Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!

Icon

Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia

Mlango wa Kumi na Tano: Fikra za Kuunda Shirikisho la Nchi za Afrika Mashariki

Oscar Kambona alifafanuwa kuwa fikra ya Shirikisho la Afrika Mashariki linalotawaliwa na Tanzania sio fikra ya Nyerere bali ni fikra ya Muingereza na ililengwa kuwadhibiti Mau Mau wa Kenya. Ilipokuwa Kenya si tishio tena kwa maslahi ya Magharibi, anahoji Kambona, fikra ya Shirikisho ikatupiliwa mbali.

 

Sheikh Ali Muhsin

Hizi fikra za kutaka kufanya Shirikisho la Afrika ya Mashariki hazikuanza leo. Kwa hakika tokea zamani Afrika Mashariki ilikuwa kitu kimoja. Hata pale ilipokuwa watawala ni maimamu wa Omani waliowatangulia Wafalme wa ukoo wa sasa, Afrika Mashariki ilikuwa ni moja. Lakini aliyeifanya khasa kuwa ni moja ni Sayyid Said bin Sultan, wa ukoo huu unaotawala hivi sasa Oman.

Seyyid Said bin Sultan ndie aliyekuja, kwa kutumia lugha ya kizungu—kui “consolidate the whole of East Africa” [kuileta pamoja Afrika Mashariki yote]. Na akafanya makao yake makuu Zanzibar na Unguja ndio ikawa makao yake makuu. Akayahamisha Maskati akayaleta Unguja, na mwenyewe akawa anakwenda huku na huku (mara Maskati mara Zanzibar) na mwisho wake akafia Zanzibar. Japo kama alizaliwa Omani, lakini alifia Zanzibar.

Nchi zote za Afrika ya Mashariki zilikuwa moja na kitu kimoja. Watu wakiendeana, wakifanya biashara na kila kitu kwa pamoja na kwa maelewano. Ni Wazungu, walipoingia na kufanya kinyanganyiro, kama ilivyoelezewa katika kitabu cha bwana Issa Nasser Al-Ismaily [Kinyang’anyiro na Utumwa] baada ya kukutana huko ulaya na kugawana Afrika yote kwa kuifanya kinyang’anyiro—“The Scramble of Africa”.

Kabla ya kinyang’anyiro hicho, katika nchi zote hizi ilikuwa hakuna mambo ya Kenya, Tanganyika, Uganda, wala Zanzibar kuwa mbalimbali. Zilikuwa pamoja mpaka Kongo—zote zilikuwa nchi moja. Baada ya kuingia ukoloni wa wazungu kukaanzishwa majina mapya. Tanganyika akaichukua Jerumani, na Rwanda na Burundi na Kongo wakazichukuwa Belgium, Kenya akaichukuwa Mngereza, Uganda ikafanywa Mahamia ya Mngereza, na halafu yake hata hiyo Zanzibar yenyewe ambayo ilibakia visiwa viwili tu vya Unguja na Pemba na Mwambao wa Kenya, lakini hata hivyo, mwisho wake vilichukuliwa na Waingereza katika mwaka 1890. Hivyo basi Afrika ya Mashariki kuwa nchi moja ndio maumbile yake na ndio asili yenyewe. Kugawanyika kwake ni mamboleo tu yaliyoletwa na wakoloni. Kwa hivyo hizi fikra za kutaka kufanya Shirikisho la Afrika ya Mashariki ni kujaribu kurejea kwenye uasili na pia hazikuanza leo na jana kama tutavyoona.

Nakumbuka, kama sikosei, walialikwa katika mwaka 1957, viongozi wa siasa wa Kiafrika na Kwame Nkrumah aliyekuwa Rais wa Ghana baada ya Ghana kupata uhuru wake kwa mwaka wa pili yake. Alitualika viongozi wote kutoka katika nchi zilizokuwa zinatawaliwa na wakoloni wakati huo. Katika hao walioalikwa baadhi yetu tulikuwa viongozi wa vyama vya kisiasa na wengine wa vyama vya Trade Union [wafanyakazi] na Cooperatives [vyama va ushirika] za nchi mbalimbali. Alitualika kusheherekea mwaka wa kwanza wa kupata uhuru wa Ghana. Mimi ndie niliealikwa kutoka Zanzibar. Kule nikawakuta wenzangu wengine kutoka Afrika Mashariki kama vile Julius Nyerere kutoka Tanganyika, Joseph Murumbi na Peter Kaunange kutoka Kenya, na Mudira kutoka Uganda.

Nkrumah, baada ya kwisha zile sherehe alituita nyumbani kwake ambako vilevile tulimkutia George Padmore ambaye alikuwa mshauri wake juu ya mambo ya Afrika. George Padmore ni mtu mweusi kutoka Trinidad, West Indies. Ni mtu aliekuwa mjuzi kwelikweli wa nchi za Kiafrika zilokuwa chini ya ukoloni. Yeye alikuwa amehamishwa kutoka nchi yake iliyokuwa inatawaliwa na Muingereza na akawa hana ruhusa ya kwenda nchi nyingine; na akawa anakaa England. Ilipopata uhuru wake Ghana, Nkrumah ambaye alikuwa ni rafiki yake akamleta Ghana na kumfanya mshauri wake. Wote wawili, Nkrumah na Padmore, walitoa shauri kuwa ufanywe mkutano wa viongozi wa nchi za Afrika na wakutane Ghana watengeneze mipango ya namna ya Ki-Ghandi iliyokuwa ikiitwa “Passive Resistance” na ambayo aliifanya yeye [Mahatma] Ghandi kule India katika kupigana na kupambana na ukoloni kwa njia ya kisalama.1 Tufanye mipango hiyo ili kuokoa nchi zote za Kiafrika kutoka na ukoloni.

Mazungumzo haya yalikuwa katika mwezi wa March na mkutano huo wa kufanya mipango hiyo ya ukombozi wa kutoka na ukoloni ulikuwa ufanywe katika mwezi wa December. Mimi niliwapa shauri wenzangu wa Afrika Mashariki kwamba kabla ya sisi kwenda Ghana sisi wenyewe kwanza tutengeneze kukutana nyumbani Afrika ya Mashariki ili tuwe shauri moja na tujuwane na tufahamiane kabla ya kurejea Ghana. Wenzangu wote waliwafiki sana shauri hiyo na hapo tena nikatoa shauri kwamba niwaalike Unguja [Zanzibar] kwa ajili ya mkutano huo. Nikawaarifu ya kwamba nilikuwa safarini nakwenda Egypt, lakini wenzangu huko Zanzibar watatengeneza kila matarayisho yanayohitajika kwa ajili ya mkutano huo. Haitadhurisha kitu mimi mmoja ikiwa sipo.

Safari yangu ya Egypt ilinichukua miezi mingi kukaa huko. Na kwa kutokana na taakhira hiyo huku nyuma Nyerere akauteka nyara ule mkutano. Badala ya kufanywa Unguja, Zanzibar, akaufanya Mwanza, Tanganyika, na hapo ikapatikana sura katika ulimwengu kuwa Nyerere ndie alieanzisha kuundwa kwa PAFMECA. Lakini ukweli ulikuwa ni Zanzibar ndio iliyoanzisha fikra ile ya ule mkutano wa mashirikiano na ulikuwa ufanywe Zanzibar.

Mimi kule Misri nilichelewa sana kupata fursa ya kuonana na Gamal Abdel Nasser aliyekuwa Rais wa Misri. Nilipata taabu sana ya kupata fursa ya kuonana naye. Nafikiri ilipita kiasi ya miezi mine nimo kusubiri tu kupata miadi ya kumuona, lakini nilipopata kumuona njia zote zilifunguka kwa upesi na wepesi. Wakati niko chumba cha wageni nangojea zamu yangu ya kuingia ofisini mwake kumuona, seketeri wake aliniambia unazo dakika kumi na tano tu za kuonana nae kwa sababu memba wa Baraza la Mawaziri wanangojea kufanya mkutano nae. Na ni kweli—maana nilipokua naingia kuonana nae nimewaona wako katika chumba kingine wamekaa. Ilipofika dakika kumi na tano alikuja yule seketeri kumkumbusha Abdel Nasser kuwa wakati wake umefika wa kuonana na Mawaziri ambao walikuwa wakingojea. Gamal Abdel Nasser akamjibu awambie wangojee zaidi. Watafurahi kuyasikia haya anayoyasema ndugu yako hapa.

Mazungumzo yetu yalimchukuwa mbali kabisa katika mawazo mpaka nikamuona machozi yanataka kumtoka. Kabla ya kumalizika mkutano akanambia atanipa scholarship [nafasi za masomo] kwa vile nimekwenda kuwaombea watoto wetu fursa ya masomo. Sikwendea jambo jengine lolote. Zanzibar kulikuwa hakuna nafasi za kutosha za masomo ya juu. Secondary schools zenyewe zilikuwa hazitoshi Zanzibar na baada ya masomo ya secondary school kulikuwa hakuna masomo ya juu zaidi Zanzibar katika wakati ule. Tulikuwa tukiokoteza misaada ya udohoudoho kutoka nchi zingine. Pale pale akanambia, atanipa scholarship arubaini za wanafunzi kwenda kusoma Egypt na watawalipia gharama zote, chakula, nguo na gharama zinginezo. Watasoma mpaka wachoke wenyewe. Vilevile akanambia atanipa idadi ninayotaka ya walimu wa kwenda kusomesha Zanzibar na pia watawalipa wao mishahara yao lakini sisi tuwape makaazi—yaani nyumba za kukaa. Kwa hivyo alinitaka nikashauriane na wenzangu jinsi ya kutayarisha nyumba za walimu. Ama kuhusu zile scholarship arubaini za wanafunzi kwenda kusoma Egypt, pale pale mimi nilimwambia Abdel Nasser kama sisi Afrika Mashariki tuna desturi ya kufanya mambo yetu pamoja, pamoja na wenzangu kwa hivyo, nakuomba uniruhusu katika hizi scholarship arubaini, tuwagaie Tanganyika na Kenya. Sikuitaja Uganda kwa vile wao walikwisha kuwa na wanafunzi ishirini na tano tayari wanasoma kule Misri. Jibu lake lilikuwa nimekupa wewe hizi scholarships basi wewe na wenzio fanyeni mnavyotaka. Mazungumzo yetu yote yalituchukuwa dakika sitini, na dakika kumi zingine za kuagana na kupiga picha.

Niliporejea Zanzibar niliwakabidhi scholarships hizo Parents Association [Jumuiya ya Wazazi] wazigawe kama wanavyoona inafaa kwa maslaha ya nchi zetu, Zanzibar, Tanganyika na Kenya. Wakatangaza kutaka watu kutoka Kenya na Tanganyika wanaotaka kusoma. Watu walitaka, lakini kwa kinyume cha chini-kwa-chini alizuka Kenya mtu mmoja aliekuwa akiitwa Francis Khamisi ambaye alikuwa mwanasiasa wa Mombasa, na Nyerere nae kwa upande wake (vilevile chini kwa chini) wakawa wanaziambia serikali zao kwamba hatari sasa imekuja hii. Watu watakwenda Misri na wanafunzi hao watakaporejea watakuwa wanawapendelea Waarabu. Nchi zetu zitachukuliwa na Waarabu. Hivyo basi serikali ya Tanganyika, serikali ya Kenya, za Waingereza, sio za wananchi katika wakati ule, zikatoa marufuku hapana rukhsa kwenda mtu Misri. Zanzibar serikali haikuweza kufanya hivyo kwa sababu ya makhusiano ya asili na asili na Misri. Hawangaliweza kufanya hivyo kwa sababu ya makhusiano ya asili na jadi na Misri, tangu zama za zamani za Uislamu na Al-Azhar walipokuwa watu wanakwenda na kurudi baina ya Zanzibar na Misri, bila ya pingamizi ya aina yoyote.

Baada ya kwenda watoto na kusoma Cairo, ikawa Misri itayari kujenga University [Chuo Kikuu]. Na University tuliotaka sisi kujengwa Zanzibar ilikuwa ni ya Waislamu wa Afrika ya Mashariki na ya Kati.2 Hatukutaka kuifanya kuwa ya Zanzibar tu. Misri ilikuwa tayari kusaidia na pia hata America alikuwa tayari kuchangiya kusaidia Teachers Training katika University hiyohiyo iliokuwa iwe ya wanafunzi wanaume na wanawake. Lakini mara tu baada ya kupata uhuru wetu tukapinduliwa baada ya mwezi mmoja. La kwanza walilolifanya Nyerere na Karume ni kwenda Misri wao wenyewe na kudai kwa Abdel Nasser avunje misaada yote aliotuahidi sisi na si kama aliahidi misaada ile kwa serikali ile tu, bali alikuwa tayari kuitoa hata kwa serikali yao lakini wao hawakutaka kuwa na mahusiano yoyote na Misri. Walilolitaka ni kwamba wanafunzi walioko Cairo warudishwe. Wakati Abdel Nasser akitoa scholarships vilevile akaweka nyumba ya wanafunzi wa East Africa na ndio ikawa sababu ya nyumba ile aliyoitoa kufanywa bweni la kukaa wanafunzi wakaiita “East Africa House”, kwa madhumuni ya kwamba msaada huo wa nyumba utawafaa watu wote wa Afrika ya Mashariki siyo Zanzibar peke yake. Lakini kama walivyotaka Nyerere na Karume, wanafunzi waliokwishakuwa tayari wanakaa katika nyumba ile, wakakamatwa kwa nguvu na kurudishwa makwao na nyumba ile ikafungwa na mpango wote ukafisidika.

Sijui namna gani, Nyerere alikuwa anacheza mchezo huku na huku, bila ya kumtambua. Huku kwa dhahir alipigania kuwepo East African Federation. Tukakutana Dar es Salaam. Wakati huo sisi hatujapata uhuru wetu lakini Tanganyika ilikuwa wapo katika Serikali ya ndani. Basi tukakutana Dar es Salaam. Kutoka Zanzibar nilikuwa mimi na Dr. Baalawy na Attorney General wetu, Australian, Mr. Rumble aliekuwa mshauri wetu wa mambo ya sheria. Na chairman alikuwa Oscar Kambona ambaye siku zile alikuwa bado hajagombana na Nyerere. Yeye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanganyika. Na mshauri wake [Nyerere] ndie alotengeneza kila kitu, George Brown, Mngereza. Sisi tulikuwa tumelikubali lile shirikisho lakini katiba walioitaka wao iwe tuliiona haifai kwa sababu nguvu zote zilikuwa zinampa mtu mmoja au nchi moja na ilikuwa dhahir kwa kuwa itapata Tanganyika na Raisi wake Nyerere. Sisi tulolipinga siyo Shirikisho lakini hilo la nguvu zote kupewa nchi au mtu mmoja. Hili ndilo tulokuwa tunapinga. Zanzibar na Uganda ndio waliokuwa wakipinga. Kenya ikawa wamekaa kimya, wanaachilia tu. Hata, Charles Njonjo aliekuwa Attorney General wa Kenya, alikuwa takriban anasinzia tu, hashughulikii. Na Kenyatta alisema baada yake, sisi hatutaki Shirikisho, hatutaki chochote, tulikuwa tunawahadaa tu.

Nyeyere aliposhindwa kupata ukubwa kwa nafsi yake kwa njia ile alioshauri katika katiba ndio akatumia mabavu. Uganda, alikuwepo Godfrey bin Issa, kama Attorney General na mwengine Kioni alikuwa bin ami yake Obote lakini yeye Muislamu shadid, kakaa pale na translation [tafsiri]ya msahafu (Qur’ani). Wao walikuwa shadid sawasawa na sisi. Walikuwa hawataki nchi moja iwe na nguvu za utawala peke yake kuliko wengine. Lakini baada yake ikaonekana kuwa ndio sisi wapingaji. Sijui kama hii ni moja ya sababu hiyo au sababu nyengine zipo lakini tukajapinduliwa. Serikali yetu ikapindiluwa na wale wapinzani wetu wakatumiwa wakawa ndio serikali mpya ya mapinduzi ambayo ilioachilia kuundwa Tanzania. Na Zanzibar nchi ilokuwa huru na Tanganyika ilokuwa huru zikawa zimekwisha ikaundwa Tanzania.

Sisi tuliosoma Uganda tulipokuwa ndani gerezani Dar es Salaam pale Keko, mimi, na Dr. Baalawy, na Maulidi Mshangama, na Seleman Said, tulisema yoyote atakaetoka hapa gerezani mwanzo ende haraka Uganda akawatahadharishe wao watakuwa wa pili, maana yake inaonekana kwamba sisi hatutakiwi kwa sababu nchi yetu ina mfalme na kwa hiyo ndio imezwe, na wa pili itakuja kuwa Uganda. Hatukuwahi kufunguliwa yoyote katika sisi, mara ikawa Kabaka kule akapinduliwa na Uganda yenyewe ikapinduliwa yote na wafalme wote wakawa si kitu, si chochote si lolote na akasimamishwa Obote.

Kabla ya hii fikra ya kuundwa Shirikisho la East Africa, kulikuwapo na “East African Common Service Organisation”. Nchi zote za East Africa zilikuwa pamoja katika mambo ya kibiashara. Sarafu ni moja, postal service [huduma ya posta] ni moja, isipokuwa Zanzibar ilikuwa haimo bado katika huduma ya posta. Na custom [mizigo] ni moja lakini Unguja [Zanzibar] ilikuwa forodha yake bado haijaingia. Lakini zilobaki mambo mengi ya siha, ya afya, ya research [utafiti], na railway [reli], na aeroplanes [ndege] yalikuwa pamoja. Ilikuwa ndege za East Africa Airways zikenda East Africa kote, hata Zanzibar. Na sarafu, shilingi ya East Africa ilikuwa na nguvu. Shilingi ishirini za East Africa kwa pound moja sterling [ya Kiingereza]. Ghafla, katika mkutano wa Mawaziri wa fedha uliokuwapo Zanzibar, Waziri wa Tanganyika akawaambia wenziwe wa nchi nyengine za Kenya na Uganda na Zanzibar, kwa sababu sisi tunakwenda mwendo wa Kisoshalisti, wa kijamaa (wanavoita wenyewe), na nyinyi mnakwenda kibepari, basi hatuwezi kuwa pamoja kwenye mambo ya sarafu. Sisi tunatoka katika sarafu tuwe na sarafu yetu wenyewe. Walipata mtikiso mkubwa wale Mawaziri wa East Africa. Hawakutarajia yale. Hapa ndipo ilipovunjika East African Currency Board pamoja na kuanguka shilingi ya Tanganyika na khasa ikaanguka zaidi kwa sababu wao ndio waliokuwa maskini zaidi. Wao wanaojigamba kujenga, wakati mwengine wao ndio huwa wavunjaji—mjengaji ndie mvunjaji.

Lakini sasa alhamdulillah inaonekana hapana viongozi wenye tamaa ya ubinafsi ya kutaka kutawala East Africa nzima au Afrika nzima mtu mmoja. Hapana katika East Africa, la Tanganyika, wala Kenya, wala Uganda, wala Zanzibar, mtu wa namna hiyo. Hao walokuwa wenye tamaa hizo wamejifia. Kwa hivyo, tunaweza kufikiri tena upya juu ya muundo wa Shirikisho na mustakbali wake. Mimi na wenzangu wengine vilevile, tunaona kuwa Shirikisho linaweza kuwa na maslaha sana sasa kwa sababu tumeona mifano ya nchi sehemu mbili kubwa zilofanya mambo ya namna ya Shirikisho, na namna ya Muungano. Na moja ni huu wa Ghuba [Gulf] nchi za Khaleej zimekusanyika pamoja, zimefanya umoja wao na wamekaa kwa uzuri. Europe, nchi kadhaa wa kadhaa na zinakuwa kila siku, na mamilioni ya watu wamekusanyika pamoja vilevile. Wameweza kufanya namna ya Shirikisho. Na ziko nyengine. Bara Hindi [India] tokea hapo mwanzoni ni Shirikisho kwa hakika. States zao kadhaa wa kadhaa zina serikali zake zimo ndani ya muungano wa India. America ni mfano vilevile wa Shirikisho. Basi tunaweza kuona mifano hiyo ya watu wakakusanyika wakasikilizana East Africa. Kenya na Uganda, na Tanganyika na Zanzibar (nchi zilizokuwa zimetawaliwa na Wangereza kwa miaka) zikawa moja. Mwendo wao wa Kiingereza na lugha yao ya Kiswahili, imeenea na inaweza kuendelea zaidi. Imeanza pwani ya Afrika ya Mashariki na imeenea, na Tanganyika inaweza kusaidia sana kueneza zaidi uswahili wake. Na jambo moja jingine ambalo Tanganyika imeweza kufanya na inafaa ishukuruwe nikuondoa kutojuwa kusoma, kwa kufundisha kusoma watu wazima. Watu wengi sana sasa Tanganyika wanajuwa kusoma Kiswahili. Hata ukabila katika Tanganyika ni mchache kuliko kwengineko.

Kenya, imeonyesha uhodari wake na uzuri wake wa ujirani mwema. Imeweza kutumia uwezo wake kusuluhisha ugomvi wa Sudan na Somalia. Haujesha kabisa lakini wamo katika kusuluhisha. Wamefanya kazi kubwa sana na wanafaa kushukuriwa. Hawakufanya wao kama alivyofanya Nyerere, watu wa Zanzibar hawapatani basi dawa yake ya kuwafanya wamoja ni kuwaua wengine. Kwa kufanya mapinduzi, na natija ya mapinduzi, ndio Zanzibar imedorora mpaka sasa haina kheri yoyote inayotengenea. Watu wakafukuzwa, wengine wakafungwa. Mimi ndio katika hao tuliofungwa gerezani zaidi ya miaka kumi bila ya kuhukumiwa. Wengi wengine wakauliwa kwa maelfu. Watu wakanyanganywa mali zao. Hapana hukumu, hapana chochote. Lakini Kenya mpaka leo iko serikali na inayo mahakama zenye sheria. Kumiliki mali binafsi (private property) kunaheshimiwa. Vilevile, Uganda, Museveni baada ya kushinda amewaalika Wahindi wale waliofukuzwa na Idi Amin warudi na wakarudishiwa na mali zao. Wafalme walofukuzwa, kina Kabaka, na wafalme wengine wa Uganda, Bunyoro, Toro na Busoga wakarudishwa. Museveni akasema hawa si watu wa siasa. Hawa, ni mila yetu, ni mila yetu asli. Wakae, siasa zimo katika watu watakaochaguliwa katika serikali lakini hawa wafalme ni mila yetu na tuiheshimu. Kwa hivyo wamerejeshwa na heshma zao. Basi kila mmoja inayo jambo la kuleta faida.

Sisi Zanzibar tuna nini cha kuleta? Sisi Zanzibar tunayo faida ikiwa tutapata uhuru wetu kamili na kuingia katika Shirikisho kwa kuwa ni nchi yenye kutambulika. Tukiingia kama ni nchi yenye kutambulika, kama Tanganyika, kama Kenya, kama Uganda, kwanza tutaipa nguvu hiyo Tanganyika yenyewe vilevile. Itakuwa sisi ni wawili badala ya kuwa mmoja, kuliko sisi kuwa ni mkia tu au tumemezwa na Tanganyika. Tunaburutwa tu. Kwanza itakuwa hapana imani ya Shirikisho lenyewe, tutakuwa kila siku tunataka kujitoa. Hivi sasa watu wengi hawataki kuendelea na huu muungano wa Tanzania kwa namna ulivyo kwa kutokana na vituko vya kumezwa na aibu zake. Basi ilioko khasa Zanzibar irejeshewe uhuru wake kwa sababu imepigania uhuru wake mbali na iliupata. Muingereza katoka na Zanzibar ikawa huru na pia ikawa nchi yenye kutambulikana katika Umoja wa Mataifa na ikawa na kiti chake na bendera yake huko. Ijapokuwa uhuru huo ulidumu kwa mwezi mmoja tu kabla ya kupinduliwa, lakini vilevile inajulikana wazi kwamba mapinduzi hayo hayakuwa ya halali na kwamba Zanzibar, kwa dahari na dahari ilikuwa ni nchi huru. Haikupatapo kutawaliwa katika taarikhi yake yote.

Sasa Zanzibar ikiwa kama ni mkia wa Tanzania haitoleta faida yoyote. Lakini ikiwa huru inaweza kuleta faida nyingi na kubwa. Hii ni kwa sababu Zanzibar inayo mahusiano ya asili-na-asili na nchi nyingi nyingine. Inayo mahusiano na Oman, Yemen, Misri, India, Pakistani, Sri Lanka, Indonesia, Iran, na nchi nyingi nyingine. Kwa mahusiano haya ya wema baina ya watu wa Zanzibar na watu wa nchi nyingine; na Zanzibar ikaja ikapata nafasi yake kuingia katika Shirikisho hilo ikiwa kama nchi huru yenye kutambulikana, basi inaweza kuleta faida nyingi na kubwakubwa katika kuineemesha Afrika ya Mashariki kiuchumi na kisiasa na hata ikawa ndio chanzo cha kuleta Shirikisho la Afrika yote kwa kutokana na mahusiano mema ya watu wa Zanzibar na ulimwengu wote kwa jumla. Itakumbukwa kwamba katika miaka arubaini hii ya tangu mapinduzi Wazanzibari wengi wamezagaa ulimwenguni. Na wengi wamesoma na wana ilimu za juu mbali ya wale ambao wamekwisha tajirika. Wapo vilevile wenye experience [ujuzi] za kazi kutoka nchi mbalimbali za ulimwengu. Wote hawa watakuwa tayari kuchangia katika hilo Shirikisho la Afrika ya Mashariki kama tu itaonekana ipo insafu na itatenda haki kwa Zanzibar.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: