Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!

Icon

Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia

Mlango wa Kumi na Nane: Kosa la Mzee Nyerere

Sisi Wazanaki tuna sifa mbili kwa majirani zetu…Kwanza, ni wajanja, na sifa ya pili ambayo inaifuata sifa ya kwanza, ni kuwa si waaminifu. Watu husema ‘Rafiki wa Kizanaki atakuuwa’ ambayo si kweli. Sijui vipi tumeipata sifa hiyo… —Mwalimu Julius Kambarage Nyerere

Ningekuwa na uwezo, ningevikokota visiwa va Zanzibar nikavitupilia mbali katikati ya Bahari ya Hindi. —William Edgett Smith

Wanayaita mapinduzi, lakini sisi tunasema mavamizi. —Sultan Sayyid Jamshid bin Abdullah

 

Mzee Faraji

Nilipata kusikia kutoka kwa mmoja wa Marais wa zamani wa Zanzibar, kuwa manunguniko na madai ya Wazanzibari yaliyoanza katika miaka ya 70; kuhusu kuvunjwa mkataba wa 1964, kwa manufaa ya Tanganyika; madai hayo yalikuwa yakiwaudhi sana viongozi wa Tanganyika. Hivyo siku moja Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, akamwambia Raisi wa Muungano (wakati huo) Mwalimu Nyerere, kwamba kwanini hawavunji mbali muungano ili wapumzike na “kelele” za Wazanzibari? Inasemekana Mwalimu Nyerere alimjibu kwa kumkatalia kwa kusema mengi pamoja na “…tukiwaachia tu, utaona jinsi mapesa ya Waislamu na Waarabu yatakavyo miminika Zanzibar…hapana, hatuwaachii.”

Laiti shida ya Mwalimu Nyerere ingelikuwa nae anazitaka pesa hizo kwa ajili ya Tanganyika, kisa kifuatacho kisingelitokea. Kwa mujibu wa kisa hiki kama kilivyosimuliwa na Rais huyo wa zamani [wa Zanzibar], Mwalimu Nyerere, wakati huo akiwa ameshastaafu, alipita akiwa safarini, katika uwanja wa ndege Jeddah, Saudi Arabia. Balozi wa Tanzania aliyekuwepo Saudi Arabia ilimlazimu ki-protokoli, kwenda uwanja wa ndege kuzungumza nae katika muda wa transit. Pamoja na mambo mengine, Balozi huyo alimwambia Mwalimu Nyerere “…katika nchi hizi kuna mapesa mengi, na jamaa yaelekea wapo tayari kutusaidia mipango yetu mingi ya maendeleo, ilimradi tu, tuwaombe.” Nasikia Mwalimu alimjibu kwa mkato na kwa kiasi cha kuonekana kakasirishwa: “Hapana. Acha kabisa!”1

Ni dhahiri, mpishi wa mapinduzi na muungano, Mwalimu Nyerere, alikuwa ameacha “grand design” [mpango mkubwa] katika kuipata Zanzibar, bila shaka si kwa manufaa ya nchi (Tanganyika na Zanzibar), bali kwa manufaa ya wale wasiowatakia mema Waislam (pamoja na Waarabu ambao wengi wao ni Waislam).

Niliwahi kumuuliza mmoja wa Maraisi waliopita wa Zanzibar kama aliwahi kuuona waraka asilia [wa Muungano baina ya Zanzibar na Tanganyika] uliotiwa saini tarehe 26 April 1964, akaniambia hapana, hajawahi kuuona. Nikamuuliza tena, je, yule uliyemuachia nafasi yako unaweza kumuuliza kama kawahi kuuona? Akanijibu: “hapana haja ya kumuuliza, kwa sababu nafahamu kuwa nae pia hajauona.”

Kwa kawaida nchi inapotaka kujiunga na Umoja wa Mataifa (UN), hutowa taarifa ya mwezi mmoja na kisha kuwasilisha maelezo/vielelezo na vithibitisho kuwa ni nchi (yenye sifa ya kuwa na Utaifa), inayostahili heshma ya uwanachama huo. Nchi zilizokuwa zinapata uhuru wake toka ukoloni zilitoa taarifa ambayo tarehe yake ya mwisho ilisadifia na tarehe ya kupandisha bendera mpya.

Hivyo nchi iliyojisajili UN na kupewa kiti, bila shaka ilipobadili nafasi iliyoiondosha uwananchi wake, haikuondoka katika umoja huo bila ya taarifa yoyote. Bila shaka patakuwepo maelezo na vielelezo vilivyokubalika kiti chake kurudishwa, bendera yake kushushwa katika mlingoti wa UN, na majukumu yake kame vile michango n.k., kufutwa. Vipi leo nchi kama hiyo isiwe na hati halisi ya makubaliano ya muungano ambayo wananchi waliona Sheikh Karume na Mwalimu Nyerere wakisaini na kupeana April 26, 1964? Na vipi nchi isiwe hata na zile nakala halisi za vielelezo japo vile vilivyopelekwa UN kuhusu suala zito la utaifa wake? Au hata ushahidi wa kisheria kuwa hakuna nchi inayoitwa “Tanganyika” au yakuwapi maelezo/vielelezo kuhusu kuongezeka kwa mambo ya muungano na nani alotia saini kwa niaba ya Zanzibar? Ni saini yake au ni ya nani na kwa ushahidi gani wa kisheria?

Wenye kuumizwa na yote hayo khasa ni Wazanzibari na si Watanganyika. Mapinduzi ndo yalioipinduwa nusu ya jamii ya Zanzibar ilioshinda uchaguzi [wa Julai 1963]. Mapinduzi ndo yaloleta muungano na kuyapinduwa makubaliano ya mwanzo ya muungano. Mapinduzi ndo yaliokifuta kiti cha Zanzibar UN kwa nia ambazo Wazanzibari bado hawajazitambuwa. Mapinduzi ndio yaliomuondowa Al Hajj Aboud Jumbe madarakani, na kilichomponza khasa Mzee Jumbe ni pale alipolianzisha Baraza la Misikiti Tanzania (BAMITA); yakamtia ndani Maalim Seif Sharif Hamad; na ndiyo yaliyopelekea Dk. Salmin Amour akataliwe kuiingiza Zanzibar/Tanzania katika OIC na kuiakhirishia Zanzibar kutojiunga na taasisi hiyo. Ndiyo yaliyoifanya Katiba ya nchi itamke kuwa Raisi wa Zanzibar siyo tena Makamo wa Kwanza wa Rais wa muungano, kama ilivotamkwa 1964. Na ndiyo yaliyo “thibitisha” kuwa nchi ya Zanzibar sasa ni Mkoa kama mkoa wowote Tanzania. Na kubwa zaidi, hayo ndiyo yaliyofanywa kuwaonesha rasmi Wazanzibari kuwa hata ndani ya chama kilichoundwa kwa kuunganisha ASP na TANU, TANU, CCM Bara, ndiyo itakayoamua nani atagombea Uraisi Zanzibar.

Hivi sasa hakuna udhibiti kwa watu kutoka bara kuingia na kuishi Zanzibar. Lengo ni kubadilisha “demographic situation in favor” [hali ya wingi wa watu] ya bara katika miaka michache ijayo. Na hiyo population [idadi ya watu] mpya inaandaliwa kuwa “superior” katika uchumi, ilimu na ushawishi wa kisiasa. Wapemba kuunga mkono chama kinachoongozwa na Maalim Seif Sharifu, Mpemba, university graduate [mhitimu wa Chuo Kikuu] na mzoefu katika serikali na siasa; mtu ambae alikhitalifiana na Mwalimu Nyerere inakaa vizuri katika “grand design” [mkakati mkubwa] ya Mwalimu ya kuwatenga Waunguja. Nyerere alipoenda Zanzibar kueleza kwa nini CCM iliwafukuza Seif na wenzake, alimtaja Seif kama watu “…tuliokuwa tukiwapokea katika chama pasipo kuwachunguza kwa undani ili kujua asili yao na huko watokako…” Mbali ya maneno hayo, Nyerere pia alianzisha propaganda za kwamba watu wenye rangi ya kuchovya kama ya Seif, japo si Waarabu, alitaka watazamwe kama Waarabu. Siasa zao zitakuwa za kutaka kumrudisha Mwarabu Zanzibar.

Nyerere pia alianzisha lugha ya kampeni ya “kuwanasihi” watu wa bara (Tanganyika), kama moja ya propaganda zake za kujenga hoja ya kujitetea pale itakapoonekana kuwa bara inatumia nguvu kulazimisha muungano. Ikawa akisema mara kwa mara kuwa “…hawa wanataka kuuvunja muungano, mkiwaachia, watauana ovyo…sasa wameshaanza kugawanyika na kubaguana, kati ya Wazanzibari na Wazanzibara…Wapemba na Waunguja…” Ingawa hoja hiyo inakusudiwa kuwaomba Watanganyika “kuwanusuru” Wazanzibari ili wasi-jeuana, haikumpitikia Mwalimu wala wengineo kuhoji; kama Wazanzibari wamegawika kiasi hicho, msimamo wa uhalali wa muungano ukoje hivi sasa? Tanganyika hivi sasa imeungana na nani; Wapemba, Waunguja, Wazanzibari au Wazanzibara? Siri ya mapinduzi ya wazee inatowa jawabu lililo safi; Tanganyika iliungana na Waafrika kutoka bara kuwapinduwa Wapemba na Waunguja—Wazanzibari.

Katika mambo ya kudhulumiana nchi, wajanja hufanya kila njia kuepuka masuala ya mfumo. Watakupelekeni kwenye utendaji kazi. Huko mtazungumza na wale waliopewa kazi ya ku “run” government [kuendesha serikali]. Hamtokutana tena na wale wanao “rule” [wanaotawala]. Sioni sahihi kuutegemea Muwafaka badala ya Mkataba wa Muungano na Katiba na sheria za nchi, kutupa muelekeo wa kule tunakostahili kwenda. Hivyo hivyo, siamini kuwa mtu atayewekwa na madhalim katika madaraka ya nchi, ana uwezo wa kujua na kuipeleka nchi hiyo pahali pasipokuwa pale panapo takiwa na madhalim hao.

Kwa vyoyote vile, endapo tutatanabahi, tukatambua kuwa nguvu za wananchi ni muhimu kuliko chochote, na kwamba nguvu hizo hazipatikani ila kwa kuwatoa katika umasikini wa kiza cha ujinga wa ilimu duni; tunakoelekea si kubaya. Kuwatowa wananchi kunako giza la tunakotoka na Zanzibar kujiwakilisha nchi za nje, kuujenga na kuulinda uchumi wake, pamoja na kulindwa na Wazanzibari, ni kuzuri, na huko ndiko kwa kuanzia.

Mzee Ayubu

Kisera Mzanzibari mwenyeji hakushirikishwa kunako mapinduzi. Na ndo mpango ulivokuwa! We ndugu yangu na ukisikia nimekufa leo lazima ufike. Ukitoka leo mimi nijuwe. Ndo alivotuwacha mzee hapa.

Mimi nilipewa kazi na Afro-Shirazi. Nakumbukia mimi niko mle nakwenda na yale. Karibu yangu akawa huyu marehemu Hafidh Suleiman alokuwa memba wa Baraza la Mapinduzi. Huyu mtu wa Tanga lakini ndo katika hawa waliozaliwa hapa. Mdigo. Wazee wake walipofika walifikia wapi…Kinduni na ndo alipokwendazikwa alipokufa. Lakini wakahamahama ndo wakaja pale Kizimbani kwa wajomba zake kina Mbaruku Juma. Saidi Bavuai ni watu wa Mlingotini, hapa Bagamoyo.

Kwani ukafata sana, watu walopinduwa ni kutoka nje. Daislama, Tanga. Wengi na ndo wamezalika hapa, kwa muda mrefu wamekulia hapa. Nilipoingia hasa nikawa nayapata ya juu kidogo, nadokolewa. Ya chini ndo nilikuwa nayo yote! Ya juu yakidondoka nilikuwa napewa.

Sasa kuhusu kuitowa siri ya mapinduzi, ujumbe huo sasa hivi utoke kwa vijana bila ya kuogopa lakini kuwe na watu wenye historia nzuri ye kuweza kuwaeleza vijana. Sasa ni kuanza upya kuwaekea sawa na kuendelea na umoja wetu. Kwanza. Mpaka hali ya Unguja yenyewe, sisi tulioko hapa, tukubaliane. Hiyo ije iwe ni nafasi ya pili sasa ya kutaka kuja kupafatuwa, tushikamane. Kwa sababu sisi wenyewe hapa bado kuna kundi liko tayari kutuangusha. La kwanza tuondoshe haya yaliopo hapa tukamatane.

Tuondoe mfarakano uliopo hapa…Sikiliza. Tuondoshe la Upemba na Uunguja maana lipo na lina nguvu. Sasa itakuwa watu wakeshatambua kama hivi watu wanabaguwana, huyu ndie, huyu sie, kiini hawakijuwi. Hao walopinduwa inasemekana ni watu wa nje. Si Wazanzibari. Ufasaha na hivo ilivokuwa hapaelezwi. Sasa kueleza ni hawa walohusika, ni vipi? Hawa walikuja ni kama mafundi tu lakini wenyewe waloifanya hii asili zao na walivo ni hivii!

Mfaranyaki alikuwepo Songea. Akenga akachukuliwa John Okello. John Okello ndo alokuwepo hapa. Wakapewa maelekezo kwa dhamana ya kwamba mnakuja kufanya haya lakini si kwakua mtakuwa watawala. Nyie mtapata malipo mpaka kufa kwenu. Watu watatu wale [Okello, Ingine na Mfaranyaki]. Sasa vipi itakavokuwa? Hawa watu watatu ndo watakuwa viongozi. Lakini wapatikane vilevile watu watakaokuwa wanakutana na hawa. Nguvu kazi. Ndo wakachukuliwa waliokubali maana baadhi ya wengine sikudanganyi kwenye plani ya hayo mambo hawakuwemo. Kama Aboud Jumbe. Kuna watu wengi hawajahusishwa makusudi.

Aboud Jumbe hajakuwemo makusudi. Pakapimwaaa, pakaonekana wapatikane watu sasa na ikafatwa asili. Hayo nokwambia ni ya hakika hayo. Asili zao! Hao wote asili zao bara. Mizizi yao ya karibuni. Hao wote Kamati ya Watu 14 asili zao bara lakini wako walozaliwa Zanzibar. Ibrahim Makungu pia. Kwao Bweleo hapo na walitokea Kunduchi. Sasa wakatafutwa asili, wazee wao.

Hiyo nakwambia nakupa ya uhakika. Wakadurusiwa wote hawa asili zao. Wengine wametokea Mafia na Kilwa huko. Wandengereko, Wayao. Wana asili zao. Na wanaeleweka. Wanatambulikana. Hawa asili wataweza kuizuwia mpaka tutafikia tutakapopafikia. Hiyo ndo ikaitwa klabu ya mapinduzi ya watu wenye kukamata siri mpaka tufanikiwe. Isivuje! Katika shughuli za ku mobile [kusukuma] wakapatikana wawili, yuko kijana mmoja anaitwa Agostino Mikaili, yuko Chuini, na mimi mmoja. Vijana! Ndo tukaja tukaelezwa na Hafidh Sulemani na Saidi Washoto. Tukajakufanya kikao mwenyekiti alikuwa Aboud Jumbe, Mwembe Makumbi.

Hiyo ilikuwa ni final [ya mwisho] sasa lakini hii siri [Jumbe] haijuwi. Siri haijui yule. Atakuja kuupiga mtindi atasema. Ikawa sisi tunafundisha yale mafundisho sasa. Wafundishaji ni walewale kina John Okello. Dakika 15 tunatoa maelekezo. Sisi tulikuwa Kichwele, na Jozani, na Masingini, wanakuja kutoa yale maelekezo. Yusuf Himidi alihusika na ubebaji wa silaha za mashoka na mapanga. Wakati ule anafanya kazi PWD (Public Works Department). Ana yale magari ya malori. Silaha liziwekwa kwa Mzee Mwinkondo, mtu mzima, keshafariki zamani. Mfaranyaki, Ingine na Okello walikuwa wanapita siku maalum katika wiki wanatoa mafundisho silaha na mbinu za kivitavita. Sasa bado. Kama bado iwe vipi? Mimi na huyo nlokutajia (Agostino Mikaili) ndo tukapata kazi ya kuingia Mtoni. Nani atamuingia Juma Maneno Muheza? Yeye alikuwa msaidizi wa kituo cha Police Mobile Force (PMF). Wa kumuingia alikuwa Saidi Washoto, Myamwezi mwenzake. Siku ikifika atuwekee watu wenye kulifahamu lengo letu. Wakatafutwa akina Kisasi. Akafungashwa Kisasi na watu. Mzee Adam wa Magereza na yeye akafungashwa na watu. Akapigwa msasaa, akakaa sawa!

Wazungu hawakulijuwa. Hawakujuwa na wangejuwa pangelikuwa na standby [tahadhari] kubwa. Kulikuwa na mazungumzo ya blah blah [ya kubabaisha] tu. Kwa sababu walikuwa ni watu ambao hawako karibu na watu wengi kuweza kujuwa mambo. Kwa hiyo mtu wake Mzungu wa kumsogelea ni wale waliokuwa karibu naye tu na si askari wadogowadogo. Si rahisi. Ilipobadilika Magereza, Ziwani na Mtoni, ikawa rahisi. Tengenezeni mchezo. Ikatayarishwa Fete na pakatayarishwa na madansa hapa Raha Leo.

Siri ya mapinduzi imefichika kwa sababu ilikuwa kwenye vikao vikuu vijana walikuwa hawakuelezwa! Hii nokwambia mie ni kubwa sana hii. Wataelezwa vipi na hao nnaokuambia [Wazanzibari] pengine hawaaminiki? Kina mzee Mloo wanajuwa! Viongozi wale watu wazima ndani ya CUF wote wanaujuwa undani wa mapinduzi.

Kuna suala la yule Sayyid [Jamshid] kule alikuwa anadai kuwa hajapinduliwa na Wazanzibari, nimepinduliwa na watu kutoka njee! Kabisaa! Aliitoa hiyo Jamshid alipokuwa Ulaya na ikitisha ndani ya Zanzibar. Alisema eti. Mimi sikupinduliwa na Wazanzibari. Mimi nimepinduliwa na watu kutoka nje!

Ikiogopwa hiyo! Hiyo ndo point [nukta] nakupa mimi. Point [nukta] hiyo! Uingereza katika kuhojiwa hilo alilijibu. Watu wakaona sasa hatari. Sasa ikabidi wazee walinganganie hilo kutolitowa. Kwa sababu ilikuwa yule asipate pakushika. Angeipata hiyo angelifanya uchunguzi wa hali ya juu. Uhalali wa mapinduzi ya nchi ya Zanzibar! Na sasa wale ilijulikana wazi kuwa ni watu kutoka nje. Sasa ikaogopwa moja kwa moja hiyo!

Na wakati huu, nakwambia, bado wengi hawawezi kuitoa na wengi hawapewi na wanaiosoma tu ndani ya history. Blah blah [babaisha] tupu kuisoma kwao. Sasa wataificha mpaka lini? Sasa hiyo ndo question mark [suala la kujiuliza] ya kuikalia na kuiweka sawa. Kwa sababu pasipoeleweka pakawekwa sawa bado itakuwa inakwenda na huko mbele itakuja na kutokea hatari kubwa zaidi.

Sasa hapo hawa waliopo hivi sasa hivi midam ndio watu wa bara waliifanya hiyo kazi na wamezaa watoto wao na ndo hawa walionao. Sasa hapo ndo pakuzingatia. Wakubalike.2 Kweli waloifanya kazi hiyo wazee wao walikuwa wametoka bara, si Wazanzibari. Waloifanya kazi hiyo si Wazanzibari, walitoka bara lakini hivi sasa watoto na wajukuu zao ni Wazanzibari kutoka hapa.

Lakini Wazanzibari wa hapa watakubali? Hapo! Ndo hio iliomfanya kukataa moja kwa moja Nyerere ni hiyo. Manake hapa tatizo hilo alilisababisha Mwalimu Nyerere.

Ehe! Alipokwenda [Karume] yule kule kwa agizo la Baraza la Mapinduzi, ukifika kule unapanda mti huu nchi moja, serikali moja, Nyerere Raisi. Nyerere akakataa. Alipokataa alitia sababu zake pale. Manake tukiungana moja kwa moja watoto watakujakosa historia ya nchi yao. Kwa hivo wacha tuwawache itakuja kuwa nchi moja, Serikali moja, automatically [wenyewe]. Si tatizo kwa sababu watakujakukubaliana wenyewe baina ya wa bara na wa visiwani. Nyerere aliparoweka hapo na ndipo palipoharibika. Akaona asubiri. Kumbe kuna watu sasa watakuja kupafatilia na kupakumbusha.

Mimi hilo hata viongozi wenzangu nnaowafahamu hukaa tukazungumza “makosa yetu.” Kama Zanzibar itakujafika pahala kwenye mfarakano wa kuumia yakuwa ni makosa yetu lakini aliyesababisha mzee wetu Mzee Nyerere. Kulikataa hili la nchi moja, serikali moja! Alilikataaa kwa kuliogopa lakini hapo ndipo alipoliharibu.

Wakati huo kulikuwa pana khofu kwa watu, akaona aliwache. Yeye matumaini yake kwa namna tulivokwenda na jazba na namna wale watu tulivoshikana, akaona hili halitokujaleta uchunguzi kuona huyu wa hivi, huyu wa hivi. Huyu mzalia, huyu mgeni. Litakufa wenyewe. Alitaraji hivo Nyerere lakini Karume yeye alijuwa litakuwa gumu. Ndo ukaona wakaingia khofu kwa sababu tangu mapema ilivokuwa watu kimya na watu hawana la kusema, kuelemishwa kila wakati, sasa lina kazi kubwa! Wazanzibari hawakuridhika. Wana kazi kubwa kuridhika. Wanataka nchi yao!

Bila ya kuwachukulia kidogokidogo na kuwachukulia hadhari wale ambao wenye majority [wengi wape] na watu kuzungumza nao kwa uhakika kutaka mawazo yao na kupima faida na hasara. Tupate watu kama hao. Bado umoja tuuweke sawa wa sisi tuliokuwepo hapa. Tujitizame sisi wenyewe kwa wenyewe hapa tunavokwenda. Hapo patakaponogea ule ukaribu wetu sasa unaanza na wale watu wenye fahamu. Lakini pia patakuwa bado hapana muamko wa ukweli wa mapinduzi.

Sasa hilo walokuwa CCM wakilikataa zamani sasa ndo wanalolitaka sasa. Lile walokuwa wakilitaka Chama cha Hizbu. Wametumbukia huku sasa, wako against [dhidi]. Wametumbukia Hizbu. Mfano hai Mohammed Gharibu Bilali hakupita, alipita [Amani] Karume. Mimi nikikutizama wewe ni wangu na nakupa la uhakika kabisa. Huko unakokwenda unajua, mzee, ndugu yangu, kaka, kanambia hapa. Kufika kule ikakubalika kuwa huyu (Bilali) akipata anatupeleka siko! Atatupeleka kwenye Hizbu! Mwengine asikudanganye. Na alifahamika hivo. Huyu Bilali yuko mwenziwe [Dkt. Salmin Amour] huyu na atakapofanikiwa huyu atatupeleka siko.

Kinachoogopewa atakujaleta sura ya kudai anataka serikali ya nchi ya Zanzibar, na Raisi wake, na mambo yake. Na huko mwanzo nimekuambia, Zanzibar ni koloni la Tanzania (Tanganyika). Nilikwambia mapema hivo. Ukimpa mwanya atafundisha na ataleta tabu ya kuondosha azma yetu ya serikali moja, nchi moja manake mpaka sasa hivi kule [Tanganyika] ndo lilioko. Mambo ya haki za binaadamu na hii sheria ilioletwa ya demokrasia si kweli. Hii (demokrasia) iko kwenye mabano hata huko kwa wakubwa. Kwetu sisi imewekwa uwatawanye uwatawale. Hivi tumo katika kutawanywa tuendelee kutawaliwa. Mwananchi kachagua anachokitaka. Alokuwepo pale anasema hapana!

Tanzania Bara itaendelea sana kuleta majeshi Zanzibar kila wakati wa uchaguzi kwa sababu ule muelekeo wa madukuduku ya kusema Zanzibar na wao wanataka pao, wanataka kuwa na nchi yao na sio lengo! Lengo tuna sera au tuna utaratibu wa mda mrefu wa kufikia serikali moja.

Nyerere mpaka amefariki dunia hakufaulu kwa sababu hakupata watu wakumuunga mkono huku Zanzibar kuiendeleza ile sera. Hakupatikana kiongozi. Hakupata kwa sababu wote wale aloungana nao wamepotea, wamekwisha ati na ikaifanya nchi kwenda hivo. Wenzake kama hao kina Karume na wenzake wakubwa na wale wazee ambao walikuwa na Karume, baadae waliogopa kufata utaratibu wa yanaozungumzwa na vijana ya kuwa na nchi yetu na iwe na msimamo wake, mpaka Uingereza Jumuiya ya Madola inajulikana, nchi yetu inasagwa wazee, tutafikia wapi…sisi mnatuelewa vipi, sasa ikawa hawasemi ukweli. Wakifika kule wanakaa pembeni, wakija huku wanasema vipembeni.

Alikosa watu wa kumfuata huku. Amekosa watu wa kumfata huku. Wale wazee wakawa wazito wa kuliendeleza shauri zito! Hapa hapana serikali, pana mgawano tu. Huyu awepo pale aendeshe shughuli za Zanzibar na watu wake. Maamuzi ya kitu na uzito hakuna! Yako kule! Ushindi hapa Zanzibar shabaha yake ilikuwa hakika. CCM watu walikuwa wamekwisha choka nayo. Walikuwa Wazanzibari wote wanataka mabadiliko. Ndo hali halisi. Lakini sasa, kuna kitu tayari, na wakulaumiwa zaidi ni nyinyi vijana mnokwenda kule mkalishwa kuku wa kukaanga, mkapigwa moto wa kibara kule, mkawekwa lodging kule mkakaa, mkanywa soda, mkalala, mkaamka, na vitumbo vinashuka, mkaja hapa mkapewa nafasi “Mheshimiwa”, nani, mkababaika. Mkafika kule ukweli mkashindwa kuusema.

Wakifika kule watu wa Zanzibar kwenye Kamati ya Chama [cha CCM], wacha Bunge, katika Wazanzibari hakuna wanaozungumza kuhusu Zanzibar! Na atakayejitokeza hivo ataanzwa kuchujwa tangu huku, asifike kusema kule. Sasa kule kujitokeza mtu namna ile anashindwa. Bilali alifanya hivo alipompinga Karume kipindi cha pili. Akajaza fomu kupeleka kule. Akaambiwa wewe huna akili? Tanzania bara umepata kumuona mtu akampinga Raisi anapoingia kipindi cha pili? “Lakini katiba.” Akaambiwa “hapana Katiba. Utaratibu.” (Vicheko). Akazungumzwa mle. Akaambiwa sasa unatupeleka wapi? Subiri amalize. Akimaliza tunaweza tukakupa kama alivofanya Kikwete kwa Mkapa. Anaweza kuwekwa lakini yuko ndani ya mtihani hapo. Hivi unavomuona yule anapokwenda msalani usalama wanataka wapajuwe. Anozungumza naye. Kabisa! Ikiwezekana hata mkewe, hivi sasa hivi nnavokwambia ana usalama unamfuata. Na ndugu zake watamfuata kupata mawazo yake, fikra zake. Kabisa! Hata ndugu zake wa karibu wana usalama. Wanazungumza nini watu wakapeleke.

Sasa akivuka anaweza akapenya. Akapigiwa debe kule wakampa support [wakamuunga mkono] akapewa kule. Lakini wakapata dosari kidogo tu atajaza fomu atapeleka kule wale watatawanya akivuka malengo. Hayo ndo yalioasisiwa. Nchi moja, serikali moja na bado Zanzibar ni Mkoa na itaendelea kuwa Mkoa. Na aneyezungumza hapo hapataki basi hata uongozi wa Uraisi kwa hapa Zanzibar hapati! Anokwenda kwa msimamo kuwa akipata Zanzibar anataka kuiweka kwenye utawala wa serikali na nchi yake hapati! Labda anyamaze kimya mpaka akae juu ya kiti na ikijulikana basi anaweza hata akauliwa kwa kusingiziwa ajali ya gari! Huo ndo ukweli ulivyo.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: