Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!

Icon

Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia

Mlango wa Kwanza: Siri Nzito

Mtawaliwa siku zote anataka kumuigiza mtawala katika maumbile yake, mavazi yake, kazi zake na yote yanayokhusiana na hali yake na dasturi zake. —Ibn Khaldun

 

Mapinduzi Tanganyika na Kenya 

Picha kubwa ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 haiwezi kufahamika bila ya kuyafahamu ijapokuwa kwa mukhtasari mfupi mapinduzi ya kabla yake yaliofanyika Tanganyika, na baadaye Kenya. Mapinduzi ya Tanganyika, ya Zanzibar, na ya Mwambao wa Kenya ni mifano ya mapinduzi ya kalamu na ya umwagaji damu.

Tanganyika iliupata uhuru wake tarehe 9 Disemba 1961 na Waislam wa Tanganyika walikuwa na mchango mkubwa sana katika kuupiganiya uhuru huo. Hayati Julius Kambarage Nyerere alitowa mchango mkubwa na yeye mwenyewe alikiri hivyo kwenye hotuba yake ya kuwaaga wazee aliyoitowa Dar es Salaam katika mwezi wa Novemba mwaka 1985. Kwa mara ya kwanza Mwalimu alielezeya namna alivyopokelewa, kujuulishwa na kusaidiwa sana na wazee wa Kiislamu wa Dar es Salaam. Kwenye shughuli za TANU yeye alikuwa ni Mkristo peke yake na mara nyingine alikuwepo John Rupia.

Muhimu pia na kwa mara ya kwanza Mwalimu alisikika akisema kwenye hotuba hiyo kuwa hata jina la Tanganyika African National Union (TANU) lilifikiriwa na kuundwa na akina marehemu Abdulwahid Sykes walipokuwa askari Burma katika vita vya pili vya dunia.1

Historia iliyofichwa ya mchango wa Waislam katika kuupiganiya uhuru wa Tanganyika imeandikwa na kuelezwa kwa ufasaha mkubwa na mwandishi maarufu wa Tanzania Bwana Mohamed Said kwenye kitabu chake kwa lugha ya Kiingereza, The Life and Times of Abdulwahid Sykes (1924–1968), na kwa Kiswahili Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes (1924–1968) Historia Iliyofichwa Kuhusu Harakati za Waislam Dhidi ya Ukoloni wa Waingereza katika Tanganyika. Kitabu hicho ni muhimu sana kwa wanaotaka kufahamu vipi Waislam waliupiganiya uhuru wa Tanganyika na namna walivyopinduliwa kwa mapinduzi baridi kwanza kabla ya kupinduliwa kwa Dola ya Zanzibar tarehe 12 Januari 1964. Kilele cha mapinduzi ya Tanganyika ni kudhoofishwa nguvu za umma wa Kiislamu pale ilipovunjwa East African Welfare Muslim Society (EAMWS) na zilipozimwa juhudi za kuanzisha Chuo Kikuu cha Kiislam mwaka 1964.2

Bwana Mohamed Said pia amefafanuwa katika kitabu chake Uamuzi wa busara wa Tabora namna gani uongozi wa Waislam kutokeya African Association mpaka kuundwa kwa TANU walivyopinduliwa kwa mapinduzi ya kalamu. Baraza la Wazee la TANU ambalo Mwenyekiti wake alikuwa marehemu Mzee Suleiman Takadiri lilipinduliwa chali kwa kazi iliofanywa na kiongozi na viongozi wa Kiislam waliouweka mbele uzalendo wa Kiafrika kuliko mafundisho ya dini yao. Chanzo cha mapinduzi hayo yalikuwa masharti matatu yalioikabili TANU katika kushiriki uchaguzi wa kwanza wa Tanganyika wa kulichaguwa Baraza la Kutunga Sheria. Mkutano wa TANU wa Tabora wa tarehe 21–26 Januari 1958 uliamua kuingiya uchaguzi wa kibaguzi wa kura tatu ambao ulikuwa na masharti matatu magumu:

1) Ili Mwafrika aweze kupiga kura alitakiwa awe na kipato cha pauni mia nne za Kiingereza kwa mwaka.

2) Awe na kiwango cha elimu ya darasa la kumi na mbili.

3) Na awe ameajiriwa katika kazi maalumu.3

Uamuzi wa busara wa Tabora haukuwanasa Waingereza kama ulivyowanasa Waislam wa Tanganyika ambao wengi wao hawakuweza kuwachaguwa viongozi wao kwa sababu uchaguzi wa kura tatu “ulikuwa ukizuia uongozi wa kuchaguliwa kuingia kwenye madaraka.”4

Kwa upande mwengine, Kenya kabla ya kupata uhuru wake tarehe 12 Disemba 1963, siku mbili baada ya uhuru wa Zanzibar, ilikuwa imegawanyika sehemu mbili: Koloni la Kenya, au bara, na Himaya ya Kenya, au Mwambao. Sheikh Abdillahi Nassir ni mmoja kati ya viongozi wa Mwambao ambaye alihudhuriya mkutano wa Mwambao uliofanyika Lancaster House, London, baina ya tarehe 8–12 Machi mwaka 1962.

Anaelezeya Sheikh Abdillahi kwenye kanda iitwayo “Mwambao: Historia ya Pwani ya Afrika Mashariki,” kuwa Himaya ya Kenya ilikuwa ni nchi kabla ya Koloni la Kenya kuwa ni nchi kwa miaka isiyopunguwa 1,300, na namna chuki za uzalendo wa Kiafrika zilivyowaathiri Waislam na khasa chuki za kikabila na propaganda ya utumwa na Uarabu.5

Sehemu hizo mbili za Kenya, Koloni la Kenya na Himaya ya Kenya au Mwambao, zikawa ni nchi moja ya Kenya kwa makubaliyano ya mabadilishano ya barua baina ya Waziri Mkuu wa Kenya, Mzee Jomo Kenyata na Waziri Mkuu wa Zanzibar Bwana Mohammed Shamte walizoandikiyana London tarehe 5 Oktoba 1963. Barua zote mbili zilikubaliyana juu ya mambo matano yafuatayo:

1) Uhuru wa kuabudu wa watu wa dini zote katika sehemu hiyo utalindwa kwa mujibu wa dini zao; na khasa wale raia wa Sultani na vizazi vyao, ambao ni wa dini ya Kiislamu, watahakikishiwa uhuru wao wa kuabudu katika nyakati zote na hifadhi za nyumba na sehemu zote za dini yao.

2) Uwezo wa Kadhi Mkuu na Makadhi wengine wote kuhukumu kwa sharia ya Kiislamu utahifadhiwa kufuatana na sharia ya Kiislamu katika kesi zote za ndoa, talaka na mirathi.

3) Katika zile sehemu ambazo wakaazi wake wengi ni Waislamu, watawekwa, kila inapowezekana, Maafisa Utawala (Mabwana Shauri) Waislamu.

4) Watoto wa Kiislamu, kwa kadri inavyowezekana watasomeshwa lugha ya Kiarabu katika kudumisha dini yao ya Kiislamu kwa vile lugha hii ndiyo lugha ya dini yao. Ule msaada wa fedha unaotolewa kuzisaidia skuli za msingi za Kiislamu katika hilo jimbo la Mkoa wa Pwani utaendelea. Hautakatwa.

5) Umilikaji wa ardhi kutokana na mikataba iliyokwisha kusajiliwa utatambulikana na kukubalika wakati wote. Mwenendo huohuo utaendelea na kuhifadhiwa katika kusajili mikataba mipya ya kumiliki ardhi isipokuwa tu pale itakapokuwa ni lazima kuchukua ardhi kwa masilahi na faida ya umma; lakini papo hapo wale wenye ardhi zao watabidi kulipwa fedha.6

Kwa mujibu wa Sheikh Abdillahi, makubaliano hayo baina ya Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Kenya hayakutimizwa na amethibitisha namna nguvu za umma zilivyoporwa na umuhimu wa kujenga muamko wa kuelewa badala ya muamko wa hamasa. Mfano mkubwa ambao ameutowa Sheikh Abdillahi am-bao ni kinyume na makubaliano waliyotiya sahihi Mawaziri Wakuu wa Zanzibar na wa Kenya, ni kunyanganywa Waislam, wa makabila yote, Taasisi muhimu sana ambayo ikijulikana kwa jina maarufu la Mombasa Insititute of Muslim Education (MIOME) ambayo ilikuwa ni:

baraka kubwa kwa Waislam wa Afrika Mashariki. Hapa ndipo mustakbal wa vizazi vya Waislam vinapewa mafundisho katika masomo ya ufundi chini ya Maprofesa mabingwa ambao wameajiriwa na Serikali kutoka Ulaya. Sir Phillip Mitchell ambaye alikuwa ni Gavana na sasa ni Mwenyekiti wa Baraza la Waendeshaji wa Taasisi alikuwa ndiyo nguvu ya usukumaji wa Taasisi [MIOME]. Mtukufu Sultan wa Zanzibar alitowa mchango wa Shs. 2,000,000/-kutoka mfuko wa Colonial Welfare Fund, Mtukufu Aga Khan alichangiya Shs. 2,000,000/-: Mtukufu Sheikh Mkuu wa jamii ya Kibohora amechangiya Shs. 1,000,000/-; na Sheikh Khamis Mohammed bin Juma [El Mutwaji] amekodisha ekari 34 na nusu za ardhi nzuri na kwa muda mrefu kwa matumizi ya Taasisi, na kwa bei khafifu kwa kila mwaka.7

Mbali ya Muslim Teachers’ Training College iliyokuwepo Kibuli, Kampala, Uganda, Khamisi Sekondari ya Mombasa, Muslim School ya Soroti, ya Jinja, na kadhalika.

Iliyovunja rekodi zote na ambayo marehemu Sheikh Ali Muhsin akiamini kuwa ndiyo moja kati ya sababu za kupinduliwa Zanzibar, ilikuwa ni fikra na mipango ya kuanzisha Chuo Kikuu Cha Kiislam cha Afrika Mashariki na Kati. Kwa mujibu wa Sheikh Ali Muhsin, Chuo hicho kilikuwa na lengo la kuwafundisha Waislam kutoka sehemu zote za Afrika Mashariki na Kati. Mwandishi wa ramani wa Chuo hicho alikuwepo Zanzibar mapinduzi yalipotokeya na alisaidiwa kuondoka na Bwana Ahmed Omar Jahadhmy. Wamasri waliishauri serikali ya Zanzibar wasubiri mpaka watakapokuwa na wanafunzi wa kutosha ambao wataweza kufundishwa kwenye Chuo hicho. Fikra iliyoona mbali kwa wakati huo ni hii ambayo leo inaitwa Open University. Redio na televisheni vilikuwa viwe ndiyo vyombo viwiili vikubwa vya kufundishiya kote Afrika Mashariki na Kati. Majaribio ya kwanza yalifanywa kabla ya mapinduzi lakini yalifeli.8 Baada ya kuvunjwa kwa East African Muslim Welfare Society ambazo khabari zake zinapatikana kwa urefu kwenye kitabu cha Kiswahili cha Bwana Mohamed Said cha Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes, taasisi na mali zake zote zikataifishwa na badala yake pakaundwa BAKWATA Tanzania, SUPKEM Kenya na UMSC Uganda. Hali ya Waislam chini ya utawala wa Kiingereza ilikuwa ni ya kuridhisha zaidi kuliko hali waliyokuwa nayo baada ya kupatikana uhuru Tanganyika, Kenya na hata Uganda.

Waingereza Walijuwa Nini Kuhusu Mapinduzi?

Ukiangaliya kwa makini utakuja kuona kuwa walikuwepo Waingereza na mamishionari ambao walikuwa hawana chuki dhidi ya Wazanzibari wenye asili ya Kiarabu lakini kwa bahati mbaya sauti zao sio zilizokuwa zikisikilizwa na kupewa nafasi. Kwa mfano alikuwepo Dk. Gerald Broomfield ambaye alikuwa ni mmishionari wa Kianglikani aliyekuwa na uzowefu mkubwa Zanzibar. Dk. Broomfield alinukuliwa na Arab Association ya Zanzibar kutoka kitabu chake Colour Conflict in Africa kwa maneno yake yafuatayo:

Afrika iliyobakiya ina jambo la kujifunza kutoka Zanzibar…Zanzibar inaonyesha uwezekano wa kuwepo amani na kuhishimiana baina ya makabila. Huenda likawa ni jambo zuri kwa roho zetu kukumbuka [Zanzibar] inafanya hivyo kwa sababu Sultan wa Kiarabu ndiye mkubwa wa Dola.9

Hilo halistaajabishi kwa sababu Ukristo uliingiya Zanzibar na bara kwa kupewa hishma na Masultani waliokuwa ni Waarabu na Waislamu. Lakini Muingereza mtawala alipoona kuwa Ufalme umegeuka na kuiunga mkono siasa ya kizalendo ya chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP) ambayo ilikuwa karibu sana na siasa ya uzalendo wa Kiarabu (Pan-Arabism au Arab Nationalism) wa Gamal Abdel Nasser wa Misri, akaamua kuwatupa mkono ZNP-ZPPP na kuubwaga uhuru wa Zanzibar ambao ulikuwa hauna salama kwa Waingereza au kwa Mwalimu Nyerere kwa sababu, na kama alivyoelezeya Sheikh Abdillahi:

Zanzibar ilikuwa ni nchi pekee katika Afrika nzima ambayo isingelihitajiya Mzungu hata mmoja. Zanzibar ilikuwa ina watu wa kuendesha nchi na kuwaazima majirani kuendesha nchi zao.10

Sababu kubwa ya Wazanzibari wenye asili ya Kiarabu kuwageuka watawala wa Kiingereza na watawala hao kupanga kuwakomowa Wazanzibari wenye asili ya Kiarabu, kulianza kwa kupigwa mabomu Misri na Muingereza mwaka 1956.11 Wazanzibari wenye asili ya Kiarabu walihisi kuwa Uingereza haiaminiki na kuwa ilikuwa dhidi ya Waarabu. Hisia hii ilisababisha kudai uhuru kamili bila ya kungojea maendeleo zaidi ya baadae.

Mwisho wa mivutano Muingereza alikataa kuisaidiya serikali ya Zanzibar ilipopinduliwa tarehe 12 Januari 1964 na sababu kubwa iliyowafanya kukataa ni imani yao kuwa Mapinduzi ya Zanzibar yalikuwa ni suala la ndani ya Zanzibar na kuwa hakukuwa na mkono au uvamizi kutoka nje ya Zanzibar. Kwa upande wa Tanganyika Muingereza aliamuwa kuzuwiya fujo na kumrejesha kitini Mwalimu Nyerere pale jeshi la Tanganyika lilipoasi tarehe 20 Januari 1964 na Nyerere akakimbilia mafichoni siku tisa tu baada ya mapinduzi ya Zanzibar.12 Viongozi wa Serikali ya Tanganyika haraka walikwenda kuomba msaada kutoka kwa wakubwa wa Kiingereza. Anaelezeya Brigadier Douglas:

Kambona, akifuatana na [Paul] Bomani, Waziri wa Fedha, akionekana ana jambo ameficha, na ana khofu zaidi kuliko kabla, walikuja nyumbani kwangu na barua kutoka kwa Naibu Raisi Kawawa ilosema: Nimeelekezwa na Raisi wa Jamhuri ya Tanganyika kuiletea ombi la msaada wa kijeshi serikali ya Kiingereza ili utuwezeshe kuweka sheria na amani ndani ya nchi.13

Mara nyingi uasi wa jeshi la Tanganyika umekuwa ukihusishwa na mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwa wanajeshi wa Tanganyika, Kenya na Uganda waliingiwa moyo wa kuasi kutokana na kufaulu kwa Mapinduzi ya Zanzibar ingawa hakukuwa na uhusiano wowote baina ya matukio hayo mawili. Uamuzi huu unatokana na kukosekana kuyafahamu Mapinduzi ya Zanzibar kwanza, na pili, kukosekana huko kufahamika kwa mapinduzi ya Zanzibar kumeondowa hoja ya kufanywa utafiti wa mahusiano baina ya mapinduzi na uasi wa kijeshi wa Tanganyika.

Suala moja muhimu ambalo linavutiya hoja ya uhusiano baina ya mapinduzi ya Zanzibar na uasi wa kijeshi wa Afrika Mashariki ni suala la kukamatwa kwa viongozi wa vyama vya wafanyakazi baada ya kutokeya uasi huo Tanganyika. Tarehe 29 Januari 1964 Balozi wa Kiingereza kwa niaba, alipeleka ujumbe wa telegram kwa Commonwealth Relations Office, London, uliopitiya Ubalozi wa Kiingereza Kampala, Nairobi, Aden na Washington:

Matokeo ya kuasi kwa jeshi la Tanganyika ni kundi kubwa la viongozi wa vyama vya wafanyakazi kukamatwa Jumapili usiku Tanganyika nzima pamoja na takriban viongozi wote wa chama cha Shirikisho la Wafanyakazi wa Tanganyika (Tanganyika Federation of Labour). Wote walipelekwa kwenye vituo vya polisi kwa kuhojiwa na baadhi yao baadaye waliwachiwa huru. Rais [Nyerere] kwenye hotuba yake ya redio ya jana usiku aliligusiya suala hili na aliongeza kwa kusema kuwa Mkuu wa Wilaya mmoja pia amekamatwa.

Nyerere alitamka kwenye hotuba hiyo ya redio kuwa watu hawa, wa vyama vya wafanyakazi, walikuwa wamekula njama na viongozi wa uasi wa kijeshi “kusababisha mtafuruku zaidi.” Kulikuwa na uvumi mwingi wiki iliyopita kuwa vyama vya wafanyakazi vilikuwa vinapanga mgomo wa jumla au angalau mgomo wa wafanyakazi wa gatini na wa reli. Pia inaaminiwa kuwa viongozi kadhaa wa vyama vya wafanyakazi walikuwa wakipitisha wakati wao mwingi kwenye kambi ya kijeshi ya Colito.14

Msomaji anaombwa baadaye aunganishe mchango wa vyama vya wafanyakazi katika mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari 1964 na uasi wa jeshi la Tanganyika wa tarehe 20 Januari 1964.

Waingereza hawakuwacha kuuhusisha uasi wa jeshi la Tanganyika na mchango wa Oscar Kambona ambaye wakati huo alikuwa ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi. Walimuandikiya makala kwenye ukurasa wa nyuma wa gazeti la Daily Telegraph la tarehe 22 Januari 1964 ambayo ilimuudhi sana Kambona. Balozi wa Kiiengereza aliyekuwepo Dar es Salaam alielezeya kwenye barua yake aliyompelekea Bwana W.G. Lamarque wa Commonwealth Relations Office, Downing Street, London, kuwa “Stephen Miles alipokutana na Rais [Nyerere] wiki iliyopita waligusiya kuwa Kambona alikuwa kiongozi wa uasi wa kijeshi, na Rais, kama unavyojuwa, alimwambiya Oscar kuwa ‘Masikini Oscar, maisha yeye ndiye mwenye kulaumiwa.’ Kwa kusema kweli, Oscar alikasirishwa sana alipozisikiya habari hizo na akaanguwa kilio na ikabidi apewe siku moja nzima ya mapumziko.”15

Waingereza walimtiliya shaka sana Kambona kuwa alikuwa amehusika na uasi wa jeshi la Tanganyika kwa kuzingatiya kuwa katika siku mbili za kwanza za uasi, Kambona alikuwa akitangaza kwenye redio kila baada ya nusu saa na kuwa alikuwa tayari achukuwe khatamu za serikali na ajitangaze kuwa ni Rais lakini aliogopa dakika za mwisho. Pia walilalama kwa kusema “Lazima iulizwe kwanini ulinzi wa ndani wa Tanganyika dhidi ya tukio kama la uasi wa jeshi ukawa dhaifu namna hii. Hapana shaka kukosekana kwa taarifa kutoka vyombo vya usalama kuipa serikali kumetokana na Kambona na [Job] Lusinde kulibomowa Tawi la Usalama na badala yake kuwaweka watu wa T.A.N.U. aliowachaguwa Kambona.”16 Licha ya kuwa hawakuwa na taarifa za kiusalama watawala wa Kiingereza waliamuwa kupeleka jeshi la Makamandoo kurudisha amani na utulivu Tanganyika na kumrudisha kitini Mwalimu Nyerere.

Na Zanzibar ikapinduliwa, mauwaji ya halaiki yakafanywa, na Bwana Adrian Forsyth-Thompson aliyekuwa Permanent Secretary katika ofisi ya Waziri Mkuu Bwana Mohammed Shamte akaondoka Zanzibar tarehe 8 Februari 1964, na alitarajiwa kuondoka Nairobi kuelekeya Cape Town, Afrika Kusini, tarehe 11 Februari 1964. Baba yake Adrian alikuwa ni ofisa katika serikali ya kikoloni ya Kiingereza na alistaafu Cape Town. Adrian aliondoka Cape Town tarehe 18 Machi kwenda kwenye kazi yake mpya katika visiwa vya Seychelles.

Forsyth-Thompson alikuwa ni ofisa wa usalama kwenye ofisi ya Balozi wa Kiingereza Zanzibar na punde tu kabla ya mapinduzi alikabidhiwa kazi na Katibu Mkuu wa Kiingereza, Bwana Mervyn Vice Smithyman, katika ofisi ya Waziri Mkuu Bwana Mohammed Shamte kuleta mabadiliko katika vyombo vya usalama vya Zanzibar. Alipokuwapo Nairobi na tayari kuondoka kwenda Cape Town, Forsyth-Thompson alitowa ripoti muhimu ambayo ilipelekwa Commonwealth Relations Office, London kwa njia ya telegram na kopi zikapelekwa ubalozi wa Kiingereza Dar es Salaam, Aden, Kampala, Washington na Cape Town. Ujumbe huo ulikuwa ni mfupi ukiufananisha na ripoti yake yenye kurasa nane aliyoiandika alipokuwa Nairobi tarehe 10 Februari 1964.

Kwenye ripoti fupi aliyoitowa Nairobi na iliyopelekwa London na Washington, Forsyth-Thompson aliziwasilisha nukta tano lakini hapa tutainukuu nukta ya kwanza na nukta ya nne:

1) Hakuna (rudia hakuna) ushahidi wa mkono kutoka nje katika mapinduzi ambayo yalikuwa ni mapinduzi ya Afro-Shirazi Youth League dhidi ya siasa ya Kiarabu ya Serikali iliyokuwepo, na mapinduzi yalifanywa katika kipindi ambacho viongozi wa ASYL na washabiki wao wakiamini patatokeya ukamataji wa viongozi wakati wowote. Babu alichupiya, na Karume (? Alichaguliwa) na wanamapinduzi kuwa ndiye kiongozi anayejulikana na Okello alichomoza tu.

4) Kwa mtizamo wa mbali mustakbal wa Zanzibar umo katika uhusiano wa karibu na maeneo ya bara ikiwa ndani ya Shirikisho au kuunganishwa na Tanganyika. Hili litafanyika kwa urahisi ikiwa Tanganyika au Kenya watakuwa tayari kupeleka vikosi vya polisi (kwa mfano kikosi cha huduma) kutokana na ombi la Karume ambaye atakubali kutokana na hali ya mambo ilivyo ikiwa Watanganyika na Wakenya watampa ishara kuwa wako tayari.17

Kwenye ripoti yake ya kurasa nane, Forsyth-Thompson anaelezeya kuwa:

Umma Party na viongozi wa ASP wenye mitizamo isiyo mikali hawakujuwa chochote [kuhusu mapinduzi]. Saleh Saadalla labda akijuwa…Alkhamisi tarehe 9 [ASYL] walisikiya kuwa mzigo wa meli wa silaha kutoka Algeria ulikuwa utaletwa na Serikali…Hadithi za silaha kutoka Algeria zilikuwa zimezagaa kwenye wiki baada ya mapinduzi: na kwa hakika ulikuwa ni upuuzi mtupu.18

Kuhusu mapinduzi yenyewe, anaelezeya Forsyth-Thompson, “yalipangwa na kutekelezwa ndani ya muda mfupi na hii ni dalili ya kukosekana kabisa taarifa zozote kutoka kitengo cha usalama (Special Branch) kuwa kulikuwa na mpango. Kwa muda mrefu kulikuwa na mazungumzo ya kufanya fujo, lakini hakukuwa na pendekezo la mpango wa kuipinduwa Serikali kwa kutumiya nguvu.”19

 

Kamati ya Ukombozi wa Afrika

Mkutano wa nchi huru za Kiafrika uliofanyika Addis Ababa mwezi wa Mei 1963 uliunda Kamati ya Ukombozi wa nchi tisa yenye makao makuu Dar es Salaam. Nchi zilizounda kamati hiyo zilikuwa Tanganyika, Nigeria, Uganda, Algeria, Umoja wa Jamhuri ya Kiarabu (U.A.R.), Guinea, Senegal, Ethiopia na Kongo. Ghana haikuwemo.

Nyerere hakupendeleya makao makuu ya Kamati ya Ukombozi ichukuliwe na Ghana, U.A.R. au Algeria. “Alikhofiya kuwa kati ya nchi hizo Kamati ingelitumiliwa na Rais wa Dola kujijengeya sifa, na mtizamo wa kamati ungelikuwa juu ya utumiaji nguvu badala ya shinikizo la amani.”20

Baada ya uchaguzi wa mwisho wa Zanzibar wa kabla ya mapinduzi wa tarehe 8 Julai 1963, Mwalimu Nyerere alifanya ziara ya Marekani na alionana na Rais John F. Kennedy, na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa U Thant. Pia aliitembeleya nchi ya Canada kwa muda mfupi na alikuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Bwana Lester Pearson. Tarehe 21–25 Julai alikuwa mgeni wa Serikali ya Uingereza. Mwalimu na ujumbe wake uliondoka London siku ya Alkhamisi tarehe 25 Julai kuelekeya Algiers, mji mkuu wa Algeria.

Katika msafara wa Rais Nyerere walikuwemo:

 Rais Nyerere

Bwana Oscar Kambona, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ulinzi

Bwana I. M. Bhoke Munanka (Waziri Mdogo, Ofisi ya Makamo wa Rais)

Bwana A. B. C. Danieli (Katibu Msaidizi, Mambo ya Nje)

Bwana G. Rockey (Katibu wa Habari)

Bwana F. Sangu (A.D.C.)

Bwana P. Mwinbo (Mkuu wa Maofisa Wafanyakazi)

Bwana J. M. Simba (Katibu Khasa wa Rais)

Bwana U. Nyondo (Ofisa Mfanyakazi wa Rais)

Bwana K. Kondo (Ofisa Mfanyakazi wa Bwana Kambona)

Ziara rasmi ya Rais Nyerere na msafara wake nchini Algeria ilikuwa kuanziya tarehe 25 mpaka tarehe 28 Julai. Inavyoonesha Ubalozi wa Kiingereza mjini Algiers hakuambuliya kitu chochote cha maana kati ya mazungumzo ya Rais Nyerere na Ahmed Ben Bella, Waziri Mkuu wa Algeria na baadaye Rais wa nchi hiyo.

Katika mwezi huohuo wa Julai 1963 Waingereza walikuwa wameshazipata habari kutoka jeshi la Tanganyika kuwa kulikuwa na silaha zikitarajiwa kutoka Algeria. Baina ya mwezi wa Agosti na Septemba 1963 listi ya silaha ilionekana Wizara ya Ulinzi. Halafu kimya mpaka wiki ya kwanza ya Januari 1964.21

Tarehe 2 Januari 1964, meli iliyopewa jina la mwanafalsa maarufu duniani wa historia, MV Ibn Khaldun kutoka nchi ya Kiarabu ya Afrika ya Kaskazini ya Algeria, ilitia nanga Dar es Salaam huku ikibeba shehena ya silaha zilokusudiwa kupelekwa Msumbiji na kwa ajili ya mapinduzi ya Zanzibar. MV Ibn Khaldun haikuwa Sultana iliotiya nanga New York Alkhamisi, tarehe 30 Aprili mwaka 1840 na iliyobeba ujumbe wa amani na biashara kutoka Zanzibar kwa Sultan Sayyid Said bin Sultan.

Meli ya MV Ibn Khaldun ilikuwepo Dar es Salaam kwa siku nane, kuanziya tarehe 2 Januari 1964 na iliondoka tarehe 9 Januari 1964. Ilipowasili mara ya kwanza meli hiyo “ilikaa nje ya bandari ya Dar es Salaam kwa muda wa masaa arubaini na nane. Kutokana na kuhojiwa kwa maofisa wa Kiafrika waliohusika na upakuwaji wa mizigo ya meli ilikuwa dhahiri baadhi ya mizigo iliondolewa na inawezekana sana kuwa baadhi yake iliondolewa kabla ya meli kufunga gati.”22 Rais Nyerere aliongozana na Bwana Djoudi aliyekuwa Charge d’Affaires katika Ubalozi wa Algeria Tanganyika katika kuikaguwa meli hiyo. Djoudi pia alikuwa mhusika wa mafunzo ya kijeshi wa Kamati ya Ukombozi wa nchi tisa za Kiafrika. Kijana mdogo mwenye umri wa miaka 24 aitwaye Racchid Ben-Yelles alikuwa Kepteni wa meli hiyo ya MV Ibn Khaldun.

Kepteni Ben-Yelles alitowa maelezo kuwa meli hiyo ambayo alichukuwa dhamana ya kuiyendesha miezi mitatu nyuma ilikuwa kwa kawaida yake ikifanya kazi kwenye Bahari ya Mediterranean. Mzigo wa kawaida wa meli hiyo ulikuwa ni ulevi wa zabibu na meli hiyo ambayo ikimilikiwa na Serikali ilikuwa na matenki yenye uwezo wa kubeba tani 2,000. Meli ilipoondoka, Rais Nyerere aliwapungiya mkono kepteni na wafanyakazi wake na kuwaombeya safari njema. Wakati inaondoka meli hiyo ilikuwa imebeba shehena ya tani 80 za kahawa na tani 100 za mbao kutoka Tanganyika na ilielekeya Tanga kuongeza mizigo zaidi.23

Kwa mujibu wa ripoti ambayo haiyoneshi imetoka kwa nani na inakwenda kwa nani, Serikali ya Tanganyika iliwalipa Waalgeria “thamani ya pauni za Kiingereza 260,000 za kahawa na bidhaa nyengine.”24 Wapi pesa hizo zilitoka bado ni suala la michirizi yake kufuatiliwa. La muhimu ni kahawa na mbao yalikuwa ni malipo kwa ajili ya silaha zilizoletwa kutoka Algeria na meli ya Ibn Khaldun. Kwa amri ya Oscar Kambona, kazi ya upakuwaji wa mizigo ya silaha hizo alipewa Kepteni Nyerenda na aliamrishwa mzigo wote wa silaha auweke kunako ghala za P.W.D. (Public Works Department).25

Huo ulikuwa ni wakati wa uanzishaji wa harakati za ukombozi wa Msumbiji na baadaye kuanzishwa kambi za kuwapa mafunzo wapiganiya uhuru wa Msumbiji Tanganyika. Oscar Kambona aliwababaisha waandishi wa habari kwa kuwaambiya kuwa silaha kutoka Algeria zilikuwa kwa ajili ya Tanganyika Rifles lakini Waingereza walipotaka taarifa zaidi kutoka kwake aliwajibu kuwa “…ni za Tanganyika Rifles isipokuwa maboxi yaliopigwa krosi nyeusi. Maboxi haya yanatakiwa yawekwe karibu na mlango wa ghala ili yaweze kuondolewa kwa haraka. Pia alisema kuwa maboxi hayo yasifunguliwe. Tuliyafunguwa baadhi yake…Zanzibar ilitokeya Jumapili iliyofuatiliya, tarehe 12 Januari na maboxi yale bado yalikuwepo kunako ghala. Baada ya hapo yakawa hayana umuhimu wowote.”26

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: