Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!

Icon

Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia

Mlango wa Kumi na Sita: Wagawe, Wasahaulishe, Watawale

Historia ya Algeria inaendelea kufunguka: kila rika ni lazima lianze tena upya kubuni kila kitu, kwa sababu tabaka ya watawala inachukuwa sura tafauti lakini bado haioneshi sura ya kubadilika, na haijali kuwacha kumbukumbu yoyote ya mpito wake, kama kwamba lengo lake la msingi la kisiasa ni kuwa ni rahisi kuwatawala watu waliopoteza sahau. —Ghania Mouffok

 

Mzee Issa Kibwana

Hawa wana ila moja. Hawasomi historia. Wale wanajuwa mwanawe yumo mle anasoma alif, be, te, basi, kamaliza. Lakini hawasomi historia. Mawaziri wetu wote! Wawakilishi, wabunge. Hawasomi kitu hicho. Hata! Kwamba hawakipendi. Hawapendi kumbukumbu. Nadhani zilikuwepo kumkukumbu nyingi pale. Wengi wao waliamua zikachomwe moto. Kwa jicho langu hili na mashikio yangu haya. Wenyewe hawataki. Kabisa! Hiyo kitu kweli. Hawataki. Mtu yoyote unomsikia huyu mbunge, huyu muwakilishi, ukimuuliza suala kama hili mwishoni atakwambia “kwani nishughulike nalo lina mana gani na mimi?” Hilo ndo jibu atakalokujibu. Lina mana gani na mimi? Sina mana nalo mie kwa vile hana haja nalo kulishughulikia. Linataka mtu anojuwa hatma kunakuja nini? Kizazi changu kitapata nini? Yule ndo atoshughulika na jambo hilo. Yeye kapata nyumba zake mbili tatu, anajuwa watoto zangu washarithi basi. Hana haja ya kumbukumbu. Kwa vile bwana kumbukumbu hizo pana watu wanazijuwa na pana watu hawazitaki kuzijuwa! Sasa utakuta wengi hawazitaki. Kidogo wanazitaka.

 

Mzee Mchingama

Nataka niongezee. Labda kasumba hii pia ilitokea katika kipindi, sisemi kwa nia mbaya, kwa vile tuko katika mfumo wa vyama vingi na wewe humo katika mambo haya, lakini alokuwa Waziri Kiongozi huyu Maalim Sefu, alichochea kufutwa kwa historia. Kwa sababu mashuleni pia ilikuwa imetolewa historia, Maalim Sefu alipokuwa Waziri wa Elimu. Kwamba alifuta kwamba lisikuwemo somo la historia. Alifuta. Kwa mana hiyo bila shaka alikuwa na lengo maalum kwa sababu watu wakijuwa historia wanokotokea inaweza kuleta muamko fulani.1 Kwa hivyo ikabidi imezama kabisa historia ya Zanzibar haikupatikana. Moja ilochangia hiyo. Ikawa somo la historia halijapewa umuhimu. Na kwa hivo hao viongozi walioko sasa hivi na wamekulia katika masomo hayo hawawezi kuelewa historia yoyote kwa sababu historia hiyo ilikwisha futwa. Lakini sasa hivi nashukuru kama hivo nyinyi vijana mmepata muamko wa kutaka kutafuta historia chimbuko. Mmefanya jambo la busara kuwawahi hawa wazee kabla hawajaondoka, hawajamalizika. Kwa hapa nafikiria tumpate huyu Mheshimiwa Ramadhani Haji, Mzee Natepe, akina Amboni Matias, Joseph Bhalo. Hawa nafikiria watakuwa wanazifahamu vizuri tu kwa sababu ni washiriki.

Mzee Isa Kibwana

Nawaambia ilokuwa ofisi ya Afro-Shirazi pale Kijangwani tuifanye makumbusho au tuifanye tawi la CCM. Jibu: ah! Hili bwana, jumba hili, labda sasa hivi tuwaambie hawa jamaa kwa sababu eneo hili lote limechukuliwa na posta. Ndo jibu nnopewa. Na kumbe posta haihusiki na jumba lile! Lakini wao wanakwambia linahusika eneo lote hili la posta. Ndo jibu wanokujibu. Lile chimbuko la historia safi kabisa! Ndo shina hasa!

 

J. J. Mchingama

Mawazo yao yako wapi wakati wanakuja watalii wanawapeleka kwenye makumbusho mengi ya zamani. Historia ya utumwa, au historia gani…mbona wanawapeleka!? Kwanini basi pale wasipelekwe watalii wakaonyeshwa kwamba hapa ni pahala penye chimbuko la ASP? Lakini ni watu kufanya ubadhirifu, ni kupuuzia jambo ambalo kwa kweli kwa wakereketwa khasa linaskitisha. Lile jengo lisingekuwa la kuweza kuvunjika. Nafikiria kwamba labda vijana hawachukulii umuhimu wa haya masuala. Wanataka kuongozwa. Labda mwenye kuwaongoza, mwenye nguvu zaidi hayuko na hao walioko wakitoa ushauri hawendi mbali. Wanaona kama huyu analeta kitu cha upuuzi. Lakini ukweli ni kuna mambo mengi ya historia ya Zanzibar yanayohusu ukombozi wa nchi hii, mapinduzi ya nchi hii, yanatupwa na yanakufa. Yanakufa kabisa. Jambo ambalo linaskitisha. Unapofanya ukumbusho au kuchukuwa historia hatuna mana kulipa visasi. Tuna maana kuvikumbusha vizazi vijavo wajuwe asili yake alipotokea na nchi hii. Ndo shabaha kubwa. Lakini sasa watu hawajali hivo madhali anapata maslahi yake basi. Inatosha. Hayo mengine wanaona kwamba yataleta uchochezi, yataleta vurugu, labda mawazo yao yako hivo, jambo ambalo linawafanya waone bora mambo yaachiwe hivihivi.

Mzee Isa Kibwana

Mashamba yote hapa Unguja yalikuwa ya Waarabu. Mashamba yote ya Wamanga.2 Sasa unakwenda lima weye kwa hii hekaheka ya mambo ya kisiasa ikabidi tuanze kuchukiana. Wenye mashamba na mkaazi alokuwa kwenye shamba lile. Unachokipanda huitwa watu wanaitwa “Maburuki.” Huambiwa “kangowe mhogo ule, tupa! Kangowe mpunga ule, tupa!” Unangolewa, una-tupwa. Asubuhi unakwenda unakuta peupe, ardhi mtupu. Wapi utakwenda sema. Huna. Ndo ngoma yenyewe ilipoanza. Huna mahala pa kulia. Kulia kwako utamtafuta Mzee Karume yuko wapi. Kwa sababu ndo mkuu wa chama chetu. Utakwenda utakutana nae uzuri sana na atakujibu maneno mazuri sana. Atakwambia hivi: kama wewe unanifuata mie, mimi hayo yananipata lakini nastahmili, na wewe ustahmili. Allah mwenyewe anajuwa. Iko siku hamaki zako, wahka wako na nini, utapoa. Endelea kustahmili. Kwa vile tunaendelea, 55, mpaka 56, 57, 58. Tumo katika shughuli hizo.

Hapa Unguja yote. Hakuna shamba hata moja wasiofanya vituko hivo. Zaidi ilikuwa hasa, zaidi zaidi, kutoka Kinduni, Donge, Muwanda, mpaka unakwenda Potowa yote ile, unakwenda zako Kilombero alikotununulia shamba Mzee Karume. Ile yote ilikuwa kazi yake ni hiyo. Kwa ile watu wanavomwendea yule bwana ikabidi afanye kula njia apate shamba la kuwapa wanachama wake. Kwa vile alifanikisha mwaka 1959 kununuwa shamba hilo la Kilombero. Mwaka 59 ule baada ya kulipata lile shamba aliweka mkutano mzuri sana hapa Maisara. “Jamani wanachama wangu nimenunua shamba. Kwa vile mtu yoyote anoona mambo yamemzidi pale anapokaa wako wasimamizi kule Kilombero, aende atafutiwe mahala pa kulima. Hakuna kodi. Kodi yako jembe lako ulime mwenyewe.” Kwa vile jamaa wengi wakahamia kule kwa kulimalima.

Kwa vile mie nilikabidhiwa kwa yule bwana na sina kazi hata moja akaniita “njoo.” Chukuwa basikeli hii, lakini baiskeli yenyewe ilikuwa dungudungu. Mimi mdogo kuliko ile basikeli. Wewe utakwenda Umoja wa Vijana kazi yako kuchukuwa magazeti wende unauza hukohuko mtaani kwenu. Nikawa mimi muuza magazeti. Lakini magazeti yangu yale yana tija kwa mie. Yana kujuwana na watu wa mitaani kote. Gazeti lilikuwa la “Kipanga”. Nikatembea nalo gazeti la Kipanga kama miezi mitatu. Likaja gazeti jingine kubwa. Linaitwa nani? “Tai.” Ni mnyama mmoja ana mdomo mkubwa kama kasuku hivi kakamata jiwe anaruka nalo. “Sasa wewe muuza magazeti ujuwe tafsiri hii manake nini.” Nikawekwa mie kitako. “Unajuwa fasiri yake hii nini?” “Karume anangowa serikali ya Kiarabu. Ndo huyu. Hili jiwe serikali, huyu kipanga ndo Mzee Karume anaondoka nae kwenda mtupa baharini.” Sasa imekuwa mie hadithi yangu “kipanga sasa anawachukuwa watu anakwenda kuwatosa baharini. Litazamane gazeti la Tai na Kipanga!” Sasa wengi walio vijana… e bwana nletee…Tena bei yake senti kumi.

Halafu nna umaarufu kwa Wamanga. Wamanga umaarufu wangu umekuja vipi. Mimi nilikuwa na nguvu nyingi. Basi tulikwa na Mmanga mmoja Kitope pale, anaitwa Abdul Salaam Yusuf. Yule kazi yake kukodi karafuu. Sasa mahala popote alipokodi karafuu lazma aje anchukuwe mie. Muanikaji mie na mimi ndo mbebaji magunia ya karafuu kwenda kuuzwa. Alikuwa ananiamini uzuri sana. Lakini alikuwa ananambia “wewe bwana, mtu wa Karume lakini nakuona mie mtu wangu. Panapo kazi yangu na mie nsaidie.” Namwambia “nakusaidia.” Kumbe Mwenye Enzi Mungu yote anasema “hii ndo inokupa umaarufu kwa huyu Mmanga huja ukapata kitu kwake.” Ikiwa inakuja habari ya karafuu mimi nlikuwa nakwendachukuwa magazeti. Sasa pale kambini watu wananyambuwa karafuu mimi nauza magazeti. Nauza magazeti, nachambuwa karafuu, nauza karafuu.

Tunaendelea. Karafuu zimekwisha. Sasa jamani eh! Mambo yamekuja sawa. Huyu bwana keshapasi kupata serikali. Bendera yake ishapasi. Sasa nnachokuombeni, ile nnokwambieni mstahmili ndo ileile. “Sasa mhakikishe tunapata serikali.” Mpinzani wetu Mzee Yusuf Himidi yupo pale. “A! Sasa tutapata vipi?” Mzee Karume akamjibu: “Kitu kinakujia miguuni kwako bado tena unataka kukisoma!” “Hapana Mzee, tunaiyona hali yenyewe…haya bwana twendeni.”

Wamekwenda kwenye Baraza la Kutunga Sheria baada ya kumaliza lile baraza lao, anakuja Karume anasema “imepasi Ali Muhsin tarehe 9 Disemba anapewa serikali yake. Bendera yake tarehe 10 inapanda. Sasa mfanye mipango hii serkali isitoke nje watu wakaijuwa. Ife kabisa. Mimi naanza kuiuwa hukohuko Ulaya.” Sisi, Mzee Kaujore, Yusuf Himidi, na wengineo, sasa tuko Upenja msituni kule. Humu midomo yetu yote imeoza. Chakula chetu mananasi mwitu. Au wale wanavijiji wa Upenja kwa vile wanafahamu shabaha ile wakituletea vyakula kule msituni lakini vyakula vyenyewe si vyakula. Tumejikalia kule tunafanya mazoezi yetu.

Taarifa Mzee Karume alivokwenda kule Ulaya akauliza. Mwenye kupewa serikali kuna serikali nyengine inamuongoza? Hakuna. Sasa pale pana Sultani na pana serikali ya Kiengereza. Hizi serikali zote zinakuwa wapi? Jibu, hizi serikali zote madam zinatiwa saini hapa, hizi serikali zote hazipo. Itakuwa hiyo ya Ali Mushin peke yake. Ali Mushin akasema Sultani ntamuhifadhi, Mngereza ende kwao. Karume anasema: “Kuanzia leo tunatia saini Mngereza umetowa mkono wako Zanzibar. Humo tena. Chochote kitakachotokezea humo. Tukubaliane.” “Karume maneno yako sahihi. Kuanzia hivi sasa tukitia saini Balozi anakwenda zake Zanzibar anakwenda zake hamisha vitu vake,” anasema Ali Muhsin. Yule bwana alipiga makofi makubwa sana pale. Karume alipiga makofi makubwa sana. Hawajui shabaha ya yule bwana shabaha gani. Kumbe yule bwana si msomi lakini kasoma kweli, kichwa chake.

“Sasa nyinyi mipango yetu vipi serikali tutaipata hii.” “Kitu rahisi. Sie tumejiandaa. Sisi tuko wengi. Hatuna tatizo kuchukuwa serikali. Dakika tano tu tunachukuwa serikali.” “Haya fanyeni kazi yenu.” Makunduchi haimo. Mikoa miwili tu: Mjini Magharibi na Kaskazini. Hawa watu ndo wanojuwa mambo ya mapinduzi. Ndo watu washiriki wa mambo ya mapinduzi. Japokuwa huko Makunduchi wamo lakini nadhani utampata wa kuokotea.

Mwalimu Hanga asubuhi walikuwa na msimamo wao kama mpinzani, wanapinga pinga ile. Wanampinga yule bwana—Mzee Karume. Kwa ukaribu sana hawakuwa naye. Walikuwa naye tu. Lakini msimamo wao ulikuwa wa peke yao. Hanga, Othman Sharifu…wamo tu kama bendera.

Mzee Karume muongozi wa mapinduzi. Huyo anaozungumza kuwa mzee Karume hayumo ni muongo. Hao ndo hao walokuja katikati yake wakaanza kuligawa jeshi la kimapinduzi mafungu matatu. Kuna fungu moja lilikuwa Mchangani alikuwa nalo Mfaranyaki. Kulikuwa fungu moja liko Pemba. Alikuwa nalo nani? Alikuwa nalo Okello. Kulikuwa fungu moja lipo hapa Mtoni. Hilo ndo lilikuwa fungu la Mzee mwenyewe Karume. Hilo ndo lenye kujuwa mambo hayo. Mfaranyaki alikuwa ameshajitenga. Yuko Chwaka na kikosi chake kamili. Anasema askari wangu yoyote alokuwa yuko kwenye kambi yangu hana haki kwenda mjini. Akitaka bibi mnao humuhumu ndani ya kambi yetu. Mimi nilikuwa niko Pemba. John Okello kakalia kisima cha pesa. Tena wapi? Mkanjuni, nyumba ya kasuku, kwamba yeye mpinduzi mkubwa! Ndo aloyapanga mapinduzi hasa!

Mfaranyaki anazungumza Chwaka. Anasema: “watu wanasema tu kwamba Karume ndo anojuwa mapinduzi, ndo muongozi wa mapinduzi. Mapinduzi yangu! Kundi langu! Kwa vile sasa hivi najiandaa kuingia ndani ya mji.” Vile vitatange, kwenye kundi lake vimo, kundi la Pemba vimo. Haraka vinamletea ripoti huyu bwana—Karume. “Bwana, Chwaka kuna jambo kadhaa, kadhaa, kadhaa. Jambo hili unalijuwa?” Anasema “silijuwi.” “Siku mbili tatu huja ukasikia yameanguka mapinduzi mengine tena hapa. Kwa vile tufanye utaratibu.”

Ndo hao unaowasema, kwamba kuna watu wanazungumza hiki kikao Karume kaweka wapi? Watu wenyewe nshakutajia. Mmoja Chwaka, mmoja Pemba. Unguja yuko mwenyewe. Sasa harakati za kwanza tumchukuwe huyu alokuwa karibu—Chwaka. Katumwa Khamisi Daruweshi, Saidi Washoto, Idi Bavuai, Yusuf Himidi, Sefu Bakari, na Makomred. Mfanye kula njia. Huyu mtu [Mfaranyaki] ana silaha kule. Mfanye kula njia mumkamate. Atatuharibia huyu.

Mchango wake Mzee Karume wa kwanza kwamba yeye ndo alokuwa akitumia ndani ya Baraza la Majlis Tashrii. Halafu mtu mmoja yule katika kisiasa chake baada ya kuamkia kwamba sasa serikali ishapatikana kwa hawa jamaa, yeye ndo alotowa mchango mkubwa kwa kumfukuza Mngereza na serikali ya Sultani. Kama si Mzee Karume kwenda Ulaya na Ali Musini nadhani pangelikuwa na kazi hapa!

Serikali isingepinduka. Mchango wake kwanza mkubwa yeye ndo alokwenda muondowa Mngereza. Karume. Kumbe tunakubaliana mimi mpinduzi Karume lakini serikali hii ya Kiengereza ianze kuhama. Isiwepo pale. Ili tupate nafasi huyu bwana kutandika serikali yake. Mie Karume mpinzani. Mngereza ndo nguzo yake atamlinda mtu huyu. Sasa suala lile kalikubali na Ali Musin kwamba kweli maneno unosema. Huu mchango mkubwa. Tuliuamini sisi sote tuloshiriki kwenye mambo ya kisiasa na mapinduzi. Hili suala tulikubali. Angekosea yule bwana (Karume) mapinduzi yasingekuja. Yasingekuja. Yasingekuja kabisaa!

Bwana, mimi nilikuwa, hao watoto hawatambui…lakini mimi nadhani nilikuwa begani kwa Mzee Karume. Yanazungumzwa na mimi niko begani kwa Mzee Karume. Wanapeana picha. Mzee Kaujore ndo alokuwa mshirika wake hasa! Idi Bavuai ndo alokuwa mshirika wake hasa! Saidi Washoto ndo mshirika wake hasa! Ramadhani Haji. Hawa watu maisha kundi lao ni moja.

Bwana mimi nakataa kutupiwa watu wa bara. Mapinduzi ya Zanzibar hayana mmoja. Kila mwanachama wa Afro-Shirazi Party ni mpinduzi wa Zanzibar. Hakutoka mtu nje kuja kupinduwa serikali ya Zanzibar. Kama nnavokwambia, sisi wengine wote tumetoka huko nje. Na ukiizungumza sana, hata hao wote walokuwa wakiitwa Memba wa Baraza la Mapinduzi (MBM) hakuna hata mmoja anojuwa kwamba ametoka bara. Wote ni watu wa hapahapa, ambao hakika, jadi yake yote iko bara, lakini yeye mwenyewe ni mtu wa hapa. Hakuna mtu alotoka bara kujapinduwa serikali. Hakuna. Hakuna.

Bwana, hapa palikuwa na miji miwili, hii miji ndo ilokuwa inatisha, inampa nguvu Sultani. Mji wa kwanza Bomani hapo. Mji wa pili Mtoni. Ambapo silaha zote zile ziko sehemu hizo mbili. Mtoni na Bomani. Washiriki, mkusanyiko wa washiriki—Chumbuni. Kama nilivozungumza mwanzo, Kusini hawajuwi. Mjini Magharibi, Kaskazini. Hao ndo watu wanojuwa. Mapinduzi hasa ni ya watu hao. Na wapinduzi hao hakuna Mmakonde, hakuna Mmanyema, hakuna Mturuki, hakuna nani. Yoyote anokubali kwamba kuna madhila ya Mmanga, kashiriki mapinduzi. Hakuna Mmakonde alotoka huko, au Mruguru alotoka huko kwamba nakwenda Zanzibar kushiriki kwenye mapinduzi. Yaliomkuta hapa kashiriki. Mzalia alokuwa tatizo hilo analo kwamba hili dhila tulonalo, kashiriki. Wako wengine majina siwataji. Tumewafuata milangoni mwao na kuwaambia na wakasema “mimi Muisilamu siuwi”.3

Wapo hapa na ndo wazalendo wa hapahapa. “Siuwi tena mkome kunijia kwangu.” Anaingia mvunguni. Wapo hapa. Baada ya kumalizika suala hilo yeye ndo wa kwanza kupata jina la “MBM.” Wengi tukakaa tukacheka hasa. Tena humwambia hivihivi. “Wewe jina hili umelipata wapi? Wewe si ulisema wewe kwamba hutaki kuuwa? Leo umelipata wapi jina hili. Lakini haya na tuendelee. Tunakwenda naye.” Kwa vile bwana mtu anokwambia kwamba wametoka Wamakonde kuja kupinduwa serikali Zanzibar, hiyo mimi nakataa mpaka mwisho wangu.

Baada ya kupinduwa Mtoni na Bomani, watu wote mkusanyiko ulikuwa Raha Leo. Raha Leo walikuweko watu wa sehemu zote za Unguja hii na wanatambua kwamba mahala fulani pana watu flani, hawa wapinzani wetu wakubwa. Siku ile bunduki zilikuwa hazizuiliki pale ndani. Na mfundishaji yuko mlangoni. Mfundishaji nani? Juma Maneno, Anthon Musa, na Natepe. Wale wako pale, kazi yao wanachukuwa bunduki ndani unaambiwa “Fanya hivi. Risasi tia hapa. Haya piga. Piga juu, piga juu. Buuu! Ushajuwa. Haya, nenda!” Sasa unakwenda weye unamfuata fulani, huyu ndo akiniadhibu mimi kwenye shamba lake. Sasa atakiona huyu! Anakuona wewe, bunduki lako umelitia ndani ya kanzu au shati. Hajui. Mauwaji yakaingia sasa. Mji mzima utasikia hapa wamekufa watano, hapa wangapi. Wale wale wenyewe wanotoka mashambani mle. Wenye hamaki vyakula vyao vilikuwa vikingolewa. Hawa ndo waloleta mauwaji hayo ya kulipiza kisasi. Mpaka akaja mwenyewe Karume akapanda juu Raha Leo. “Jamani basi, serikali tushapata, msiuwe watu mashamba humo! Basi, basi, basi. Bunduki haraka zirudishwe. Mnohusika mchukuwe watu wenu mrudishe bunduki.”

Ikasimama sasa, cabinet [kikundi] nyengine mpya ya kwenda Pemba. Wanatakiwa watu kwenda Pemba kwa sababu Pemba msukosuko watu wanasikia tu lakini haujaingia. Wakachukuliwa jamaa hapa. Haraka nendeni zenu Pemba. Karume anazungumza. Hakuna kuuwa mtu. Nendeni kwenye mapolisi mle kwa sababu polisi wamo watu wasije wakatuuwauwa. Kwa vile kachukuweni zile bunduki. Mzee Kaujore, Yusuf Himidi, Sefu Bakari, Mzee Natepe, chaguweni watu wa kwenda Pemba. Wakachaguliwa watu. Kiongozi wao nani? Anthony Musa. Miji mingapi kule? Miji mitatu. Kombo Juma Kombo, simama hapo kwa Mzee Anthony. Isa Kibwana Sanze, simama hapo kwa Mzee Anthony. Feruzi Kayanga, simama hapo kwa Mzee Anthony. Mzee Anthony watu hawa tunakupa na tutakupa na askari. Kugawa kwako unajuwa mwenyewe huko unakokwenda. Miji mitatu tumekupa viongozi watatu. Meli iko pwani. Makofia tunaazimiwa, yale makofia ya chuma kwamba tujulikane asikari. Utakuta suruali ya asikari, shari la kiraia. Au utakuta shati la kiraia, suruali ya polisi. Tukatiwa ndani ya meli.

Tukafika Pemba. Tumefika Pemba saa ngapi? Saa saba ya usiku. Lakini bahati mazungumzo tumewakuta watu maalumu wanatungoja. Tumewakuta watu wanasema hao watu wanokuja wasikae katika mji hapa. Wapelekwe wapi? Kigomasha! Mnarani, msituni, mpaka amri ije kutoka Zanzibar ya kuingia ndani ya mji. Kama mizigo bwana, valantia wamekusanywa pale chakula kinapikwa Wete tunapelekewa kule tuliko. Nadhani kama sikosei, tuko watu wa ngapi? Hamsini. Tukaaga. Kufika kule Mzee Anthony akagawa. Gora Kombo, Wete. Isa Kibwana, Chake Chake, Feruzi Kayanga, Mkoani. Gari tumechukuwa gari za wapi? Gari za publiki. Gari za njia. Lakini kuna watu special wanojuwa kitu kile kinafanyika vipi. Wale ndo wapokezi wenyewe na wale ndo wenye kutafuta gari hizo. Mimi siwajuwi. Wewe ingia gari hii dereva yumo, wewe ingia gari hii dereva yumo.

Tukaondoka tukafuata saa yetu ya Zanzibar kwamba mimi jukumu langu naikamata Madungu. Gora Kombo jukumu lake anaikamata Wete. Polisi tu. Feruzi jukumu lake anaikamata Mkoani. Lakini saa yetu iwe hii, kama ilivokuwa Unguja. Kiongozi wetu kaipanga safari ile ile na saa ile ile. Bwana we, saa tisa ya usiku tufanye kazi hiyo. Wale jamaa wasiopenda mabadiliko ya nchi washaanza kunongona mle kwenye vituo va polisi. “Leo mtakuja kamatwa hapa. Jana jeshi limekuja. Liko Kigomasha msituni! Miadi yao leo. Kula boma litakamatwa leo.” Polisi wamekaa standby. Pale Chake Chake ndo alipo Inspekta Mkuu akiitwa Harry, Inspekta Harry, Banyani. Mkorofi kafiri huyo! Basi tumetoka kama kawaida, saa ile tunajuwa saa yetu. Wale wanapiga hodi polisi, wale wanapiga hodi polisi. Hakuna zogo. Hodi, karibu. Bwana wewe, silaha zote tunazitaka hapa. Kwa vile wale polisi walivokuwa washapata ile fununu kwamba hiki kitu kipo tutakuja uliwa, wenyewe wamezileta. Hata ukaidi hakuna. Anatokea Inspekta mmoja huyo nlokwambia anatoka Kibirinzi. Moto mkali anakuja, kuja kuihami polisi. Sisi tuko Chake Chake hasa pana jumba moja linaitwa la maaskari ndo jumba moja lilikuwa kubwa la tajiri mkubwa wa karafuu. Pale ndo kambi yetu sie watu wa Chake Chake. Kuna jamaa mmoja anatwambia “jamani eee, huyo Inspekta anakuja na ana hatari na ana bunduki mfukoni mwake.” Kulikuwa kijana mmoja nilikuwa namwita mpaka leo “Humudi” lakini siye Humudi aliemuuwa Mzee [Karume]. Humudi mwengine. Basi ile anafika pale kakuta watu wamesimama pale. Yule Banyani akashuka pale na bastola yake “nini, nini hapa.” Aaah! Hakuwahi hata kupiga alishtukia tu anaanguka. Pemba nzima wamekufa watu wawili tu.

Jicho langu ukilitaka la Unguja nadhani nilikwisha kupa kitu. Unguja kulikuwa wako viongozi. Mfaranyaki Zanzibar, Kaujore Zanzibar, Yusuf Himidi Zanzibar, Sefu Bakari Zanzibar, Natepe Zanzibar, Idi Bavuai Zanzibar, Ramadhani Haji, Washoto, Rajabu Kheri, Zanzibar. Katika vituo viwili, mgawanyiko ulogawanyika kutoka Chumbuni. Kikundi kinokwenda Bomani kinaongozwa na Yusuf Himidi akisaidiwa na Idi Bavuai akisaidiwa na Saidi Washoto. Kikundi kilokwenda Mtoni kikiongozwa na mzee Kaujore, Mfaranyaki, Juma Maneno, na wengine wadogo wadogo kama sie. Lakini uingiaji katika boma la Mtoni kaingia Mzee Kaujore na Isa Kibwana. Hao ndo watu wa kwanza kuingia kwenye nyumba hiyo. Viongozi wengine wako watatu pale lakini wamezuwia kundi la watu lisije likaingia ndani kabla hatujafanikisha lile lengo lilokuwa mle. Bora watolewe watu kama wanosema hawa wanatolewa muhanga. Sisi ndo tuliyojitolea muhanga tupate zile silaha ziliopo pale kwa sababu picha tushapata.

Picha ile ya kwenda mashamba haina kiongozi. Mimi nakaa Donge, kuna Wadonge wengi wanankera au kuna Wamanga fulanifulani wanankera sasa nimeshapata silaha mimi nakwenda Donge. Nikifika siwasalimu, mimi nawauwa wale. La mashamba halina kiongozi. Ni mripuko tu. Maana utamsikia mtu hasa atakuona na silaha “mahala fulani pana Wamanga bwana pale wamekaa kitako.” Unakwenda. Ukifika huulizi. Kwamba wale basi. Kwa mashamba Komredi hakuingia. Manake shabaha yetu sisi, tulipomaliza Malindi tukatawanyika. Watu wa mashamba tukarudi kwetu mashamba. Mimi kwa safari ya Pemba nilikujachukuliwa Mkokotoni lakini tumo kwenye kazi hiyo hiyo. “Hapa walikuwa watatu wakitukera hapa. Tunajuwa bonde la Mnyimbi hapa tukilimalima si Mmanga fulani akitufanyia.” Ah! Mnajuwa nyie, wamo wamejifungia ndani humo. Leteni petroli. Piga dirisha rusha ndani. Piga, tupa bomu, buuu! Mabomu ya chupa za petroli. Hii kazi ilifanyika. Haina kiongozi. Mtu akikwambia ina kiongozi, aa. Hivo ndo ndivo ilivo. Wamanga waliuliwa lakini wenyewe wahusika wale hawakuuliwa. Wengi wao walihifadhiwa kwa sauti ya mwenyewe Mzee Karume, kwamba midam mtu ameshafika miguuni kwangu hamna amri. Kazi yenu mgeifanya huko huko lakini hapa basi.

Idadi ya watu waliouliwa hasa kimapinduzi, ningekupa hasa waliouliwa kimapinduzi ntakosea. Ntakupa watu walouliwa kwa njaa. Kwa sababu kuna watu wameuwana wenyewe kwa wenyewe. Sehemu ya kwanza pale Mlandege kituo cha mafuta. Wamekufa watu wengi saana. Kwa nini? Kwa kutaka mle ndani mna pesa. Unaona bwana. Halafu tukatoka pale tunakwenda duka la Malindi, duka la ubavuni pale, watu wanatafuta ngawira. Wamekufa watu wengi sana. Utazunguka utakwenda zako Darajani, ukifika Darajani utamkuta mtu kaanguka na gunia limemlalia. Huyo alikusudia kupora gunia anataka kwenda nalo kwao akapigwa risasi. Hii ilikuwa kubwa kuliko ile siku yenyewe ya mapinduzi. Kwenye yale mapinduzi yenyewe yakuingia ndani ya maboma hata watu waliouliwa kumi hawakufika. Ukizungumza sana kifo zaidi kimekwenda mashamba kuliko mjini. Kwa sababu kule mashamba wale watu walikuwa na vitu vao viwili. Kwanza, tunasema mkono wa mzee Karume ulikuwa unalia kuuwa watu kwa sababu wakingolewa vyakula vyao. Sasa kile kisasi cha kungowa chakula na kuzuwiliwa visima kuteka maji ndo wakaanza kuuliwa Wamanga wa mashamba.4 Wewe kama hukuambatana na Mmanga yoyote shamba au mjini huli. Kuna kitu ilikuwa nguvu iko kwa Wamanga.

Sasa suala lile watu wanaojuwa historia kwamba hii si nchi ya Wamanga. Hii nchi ya Waefrika. Kwanini hawa wanazidi kutuonea sie? Hii ukitizama wanojuwa historia ndo asili ya kuja mapinduzi haya. Mmanga umeletwa weye kuja kumuondowa Mreno sisi wengine tulikuwa tuko nje bado huko.5 Lakini wenyewe wanajuwa kuwa Mmanga kaletwa kuwakombowa Waswahili hapa kutoka kwa Mreno halafu akageuka kuwa Mmanga.

Ilitakiwa iwe anolizungumza Mswahili Mwarabu alikubali midamu ni la uhakika na analolizungumza Mwarabu Mswahili alikubali midam ni la uhakika. Mambo ya mazogomazogo, ya mdomomdomo, ndo ya kukataliwa. Na waliku-weko Waarabu wa namna hiyo ambao hawakuguswa na tukawekwa sisi tunayalinda magari na mali zao. Manake walikuwa hawamo kwenye mambo ya vyama na mdomo mdomo. Vyama hawataki na mambo ya maneno maneno haya ya kisiasa walikuwa hawayataki.

Komredi alikuwa hayumo. Kachupia. Na kuchupia kwao kwa kujipendekeza. Ali Sultani huyu huwa anawaambia CUF “Hata mkifanya vipi, tulishindwa sisi mtakuja kuwaweza nyinyi hawa?” Ali Sultani alianza zamani yule kujitowa kwenye kundi la Waarabu. Yule kajitowa mapema sana. Mwenyewe alikuwa ana mawazo anasema “karne inokuja Mswahili atajitawala, si karne ya Mwarabu tena, kwa hivo mimi somo naanza kujitowa nakwenda Uswahilini.6 Kajitowa mapema bwana. Kabisaa. Babu alikuwa mwanasiasa mkubwa sana na kwa kupendelea kuwa kuna kitu anataka. Alomgamua Babu ni hayati Saidi Idi Bavuai ndo akamwendea hayati Karume kwamba kila ukikaa umtizame mtu huyu. Yule mtu bwana alikuwa kama tukizungumza sana, ana kitu kinamjia, na kikimjia ndicho. Usisikie kwamba kuna watu wamenyongwa, kuna watu Karume kawauwa, kuna watu kawafanyaje. Hata. Nia zao na nyoyo zao zilivyo kwa sababu wengi wao walikuwa hawampendi yule bwana. Wengi walikuwa hawampendi mzee Karume kwa sababu mzee Karume alikuwa na uamuzi wa uhakika. Hakumchukia mtu. Karume alikuwa kula mtu wake lakini tukaanza kubaguana.

Sasa wale wanojidai kwamba wao wazaliwa mara tatu mpaka mara nne Zanzibar, wale walikuwa ni Wazanzibari wenyewe. Sasa sisi tulozaliwa mara moja Zanzibar watu wa bara. Hatufai kukaa hapa. Suala hilo likaanza kuingia hapa. Mpaka sasa hivi hilo suala liko.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: