Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!

Icon

Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia

Mlango wa Kumi na Tatu: Misha Finsilber na Mapinduzi

Hakuna aliyetokwa na machozi Israel kwa kuondoka kwa Sultan [wa Zanzibar]. Ngome nyengine ya Kiarabu ya Afrika imeanguka, na dola nyengine imeufungulia ushawishi Israel. Dave Kimche “alisadifia” kuwepo Zanzibar siku ya mapinduzi. Kuwepo kwake kuliiongezea sifa Mossad kwa wanadiplomasia wa nchi za Magharaibi na wachambuzi wa kiusalama, kuwa [Israel] ina uwezo wa kufanya jambo lolote. —Every Spy a Prince

 

Mzee Ahmed Ali Ghulam Hussein, maarufu “Shebe”

Nimejuwana naye Misha Finsilber katika mwaka 1955, 1956.1 Nikimfikiria kama Girigigirigi. Tukikutana Zanzibar Hotel na alikuweko Girigi mmoja akiitwa Kilosa, na kwa vile alikuwa sana na Kilosa nikamhisi na yeye Girigi vile vile. 1958 aliponiajiri ndo nlijuwa kama yeye ni Myahudi. Yeye amechanganya, nafikiri German Jew. Baba yake ni Mjerumani. Kazi yake yeye ni bingwa wa kupasua mabomu. Kaanza wakati wanatengeneza barabara ya Njombe sijui, Mbeya kule, yeye kazi yake ilikuwa kwenda kuvunja milima ile. Kabla hakuja Zanzibar. Hapa kaja baada miaka chungu nzima keshakaa Tanganyika. Miaka mingi kafanya kazi kubwa.

Misha ni mtu mfupi, mpana, ana kifua hivi. Sasa hivi anaweza kufika hata [miaka] thamanini na. Mara ya mwisho nilisikia alianguka chooni kavunjika bega sijui na mguu, akaja kuchukuliwa hapa. Daktari katoka huko, Israel, amekuja kumtowa [hospitali ya] Aga Khan, wamempeleka Israel. Anaonyesha mtu muhimu kweli. Sasa huko kakaa muda mrefu sana. Mimi nimekaa pale miezi miwili na nikiwaona watoto wa ndugu yake wakinambia, yuko huko anatibiwa. Hakuwa mtu wa utaniutani. Mazungumzo yake hayana mzaha. Mpaka kaondoka Zanzibar biashara aliyobaki nayo ni uchimbaji wa maadini hii. Yuko Arusha kwenye madini. Hata mara ya mwisho mimi nimefanya kazi kwake kaja nchukuwa Tanga tukenda kwenye migodi huko, nisimamie zile machine za compressor. Si wanachimba kwa manyundo yale. Kulikuwa na compressor tatu kwenye migodi mbalimbali. Sisi tulikuwa sehemu za Mito Mingi, kutoka Tanga njia ya kuendea Mombasa lakini ndani kwenye milimamilima kule. Anakubali tabu. Manake yakhe kwenda kukaa wiki mbili ndani ya hema? Mashida shida yalikuwa hayamshughulishi. Hiyo ya huko mie kanambia “sikiliza Shebe. Sisi tunakwenda porini bwana. Porini tunakaa wiki mbili. Weekend ya baada ya wiki mbili ndo tunakuja mjini.” Ndani ya hema. Pahala hapana mfereji wa mvua, hapana nini. Anajuwa kutafuta pesa bwana.

Alikuwa maarufu kwa kuwapa watu vyombo va kuvulia. Mashua ni yake, bunduki ni zake, masks na nini na kila kitu, kwa wale wanojuwa kuogelea. Nini yeye akitaka, mumpelekee kamba, lakini samaki uzeni wenyewe. Akiwasafirisha nje. Hapa Unguja wakati ule hakuna aliyekuwa hamjui Misha. Kila penye bahari basi yule mtu anajulikana. Unguja tu. Hii habari ya kuvuwa huwezi kuwa na vyombo kila pahala namna hiyo. Kwa sababu uvuvi wa kuzamia kuna siku za kusi, huwezi kuvua bahari za kusini, bahari inachafuka, vumbi tupu. Siku za kusi watu wa kusini wanakwenda kupiga dago kule kulotulia. Akijuwana sana na mzee moja wa Nungwi akiitwa Mzee Haji. Huyu alikuwa mtu mzima sana na Misha alikuwa yupo karibu nae sana. Alikuwa hawezi kazi nyingine yoyote kwa sababu mkono wake mmoja umelemaa, na Nungwi alikuwa ni mtu akihishimika sana. Yeye ndo nkimuona akijakija sana pale. Na Uroa rafiki yake alikuwa Muhsin. Alikuwa mzamiaji mzuri. Muhsin alikuwa ndo kiongozi wa wavuvi wa kuzamia kwa upande wa Uroa. Kama Fumba si pahala palikuwa pakipatakana vitu hivo sana. Inatokea tu. Khasa mavuvi yanakuwa Kizimkazi, Uroa, Nungwi ndo khasa, Mkokotoni. Kaskazini yote kule ndo kwenye bahari kubwa kuliko huku kusini. Na biashara yake nyengine ilikuwa chokaa ambayo akisafirisha kupeleka Dar es Salaam. Kila baada ya siku moja akipeleka tani kumi na moja za chokaa Dar es Salaam.

Kulikuwa na boti moja hapa ikiitwa “Cheetah” ambayo kabla ya mie kuwa na yeye, mimi nilikuwa engineer mle ndani. Aliikodi yeye kuwa usiku inaondoka hapa na tani kumi inafika kule, wanapata mzigo, wakirudi hapa, hapa hapakii kitu chengine ila chokaa na passenger [abiria]. Pale Dar es Salaam kulikuwa na Mhindi mmoja ana duka la zana, Ithnaasher nafikiri yule, yule ndo anaichukuwa kwa wingi. Hapa Misha alijenga ile tanuri ya chokaa mbali anonunuwa kutoka kwa wenyeji. Chokaa yake yeye inatoka saa ishirini na nne. Inawaka tu moja kwa moja miezi mitatu. Alikuwa na tanuri hapa, Dunga. Mnatia vifuu, mnatia mawe, inawaka tu, na huku chini ikishakuwa jivu, inadondoka mnatowa. Mwaka 1999 walikuja hapa Zanzibar wachomaji wa kienyeji wa chokaa kutoka Ulaya walifanya semina hapa kuwaeleza wachomaji chokaa, namna nzuri ya kuchoma chokaa kwa kiln [tanuri]. Na katika kutembezwa walitembezwa kuwa hapa hichi si kitu kipya. Tukenda kule Dunga. Majenzi ndo walofanya semina ile na Ahmed Sheikh ndo alokuwa Mkurugenzi wa Majenzi wakati ule.

Katika viongozi wa Afro-Shirazi waliokuwa wakija kwenye ofisi ya Misha, ya Zanzibar Sea Products, pale karibu na Bwawani, walikuwa marehemu Mzee Thabit Kombo na Mzee Mtoro Rehani [Kingo]. Kwanza wakija milango inakuwa imefungwa, ofisini kwake Misha kuna air conditioner, kuna vioo, mapazia yanafungwa. Kwa hiyo hata ile kumuona mtu mdomo kuwa anasema humuoni. Mara nyingi wakija walikuwa wanakuja wao. Niliwahi kumwambia Misha, kama kighadhabu tu mara moja, kwenye uchaguzi wa pili wakaja kufanya mashirikiano baina ya ZNP na ZPPP. Usiku wa kuamkia kesho uchaguzi, mimi na Misha siku zote ilikuwa kwenye saa mbili ya usiku lazima tunakutana Zanzibar Hotel. Tunakaa palee, kwa kungojea abiria wa hiyo boti nilioifanya, glass boat, na wakati ule kuna kituo cha Kimarekani Tunguu, Project Mercury. Sasa tulikuwa na bodi letu pale Zanzibar Hotel. Mtu anotaka kwenda anaandika jina lake pale. Sie tunaandika time, boti itaondoka saa fulani, maji yanapokupwa, tunawatembeza kwenye miamba wapate kuona samaki, majani, halafu tunawatoza pesa. Sasa ikawa siku zote lazim mie nende Zanzibar Hotel kujuwa kesho tuna abiria wangapi, na saa ngapi tutaondoka. Halafu ananrudisha nyumbani. Sasa kesho sie tunaamkia uchaguzi amenleta nyumbani Kikwajuni. Basi tuko juu pale kabla ya kushuka akataka fikra yangu mimi, akanambia “Shebe unaonaje huu uchaguzi wa kesho.” Nkamwambia “hakuna wasiwasi wowote ZNP watashinda.” “Unafikiri hivo?” Nkamwambia “nna uhakika.” “Kwanini?” Nkamwambia “kwa sababu chama kile wamejipanga vizuri, watu wamefahamu nini wanaambiwa. Kwa hiyo nna imani na watu wengi wanojuwa mambo hayo wana confidence kama hawa watashinda.” Akanambia “lakini unajuwa kama wengi wa watu walioko hapa ni Waafrika.” Nkamwambia “hata hivyo.” “Unajuwa kuwa nchi zote za Kiafrika zinawasaidia hawa Afro-Shirazi?” Nkamwambia “nnajuwa, wanawasaidia kimapesa. Hawatoweza kuwasaidia kwa kupiga kura. Watawasaidia fedha, wao wenyewe wanagombana kwa mapesa. Kwa hiyo hawatashinda. Na nyie Mayahudi mnawasaidia pia.” Alikasirika sana. Inafika wiki hatujasema mie na yeye, na ndo tunafanya kazi. Siku ya pili yake ile baada ya kutoka matokeo ya uchaguzi, na wakashinda ZNP-ZPPP, ah!, alishindwa hata kuntizama macho hivi. Kwa kuwa mie nilimwambia kabla aliona haya hata ile kuntizama. Na hasa ile kumwambia, najuwa kuwa nchi zote za Kiafrika zinawasaidia pamoja na nyie Mayahudi, Israel. Alinyamaza kimya. Na ndo ikawa mwisho wa hadithi nkashuka ndani ya gari.

Kuhusu safari ya kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar baada ya mapinduzi, mimi nilijuwa asubuhi ya Jumapili. Kwa sababu Jumaamosi usiku nilikuwa Anatoglo na Director-General wa Tanganyika Broadcasting Corporation (TBC), Mikimdowe. Alikuwa kamualika lecturer mmoja wa chuo kikuu ende kula chakula cha mchana kwake. Sasa tulivokutana usiku mimi na rafki yangu Mustafa akasema napenda muje muwe na mimi, nna mgeni na hivi, mtakuja kuzungumza nyumbani. Mimi Misha aliniweka Excellssier Hotel, pale Clock Tower. Asubuhi hatuna mpango wa kwenda baharini, Jumapili manake. Kwa hiyo Mustafa rafki yangu akanambia “basi mie ntakupitia hotelini kwako asubuhi kama saa nne, Jumapili.” Basi kaja Mustafa Jumapili, “unayo habari ya Unguja?” Nkamwambia “sina.” Tumetoka moja kwa moja mpaka kule kwa Mikimdowe. Tunafika anasema “unayo habari ya kwenu weye?” Kuna mapinduzi na Sultani ameshakimbia…Mimi nimetaka kwenda Unguja sasa hivi lakini hakuna ruhusa, hakuna chombo kwenda…wala…yupo pale Director-General wa TBC, na makanda yake pale. Anasema mimi nimeanza kuskiliza BBC [British Broadcasting Corporation]. Basi tukashinda pale, manyimbo hayoo, mpaka mchana ndo inaanza kutangazwa, mapinduzi yamefanikiwa, anatakiwa Mzee Abedi Amani Karume popote alipo aje, na hivi. Basi, tumeondoka kama saa nane pale. Mustafa kanrudisha hotelini kwangu, nkasikia “kaja hapa yule tajiri wako anakutafuta, na anasema ukija usiondoke.” Nkaona sawa, basi akija mie nipo hapa, hoteli ya pili. Akaja kama kwenye saa moja hivi ya usiku, Jumaapili. “Una habari Shebe?” Eh, mie nimesikia kule kwa Mikimdowe, nilialikwa chakula mchana na yeye ndo kanambia mapinduzi, na hivi… Akanambia “huyu Abdul Faraji kantafuta sana, mpaka kaja kaniona nimechelewa anataka tuwapeleke watu hawa Unguja.” Nikamwambia “sawa.” Haya twende chumbani kwako. Nkenda chumbani kwangu, nataka kuchukwa begi ananambia “ewe bwana unakwenda wapi? Hili begi unataka kwenda tembea huko? Vaa hivohivo.” Basi nikachukuwa nguo nzito, tukatoka pale usiku moja kwa moja mpaka huko tulokoweka boti Kunduchi.

Kabla ya kufika Kunduchi kwanza, akasema “twende tukachukuwe mafuta Agip Petrol Station pale new post office [posta mpya] pale.” Tumekwenda pale tukachukuwa drum moja la petroli, na geloni kama nne za mafuta, zikapakiwa kwenye Land Rover, ikawa tunasubiri pale. Misha akitumia Land Rover ya “Mwananchi.” Abdul Faraji wakati huo alikuwa ndo General Manager wa “Mwananchi Trading” ya TANU. Basi tumeondoka pale tumekwenda zetu sisi mpaka Kunduchi. Zikaja gari kama tatu, Mercedes, lakini ilivokuwa usiku tena, huoni kitu, hujui nani, wala vipi. Hizo Mercedes zilikuja Kunduchi. Sie tunatowa engine ndani ya store ili tupeleke pwani, basi nkaona hivo, lakini sikujuwa nani. Akanambia, sasa tunakwenda Unguja, na tunakwenda Kizimkazi. Nkamwambia sawa. Mie najuwa compass ya kwenda Kizimkazi. Ni masaa mawili tu mpaka Kizimkazi. Tukaingia ndani ya boti kama saa sita ya usiku hivi, sijuwi nani aliomo ndani ya boti wakati ule, mpaka alfajiri tena. Tungefika usiku lakini engine moja iliharibika njiani, ikawa tunakwenda na moja.2

Tumeingia alfajiri Kizimkazi, kama kwenye saa kumi na mbili alfajiri hivi. Kunaanza kupambazuka tena ndo nakuja kuona nani na nani wamo kwenye boti. Kwa sauti nlikuwa najuwa kama Babu nlikuwa nikimsikia sauti yake alipokuwa akizungumza. Na Colonel Ali Mahfudh. Hao ni watu ambao mara nyingi tunakuwa pamoja kwenye kunywa, kwenye nini, kwa hiyo hawanpotei. Wengine sikuwaelewa lakini nlikuwa nnajuwa hao wamo ndani ya boti. Na ndivo ilivokuwa. Kulipopambazuka ndo nimekuja kujuwa alikuweko Mzee Karume, alikuweko Abdalla Kassim Hanga, Babu, Ali Mahfoudh, Ali “Nyau,” Jimmy Ringo, na watu wa usalama wawili wa Dar es Salaam, nimewasahau majina yao kwa walikuwa si watu close na mie, mmoja anaitwa “Makenzi,” kwa jina la kiutani, wa pili simjui kabisa jina lake, si la kimasihara wala hivi, kisura tu nikimjuwa. Fuko alikuweko. Jimmy Ringo, Fuko, na Ali Nyau ni watu wa hapa, pamoja na hao nlokwambia.

Ile boti ilikuwa futi thalathini na mbili, ilikuwa life boat ya katika meli. Imetupwa na maji, imeokotwa, akauziwa Misha. Misha ndo akanambia “mie nlivotoka huku Port Sudan safari hii nimeona boti imetiwa kioo chini. Shebe unaweza kufanya?” Nkamwambia “hapa sijapata kufanya lakini kwa kiasi ya kimaarifa ntaweza kufanya.” Mie alonfundisha kazi kanambia “usiseme huwezi kufanya kitu. Jaribu.” Sasa kama unataka tujaribu nitajaribu. Ndo tukafanya tukafaulu. Sasa namna nlivoifanya, matengenezo yenyewe, mimi kama ntakaa kwenye usukani huku nyuma huku, humuoni mtu alioko pale, labda akae mbele kabisa, nimejengea ninhii hivi, na wao ndo wako chini huko, isipokuwa uinuke khasa kwa kutizama hivi ndo utaona. Sasa hata wakati nnawatembeza watalii kwa kuona chini [ya maji], mie nakuwa siwezi kukaa kwenye kiti changu, itakuwa lazima nisimame na mie nione pale kwenye kioo, kama ndo pana mawe hivi, hapa pana hivi.

Tukafika mpaka Kizimkazi. Tumeshuka Kizimkazi pale, watu tele wamejaa pale pwani, na katika walokuweko mtu nnomjuwa Maalim Ubwa Mamboya, yeye ndo alokuwa Mwalimu Mkuu wa skuli pale Kizimkazi. Hakuna mawasiliano, simu zimekatwa. Akatoka Jimmy Ringo na Ali Nyau, kama kwenye saa mojamoja [za asubuhi] tena hiyo, wakapewa gari ya Maalim Ubwa Mamboya, Standa, wamekuja zao mjini halafu walivorudi wamekuja na Land Rover tatu. Ndo tukaingia Land Rover moja mimi, Misha, Mzee Karume, na Ali Mahfudhi nnafkiri, wao wamekaa mbele kwenye Land Rover, sisi tumekaa huku nyuma. Gari ingine ndo wameingia walobaki, lakini tumefika Raha Leo ndo tunaona hali hiyo. Watu na mabunduki. Njiani peke yake huko Fuoni, wapi wapi, maiti ziko njiani. Hiyo Jumatatu hiyo asubuhi. Jumapili ndo watu wamefuswa kwelikweli. Hakuna mazungumzo. Kimya! Sie tulikuwa na Jimmy Ringo anasema “hii tangu jana bwana. Leo asubuhi sisi tunatoka kule kuja huku, lo! Ndo tumeyaona hapa, sijui watu gani walokujia upande huu.”

Kufika Raha Leo, tumeshuka pale, ndo wanakuja mawaziri kuja kujisalimisha. Kwanza kaja Amirali Abdulrasuli, kapokelewa vizuri. Halafu kaja Ibuni Saleh kaja Idarus [Dr. Ahmed Idarus Baalawy]. Sasa anakuja Ali Muhsin. Kushuka pale akapigwa pale pale nje kwanza. Jamaa gani sijui kampiga kigongo hapa, kamchana, anapanda ngazi ile, nakumbuka kavaa shati jeupe la nylon, limerowa damu. Basi, walioko juu wakakasirika sana. Hasa mtu sauti hasa aliotowa Mtoro Rehani “nani kafanya mambo kama haya bwana. Nyie mnafanya mambo ya kishenzi, na hivi…” Sasa sie tulioko juu habari imekuja kuwa yule mtu alompiga Ali Muhsin na yeye kapigwa, kauliwa palepale. Nkichungulia uwani huku, namuona Nassor “Mlawwaz” anasema mimi sikubali, lazima mtanipeleka kwangu. Tunamsikia hasa. “Nataka munipeleke kwangu, Sijui hali ya watoto wangu ikoje. Haiwezi kuwa kabisa.”

Misha alikuwa na Mzee Karume most of the time. Anazungumza na Karume, anazungumza na Mtoro Rehani. Akipiga simu Mzee Karume “tusaidieni dawa na silaha.” Mimi nkawa nnacheka. Hivo vitu mbona havifuatani? Anasema na simu na Dar es Salaam. Akizungumza na Mwalimu. Anataka dawa na risasi! Sasa sie tulivopanga pale na Misha akasema leo tutalala kwa Erickson [Erick Steven] Administrator General, manywele. Lakini baada ya kufika saa nane Misha akasema, Shebe hapalaliki hapa. Tusilale kabisa. Manake hapana usalama wowote. Watu wamemahanika. Hanga yeye ndo mtu alokaa kimya sana. Hanga ndo mtu katika walokaa kimya sana yeye. Hakuwa akitembea sana kuwa kama ndo kasheherekea na nini lakini wengine harakati zao unahisi wanasheherekea hasa.

Ilipofika saa nane, Misha akasema bora twende zetu Kizimkazi. Tukapewa Land Rover pale, na walinzi, tukatoka moja kwa moja, tukenda mpaka Mtoni kwenda kuchukuwa petroli. Hali wakati huo hapana mtu anayetembea. Anotembea mtu ana mrao, ana bunduki. Na wengi utamkuta mtu keshalewa, ana bunduki na mabostala kavaa huku, almuradi, tukasema hapa hapakaliki. Na sisi ilikuwa twende kwa Erick Steven ili tuazime mashine yake moja. Ile moja imeshaharibika, halafu turudi na moja tu. Erik alikuwa ni mtu anayependa sana mambo ya baharibahari tu. Jambo kama lile mtu kukupa kitu chake itakuwa si tabu. Tukenda Mtoni tukachukuwa petroli, tukasema tusiondoke hii jioni bwana madam tuna mashine moja. Tulale hapa hapa Kizimkazi asubuhi tutaondoka Kizimkazi tutakwenda zetu Kunduchi.

Tukalala Kizimkazi, Jumatatu. Tukaondoka Kizimkazi asubuhi Jumanne kwenda Dar es Salaam na mashine hiyohiyo moja. Mimi, na Misha, na baharia wetu mmoja, kijana mmoja mdogo wa Kimakonde, ambaye alikuwa akikaa palepale. Na hiyo usiku na yeye alikwenda kuamshwa hivohivo hajuwi hata anakwenda wapi. Tulivoondoka Dar es Salaam kuja Zanzibar. Tukafika Dar es Salaam kama saa nne hivi asubuhi. Tulipofika Dar es Salaam, siku ya tatu yake Misha akaondoka kwa ndege kutoka Dar es Salaam kuja Unguja. Sijui ilikuwa ni ndege ya kukodi au ndege maalumu? Ijumaa nafikiri alikuwa kaondoka kuja huku Unguja. Mie nkabaki kule. Mie nkawa kazi za pale si lazim yeye aweko. Watu wanakuja wanasajili na mapema, ewe bwana tuko watu kumi tunataka kwenda nje saa tisa. Watu wanopenda mambo kama yale anajuwa ile jaduweli ya kujaa na kukupwa maji. Maji yanajaa saa ngapi, yanakupwa saa ngapi kwa hiyo time nzuri ipi ya kwenda pahala.

Halafu kutoka hapo ikawa Misha kila wiki anakuja Unguja. Anaondoka Dar es Salaam Jumanne, anarudi Alkhamis au Ijumaa, kila wiki. Manake anakuja huku kunako kazi zake za chokaa zile vilevile. Sisi, mimi na Misha, tuliondoka Zanzibar 1963. Manake nakumbuka Babu mara moja alisema, hapahapa kwenye mkutano, hapa Weles tena ilikuwa, mwezi wa Ramadhani, akasema “sisi tunawajuwa watu wanaowasaidia hawa, na tukipata uhuru watu wa mwanzo tutowaondowa hawa Mayahudi walioko hapa.” Yeye si akiona watu wa Afro-Shirazi wakenda kwa Misha pale.

Moshe Dayan aliwahi kuja Zanzibar baada ya fujo [za June 1961]. Alikuja peke yake. Misha alinambia kesho asubuhi kwenye saa mbili nna mgeni nataka kumtembeza tutakwenda Kizimkazi. Haya. Akawaambia na mabaharia na hivo. Tukatayarisha boti, asubuhi, kaja yule bwana, ambapo siku ile walikwenda familia yote, alikwenda Misha, alikwenda shemegi yake Abraham na mkewe ndugu yake Misha mwanamke alokuweko hapa. Abraham sasa alivokuja hapa, mbali ya hiyo biashara ya kamba, na kutia katika mifuko na nini, ikawa anaagiza mboga kutoka Nairobi. Wiki mara mbili kwa ndege zinakuja hapa Zanzibar. Vitu visopatikana hapa, lettuce, beetroot, cabbage, cauliflower, spinach, spring chickens. Na customers [wateja] wake wengi walikuwa wale watu wa Project Mercury ile. Wamarekani wa ile tracking station [kituo cha uchunguzi wa anga] walikuwa wateja wake wakubwa. Wakikaa Mazizini nyumba ya hayati Rashid Mohamed bin Mbaruk. Wote watatu wakikaa pamoja. Wao ndugu wanaume watatu, mwanamke mmoja. Ndugu mmoja mwanamme alikuwepo Dar es Salaam, mdogo kabisa wa mwisho wao. Akiondoka Misha kwenda Israel yeye huondoka Arusha akaja Dar es Salaam. Wanasema Kiswahili kama kawaida na ni raia [wa Tanzania]. Basi tukatoka na yule bwana moja kwa moja mpaka Kizimkazi, hatukusimama pahala kuwa labda tuzamie tupige samaki. Si kawaida, tukitoka lazma tutasimama pahala kwenye mwamba tupige samaki, tupige hivi, lakini sku ile haikuwa hivo. Wameshuka, wakasema sasa nyinyi rudini kama mnataka kupiga samaki au nini. Wao wote wakashuka. Gari zao zinawangojea pale. Wakaja kwa njia ya juu, mimi nikarudi na mabaharia wangu na boti. Tukarudi.

Halafu ndo tena akanambia “yule ni mtu mkubwa sana kwetu.” Ah! baadae sana tena ndo nakuja kuona mapicha “Moshe Dayan, Moshe Dayan.” “Huyu mtu si alikuja huyu Unguja, tumekuwa hivi hivi…?” Nimekuja kujuwa baadae kabisa. Misha alianza kuondoka kabla ya mapinduzi kwa usemi wa Babu kuwa tukipata nanhii [uhuru] watu wa mwanzo watakaoondoka watakuwa wao. Kwa hiyo kaondoka mapema yeye. Kaisikia, na yale mambo aliyaona kweli. Babu siku zile akikaa Funguni kule karibu na Ali Mdogo, ilikuwa lazima apite pale kwenye ofisi ya Misha. Anaona kila kitu. Kwa hiyo sie tumeondoka hapa 1963, mwaka mzima kabla ya mapinduzi. Maisraeli wakaja wakafunguwa ubalozi hapa. Kampuni ya Misha haikutaifishwa. Walimwambia aiendeshe yeye, iwe ya serikali. Akafanya hivo, senti moja hajalipwa. Yeye mwenyewe akawa taabani na hawa watu. Gharama zake za ndege, kwenda na kurudi, akija hapa ndo anakaa Zanzibar Hotel, production [uzalishaji] inakwenda kule, pesa zinaingia huku kwenye mfuko wa Afro-Shirazi. Senti moja hakupata. Mambo hayo alimwachia Hanga, Hanga tena wakamtenga akawa hajuwi ashike wapi. Hanga kawekwa ndani, ikawa yeye sasa na Saleh Saadalla, Saadalla na yeye kawekwa ndani. Saleh Saadalla akiingiliana sana na Misha. Hata hiyo baada ya mapinduzi, Saleh Saadalla alikuwa kila vinapofanywa vikao va serikali Dar es Salaam, anakuja na mkewe anakaa hotelini kwa Misha, siku tano, sita, wiki. Misha si alikuwa na hoteli “Silver Sands?” Akija Dar es Salaam akikaa kwa Misha khasa pale hotelini. Hanga sijapata kumuona hata sku moja. Hanga alikuwa si mtu wa raha namna hiyo. Mambo yake peke yake peke yake tu. Mara nyingi.

Abdul Faraj kwenye fishing survey yetu ya prawns, kwenye hiyo Mwananchi Ocean Products, tulipokuwa Mafia alikuwa akija Mafia. Kuna Mwananchi Trading, kuna Mwananchi nini…Na Abdul Faraji alikuwa General Manager wa zote hizo. Faraji alikuwa mwezi mara moja anakuja kule Mafia. Misha alikuwa kama treni. Ana njia maalum. Akitoka huku Mazizini anakuweko pale ofisini. Alipokuwa akikaa Mwera pale, baada ya kilima cha Koani, mkono wa kushoto, nyumba ilokuwa ya ukoo wa kifalme wa Zanzibar. Akitoka pale nyumbani kwake akenda Dunga kwenye biashara yake ya tanuri ya chokaa. Misha alikuwa ana mabaharia wengine. Watu waliobakia na chombo wakati wote ni mimi peke yangu, kwa kuwa ni kepteni, lakini wengine akipata kazi nyengine bora anawachilia mbali. Kwa hiyo alikuwa nao wengi. Ikiwa kwa vyombo vidogovidogo sijui vinatokea wapi…kulikuwa na harakati kubwa Bagamoyo na Kunduchi, hizo ndio bandari za magendo toka zamani. Kule Kunduchi kuna watu wamejenga nyumba maji yakijaa wewe unaweka boti anaingia mlango wa nyuma kwake. Hutaki kubeba mzigo kuupeleka wapi sijui. Watu maarufu wako kule. Akina Mzee Masanga, Bwana Khamisi, Mzee Kibosha. Mzee Masanga na Bwana Kibosha watu maarufu sana hao.

Watoto wa mdogo wake [Misha], mmoja anaitwa Victor. Wewe ukenda Rungwe Oceanic Hotel nyumba yao iko hapohapo, na Silver Sands haipo mbali. Hao wamezaliwa hapahapa. Wana duka Oysterbay la milango na madirisha ya aluminium. Ndugu yake mwengine yuko Arusha.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: