Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!

Icon

Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia

Mlango wa Kumi na Nne: Kuanguka kwa Ngome ya Kusini

Mshikamano wa kijamii unapobomoka, kabila linakuwa halina tena uwezo wa kujihami, mbali ya kuweza kutanguliza madai yoyote. Lifikapo hapo litamezwa na mataifa mingine. —Ibn Khaldun

Mahojiano yafuatayo yamesajiliwa Cairo mwaka 1975 na hayakufanywa na mwandishi wa kitabu hichi. Marehemu Sheikh Ali Muhsin wa mwaka 1975 pale ndo kwanza alipotoka jela ni tafauti na Sheikh Ali Muhsin wa siasa za baadae za Zanzibar katika kipindi cha siasa za vyama vingi.1

Kuanguka kwa Ngome ya Kusini

Hivi karibuni jamaa mmoja katika ndugu zetu ambaye nna yakini naye kuwa ni mukhlis wetu na ana imani na sisi, katuunga mkono tangu mwanzo wa juhudi zetu na jihadi zetu, na akapata misukosuko, akafungwa, pamoja na sisi, akatolewa kabla yetu sisi, lakini amepata taabu, amenyanganywa yake, ameuliwa watu wake, alikuwa anazungumza na mimi kuniuliza mambo yalotokea. Akanambia, kwanini hamkufanya hivi, kwa nini ilikuwa hivi? Siku ya mapinduzi na kabla ya mapinduzi. Kwanini msifanye hivi, nasikia mmefanya hivi, mmedharau hivi, mmekataa msaada hivi. Nkastaajabu. Nkamwambia “fulani wewe? Kwani hukuwapo?” Ah, nlikuwepo. Vipi, hata ukawa na mawazo hayo? Sasa nieleze, manake utansameh, manake kwa hakika sijui, mimi ninavofikiri ni hivi na watu ndo wanavosema.

Nikamueleza ilivokuwa akastaajabu sana. Akasema, basi hakika nataka uwaeleze watu wajuwe upesi. Nataka muandike upesi. Nikamwambia kwa hakika tutayaandika lakini uandishi unachukuwa siku kutengenezwa, mpaka upigwe chapa, lakini kama hata watu kama wewe wana mawazo kama hayo, mimi nilifikiri walokuwa hawayajui walokuwa mbali au wana chuki tu. Lakini ikawa hata wewe ulokuwapo? Na wewe ni mukhlis, tangu mwanzo na mpaka sasa. Si mnafik wala si chochote, wala huna makusudio kwa kuwa…imani yako haikurega kwa sababu unaamin tu habari unazosikia au unavofikiri ndio ndizo, basi naona yafaa kwa hakika jambo hilo ni la haraka kueleza kwa sababu huenda watu wa karibu na sisi sana hawayajuwi, wanasema maneno. Basi kwa hivo nikaona rai nisajil upesiupesi maneno nieleze kwa mukhtasar yale yalokuwa siku zile za mapinduzi, au siku za kushambuliwa na watu wa nje. Watu wapate kujuwa hakika ya mambo yalivokwenda ili walau jamaa huko mliko Dubai mpate kujuwa na wengine watayasikia na wengine wanaotaka watapata kusajili kukopi maneno haya wayatangaze, lakini wenzetu wapate kuyajuwa walokuwa hawayajuwi.

Siku ile ya Aljumaa, mapinduzi kama mnavojuwa yalitokea Jumaapili, alfajiri Jumaapili. Siku ya Aljumaa Sheikh Muhammed Shamte alinipigia simu nyumbani kunita nende kwake. Jioni. Kwenda akanambia kuwa nimepata habari yakini kwa kuwa siku ya Jumaamosi kuamkia Jumaapili watapofanya fete Afro-Shirazi pale Kisiwandui watafanya ghasia. Watatafuta fursa ile ya fete kufanya ghasia. Ghasia zenyewe kwa hakika hatujuwi namna gani na Sheikh Muhammed aliniambia kuwa watafanya ghasia na mimi nimeshachukuwa khatwa, nishamwita Kamishina wa Polisi na nimeshampa amri askari wawe tayari, kwa hivo sina khofu wala wasiwasi kwa hapa mjini lakini nnakhofia hawa watu wa kihizbu walioko shamba, watu wetu walotupikatupika, tengeneza wewe kwa mpango wako waambie watoto wa Hizbu wapeleke habari waondoke kama mipango yetu tulivyo, waondoke kule katika vijijivijiji walioko mbalimbali wakae mwahali kwenye dhamana. Pale pale nkatoka. Natoka kwa Sheikh Muhammed nkaonana na mtoto wangu Muhsin Muhammed nikamuagizia ende amwite Muhammed Abudu Mkandaa. Mimi nkenda zangu nyumbani. Muhammed Abudu mara akatokea nikamuagizia, nikamuagizia kuwa afanye na watu wake kama desturi yetu kwa kuwapelekea habari watu.

Hizbu tulikuwa na majlis, baraza, Kamiti ya Usalama. Yakitokea mambo namna hiyo waweze watu kupashwa habari upesi. Na yeye Muhammed Abudu ni mmoja kati ya watu wenyewe waliokuwako. Bas. Muhammed Abudu kutoka pale akatengeneza na jamaa alokwenda nao kina Muhsin Badar, Mngu amrehemu, na nafkiri Muhammed Noor na jamaa wengine, Abdalla Bachu sijui, na jamaa wengine, lakini jamaa jamaa walokuwa na gari. Wakatawanyika palepale. Mimi alfajiri, siku ileile Aljumaa, tena kuamkia Jumaamosi, Muhammed Aboud akanletea habari kwa kuwa wamekwenda koote, tangu Nungwi mpaka Makunduchi, watu wote wameshapata habari. Yaani, mipango yetu ilikuwa tunajuwa wapi nyumba zenye usalama katika nchi yote. Tunajuwa wapi kwenye bunduki, bunduki zao wenyewe watu waliokuwa nazo zenye license [leseni] na zisizokuwa na license [leseni], za magendo tunajuwa, wenye bastola tunajuwa, na za halali tunajuwa. Walotengenza wenyewe tunajuwa. Wote wanajulikana na listi yao inajulikana na walokuwa vijiji mbalimbali katika baraza ya usalama. Mimi sikuwa memba wa Kamati ya Usalama. Napata ripoti yao wanapotengeneza kama tunavopata watu wengine wakubwa. Najuwa katika mipango yao ikiwa jambo la hatari kama vile ilivotokea mwezi wa June 1961 zamani na kama itakavotokea basi kwa kuwa watu walotupikatupika wende kwenye nyumba ambazo zenye bunduki na zinaweza kulindika. Nyumba yenyewe madhubuti, nyumba ya mawe na bati haina hatari ya kutiwa moto wala nini, au kushambuliwa mara moja ikahujumiwa. Bas. Wende wakusanye watoto na wanawake wakae katika pahala pa salama na bunduki zikae madhubuti waweko watu na ulinzi.

Hata alfajiri na ndo kama nnavosema, gari zimejaa umande, Muhammed Abudu kaja kanipa ripoti, timam, tumekwenda kote. Mimi nimekwenda ofisini kazini katika wizara, nimerudi mchana kuja kula, Sheikh Amour Ali Ameir kaja akanita hata sijawahi kula. Akaja nyumbani akanita pembeni kuniambia nimepata habari kwa wanangu jinsi kadhaa kadhaa kadhaa. Nikamwambia sisi tumeshapata habari na tumeshachukuwa khatwa kadhaa kadhaa. “Oh! Basi vizuri. Basi kama polisi imeshapata khabari basi na wafanye!” Na mimi namwambia, natamani wafanye jinsi tulivokuwa tayari. Isitoshe vile, mimi nikaondoka nikenda shamba kucheck mashamba kule. Na kabla ya hapo…Kamishna wa Polisi alikuwa Sullivan, Mzungu, na naibu wake wake alikuwa Sheikh Seleman Said Kharusi, na chini yake alikuwa marehemu Sketty.

Waziri Mkuu ndo alokuwa mas-ul wa usalama na yeye keshamuendea Commissioner wa polisi. Hayo yanatosha lakini sisi wenyewe kwa kienyeji kutengeneza kuambizana na wenzetu kina Sheikh Seleman na jamaa wengine wanofanya kazi polisi tunaowajuwa. Pale mimi nikajaribu kuttasil nao wote, Sheikh Seleman na Sketty. Nikipiga simu kwao siwapati. Tukawatuma jamaa kwenda kuwatafuta. Kila mtu kwa upande wake. Muhammed Aboud anakwenda kuwatafuta. Haji Husseni anakwenda kuwatafuta. Seleman hayupo, Sketty hayupo. Kila pahali tunakokwenda tunasikia wamekwenda shamba piknik. Hilo moja katika lilotupa moyo sisi. Tukaona labda huu ni uvumi manake kama jambo kama hili limeenea Unguja na sisi sote tumejuwa, na mimi kabla ya Muhammed Shamte nimeusikia uvumi huo. Tumesikia na ulikuwa umeenea kwa kuwa watataka kufanya ghasia. Lakini tulipojuwa Sheikh Seleman na Sketty, marehemu, wameondoka wamekwenda mashamba tukaona kuwa pengine si kweli manake haiwezi kuwa wao wasijuwe na Unguja nzima wanajuwa. Na vilevile, Kamishna keshaambiwa na yeye tena awape ruhsa wende zao kutembea shamba basi imeelekea kwa kuwa hapana jambo hapa.

Lakini mimi baada ya kwisha kula pale mchana nikachukuwa gari nikenda, nafsi yangu, nikenda mashamba kucheki. Nimekwenda Mwera, Kiongoni. Nimepita Dunga, Kiboje, Ndijani. Yaani, kutizama kule kama kila nikipita katika branch pale naonana na watu, nauliza, napita kote jamaa wameshafika. Nikajuwa kuwa huku kwa hakika wamefika jamaa na watu wamepata habari. Wengine wakanambia, kwani tuna khofu nini? Nikawaambia, la, pengine huu ni uvumi lakini mara tisa utisiini inaweza kuwa ni uvumi wa uongo na mara nyingi yametokeya mambo kama hayo ya uvumi haikuwa kweli. Lakini huenda mara ya Kuanguka kwa Ngome ya Kusini 227

mia ikawa ndio basi mwanamme hata akikaa huchutama. Hakai na kulala. Basi tuwe hadhar [macho].

Bas. Huku kurudi, mimi sku ile sikulala. Vile vile nimepeleka jamaa zangu wa kupeleleza na nini, kunipa habari. Wakawa wanapeleleza na walikuwa wanaitizama ile hali inavokwenda na nikakaa ila mnamo saa saba za usiku nimekuja kupata ripoti kuwa mambo salama, fete imekwisha na mambo kimya, na walokwenda kutizama mpaka sehemu za mashamba, mpaka pande za Maruhubi na Bububu, wanaona jamaa vijana wa Kihindi wengine wanatoka katika mandal zao, wanaimba njiani wanarudi na maaccordian. Hapana kitu. Salama. Pale ndo nikasinzia.

Haikufika mda, saa hivi na nini, nikasikia simu na huku nnasikia bunduki. Mambo yamechafuka. Mle nilivosikia vile kwanza niliona ni kwa kuwa hawa zitakuwa ghasia kama za June labda kwa kuwa watakuja na mapanga na mimi nyumbani nilikuwa na bunduki ya .22 na bastola. Nikaona hawa jamaa wakija hapa na mie nnaye Sheikh Hilal Muhammed, bin ammi yangu, na shemegi zangu wengine, nna vijana hapa watu madhubuti, wakija hapa na waje, lakini nikapata habari Smithyman kanipigia simu kwa kuwa Ziwani imeshaanguka. Smithyman alikuwa ni Katibu wa Sheikh Muhammed Shamte. Mzungu yeye. Akanipigia simu kuwa Ziwani imechukuliwa. Na Mtoni imechukuliwa. Imebaki Malindi Station tu. Bunduki nazisikia jela pale ambapo ni kama khatua mia mbili kutoka kwangu. Nazisikia karibu pale. Sasa nikaona khatari sasa. Nikamwambia Abdalla Sudi uchukuwe ndugu zako na wanao hawa mwende mjini. Kwa mkwe wangu mjini. “Wewe mwenyewe?” Nikamwambia ukiweza kuja nchukuwa njoo. Hukuweza basi.

Muda si muda akenda Abdalla Sudi akanipigia simu yuko hospitali anasema baina yangu mimi hapa hospitali na kwako, katika njia ya mivinje pale, gari ya 99 imepindiluwa na askari hatujuwi wamekwenda wapi.2 Wameshambuliwa. Kama wameuliwa au wamekimbia, hatujuwi. Basi hapapitiki. Nikamwambia usije. Mimi nitatafuta njia mwenyewe.

Muda si muda, Abdalla Sudi jabbari, naona kapita katika minazi, kazima taa gari yake, kaja pale tukapanda sie tukenda zetu mjini. Kufika mjini… Nimesahau kitu kimoja kwanza. Nililetewa askari. Alikuja Misra kunambia kuwa tumepata habari kuwa kumefanywa nini na nini…askari wenyewe na marungu na ngao za majani za mabuwa. Tumesikia kuwa wewe ni katika mtu anayetakiwa kuuliwa. Mimi nkacheka. Nikamwambia “haya.” Sikumwambia kuwa mimi nategemea bunduki yangu mwenyewe na bastola na imani za wenzangu nlonao kuliko hao askari. Nkaona ndo ulinzi wenyewe ndo huu? Askari wale wakabaki.

Nkenda zangu mjini, watoto walikuwa wameshatangulia, na wenzangu wale tukenda nao kwenye gari ile. Tukenda mpaka nyumbani kwa Sheikh Muhammed Shamte. Tukasikia kuwa yuko katika nyumba ya pili kule Shangani. Tukenda Shangani kule tukawakuta jamaa wengine, tukawakuta Mawaziri wengine wamekuja, halafu tukafanya mkutano katika nyumba ya Sheikh Amour Ali Marhubi karibu pale. Halafu tukaondoka, mimi na Sheikh Muhammed Shamte, nafikiri na Sheikh Hilali nadhani, sijui na Sheikh Juma [Aley] tulikuwa pamoja…tukenda Malindi police station. Kwenda kule tukaona pale ndo kuna ulinzi na nini. Tukamkuta Kamishna wa Polisi na akasema kuwa hali mbaya lakini piteni…kabla ya hivo tukataka kuttasil [kuwasiliana]…tunajuwa wako askari wa Kiengereza Kenya. Wa jeshi la Kiingereza. Na desturi yetu mambo yakitokea, na sisi ni memba wa Commonwealth [Jumuiya ya Madola], japokuwa tumepata uhuru wa mwezi mmoja, lakini ni memba wa Commonwealth, na tumesimama katika miguu yetu, ni wajibu wetu kusaidiana katika jambo linolotokea katika mji. Fujo na ghasia zinafanywa katika mji. Manake kuna sheria zimevunjwa na watu wasojulikana manake mpaka wakati ule hakuna kitu chochote rasmi kama ni Afro-Shirazi, nani, na nini. Lakini fujo katika mji tu. Si askari. Ni watu tu wanafanya ghasia.

Sasa, tukataka msaada ule wa askari wa Kiingereza. High Commissioner, Balozi wa Kiingereza alokuwako pale, alisema askari wa Kiingereza hawawezi kuja hapa ila wapewe rukhsa na Serikali ya Kenya, wao ndo wenyeji wao. Sheikh Muhammed Shamte akapiga simu Nairobi. Kule asimpate Kenyatta lakini akampata Makamo wa Raisi naye alikuwa Joseph Murumbi. Joseph Murumbi akasema Raisi yuko shamba sasa hivi lakini nna yakini atakubali kuwaruhusu. Kuona taathira ile, tukamwambia tutachelewa ikiwa mpaka asubuhi Kenyatta aje na nini, tukaona kwa kuwa tuwasiliane na Tanganyika japo kuwa hatuna maskilizano mema na Nyerere, lakini rasmi hatuna ugomvi. Kwa pale kwa hakika hatuna maskilizano mema lakini kiserikali tulikuwa tukisaidiana kila likitokea jambo Tanganyika au Kenya au Uganda wanatusaidia, na Tanganyika likitokea jambo Zanzibar inaisaidia vilevile. Tunapelekeana askari na nini. Hili ni jambo la siku zote. Tukaona ni mazoea yale ya ujirani mwema tulokuwa nao tokea wakti wa Mgereza basi sisi wenyewe tuendelee nao. Sheikh Muhammed Shamte akampigia simu Nyerere kutaka kusema naye. Akaambiwa bwana kalala. Mwamshe mwambie mimi ni Prime Minister [Waziri Mkuu] wa Zanzibar nataka kusema nae. Akasema hatuwezi kumwamsha. Saa kumi ya alfajiri. Hapo tuliona japokuwa hatusikilizani mtu akikosa ziwa la mama hata la mbwa hunyonya basi na tuombe msaada wa Tanganyika lakini tukaambiwa bwana hatuwezi kumuamsha! Tizama uwongo huo? Na hali wakti huo Karume, Babu, Ali Mahfudhi, Saleh Saadalla, wote wako pale, na bwana kalala ati hajuwi!

Sisi hapohapo, tukamwambia yule Balozi wa Kiengereza, basi wako askari wa Kiengereza Aden itachukuwa saa tatu nne hata kufika hapa kwa aeroplane au zaidi, lakini haizidi kuliko hivo.3 Wataweza kufika. Akasema jeshi la Kiengereza haliwezi kuja hapa bila ya rukhsa ya serikali London Tukamwambia, basi taka rukhsa huko! Akasema leo weekend, weekend Jumaamosi na Jumaapili, hapana mtu. Hebu serikali ya Kiengereza hulala weekend! Sijapata kusikia serikali ya Kiengereza kulala au serikali yoyote. Ina weekend kuwa haiwezi kupatikana watu kufanya kazi. Waziri popote pale alipo anapatikana hata akiwa wapi. Hata akiwa wa upelelezi. Akasema, tena akaongeza hivi. Ala kulli hali, mimi siwezi kupendekeza, siwezi kupendekeza, kupendelea, kuwa nyinyi mpokee msaada, serikali ya Kiengereza iingilie mambo ya ndani ya Zanzibar yanotokea, na ya pili kwa kuwa nyinyi ni serikali ya watu wachache.4 Nikamwambia sikiliza bwana we: si serikali ya wachache. Sisi tulikuwa na viti 18 dhidi ya viti 13 va wapinzani tunaambiwa ni serikali ya wachache iloshinda kwa uchaguzi wa halali kwa mujibu wa katiba na sheria zote zilokuwa duniani. Anatwambia ni serikali ya watu wachache. Lakini ukishashindwa huna lakusema. Huyo mtu ndo hataki.

Ndo tumeshindwa hivo. Mimi nafsi yangu nikapiga simu Dar es Salaam kumpigia simu na Balozi wa Misri, El Isawi, ili kumtaka msaada wa Misri ije kutusaidia. Hiyo tena yane. Ya kwanza Kenya, ya pili Tanganyika, ya tatu Waengereza, yane Ubalozi wa Misri. El Isawi, Balozi, ananjibu boi, boi wa Kiswahili, wa Kiafrika, ananjibu kwa kuwa bwana hayupo. Sasa, hatuna la kufanya. Tuko kwa Balozi wa Kiengereza tunashindana nae, nikapata mimi simu kutoka kwa Inspekta General wa Polisi (Hamza Aziz), mkubwa wa polisi wa Tanganyika. Ananambia mimi “kumetokea nini huko?” Nikamueleza kwa kuwa kumetokea fujo na nini. Akaniambia je wanapigana Waarabu na Waafrika? Nikamwambia si masala ya Waarabu na Waafrika. Katika hao wanofanya kazi wamo Waarabu na Waafrika. Lakini ni watu tusiowajuwa kama ni wahuni tu. Hawakujitambulisha kuwa wao ni nani. Ni watu wanafanya ghasia, wanauwa watu, wanawake. Manake akasema Raisi anataka kujuwa. Baada ya muda Nyerere akapiga simu. Tena mchana mnamo saa tatu kama hivi. Nyerere akapiga simu kusema na Sheikh Muhammed Shamte. Akamwambia kumetokea kadhaakadhaa, nilipotaka kusema na wewe alfajiri nilitaka msaada wa askari. Sasa, sisi mambo yameshaharibika na sisi tutayari kujiuzulu. Wao wanataka kuendesha serikali na waendeshe serikali.

Tunataka hapa Waengereza wawete, wao waendeshe serikali lakini wasiuwe wanawake na watoto wasiokuwa na makosa. Sisi Mawaziri mbali lakini raia wasiwaguse na sasa tutawapa serikali. Hawataki hata kuja kusema na Balozi wala kusema na sisi, basi sasa tunaomba aje Waziri kutoka kwako huko watamsikiliza. “E bwana mimi nnaambiwa…” Raisi Nyerere anavosema. “Mimi nnaambiwa siku zote naingiliaingilia lakini naapa kwa haki ya Mungu, mimi siyaingilii mambo…siyajuwi mambo hayo hata kidogo. Siku zote naambiwa naingilia mambo…hata. Sina habari nayo wala siyajuwi.” Akamwambia, wacha hayo bwana. Watu wanakufa bwana na watoto na mambo yote, wanauliwa bure, si watu wa siyasa, wala nini, wanauliwa bure. Si watu wa siasa. Kuna mauwaji, tunataka mtu aje, ataskilizwa tu. Akasema, haya ntafanya shauri. Hakuja mtu yoyote! Watu wakaendelea kuuliwa wiki nzima! Na Nyerere hakumleta mtu kuja kuzuwia mauwaji.

Wakti huo tena, hapana la kufanya. Hapana la kufanya ila kila mtu alokuwepo pale…mimi nkenda kwa wakwe zangu pale kwa miguu. Sheikh Juma [Aley] akenda kupanda motokari na Muhammed Shamte, Abdalla Sudi akawachukuwa. Mie nkashuka salama pale, risasi zimo mote majiani mle lakini na mimi nilikuwa na bastola. Sikufa lakini nisingekufa peke yangu. Nkenda mpaka nyumbani halafu nikasikia, Jumaatatu jioni, wakati nasinzia, siku ngapi skulala, mke wangu akanambia kuwa wamesema katika radio Mawaziri wende….Kwa hakika, sisi tulitengeneza palepale Mawaziri tulipokuwa kwa Sheikh Amour Ali Ameir, tangu niko Malindi, nikampeleka Haji Hussein nafkiri ende akamwambie Sayyid Jamshid aoondoke yeye asafiri. Akasema Sayyid Jamshid sendi mie ntakufa na wanangu. Ntakufa na watu wangu. Nikampeleka Sheikh Hilal [Barwani], nkamwambia lazma aondoke. Kama anataka salama, hata salama ya watu wake ni bora yeye aondoke. Tukatengenezewa meli pale, ikaagiziwa. Dr. Baalawy nadhani ndo alokuwa amehusika. Akatengeneza meli ikawachukuwa yeye pamoja na jamaa…na kabla ya hivo, Malindi pale, Kamishna wa Polisi, akawaambia waje jamaa, kila mtu mwenye bunduki, hata wenye bunduki za shotgun zile za kupigia ndege za mchezo. Tukawapelekea habari jamaa, alhamdulillah walokuja wamekuja. Wengine wamekaa, hawakuja. Wengine wamekuja katika sahib zetu. Kina Said Badr, Salum Ahmed, na kadhaa kadhaa watu wengine, Muhammed Msellem, wamekuja Malindi pale, wakawa wanajibizana risasi zile, nipe nikupe, wao na watu wa upande wa pili kule.

Sasa wale walokuwa Malindi ndo waloweza kusaidia hata Sayyid Jamshid na wengineo wakaweza kusafiri na kwenda na meli kuondoka. Wao ndo walokuwa walinzi wa mwisho Malindi pale.5

Kutoka hapo sisi tukenda kupanda gari na Abdalla Sudi akanchukuwa kwenye gari ya Sheikh Ali Masoud Riyami, kuukuu, ndogo, mpaka Makao Makuu ya Polisi juu ya jela. Nkenda kule, nikatoka mimi katika upande mmoja wa gari, na Abdalla Sudi akatoka hivi, mikono juu kama “hands up” hivi. Kule juu katika roshan ya ofisi, si mbali, haifiki, haizidi kuliko futi thalathini kutoka nlipo pale, kuna watu wawili, mmoja ana machine gun na mmoja ana bastola, wanapiga mfululizo. Wananipiga mimi na Abdalla Sudi lakini hazilii. Wameshika wamekazana lakini Mungu kajaalia hawajui kufungua safety pin nafikiri. Hawajuwi. Wote walokuwepo pale, wanapata watu sita, saba, wanane. Watu wachafuwachafu hivi na nini. Mmoja akatoka ananijuwa akanita “Sheikh Ali.” Wale wengine hawanijuwi. Wale ni dhahir si watu wa Unguja kwa sababu hakuna mtu wa Unguja asonjuwa. Nikamwambia tumepata radio kwamba nije huku, tuje huku. Akasema “si huku bwana. Raha Leo.” Wakanchukuwa katika gari ya 99 [ya polisi] imevunjikavunjika. Tuko njiani ndani ya gari moja katika alochukuwa bastola katika wao…kwa hakika pale sina woga, sina ushujaa. Manake sikuogopa. Nnaona kiama kimefika, watu wanakufa na mimi mmoja katika wao. Nimeona maiti njiani kadhaakadhaa na watu walivouliwa. Sioni athari yenyewe kitu nini kile. Sioni kitu. Njiani ikawa watu wengine wanapiga kelele. Mkungu Malofa kule “huyu Zaimu, huyu Zaimu. Zaimu huyu.” Mimi nkawaambia, jamaa wako kule wanataka wakapelekewe gari. Wakasema “sisi tunakutaka wewe, hatuwataki wao.” Gari ya Abdalla Sudi tukaiwacha pale pale.

Tukenda mpaka Raha Leo. Wasinteremshe mlangoni khasa. Watu wamejaa mamia kwa mamia. Marisasi yanalia, maghasia, harufu ya bangi na tende tu basi. Tumeshuka kidogo khatua kidogo nyuma hivi kabla ya ule mlango mkubwa wa Raha Leo, ikawa tunakwenda kwa miguu, mimi niko mbele na huku nyuma nafatwa na mabunduki na masilaha na mabastola. Nakwenda juu. Akaja mtu nyuma akanipiga rungu la kichwa. Sikugeuka mimi kutizama. Nimepasuka, madamu yanamwaika. Sikugeuka. Naomba. Kufa siogopi lakini kupondwa hivi hivi mbele za watu naona fedheha. Basi nilikuwa naomba nisianguke. Nisianguke. Nikawa natizama mbele tu. Hata sikumtizama nani aliyenipiga. Kwenda, naingia mlangoni, namuona Babu, namuona nani sijui, Khamis Abdalla Ameri na bunduki yake, nikacheka nao hivi, kama kutabbasam hivi, manake mashujaa, mmefanya kazi yenu barabara. “Haya” katika akili yangu. Mmefanya. Ndio, haya. Bas. Nikapanda juu. Kupanda juu, Karume kuingia kuona damu ile. “Ah! Nani huyo?” Nikamwambia basi jamaa wengine wako kule, wako Shangani wanangojea English Club chini. Wakawachukuwe, manake yatawapata kama yalonipata mie.

Kwenda juu, watu walonpokea, ni Karume, amezaliwa Kongo, John Okello, ambaye hata Kiswahili hakijuwi, Mcholi kabila ya Obote, na Misha, Yahudi Muisraili, aliyekuwa na kampuni ya samaki pale Malindi. Yeye Misha ndo akanipa sigireti. Nikamwambia sivuti. Pale nalomkuta alikuwa Amir Ali Abdulrasuli (cabinet minister), Mungu amrehemu. Akatoka John Okello akawa yuko mtu anatulinda pale na ana bunduki. Sisi tumekaa na yule mtu amekaa na heshma yake kwa hakika, mchafu na miguu chini na bunduki na nini, lakini kakaaa kwa utulivu. Hakutufanyia utovu wa adabu wowote. Akatoka John Okello akamwambia atampa bastola mbili, moja ya Ali Muhsin, moja ya Amir Ali. Wakifanya vyovyote vile wapige risasi. Sijui kwa nini sharti bastola mbili sijui. Lakini hakumpa. Basi ikawa hivo halafu ndo akaja Karume akaja kututaka, na walikuwa wamekuja jamaa wengine tena, wamekwenda kuchukuliwa. Karume kapeleka gari kuwachukuwa. Halafu Karume akatutaka na Shamte kutuliza watu. Haya mambo ndo yameshatokea, na nini na nini, yasizidi watu wasifanye upinzani. Sisi tukaona hapana maana. Kweli, sisi tunataka liliopo jambo kubwa ni kuokoa roho za watu. Tukasema nao katika radio, Sheikh Muhammed Shamte akasema, na halafu nikasema na mie, kuwatuliza watu wasifanye papara, watizame kama haya ni majaaliwa ya Mwenye Enzi Mgu, zaidi baada ya haya Mwenye Enzi Mgu ndo mwenye kujuwa. Lakini iliopo, kwa sababu ya kuokoa roho za watu zisitilifu zaidi zilivotilifu, watu wasifanye upinzani, waitii hiyo serikali mpya, utawala mpya, kwa maslaha ya nchi yote na wao wenyewe.

Hayo basi kwa mukhtasari ndio yaliotokea siku ile. Sasa kuna lawama kadhaa kadhaa kadhaa. Kuna watu wanalaumu kwa kuwa sisi tulikuwa waregevu. Kwa kuwa hatukuchukuwa khatuwa za kutosha za ulinzi kabla yake. Kwanza watu wafahamu kwa kuwa ni mwezi mmoja tangu sisi kushika ulinzi wa Zanzibar. Kabla yake ulikuwa ulinzi uko katika mikono ya serikali ya Kingereza kamili. Sisi kwa mwezi mmoja tu tumepewa mambo hayo na mwezi mmoja ndo mambo yametokea. Kama lawama ya kujenga uaskari au nini au nini lawama hiyo ni ya Mngereza, si yetu sisi. Lakini juu ya hivo, tuliokuwa tukiyafanya wakati wa Mngereza ni ya kudai na kuomba na kudai, nguvu za kutekeleza hazikuwa katika mikono yetu.6 Jambo lolote lilohusu ulinzi halikuwa katika mikono yetu ya Hizbu au ZPPP. Ilikuwa katika mikono ya serikali ya Wangereza. Na juu ya hivo, ilipotokea yale machafuko ya mwezi wa June mwaka 1961 sehemu ya askari wa Kizanzibari katika polisi ilikuwa thuluthi moja tu. Thuluthi mbili zilikuwa ni wageni. Na kabla ya hivo ilikuwa hapana kabisaa! Yalianza hayo kwa hakika, siwezi kukumbuka katika mwaka gani, mwaka 1950 au kabla yake, nimo katika Majlis Tashrii [Baraza la Kutunga Sharia], tulidai habari hiyohiyo, tuko Majlis Tashrii tukiteuliwa na serikali ya Kingereza, jina ni Sayyid [Mfalme] lakini hakika ni Resident ndo alokuwa na nguvu japokuwa kama tulikuwa tukipendekezwa na jamiiyati zilokuwako.

Mimi na wenzangu katika gazeti la Mwongozi tulikuwa tukidai habari ya polisi waingizwe Wazanzibari. Ilikuwa daima serikali ya Kingereza ilikuwa ikitaka kuandikisha watu inakwenda Dar es Salaam na Mombasa kuandikisha watu wa bara, sio watu wa Zanzibar. Na huo ndo mtindo wao wakoloni, si hapa tu. Tanganyika walikuwa wanachukuliwa askari kutoka Kenya, Kenya wanachukuliwa askari kutoka Tanganyika, mpaka Sudani na nini. Uganda wanachukuliwa askari kutoka Sudani, au Malawi, na Malawi wanachukuwa watu wa Tanganyika. Manake Wangereza walikuwa hawaamini askari wa kienyeji. Basi sisi ndo walikuwa kabisaa hawatuchukuwi. Tulipodai saana nikapinga katika kamiti ya pesa, ikawa mimi khasa nafsi yangu nikachukuliwa kwa Kamishna wa Polisi akasema hatuwezi kuwatia watu wa Zanzibar kuwaandikisha kwa kuwa mishahara iko chini, nyumba za kukaa ziko chini. Nikachukuliwa mimi nikaonyeshwa Bomani kule, nikaona kweli kwa hakika nyumba zilikuwa za mabati na kuta zake ni mabati, hapana chochote, hapana njia kufikiri kwamba mtu wa Zanzibar ataweza kuishi katika maisha yale.

Tukakubali sisi serikali itumie mapesa zaidi kutengeneza hali za askari wa polisi.7 Ndio zikajengwa hizi nyumba za polisi, mishahara ikaongezwa, wakapata viatu, ndo wa Zanzibar wakaanza kuvutika kuingia chumba cha nane, watu waliosoma, basi hapa Zanzibar wakaanza kuandikisha. Hata tulipofika mwezi wa June 1961 ilipotokea machafuko yale wakauliwa watu wetu wanafika 64 walivouliwa na Afro-Shirazi ilikuwa jeshi la polisi thuluthi moja watu wa Zanzibar, thuluthi mbili za wageni. Hivohivo, tukashika sisi serikali ya madaraka, hatuna nguvu kamili lakini tunadai na kusema na Wangereza, tukaandikisha watu askari mpaka tukaongeza tukafika thuluthi mbili. Kuja mapinduzi thuluthi mbili za jeshi la polisi walikuwa ni watu wa Zanzibar na thuluthi moja walikuwa watu wageni. Na hawa watu wageni tulikuwa tushafanya mipango kuwabadilisha na askari wetu wa Zanzibar walioko Kenya, Tanganyika na Uganda waje huku na sisi tutawapelekea wao. Kama hatukupata nafasi. Ilikuwa ameshakwenda Seleman Said [Kharusi] kusema na serkali na polisi za kule habari za kubadilishana watu. Na haya nahakika ndio yaliotokea hata kwao Kenya wakafanya na nchi nyengine za Afrika Mashariki. Kila nchi inataka kuwa na polisi wake na jeshi lake liwe la wananchi wake. Lakini ilikuwa wakti hatujamaliza ikawa thuluthi moja watu wa bara, au watu wa nje, na thuluthi mbili wenyeji. Watu wengine wanasema vilevile kwa kuwa kwa sababu hatukuwa na jeshi, hatukuunda jeshi. Kama ni kuunda jeshi ni baada ya uhuru manake kabla ya uhuru kama tunavosema ni serikali ya Kingereza ilokuwapo na serikali ya Kingereza hakuna jeshi. Na vilevile, jeshi sio linolinda mapinduzi ya nchi. Jeshi linahami kwa mambo yanotokea nje. Pengine hilohilo jeshi ndo linoweza kupinduwa. Kama jeshi linalinda lingemzuwia Nkrumah asipinduliwe, lingemzuwia Ben Bella asipinduliwe. Nchi ishirini na mbili zimepinduliwa baada yetu sisi Zanzibar katika Afrika tu.

Majeshi yangeweza kuwazuwia hao watu zenye serkali hizo zilokuwa zenye majeshi makubwa. Alakulli hali ilikuwa polisi kazi yake ya ulinzi wa nchi na ndo kazi yake ya upelelezi na kutafuta usalama wa nchi. Lakin jambo moja nitaeleza kuwa, nimepata habari baada yake, kwa kuwa Kamishna wa Polisi Sullivan baada ya kupewa amri na Sheikh Muhammed Shamte kuwa aweke askari tayari, kaitikia naam, hewalla bwana, na Sheikh Muhammed Shamte wakati ule keshatekeleza wajibu wake wa kuwa yeye ndie aliyekuwa mkubwa wa usalama, si Ali Muhsin, wala si Juma Aley, wala si Amir Ali, wala si Rashid Hamadi, wala si Maulidi Mshangama, wala si Baalawy, wala si yoyote katika sisi, bali hata si Salum Kombo aliyekuwa ndie Waziri wa Mambo ya Ndani. Manake Waziri wa Mambo ya Ndani ndiyo kazi yake habari ya amani lakini, kabla ya hivo, mimi nalikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani katika wakti wa Serkali ya Utawala wa Ndani wa madaraka na nalikuwa na nufudhi za mambo ya ndani. Lakini tulipokuja kupata uhuru mimi nkashika Wizara Kharijiya, mambo ya nje, na Salum Kombo akashika Wizara ya Mambo ya Ndani, lakini khasa mambo ya amri ya polisi na mambo ya security yalikuwa katika mikono ya Waziri Mkuu mwenyewe. Sheikh Salum Kombo alikuwa ni Idara tu habari ya mishahara yao, kutizama hali zao na nini, hakuwa na nufudhi na amri ya polisi. Sheikh Muhammed Shamte, na mkubwa wa serikali popote pale ndie mwenye amri ya mwisho katika mambo ya usalama wa nchi. Hata huyo Waziri wa Mambo ya Ndani hana nguvu ila kwa amri ya Waziri Mkuu. Na Waziri Mkuu ndiye aliyemwita Kamishna wa polisi ambaye ndiye executive, mtu wa kutekeleza amri. Akamwita Kamishna wa polisi akamuamrisha nini la kufanya. Ndiye kama commander-in-chief kama tungekuwa tuna jeshi. Sasa naye vilevile akamuitikia hewalla. Kazi ya kisiasa, kazi ya uwaziri, kazi ya utawala, pale imekwisha. Yeye ni kazi yake kuamrisha keshaamrisha. Bado ingehitajia kwa kuwa yeye khabari ile badala ya kuwa Sheikh Muhammed Shamte kaipata mbele yeye, yeye ndo kawaambia polisi.

Inataka polisi, sehemu ya “special branch” [usalama] tulokuwa nayo, ndo sehemu ya upelelezi, itupe khabari, impe khabari Commissioner of Police atwambie sisi, amwambie Sheikh Muhammed Shamte, ampe khabari ya kuwa kuna khatari hivi na nini na nini atowe mapendekezo yake, nini anataka tufanye. Lakini polisi haikufanya hivo. Badala yake sisi, sisi wanasiasa ndio tuliopata khabari kwa njia ya vyama na njia nyengine tulizonazo, ndo tukapata khabari. Sisi si polisi, si serikali. Sisi ndio tulopata khabari, Sheikh Muhammed Shamte, ndiye yeye akamwambia Kamishna wa polisi na Kamishna wa polisi katoka pale, hakutekeleza amri aliyopewa. Badala yake, ninavosikia, Speight alokuwa ndio mkubwa wa “special branch” alipoelezewa na Kamishna akasema “a, huu uzushi, Hizbu kazi yao kuwazushia Afro-Shirazi.”8 Fikra zake zile zile za kizamani, ilipokuwa Afro-Shirazi ndio kipenzi cha serikali ya Kiingereza na sisi ndo maadui, ndo tunotaka kupinduwa serikali ya Kiingereza. Basi yeye hajuwi sasa sisi ndo tumekuwa serikali na wajibu wake afate. Lakini waongo hao. Wametengeneza, wanajuwa! Maana yake ingelikuwa hawakuamini kwa kujuwa hivo wasingeondowa family zao, family zao na watoto wao, kuwatowa Ziwani kule na wapi na nini, wakawaleta mjini kwa usalama. Wakaachilia ndugu zetu, askari wale, wakiuliwa vitandani, bila ya bunduki bila ya chochote, wamepewa marungu tu basi.

Basi hali ni hivo, hakuchukuwa khatuwa yoyote Sullivan.9 Wamekwenda wamewaachilia wale ikawa watu wale waharibifu walokwenda kushambulia wakachukuwa armoury [ghala ya silaha] kwa mipango yao, silaha zile za Bomani na nini. Kitu kinafaa mtu kushukuru vilevile kwa kuwa polisi yetu haikuwa khain. Wachache kama Edington Kisasi na wengine, lakini wengi wao walikuwa ni watu madhubuti hata hawa watu wa bara. Watu kama Kilonzi, mtu wa Kenya, yeye ndo maana wakamfukuza mwisho. Mmoja kabila yake mwenyewe Nyerere! Prison yote ilikuwa ni tiifu, wamepigana mpaka mwisho. Mmoja chief officer wa Kitende, kabila yake Nyerere, Langoni. Kafa huku kwa kuhami na kukataa kuwatii hao waasi.10 Sasa tizama mambo yalivokuwa. Ingelikuwa si Mgereza kujuwa mambo haya na kutengeneza mbele na kujuwa, kwanini Sullivan kafanya vile na wakakataa kutii amri ya Prime Minister kuchukuwa hadhar, hawakuchukuwa hadhar, hadhar yenyewe ilikuwa kama kuna mechi ya mpira au nini. Lakini hapana khatwa yoyote ilochukuliwa ya ulinzi kamili. Kina Seleman Said na Sketty walipotaka rukhsa kwenda shamba wakaambiwa mnayo rukhsa kwenda shamba, hapana chochote, iko fete tu basi hiyo. Almuradi imekuwa katika hali ya kutojiaandaa na kuwa hapana chochote. Ndo Sketty maskini ya Mgu akaja akauliwa anatoka shamba hana habari, hajuwi lolote linalotokea.

Sasa kama nnavosema kuwa ni wajib wa polisi na security kuwaambia wakubwa wa siasa, yaani Mawaziri, kuiambia serikali ambayo ndo Mawaziri, nini kinachotaka kutokea, na watoe pendekezo nini lifanywe, khatwa gani ichukuwe. Tena Mawaziri wale, au serikali ile, ndo inatowa amri kuwaambia wale polisi nini cha kufanya. Hapa kinyume chake. Kinyume chake kabisa. Sisi ndo tulojuwa. Serikali ndo ilojuwa. Wanasiasa ndo walopata khabari. Wakawaambia polisi na wakawaamrisha, naam, polisi hawakufanya kazi. Na polisi yenyewe ni kwa sababu ni mkubwa wa polisi alikuwa huyo Sullivan ambaye hakutii amri aliyopewa.

Sasa watu wengine watasema kwa nini mkawaachia Wangereza? Wako wengine wanasema hivo. Kwa nini mkawaachia Wangereza mpaka mkapata uhuru. Kinyume chake, watu wengine wanasema, mmewatoa Wangereza upesi ndo mana ikaleta haya. Hakika basi, ukifanya hivi utalaumiwa, ukifanya hivi utalaumiwa. Jambo likishatokea, kila mtu anakuwa na akili kuliko mwenziwe. Kila mtu anaweza kutowa habari kwanini ikawa. Kwanini msingefanya hivi? Kwanini msingefanya hivi. Limeshatokea. Kabla yake hapana mtu anoweza kukupa busara ikawa na kila mtu atasema lake. Haya ni hadithi kama yule mtu, mzee yule, na mwanawe, na punda. Kila analofanya, wakipanda wote wawili, lawama, akimpandisha mtoto, lawama, akipanda mzee, lawama, mwisho wake wakaangukia labda tumbebe punda huyu, nayo pia lawama. Au wote kutokumpanda. Pia lawama. Binaadam hana atendalo, kila analotenda ndo lawama.

Sisi tumelaumiwa, kuna wengine wanalaumu kuwa, kwa sababu mmewatowa Wangereza upesi, na hakika sisi katika nchi zote za kikoloni, ndo tulowatoa sana Wangereza upesi. Na tuna sababu. Tuna maendeleo, tulikuwa tunastahiki kutawala nchi yetu zamani kwa sababu nchi yetu kutokea hapo huru. Mipango yetu tulioitengeneza, alhamdulillahi, tumeyatengeneza, tumesomesha watu wetu, tumewafundisha mbele. Tumepigania ilmu kwanza, kwa kuwaweka tayari watu wetu. Na ilikuwa mwaka uleule, 1963 Disemba, katika mwaka 1964 kiasi katika mwezi wa September, hatokuwapo Mzungu hata mmoja katika polisi. Na nyadhifa chungu nzima zitakuwa hapana. Hata madaktari wengi isipokuwa ma specialist officers tutakuwa nao wenyewe wa kutosha. Kila kazi tena. Jeshi ilikuwa sisi tunaliunda baada ya uhuru manake tulikuwa hatuna nufudhi za kujenga jeshi. Mngereza hakutuwachia jeshi. Kaachia jeshi Tanganyika, kaachia jeshi Kenya, na nini, Zanzibar kaiacha hivihivi. Kwa sababu Zanzibar alikuwa makusudio yake, plani ya Mgereza sku zote ni itekwe na nchi hizi ambazo walizitengeneza wao ndio watoto wake mwenyewe. Huu ni mpango. Katika jela nimesoma buku moja la mwandishi mmoja Towards the African Unity anasema kuwa si jambo la kuwa ni bakhti nasibu tu kuwa nchi nyingi za katika Afrika kuwa hata zenye kuwa na Waislamu wengi zinatawaliwa na watu Wakristo walofundishwa na mamishionari. Huu ni mpango ulotengenezwa tangu mwanzo kwa sababu kwa kuwa hata bendera itakapoondoshwa lakini nguvu za ukoloni zibakie katika nchi ile. Basi ilikuwa sisi, kwetu sisi hawezi kumweka mission [Mkristo], na sisi ndo tulokuwa mbele kushika serikali.

Sasa iliokuwapo ni kuondowa nguvu zetu sisi ni kuiondowa ili Zanzibar yote imezwee! Imezwe. Kule wameshajenga wenyewe bwana Nyerere alofundishwa katika skuli zake za mission, na nini, kalelewa kwa kuwa atabaki vovote vile. Zanzibar ilokuwa imeendelea kuliko nchi zote katika East Africa lakini imebaki ndo ya mwisho ya kupata uhuru kwa sababu kwa kuwa isiwe na nufudh na hatuna jeshi, hatuna njia yoyote. Mngereza katoka, bas! Kawacha mikono yake hakutengeneza kitu. Liliopo sisi kujenga, lakini sisi, vovote tulivokuwa tunafikiri hatukuwa na, kweli tunajuwa, tumechukuwa khatwa, tumechukuwa khatwa za kutaka kujenga jeshi letu, ulinzi wetu. Tulikuwa tumeshasema na nchi za kuweza, za kirafiki, za kuweza kutusaidia sisi kujenga jeshi letu. Mngereza katuwacha mkono, lakini nchi nyengine zilikuwa tayari kwa kuja kutusaidia, za urafiki, lakini lazim tupate uhuru mwanzo. Hatuwezi kumuingiza, kuwa na alaka na mtu mwingine na Mngereza yuko ndani na ambaye hataki. Kwa sababu wameogopa. Moja katika jambo lilotuletea khasama kubwa sisi ni siasa yetu ya kupinga ukoloni kwa kupinga Uzayoni na mambo ya Mayahudi na kuunga mkono nchi za Kiislamu na za Kiarabu katika siasa zao za kupata uhuru wa nafsi zao. Hii alaka zetu na wao ndo zilotuletea khasama sisi na haya hayakuanza sasa. Yameanza zamani! Na ni siasa yao wanatuona sisi ni hatari. Ni hatari kwa sababu inakuwa ni kinyume na siasa yao. Inakuwa ni kama mwiba katika nyama.

Sasa, kama nnavosema, ilikuwa September 1964 polisi yetu ingekuwa yote Wazanzibari na Slemani Saidi atakuwa Kamishna. Ukitizama nchi nyingine zimeendelea miezi, bali miaka na Waengereza na wakoloni wako. Na ziko mpaka sasa bado zinaendeshwa na wao, na nini. Hayo hayakuwa kwetu sisi kwa sababu siasa yetu ilikuwa siasa ya uhuru. Lakini watu wengine wanasema kuwa kwanini mkawaweka Wangereza? Hatukuwaweka ila kwa kiasi ya kuwa sisi tulifika katika hali ya wasat, hali ya katikati. Hatukuwatowa kabisa kabla ya uhuru, na hatukuwa na mipango ya kuwaachilia kuendelea kwa muda mrefu. Tulikuwa katika hali ya wasat nayo haikutufaa. Hatukwenda extreme [taraf] ya huku wala extreme [taraf] ya huku. Sasa sijui tungefanya nini. Tungefanya hivi ingekuwa watu wana haki ya kutulaumu, ingekuwa tumefanya hivi ingekuwa watu wanatulaumu. Imekuwa hali ya kati nayo bado watu wanatulaumu.

Lakini haya ndio lazim yatokee na katika watu, haya hayakutupata sisi tu, yamempata hata Mtume Muhammad (SAW). Ameambiwa hivohivo na wanafik. In tusibhum hasanatun yakulu hadha min indi Allah, wa intusibhum sayiatin yakulu hiya min indak. Kul kullu min indi Allah. Fa ma lihaulail qawm la yataduna la yafkahuna hadeeth, “likiwapata jema wanasema limetoka kwa Myezimgu, likiwapata ovu wanasema limetoka kwako wewe Muhammad, sema yote yanatokana na Myezimgu.” Watu hawa. Watu hawa wana nini? Hata hawakaribii kujuwa kuzungumza! Mazungumzo hawajuwi.

Jambo jingine kuwa inaonyesha kwa kuwa mipango hii wao wameyapanga wakubwa wakoloni wenyewe. Balozi wa Kingereza amesema mimi siwezi kupendekeza kwa kuwa waje Wangereza waingilie kati katika mambo ya ndani haya na nyinyi ni serikali ya wachache. Huku wiki moja baada ya pale, yametokea maasi Tanganyika ya jeshi! Si wahuni kama hawa wetu. Ni jeshi! Discipline force [nguvu yenye kufuata nidhamu]. Ambapo likiasi jeshi basi kweli ni waasi. Manake inakuwa ni watu wa mwisho kuasi manake jeshi ndo linofata amri sio wahuni ambao hawana pesa, hawana chakula, hawana chochote, wana dhiki. Ni jeshi lilofunzwa kulinda serikali, likaasi. Sisi alhamdulillah, halikuasi jeshi letu. Jeshi la Tanganyika liliasi wakampinduwa Nyerere hajulikani yuko wapi. Ingelikuwa si Kambona, wote wamekimbia, Mawaziri wote wamejificha, na Nyerere pia. Oscar Kambona ndo alobaki akawaokowa. Wakaja Wangereza wakateremka kwa nguvu. Wakapiga mizinga. Wakateka. Wakawanyanganya silaha askari wa Tanganyika, wakamrejesha Nyerere katika kiti chake. Halafu likaletwa jeshi kutoka Nigeria.11 Likaja likashika uangalizi mpaka wakajenga jeshi jipya la Tanganyika. Basi Mngereza huyuhuyu aliokataa, na Kenya ilitokea uasi akatumia, Uganda vilevile, akatumia. Lakini khasa Tanganyika kwa sababu kwa kuwa yeye ndiye anapendelea utawala ule wa Nyerere uendelee. Sisi ilikuwa tuondoke. Wiki moja tu khitilafu baina yetu! Mbona kule kaweza kuingia? Kaweza kuingia kule katika Tanganyika akaja akamrudisha Nyerere ambapo serikali yake Tanganyika ya Nyerere ilikuwa imechaguliwa kwa 9% ya voti bas! Watu walopiga voti, walopiga kura, hata Nyerere akapata serikali yake ya TANU ikapata, ni chini kuliko tisa katika mia! Sisi zaidi ya 33% watu walopiga voti hata tukachaguliwa sisi kuchukuwa serkali. Sasa wepi walokuwa wachache? Walopigiwa voti na watu 33% ya jumla ya population [idadi ya watu ndani ya nchi] au 9% ilokuwa chini kuliko ushur [1/10] au walokuwa thuluth [1/3]? Lakini wanalolitaka ndo liwe.

Jengine linaonyesha, palepale Mngereza manwari yake Mngereza ipo, manwari yake Mmarekani ipo imekuja kuchukuwa raia zake na watu wake. Na tizama, katika watu wote waliouliwa, kila kabila limeuliwa, kila watu wameadhibiwa na nini, kila kabila. Waarabu, Waswahili, Washirazi, Waafrika, Wangazija, Wahindi, wote wameuliwa. Ila Mngereza, Mzungu hata mmoja hakuguswa! Licha kuuliwa. Hata kupigwa. Hapana Mzungu hata mmoja alopata masaib yoyote. Hili ni jambo la ajabu. Katika fujo lote lilotokea Mzungu hata mmoja hakuguswa. Basi haya watu na wayapime wenyewe katika akili zao. Katika watu waliouliwa maalafu ya watu, maalafu katika watu, wenyewe wanavosema zaidi ya 11,000 elfu, anosema mwenyewe.12 Basi katika watu hao hakutokea Mzungu hata mmoja aliyekatwa ukucha. Au aliyefinywa? Hili ni jambo la kupima watu wajuwe. Na vilevile manwari za Mngereza na Kimarekani zimetokea wapi pale pale? Mara! Na hali zilikuwa haziwezi kutuletea sisi msaada? Walikuwa wanajuwa yepi yatakayotokea na wakawapo.13

Basi sisi jamaa yakuwa mambo wanayafanya ni madogo haya yaliotokea Zanzibar. Kwa sababu wanasema kwa nini hamkufanya hivi, kwa nini hamkufanya hivi? Kwanza unataraji Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, mimi nilikuwa Waziri wa Kharijiya, mambo yangu ni mambo ya nje, sikuwa hata Waziri wa Ndani. Waziri wa Mambo ya Nje, mimi niwe dhamana wa usalama wa nchi, hili ni jambo la ajabu. Kutarajiwa kuwa mimi, amani ya nchi niwe nayo mimi. Sijui jeshi, sikufundishwa jeshi. Mimi si polisi, si askari jeshi, wala si Waziri wa Mambo ya Ndani, wala si Waziri Mkuu. Mas-uliya yote yaniangukie mimi, nakubali yaniangukie mimi mas-uliya, kwa sababu mimi siogopi mas-uliya, lakini kweli lazma isemwe. Hapana nchi ambayo Waziri Kharijiya anakuwa responsible [dhamana] for security, anakuwa yeye ndo jukumu yake habari ya amani. Si kazi yake.

Pili, yakwakuwa, aa, kwa sababu ni kiongozi wa Hizbu. Kiongozi wa Hizbu au si wa chama chochote, Wilson, England, sio anayehusika kwa kuwa yeye ni mkubwa wa chama, au Mrs Hat wakuwa ni mkubwa wa chama cha Conservative kwa hivo ndo mkubwa wa security au Wilson. Licha hivyo, mtu serikali kama hii—President Saadat, ni mwanajeshi, ni Rais, ni mwanajeshi na rais wa kwelikweli. Naye ni mkubwa wa majeshi. Leo waliadh billahi, akipinduliwa Anwar Sadaat au kama alivopinduliwa Ben Bella, lawama si ya Ben Bella alopinduliwa, wala si ya Nkrumah aliyepinduliwa, ila ikiwa siasa yake ni mbaya, unamlaumu kuwa siasa yake ndo ilopelekea mapinduzi. Lakini kwa sababu ya kupinduliwa tu si mas-ul yeye. Hata Saadat akitaka kupinduliwa, waliadh billah, sio masul. Lawama ya polisi ambayo haikulinda serikali ya Saadat. Lawama ni ya usalama haikujuwa mapinduzi mbele si lawama yake.14 Yeye kazi yake ni kulindwa na serikali, Mawaziri na nini, kazi yao ni kulindwa na security, polisi, ndio kazi yake ulinzi, ilinde serikali. Halipwi mshahara Waziri, Waziri mkuu, au Waziri wa Mambo ya Ndani, au Waziri wa Mambo ya Nje, wote Mawaziri, hawalipwi kwa sababu wao ndo walinde usalama wa nchi. Wao wanafanya mipango ya siasa ya kuendesha nchi. Polisi kazi yake wanalipwa, sasa, ikiwa wale hawakufanya kazi yao sawa ndio walaumiwe.15 Sasa sisi tunatarajiwa kwa kuwa kama lawama basi sisi tulikuwa na security [usalama] mbovu, tulikuwa na polisi mbovu, lini tulipata nafasi ya kuijenga hiyo polisi mpya au security mbovu? Mwezi mmoja?

Haya ni mambo basi watu wapime wenyewe kwa nafsi yao. Na mengi yako ya kueleza lakini naona kwa kuwa sina wakti na sasa kwa hakika nna haraka ya kuiwahi hii tepu apate kuchukuwa Sayyid Muhammed Abdul Muttalib (Mutta) anataka kukimbilia mambo ya tarawehe na nini, naye pia anaondoka kesho asubuhi, basi siwezi kuendelea zaidi. Nna mengi, mengi, mengi sana ya kueleza na Inshaalla itafika wakti watu watakuja kusoma wenyewe kwa utulivu watapoyajuwa na tutapoyasema. Lakini moja ni kwakuwa watu likisha, wanasema Wapemba “lishawavusha ni gogo.” Mkishavuka, mkavuka kwa dau mkenda upande wa pili, hamneni tena kuwa hilo ni dau. Hilo ni gogo! Basi waliovuka wakapata uhuru wao, wakamtowa Mngereza na nini, wakavuka na nini, sasa lilobaki ni gogo tu, tulitukane tu manake kwa kuwa ndo basi, tambara bovu tena limekuwa. Lakini Inshaalla kweli itakuja kudhihiri, watu watakuja kuisikia, watakuja kuifahamu, na wataelewa itakapokuja wakti wake, watakapoona ukweli, na leo ni hivi kesho ni hivi.

Na haqqi al haqq yaalu wala yuula alayhi. Na haki maisha inakuja juu wala haijiwi juu. Itakuja itadhihiri itadhihiri mpaka watu watafahamu. Na hao wanozuwa na kutafuta fursa kuleta fitna na nini tokeapo wao wako walokuwa wamepandia katika Hizbu kwa makusudi yao wapate malengo yao. Walipokuwa hawajayapata maarib yao basi wamevunjika moyo lakini watu wakweli wenye moyo wao watu wanostahmili tabu, na hii ni mitihani tunopata, na hii ni mitihani. Hakupewa mtu kwa kuwa kupata adhabu hizi, taabu hizi, ila kwa sababu kwa kuwa tumtahiniwe ili Mnyezimngu apate kujuwa wepi waliobora. Liyaalamu Allah aladhina aamanu walladhina minkum almunaafiqin. Mnyezimngu apate kuwajuwa wepi walioamini kweli na wepi wanafik. Wepi makhain, wepi wanafik, wepi wanoregarega, wepi wakweli. Na hii ni mitihani na ni sunna ya Mnyezimngu. Wa min qariyaatin ila nahnu muhlikuha wa nuadhibuha kabla yawmil qiyama. Hapana mji ila utahilikishwa, utaadhibiwa kabla ya qiyama na hii tumepata adhabu hii Mnyezimngu iwe ndo ya mwisho ya kutuonyesha sisi katika nchi yetu na Inshaalla baada ya hapo itakuwa ni faraj na faraj iko karibu. Inna fatahna laka fathan mubiinan yaghfir laka Allah ma taqaddamma min dhambika wa ma taakhara [Hakika tumekufungulia ushindi wa dhaahiri Ili Mwenyezi Mungu akusamehe makosa yako yaliyo tangulia na yajayo, na akutimizie neema zake, na akuongoe katika njia iliyo nyooka (Qur’ani 48:1–2)] Inshaalla itakuwa karibu al fath wal nasr minal Allah wa fathin karib. Inna aaidun! Tutarudi!

Labda kosa letu sisi mawaziri kosa moja. Nao kuwa hatukutoroka hapo mbele tukawawacha watu wetu katika hilaki, peke yao. Ilitolewa shauri hiyo, tuondoke pamoja na Sayyid Jamshid katika meli.16 Mimi nikakataa na Mawaziri wote kwa umoja wao wote walikataa kuondoka. Tukataka sisi tukae. Vipi tutatoka sisi na watu wetu bado wanauliwa? Tukimbize nafsi zetu sisi, au sisi na aila zetu, tuwawache watu wanauliwa. Itakuwa namna gani? Sisi tukae mpaka tulete salama katika nchi ndo tukakaa pale tunafanya juhudi ya kutaka kusema na Nyerere na nini, alete Mawaziri na nini, wakutane na wale maasi, wanaofanya ghasia zile, ili waje tukutane nao tuwakabidhi serikali, wasite kuuwa watu tu. Sisi watufanye wanavotaka. Na hii tumekaa sisi tubaki mwisho. Sisi tunafata mwendo aliotuachia Mtume Muhammad (SAW). Hata katika Hijra, ilikuwa yeye ndo wa mwisho.17 Kwanza kawasalimisha watu wake halafu ndo kakimbia yeye mwenyewe na Sayyidna Abu Bakar na Seyyidna Ali. Lakini yeye kwa kuwa akimbie yeye Mtume kwanza awaache watu wake nyuma. Vipi? Na sisi tumeambiwa tuna kiigizo kizuri katika Mtume wa Myezimgu. Je tumeambiwa na Myezimgu hivo leo twende mwendo mwengine sisi tuondoke sisi mbele tuwaache watu wetu nyuma. Tukaona la, hapa sivyo. Inaweza kuwa tumekosa, inaweza kuwa ni khataa katika mambo ya siasa, au vyovote vile, lakini kwa njia, basi kama tumekosa tumekosa kwa njia safi. Hilo ndo kosa letu kwa kuwa hatukukimbia wenyewe, tukaawacha watu wetu. Na tukakaa tunaadhibika mpaka mwisho, tukawa ndo wa mwisho kutoka. Wallahi nakwambia. Nlikuwa naomba, jela, mimi niwe wa mwisho kutolewa. Na kila waziri alokuja. Kaja Twala, wamekuja kina Karume…waachieni wana makosa gani. Tuwekeni sisi mawaziri tulofanya mambo haya. Tumeweka rekodi, tumetoka sisi watatu wa mwisho ni Rehma ya Mnyezimngu. Tunaona ni fakhri na ni wajibu wetu kukaa namna hii. Tumefanya jitihada yetu kama tulivoweza, tumeshindwa katika hayo lakini kushindwa kwetu namna hii sio kwa kuwa kushindwa. Hii ni Uhud hii.18 Hii ni Uhud. Vita va mwisho bado havijaja. Na iwe Uhud…lakini vita va mwisho havijesha bado. Vitakuja na vitakuwa, Inshaalla, vitakuwa upande wa hakki.

Watu wasighurike, wasivunjike moyo, kwa sababu ya…sisi tulikuwa na amana ya kuweka kule ikhlas, kuweka Uislamu, kuweka ustaarabu. Sisi ni ngome ya kusini. Sisi na visiwa va Ngazija ndio ngome ya kusini ya kuweka Uislamu, Ustaarabu. Miaka kadhaa wa kadhaa wamejaribu watu kutuvunja. Kwa karne kadhaa kadhaa. Wamejaribu Wareno miaka 200 wamepigana. Wamekuja Wangereza na Majermani na Wafaransa, na sasa na wao wafurahi kidogo hivi. Falyafrahu qalilan wa yabku kathiran [Wache wafurahi kidogo lakini watakuja kulia sana]. Itakuja siku yao ya kulia. Itakuja siku yao, lakini mwenge wa Uisilamu utaendelea na ustaarabu utaendelea. Watu wanokaa yakatokea haya halafu wengine wakafurahi wakakimbia upesi, kukimbia ni kukimbia, walokimbia kule wakenda kwengine wajuwe kwa kuwa wanakimbia, lakini kuna lazma warejee huko walokokwenda…siku moja lazima warejee. Na waondoke na wakimbie, wakimbie wao kuwa wamekimbia tumeshindwa, wakti wenyewe mdogo, lakini ni kwa sababu ya kwa kuwa, zile nguvu zimekuwa nyingi kweli. Nguvu, si mapinduzi hayakutokea Zanzibar, ni wazi kuwa ni maadui wakubwa kuliko Afro-Shirazi. Afro-Shirazi ni alama tu, ni chambo tu kimetumiwa, lakini adui zetu ni wakubwa zaidi. Adui zetu ni wakubwa zaidi. Ni ubeberu, imperialism, na uzayoni, Zionism. Yamejikusanya pamoja! Hizi ndo zilokuja kutaka kuvunja Uislamu ulojengwa kwa juu ya miaka elfu sasa. Juu ya miaka elfu Uislamu uko katika visiwa vetu va Zanzibar na Afrika Mashariki. Mimi siku zote nnasema kuwa Uislamu umekuja Afrika Mashariki mbele kuliko kufika Madina kwa sababu ya Hijra walokuja wakaja Ethiopia ambayo Ethiopia ni sehemu ya Afrika Mashariki na khasa ilikuwa imeeenea mpaka katika Kilimanjaro na zaidi. Habash ya zamani, manake kote huku kukiitwa Habash.

Hivi karibuni Dr. Mustafa Mu’min, ametoka kutoka mkutano wa Muslim Student Association ya America, United States na Canada. Amekuja Profesa wa Kimarekani mwenye asli ya kipalestina, Muislamu, alikuja kutowa khutba katika mkutano ule, amethibitisha kwa ithbati za kisayansi na nyaraka, wathaiq amekuja nazo, kwa kuwa amethibitisha kwa kuwa Uislamu umeingilia Zanzibar, umeingilia Zanzibar kuingia East Africa, kabla kwenda Madina, kabla ya kufika Ethiopia. Sijaipata khutba hiyo mwenyewe nikaisoma lakini nimesimliwa na Dr. Mustafa Mu’min. Alakullihal, sisi ni Waislamu wa zamani na tulikuwa sisi ndo muraabitin kule, tunashika ngao, ngome. Kutoka kule, nguvu hizi tulizokuwa nazo za miaka elfu na zaidi. Si nguvu bali kwa kuwa sisi tulikuwa ndo askari wa kule wa kushika ulinzi. Ni wajib wetu kuendeleza Uislamu wende mbele. Sio kuwa sisi ndo tuutupe kwa sababu ya hayo mapinduzi ya saa chache yalotokea. Tuseme tujifakhari kwa kuwa sisi basi yamekwisha leo. Tusahau. La, siyo. Inna aidun, Inna aidun—Inshaalla. Tutarudi, tutarudi—Mungu Akipenda.

Alikubali Mtume (SAW) na masahaba kurudi baada ya sulhi ya Hudaybiya.19 Kurudi Madina bila ya kuingia Makka haikuwa pale kwa kuwa ni kushindwa. Waislamu wengi, masahaba wengi wakubwawakubwa waliona tumeshindwa jama na wakaona haya kubwa na wakawa wanawachukia lakini Myezimgu akamjuvya Mtume wake “Inna Fatahna Laka Fathan Mubina Liyaghfiraqa Allah ma takaddma min dhambika wa ma taakhara.” Haya siyasahau, na hata nlipokuwa Morocco baada ya kushindwa mazungumzo yetu ya katiba ya mwanzo. Nikenda Morocco nikaonana na Malik Hassan nikamwambia ya kuwa mkitwachia tukashindwa sisi katika mambo haya, sisi tukashindwa, basi nakwambia taarikh ya Al Andalus [Spain] itaandikwa tena. Zanzibar ukiondoka Uislamu basi Uislamu ndo kurudi tena nyuma. Akanambia, “usinkumbushe hayo na Inshaalla hayatatokea. Na sisi tunaona uchungu haya ya Andalus.”

Siku zilezile, niko kulekule, nalionyeshwa nyumba ya mayatima, mayatima wa mashahidi walookufa katika kupigania uhuru wa nchi yao (Moroko) dhidi ya Mfaransa. Nyumba ya mayatima. Basi nikalala sku moja. Huku niko jela Tanganyika. Nimelala nikaota nyumba ileile, ile ya mashahidi imeandikwa kwa khati kubwa! Ukuta mzima! Mbele pale. Inna fatahna laka fathan mubina liyaghfira laka Allah ma takaddama min dhambika wa ma taakhara. Basi Inshaalla itakuwa kheri. Assalam Alaykum wa rahmatu Allah wabarakatuh.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: