ile, ndo tulijuwana, nani anaongoza wapi, nani anaongoza wapi.

Mapinduzi na Muungano

Ama muungano hatukufikiria kabisaa. Sisi tulifikiri tuiwache iwe Jamhuri ya Zanzibar, na bendera tulitengeneza, na wimbo tukautengeneza. Alofanya habari ya wimbo, na habari ya bendera, ni Sergeant Juma. Mimi niliposikia imetangazwa Muungano kwamba Zanzibar imeungana na Tanganyika, mbona nilipata shoki ya maisha yangu. Kwa sababu mimi nimesikia asubuhi katika radio hapa alipokuwa akitengeneza kofia Mohamed Ashrak. Ushapita kwa Sapriji [Sapurji] hapa, kwenda kazini.

Lakini Hanga alikuwa anajuwa habari ya muungano. Sisi tulikuwa tutaungana na nchi za Afrika ya Mashariki, East African Federation. Ilikuwa msemo upo kabla ya uhuru. Sisi tuliunga mkono hii. Saadalla ni hiyo nlokwambia, Jamhuri.

Sera zetu hazikuwa zikifahamika khasa. Hakuna kikao kilokaa kupanga sera. Hata. Asikudanganye mtu bwana wee. Sie hamu…tazama kitu kilikuwa…Kutawaliwa tena tulikuwa hatutaki lile lilokuwa mbele ya macho. Hayo tuliwachia tukishinda watu wafikiri. Kutawaliwa tena iwe basi. Zanzibar lazima iwe Jamhuri. Na haijakuwa na dhamana au fikra za kusema tutauwa Ufalme, hakuna. Tutakuwa hatuutaki Ufalme. Na katika kukubaliana kwetu, jamii ya Kifalme ijengewe mahala. Tuseme kwa mfano. Kama Kizimbani, inafanywa hivi kipande cha ardhi, lakini sio Kizimbani. Hapajaamuliwa wapi watajengewa. Lakini hiyo imoo. Wasidhuriwe manake. Awekwe mahala akae na kipande chake cha shamba kujitafutia maisha yake kama watu wengine. Na sijui ilikuwa kama muda gani wa kupewa maisha ya kujitegemea. Iko hiyo. Tuliandika kibuku hichi, kijitabu kidogo, “How to deal with the royalty” [Vipi kuushughulikia ufalme]. Tukishapata serikali, hawa watu tutawafanyaje? Kwa mfano imekubaliwa Kibweni, tuseme hii nyumba ya ufalme, na kipande hiki chake cha kutumia, katika maisha yake, na muda wake, sijui mda gani, wa kuweza kupata usaidizi wa kifedha na matumizi ya kila siku, kwa ajili ya kuweza kujirekebisha.

Sote watu wane. Lakini mwandishi dhamana ni Twala, “the high code commando.” Ewe bwana, Twala alikuwa mtu bwana! Ah! Yakhe, wamewauwawauwa hawa fitina tu, ehe. Baada ya mapinduzi ndo wameuliwa ati. Hanga, Twala, Saleh.

Walouliwa pamoja ni Hanga, Twala, na Khamis Salum Beni.10 Ile kabila yake ya Kiarabu siijui, nimeisahau. Siku moja hao. Mohammed Omar “Masharabu” alitiwa ndani, lakini hakuuliwa, aliteswa kidogo tu. Mtu wa Dar es Salaam pale. Huyu alikuwa auliwe naye pamoja, yeye na Simba Ismail. Lakini hawa kwa sababu ni watu wa Tanganyika [na Uganda], walitolewa wakarudishwa kwao—Okello, Mfaranyaki, nk. Wakawachwa huru. Mohammed na Simba walinieleza namna walivouliwa Hanga, Twala na Khamis Beni. Walifungwa kamba kwenye mti mkubwa, na…[memba watatu] wa Baraza la Mapinduzi wakawa wanaivuta hivi na kuiwacha, na katikati yuko mtu na pauro akimpiga nalo kichwani Hanga mpaka kampasuwa.11 Kikatili kabisa wameuliwa. Wacha bwana, tusiongee habari hii. Juma Maneno tena alikuwa opportunist [mbinafsi]. Alikuwa tena hata sisi alikuwa kutuona hataki. Akatuacha mkono. Alifika kuwa Kanali na nafikiri alipigana vita va Uganda.

Yakhe unajuwa. Sijui kiasi gani utaweza kukubali. [Mapinduzi] yamefanyika bila ya fedha. Lakini kuna kitu kimoja. Kwa sababu, wale watu wawili, walikuwa memba wa parliament, wakipata marupurupu. Sasa ile allowance [marupurupu] yao ndo tukigawana sisi tunokwenda mbio. Wakitoa kutoka mifukoni mwao. Hatuna pesa zozote. Si Oscar, si nani. Hakuna alotusaidia pesa “bunda hili, hii fanyeni.” Basi sijui, kama mtu kapata akiiba, haya. Lakini mie najuwa hakuna. Kwa sababu watu tulokuwa nao na watu wangepokea pesa ni watu waaminifu. Hanga na Saleh ni watu wakweli sana. Kama Twala alikuwa hana pesa. Hana allowance yoyote. Ana allowance ya trade union. Labda wakimgaia senti ishirini na tano, kumi, bas. Lakini hao watu wawili ndo walokuwa na allowance.12

Yusuf Himidi silaha kazitowa wapi? Maneno ya uongo hayo bwana. Achana nayo. Mimi habari hizo za watu kina Yusuf Himidi, mimi sizijuwi. Mimi naamka asubuhi nasikia wao waheshimiwa. Vipi, namna gani, sijuwi. Kwa hivyo kila ntakachosema ntasema uwongo. Inaweza kuwa ndiyo, inaweza kuwa siyo. Kwa sababu kuna kikundi cha Youth League, lakini kwa gari ya PWD kubebea mchanga wakati ule na akabebea silaha, ni jambo lisilowezekana kabisa. Security ilikuwa very highly tight.13

Mambo ya hao wa Chumbuni, na wapi na wapi, mimi siyaelewi. Lakini najuwa kuna section ya Youth League, ambayo wakija chukuwa ripoti kutoka kwa Saleh Saadalla, wakati wote. Hawa, wakiongozwa na Natepe na Seif Bakari. Sasa mambo yao… manaake kuna kitu kimoja utaona ajabu. Nikikwambia mie hata huyu mtu mmoja akiitwa nani?…Okello, mie simjui. Organization [mipango] iliachiwa Youth League.

Twala ndo alokuwepo hapa. Na Twala alikuwa ndani ya action. Kaingia Ziwani. Saleh na Hanga tuliwaondowa. Hata Karume aliondoshwa na yeye. Jimmy Ringo ndo alomuondowa. Habari ya Nyerere mimi baada ya kiasi hicho siwezi kukwambia, kwa sababu hatujapata kukutana mimi na yeye. Baada ya siku ya pili ya mapinduzi, serikali ya Tanganyika walileta kikosi kimoja cha polisi, hawa Field Force, chini ya Captain Baruti. Mimi ndo nlokwenda ipokeya gatini.

Oscar alikubaliana na sie. Oscar kakubaliana na sie. Lakini, ikiwa kashauriana yeye na Raisi wake hayo mambo mie siyajuwi. Kulikuwa hakuna kiongozi yoyote ziada ya hao nilokutajia wanojuwa mapinduzi hayo. Chama cha Afro-Shirazi hakijaingia ndani ya mapinduzi. Wanachama wa Afro-Shirazi ndo walopinduwa.14

Kina Sefu Bakari na Natepe walikuwa hawawezi kuwaambia viongozi wakubwa wa ASP, kwa sababu ni kitu cha siri. Chama cha Afro-Shirazi hakijapinduwa, hakijakaa katika kiti kuamua kupinduwa. Mapinduzi yamefanywa na wanachama wa Afro-Shirazi bila ya kujuwa Chama cha Afro-Shirazi. Baada ya mapinduzi wanachama wakawakabidhi chama chao. Hanga, Twala, Saadalla, hawa walikuwa viongozi wenye nguvu za utekelezaji katika chama. Hawa katika Chama cha Afro-Shirazi, ni executive [wana nguvu za utekelezaji]. Ndo mapinduzi yalivyo. Hata ukisoma historia ya Urusi Lenin hakuwa Raisi wa chama chao. Na chama chao kilikuwa hakijuwi mapinduzi. Kimefanywa na Lenin. Na ingekuwa kimeambiwa chama yasingelikuwepo mapinduzi. Hawana hamu hiyo wale watu. Watu wengine walikuwa hawataki. Sasa ungelikuwa mvutano, maneno, mpaka habari zote zikatoka nje.

Babu ni Hizbu, moja kwa moja. Na akitumiwa na China. Na wakafukuzana na Ali Muhsin. Babu hakuwa mwanachama wa Afro-Shirazi. Hajapata. Saleh Saadalla ndo alomuondosha Babu, kwa kumtumia mkewe na buibui la mkewe, kwenda kumtowa kule nyumbani, akenda akavishwa. Ilikuwa akamatwe na nanhi… Basi ikiwa kuna mazungumzo ya mapinduzi, na nini, kaongewa na kina Saleh, hukohuko Dar es Salaam, lakini siyo Unguja. Kaambiwa tu, watu watapinduwa.

Hanga na Saadalla wakimuamini Babu labda aslimia sifuri. Haaminiki ati Babu, tunamjuwa ni muongo kutokea mwanzo. Watu wote wanamjuwa hapa, viongozi wa Afro-Shirazi, wa Hizbu. Anajulikana Babu. Ni mtu rahisi. Ni rahisi kutumika.

Kusafirishwa kwa Babu kutoka Unguja…alikuwa Ali Muhsin, au serikali ilokuwepo, ni serikali, maanake Ali Muhsin peke yake si kitu. Serikali ilikwisha pendekeza kumtia ndani Babu. Sijui kumfungulia kesi gani na gani. Ikabidi atoroke. Ile kesi ilivopatikana habari, huku upande wa Afro-Shirazi, Saleh kama ni mtu mwenye kufikiri…tumemkosa mtu mzuri sana sie Unguja, akasema “kwa nini hatumsaidii?” Ikakubalika. Akenda usiku, kama saa ngapi sijui, akapelekewa habari Babu akakubali, tukenda. Mimi, Khamis Beni, na mkewe Saleh Saadalla, Sauda bint Haydar wa Kisutu, Dar es Salaam, kwao Bagamoyo. Tukenda. Sasa sisi tulipokwenda tulikutana na asikari pale, lakini tumeteremka watu watatu na mwanamke. Tukaingia ndani, Migombani huku, buibui la Sauda akavaa Babu, sasa tunamwambia “wewe tukitoka uringeringe kidogo”. Dereva wa gari alikuwa Ali Saidi, taxi-driver, tulimchukuwa, kwa sababu yeye huyu alikuwa ni memba wa mapinduzi. Alikuwa ni mwenzetu. Tukampita asikari, akaingia ndani ya gari ile, tukatoka tukenda Kizingo. Kizingo Babake Fuko, mzazi, alikuwa na ngarawa na mwanawe mdogo, Huseni, ndo akapakiwa Babu kupelekwa…kateremkia Mlingotini. Akateremshwa pale, sie tukarudi huku. Sauda sijui karudi na chombo gani.

Na ndo hivo hivo alovokwenda Mzee Karume. Hapo hapo kapakiwa ndani ya ngarawa na Jimmy Ringo, kenda Bagamoyo. Jimmy Ringo ndo alomuondowa. Jimmy Ringo akijuwa mapinduzi. Alikuwa katika group la Youth League. Tulikuwa tunajuwa sie. Ndo alokwenda mchukuwa kule, na alomsafirisha ni babake Fuko. Jimmy Ringo hakuingia Bomani wala Mtoni. Alikuwa na Karume pamoja huko, kakimbia na yeye. Hajakuwepo hapa. Aliondoka naye Karume yule.

Mie nakwambia, silaha zilivotolewa Ziwani zikaletwa Kijangwani. Wakati jengo la radio hatujalipata! Bado! Asubuhi nimekwenda kwa Mzungu alokuwa na ufunguo wa radio. Alikuwa hukuhuku Migombani. Tukamfata. Iko nyumba moja ukishapita, hii ya Karimjee mbele ina vigae vitupu hii, basi nyumba ya pili yake ndo akikaa. Nimekwenda asubuhi mie anakula chakula cha asubuhi. Ujuwe mapinduzi yamekwisha wakati huo. Ziwani ishachukuliwa, Mtoni ishachukuliwa, pa kuweka bunduki hatuna. Bunduki zinatolewa kulekule…tukenda tukaja funguwa, tukafunguwa na mlango wa pili, ule mlango ulokuwa na dirisha kubwa linotazama uwanjani, ndio zilipotiwa silaha. Na katika silaha zile, alikuweko Sergeant Simba Ismail, dhamana wa silaha, na Sergeant Ngusa, wakitia zile bolts. Halafu akaja Abdalla Juma Bulushi wa Umma Party, akaja pale na kuwasaidia.

Mzungu alikataa kwanza kutoa ufunguo, alisema ufunguo uko kwa Mmarekani kwenye ubalozi wao. Nimemkuta anakula, yeye na mkewe pamoja, na mtoto wao, apata hivi [mdogo]. Mimi binafsi, nilikwenda kule, tulifuatana, tulikwenda na gari ya Land Rover ilokuwa polisi, dereva akiendesha yuko kijana mmoja, alikuwa polisi hapa, alipewa upolisi na serikali akawa hana sehemu. Nani jina lake? Mohamed yule? Mohamed ndio. Yuko mwengine yuko Raha Leo mpaka leo yuhai, anaitwa Muadhi, aliajiriwa usalama, na yuko mmoja, huyu watatu sijui nimemsahau. Huyu Mohamed alokuwa akiendesha gari mtu wa Kilwa. Huyu Muadhi sijuwi wapi kwao, yupo Raha Leo hapo. Na huyu mmoja nimemsahau jina lake. Mie nikamwambia yule Mzungu, “Kuna moja kati ya mawili.Tupate ufunguo au niitowe roho yako!” Nimekaa tayari. Nna bunduki Mac 4 na pistol. Nna vitu hivi viwili. Akainuka akachukuwa ufunguo tukenda akafunguwa tukaingia ndani, radio ikatangaza, yale mambo yakawa yanafanya kazi. Mimi Mzungu huyu nikaja tukakutana tena Dar es Salaam, katika benki ile, inaitwa “Clock Tower Bank”. Pale ndo nilipokutana naye. Akantazamaa! Akaniambia, ndie wewe Mr.…? “Ndiye yuleyule, hakuna mabadiliko.” Tukazungumza kutaniana pale, akenda zake. Sikumuona tena mpaka leo.

Ama mimi kutoka pale baada ya kazi hiyo ndo nkenda kumchukuwa Aboud Jumbe. Kwake. Tena aliponsikia sauti yangu akaingia chooni. Akafungua maji akajitia na sabuni na mwanawe mwanamke mdogo, Fatma. Ananiambia “nini?” Namwambia “hapana,” twende zetu huku, mambo tayari na wewe ndo Seketeri wa Mipango wa Chama [cha ASP]. Kituo cha polisi cha Malindi hakijakamatwa bado. Kashtuka. Mpaka aliponiona mie. Mie ndo nlokuwa seketeri wake kwenye mambo yote. Ndo mwisho alikuja kunlaumu, anasema “basi mnafanya mambo hamtwambii?” Nikamjibu “ndo mambo yenyewe yalivyo.”

Akenda Raha Leo. Kikosi cha mwisho alichokipeleka kilichokwenda alikipeleka yeye. Aliwaita pale watu, nani…, akampa chaji Ahmed Gharibu, kwenda. Hichi ndo kilokwenda kikamaliza, basi. Lakini zilikuwa ghasia zimemaliza. Na kule zimekwisha vilevile.

Aboud Jumbe hakuambiwa na mtu. Aboud Jumbe kujuwa mapinduzi kumwendea mimi kumchukuwa. Mimi binafsi kwa mkono wangu, na kwa mguu wangu, ndo nlokwenda mchukuwa Hasnu Makame kwake, Idris Abdul Wakil, na Aboud Jumbe, kuwaleta Raha Leo. Walikuwa hawajuwi chochote. Usihangaike bwana. Hii ndo picha halisi. Na unaweza kumuuliza Aboud Jumbe. Nimemkuta chooni. Kanikimbia mimi. Kaingia chooni. Na mwenyewe kwa kauli yake, akaja akaungama mbele ya nduguye, kwamba nyinyi mnafanya mambo haya hata hamtwambii sie? Tuko Dar es Salaama! Yupo Yusuf Jumbe, yuko Aboud Mwinyi Mgeni, yuko Hamisi Mparama, yuko nani huyu? “Mmanga”, yuko Maalim Ramadhani alokuwa na nanhi pale…, yuko kijana mmoja “Mwinyi”, yuko ndugu yake Ahmed Gandhi. Pale ndo kasema. “Nyie basi mnafanya mambo hamtwambii?”

Karume alikuwa hanipendi. Sijui kwa nini, akinchukia tu. Akiniona nakwenda zile safari zangu nnazoenda ni nyingi na hazijui, na za kisiasa, alichukia, alikuwa ananchukia, kweli najuwa akinchukia. Na mie nilipojuwa kuwa ananchukia baada ya mapinduzi ilipoundwa serikali, mie nlikataa. Nlikataa kabisa kwa kutafuta amani yangu. Kwa sababu mie simchukii.

Serikali ya mwanzo alikuwa Karume ni Raisi bila ya nguvu za utekelezaji. Waziri Mkuu na mwenye nguvu za utekelezaji alikuwa Abdalla Kassim Hanga. Waziri wa ilimu alikuwa Othman Sharifu. Waziri wa Afya, Aboud Jumbe. Waziri wa Mawasiliano na Kazi Idris Abdul Wakil. Waziri wa Mambo ya Ndani na Ulinzi, nlikuwa mimi kwa siku tatu. Mambo ya Nje hakuwa Babu. Babu alikuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje baada ya mageuzi.15 Alikuwa mtu mmoja nimemsahau. Hasnu Makame alikuwa Waziri wa Fedha. Twala alikuwa Naibu Waziri wakati ule. Alipokuja kuwa Waziri wa muungano ndo akawa minister. Sikumbuki uzuri, ndo mpaka hapo.

Sasa hao, kwanza ilotangazwa mwanzo ndo hiyo. Hii ilitangazwa bado Karume yuko bara, hajafika hapa. Bado kabisa! Na ikatangazwa, tena ilitangazwa asubuhi. Sasa nani alitangaza hii? Kuliingia matatizo mengi sana hapa baada ya kazi kumalizika. Katika kupanga vyeo uliingia ugomvi, mvutanovutano, ufisadi wote uliingia siku hiyohiyo. Mara moja, wakati mmoja.

Nadhani ilichapishwa. Ilichapishwa ndio. Mmmh! Mimi sikuona gaazeti. Mimi binafsi sikuona gaazeti. Kama imechapishwa…mimi sikuona. Manake, baada ya kutangazwa tu Karume kuwa Raisi, mimi hamu yangu ilikufa kabisa. Kwa ukweli. Kwa sababu nilijuwa hakutokuwa na amani. Baada ya Karume kuwekwa Raisi, ndo akafanywa Waziri Mkuu [Hanga] kuwa ni Makamo wa Raisi. Yakhe, hilo ndo jambo limenikera mimi zaidi hata kuliko yote. Kukubali Hanga mimi kumenikera.

[Mimi] sikutia saini document yoyote. Hata sku moja. Hata ofisini skuingia. Na karibu wote walokuwa kwanza hawajuwi lini wameingia. Mpaka alipokuja Karume akachaguliwa na nini. Sijui ile picha imekwenda wapi? Ilikuwa picha hapa kwangu ya Baraza la kwanza la Mawaziri. Hata ile picha tulopiga na kikundi cha wanamapinduzi tunatoka juu hapa, People’s Palace. Na wale watu wote ungeliwaona mle. Hata huu mkono wangu ulokuwa umeumia, ile kwenye picha ipo, na ile kitu nlotiwa hapa, ambayo ndo sababu ya maumivu yangu ya macho. Huu mkono nimeufunga hivi. Anyhow, mapinduzi yalikuwa mazuri. Yalifaulu vizuri. Viongozi walikuwa wote wasomi. 100%. Pale mambo yalipokwisha kuwa tayari asubuhi, mawasiliano yalikuwa kupitia Radio Zanzibar. Hatukuwa na njia nyingine za mawasiliano.

Mimi sikwenda hata sku moja. Sijapata kuwa Memba wa Baraza. Watantia wapi na Mwenyekiti Karume? Mie nlikataa hasa kazi. Baada ya mapinduzi nlikaa kama miezi mine. Hapo, kwanza nimekaa nimetangazwa nende Kilimo. Nlikuwa ndani ya radio nimesikia, siku ripoti kokote. Nikaja nkakaa. Akanjia Hanga hapa ananambia Raisi anakupeleka uwende polisi utavaa nyota tatu, Captain, nikamwambia “mie staki.”

Mie sina imani na Karume. Kwa kunchukia kwake. Na ndivo nlivyo. Maanake, hata huko kilimo nlokopelekwa na yeye Karume nikawa Assistant Secretary…kutoka hapo nikafukuzwa 1965. Haya mtu uliyeajiriwa kazi na serikali unafukuzwa kama mtu alochukuwa maji ya taka kama nilivotupa mie nje hivi umepata kuona wapi? Naelewa ile kazi au vipi? Sio leo unamuondosha Trimblet, Assistant Agricultural Director, unakuja kuniappoint [kunichaguwa] mie! Kuchukuwa nafasi yake. Sasa bila ya sababu, kujuwa kwa nini nimefukuzwa, nikaandikiwa, nikaambiwa, hakuna. Watu walivokuwa wabaya hawa. Kwa sababu hiyo ndo kauli mbiu ilokuwa ya Mzee Karume. Wazi, kila mtu anajuwa. Akisema hadharani “wakimbieni wenye ilimu.” Sasa yeye kapata utawala ndo wenye ilimu atawapa kazi kweli?

Basi wewe utakwenda mchukuwa Sergeant-Major Saleh Saadalla Akida, the ex-military Sergeant-Major, the Sergeant-Major in the British Army, Second World War, Education Department, huyu ni mwalimu wa skuli. Nadhani alikwenda Burma, alikuwa katika Education Department. Nafasi yake inakuja kuchukuliwa na Hassan Nassor Moyo. Afadhali Moyo ni seramala. Akaja akabadilishwa akapewa Saidi Idi Bavuai!

Chama cha Wafanyakazi wenyewe kilijiunga na Chama cha Afro-Shirazi. Ni Twala ndiye aliyehusika na mapinduzi. Yeye alikuwa ni seketeri wa chama cha wafanyakazi. Lakini yeye ndo alokuwa anahusika kuwashawishi wale wenzake kwenye trade union kuunga mkono. Wengi walikuwepo wengine. Siwajuwi, siwakumbuki.

Wazungu ingekuwa wameshirikiana tungemkamata Jamshid ati. Nakwambia wameizuwia Malindi na upande ule ukawa safi, wakampeleka Jamshid na watu wake wanotaka wote katika meli wakaizuwia na wakaiongoza meli chini ya ulinzi, mpaka ikafika Mombasa, ikakataliwa, ikaja Dar es Salaam, Nyerere akawapokea akawafanyia safari wakenda zao England, wote.

Isa Mtambo tulikuwa “signal” pamoja na hapo siku tulokwenda sisi mara ya kwanza kuweka miguu yetu kwenye ofisi ya Waziri Mkuu, yeye yuko pale, assistant secretary. Tena assistant secretary wenyewe, mapokezi, kupokea watu. Baada ya mapinduzi alipewa cheo cha Mkuu wa Mkoa, sijui Tanga, au wapi.

 

Kifo Bila ya Matanga—J. J. Mchingama

Katika kifo cha Abdalla Kassim Hanga na wenzake, kilipotokea, Othman Sharifu alikuwa na kaka yake ambaye ni mkuu wa mkoa Pemba akiitwa Ali Sharifu. Wakati waliponyongwa, mwaka 1967 au 1968 katikati hapa, ukatumwa ujumbe kupitia jeshini.16 Ukapitia jeshini akapelekewa Mkuu wa Mkoa ambaye ndugu yake ndio ameuliwa. Wakenda kumchukuwa Ali Sharifu kutoka ofisini kwake mpaka makao makuu ya jeshi Pemba. Kule akasomewa ujumbe kwamba imetumwa taarifa ya kuuwawa kwa ndugu yako Othman Sharifu. Baraza la Mapinduzi limeamua kuwauwa Othman Sharifu, Abdalla Kassim Hanga, na wenzake, kwa sababu walikuwa wanakwenda kinyume na matakwa ya chama na Baraza la Mapinduzi. Kwa taarifa hiyo huruhusiwi kuweka msiba wala tanga, na popote mtakapokutikana, watu wawili au watatu katika familia mmekaa, Baraza litajuwa kwamba mnafanya msiba na mtachukuliwa hatua.

Baada ya kusomewa akaambiwa umefahamu, akajibu nimefahamu, lakini nataka kuuliza. Akajibiwa kwamba utaziuliza salamu? Wewe umepokea, sema nimepokea! Imekwisha! Anajibiwa na mkubwa wa kikosi pale Pemba. Mkuu wa kikosi wakati ule alikuwa akiitwa Tirace Lima kwao huko huko Pemba sehemu za Kangani, lakini sasa ni marehemu. Basi Mkuu wa Mkoa akatia saini kwamba ameiona na ameipokea hiyo message na akaondoka. Lakini bahati mzuri kutokana na mwenendo huo hayati Mwalimu Nyerere aligunduwa akampa uhamisho Ali Sharifu kutoka Mkuu wa Mkoa Pemba na kumpeleka Tanzania Bara. Huko sijui alimalizikia wapi. Hiyo ndo hali ilikuwepo hapa. Kwa hivo zile chuki na kutiliana mashaka kulikuweko ndani ya uongozi wenyewe kwa wenyewe. Vurugu gani lilitokea ndani yake hata hawa ikabidi wauliwe sikuelewa ni nini. Message ilitumwa tu hivi. Ina maana Baraza la Mapinduzi liliamua hivyo. Sasa inawezekana ni hitilafu iliotokea tokea mwanzo, kutoelewana kati ya wasomi na wasiosoma. Inawezekana ni hiyo iliendelea mpaka kufikia 1964. Kwa hiyo hali kama tutaendelea nayo kuwa tunakumbuka ya nyuma itakuwa kila siku tunaendelea kulipizana kisasi, jambo ambalo hatuwezi kujenga hii nchi. Hatuwezi kuendelea. Kilochobaki ni kusameheana yalopita. Wote tuwe kitu kimoja tuweze kuitengeneza hii nchi kwa sababu sote ni kitu kimoja. Hata kama tuna hitilafu za kirangi, kidini, hiyo isisababishe kwamba tusiwe watu wamoja. Nchi mbalimbali tunaziona zina watu wa makabila mbalimbali, matabaka mbalimbali, lakini wanajenga nchi yao. Hivi ndo navoona mimi maoni yangu.

Hawakuweka msiba. Kulikuwa na vikosi maalum vikitembea kila family ilotolewa hukumu ile basi kila familia ilikuwa inafuatiliwa. Ilikuwa mimi na wewe kama ni familia moja tusikae pamoja baada ya tukio lile. Wakitukuta tumekaa pamoja wanakwenda kuripoti.

Mimi nafikiri kwamba kwanza kule nyuma tulikotokea Baraza la Mapinduzi lilikuwa na nguvu na watu wengi walikuwa wanaliogopa lile baraza. Kwa hivo hata kama kuna Mwenyekiti mwenyewe lakini alikuwa anaogopa nguvu kubwa kutoka kwa wajumbe wa baraza. Kwa hivo anaweza kusema nikisema hivi baraza linaweza kunigeuka likanifahamu vibaya kwa hivo wacha nende ninavokwenda. Nafkiria kitu kama hicho. Sidhani kama serikali itajibu. Haitojibu kwa sababu yenyewe hiyo serikali yenyewe haina hata hiyo historia yenyewe au kumbukumbu yoyote ile na kama inayo basi imehifadhiwa isikumbushwe. Ukikumbusha utaleta balaa la familia la wale waliouliwa kuwa wanaweza wakafanya, pengine wakashtaki kwenye mahakama za kitaifa, wanaweza kuyalalamikia mataifa, ili wajuwe pengine kitu kama hicho.

Kwa hivo wanapojaribu kufatilia wanaweza hata kushindwa kupata maelezo kamili. Wao wanahisi kwamba kutoa habari hizi kwa familia ni kuibuwa mzozo mpya. Linyamaziwe hivohivo ingawa wale wanaungulika, wanaumia, lakini bora linyamaziwe hivo hivo. Lakini sasa hatari zake kuna siku litakuja kuibuka likawa mzozo mkubwa zaidi kuliko hivi sasa pengine wangefanya likajulikana kuliko kulimezea. Kwa sababu wanasema kwamba moto unaotisha zaidi ni moto wa makumbi. Lakini hawa watu kweli wameuliwa. Wameuliwa na ni watu wa Afro-Shirazi. Lakini migongano ndani ilikuwepo.

Wale [watu kumi na tisa] inasemekana waliuliwa Kibweni, KMKM [kikosi cha wanamaji na kuzuwia magendo] pale. Ndo walivonizungumzia wale [platoon yangu] mimi baada ya kurudi safari zangu kunihadithia kwamba wanatoka Kibweni walikwenda kutekeleza majukumu hayo [ya kuuwa]. Ilitangazwa hata kwenye vyombo va habari, tarehe fulani kutakuwa na mazoezi ya shabaha ya KMKM, hawaruhusiwi wavuvi kupita maeneo hayo. Kama sku tatu mfululizo iliendelea kutangazwa. Lakini watu wengi tukajuwa hivo, kuna zoezi, na pale wao wanafanya mazoezi na kumbe mazoezi yale siku ile yalikuwa na shabaha nyengine. Mambo yalikuwa makubwa sana. Manake kama hali ile tungeliendelea nayo tungekuwa katika hali mbaya sana.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: