Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!

Icon

Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia

Mlango wa Kumi na Tisa: Kwaheri Ukoloni, Karibu Uhuru!

Ikiwa watu wa Zanzibar, bila ya kuingiliwa na watu wa nje na ikiwa wana sababu zao, wakaamua kuwa Muungano umekuwa kero kwa maisha yao, na kwamba hauna maslahi na wao sitowalazimisha kubakia na Muungano huo. Muungano huu utasita pale tu nchi shiriki itapoamua kujitenga. —Mwalimu Nyerere

 

Dharau za Uwakilishi wa Nguvu za Umma

Kosa walilolifanya akina marehemu Abdalla Kassim Hanga ni lile ambalo limeelezwa kwa ufasaha na Ibn Khaldun ambalo ni “kudharau umuhimu wa nguvu za kijamii, za umma, katika kufaulu kwenye mambo kama haya. Ikiwa khadaa imetumika, ni vizuri kwa mtu kama huyo asifaulu na alipishwe kwa makosa yake.” Kwa daraja la kwanza mapinduzi ya Zanzibar ni mapinduzi dhidi ya Wazanzibari waliyoipigiya kura serikali ya ZNP-ZPPP, na kwa daraja la pili yalikuwa dhidi ya Mzee Karume ambaye alikuwa ameukamata uongozi wa nusu ya pili ya jamii ya Kizanzibari. Khadaa kubwa ni mapinduzi ya Hanga na Kambona yaliyopewa nguvu na Dola ya Tanganyika na kupuuzwa na watawala wa Kiingereza kwa sababu chaguo lao la uongozi lilikuwa ni Mwalimu Nyerere na Mzee Karume, na si Kambona na Hanga.

Kilichoiparaganya mipango ya mapinduzi ya Hanga na Oscar ni khadaa yao ilipokutana na khiyana ya Sefu Bakari na Abdalla Said Natepe pale alipochomozeshwa John Okello ambaye hawakumjuwa na mapema mbali ya kuwa hawakumtarajiya kuwa atakuja kuwa mbele ya mapinduzi ambayo Kambona na Oscar walikuwa ndiyo wapishi wakuu. Kutokuwemo kwa Mzee Karume na Chama cha Afro-Shirazi ndani ya mipango ya mapinduzi yaliyoandaliwa na Hanga pamoja na wenzake ndani ya ASP, kuliweka pengo ambalo lilikuja kuzibwa na Okello. Kama Mzee Karume alikuwa anajuwa kuhusu mapinduzi basi ilikuwa ni kwa kuambiwa na bado hakujatolewa ushahidi wa kinagaubaga kuwa yeye ndiye aliyekuwa na mipango ya kufanya mapinduzi Zanzibar.

Tatizo jingine ni Hanga hakuwa na kiongozi mwenye sifa za kuwaongoza wanamapinduzi wenye silaha kama alivyokuwa nazo John Okello. Kwa Hanga kumkosa mtu kama Okello kulisababishwa na kukosa kuwa nao karibu sana watu kama Sefu Bakari na Abdalla Said Natepe. Siasa za kutoaminiyana hazina mwisho mwema. Mwanzoni viongozi hao wawili walikuwa na Hanga na Saleh Saadalla katika kuyapanga mapinduzi lakini baadaye wakawageukiya na kumuunga mkono na kumpa madaraka khasimu wa Hanga na Saadalla—Mzee Karume. Anthony Clayton ameandika kuwa:

Ingelikuwa mipango ya Hanga imefaulu basi angelikuwa yeye ndiye angelikuwa kiongozi khasa wa Zanzibar, na si Karume. Tamaa hii ya Hanga ikijulikana na Okello ambaye alimuona Karume, katika nafasi yake kama ni kiongozi wa A.S.P., kuwa ndiye kiongozi halali wa serikali ya baada ya mapinduzi; Okello alimtizama Hanga kuwa ni kiongozi mwenye uchu wa kujitwaliya madaraka, ambaye ameungamana sana na siasa za Tanganyika, wakati Okello mwenyewe alipendeleya uwepo uhusiyano na Kenya. Kwa kweli, Kassim Hanga alikuwemo kwenye listi ya Okello ya watu aliyotaka wauliwe na wakati wa Mapinduzi Okello alimtangaziya ajisalimishe.1

Upinzani ndani ya Afro-Shirazi baina ya kundi lililokuwa likimuunga mkono Mzee Karume (Karume Yeka) na waliyokuwa wakimpinga uliingiya moja kwa moja katika ushikaji wa madaraka mara tu baada ya mapinduzi kufaulu. Ugomvi baina ya viongozi wa ndani ya chama cha ASP ulikuwa haujulikani na wafuasi nje ya chama kwa hiyo suala la uongozi wa mara tu baada ya mapinduzi lilipochomoza, viongozi waliyoyapanga mapinduzi kwa siri bila ya kumshirikisha Mzee Karume walijikuta wako katika hali mbaya na ya hatari mbele ya wafuasi wa chama cha ASP. Hawakuwa na njia isipokuwa kuukubali uongozi wa Karume na wao kupoteza nafasi zao na hata maisha yao.

Tutakumbuka na kurudiya kuwa kina Sefu Bakari na Abdalla Said Natepe walikuwa wakenda kuripoti Gongoni kwa Saleh Saadalla Akida. Hapo piya panaonyesha kuwa utiifu wao haukuwa moja kwa moja kwa Mzee Karume peke yake. Baada ya serikali kupatikana baada ya mapinduzi kina Sefu Bakari na Abdalla Said Natepe walikuwa katika upangaji mikakati ya kuwamaliza wapishi wakuu wa mapinduzi, Abdalla Kassim Hanga na wenzake. Mchango wao wa kushirikiyana na Saadalla na Hanga ukafunikika na utiifu wao ukarudi kwa Mzee Karume mpaka alipokuja kuuliwa kwa kukosa kuwekewa mipango yoyote ile ya ulinzi mkali wakati kina Sefu Bakari na Mzee Natepe wakijuwa kuwa kuna mipango ya kuipinduwa serikali.

 

Mkataba wa Maofisa wa Umma wa Kiingereza

C. L. R. James, mwandishi maarufu kutoka kisiwa cha Trinidad, ameandika kuwa katika riwaya ya daraja la kwanza ya mwandishi wa Kimarekani Herman Melville iitwayo MobyDick, kuwa kuna sifa mbili za binaadamu wawili ndani ya kitabu hicho. Mmoja ni Ishmael, na wa pili Ahab. Ishmael ni msomi lakini hana msimamo wala hana dira—anayumba:

Ishmael anauwona wazimu wa Ahab, anakumbwa nao, ana akili za kutosha za kuupinga; lakini kama Melville mwenyewe, hana mtu mbadala, wala nguvu za kumpinga nahodha mwendawazimu. Usiku ule Ishmael alikuwa kwenye usukani na hakuona kitu mbele yake isipokuwa maafa. Melville aliona na kutokana na uzowefu wake kuwa hakukuwa na dawa; lakini inaonekana kuwa huyu Mmarekani, ambaye ni tunda la kujivuniya la uhuru wa nafsi wa miaka 1776 mpaka 1850 alikuwa hana imani na usomi au uokovu wa kukimbiya au wa aina yoyote ile. Jamii ilikuwa imeshaangamiya na akaisukuma kunako maangamizi yake. Ahab alijuwa nini anataka; na Melville sio tu kuwa anamuhusudu Ahab, bali hana isipokuwa dharau kwa msomi asiyekuwa na msimamo.2

Tutamuachiya msomaji kuamuwa nani ni Ishmael, nani Ahab, na nani Melville, katika historia ya uongozi ndani ya bahari ya Zanzibar na ya Tanganyika ya kabla na ya baada ya mapinduzi. Ushahidi wa Kiingereza unaonyesha kuwa sababu kubwa ilioifanya serikali ya ZNP-ZPPP kuyumba katika kuchukuwa maamuzi ya kuulinda uhuru wa Zanzibar ni kuikumbatiya siasa ya kutokufungamana na upande wowote (Non-alignment). Anaelezeya Kamishna Sullivan:

…niliakabili Serikali wiki iliyopita juu ya suala lenye unyeti ya hali ya juu wa kutafuta mipango ya msaada wa kijeshi kutoka nje, suala ambalo Serikali ilikuwa ikilikwepa bila ya kiasi kwa inavyoonyesha walikuwa wanasumbuliwa na suala la kufungamana ikiwa watafunga mkataba wa kijeshi na nchi moja wapo kati ya madola makubwa. Waziri Mkuu alinihakikishiya kuwa mazungumzo yalikuwa yanaendeleya lakini hakunipa dalili yoyote yalikuwa na nani.3

Wakati wa Mkutano wa Uhuru wa Zanzibar, Zanzibar Independence Conference uliofanyika tarehe 31 Agosti mwaka 1963, Mawaziri wa Zanzibar waliombwa: “…kufikiriya kama watapenda kuzungumza kuhusu Mkataba wa Kijeshi na Uingereza na kama watataka wampe maoni na mahitajiyo yao Mheshimiwa [Mwenyekiti wa mkutano], ili amuarifu Secretary of State…”4

Waingereza waliona kuwa Mawaziri walikuwa wanafikiriya kutafuta Mikataba ya Kijeshi na Misri, Tunisia au Algeria na walieleza wazi ugumu wa kuwa na mkataba wa kijeshi na nchi zilizokuwa ziko mbali sana na Zanzibar kwa sababu za upelekaji wa vifaa, na kadhalika.

Katibu Mkuu wa Waziri Mkuu Bwana Mohammed Shamte, Bwana Mervyn Vice Smithyman alilalamika kwa kusema:

Tena, baada ya Uhuru, nilizungumza na Waziri Mkuu mara sita tafauti kumuelezeya kuwa vikosi viliyopo havitoshi ikiwa kutatokeya ghasiya kubwa na ashauriyane na Serikali ya Kiingereza au Serikali ya Kenya, kujaribu kupata Mkataba au kufanya mipango ya kuongeza nguvu za aina yoyote ile. Baada ya kumkumbusha kwa mara ya sita ndipo alipofanya mpango wa mazungumzo yaliyofanyika na Balozi wa Kiingereza pamoja na Sheikh Ali MUHSIN juu ya maudhui hiyo. Mawasiliyano yalipelekwa kwa Serikali ya Kiingereza lakini kwa bahati mbaya ilijibu kuwa haiwezi kukubaliyana kufunga mkataba wa aina hiyo. Waziri Mkuu, mbali ya shinikizo langu, alikuwa hayuko tayari kuruka kwenda Nairobi kwa mazungumzo na Jomo KENYATTA juu ya maudhui hii. Wakati huo alikuwa ana mahusiyano mazuri na Jomo KENYATTA kwa sababu ya mazungumzo ya Mwambao, bado ingeliwezekana kwa wakati ule kwa Jomo KENYATTA kukubali kuitowa G.S.U. au vikosi na kama angeliombwa vingelikuwa tayari viko visiwani kabla ya maamuzi kufanyika katika mustawa wa kisiasa.5

Mwandishi wa Kiomani Nassir bin Abdulla Al-Riyami katika kitabu chake kwa lugha ya Kiarabu Zinjibar: Shakhsiyyat wa Ahdaath ameelezeya juu ya suala la ulinzi wa Zanzibar kabla ya Mapinduzi. Pia ameelezeya namna Naibu Kamishna wa Polisi wa Kizanzibari, marehemu Sheikh Suleiman Said Al-Kharusi, alivyowaomba Mawaziri wa serikali iliyopinduliwa kuukubali ushauri wa Bwana Biles kuwaomba Waingereza kwa njiya iliyokuwa rasmi wakibakishe kikosi cha Gordon Highlanders ambacho kilikuwepo Zanzibar wakati wa sherehe za uhuru. Waziri wa Fedha, marehemu Sheikh Juma Alley Al-Abrawi alifanya istihzai na kusema “Unafikiriya serikali ni kombe cha chai kinaweza kupinduliwa kiurahisi!” Anaelezeya Nassir Al-Riyami kuwa mjumbe mwengine wa Baraza la Mawaziri, Bwana Maulidi Mshangama ambaye alikuwa Waziri wa Ilimu na Ustawi wa Jamii alimjibu Al-Kharusi kuwa:

Ikiwa tutalikubali pendekezo hili hatutakuwa popote pale karibu na uhuru na anaona ni bora kuondoka kwa kikosi cha kijeshi cha Kiingereza kusadifiye na kuondoka kwa ukoloni wa Kiingereza nchini. Na hivi ndivyo alivyoonesha Al-Kharusi namna gani Baraza la Mawaziri lilikataa kuzikubali nasaha za Polisi kwa umakini na badala yake wakaziyona kuwa ni kejeli juu ya kejeli, mbali ya Al-Kharusi kushikiliya kuwa hali ya usalama wa nchi iko katika hali ya hatari na kuwa nchi itakuja kushuhudiya ghasiya kubwa zaidi kuliko zile zilizoonekana mwaka 1961.6

Hakuna kati ya wanasiasa wa Zanzibar wa wakati huo, ambaye aliiyona hatari kubwa ya Muingereza kuiwacha Zanzibar bila ya ulinzi ndani ya kipindi baina ya kuondokana na utawala wa kikoloni na kuingiya ndani ya uhuru. Baadhi yao walifikiriya kuwa aliyepinduliwa ni Muingereza pamoja na utawala wa Kikatiba wa Sultan Jamshid kama vile alivyo Mfalme wa Uingereza. Wengine wakiwemo Waingereza wenyewe, waliyaweka macho yao yote juu ya chama cha Umma na kuudharau mvutano uliyokuwepo ndani ya ASP.

Wakati ule Ufalme ulikuwa na jina baya duniani hata kama ulikuwa si mbaya, na Jamhuri ilikuwa pepo ya siasa na ya wanasiasa hata kama mlikuwa na hilaki. Mfalme wa Zanzibar alikuwa hana madaraka ya kuingiliya kati taasisi za kisiasa na za kisheria za serikali isipokuwa tu pale anapotakiwa kufanya hivyo. Mambo yote ya kiutawala yalikuwa mikononi mwa Waingereza yaani British Resident na Chief Secretary wake. Ilitosha Ufalme kuchukiza kwa sababu Mfalme aliyekuwa akitawala Afrika Mashariki alikuwa ana asili ya Kiarabu na Muislam. Ethiopia mambo yalikuwa vyengine na Mfalme Haile Selassie alikuwa kati ya viongozi wa mwanzo kwenda Zanzibar kuwapongeza wanajamhuri kwa kumpinduwa Mfalme mwenzake.

Picha kubwa inaonyesha kuwa lengo la Mapinduzi ya Zanzibar ilikuwa kuupinduwa uzalendo wa Kizanzibari ambao ulikuwa ukiipinga siasa ya Kiingereza na ya Tanganyika chini ya Mwalimu Nyerere. Kwa mtizamo wa Waingereza wa wakati ule, Zanzibar ilikuwa imeshaingiya ndani ya mikono ya nchi adui ambayo ni Misri chini ya uongozi wa Gamal Abdel Nassir, ambaye angelikuja kuyahatarisha maslahi ya Uingereza na vibaraka vyake vya Afrika Mashariki. Sheikh Ali Muhsin alilifahamu hilo na ndiyo maana pale alipokuwa anapelekwa gerezani haraka alimtuma mtu akampe salamu seketeri wake wa Kigoa auchane muswada wa waraka ambao alikuwa anautayarisha kuupeleka kunako Baraza la Mawaziri baada ya kurudi safari kutoka nchi ya Misri. Kusitasita kwa uongozi wa ZNP-ZPP kwenye suala la ulinzi wa Zanzibar baina ya kuwategemeya Wamisri na kuwarudiya Waingereza ambao hawakutaka kuamini kuwa Zanzibar itaweza kuvamiwa na Tanganyika, ndiko kulikoiyangusha Dola ya Zanzibar na kuzuwiwa kuinuka mpaka hii leo.

Si ajabu pia kwa Maofisa wa polisi wa Kiingereza, kama Kamishna Sullivan na wenzake ambao wakilipwa mishahara mikubwa kutaka uwepo mpasuko baina ya Wazanzibari wenye asili zinazotoka bara la Asia na bara la Afrika ili pasikuwepo na masikilizano Zanzibar na Afrika Mashariki ambayo yatawaharibiya mambo yao. Ikumbukwe kuwa Kamishna J. M. Sullivan alikuwa ameshapewa barua ya kuwachishwa kazi tarehe 15 mwezi wa Novemba 1963. Naibu Kamishna wa Kizanzibari, Bwana Suleiman Said Al-Kharusi alipotakiwa awe Kamishna wa Polisi, aliomba awachiwe mpaka mwezi wa Septemba 1964 baada ya kuzielezeya “…hadhari zake za kufanya haraka kushika nyadhifa katika polisi, alisisitiza haja ya kupewa miezi michache kabla ya yeye kuchukuwa wadhifa wa Mkuu wa Polisi, alitaka aendelee Mkuu wa Polisi, Sullivan katika wadhifa wake.”7

Wakati wa Mkutano wa Katiba wa Zanzibar uliofanyika mwaka 1962 kulikuwa na makubaliyano uwepo Mkataba wa Maofisa wa Umma (Public Officers Agreement, POA), baina ya Serikali ya Malkiya na Serikali ya Sultan wakati Zanzibar itakapopata uhuru.8 Kwa kawaida Mkataba huo huwa unasimamiwa siku ya uhuru katika hafla ndogo na unatiwa saini na Balozi wa Kiingereza (High Commissioner) kwa niaba ya serikali ya Kiingereza. Kulikuwepo na Mkataba wa aina hiyo ambao:

uliwahusisha maofisa wa Kiingereza 60 wa mkataba na maofisa 70 wa kudumu na wanaofaa kupewa mafao baada ya kumaliza kazi…Ina maana wakati mishahara yao inakadiriwa na Serikali ya Kiingereza hakuna malipo yoyote yanayofanywa na Serikali ya Kiingereza kwa ofisa yoyote yule. Tunachokifanya ni malipo ya jumla kwa mujibu wa makubaliyano ya makadiriyo ya mwaka kwa Serikali ya Zanzibar kufidiya gharama za maslahi waliyowapa maofisa waliyokuwa chini ya Utaratibu huo.9

Mkataba wa Public Oficers Agreement uliipa dhamana ya moja kwa moja Serikali ya Kiingereza juu ya Maofisa wake kuliweka jeshi la polisi (na usalama) la Zanzibar chini ya Maofisa wa Kiingereza.10

Mshahara wa Kamishna Sullivan ulikuwa pesa za Kiingereza za wakati huo pauni 3,125 (Shilingi za Tanzania milioni 6,572,967.40 za leo). A. B. P. J. Derham, Superintendent, akilipwa pauni 1,956 kwa mwezi (Shilingi za Tanzania milioni 4,114,151.75 za leo). Wa chini yake kwa niaba, R. M. Misra akilipwa pauni 1,128 (Shilingi za Tanzania milioni 2,372,578.30 za leo) na Assistant Superintendent, T. Waring, akilipwa pauni 1,425 (Shilingi za Tanzania milioni 2,997,273.15 za leo).

Cha kuzingatiya pia ni Kamishna Sullivan aliwahi kutumika Palestine baina ya mwaka 1936 na 1945. Mbali ya Cyprus, Kamishna wa kabla yake, R. H. V. Biles alitumika Palestine baina ya mwaka 1937 na 1946. British Resident mpya, Sir George Mooring alitarajiwa kufika Zanzibar kuanza kazi mwezi wa Januari 1960. Katika kikao cha mkutano uliofanyika London tarehe 11 Julai 1961 Bwana Mooring, baada ya fujo za Juni za 1961, alifahamisha kwamba ni:

…wazi kama mivutano iliyopo [Zanzibar] itaendeleya basi kuondoka kwa Muingereza itakuwa ni operesheni sawa na ile iliyofanyika Palestine. Na Bwana Morgan alisema kuwa inawezekana Kamati ya Uchunguzi ikatowa picha safi ya Zanzibar iliyogawanyika baina ya makundi mawili ya kikabila na itakuwa wazi kwa kila mtu kuwa kutakuwa na hatari nyingi ndani ya harakati kuelekeya kwenye uhuru. Utaratibu kama wa Palestine au Cyprus itabidi ufikiwe. Naye Bwana Mooring alisema kuwa anafikiriya kuwa suluhu baina ya makundi mawili inaweza ikapatikana kwa njiya ya:

a) katiba maalumu

b) kuunda Shirikisho la nchi za Afrika Mashariki [na Zanzibar ilindwe ndani ya mfumo wa Shirikisho]

c) kwa kuhakikisha kuwa hakutofanyika maendeleo mengine yoyote ya kikatiba mpaka uchaguzi mwengine utakapofanyika.11

Yote matatu hayakufanywa kwa sababu picha iliyotolewa na Kamati ya Uchunguzi wa fujo na mauwaji ya Juni haikukiangaliya kiini cha matatizo ambacho kilikuwa ni wageni waliyokuwepo Zanzibar na waliyoletwa kutoka nje, kuamini kuwa wana haki zaidi Zanzibar kwa sababu ya Uafrika wao kuliko Wazanzibari na Uzanzibari wao. Ingawa vikosi vya askari (1,000) vililetwa kutoka Kenya kutuliza hali, vyombo vya usalama havikuingiya na kuzama ndani ya jamii za wageni na za wenyeji na kuuchunguza kwa kina mtandao wa viongozi wa mipango ya maafa ya Juni 1961. Kufikiya tukio la Januari 1964, usalama chini ya uongozi wa Kiingereza ukafeli tena kuutambuwa na kuuingiya mtandao wa vichwa na mikono ya Mapinduzi.

Wakati wa mapinduzi marehemu Bwana Nassor Abdulla Nassor Al Shihemy, maarufu “Mlawwaz”, alikuwa ofisa wa tatu katika jeshi la Polisi la Zanzibar katika kitengo cha Criminal Investigation Department. Marehemu Iddi Mjasiri alikuwa ofisa wa tatu katika Special Branch pamoja na marehemu Inspekta Marjebi. Kwa mujibu wa Nassor “Mlawwaz”, Harub Said Busaidy, ambaye akikaa kwa marehemu Bwana Ali Ahmed Riyamy, aliwahi kumpelekeya taarifa kuhusu Mapinduzi na akampeleka kutowa statement na ikatiwa saini lakini Waingereza hawakuchukuwa khatuwa yoyote ile.

Ni jambo linalowezekana kabisa kuwa watumishi wachache wa Kizungu wa serikali ya Zanzibar waliyopewa muda wa mwisho wa kazi zao na waliyokuwa na chuki na tamaa zao walishiriki kichinichini katika Mapinduzi ili wapate kubakiya katika kazi zao na khasa wale wa polisi. ASP walipewa muongozo na Nyerere wasiwaudhi Waingereza na sera yao ilikuwa hatukusoma kwa hivyo tutakuhitajini. ZNP ilikuwa itawaweka Wazanzibari wengi sana katika kazi nyingi ambazo zilikuwa zimeshikwa na Waingereza ambao walijuwa kuwa ikipata ZNP wengi wao hawatokaa na ikipata ASP itabidi waombwe wakae kwa sababu ASP walikuwa hawana watu kama ZNP na ASP ilikuwa haina wasomi kama ZNP.12

Hapa kuna suala la wazi la kisheria kwa upande wa Uingereza kushindwa kuweka amani na utulivu Zanzibar, na kuzuwiya mauwaji ya halaiki, pamoja na kushauri Zanzibar itawaliwe na Tanganyika ili kukamilisha siasa yake ya kuikataliya uhuru Zanzibar, na kurithiwa kwa siasa hiyo na Dola ya Tanganyika ili Zanzibar isiingiye ndani ya mikono ya “adui” yao.

Kilichokusudiwa khasa ni propaganda ileile yenye kutamka kuwa Zanzibar ilikuwa kituo cha mwanzo cha ubeberu Afrika Mashariki na cha “utumwa wa Waarabu.” Kinyume kabisa na ukweli wa kihistoria ulivyosajili, Zanzibar na sehemu kubwa ya Afrika Mashariki ilikuwa ikijulikana kwa jina la Ethiopia au Wamisri wa kale wakilifahamu eneo hilo kwa jina la Punt.13 Katika karne ya kumi na saba nchi ya Oman ilisaidiya kwa hali ya juu ukombozi wa Afrika ya Mashariki kupata uhuru wake kutoka ubeberu wa Kireno, kutangaza maadili yake ya kiutamaduni na akhlaki njema, pamoja na kuwacha mchango mkubwa wa kijamii na wa kiuchumi.

Wangapi leo wanayajuwa au wanayaona kwenye nyumba za kumbukumbu za kitaifa za Afrika Mashariki majina ya wakombozi mashujaa wenye asili ya Kiarabu ya Kiomani kama Muhammad bin Khalfan Al-Barwani, maarufu “Rumaliza” aliyepiga risasi kwenye tundu na kumuuwa askari wa Kijerumani aliyekuwa akiwamaliza Wahehe kwa marisasi Tanganyika? Au Bushir bin Salim Al-Harthi aliyekamatwa na kunyongwa Pangani baada ya vita vyake vya kuwatowa Wajerumani Tanganyika? Au Kanali Ali Mahfudh aliyepigana na majemedari wa Msumbiji Albarto Sipande na Raymundu Pasinuwapa katika ukombozi wa nchi hiyo kutoka kwa ukoloni wa Kireno? Au mchango wa chama cha ZNP katika kuupiganiya uhuru wa Zanzibar na kuupata, au wa Misri katika Sudan, Somalia, Kenya, Algeria, Zambia, Kongo, Uganda, Burundi, Mali, Eritrea, FRELIMO, ANC, MPLA, nk?14

Kinachopigiwa debe na kuitwa “kituo cha ubeberu” ni uhusiano mkongwe duniani wa binaadamu wenye asili zenye kutoka mabara ya Afrika na Asia. Ubeberu wa Kiingereza kuiwachiya Tanganyika kuibomowa Dola ya Zanzibar umefichwa na kupuuzwa kwa makusudi ili uhusiano mkongwe wa Afrabia usipate fursa ya kuendeleya na kuwanufaisha washiriki wake.

 

ZNP Ikiota Watu Wanateremka Zanzibar

Kamishna Sullivan na Katibu Mkuu wa Waziri Mkuu Mohammed Shamte, Bwana Mervyn Vice Smithyman, walitambuwa kuwa kulikuwa na upungufu mkubwa wa tahadhari za kiusalama na za kiulinzi katika kuulinda uhuru wa Zanzibar. Bwana Smiythman amekiri kuwa kulikuwa na ripoti nyingi kuhusu fujo zilizokuwa zikitarajiwa usiku wa tarehe 11 Januari 1964 na:

…ingelikuwa ripoti zote hizi zingelifika zinakofaa kufika, basi japo tahadhari ndogo zaidi zingelichukuliwa…na somo liliopo ni hizi ripoti zingelifikishwa kwa polisi na tathmini zake wangeliwachiwa wale ambao wamo katika nafasi ya dhamana na wenye ujuzi wa kuzifanyia kazi. Hapa polisi wanaweza kuwa walikuwa wana makosa.15

Bwana Smithyman amekaribiya kukiri baada ya kutokeya Mapinduzi kuwa Zanzibar haikupinduliwa na Wazanzibari lakini kufahamu huko hakukuibadilisha sera ya Uingereza juu ya kudhibitiwa Zanzibar na Tanganyika:

…ukweli ni kuwa sasa tunajuwa kuwa watu waliletwa kutoka nje ya nchi na kutowa mchango mkubwa katika mapinduzi. Historia ya jambo hili ni muhimu. Suala la uhamiaji usio wa kisheria lilichomoza wakati wa uchunguzi wa machafuko ya Juni 1961, na chama cha Z.N.P. na Sheikh Ali MUHSIN, walishadidiya kwa nguvu kuwa wengi kati ya waliyokuwa wakifanya fujo na waliyoanzisha machafuko ya Juni 1961 walikuwa ni wabara ambao ni wageni Zanzibar na walitambulikana kuwa ni watu kutoka nje ya nchi. [Suala] hili lilikataliwa kwa nguvu sana na vyombo vya usalama vilivyokuwepo, polisi, na wote waliokuwa na madaraka, kwa sababu haukupatikana ushahidi wa hilo. Kutokeya wakati huo, na miaka miwili sasa, kumekuwa na ripoti zenye kujirudiya kuhusu watu kuingiya kutoka bara kwa njiya za magendo…Nafikiri ni uadilifu kusema kuwa imani ya wengi ndani ya vyombo vya usalama, makao makuu ya Polisi, na ofisi ya British Resident [Balozi wa Kiingereza] ni kuwa Sheikh Ali MUHSIN na Z.N.P. walikuwa wakiota watu wanaingiya [Zanzibar] wakati haikuwa kweli.16

Assistant Sperintendent Thomas Waring naye ameandika kwenye ripoti yake ya tarehe 16 Januari 1964 juu ya Mapinduzi ya Zanzibar:

Wakati niko Zanzibar, na hivi sasa ni miaka miwili na nusu, nimekuwa nikiambiwa mara kwa mara kutoka kwa Waarabu kuwa wanakhofu ya kuvamiwa kwa silaha kutoka Tanganyika. Wakati nafanya kazi ndani ya Himaya [ya Zanzibar] nilifanya kazi Zanzibar [Unguja] na Pemba. Daima nikisikiya uvumi, ambao kama utakuwa ni kweli, basi matokeyo yake yatakuwa na athari za kutisha. Chache kati ya maneno yaliyokuwa yakivuma yalikuwa na msingi. Nilijifunza kuzipuuza hadithi za uvumi.17

Pia anaripoti Waring kuwa:

Waziri bila ya Wizara, Ibuni SALEH, wa serikali ya zamani aliniambiya kuwa anaingaliya Police Mobile Force kuwa ni kiini cha Jeshi jipya la Zanzibar. Ameniambiya nifanye mipango ya kuliongeza jeshi na nianze kuwaandikisha askari. Ameniambiya kuwa anaona umuhimu wa hili, na kikundi changu kiongezeke mpaka kifikiye watu 500. Amesema kuwa hili ni muhimu kwa sababu kuna uwezekano huenda Tanganyika ikaivamiya Zanzibar.18

Mwisho wa ripoti za Kamishna Sullivan na Bwana Smithyman ni masomo ya kuzingatiya kwa yaliojiri katika Mapinduzi ya Zanzibar. Khitimisho la Kamishna Sullivan lilikuwa kama ifuatavyo:

1. Si ushauri mzuri kwa nchi ambazo zina ufukwe wa bahari kuwa hazina mfumo wa vikosi vya wanamaji vya sawasawa.

2. Si ushauri mzuri kwa nchi ndogo kama Zanzibar, Mauritius, Seychelles, kuziweka silaha nyingi kwenye ghala moja au mbili, ingawa kuzigawa pia kunaweza kuleta matatizo mengi ya kiusalama.

3. Katika nchi ndogo usalama wa nchi unakuwa imara ikiwa kila sehemu ndogo ya idadi ya watu ina polisi mmoja.

4. Kama inavyoonekana ni kuwa operesheni nzima ilikuwa imepangwa vizuri sana na kwa nidhamu na watu wenye kuyadhibiti mambo ambao walikuwa na ujuzi wa kutosha wa mbinu za kivita na waliyofuata, katika matukiyo yaliofuatiliya, ni kwa karibu sana kile nilichokisoma kuhusu mbinu za kupinduwa serikali kutoka kitabu cha kumbukumbu (diary) cha BABU.19

Mwisho wa ripoti ya Smithyman ni mukhtasari wa masomo matano kutoka tukiyo la Mapinduzi ya Zanzibar:

a) Taarifa za Usalama

Wakati wa kuzitathmini ripoti ni lazima tuuweke akilini mgogoro baina ya Mashariki na Magharibi [Vita Baridi]. Katika mazingira ya Afrika ina maana kuwa kuna mpango wa siri wa kuzipinduwa serikali zote za kidemokrasia. Kwa hivyo ripoti zozote zile za usalama ambazo zinaonekana kuashiriya mpango maalumu wa siri zisidharauliwe kiurahisi.

b) Wafanyakazi wa Polisi

Mchujo wa wafanyakazi wote wa polisi na Usalama uwe ni wa kila wakati na kusiwe na huruma kuwafukuza au kuwapa uhamisho.

c) Vyombo vya Usalama

Baraza la Mawaziri lazima likubali kuwa vikosi vya usalama lazima vipewe nafasi ya juu ya kifedha. Mawaziri wa Serikali ya Zanzibar ya zamani ambao leo wamenyongoyeya jela watalikubali hili kwa moyo mkunjufu.

d) Ghala za Silaha

Zanzibar inaonyesha kuwa kuna uwezekano wa uvamizi wa ghafla kutokeya kwa hiyo uchoraji wa ghala za silaha ni lazima ziwe ndani ya mikono ya polisi hata kama zitavamiwa na mamia ya watu.

e) Uhuru wa Kujieleza na wa Kutembeya

Ili kuzuwiya kufanyika mazingira ambayo yataleta hali tete ya kiusalama, dola lazima itafute njiya ya suala la uhuru wa kuzungumza na kutembeya. Kwa Zanzibar mizani iliangukiya upande wa uhuru wa kuzungumza na uhaba wa usalama wa dola.20

Utumwa, Ukristo, Uislam, na Mapinduzi

Sababu ya zamani ya kuangushwa kwa Dola ya Zanzibar ni Uislam wa Afrika Mashariki:

Kwa namna ulivyokuwa na uadui na Ukristo una ‘uwezo mkubwa wa kuendeleya kunako muelekeyo wa ustaarabu wa kileo’, na kwa hiyo serikali uutumiliye, kama wanavyofanya Ufaransa, Uingereza, na Uholanzi, kama ni chombo cha kuwailimisha wenyeji, na uwepo mtizamo wa usiokuwa na nguvu juu yake. Wakati huohuo…Uislamu wenye nguvu usiwemo kwenye Makoloni ya Kijerumani, na njiya pekee ya kuuzuwiya ni kujenga vituo vya Kikristo vyenye nguvu, kama ilivyokusudiwa na Misheni.21

Ushahidi wa malengo haya unaonekana wazi kwenye vitabu vya Jan P van Bergen Development and Religion in Tanzania: Sociological soundings on Christian participation in rural transformation, John C. Sivalon Kanisa Katoliki na Siasa ya Tanzania Bara 1953 Hadi 1985, Frieder Ludwig Church & State in Tanzania: Aspects of a Changing Relationship, 1961–1994. Uchunguzi wa vitabu hivyo pamoja na vya Bwana Mohamed Said na Dkt. Hamza Njozi unaonyesha vipi Kanisa lilivyoitumiya Dola ya Tanganyika na baadaye ya Tanzania kujiimarisha ndani ya nchi kwa kuwazuwiya Waislam wasipige hatua za kimaendeleo zitakazoweza kuwapita Wakristo.

Tafauti na Waislam, wakala za kujitoleya na taasisi za Kikristo zinatowa mchango mkubwa katika huduma za kiafya na za kiilimu Tanzania. Huduma nyingi za kiafya katika sehemu za vijijini huwa zinatolewa na taasisi hizo ambazo zinapata misaada kutoka kwa wafadhili wa taasisi za kimataifa. Inakuwa ni vigumu kwa Waislam kupata misaada kutoka nchi za Kiislam na taasisi za kimataifa. Upande mmoja wameelemewa na vita vya kipropaganda dhidi ya Waarabu Waislam na utumwa wa Waislam ambavyo vinawaghadhibisha na kuwakimbiza wafadhili Waislam na taasisi za Kiislam. Au zitatafutwa taasisi za Waislam ambazo zimejaa ufisadi na kuwafanya wafadhili Waislam na taasisi za Kiislam zikataye kuwasaidiya Waislam kwa kupitiya taasisi hizo. Baina ya mifarakano yote hiyo Wakristo wanaongeza na wanaongezewa nguvu na waumini wenzao kutoka nchi za Magharibi.

Tarehe 21 Februari mwaka 1992, Baraza la Kikristo Tanzania na Baraza la Maaskofu Katoliki walitiya saini Mkataba wa Maridhiano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliyoandaliwa na Profesa, Dokta, C. R. Mahalu wa Kitengo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na kutiwa saini na Edward Ngoyai Lowassa kwa niaba ya Serikali, Elinaza Sendoro kwa niaba ya Baraza la Kikristo Tanzania, na Josephat Lebulu, kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki.

Mkataba wa Maridhiano una lengo zuri la kuendeleza huduma za afya na ilimu katika jamii na unaikalifisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania:

…itajitahidi kujumuisha misaada ya kifedha kwa ajili ya huduma za jamii zinazomilikiwa na ‘Makanisa’ itakapokuwa katika mazungumzo ya kuomba misaada husuusan mazungumzo yake na Jamhuri ya Kifedirali ya Ujerumani. Uwezekano kama huo uangaliwe pia itakapokuwa na mazungumzo na wafadhili wengine.22

Wakati Zanzibar ilipotaka kujiunga na shirika la Kiislam la Organization of Islamic Conference (OIC), Askofu E. Sendoro wa Mkataba wa Maridhiano alitahadharisha juu ya uamuzi wa kitendo hicho kwa kusema: “Zanzibar ikiwa ni Dola ya Kiislamu, itaendeleya kuwa sehemu ya Muungano? Bunge la Muungano litakuwa na dhamana juu ya Zanzibar au lipo kwa ajili ya Tanzania Bara?”23

Askofu Sendoro kalikozesha suala la Zanzibar kutaka kujiunga na OIC na kulifanya ni suala la Zanzibar kutaka kuwa Dola ya Kiislam. Kwani Mkataba wa Maridhiano ambao lengo lake kubwa ni kuendeleza huduma za kijamii za Kanisa katika sekta za ilimu na afya ulikuwa na lengo la kuifanya Tanzania kuwa Dola ya Kikristo? Kwa vile Mkataba wa Maridhiano ni mkataba baina ya Taasisi zisizo za kiserikali na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jee, ulipata baraka za Baraza la Wawakilishi la nchi ya Zanzibar na Bunge la Jamhuri ya Muungano au ilionekana kuwa hakuna haja ya kufanya hivyo? Mambo hayajaanziya hapo.

Mwaka 1970 shule zote za msingi, sekondari na za kuwafundisha walimu zilitaifishwa. Hali iliporuhusu Kanisa likaanza tena kujenga shule na Waislam walikuwa wamelala mpaka mwaka 1982 ilipojengwa Morogoro Shule ya Sekondari ya Jabal Hira. Mwaka 1991 Kanisa lilikuwa na shule 413 za chekecheya, skuli za sekondari 82 pamoja na seminari, skuli 73 za ufundi, vituo 48 vya kazi za kisanii kwa wanawake, college mbili za kuwafundisha walimu, na shule 6 kwa ajili ya wanafunzi walemavu.24

Kufikiya mwaka 2008 shule hizo zimekuwa za daraja la juu katika mashindano ya kitaifa. Shule za Sekondari 10 bora katika matokeo ya mitihani ya Kidato cha Nne ni seminari za Kikristo na tano za chini katika mashindano ni za Kiislam kwa sababu ya mazingira mabovu, walimu wasiyokuwa na ujuzi na kukosa misaada ya kifedha kutoka taasisi na nchi za Kiislam. Bado hujahisabu vyuo vikuu, vyombo vya habari yakiwemo magazeti, televisheni na redio. Mwaka 2005, Waislam walitunukiwa na aliyekuwa Rais wa Tanzania, Benjamin William Mkapa, majengo ya iliyokuwa Taasisi ya TANESCO ya Morogoro kwa lengo la kuanzisha Chuo Kikuu cha Waislam.

Hata hivyo, Waislam wa Tanzania bado hawana Taasisi zisizo za kiserkali zenye nguvu ya kufunga Mkataba wa Maridhiano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Watakapojijengeya nguvu za kisiasa na za kiuchumi ndipo watakapoweza kuwa na ubavu wa kuingiya kwenye Mkataba na Serikali na kuweza kusaidiwa na waumini wenzao kati ya Waafrika Waislam, Waarabu Waislam milioni 200, na Waasia Waislam bilioni 1, na kuweza kufunga Mikataba ya kibiashara na ndugu zao wa Kikristo na majirani zao. Miradi ya kheri kama ule wa Loliondo wa Dubai au wa Qatar wa kuendeleza kilimo cha chakula Kenya, itaendeleya kupigwa vita vya chini kwa chini mpaka Waarabu na Waislam watakapokuja na sera moja yenye: “Kushadidiya hoja ambazo zitawapa tabu viongozi wa kisiasa na wenye kasumba ya kutangaza habari ambazo hazikufanyiwa uchunguzi wa kina na zenye uwezo wa kuzichafuwa akili za binaadamu wa kawaida kwa kuwakosesha ustahmilivu na kuwatiya chuki.”25

Makosa yaliyofanywa na wanasiasa wengi wa Kizanzibari pamoja na viongozi wa Kiislam wa Tanganyika ni kuona haya kuzipiga vita hadithi chafu za “utumwa wa Waarabu” ili wasije wakatupiwa doo la matope kwa kuitwa “Waarabu” au “Mahizbu” au “Masultani”; majina matatu ambayo yamekuwa yakitumika kwa muda mrefu kuwanyamazisha watu au mijadala yenye nguvu za hoja. Kwanza, akili inachafuliwa kwa kulishwa uzushi wa historia iliyopotoshwa kwa makusudi, halafu mwenye kutaka kufikiri na kujiteteya kwa hoja hutupiwa kombora jingine linalomfanya ashindwe kujiteteya kwa sababu tayari ameshaitwa “Hizbu”, “Mwarabu” au “Sultani.” Lengo ni kuwatisha waliyoko ndani na nje ya nchi wasishikamane na kusaidiyana.

Chanzo kinasema kuwa mradi wa Loliondo umejenga visima, unawalipiya wanafunzi kusoma shule na vyuo vikuu, na kila mwaka unatowa zaidi ya shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Juu ya yote hayo uvumi unaendelezwa kwa makusudi kuwa Waarabu wanawachukuwa wanyama wa pori nchini kwao kinyume na sheria au wanawauwa bure katika kipindi cha uwindaji wakati wanajuwa fika kuwa wanyama ambao wametolewa ruhusa na wenye kulipiwa kuwindwa ni wachache sana kuliko wenye kuuliwa.

Wenye kuyajuwa mambo wanakiri kuwa Dubai ikiuondowa mradi wake Loliondo basi Wamasai wa sehemu yote watakhasirika bila ya kiasi. Ndugu yetu mmoja wa Kichaga alisema “tungeliweza kumpata Sheikh wa Dubai basi uchagani kote kungelingara.” Matunda ya chuki na fitina za muda mrefu zimewafanya Waislam na Wakristo kutopendana na hata Waislam wenyewe kwa wenyewe kuchukiyana, kutooneyana huruma, na kutoaminiyana.

Ukirudi nyuma zaidi mwaka 1904 utakuta tayari J. J. Willis wa Usalama wa Ujumbe wa Kanisa (Church Mission Intelligencer) ameandika kuhusu “Ukristo au Uislam katika Jimbo la Askofu wa Uganda”:

Ikiwa uwezekano wa Uislam kuingiya kutoka Kaskazini [Sudan na Misri] ni tukio ambalo halina budi kutarajiwa, basi hatari kubwa zaidi na yenye kutisha itatokeya Mashariki. Kuwa karibu na pwani, ambako zamani mtu alikuwa akifika [Uganda] kwa miezi, sasa anaweza kufika kwa masiku. Jambo ambalo lisingeliweza kuzuwilika ni kuingiya kwa mkumbo wa Waswahili watakaoletwa kwa treni [Afrika Mashariki]; na lisiloweza kuzuwilika ni uzowefu wao [Waswahili] mrefu wa ustaarabu ambao utakuwa na ushawishi mkubwa juu ya makabila ya Afrika Mashariki ambayo bado ni wanagenzi.26

Ni muhimu kutoyachukuwa maelezo ya kitengo cha usalama wa Kanisa na kuyaunganisha moja kwa moja na Mapinduzi ya Zanzibar kwa sababu bado hakuna ushahidi wa moja kwa moja wenye kuonyesha mchango wa Kanisa katika Mapinduzi ya Zanzibar. Lakini tunawaeza kusema kuwa kutokana na fikra ya Mwalimu Nyerere ambayo ilipokelewa na viongozi Waislam wa TANU na wa ASP ni kuitazama Zanzibar kwa mtizamo wa ubeberu wa Kiarabu na Usultani na kuongozwa na hamasa za kizalendo ambazo undani na upeo wa athari zake haukutambulikana na kuzingatiwa ipasavyo na wanasiasa wa zamani, Waislam na Wakristo.

John Okello kwenye kitabu chake Revolution in Zanzibar ametumiya lugha ya maamrisho ya Ukristo na chanzo kinasema kuwa mmoja kati ya Marais wa Zanzibar amesema kuwa Mwalimu Nyerere aliamuwa kumuondowa Okello Zanzibar kwa sababu alikuwa ameingiliwa sana na hamasa za dini ya Kikristo. Okello ameandika waziwazi kuwa washiriki wa Mapinduzi walichujwa kisawasawa na kati ya watu 4,000 walichaguliwa askari 270 na 245 kati ya hao “walitoka nje ya Zanzibar (Kenya, Uganda, Tanganyika, Msumbiji, Malawi, Congo na Zimbabwe, wote waliwakilishwa).”27

Si muhimu kuwa Okello hakututajiya wangapi kati ya hao walikuwa Waislam na wangapi Wakristo kwa sababu sumu ya fitina dhidi ya Waarabu Waislam iliwakumba Wakristo na Waislam pamoja. Wengi wao walikuwa tayari wameshamezeshwa sumu ya biashara ya utumwa wa Waarabu pale John Okello alipowahutubiya wanamapinduzi kwa kuwaambiya:

Wapenzi ndugu zangu. Nimesimama mbele yenu na naapa kwa mchana na kwa usiku kuwa niko tayari kuwaonyesha vipi tutaweza kujitawala. Mababu zenu, baba zenu na sasa nyinyi wenyewe mmeteseka na ukandamizaji wa Waarabu kwenye Kisiwa hichi. Mnajuwa kuwa matumbo ya mama zenu yalifunguliwa ili mabibi wa Kiarabu wapate kuona namna ya mtoto anavyokaa ndani? Mnajuwa kuwa babu zenu walichinjwa chini ya miti hii ili mabibi wa Kiarabu wapate kuona namna binaadamu waliokufa wanavyoanguka? Si mahala hapahapa walipokandamizwa mababa zenu? Nikaendeleya kuwakumbusha kuwa masoko ya utumwa pamoja na vyuma na minyororo waliyokuwa wakifungiwa ndugu zenu bado inaonekana Kisiwani, pamoja na makaburi ya halaiki walimozikwa Waafrika waliouliwa; wao wenyewe wameyaonyesha mapango mengine ambayo damu ya Waafrika ilimwagika juu ya ardhi. Damu ya mababu zenu ilimwagika chini ya utawala wa Kiarabu; mnataka kuona damu za watoto wenu zikimwagika pia? Nani ataweza kuniambiya vipi Waarabu waliingiya kunako Kisiwa hichi na vipi walivyokitawala?28

John Okello alikuwa hazungumzi na Wazanzibari bali alikuwa akizungumza na watu ambao wengi wao, tena kwa sana, walitoka nje ya Zanzibar kwa sababu hakuwaamini Wazanzibari:

Nilihisi wengi kati ya Waafrika wa Zanzibar walikuwa hawaaminiki, kwa sababu walikuwa na uhusiano mkubwa na Waarabu wa Kisiwani, na wangeliweza kuwa ni majasusi na wangelizitobowa siri zetu ili wapewe vyeo kutoka maofisa wakubwa wa Kiarabu. Waafrika kutoka bara wasingeliweza kuwa na tamaa hiyo, na kwa kweli baadhi yao walikuwa wameshafukuzwa kutoka kwenye jeshi la polisi ambalo walikuwa wanaingizwa Waarabu kwa nguvu.29

Mpaka binaadamu akaamuwa kumdhuru binaadamu mwenzake na bila ya sababu basi huwa imepita fitina kubwa na fitina ya “utumwa wa Waarabu” na si “utumwa wa Afrika Mashariki” au “utumwa wa Bahari ya Hindi” ni fitina/propaganda kubwa Zanzibar ambayo iliuondowa utumwa mwaka 1897 wakati utumwa uliendeleya Tanganyika mpaka mwaka 1920. Oscar Kambona alimuelezeya Sheikh Ali Muhsin kwamba: “ilikuwa ni kawaida kwa baadhi ya makabila ya Kiafrika huko Tanganyika ya kwamba chifu akifa huzikwa pamoja nae kundi la watumwa wake (wahai) wakiwa wamebeba maiti ya bwana wao…mtindo huu ulisita pale tu ulipoingia Uislamu na Ukristo huko Tanganyika.”30 Ameelezeya Kambona mwenyewe kuwa “Babu yangu alikuwa ni chifu na mamishionari walipoomba wapewe mtoto wamsomeshe, babu yangu akawapelekeya mtumwa tu.”31

Kanisa la Anglikan la Zanzibar lilijengwa mwaka 1905 miaka 32 baada ya soko la utumwa kuondolewa na miaka 8 baada ya kuondolewa utumwa Zanzibar. Kwa mujibu wa mtafiti wa Kimarekani, Profesa Jonathon Glassman:

Jengo lenye mahandaki ya watumwa lilijengwa kama ni hospitali na mamishionari wenyewe, miaka ishirini baada ya soko la watumwa kufungwa. Mabaraza yasaruji kwenye ghorofa ya chini ya nyumba yanatambulikana wazi kama ni sehemu ambayo haifai kuingia maji, na hapana shaka ilikusudiwa kwa ajili ya kuwekea madawa.32

Lengo si kuufuta au kuingiza siasa ndani ya Ukristo Zanzibar lakini ni kuuingiza ukweli ndani ya uwongo ambao wenye kuuendeleza hawana hoja wala ushahidi wa kuziteteya na badala yake huamuwa kuwarushiya matope wale ambao hawawezi kusimama nao kwa hoja. Mwenye kurusha matope maisha hupata ushindi wa muda mfupi kwa sababu mwenye kurushiwa huwa hana njiya ya kujiteteya bila ya kurushiwa matope zaidi. Wakati umefika wa kufanya utafiti wa kina juu ya masoko ya utumwa yaliyokuwapo sehemu nyingi za Tanganyika, za pwani na za bara, makabila yaliyokuwa yakinunuwa watumwa, na makabila yaliyokuwa yakiwauza watumwa, na kazi ambazo watumwa walikuwa wakifanyishwa na Waafrika wenzao ili ipatikane ilimu yenye uthibitisho juu ya suala muhimu kama hili. Na pia ipo haja na hoja kubwa ya kuonyesha kwa ushahidi, kuwepo na kutokuwepo kwa mchanganyiko wenye kuhishimiwa baina ya watumwa waliyokuwa ndani ya mikono ya Waarabu na watumwa waliyokuwemo ndani ya mikono ya Wazungu. Nchi za Magharibi hazijapatapo kuuhishimu au kuupa madaraka ya kiutawala mchanganyiko wa mabwana na watumwa zao wakati Wafalme, na majemedari wengi wa Kiislam walikuwa wamezaliwa na mama weusi. Lakini nyuma ya tuhuma zote dhidi ya Waarabu na Waislam kuna khofu za kisiasa na za kiuchumi na ni jukumu la Waislam na Wakristo kuzitambuwa na kuja na mfumo wa mashirikiyano ambao utakuwa na manufaa ya haraka kwa waumini wa dini zote mbili.

Si ubeberu wa Kiarabu/Kiislamu, “utumwa wa Waarabu”, wala kunyanganywa ushindi kwenye chaguzi, ndizo sababu kubwa ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vyote hivyo ni visingiziyo vya kumpa mbwa jina baya halafu ukamuuwa. Kama ni ubeberu ilikuwaje Waarabu waliokwenda Afrika Mashariki wakaisahau lugha yao ya Kiarabu na badala yake wakawa wanasema lugha ya Kiswahili? Kama Zanzibar ilikuwa ni kiti cha kwanza cha ubeberu Afrika Mashiriki basi mbona Zanzibar imeendeleya kudhibitiwa na watawala wa Tanganyika hata baada ya kupinduliwa “uhuru wa Waarabu?”

Washirazi na Waarabu hawakuaminiwa kushirikishwa katika Mapinduzi kwa sababu wameingiliyana na kuchanganya damu na Waarabu. Na zaidi ya hilo ni kuwa Washirazi, kama Waarabu, wana asili yenye kutoka bara la Asia kwa hiyo wameonekana kuwa hawana haki ndani ya bara la Afrika. Marekani ni mfano adhimu wa watu waliyohamiya kutoka sehemu mbalimbali za dunia na katika vipindi tafauti. Hivi juzi tu Rais Barack Obama ambaye baba yake mzazi ametoka Kenya na aliyezaliwa na mama mweupe amevunja rekodi zote kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa kwanza mweusi katika nchi ya watu weupe na yenye nguvu kuliko zote duniani.

Vipi leo wenye historia ya zaidi ya miaka elfu mbili wawe wageni Zanzibar au Afrika Mashariki au aliyekuja jana Zanzibar na kuishi kinyume na sharia awe ana haki zaidi ya wenyeji kwa sababu ni “Muafrika?” Basi kwanini asende Uganda au Nigeria akadai kuwa ana haki kuliko wenyeji wa huko na waliyojaribu kufanya hivyo walifikwa na nini? Hata Yesu Kristo na Mtume Muhammad (SAW) wametokeya bara la Asia. Basi wafuasi wao wasizifuate dini zao kwa sababu si Waafrika na ni Waasia?

Zanzibar imefika mahala kuwa haitawaliki isipokuwa kwa chama kimoja cha jamii ya watu wenye mchanganyiko wa karne nyingi na ndani ya mchanganyiko huo imezaliwa lugha ya Kiswahili, dini ya Kiislam, dini ya Kikristo na dini nyenginezo na wasiokuwa na dini, musiki, vyakula, na mavazi tafauti na mambo mengineyo ya kimaisha. Mwalimu Nyerere aliiogopa Zanzibar na akatanguliza dhambi ya ubaguzi wa kuwabaguwa Wazanzibari wenyeji kuwa Zanzibar si kwao bali ni ya Waafrika Wabantu kutoka bara. Sasa dhambi hiyo inaiandama na kuifisidi Tanganyika na Muungano wake na Zanzibar.

Mwalimu Nyerere aliifanya Zanzibar kama haina wenyewe na kuitendeya mambo kama yaliyotokeya katika nchi ya Kusadikika. Matokeo yake Dola ya Tanganyika iliivamiya Zanzibar tarehe 12 Januari 1964 na badala yake tatizo la Zanzibar limekuja kufanywa kuwa ni tatizo baina ya Wazanzibari wenyewe kwa wenyewe na Tanganyika kuwa mpatanishaji na muweka amani. Wazanzibari ambao walionekana kuwa hawana matatizo na ndio maana hawakuweza kuaminiwa kuivamiya nchi yao wamegeuzwa kuwa wakiwachiwa watakuja kuuwana wenyewe kwa wenyewe. Hivyo kweli Wazanzibari wanaweza kulaumiyana kwa mambo waliyofanyiyana wakati chanzo cha fitina walikuwa hawakijuwi?

Sera, agenda, ya “strategic denial” ya Kiingereza ya kuizuwiya Zanzibar isiingiye ndani ya mikono ya maadui wa Uingereza ilirithiwa na kuendelezwa na Dola na Serikali ya Tanganyika kwa kwanza kuibomowa Dola ya Zanzibar iliyobakia, na baada ya muda wa siku 100 kuinyanganya Zanzibar uhuru wake wa kujilinda na kujiamuliya mambo yake ya nje baada ya kuwa na kiti chake Umoja wa Mataifa (UNO) na Jumuiya ya nchi za Commonwealth.

Kwa kifupi Zanzibar ilitoka kwenye mikono ya ukoloni wa Kiingereza ikaingizwa ndani ya ukoloni wa Tanganyika. Utumwa ukawa ni kisingizyo. Uislam ukafanywa ndiyo sababu, na Ukristo ukatangazwa kuwa ndiyo muwokozi wa Muafrika aliyetiwa utumwani na Mwarabu Muislam. Zanzibar ikageuzwa kuwa ni kituo cha kale na cha mwanzo cha ubeberu Afrika Mashariki. Mwalimu Nyerere akapata nafasi aliyokuwa akiitafuta kwa muda mrefu.

Ripoti ya CIA na Mapinduzi ya Zanzibar

Ametahadharisha mwandishi Anthony Clayton katika kifungu cha kwanza cha utangulizi wa kitabu chake juu ya Mapinduzi ya Zanzibar cha mwaka 1981 kwa maneno yafuatayo: “Matukio khasa ya Zanzibar ya mwaka 1964 na baada yake hayakupewa umuhimu unaopaswa kutolewa, zaidi kwa sababu ya kukosekana utafiti wa midani visiwani.”33 Tumekwisha kuelezeya kuwa utafiti wa midani ndani ya Zanzibar una faida na khasara zake kutokana na nani mwenye kuhojiwa na kahusika vipi na chimbuko la Mapinduzi. Kuna mikono na vichwa vya Mapinduzi na asilimia kubwa sana ya utafiti wa Mapinduzi umetokana na mikono yake na kama alivyosema marehemu Mzee Thabit Kombo “na mengine ya uwongo mtupu.”

Alinihakikishiya aliyekuwa mkubwa wa jeshi la polisi la Tanganyika wakati wa Mapinduzi ya Zanzibar, marehemu Mzee Hamza Aziz, kuwa ripoti ya Shirika la Kijasusi la Kimarekani (CIA) ina maelezo mazuri juu ya kuhusika kwa Tanganyika katika mapinduzi ya Zanzibar. Kwa wakati ule hata kama ningelikuwa ninayo ripoti hiyo isingeliweza kunisaidiya sana bila ya utafiti wa midani na utafiti wa midani usingeliweza kunisaidiya kama si kuongozwa na dalili na alama kutoka nyaraka za kitaifa za Uingereza na za Kimarekani.34

Helen-Louise Hunter, mtafiti na mtaalamu wa kiuchumi na kisiasa alikuwa mfanyakazi wa Shirika la Kijasusi la Kimarekani (CIA) kwa zaidi ya miaka ishirini na ni mwandishi wa ripoti ya CIA aliyonigutuwa marehemu Mzee Hamza Aziz. Kwa ripoti iliyoandikwa miaka arubaini na tatu nyuma Hunter alifanya kazi nzuri sana. Kukosekana kwa utafiti wa midani kumemfanya mchambuzi huyo kuufikiya uamuzi ufuatao: “Ingawa viongozi fulani wa ASP, na mwenye kujulikana zaidi ni Hanga, walikuwa wapangaji wa mikakati ya mapinduzi, hawaonekani kama wao ndiyo walioyaanzisha Mapinduzi usiku wa tarehe 11–12 Januari.”35

Hata hivyo Hunter ameandika kuwa: “Mnamo katikati ya mwaka 1963, mara tu baada ya uchaguzi wa Juni [Julai], kikundi cha viongozi wa ASP, akiwemo Hanga, walikwenda Tanganyika kuomba msaada wa pesa na silaha kwa kuunga mkono mpango wao wa mapinduzi.” “Ni dhahiri”, anaandika Hunter, kuwa Mwalimu Nyerere “alijuwa na aliunga mkono jumla ya mpango wa mapinduzi. Inavyoonekana, mapinduzi yalikuwa yamepangwa yafanyike mwezi wa Machi au Aprili 1964.”36

Baada ya kuonyesha kidole lilipo chimbuko la Mapinduzi ya Zanzibar, Hunter ameandika kuwa katika kitu kilichochangiya kuupotosha ukweli wa Mapinduzi hayo ni ile: “Fikra kuwa kufungiwa kwa chama cha Umma Party kiliwaongoza Babu na wafuasi wake kuasi kwa kutumia silaha huenda ikawa ndio kosa kubwa la kutoyafahamu Mapinduzi ya Zanzibar.”37

Msomaji atakumbuka kuwa hata ripoti ya Kamishina Sullivan wa jeshi la polisi la Zanzibar ilianza na kumalizika kwa kumtwisha marehemu Babu na wafuasi wake dhamana kubwa ya kuyaandaa Mapinduzi ya Zanzibar. Khitimisho la CIA kuhusu Babu ni: “…alikuwa ni mtu wa wazi wa kutuhumiwa katika upangaji wa kuipinduwa serikali lakini hakuna ushahidi wa kukinaisha kuwa alikuwa na mchango wa maana kwenye Mapinduzi.”38

Hata baada ya Mapinduzi ripoti ya CIA pia inaelezeya kuwa: “Inavyoonyesha kwa makusudi Rais wa Tanganyika [Nyerere] aliziongezeya chumvi khofu zake kuwa Zanzibar itaingiya ndani ya mikono ya Makoministi; hii ilikuwa hoja ambayo aliweza kuitumiya na kuziridhisha nchi za Magharibi ili kupata kuungwa mkono katika njama zake za kuimeza Zanzibar ndani ya Tanganyika.”39

Mapengo makubwa ya ripoti ya CIA yanatokana na nadhariya kuwa kulikuwa na mipango mingi ya kupinduwa Zanzibar na ule wa Hanga, Kambona na Nyerere, sio uliyotekelezwa tarehe 12 Januari 1964. Kuna sehemu ya ripoti imeandika kwa njiya ya kukhitimisha kuwa “Kiongozi muhimu kuliko wote katika njama [za kupinduwa] alikuwa ni Hanga” na kuendeleya kuwa:

Karume alifadhaishwa bila ya kiasi na mauwaji ya kishenzi na kuibiwa Waarabu na Waafrika katika siku za baada ya mapinduzi lakini alikuwa hakuweza kufanya kitu. Vikundi vyake vya kuweka usalama vilikuwa havifuwi dafu na vikosi vyenye silaha ambavyo vikijinadi kuwa ni wafuasi wa Okello aliyekuwa akiranda sehemu za mashamba, akiuwa na kupora.40

Ripoti inakariri tena na kwa uwazi zaidi kuwa

Inaonyesha kuwa kiongozi muhimu katika mipango ya ASP ya kupanga mapinduzi, alikuwa Hanga ambaye alisaidiwa na memba wa mrengo mkali wa ASP, na khasa watu fulani kutoka vyama vya wafanya kazi na khasa Hassan Nassor Moyo, Katibu Mkuu wa ZPFL na kiongozi ndani ya ASP, alikuwa katika upangaji [wa mapinduzi]. Karume binafsi hakuhusika kabisa; Karume binafsi alikuwa hajahusika kabisa; inawezekana O. [Othman] Shariff na Aboud Jumbo [e] walikuwa hawana habari na mpango [wa mapinduzi].41

Hakuna popote pale ndani ya ripoti ya Hunter ambapo inatajwa Kamati ya Watu 14 chini ya uongozi wa Mzee Karume kuwa ndiyo iliyokuwa imeyaandaa na kuyashika mambo ya Mapinduzi. Hakuna. Majina yanayojichomoza sana ni ya Hanga na Kambona. Kwenye masuala kama haya ni vigumu kuthibitisha kinagaubaga mchango wa Rais au kiongozi wa juu kabisa wa nchi. Daima kiongozi wa juu wa nchi anakuwa na viongozi watekelezaji wa sera waliyokubaliyana pamoja.

Kilicho muhimu ni hakuna mgongano wa aina yoyote baina ya simulizi za wazee wa Mapinduzi na marejeo ya nyaraka za Kitaifa za Kiingereza au za Kimarekani. Hata hivyo kushiriki kwa Mwalimu Nyerere kunathibitishwa zaidi na dondoo zifuatazo:

Katikati ya mwaka 1963 pale Hanga na viongozi fulani wa ASP walipomuendeya [Mwalimu Nyerere] kumuomba msaada wa silaha na kifedha, inasemekana Rais wa Tanganyika aliwakataliya kwa sababu hakufikiri kuwa mpango wao wa kufanya mapinduzi ungelifaulu.42

Ingawa ni dhahiri Nyerere alijuwa na aliuwafik mpango wa mapinduzi kwa jumla, inawezekana Kambona hakumuarifu Rais [Nyerere] mambo madogomadogo. Ipo sababu ya kuamini kuwa [Nyerere] hakuarifiwa kuhusu silaha ambazo Kambona aliwapa ASP.43

Katikati ya mwaka 1963 inasemekana Kambona alimpa Hanga na wafuasi wake bunduki 2 za machine gun na bunduki 10 za aina ya rifle kwa njia ya siri. Kambona pia aliandaa baadhi ya mzigo mwengine wa silaha kutoka Algeria kwenda Tanganyika ambao huenda uliwafikia wanamapinduzi wa Zanzibar, ingawa labda sehemu kubwa ya hizo silaha walikusudiwa wapigania uhuru wa Msumbiji.44

Mzee Aboud “Mmasai” amesimuliya namna yeye na Twala walivyokwenda kuchukuwa silaha nyumbani kwa Kambona na walivyoziingiza Zanzibar kupitiya Bweleo. Suala linalojitokeza ni kuwa Mwalimu Nyerere aliijuwa mipango ya mapinduzi lakini alikuwa ana wasiwasi huenda yasifaulu. Sababu za kuwa na wasiwasi zinaweza kuwa ni kwa sababu ya kumuogopa Muingereza na Gamal Abdel Nasser lakini kutokana na kuwa hao wawili walikuwa ni maadui kulimpa Nyerere mwanya wa kucheza nao kuyafanya Mapinduzi yaliyokuwa na bahati naye kwa sababu Wazanzibari na Watanganyika wengi hawakuzijuwa sababu zake.

Tumeona pia kwenye simulizi za Mzee Aboud “Mmasai” kuwa waliwapelekeya barua viongozi wa nchi za Afrika Mashariki kuwaarifu kuhusu Mapinduzi kabla ya kuingiya mabomani. Hapana shaka barua hizo zilipata muongozo wa wapi pa kuzipeleka kutoka kwa Oscar Kambona. Maelezo yanazidi kuweka mambo sawa: “Kwa mujibu wa ripoti moja, Rais Kenyatta aliarifiwa kuhusu mipango ya mapinduzi lakini alikuwa hakupewa tarehe maalumu lini yatafanyika. Inaonyesha alikubali asilipeleke jeshi la Kenya ikiwa serikali ya Zanzibar itaomba msaada kutoka nje dhidi ya waasi.”45

Mashirikiyano baina ya Hanga na Kambona ni jambo ambalo limethibitishwa mara nyingi na maandishi na watu tafauti na kitabu cha Hunter kinayaunga mkono mashirikiyano hayo:

Ushirika wa Tanganyika na viongozi wa ASP waliyokuwa wakiyapanga mapinduzi ni jambo ambalo limethibitishwa ipasavyo. Hanga na Waziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi wa Tanganyika, Kambona, ni marafiki wa zamani, na waliishi chumba kimoja London. Kwa kuwa [Kambona] alikuwa anataka Waafrika wauchukuwe utawala kutoka kikundi cha Waarabu, alikuwa muda wote anaijuwa mipango ya kupinduwa; aliyaunga mkono mapinduzi kwa silaha na pesa…46

Juu ya umuhimu wa ripoti ya Hunter, bado katika khitimisho lake kuna mgongano baina ya maelezo na tafsiri zisizolingana kama alivyoandika:

Kwa mukhtasari, ingawa kulikuwa na mpango wa mapinduzi zaidi ya mmoja Zanzibar, mapinduzi yaliyofanyika tarehe 12 Januari hayakuwa yale yaliyopangwa na ima Babu na chama chake cha Umma Party, au Hanga na kikundi chake cha ASP. Yalikuwa ni mapinduzi yalozuka tu.47

Sababu ya kuufikiya uamuzi huu wa haraka baada ya kukusanya ushahidi unaweza kuwa umetokana na ugumu wa kupima bila ya ushahidi wa utafiti wa midani baina ya uongozi na viongozi gani khasa walioyapanga Mapinduzi na uongozi na viongozi wengine waliokuja kuchomoza na kuwa wakubwa na majemedari wa Mapinduzi ambao hawakuwa viongozi wa juu ndani ya jiko la Mapinduzi. Na zaidi kuloleta migongano ya nadhariya na tafsiri zenye kugongana ni kuchomoza kwa John Okello ambaye ripoti ya CIA imemueleza kuwa ni “bahati nasibu ya kihistoria.”

 

Odinga Oginga na Mapinduzi ya Zanzibar

Juu ya kuwa majina ya Hanga na Kambona yamekuwa yakitajwa kwa pamoja, kuna majina mengine pia ambayo bado hayakufanyiwa utafiti wa midani na kuthibitishwa. Kwa upande wa viongozi wa Serikali ya Kenya “Ilikuwa ni dhahir kwao kuwa oganaizisheni yenye uwezo mkubwa zaidi kuliko Sheikh Karume ndiyo iliyokuwa na uwezo wa kuyaongoza mapinduzi.”48 Jina la Oginga Odinga ni moja wapo wa majina ambayo yananasibishwa na majina ya Hanga na Kambona na ripoti ya Hunter inamtaja kwa kusema kuwa:

Kumekuwepo ripoti zenye kusema kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya Oginga Odinga alikuwa pamoja na Hanga na Kambona katika kuyapanga mapinduzi…ametamka kuwa [Odinga] amehusika sana [katika mapinduzi] kama alivyohusika Kambona. Kama alivyo na Kambona, Hanga alikuwa ana mahusiano binafsi na Odinga, ambaye alimsaidiya kumpeleka nje kusoma…Kwa hiyo, kuna hisia ya kijumla kwamba huenda Odinga alikuwa ana mkono katika matukio ya Zanzibar ingawa kuhusika kwake kwenye mapinduzi hakujapata kuthibitishwa.49

Jeshi la Kenya lilipoasi tarehe 23 Januari 1963 viongozi wa Uganda waliwasiliyana moja kwa moja na Serikali ya Kiingereza na kuomba msaada na bila ya kuwaarifu au kuwashauri Wakenya.50 Bwana Odinga:

aliposikiya kuwa majeshi ya Kiingereza yako tayari kuondoka kwenda Uganda akasababisha viongozi wakubwa wa Wizara [ya Ndani] kupiga simu Uwanja wa ndege na kuzuwiya ndege isiruke. Kwa bahati nzuri walipiga simu uwanja wa ndege sio. Inawezekana kuwa wakati huu Bwana Odinga alikuwa hajuwi kuwa tumeshaijibu Serikali ya Kenya kuhusu ombi lao la msaada.51

Kwa mujibu wa mwenyewe Bwana Odinga:

Mapinduzi ya Zanzibar yalipangwa na viongozi wake wenyewe na si na mtu mwengine—si na mimi wala Castro au Cuba au yoyote popote pale—pale katiba ilipotengenezwa kuwazuwia Waafrika walio wengi kuweza kuungoa utawala wa Kiarabu kwa njia ya sanduku la kura.52

Odinga hakueleza ni nani kati ya viongozi wa Zanzibar waliyoyapanga Mapinduzi na nini ulikuwa uhusiyano wake na viongozi hao. Kitu kimoja Odinga ametuhakikishiya nacho ni suala la mchango wa Babu kwenye Mapinduzi:

Mara moja Babu alikuja Nairobi na akakaa nyumbani kwangu. Nilijuwa kuwa alikuwa ndio nguvu nyuma ya chama cha Umma na nilikuwa nafahamu kuwa yeye na wenzake walikuwa wanapanga mapinduzi wakati ule lakini sikuwa na hakika ya chochote, na sikuambiwa chochote, na kama ingelitokea kuulizwa rai yangu basi ningelimwambia Babu kuwa ningelipendeleya kumuona ndani ya uongozi wa chama cha Afro-Shirazi. Ni kinyume na vyombo vya habari vyenye kuandika kuwa nilikuwa nyuma ya Babu ambaye alikuwa nyuma ya mapinduzi ya Zanzibar.53

Babu asingeliweza hata siku moja kuingizwa ndani ya uongozi wa Afro-Shirazi kwa kupewa cheo cha Ukatibu Mkuu ambacho kilikamatwa na Mzee Thabit Kombo ambaye alikuwa ni alama ya nguvu za Washirazi ndani ya ASP. Odinga, Kambona na Nyerere wakisumbuliwa na siasa ya kufarakanisha ya Pan-Africanism yenye kuwabaguwa Wazanzibari wenye asili ya Kishirazi na ya Kiarabu ikiwa walikuwa ni wapenda au wapinga maendeleo. Kichekesho cha historia ni kuwa ubaguzi wa kuwabaguwa Wazanzibari kuwa si Waafrika kwa maana wanayoitaka wao, ndiwo uloipa Tanganyika hadhi ya uongozi katika suala la Umoja wa Afrika! Maneno ya Odinga yamefika ulingoni:

Hapana shaka yoyote kuwa mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari 1964 ni tukio kubwa la Afrika Mashariki. Huu ulikuwa mwanzo wa tishio kubwa la vita baridi Afrika Mashariki. Athari juu ya Tanganyika na Kenya kutokana na matukio ya Zanzibar baadae yalikuwa yenye msisimko wenye kutafautiana: Tanganyika ikaelekeya kunako sera za Umoja wa Waafrika zenye msimamo mkali zaidi; Kenya ikachukuwa mkato mwengine kuelekeya kwenye siasa za kihafidhina.54

Zanzibar iliyovamiwa ikawa ni sababu ya sera tafauti baina ya Tanganyika na Kenya. Kenya ilibidi ichukuwe siasa za kihafidhina kwa sababu ikitambuwa Tanganyika iliifanyiya nini Zanzibar. Kichekesho kikubwa zaidi ni vipi dola za Mashariki, Urusi na Uchina zilirukiya kuyasaidiya Mapinduzi ambayo yaliungwa mkono na wakoloni wa Kiingereza. Na ikiwa wazungu wakiujuwa msimamo wa Babu na Makomred na kuwaogopa, kwanini waliachiliya maingiliyano na ASP na Mapinduzi? Kwanini Umma Party walihitajika? Kuufunika mkono wa Tanganyika na kuiwachiya Zanzibar imezwe na Tanganyika kwa kisingiziyo cha kuwaogopa Makomred? Inaonyesha hiyo ndiyo ilikuwa sababu ya kuwaweka mbele na kuwatumiliya Makomred. Viongozi wa Kiafrika, wa Kiarabu na wa Kiyahudi, Waislamu na Wakristo, Waafrika na Waarabu, pamoja na wanamapinduzi wenyewe, wote na bila ya kujuwana walikuwa ndani ya kambi moja katika kuipinduwa Dola ya Zanzibar.

Katika vurugumechi ya Zanzibar ni Tanganyika peke yake iliyoweza kuibuka mshindi kwa kuungwa mkono na Dola ya Uingereza kwa kumuokowa Nyerere na kumrudisha madarakani baada ya uasi wa kijeshi na kumuachiya aidhibiti Zanzibar hata baada ya kuwa na hakika Mapinduzi ya Zanzibar yalipangwa Tanganyika.

Nchi za Magharibi zilikawiya kuitambuwa Zanzibar ya Mapinduzi kwa sababu ya kuchomoza John Okello ambaye alikuwa hajulikani na mtu. Nyerere pia alikawiya kuitambuwa serikali mpya ya Zanzibar kwa sababu hali ya uongozi uliyochomoza na Okello, na khasa wa Babu, ulikuwa ni tishio kwa siasa ya kizalendo ya Kiafrika ambayo ilimuona Babu na wafuasi wake kama ni Wazanzibari Waarabu hata kama walikuwa na siasa za kimaendeleo.

Tarehe 17 Januari 1964 Mwalimu alipeleka Zanzibar askari 100 kutoka Tanganyika. Tarehe 20 Januari yeye mwenyewe akapinduliwa na jeshi la Tanganyika pamoja na vyama vya wafanyakazi. Tarehe 13 Januari Kenya iliyokubaliwa uwanachama wake siku moja na wa Zanzibar iliitambuwa serikali mpya ya Zanzibar Jumatatu tarehe 13 Januari 1964. Nyerere hakuitambuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar mpaka tarehe 23 Januari 1964 baada ya kuokolewa na Waingereza. Muingereza alisubiri na hakuitambuwa serikali mpya ya Zanzibar mpaka tarehe 23 Februari. Alikuwa akiidurusu hali ya kisiasa kutoka kwa Nyerere na kumuunga mkono Karume dhidi ya wanamapinduzi waliyokuwa na misimamo mikali dhidi ya nchi za Magharibi. Nchi za mirengo ya siasa za mkono wa kushoto ambazo hazikuwa na mchango wowote katika mapinduzi ya Zanzibar zikawa ndiyo za kwanza kuitambuwa serikali mpya ya Zanzibar.

 

Ubeberu wa Nyerere na Mapinduzi ya Tanganyika

Wakati Mapinduzi yameshamalizika na siku sita kabla ya Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar, J. D. B. Shaw wa Commonwealth Relations Office, Downing Street, alimuandikiya barua Naibu Balozi wa Kiingereza wa Tanganyika, Stephen Miles, kutaka kujuwa kama: “…mtizamo wa Serikali ya Tanganyika kwa vikundi vya wapiganiya uhuru tafauti walivyovikaribisha katika eneo lake umeathiriwa na kufuzu kwa Mapinduzi ya Zanzibar ambayo yamepangwa (mounted) kutoka Tanganyika.”55

Kupinduliwa kwa Zanzibar kulikokuwa hakujulikani na waliyo wengi, kulimpatiya sifa kubwa Nyerere na kuiweka Tanzania katika mstari wa mbele wa ukombozi wa Afrika. Maafa ya Zanzibar yaligeuka na kuwa ni neema kwa jina la Nyerere na la Tanzania. Waingereza walitaka:

…maamuzi yote muhimu ya kuulinda muungano yafanyike Dar es Salaam. Rais Nyerere amejitahidi sana kuuonyesha umuhimu kwake wa hii khatuwa ya kwanza kuelekeya Umoja wa Afrika. Kushindwa kuulinda Muungano kutamvunjiya sana hishima yake.56

Wakati Tanganyika, na baadaye, Tanzania, ikijivuniya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwalimu Nyerere kumnukuu Mzee Aboud Jumbe waziwazi kuhusu sababu zilizowafanya Wazanzibari kukamata mapanga kumwaga damu yao wenyewe na ya wenziwao ili waepukane na Usultani, na kushadidiya kuwa Tanganyika haikushika mapanga bali iliupata uhuru wake kwa njiya ya amani, nchi na jina la Zanzibar liliendeleya kudidimiya na kufifiya na la Tanzania kupanda chati duniani. Lakini bado kulikuwa kuna wasiwasi wa kumaliza kazi.

Kuimaliza kazi na kuweza kuidhibiti Zanzibar ipasavyo kulihitajiya kufanyike mambo matatu muhimu. La kwanza, ambalo liliungwa mkono na Uingereza, lilikuwa ni kuifanya Zanzibar iwe na sifa ya Mkoa. P. A. Carter wa Commonwealth Relations Office ameweka wazi:

Tumekubaliyana na mtizamo wa jumla kuwa inawezekana kuiendesha Zanzibar chini ya mfumo wa idara wa jimbo. Nakumbuka Kambona aliwahi kunitajiya zamani kidogo alipokuwa akinungunika kuhusu mtizamo wa serikali ya zamani ya Zanzibar kuhusu Shirikisho la Afrika Mashariki kuwa Zanzibar itizamwe na iendeshwe kama jimbo lolote lile la Tanganyika. Mafia ni sawasawa na ukubwa wa Pemba na inaendeshwa na Mkuu wa Wilaya chini ya Mkuu wa Mkoa uliyopo Dar es Salaam. Namnukuliya barua hii Le Bretom ambaye anaweza, kutokana na uzowefu wake wa Zanzibar na ilimu yake ya mfumo wa majimbo ya Tanganyika, akupe fikra zaidi kuhusu njiya muruwa ya kuiweka Zanzibar.57

Jambo la pili ambalo Kambona alilisimamiya kwa nguvu ni kuzishusha hadhi Balozi zilizokuwepo Zanzibar na kuziweka kunako mustawa wa Consulates. Ubalozi wa Uingereza uliyokuwapo Dar es Salaam umesajili:

Katika mazungumzo mafupi ambayo Balozi wa Kimarekani na mimi tulokuwa nayo na yeye [Kambona] tarehe 11 Juni wakati wa kuondoka Rais [William] Tubman, tulimhimiza atupe taarifa ya tarehe ya kuziteremsha balozi zote. Ameahidi atafanya hivyo na siku ya pili alipokuwa Nairobi alinukuliwa katika magazeti akisema kuwa ameshachaguwa tarehe ya kufanya hivyo. Tunaisubiri taarifa.58

Kuziteremsha Balozi ziliyopo Zanzibar na kuzifanya ziwe Consulates kulikwenda sambamba na kukifuta kiti cha Zanzibar katika Umoja wa Mataifa. Hili tutalizungumza kunako mlango ujao katika safari yetu iliyotubakiliya.

Jambo la tatu (na mengineyo) ambalo lilikuja kufanyika baadaye ni kulidhibiti jeshi la Zanzibar ambalo “Nyerere amekiri kuwa linamtiya wasiwasi mkubwa.”59

Juu ya mambo yote hayo bado Waingereza na Nyerere walikuwa wana wasiwasi kwa sababu:

Midam Zanzibar inaendeleya kujiendesha kama ni Nchi Huru, Muugano baina ya Tanganyika na Zanzibar utakuwa hauna nguvu. Rais Nyerere kama ni Mkubwa wa Muungano anajaribu kuwavuta Mawaziri wa Zanzibar waulinde Muungano. Kuna wakati utafika itambidi ama akubali kuuvunja Muungano au aombe msaada kutoka nje umsaidiye kuutekeleza.60

Waingereza walimtathmini Mwalimu kuwa “Kisaikolojiya hapendi kuchukuwa maamuzi yasiyofurahisha na yenye msimamo mkali.”61

Huko nyuma Tanganyika, na baadae Tanzania Bara, hazijawahi hata mara moja kukiri kuwa zilihusika katika mipango ya kuipinduwa Dola ya Zanzibar na Muungano uliyofuatiliya. Wako watakaofanywa waseme kuwa Tanganyika ilitowa msaada tu kwenye Mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari 1964 kwa kushirikiyana na watu wa Bara lakini siyo iliyoipinduwa na yenye kuendeleya kuidhibiti Dola ya Zanzibar isinyanyuke tena. Hoja itazungumza: kwani akina Hanga, Saadalla, Twala, Mmasai na wengineo hawakuwa Wazanzibari? Hoja itasahau kuuliza: kwani utawala wa Zanzibar ulirudi kwao? Wapangaji mikakati wa hoja wasisahau kuwa kuna mgongano mkubwa baina ya kusema kuwa Mapinduzi ya 1964 ya Zanzibar yalipangwa na Wazanzibari wenyewe halafu ukautaja mchango wa Dola ya Tanganyika!

Hoja huvunjwa na hoja. Hoja kuwa Zanzibar ilisaidiwa tu kwenye mapinduzi huenda ikapewa sauti mpya na kupokelewa na baadhi ya waandishi wa habari ili kipatikane kikundi au hata chama cha kisiasa kipya bara na chenye nguvu Zanzibar ambacho kitakuja kuzipinga juhudi za Wazanzibari kuwa kitu kimoja. Ripoti ya shirika la ujasusi la Kimarekani, CIA, imeandika bila ya kumumunya au kutafuna maneno:

Kwa miaka mingi, Watanganyika, akiwemo Nyerere, walikuwa na fikra kuwa Zanzibar ni hakika sehemu ya Tanganyika. Walikuwa wanaingojeya siku serikali ya Kiafrika itakapokamata utawala Zanzibar ili waziunganishe nchi mbili. Inaweza kuwa ni hamu ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar kulikomfanya Nyerere ajiingize ndani ya siasa za Zanzibar kutokeya mwanzo, kuanziya mwaka 1956. Ingawa [Nyerere] hatokiri kuwa maamuzi yake juu ya Zanzibar ni ya kibeberu, inaweza hili likawa ndio motisha yake kuutaka muungano. Ni wazi hivi sasa, na kama si zaidi huko nyuma, kuwa muungano uliokuwa kichwani mwa Nyerere ulikuwa ni ule ambao yeye na Watanganyika watautawala. Kwa sababu zilizo wazi, hakumuarifu Karume kuhusu masala hayo kabla ya muungano. Karume hakuwa na fikra iliyo wazi kuhusu aina ya mahusiyano yaliyokusudiwa na hakuna shaka yoyote kuwa hakutarajiya muungano wa mkazo kama alivyofikiriya Nyerere.62

Odinga Oginga wa Kenya pia anathibitisha kuwa:  

Tanganyika ambayo maisha ilikuwa ikiteteya umoja baina ya kisiwa [Zanzibar] na bara [Tanganyika]—na ilivyo, TANU, ilichukuwa hatua zilizomalizikiya kuundwa kwa nguvu za Afro-Shirazi—ilikuja kuisaidiya Zanzibar na kuuteteya sio uhuru wake kamili, bali kuipa nguvu Tanganyika kujiamuliya sera zake zilizo huru na bila ya kushawishiwa na upinzani wa kibeberu wa mabadiliko yaliyotokeya Zanzibar.63

Sio tu kuwa Mzee Karume hakuukubali Muungano utakaoifuta Zanzibar, bali hata hakushirikishwa katika Mapinduzi yaliyokuja kuibomowa na kuifuta katika ramani ya dunia Dola ya Zanzibar. Hata kama kisiasa alikubali kuupokeya ukubwa kuwa yeye ndiye alikuwa Jemedari wa Mapinduzi ya Zanzibar, ni wazi kuwa waliyompa cheo hicho walimpa kwa sababu zao na yeye alikipokeya kwa sababu zake. Ukweli ni kuwa:

Karume katamka kwa kujiamini kuwa tafsiri ya muungano na Tanganyika siyo aliyokuwa nayo yeye. Yeye [Karume] na viongozi wengine wa Zanzibar sasa wameweka wazi kuwa wameazimiya kuwa wao na nchi yao hawatojidhalilisha kwa Tanganyika. Hata Hanga, ambaye anauunga mkono sana muungano katika Wazanzibari, ambaye anadai kuwa ni mpishi wa muungano wa Tanganyika na Zanzibar pamoja na Kambona kutokeya walipokuwa wanafunzi London, amesema kuwa Watanganyika ni wajinga kama wanafikiriya kuwa watautawala muungano; wanapoteza wakati wao kuja Zanzibar kujaribu kutuambiya kipi cha kufanya. Karume hatokubali hata siku moja kuchukuwa amri kutoka kwao.64

Lakini hizo hazikuwa fikra za Nyerere na wenzake wa Tanganyika. Kuonyesha hamu ya kuwa na muungano watakaoutawala wao: “Nyerere na Kambona na viongozi wengine wa Tanganyika wamesema kuwa hawatokubali, chini ya dhurufu zozote zile, kuvunjika kwa Muungano, na kuwa wako tayari kuulinda kwa thamani yoyote ile hata ikibidi kuingiliya kijeshi…”65

Tanganyika inaweza kuingiliya kijeshi kwa kukitumiliya kipengele cha Katiba kwa ajili ya kuilinda hali ya amani na utulivu Zanzibar. Wazanzibari wachache wenye kupendeleya fujo kwa kujipatiya mavuno ya kisiasa ndiwo wa kutahadhari kutowapa viongozi wa Tanganyika wasiyoitakiya mema Zanzibar kuivamiya tena kwa mantiki ileile ya 1964 na Mapinduzi mengine yaliyofuatiliya.

Waingereza ambao walikataa kuingiliya kuzuwia mauwaji ya halaiki punde baada ya Mapinduzi ya 1964 kwa kusema kuwa matatizo ya Zanzibar yalikuwa ni ya baina ya Wazanzibari wenyewe kwa wenyewe na hayakutoka nje, walitambuwa kuwa kulikuwa na mchango kutoka Tanganyika. Chenye kustaajabisha ni Kamishna Sullivan hakuyataja hayo kwenye ripoti yake juu ya Mapinduzi ya Zanzibar aliyoiandika tarehe 17 January 1964. Kutokeya mstari wa kwanza mpaka mstari wa mwisho wa maelezo yake aliukamata uzi ule ule kuwa Makominist [Makomred] ndio waliofanya Mapinduzi wakati ripoti nyengine ya Kiingereza imeandika kuwa:

Tunaendelea kupokeya ushahidi wa mchango fulani wa Tanganyika katika mapinduzi kutoka kwa vyanzo tafauti wakiwepo maofisa wanne wa Kiingereza kutoka Zanzibar ambao hivi sasa wako Dar es Salaam, nao ni Sullivan (Kamishna wa Polisi), Waring, Derham na Misra.66

Isitoshe, kulikuwa na ripoti nyengine ambayo inashuhudiya kuwa watu kutoka Tanganyika walikwenda Zanzibar kushiriki katika Mapinduzi na ushahidi wa silaha za jeshi la polisi la Zanzibar ambazo zilikamatwa Tanganyika:

Inaaminika kuwa Waafrika kutoka Tanganyika wamekwenda Zanzibar kushiriki katika mapinduzi. Inajulikana kuwa baadhi ya Waafrika walobeba silaha wamerudi Tanganyika kwa njiya ya bahari Jumapili usiku baada ya mapinduzi na silaha zao zikakamatwa na askari wa Tanganyika. Ofisa wa Kiingereza aliyekuwepo Dar es Salaam amemuonyesha Waring orodha ya silaha zilizokusanywa na Waring aliitambuwa nambari ya bunduki aina ya Sterling ambayo ilikuwepo Zanzibar ndani ya ghala la silaha la [PMF].67

Mbali ya ushahidi wa bunduki moja iliyokamatwa Tanganyika ambayo ilikuwepo Zanzibar “ndani ya ghala la silaha la [PMF]” kuna watu walionekana kuondoka Zanzibar asubuhi baada ya kuimaliza kazi waliokwenda kuifanya usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili tarehe 12 Januari 1964:

Kiasi ya saa 5:45 za Jumapili asubuhi, Waring aliiyona meli ndogo yenye uwezo wa kubeba watu 100 ikiondoka kwenye gati ya Zanzibar. Mkuu wa Idara wa Zanzibar Steven (ambaye bado yuko Zanzibar) amesema kuwa [meli] ilikuwa ikipeperusha bendera ya Tanganyika. Uwezekano uliopo ni meli hii ilikuwa inawarudisha wanamapinduzi wa Kitanganyika Tanganyika.68

Waingereza pia walijuwa kuwa silaha kutoka Algeria alipelekewa Nyerere na zilipelekwa Zanzibar na kutumika katika Mapinduzi. Hii ni kinyume kabisa na maelezo ya miaka yenye kusema kuwa wanamapinduzi walitumiya mapanga na mashoka peke yake pale walipoyavamiya maboma ya jeshi la polisi ya Ziwani na Mtoni:

Maofisa wa polisi wa Kiingereza wanakisiya baina ya watu 200 na 300 waliyashambuliya makaazi ya askari polisi wa Ziwani, na kiasi ya idadi hiyohiyo ilikishambuliya kituo cha [PMF]. Sullivan anasema kuwa wapinduzi walikuwa tayari wana silaha na wakizipiga silaha za automatic kabla ya kuingiya ghala ya silaha na kuziiba silaha za polisi. Silaha kutoka Algeria zinatiliwa shaka kutumika.69

Na pia:

Tumeripoti kabla kuwasili Tanganyika katika miezi ya karibuni shehena ya ndege mbili ziloleta silaha kutoka Algeria na meli kutoka Algeria iliyokuwepo hapa wiki iliyopita. Inaaminiwa kuwa silaha zote kutoka kwenye meli zimefungiwa na kikosi cha Tanganyika Rifles. Djoudi, kiungo cha ubalozi wa Algeria Dar es Salaam alikuwepo Zanzibar kabla ya mapinduzi, na aliondoka Zanzibar kurudi Dar usiku wa Jumamosi. Lakini aliona haya sana na inawezekana sana kuweko kwake Zanzibar wakati ule ilikuwa ni sudfa tu. Hisiya yetu siku zote ilikuwa silaha za Algeria zilikuwa kwa ajili ya wapiganiya uhuru wa Mozambique, na kama kuna silaha zozote walipelekewa wapinduzi wa Zanzibar, basi ilifanyika bila ya Waingereza kujuwa.70

Chanzo kinasema kuwa kulikuwa na harakati kubwa za kijeshi Bagamoyo katika siku za kukaribiya Mapinduzi ya Zanzibar. J. J. Mchingama alituelezeya kuhusu gari lililopita kwa kasi kubwa kituo cha polisi cha Fuoni na nyuma yake aliwaona watu waliovaa nguo nyeusi na kujipaka rangi nyeusi. Uthibitisho wa kupelekwa maofisa fulani kutoka jeshi la Tanganyika Zanzibar umo kwenye maelezo yafuatayo:

Maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wa Tanganyika waliwaambiya maofisa fulani wa Kiafrika na N.C.Os wa Tanganyika Rifles Ijumaa tarehe 10 kuwa huenda wakahitajika kwa operesheni maalumu nje ya Tanganyika. Ushahidi huu na mwengineo unaitiliya nguvu fikra kuwa Kambona alihusika kwenye mpango [wa mapinduzi]. Kwa kweli tuna habari kutoka kwa ofisa mmoja wa Kiingereza aliyoko wizarani kuwa Kambona amejuwa kinachoendeleya siku ya Jumamosi. Waziri wa Mambo ya Ndani Lusinde hakika atakuwa amehusika. Katika miezi ya karibuni alimsaidiya Babu na marafiki wengine kutumiya vyombo vya polisi kuwapeleka baina ya Zanzibar na Tanganyika na kuwapa pasi za kusafiriya nje. Hakuna (hakuna) ushahidi mpaka sasa hivi kama Nyerere na mawaziri wengine wamehusika. Labda Odinga ambaye yuko karibu sana na Kambona atakuwa amehusika kwa upande wa Kenya, lakini pia hakuna ushahidi madhubuti.71

Huu wote ni ushahidi kuwa Tanganyika ilihusika kikamilifu katika kuipinduwa Dola ya Zanzibar, na kama alivyosema Mzee Aboud “Mmasai”, kuwa hata kama Muingereza hakuijuwa mipango ya Mapinduzi kwa tafsili zake basi alijuwa kuwa yatatokeya, na hakuchukuwa hatuwa yoyote ya kuyazuwia au kuyazuwiya mauwaji ya halaiki. Muingereza hakushiriki katika kuipinduwa Dola ya Zanzibar bali alishiriki kwa kujuwa kinachoendeleya na kuamua kutofanya kitu kwa sababu Uingereza ilikwishaamua kuutowa mkono wake Zanzibar na kuiwachiya Zanzibar itawaliwe na Tanganyika.

Ni sawa na watu wazima waliyokaa kitako karibu ya hodhi la maji na waka-muona mtoto mchanga anatambaa kuelekeya kwenye hodhi na wakaamua kutizama upande wa pili. Ushahidi wa kushiriki kwa Muingereza kwenye Mapinduzi ya Zanzibar ni ushahidi wa uamuzi wa kutochukuwa hatua ya kukizuwiya kile ambacho wakijuwa kitatokeya ambacho walitaka kitokee kwa sababu walijuwa kitamalizikiya wapi, kwa nani, na kwa nini. Kwa mujibu wa marehemu Nassor Abdalla “Mlawwaz” zilikuwepo taarifa zilotiwa saini kuwa Edington Kisasi na memba wa jeshi la polisi walikuwa wakifanya mikutano lakini hakukuchukuliwa hatuwa yoyote.72

Inavyoonyesha kitengo cha Usalama cha Jeshi la Polisi la Zanzibar kilikuwa kimekufa au kimeuliwa kwa makusudi. Kwa mujibu wa Mzee ambaye hakuta jina lake lijulikane, Mkurugenzi wa Usalama wa Tanganyika, Emil Mzena alikuwepo Zanzibar wakati wa mapinduzi. Regional Police Commander wa Dar es Salaam, Samuel Pundugu pia alikuwepo Zanzibar na alikuwa ameshukiya kwa Omar Hassan. Mzee mwenyewe alishukiya kwa Rajabu Suwedi.

Saleh Saadalla, kiongozi mtendaji wa mapinduzi aliwahi kufanya mikutano Dar es Salaam katika nyakati tafauti na Hanga, Pili Khamis, Muhiddin Ali Omar, Seif Bakari, Saidi Idi Bavuai, nk. Ilokuja baadaye kujipa na kujulikana kwa jina la Kamati ya Watu 14 ilikuwa bega kwa bega na Saleh Saadalla, Abdalla Kassim Hanga na Abdulaziz Twala. Mapinduzi yanatokeya Mzee Abeid Amani Karume alikuwepo nyumbani kwa Mzee Abbas Sykes ambaye wakati huo alikuwa ni Regional Commissioner wa Dar es Salaam.

 

TANU Hawakutaka Kujulikana—Mzee Ally Sykes

TANU ilimsaidiya sana Karume katika mambo ya siasa za Zanzibar. Kambona alikuwa anataka kuchukuwa utawala wa nchi hii na Nyerere aliona kama Kambona anaweza akamuweka pembeni. Kambona alisahau kuwa ni mimi na kaka yangu Bwana Abdulwahid Sykes na Bwana Dossa Aziz tulomsaidiya kupata kazi katika TANU. Na wakati huo Kambona alikuwa bado anafanya kazi Dodoma na Nyerere alikuwa akifanya kazi St. Francis, Pugu, hapa Dar es Salaam.

Wakati ule TANU haikutaka kuonyesha kwamba wao ndiwo walofanya njama za kupinduwa Zanzibar. Hawakutaka kujulikana wanafanya kitu gani. Ilikuwa kama ni kitu cha siri maana yake. Tulikuwa sisi wote hapa. Nyerere asingeliweza kufanya kitu peke yake bila ya kuwa sisi hapa. Alikuwa hawezi kufanya kitu peke yake. Manake yeye kaletwa hapa na sisi ndiyo tulomsaidiya mpaka akafika pale alipo. Asingeliweza kufanya kitu chochote bila ya sisi kumsaidiya, marehemu Bwana Abdul Sykes, mimi, Dosa Aziz, John Rupia, Bwana Bakari wa Tanga.

Baada ya kupatikana Zanzibar, yale mapinduzi tulivyoyapata, tuliposhinda, sasa ilikuwa hawa kina Nyerere na wenzake walichukuwa kiti cha mbele zaidi kuonyesha kwamba wao walifanya peke yao. Kwa hiyo Bwana Abdu hakupendeleya kujionyesha kwamba kulikuwa na kitu gani. Na hakupenda yatokee mambo ya kutofahamiyana. Bwana Abdu aliyaunga mkono mapinduzi ya Zanzibar. Aliyaunga mkono sana kupita kiasi. Pia nataka ufahamu kuwa Karume asingeliweza kumpata Nyerere bila ya Bwana Abdu kwa sababu Bwana Abdu ndo alokuwa karibu kidogo na Karume kwa sababu Bwana Abdu alikuwa na sauti kubwa katika TANU. Afro-Shirazi isingeliweza kuendeleya na siasa zake Zanzibar bila ya msaada kutoka Tanganyika. Alipokuwa anakuja Dar es Salaam Karume alikuwa akishukiya kwa Bwana Abbas Sykes. Karume akijitiya tu kama alihusika na mapinduzi lakini zaidi aliyekuwa akiyafanya mambo hayo ni akina Babu ambaye alihusika kidogo. Babu alikuwa ni mwanasiasa na aliona kuwa Wazanzibari wengi waliwekwa nje na Waarabu. Hakupendeleya hivyo.73

Msituonee—Mzee Badawi Qullatein

Tulikuwa wakweli kwa kile tulichokiamini nacho ni Usoshalisti. Mtuhukumu kwa hilo na msituonee kwa kusema kuwa tulikuwa waongo au wanafik. Kama kuna kosa basi iwe kwa kuutizama Usoshalisti kama ni idiolojiya na baadaye sisi.

Hanga alileta Warusi kuandika Katiba na Twala aliwaambiya kuwa Zanzibar iwe na uhuru wa kujiamuliwa (autonomous). Wakamwambiya Hanga na Hanga akamwambiya Twala “Brother Twala kwani wewe huungi mkono muungano?”

Wachina hawakuunga mkono muungano. Warusi waliuunga mkono. Chou En Lai alimshauri Karume asikubali muungano. Alimuambiwa ajenge strong base ndani ya Zanzibar. Piya alimuambiya asiunganishe vyama.

Alipokuwa Waziri, Twala aliomba nafasi ya kwenda kusoma nchi za Mashariki na za Magharibi. Haikuwa siri lakini walikwenda kuziiba fomu zake za kuombeya nafasi ya kusoma na kumuonyesha Ali Mahfoudh na baadaye Karume.

Hanga alikuwa myenyekevu sana kwa Oscar Kambona kwa sababu Oscar akimfadhili sana na kumlipiya kukaa Rex Hotel Dar es Salaam na mambo mengineyo. Hanga alikuwa hana maana. Akikopi na alikuwa hawezi kuwasilisha hoja.

Oscar alikuwa ni mbaguzi na opportunist [mbinafsi]. Hakuwa Msoshalisti wala mpenda maendeleo. Alikuwa anataka ulwa tu.

Niliishi na Twala na kulikuwa hakuna vizingiti baina yetu. Nilimpa baadhi ya makabrasha yenye kufundisha namna ya kutengeneza mabomu. Amur Dugheshi alimfundisha namna ya kutumiya silaha ingawa alikuwa amepata mafunzo kutoka sehemu nyengine pia.

Kuna vijana wenye kusema kuwa mapinduzi yasingeliweza kufanyika bila yetu. Tarehe za mapinduzi zilikuwa zikibadilika kila siku. Tulimpelekeya salamu Babu alipokuwa Dar es Salaam. Sisi hatukuitegemea Umma Party baada ya mapinduzi. Ali Mahfoudh aliona keshafika na sisi tuliamini kuwa bado. Tulijuwa kuwa hatutokwenda naye Karume mpaka mwisho. Asingelikubali Babu awe Katibu Mkuu wa ASP. Akimtaka Thabit Kombo kwa sababu akikubalika kwa Washirazi. Akijuwa kuwa Washirazi waliyosoma walikuwa hawamtaki.

Siku ya mapinduzi Aboud Jumbe alikuwa anasitasita kuunda serikali na alisema “tuwangojee wenyewe.” Mimi ndiye niliyeandika majina ya Baraza la Mawaziri. Alikuwepo Twala, Okello, na Jumbe. Watu wa Saleh Saadalla waliingiya mabomani na akina Bavuai na wengineo ambao walikuwa Wazanzibari.

Babu alipewa Uwaziri wa Mambo ya Nchi za Nje kwa sababu kilikuwa cheo cha Ali Muhsin. Khamis Abdalla Ameir alipewa cheo kwa sababu ya Chama cha Wafanyakai (FPTU), na Mohamed Mfaume pia.74

 

Sultan Jamshid kutupwa Uingereza

Mervyn Vice Smithyman aliwasili kwenye meli ndogo ya “Salama” saa tatu na robo za asubuhi na akamkuta Sultan Jamshid ameshafika “lakini wakubwa wa Serikali walikuwa hawapo. Kutofika kwao ulikuwa ni mwisho wa tamaa zote za kuirejesha Serikali halali.”75

A. W. Hawker alikuwa ni Katibu Mkuu wa Fedha katika serikali iliyopinduliwa ya ZNP-ZPPP na Smithyman alikubaliyana na Hawker kuwa akishindwa kufika kwenye meli ya “Salama” achukuwe nafasi yake kwa niaba. Wakati huo Mawaziri wote walikuwa wako nyumbani kwa Smithyman. Hawker ndiye aliyemuarifu T. S. Crosthwait wa Ubalozi wa Kiingereza uliyokuwepo Vuga, Zanzibar, kuhusu mripuko wa Mapinduzi. Hawker baada ya Mapinduzi akawa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais. Kuhusu Mawaziri kwenda kwenye meli na kuungana na Sultan Jamshid, Hawker ameandika hivi:

Kiasi ya [Jumapili] saa tisa za mchana Kamishna wa Polisi aliniambiya kuwa atamalizikiwa na risasi baada ya dakika 10 na baada ya hapo anapendekeza kuondoka Malindi na kwenda kupanda meli ya ‘Salama.’ Nikautuma ujumbe huu kwa Waziri Mkuu ambaye aliutaka ushauri wangu. Nilimuuliza nini ilikuwa tathmini yake na kama anafikiriya kama Serikali yake itaweza tena kutawala Zanzibar. Akasema kuwa anafikiriya kuwa hawatoweza; lakini kama yeye na Mawaziri wawili wataweza kuungana na Sultan na Smithyman kwenye meli ya ‘Salama’ bado watakuwa ni serikali yenye kutambulikana na wataweza kufanya kazi mbali ya Kisiwa cha Zanzibar. Nikamshauri Waziri Mkuu kuwa sifikirii tena kama hilo litawezekana kutokana na suala la usalama wao. Nikamshauri zaidi kuwa ikiwa ni fikra ya Waziri Mkuu na viongozi wenzake wakubwa, wenye wafuasi kidogo, kuwa hawatoweza kutawala tena Zanzibar, basi kwa nini asifikiriye kujiuzulu rasmi ili mapigano yasite na kuokowa maisha ya watu na mali. Waziri Mkuu akashauriyana na wenzake na akanambiya kama hakuna uwezekano wa kupanda meli ya ‘Salama’ basi atajiuzulu, ikiwa atahakikishiwa usalama wake na wa wenzake na familia zao. Akaniomba niufikishe ujumbe wake upande wa pili [wa ASP]. Akaniambiya pia nimuarifu Sultan kuhusu niya yake na nimshauri aendelee katika moja ya meli za Serikali katika moja wapo ya bandari za bara.76

Saa tisa kasorobo za jioni ulipokelewa ujumbe ndani ya meli ya Salama kutoka kwa Hawker kwenye Ubalozi wa Kiingereza wa Zanzibar wenye kusema “Tunatarajiya mazungumzo na Abeid Karume, na pia tuna mawasiliyano na Mawaziri. Kwa hisani yako musipeleke, narudiya, musipeleke ujumbe wowote kutoka ‘Salama’ kuomba msaada kutoka nje Mwisho.”77

Maandishi na kauli nyingi sana zinajirudiya kwa kusema kuwa Mapinduzi ya Zanzibar yalikuja kuung’owa Usultani ambao ulikuwa ukilindwa na Muingereza. Hata kabla ya akina Sheikh Ali Muhsin kungiya siasa za kupiganiya uhuru wa Zanzibar, Waingereza walikuwa wameshagutuka kuwa utawala wa Kifalme wa Zanzibar ulikuwa umeshaingiwa na hamasa za kizalendo za kudai uhuru. Ukweli huu unaonekana wazi kutokeya mwaka wa 1950 wakati wa uongozi wa Sayyid Seif bin Hamoud bin Feisal na kuendeleya.

Dalili zilizo wazi za Waingereza kutompenda Sultan Jamshid ni nyingi. Moja wapo ni pale walipomuombeya kwa Mwalimu Nyerere ampokee Dar es Salaam baada ya kukataliwa na Odinga Oginga kushuka Mombasa kwa khofu ya kuzusha maandamano ya kumuunga mkono kutoka kwa waliyokuwa raia zake. Angaliya namna Muingereza alivyokuwa akimzungumza Sultan ambaye anaambiwa alikuwa akimlinda:

Nina hakika kikundi cha [mfalme na watu wake] wanataka waondoke [Dar es Salaam] haraka. Wao hawataki kubakia na ni fedheha kwa Watanganyika na kwetu sisi.78

Nimezungumza na makamo wa Raisi [Kawawa] ambaye anatutizama sisi tupange safari ya [Sultan na watu wake] nje ya Tanganyika bila ya kuichelewesha. Kuweka uhusiano mzuri na mashirikiano na Serikali ambayo imeonyesha ubinaadamu ambao tunajuwa ni vigumu kwao naona ni muhimu sana sisi tuwafanyie mipango ya kuondoka.79

Si kuwa Uingereza haikutaka tena kuendeleya na utawala wa Sultan wa Zanzibar bali haikutaka kuwalinda Wazanzibari wakati ilipokuwa ipo haja kubwa ya kufanya hivyo. Manwari za Kiingereza zilipewa maagizo maalumu ya kwenda Zanzibar kuwanusuru raia zake tu ambalo ni jambo lenye kukubalika kwenye kanuni ya kimataifa. Lakini wale aliyokuwa ana dhamana ya kuwalinda na mishahara yao ikilipwa na nchi yao ya Zanzibar hawakuwa na thamani yoyote kwao.

Baada ya kuwasili Sultan Jamshid Uingereza, tarehe 7 Mei, 1964, Serikali ya Kiingereza kupitiya Commonwealth Relations Office (CRO) ilimtumiya salamu zifuatazo Balozi wa Uingereza kwa niaba aliyekuwepo Dar es Salaam za kumtuliza Mwalimu Nyerere:

Mfahamishe Nyerere kuwa Sultan alikaribishwa Uingereza si kama mkimbizi wa kisiasa bali kama ni raia wa Zanzibar ambaye anaruhusika kukaa hapa kama raia yoyote yule wa Commonwealth. Ikiwa Nyerere atauliza yoyote kati ya haya yafuatayo unaweza kumjibu hivi:

a) Hatuna ushahidi kuwa Sultan amejihusisha na mipango dhidi ya kuipinduwa Zanzibar kwa msaada wa Waarabu waliyojitoleya…na tunafikiri kuwa mpango kama huo utakuwa hauna mashiko na hautozaa matunda mazuri.

b) Muda kidogo tuliona makabrasha ya kisiasa ambayo yakitolewa na oganaizesheni yenye kujiita Organisation of Zanzibar in the United Kingdom. Oganaizesheni hii inaonekana sasa kuwa haifanyi kazi na pengine hata haipo tena. Haikupata wafuasi au kuungwa mkono hapa. Tulimuonya Sultan wakati huo asimruhusu memba yoyote wa nyumba yake kujihusisha na oganaizesheni hii.80

Hayo yalikuwa ni maagizo ya tarehe 7 Mei, 1964 ambayo yanazidi kudhihirisha kuwa kinyume kabisa na kauli zenye kusema kuwa Muingereza alikuwa akimuunga mkono Sultan wa Zanzibar kwa hakika alikuwa dhidi yake na alikuwa yuko pamoja na Nyerere na Mapinduzi yake.

Kinyume na magwiji wa kupanga mikakati ya kisiasa walivyotarajiya, tatizo la Zanzibar halikutoka ndani ya Zanzibar kama walivyokuwa wanaogopa Waingereza na baadae Tanganyika na Tanzania Bara. Tatizo la Zanzibar limetoka Tanganyika na limeshakuwa ni tatizo kubwa la Tanzania Bara (Tanganyika) na la Jamhuri ya Muungano wa Zanzibar na Tanganyika.

Inavoonyesha, bado haijawadhihirikiya watawala wa Tanganyika kuwa baada ya miaka 50 kuwa ipo haja kubwa kwa Tanganyika kuubadilisha mtizamo wake juu ya Zanzibar na kuupinduwa msimamo mkongwe wa kuinyanganya na kuinyima Zanzibar haki zake kwa kukhofia kuwa ikiwachiwa huru Zanzibar itakuwa ni tatizo la kimataifa kwa Tanganyika. Au Zanzibar itakuja kutumiliwa au kutumika kama ni mlango wa kuuingiza ubeberu wa Kiarabu na wa Kiislamu Tanganyika na Afrika ya Mashariki na Kati. Wako wengi wenye kuhadaika na udogo wa Zanzibar ingawa athari zake wanaziona lakini wameamuwa kuukataa ukweli huo. Anasema Jalaluddin Rumi “Yatizame macho yako. Ni madogo lakini yana uwezo wa kuyaona mambo makubwa.”

Waliyokuwa Karibu Machozi Yao Baridi

Suala la watu wangapi wameuliwa Zanzibar kwenye Mapinduzi ni suala ambalo kutoondoka kwake kunaviondoleya baraka visiwa ambavyo ni pepo katika dunia. Na kuondoka kwake ni kutokeya kiongozi na uongozi utakaokiri kuwa mauwaji hayo yalitendeka na nchi nzima kusoma dua na kumuomba Mwenye-Enzi-Mungu istighfari na kuendeleya kumshukuru kwa neema na njia yake iliyonyooka.

Takwimu zinatafautiyana kuhusu binaadamu waliyouliwa katika mapinduzi ya Zanzibar kuanziya watu 5,000 mpaka 18,000.81 Ingelisaidiya sana kama serikali ingewaomba watu waripoti juu ya watu wao waliouwawa ili lithibitike jambo hili. Ile filam ya Kitaliana Africa Addio, imezidisha kuthibitisha kutendeka kwa mauwaji ya halaiki katika Mapinduzi. Idadi ya watu waliouliwa haiwezi kufikiwa kwa sababu wapo watakaotaka idadi iwe ndogo sana ili wajikoshe na wapo ambao watakaotaka idadi iwe kubwa kwa sababu wanawajuwa watu katika kila familia waliyopoteza mtu au watu wao.

Pia kuna kauli nyingi juu ya sehemu tafauti zenye makaburi ya halaiki Zanzibar zikiwemo sehemu kama maeneo ya Kibanda Maiti ambazo zimekujajengwa nyumba juu ya watu waliyouliwa katika Mapinduzi. Pia kuna ambao hawakuzikwa bali wametupwa baharini kama anavyoelezeya mpiga picha mashuhuri duniani kutoka Kenya, marehemu Mohamed Amin (Mo):

Mo alipiga picha za mwanzo za wanamapinduzi, na aliombwa kufanya hivyo na Abdulrahman Mohamed Babu, mtu wa mwanzo alomshituwa kuwa kutakuwa na mapinduzi na ambaye alikuja kuchaguliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje. Alichukuwa filam za wageni wakiyakimbia maafa, makaburi ya halaiki, na maziko ya majahazi yalokuwa yakitupa mizigo yao ya maiti baharini na bila ya maandalizi yoyote huku ikifatiliwa na mkururo wa mapapa waliokuwa wakiisubiri kwa hamu.82

La msingi ni kwa mujibu wa idadi ya watu waliyokuwepo Zanzibar wakati ule, idadi ya watu waliyouliwa walikuwa ni watu wengi sana. Zaidi ya idadi, tendo lenyewe lilikuwa ni kubwa bila ya kiasi kwa sababu Zanzibar haikupata kuwa na utamaduni wa watu kuuliwa au kuuwana namna ile. Idadi ya watu waliyouliwa Zanzibar ni jinamizi la kitaifa na haiwezekani kwa njia yoyote ile kuondowa mifarakano Zanzibar bila ya suala hili kukabiliwa na kuyakubali matokeo yake ili kufikiya kusameheyana na kusikilizana.

Maelfu ya Wazanzibari wa asili tafauti waliuliwa na maelfu ya Waomani walisaidiwa na shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu kurudi Oman kwa kutumia majahazi kutoka nchi za Kifalme za Ghuba, kwa mfano, Hari Sagar, Nasrul Mulk, Samhan, Salaam, Badry, nk, na manwari ya Kidachi, Van Riebeeck.83

Katika makala ya tatu na ya mwisho yenye kichwa cha maneno “Kumbukumbu na Sheikh Abdulla Al-Khalili”, mwandishi wa Kiomani Ahmad Al-Fallahi ameandika kuwa mshairi maarufu wa Kiomani, Sheikh Abdulla Al-Khalili alitunga kasida yenye kichwa cha maneno “Watu Waliokuwa Karibu Macho Yao Yabaridi” akikusudiya:

…mauwaji makubwa ambayo waliteketeya ndani yake maelfu ya Waomani kutoka wanawake, wanaume, watoto, Mashekhe, vijana ambao wakiishi [Zanzibar] na nyoyo za Waomani siku hiyo zilijaa uchungu na mzigo wa huzuni…waliyo karibu na watu wa Oman hawakuathirishwa wala hawakuhuzunika na aliukusudiya umma wa Kiarabu kutokeya Misri kuelekeya Shaam, Iraq, nchi za Afrika Kaskazini na siku hizo hisiya za kizalendo zilikuwa zimetanda na kuzitawala akili, lakini maneno yake (Sheikh Al-Khalili] yalimuathiri Sultan Sayyid Said bin Taimur wa Oman na akamuamrisha Sayyid Hamed bin Humud ambaye alikuwa ni Waziri wake wa karibu na akamtuma ampelekee salamu Sheikh Abdullah [Al-Khalili] kupinga kuwa macho yake ambayo yako karibu hayana ‘machozi baridi’ kutokana na msiba wa damu uliyotokeya Zanzibar.84

Kuna Wazanzibari wengi ambao wanaishi na majeraha na makovu ya mavamizi ya Zanzibar. Wengi wao wamekuwa wakisononeka na kulaumiyana kwa yaliyotokeya Zanzibar tarehe 12 Januari 1964. Ukweli ni hawakuwa na umoja au uwezo wa kuyazuwia isipokuwa kwa kupambana na vifo na mateso makubwa zaidi. Ni hikma ya Mwenye Enzi Mungu kuwaweka hai ili kizazi kipya kipate kujiilimisha kutoka kwao na wao wapate kupona na maradhi ya kujilaumu na kuwalaumu wenziwao. Inshaalla kitabu hichi kitakuwa kipoza moyo na kuwapa nguvu za kuwasaidiya kuujenga mustakbal mpya wa Zanzibar na uhusiano mkongwe baina ya Zanzibar na Tanganyika, na baina ya Waafrika na Waarabu—Afrabia.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: