Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!

Icon

Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia

Mlango wa Nne: Tupendane Waafrika

Ilivyoelekea mbiu ya “Zanzibar ni ya Wazanzibari” ni yenye kukubalika kwa kila mtu kuliko ile ya “Zanzibar ni ya Waafrika kutoka Bara.” —Ofisa wa Kikoloni wa Kiingereza

 

Mzee Issa Kibwana alikuwa ni mmoja kati ya viongozi wa juu wa kikundi cha Tupendane na alikuwa memba wa chama cha kisiasa cha Afro-Shirazi. Katika mapinduzi ya Zanzibar alikuwa ni katika watu wa mwanzo kuingiya kambi ya jeshi la polisi ya Mtoni na baada ya mapinduzi alijiunga na Jeshi la Wananchi la Tanzania Zanzibar (JWTZ).

Mie ndo mwenyewe. Mimi ndo kiongozi wa Tupendane. Hapoo Miembeni. Mimi ndo mwenyewe kigogo wa Tupendane. Nadhani ukintizama sana hata ningekwenda utaona bega langu moja limekwenda upande.

Kiini cha Tupendane…hawa Tupendane ni kama kitu kilijichomoza tu hapo Miembeni. Hakina msingi hakina chochote. Watu walianza tu, tupendane, tupendane. Sasa ikawa chama kikubwa Tupendane. Sasa kilipopata nguvu alipoamuru Sultani kuwakamata wale viongozi wa Tupendane kuwapeleka Bungi meli nane kwenda kuwatupa usiku. Na mimi nikawa nimo ndani ya kundi. Sababu tunaharibu nchi kwa makosa kwamba kwanza mwendo wetu hatujui shabaha yetu nini kwenda mwendo kama ule. Halafu hatujuwi haya masuruali kuyashona yakawa namna hii. Hatujui mnataka kutia nini huko chini. Kwa vile hili neno lilimkera Sultani.

Huu mwendo ulitokezea uwanjani pale palikuwa na ngoma moja iko pembeni yetu ikiitwa Ndala Ndala. Wale Ndala Ndala na Tupendane waliweka mpaka hapa katikati. Ndala Ndala wako kule Tupendane wako huku. Sasa hawa Tupendane wakenda hivi wanakwenda wachokoza wale Ndala Ndala katika banda lao kule. Na wao watainuka “mnakuja tuchokoza!” Zikaanguka ngumi. Vikaanza vigongo vitupuu. Miembeni hapo. Vigongo vitupu. Sasa Sultani alikuwa na njia yake, akipita lazma msimame. Sasa hawa Tupendane walianza kuvunja adabu kwamba hawamjui Sultani tena. Wakimuona yule, kama wako wawili basi utaona wameongoza hivi, hata hawasimami. Yule mtu anaona “mbona hawa watu wananringia? Bwana we! Chukueni kikundi hiki kakitupeni Bungi.” Basi tukenda tukatupwa huko bwana. Usiku. Lakini hatukukaa huko. Kwa mwendo wetu ule tumerudi. Wanachama wetu wakatufata Kidongo Chekundu. Wanatufuata sie tunarudi. Bwana tunakufuateni, sisi tunawaambia bwana tunarudi twendeni. Ndo umesimama mdundiko mkubwa kweli kweli, Ndala Ndala na Tupendane. Yamezidi mambo. Makubwa. Hapiti mtu yoyote!

Kuingia kule [kwenye ghasia za Juni 1961],1 yule bwana mkubwa, Mzee Karume, alikuja Miembeni akakuta hizo ngoma mbili, Tupendane na Ndala Ndala. Sasa alisimama katikati. Wengi wao waliona yule mtu kaingia kundi la wahuni huenda wakampiga yule, lakini hataa. Walimshangiria uzuri sana yule bwana mkubwa pale. Mpaka akaamuru kwamba nyinyi wenye suruali nyeupe mwende kwenye duka moja pale la Afro-Shirazi, Mlandege pale, sasa hivi wanauza nondo, lililoelekea Bwawani kule. Pale kulikuwa na duka la vitambaa la Afro-Shirazi. “Nendeni mkapime hizo suruali za derei.” Suruali zao ni za derei, nyeupe tupu. Tukenda pima suruali za derei pale! Sasa yule bwana mkubwa akaja pale, pesa kalipa mwenyewe. Sisi tumepoa tu nguo kuvaa. Basi akifika pale, Miembeni, hakuna mtu yoyote anozungumza. Atazungumza pale eshe, amalize, anakwenda zake, haya. Hutoa pesa pale. “Haya vijana wangu, tumieni, tumieni, lakini eh, mti na macho!” Sasa huyu bwana “mti na macho” nini, tunatafuta jina hilo. Sasa mle mna wataalamu, tusishirikiane na wale watu wabaya. Sisi tuingie kundi letu la peke yetu. Kashika Tupendane. Inamla roho Sultani. Manake hata kama alikuwa anakwenda sawasawa hivi akiona gari ya Sultani basi utaona kageuka.

Yule mtu alokuja pale kutufanyia siasa zile kwenda kutupima zile nguo ndo alotuteka. Na lengo lake lilikuwa hawa watu niwapate kwa sababu hawa watu hawakimbii kitu. Hata! Walikuwa Tupendane hawamkimbii mtu yoyote. Anochotaka kufanya saa yoyote, wakati wowote, anafanya palepale. Na mfano alionyesha Juni 1961. Sasa ikawa Tupendane wamo kwenye mkono wa Mzee Karume. Mzee Karume anatoka huko anakuja zake Miembeni, “leo mna chakula gani hapo?” “Ah, leo hakuna chakula.” Basi utaona anateremsha ngombe, anateremsha mchele. Wahuni wanakula hapo hapo. Sasa imekuwa kiteko cha kumpenda Mzee Karume wahuni wote. Wote wanakuja ndani ya kikundi kwa hii, “kula.” Mtego wake alotega Mzee Karume hata akatunasa pale.

Wale viongozi wanohusika na Tupendane ndo waloanza kuambatana na Karume, ndo waloanza kushirikishana na Mzee Karume. Kwa vile walikuwa wapenzi wa Mzee Karume. Hata tukatiwa ndani ya uongozi wa kundi hilo la wakubwa na sie. Wakatupakaza pale, kwamba hawa Tupendane tuwachukuwe wale viongozi wao tuwatie ndani ya kundi. Sasa ukizungumza kule wanakwambia, bwana we, kunakuja kitu hivi hivi hivi, watu wenu wafanye hivi. Ikaenea mpaka mashamba Tupendane. Nguvu zikagawika mpaka mashamba. Leo naweza kukwambia twende Mkwajuni nakwambia tawi letu la asubuhi la Tupendane hili hapa. Tumefanywa kushirikishwa na wale askari wa kichama. Mlikuwa na zile shughuli za fete. Sasa wale Tupendane ndo walokuwa walinzi wa milangoni. Hata kwenye fete ya mapinduzi wao ndo walokuwa walinzi wa milangoni na wakifahamu kinachoendelea.

Juni, ugomvi ulisimama hapo, banda la Ng’ombe hapo. Kulikuwa jamaa mmoja anaitwa Vuai, yeye yumo katika kundi letu la Tupendane. Sasa yule bwana alikuwa na ngombe wake hawa—watatu. Sasa ugomvi wamechukuwa ngombe wa yule bwana kutiwa ndani ya kundi la ngombe kwenda kukoshwa na yule bwana hataki. Sasa kilio chake akaja kulia Miembeni “jamani e, ngombe wangu mimi sitaki wakakoshwe wamekwenda chukuliwa.” Tupendane hawana sheria. Wakachukuwa vigongo. Sasa pale ndo ukasimama muungano baina ya Tupendane na Ndala Ndala kumfuata Mzee Vuai. Hawakumuuliza mtu. Kufika pale wakamuuliza yule bwana hebu tuonyeshe ngombe wako wako wapi? Tizama basi, mambo yenyewe shetani au bilisi tu. Wale ngombe si kwamba wanakwenda chinjwa. Wale ngombe wanakwenda koshwa dawa. Sasa madhumuni yule bwana hataki ngombe wake kwenda tiwa dawa kule. Huenda dawa ile ya kuuwa. Ana wasiwasi. Tupendane na Ndala Ndala, wanafika Kiinua Miguu pale, ndo ilipodata bunduki. Mpaka kesho nikitazama lile guzo lilopigwa hukaa peke yangu nikacheka.

Vita vimesimama hapo bwana. Tupendane, Ndala Ndala na hao kushirikishwa ndani ya kundi lile. Sasa yule bwana, Mzee Karume, akajuwa mimi nna wanaume. Sasa safari zake zote ana watu wake ana nini mtego wake kashika Tupendane ndo watu anowapenda. Kula anomotembea anajuwa mwahala fulani pana kikosi changu fulani hata saa sita za usiku. Tulikuwa na Mshihiri mmoja alikuwa na kondoo wengi sana na mbuzi basi kenda kuambiwa yule Mshihiri “wewe Mshihiri wewe hawa watu kama wamepata chakula hawana kitoweo wape kondoo mmoja au wape mbuzi mmoja halafu njoo sema tukupe pesa.” Basi tukiwa kitoweo hatuna tunakwenda, “e bwana tunataka kondoo.” Tunachukuwa kondoo tunakwenda chinja. Ndo shirika, Karume na Tupendane, hapo.

Juni ndo iloshiriki hasa Tupendane na Ndala Ndala pamoja. Wakashirikiana. Ilikuwa wameshiriki vizuri sanaa Juni! Kuliko kundi jingine lolote! Kila lilipojengwa tawi la Afro-Shirazi Tupendane wapo. Walifanya kuwashirikisha kwenye jeshi la umoja wa vijana. Sasa ikawa wale kiungo sasa. Sehemu ya Darajani katika vita va Juni, wao ndo waliofunga mpaka ati. Kwamba anayetoka ndani majumba makubwa hawezi kuvuka akaingia Mtendeni. Manake mwisho ilikuwa ni ile barabara tu ya Darajani. Wa kule wa kule. Wa huku wa huku.

Kazi zao wale walikuwa hawana kazi maalum. Wakwezi wamo, wa punda wamo, wa virongwe wamo, kuokota nazi na nini. Mchango wao pesa nne nne. Kuna watu makusudi hununuwa vyakula wakenda pika pale Miembeni. Hawana kazi maalum. Tupendane khasa walikuwa zaidi kwenye punda kuokota nazi. Ndo wakawajuwa heshma za Wamanga. Tupendane kamjuwa Mmanga kwa nazi. Ile kwenda kuokota. Anamjuwa Mmanga huyu yuko hapa yuko sehemu gani. Sasa hata yalipoingia mapinduzi haraka kwenda kuuliwa yule mtu. Kwa sababu anamjuwa khulka yake. Na Tupendane walikuwa wengi. Wengi sanaa.

[Tupendane walikuwa wanavaa nguo] nyeupe. Shati jeupe, suruali nyeupe. Dereli ikiitwa. Viatu vikiitwa “kunguru wa shamba” rangi mbili, wekundu na weupe. Hakuna tai. Bega la kulia linaangushwa. Umenikumbusha mbali sana. Miembeni ndo makao makuu yao. Shamba walikuwa wako Potowa. Potowa lilikuwa tawi letu moja. Halafu unakuja zako Tunguu. Lilikuwa liko tawi letu moja. Halafu unakwenda njia hii, namba saba, pale wapi pale, walipotaka kuchimba saruji—Kisakasaka. Upite kidogo Kisakasaka. Lilikuwepo tawi letu moja. Sasa lile la karibu na Kisakasaka likishughulika na ngombe. Sasa Karume akisema “jamani e, watu wengi leo hawana nyama” wale kule wanatuletea.

Sasa iko wale wanojuwa “huyu alikuwa Tupendane huyu.” Wale wanojuwa wale, wazee, wazee. Wanawake hamna. Wanaume watupu. Kwa sababu wale watu walikuwa wa shari. Ushari mtupu wale. Wale hawakusikilizana na Ndala Ndala kwa kupigana. Vigongo! Mikunguni tu. Hapana mambo ya ngumi. Mambo ya ngumi kampige mkeo huko. Utamkuta mtu ana kirungu bichwa lake linafika hivi kachomeka hapa basi anakwenda tu. Hujui kakitowa vipi mgongoni huko. Ilikuwa kazi yao hiyo. Hata kama watu kumi utafikiri wanakwenda paredi. Wamenyoosha lakini anajuwa sasa hivi tuko kushoto, anajuwa sasa hivi tuko kulia.

Kiongozi tu, akisimama mwenyewe anajuwa sasa hivi wote wamesimama. Anageuka anazungumza na jamaa zake. “Tukamkere nani?” Ndo ilokuwa kazi yao. “Nani bedui tukamkere sasa hivi? Si fulani bwana kamkamata jamaa yetu kamwambia mwizi kamuibia nazi. Twendeni tumfuate. Halali bwana. Haki ya Mungu halali.” Moja kwa moja na si kwamba anakwenda kwa kujificha. “Hodi! Hayumo kenda wapi? Kenda mahala fulani. Atarejea saa ngapi?” “Ah sijui,” watu watatu mgonjeeni, sisi tunakwenda zetu. Tuhakikishe tumeshatenda kitendo. Kama yuko ndani anakwenda darini. Wao kazi yao ilikuwa hivo tu. Karume hukaa zake pale Mnazi Moja pale. “Hebu niitieni wale, wale viongozi Tupendane wale.” Basi huja jamaa, “Mzee Karume yuko pale anaita.” Wewe watazame sasa. Wanakwenda mstari mmoja, wakianguka, “wu!” Wote unaona wamegeuka. Wanamtizama. Basi jibu lake “askari wangu mmeiva, hahahaa haaa! Oooo! Askari wangu mmeiva! Leo vipi kwenu kuna mboga, au kuna chakula?”

“Ah, tunacho chakula, mboga tunayo.” “Hahahahaaa! Lakini nasikia nyinyi mnalewa nyinyi. Mnakula gongo nyinyi. Bwana siku za kazi hizi, msilewe gongo!” “Wamo wanokunywa Mzee, wengine hatunywi.” “Haya, mh (pesa), nendeni zenuni.” Hakuna anaeificha pesa ile mpaka uwanjani pale. Jamani Mzee Karume katupa pesa hizi. Lakini si za kulewa. Tununuwe ugari. Hiyo ilikuwa kazi yao Tupendane. Shabaha yake utakuta nywele zao hawanyoi. Hazikatwi. Kazi yao utamkuta anapokaa anafanya hivi tu, anazisokota sokota. Kama siku hizi tunaita Marasta [nywele za Rastafari], na wao zilikuwa vilevile lakini zao hazianguki.

Mtindo huu wa masuruali mapana kayaleta Mnyamwezi. Wacheza Beni Bati. Wale walikuwa Wanyamwezi, walikuwepo nao Miembeni pale, na Beni Bati. Sasa wao hutandika mablangeti namna hii, sasa wale wakubwa wakubwa wanojipenda wale, kila mmoja amesimama kwenye blanketi lake. Masuruali yao mapana mtu anaingia. Vilevile dereli. Shati jeupe, suruali nyeupe. Sasa wao walikuwa na nguo kama kitenge au kikoi au nini anafanya hivi. Aliposimama ndo hapo hapo mwenyewe anajitikisa tu. Kuna watu wakasoma pale. Hii nini hii? Hii ngoma ya utamaduni. Ikaanza kuchipuwa ile ngoma ya Beni Bati mpaka mashamba. Walipo Wanyamwezi ipo. Mashamba mle utakuta leo kuna Beni Bati mahala fulani, utawakuta Wanyamwezi wa wapi wa wapi wa wapi, wote wanakutana huko huko. Utakuta wote uwanja mzima nguo zao nyeupe. Sasa wale ndo walokuwa wameshirikiana na akina mama, wamo “Wangaruka wala. Rimo rimo rimaio. He, he, he he!” Wanashangiria. Ngoma zile zimekufa baada ya mapinduzi. Hizi ngoma zetu zikafilia mbali. Manake katika mapinduzi ngoma zote zilishiriki katika mapinduzi. Beni Bati imeshiriki, Ndala Ndala imeshiriki, Tupendane kashiriki. Wale wote walishiriki ndani ya mapinduzi. Ndo wale wale utakuta “Ah! Huyu bwana alikuwa…si mcheza Beni Bati we? Sasa hivi umekuwa kanali wa jeshi? Ama kweli Karume katuweka mambo!” Ilikuwa namna hiyo.

Viongozi wa Tupendane walikuwa na mitaa.2 Lakini viongozi wote walikuwa wako mjini tu. Sasa mle mashamba yanakwenda matawimatawi tu. Mwenyewe aloanzisha ngoma ile ya Tupendane, mwenyewe akiitwa Saidi Omari Saidi. Alikuwa akikaa wapi? Alikuwa akikaa Mahonda meli kumi na nne hasa! Kibaoni pale. Huyu ndo mwenye kuanzisha ngoma hii ya Tupendane. Kwamba ndani ya siasa yake ile Tupendane, tupendane jamani tuwe pamoja, lakini aliitia kama iko katika ubaguzi. Maana alitaka wale watu wa bara watupu. Lakini kukosa vile na kutaka kujificha akaona wote tuwe pamoja, Zanzibar, nani nani, lakini wote tuwe katika Tupendane.

Tupendane kwa sababu usoni kwetu kuna hatari. Ndo manake ile Tupendane ikaja hivo. Naye yule aloanzisha, kwisha mapinduzi tu wakamsafirisha. Serikali ikamsafirisha. Yeye pamoja na nani, pamoja na Mfaranyaki, wote wamesafirishwa. Kwamba hawa kama tutawaweka hapa, itakuwa hatari hawa. Wakasafirishwa.

[Mfaranyaki] alikuwa mshiriki mkuu wa mapinduzi. Ni mshiriki mkuu. Na kama unasikia alikuwa Mzee Hamid Ameri wa Donge, yule kapewa lakini mwenyewe hasa alikuwa huyu Mzee Saidi Omari Saidi wa Tupendane. Hamid Ameri siku ya mapinduzi alipoambiwa alisema “mimi staki kuuwa.” [Mzee Saidi] alikuwa mtu wa Tanganyika lakini alikuwa kahusika Mnyakyusa, watu wa Mbeya, lakini kaja zamani hapa. Ndo hao walokuja wakati wa mfalme anapigisha kuchimba mashimo. Saidi alikuwa msimamizi mkubwa wa bwana Yahaya wa Pongwe. Maana watu wengine ndo wanasema kulikuwa na watu wameletwa walokuwa sijui Manamba, na nini, kumbe sivo hivi. Hawakuja kwa ajili ya kushiriki mapinduzi. Wale walikuja kwa ajili ya MaSultani wale watu kuja habari ya mikarafuu kulimia. Sasa mapinduzi yamekuja yamewakuta. Sasa tusiseme wametoka watu bara kuja fanya mapinduzi Zanzibar. Kuna walokuweko hapahapa tele kama kina sisi. Maana na mie nimo msintoe.

Alikuwapo mmoja Mikidadi wa Tanga. Alikuwa huyu mdogo wake Khamisi Hemedi, Athmani Hemedi. Halafu alikuwepo shemegi yake Sefu Bakari, Ali, yule alokuwa akikaa Kwahani. Ali, hata akaingia usalama. Mpaka sasa hivi kafa yeye watoto zake bado wamo katika kazi ya usalama. Manake, viongozi wa Tupendane, tulikuwa sisi kama watu saba hivi. Hawa ndo wenye kundi hili. Lakini kiongozi wa kundi mwenyewe ni mie. Kwa sababu sasa hivi tu mimi nimeregea. Nilikuwa simkimbii mtu yoyote. Hata kama angelikuwa kama mbuyu. Na mshipa nlikuwa nao. Simuogopi mtu. Haki ya Mungu. Simuogopi mtu. Hata kidogo. Tena si kama unazungumza mimi nakutetemekea. Hata!

Kwanza huyo Sultani mwenyewe tulikuwa hatusikilizani ajabu. Ugomvi wetu, nilimpiga nani yule…tausi teke pale Kibweni. Pale mimi nnatoka Mahonda nikiingia ndani ya gari. Sasa yule mnyama alikuwa ana ila. Hukaa katikati ya njia pale. Hafungwi ati. Sasa yule akija pale hukaa katikati ya njia akajitikisa halafu hulia “hyeee!” Anainama anaokotaokota pale. Sasa tunatoka shamba sie na gari letu asubuhi tunapeleka ndizi marikiti. Kufika pale yule mnyama katoka porini kakaa katikati ya njia wala hupiti huku wala huku. Yuko katikati ya njia. Mkewe kasimama huku yeye yuko katikati ya njia. Akaanza kuchanuwa akapiga “kukukukuu, hyeee!” Tumesimama bwana, tunamsubiri mpaka aondoke. Tupite wapi? Mkipita mtafatiwa na walinzi wa Sultani. Nkamuliza “we dereva we, vipi bwana?” Akasema “Sultani yuko usoni kwangu hapa bwana we.” Mimi nikatoka nyuma huko. “Huyu ndo Sultani?” Nikampigilia mbali teke! Likaanguka huko, puu! Nikaingia ndani ya gari dereva akatia jembe! Sasa si wanakuja nitaja wenzangu wa ndani ya gari kwamba alopiga huyu. Wote ndani. Bwana alopiga huyu. Nimekwenda hapo Kiinua Miguu. Nimechezea miezi sita. Kahama yule tausi. Mimi nilikuwa namtafuta nimuuwe lakini sikumpatia tu. Kwenda kuniweka bure ndani miezi sita kuwa nimempiga tausi! Mimi mpaka sasa hivi ilikuwa kama wanatambua siri yangu na Mzee Karume nisingekuwa hivi halo. Wallahi laadhim nisingekuwa hivi. Na maisha namtafuta Karume mdogo nimpate ili nimpe siri yangu hii. Tulivo mimi na yule Mzee Karume. Bado sijampata. Karume mimi nilikuwa kama ndugu yake, ndugu baba mmoja mama mmoja. Hataki afanye jambo mimi nisilijuwe kwa ile shabaha alompa hayati Yusuf Himidi kwa mie wakati alipokwenda kunitambulisha. Bwana huyu mtu yuko hivi hivi hivi hivi. Basi yule mtu alikuwa saa ishirini na nne mimi nakwenda Ikulu wala habari sina, wala siulizwi na mtu. “Assalam Alaykum.” “Alaykum Salaam.” “Mimi bwana leo sina pesa.” “Wewe hwishi kutumia pesa kama Banyani. Haya nenda zako. Au una shida zaidi?” “Hata.” Huyo nakwenda zangu.

[Zilipotokea ghasia za June 1961] Mzee Karume kaja zake mpaka msikiti mdogo Mwembe Rikunda hapo kampata alie wake kamwita upesiupesi. Njoo, vipi huko? Akasema, huku mpaka sasa hivi kumetulizana kimyaa! Hawa maasikari wanatafuta watu waliopigana ni watu gani? Akamwambia, wewe sasa nnakutuma, nenda hapo, usipige tarumbeta. Mkamate mmojammoja, pita kidookidogoo, wanongoneze wote muwe mulivo hivi hivo, pastokezee fujo tena. Mimi nakwenda zangu. Yule bwana alotumwa akatimiza ile ahadi. Sasa hawajuwi wale [askari] shina lake nini. Hivo ndivo ilivo. Hawajuwi kabisa shina lake nini. Lakini ilikuwa makusudio yao [askari] pale wapate njia ya kuwakamata wale watu [waliofanya fujo]. [Mpaka leo] wapo walojuwa lakini hawawezi kuzungumza kitu hicho. Siri yao wanaijuwa wenyewe. Ni siri tu. Hiyo moja kwa moja. Ukiizungumza anakwambia “aaahh! Huko usende huko. Huko usende hakukufai kwenda.” Kwa sababu hiki kitu kishaambiwa kisizungumzwe hasa! Huyo anokijuwa asikizungumze.

Unajuwa kama tunakwenda mambo ya Kingereza, Mngereza mpaka sasa hivi suala hilo [la ghasia za Juni 1961] bado analitafuta hapa. Saana analitafuta hapa. Alikuja mwanamke mmoja wa Kiingereza tena alipanga nyumba hii ya Michenzani, namba moja hii, yaani kwa kutafuta kitu hicho. Kuna watu nyumba hiyo, kulikuwa na mtu mmoja jina lake la kwangu mie, akamwambia yule bibi, ukitaka kitu hichi nenda kwa fulani. Kaja hapohapo. Akachekacheka pale, kunchekesha, ananiuliza, nikamwambia mie mgeni hapa. Mie mgeni sijui hayo.

Hawapo. Na khasa wanaohusika hawapo zaidi. Sasa kula likiwa hivo ndo vizuri zaidi. Maana watakujaingia watu walokuwa siwo kwa vile bora ife hivohivo. Midamu wenyewe hawakutambuwa chanzo chake nini na kiini chake nini, bora iwe hivohivo.3

Walifanya sivyo. Wamefanya kinyume ya mambo yanavotakiwa kufanywa. Sasa likitokezea jambo lile likiwa na nguvu zaidi itaonekana aibu kwao.

Bora lilivokufa life tu. Kula mmoja anaomba dua life hivohivo na Mwenyezi Mungu kalijaalia life hivohivo. Anolijuwa, ukilizungumza, kwanza nakutizama macho hasa. Jibu lake rohoni mwake atasema “yule kuuliza jambo lile lina miaka fulani kakusudia nini huyu?” Midam jambo limepita, wenyewe hawakujulikana, basi, halina lazma. Utamtaja wapi, Mzee Issa ameshakufa zamani. Karibu miaka kumi. Hata ukimtaja si bure. Kumtaja kwako kunafaa nini? Wanajuwa wengi lakini ile hadithi yake ngumu Ndo ikafa hivohivo. Hadithi yake ngumu ikafa hivohivo.4

 

Tupendane na Ghasia za Juni 1961—Mzee Selemani

Suala la Juni, ukisikia hao “Tupendane” masuruali mapana, Waruguru, Wazaramo, pale Kizota [Darajani] palikuwa na bekari ya kuni za mikate pale, Tupendane pale wakaanza kufanya machafuko bwana wewe, piga mtu, pale pale. Piga mtu. Huku wamekwenda Malindi na huku wamekwenda Kisiwandui. Wakasema kinachotoka huku kuingia huku halali yetu. Sasa vurumai lile likaja likaingia moja kwa moja mpaka Ngambo kote huko, Ngambo unajuwa zamani Wamanga wapo, Washihiri wapo, vikaja vifo vya ghaflaghafla tu. Kitu alichoamuwa Mfalme ni kutaka askari kutoka Kenya kulinda ule usalama wa hapa. Walipokuja wale askari, walichokifanya, hawakulinda majumba makubwa. Wao wamekuja kuingia nyumba za Ngambo. Ikawa wanalinda raia wa huku Ng’ambo huku. Lakini juu ya hivyo, Tupendane kazi waliokuwa wakiifanya, askari wale wanakwenda zao huku, wakizunguka round [mzunguko] kuja zao huku, kuja kuingia tena, wanakuta maiti mmoja, wawili, pale. Hapo ndipo ikaonekana sifa ya Tupendane. Ikaonekana kwamba hawa Tupendane bwana machafuko. Na kuna baadhi yao walishiriki kwenye mapinduzi. Wale Tupendane mwananchi hawezi kufanya kitu pasi kuwa kiongozi wa nchi anajuwa. Hiyo, kwanza huyu Kisasi alishauriwa, bwana we, hapa pataingia vurumai, sijui wewe utatowa mchango gani. Yeye nafsi yake akasema, kweli mimi nna cheo, lakini utakuja kukuta siwezi leo kufanya mapambano kuingilia kati wakati mimi ni mfanyakazi, lakini langu la kufanya, nyinyi mnaweza kufanya tendo, mimi nikakuteteeni, itakapokuja kesi. Mzee Karume alikuja sema “lazima mshituko wa nchi, kujuwa na sisi tuko wengi, lazima ishtuliwe.” Kwa hivihivi tu mambo yatakwenda hivihivi, tutakuwa hatuhishimiki. Aboud Jumbe akatoa kauli kuwa hakuna la msingi la kufanya isipokuwa ni kupigana tu.

Wao Tupendane walikuja kwa muundo wa majahazi, wanatoka kule [bara] wanakuja hapa, wanafanya biashara, wanaondoka, wanarudi, wakiingia wakitoka. Zamani kulikuwa na vibali vidogovidogo hivi. Ukitoka kule unaingia hapa. Mambo yalikuwa yakenda hivo. Lilivomalizika hili suala likatulia kabisa, kwamba zile chaguzi kila wakati tunapata lakini tunaambiwa hapana, tunapata tunaambiwa hapana, ndo akina Kassim Hanga sasa hapo walipokaa ushauri, jamani e, hapa bwana hapapatikani nchi, na akina Ali Muhsin ndo nanga kama hii, na uchaguzi unaokuja karibu bendera zitapandishwa. Kwa hiyo bwana la kufanya tukaeni kikao cha kujadili tufanye nini.

Suala la Tupendane bwana…Tupendane lilikuwa na mambo makubwa na mwenyekiti wake ni mwenyewe Mzee Karume. Yeye ndo mwenyekiti aliyefanya mpango wa kuwatafuta vijana wa Tupendane, vijana wa kibara. Tupendane, kijana wa Kizanzibari hayupo. Pahala popote, mtu yoyote mkatalie. Mwambie kwamba Tupendane kijana wa Kizanzibari hakuwepo. Tupendane walikuwepo kwanza Wazaramo, Wandegereko, Wayao, Wamwera, Waruguru…hawa ndiwo waliefanya mpango wa kulizuwa Tupendane.5 Ni vijana wa kibara waliotambuwana. Mzee Karume aliwakusanya pahali pamoja akawaambia “skilizeni, mimi staki kujitokeza ila nyinyi vijana nnataka mnifanyie kazi yangu. Kwanza Hizbu lazma wataulizana kutokana na haya mavazi yenu na jina lenu litakuwa Tupendane.” Na kwa kweli walikuja wakaulizana “mambo haya vipi, hawa vijana namna gani?” Mpaka Wahindi walibidi kila wanapotokea wale vijana ikiwa wawili ikiwa watatu ule mwenendo wanaokwenda “Tupendane e, Tupendane.” Ikawa kama msemo tena ndani ya mji.

Lakini halafu kumbe Mzee Karume alikuwa na lengo lake suala la Tupendane. Aliwakusanya wale akawaita, akawaambia njoni. Baada ya kuwakusanyaa, kilichotendeka akiwepo mwenyewe Mzee Karume, akiwepo Sefu Bakari, akiwepo Natepe, unaona bwana, akiwepo na Antoni Kisasi, halafu alikuwepo nani? Mzee Adamu, alikuwepo Kamishna wa Magereza. Huyu Mzee wa Kiyao huyu. Walikuwa watu kiasi wanane hivi. Wakawaambia, “skilizeni vijana, tunachokwambieni, sisi hapa Afro-Shirazi ni wapinzani, sasa tunachokwambieni, kura kila ikipigwa tunakosa na sisi ni wengi kuliko wao. Sasa tunachotaka siku zile tutakaposema sasa tunachaguwa, uchaguzi, kazi ya Tupendane ni kufanya kurpushani.” “Kurpushani vipi?” Akasema, “eheeeeee, kurpushani yenyewe wakati mnajuwa jimbo fulani panaingia uchaguzi. Mmeshachaguwa. Mnatoka. Shati ulilolivaa wakati ulipokuja kupiga uchaguzi, si utakalokujia tena.”

Mpango ule ikabidi ukapangwa, halafu hapo ndipo alipotoka Yusuf Himidi, akasema “skiliza Mzee Karume, kazi ya Tupendane kubwa nnayoiona mimi ni hii moja, hayo yote sawa, Jee, wale wanaejiita Wangazija, wanaejiita Waarabu, wanaejiita Wamanga, na Waswahili, kuna Uwarabu wa kununuwa, kuna Umanga wa kununuwa, kuna Uswahili wa kununuwa, ni katika sie Waafrika wenziwao. Nnachosema mimi Mzee Karume nakwambiaje? Tupendane wale ndio wakuwa cover [wakuwafuatilia] kwelikweli. Kwa sababu mambo yoote sisi wale ndio wanaotuharibia.6 Kila tunalolifanya wale wako mstari wa mbele. Sasa huku sisi kila tukisema tufanye hivi tufanye hivi limeshafika. Kwa sababu nini, ni Waswahili wenzetu, kabila imekuwa ya kununuwa. Sasa badili ya kabila ya kununuwa ni kujipendekeza. Sasa ikiwa ni kujipendekeza bwana kazi ya Tupendane ni mtu akifanya…[upuuzi] rohoni! Hapana kumstahi. Rohoni!”

Mwanya ule Sefu [Bakari] ndo aliposema “sasa sisi mtu harakati kwa masuala kama haya ambaye anaweza kuifanyia harakati hii timu hii basi tumpate Ibrahim Makungu, tumpate Hassan Mandera, kwa sababu yeye ndo atakuwa benet benet [bega kwa bega] na hawa.” Kwanza, Sefu Mdengereko, ni ndugu zake hawa [Tupendane]. Mimi Yusuf nikijitia katika kundi hili, wengi watasangalia. Huyu Yusuf ana nini? Huyu Yusuf khasa, Yusuf Himidi, ana nini? Lakini Sefu hawamsangalii, watajuwa kwamba “si jamaa zake, wote hawa wabara watupu.” Mzee Karume akaja akasema “sawasawa hiyo.” [Ibrahim] Makungu sifa yake yeye ni kuuza tende [ulevi]. Kivutio. Kazi ile walimpa maksudi. Kwamba wewe ni kivutio. Akija mtu pale yale anayeyazungumza si akili yake. Huyu Mandera kazi yake yeye kama unavojuwa kazi yake ni kunyakuwa tu. Gari ya Kipanga ilikuwa inakwenda kwa siiri “bwana we, kuna mtu keshaanguka kwa Makungu na aliyetueleza haya, haya, haya, haya.” Sasa Tupendane mnasemaje? Haya chukuwa! Anachukuliwa. Ngazi Mia unakujuwa? Anapelekwa Ngazi Mia. Akipelekwa Ngazi Mia tena wao kule la kumfanya wanalijuwa wao. Sasa watu wanashtukiwa tu “Ah! E bwana we. Kuna mtu kule alilewa lakini tena mabiruko yameshambirukia.” Hakijulikani kitu gani. Kumbe Tupendane hao. Sasa imekwenda kwenda, imekwenda kwenda, imekwenda kwenda, imekwenda kwenda, Mzee Karume dakika ya mwisho…

Kazi ya Musa Maisara haijafika. Musa kazi yake itafika. Lakini hii kwanza wende watu wawili hawa. Makungu na Mandera. Wewe Sefu kazi yako, wanapokuja unaposhona vifungo, Tupendane wao wanazungumza na wewe kuwaficha hawa watu hawa. Makungu na Mandera. Suala lile lilikwenda, lilikwenda, lilikwenda, hatma yake Mzee Karume akaja kuita tena kikao. Na kikao hicho kilikuwa na watu wangapi? Baada ya Sefu, Kisasi, pamoja na huyu, Makungu, na Mandera, na yeye Mzee Karume akiwa ni mtu wa tano. Akaanza kuwauliza “jamani eee, sasa, hakika sasa tunaamini kwamba Tupendane kazi wanazozifanya ni nzuri sana. Jee, tunafikiri nini, mfumo wa baadae? Hawa si watakuja julikana? Si watakuja julikana hawa? Wakija julikana sisi roho zao tutaziweka wapi? Au tutawafanyaje vijana hawa?”

Nakumbuka mjadala huu ulikwenda wakafikia mahala pa kusema “saasa, la kufanya, hawa tuwafanye kama vijana wa Youth League.” Tuwafanye vijana wa Youth League. Sasa vijana wa Youth League itaonekana tu “hawa Youth League bwanaa.” Sefu yeye ndo mwenyekiti pale. Sasa ina maana hii timu tulioipanga hii, itafanya vipi? Timu tulioipanga itabidi ikae kitako. Makutano ya hawa kwa wakati wake. Tupendane mmoja atowe ripoti zake kwa Tupendane kwa jumla. Sio kundi. Sasa ikabidi hapo sasa wakatumia njama hizo zimekwenda, Mzee Karume akaja akasema “hapana.” Michenzani pale palikuwepo chama cha densi. Akasema “hawa waingie kwenye muziki.”

Lakini siri hasa kubwa zaidi ndo hapo alipokwambia Mzee Issa “bwana wee, haya mambo haya kweli wengine wameshakufa lakini sasa kuna wawili wahaiii! Wawili wahai.” Sasa wawili hawa wakija kuupata mnongono huu kamba hukatikia pabaya. Atajulikana ni yeye [Mzee Issa]. Wawili wako hai. Viongozi. Wanaelielewa suala hili shina. Na siri hii wameificha siri kabisa! Kwa sababu mpaka chama cha upinzani hakijuwi kwamba Tupendane hawa hasa walikuwa na shughuli gani? Unaona bwana? Sasa walio hai. Natepe yuhai, Hamid Ameri yuhai, katika memba wa Baraza la Mapinduzi hao. Sasa na hawa wanajuwa hili suala hili. Wamelifunika, manake wamechukuwa chungu wakakifunikiza “jibuuu.” Ndo maana Mzee Issa akakwambia “bwana we, hilo suala zito kwa sababu hawa watu hawa wahai, sasa wakija sikia Issa Kibwana katowa hadisi hii kwa urefu, bwana itakuwa mimi, serikali itaniandama. Itaniandama vibaya vibaya!” Wakintia mkononi itabidi waniulize. “Bwana we, ilikuwaje? Haya mambo haya. Woote wapinzani hawajuwi. Wewe umelitowa. Haya vipii? Kwa madhumuni gani? Ilianzia nini?” Nitakuwa la kusema sina. Ndo ukamuona Issa kila ukimbumbukiza anakwambia “Mmmmhh, bwana we, hebu tulia” kwa kuogopa watu hao wawili ambao walio hai wanaolijuwa suala hili.

Waliobakia wote unaowaona maofisini hawaelewi nini maana ya Tupendane. Hawajuwi kabsaa! Sasa utakuja kuta kwamba baada ya hapo, Mzee Karume sasa akaanza sasa kurpushani zake kwamba hawa Tupendane, wewe utakwenda sehemu za Ndagaa, huko utahudumiwa na chama, wewe utakwenda Mkokotoni. Sasa ripoti za mule moootee mule wanakuja mjini hapa anapewa mtu huyu mmoja. Akipewa huyu mtu yeye hasimami, moja kwa moja anakwenda kwa Kisasi, kwa sababu Kisasi yeye mkubwa wa polisi. Sasa baada ya yeye anamuwakilisha Mzee Karume. Bwana kesi nilioipata kwa Tupendane hii, hii, hii. Wakati huo huyo mtu anakuwa havai nguo za Tupendane na Kisasi havai nguo za kipolisi. Anaweza kwenda nyumbani kwake tu, halafu yeye yule anatoka Kisasi anamuendea Mzee Karume “bwana, iko hivi, iko hivi, iko hivi.”

Mzee Issa nakumbuka randa yake akitoka Kisiwandui pale, huyooo, anaelekea Malindi anaichunguza, jee huko kazi zinafanywa vipi? Zinafanywa hivi. Hayaa. Anatoka hapo Kinazini, vipi kazi inakwendaje huku? Inaendelea. Za Tupendane. Huyoo, Kikwajuni. Kazi inaendelaje huku? Inaendelea. Walichokifanya Tupendane, ile Kwahani ile, walikuwepo Washihiri, na ndo hao Wangazija Wangazija, sehemu za Michenzani humu, yaani wale walionunuwa kabila wale. Sasa askari wa Kenya wanapita huku, wanakwenda hivi, Tupendane, wanapita huku. Hawa wanakuja huku wanakuta maiti watatu wanne wamelazwa. Mpaka askari wa Kenya wakauliza “jamani, haya mambo vipi? Tumepita sasa hivi hapa hapana maiti. Huyu mtu keshauliwa huyu hapa.” Mpaka askari wa Kenya wakaingiwa na wasiwasi, kuwa juu ya bunduki zetu tunaweza kuvamiwa wakati wowote. Hawa lazima wanatumia dawa hawa kama wanazotumia sisi kwetu Kenya Mau Mau. Iko dawa wanaitumia hawa. Haiwezi kuwa. Wakaanza msako nyumba hata nyumba. Wanawakuta watu wamekaa wametulia. Jamani vipi? Kila wakimtizama mtu wanamuona wa kawaida. Kumbe, Tupendane huyo! Tupendane huyo bwana.

Wazungu walikuja kulijuwa lile suala, wakamwita Karume. Karume akajibu watu wangu hawana matatizo isipokuwa wanachokozwa. Wazungu waliona kuwa Waswahili ni wengi na wana nguvu kuliko Waarabu. Wazungu waliongeza vikosi na Karume akawabonyeza Tupendane na kuwaambia “tulieni” kwa sababu sisi hatuna ugomvi na Mngereza. Huyu akipeleka simu tu Uingereza kitakuja kikosi hapa sisi hakuna tutachofanikiwa. Muwe shwaariii! Kweli watu wakawa shwaari kabisa. Sasa watu walipoona hawa watu wametulia na haya mambo yamekwisha, ikabidi wale waondoke, waende zao, nyuma kukawa na utulivu. Karume kama anaitaka serikali Juni alipinduwa lakini alimuogopa Mngereza. Sasa Ali Mushin alitaka Mngereza aondoke kwa kuwa yeye ndie anaetuharibia. Sisi wenyewe kwa wenyewe tutaelewana. Karume alimcheka. Akamuuliza “umefikiri” Ali Muhsin akajibu “nimefikiri.” “Umefikirii?” “Nimefikirii.” Ali Muhsin akasema sisi kwa sisi hatugombani. Wakatiliana mkataba.

[Kina Hanga] hawakuwa na Tupendane. Tupendane wa mwenyewe Karume tu. Peke yake, na vikosi vake ambavyo alivokuwa ameviteuwa. Shughulikieni suala hili. Kwanza, Mzee Issa. Halafu kaja huyu nnokwambia, Mohamed “Mkunjeke.” Mdengereko huyu, anatokea Rufiji. Akaruka, Mfaranyaki, yaani Mfaranyaki ni Mngoni. Hawa watu watatu hawa.

[Mfaranyaki] alikuwa Tupendane. Lakini Tupendane yenyewe alikuwa chini ya Mzee Karume. Ripoti za kukutana na Kisasi, na nani, nani…yeye anakwenda anawakilisha moja kwa moja. Kama Mfaranyaki hayuko, Mkunjeke anaingia, au Issa anaingia. Watu hawa watatu. Mfaranyaki alikuwa karibu sana na Mzee Karume baadae alirejeshwa Songea. Saidi Washoto alitaka kuingia katika Tupendane. Mzee Karume akamwambia, “aa, hapana.” Kwa sababu alimuona huyu ni Myamwezi, hana ukweli. Kaujore kaja kuingia mwisho Tupendane. Mwisho. Sasa hawezi kuvaa suruali buga mtu mzima. Tupendane akijua tu nini kinatendeka.

Hamid Ameir alijuwa tu kwamba wako Tupendane na mwenyekiti mwenyewe ni Karume. Waliokuwemo Tupendane, Ibrahim Makungu, Musa Maisara, Antoni Kisasi, Yusuf Himidi, Sefu Bakari. Hawa watu watano hawa. Bwana wewe Yusuf Himidi aligeuka moja kwa moja. Kwani hizi silaha akileta nani? Yeye alikuwa dereva publiki. Kuna wale chipukizi wanovaa mabuga majiani. Wale mbali wale. Kuna magwiji. Hawakutaka wao kuvaa maguo yale. Hata siku moja.

Kwenye mapinduzi ya Zanzibar, mzalia wa Zanzibar, hakuaminika. Kabisaaa! Kwa sababu. Mzee Karume alisema, damu nzito kuliko maji! Mapinduzi yanataka kufanywa, wakishiriki watu Wazanzibari itavuja. Na sababu? Kuwadondowa watu wa bara. Alijuwa tu, hawa wakisema tufanye, watafanya. Mzanzibari akisema tufanye, atarudi nyuma. Na mfano mmoja ulionyesha. Hamid Ameir alisema, Muislamu kuuwa haramuu! Watu wakastaajabu. Muislamu huyu leo akaja kuwa Memba wa Baraza la Mapinduzi (MBM). Imekuwa vipi? Sasa hii pesa anayokula si haramu? Kumbe ilikuwa nini? Moga. Mikidadi ni mtu wa Tanga. Songorokirangwe ni mtu wa Donge, lakini ana asili ya kibara.

Mzee Karume akisema, Wazanzibari waliokuwa hawaaminiki sio nlokuwa nao mimi mikokoni mwangu. Mizizi yao ya karibu si ya hapa Zanzibar. Inatoka bara. Hafidh Suleman Mdigo yule. Bavuai yule ni mtu wa hapa, kazaliwa hapa, kama si baba yake, basi babu yake si mtu wa hapa…Hawakuaminika watu wa kusini. Makunduchi. Na Pemba ndo kabisaa! Kwenye listi ya wazee wa mapinduzi, Mmakunduchi mle hayumo. Huyu Ibrahim Amani katiwa tu. Hakushiriki mapinduzi. Kabisaa! Bambi wako wapinduzi. Bambi hiyo, Kinyasini, Mkwajuni palikuwa na wasiwasi, wakadokolewa kidugu Kidoti, wakaja kudokolewa kidugu, wapi? Donge. Wakadokolewa kidugu Mfenesini. Wakaja dokolewa kidugu jimbo la kati hilo hapo, Dole hii mpaka kuja kufikia wapi? Bumbwi Sudi, mpaka Ndagaa. Kwa sababu kule ni mchanganyiko wa watu wa bara. Jimbo la Kati hilo.

Sasa Wazanzibari watakuja itazama historia ya Ikulu. Kwa sababu zile picha zote zile wanajuwa huyu ni mtu wa wapi, huyu ni mtu wa wapi. Lakini wengi wao memba wa Baraza la Mapinduzi ni wabara. Mzee Thabit mapinduzi hakushiriki lakini kujuwa anajuwa. Lakini yeye huyu hakuwa memba wa Baraza la Mapinduzi. Sasa pale pameshajitenga. Sasa historia, chanzo chake, hawa kindakindaki [kutoka bara] ndo walolianza suala hili. Wazanzibari, kuwakera kitawakera lakini hilo suala limeshatendeka na wao hawakushiriki. Ndo ukweli wenyewe. Kwa sababu mgelikuwa mmeshiriki ndio. Mbona walioshiriki hawakutengwa? Ehe! Sasa watakuwa na masuala wengine watakuja kuuliza. Kama hukushiriki humo lakini mapinduzi ni yetu sote. Hukuaminika kiromoromo. Na madhehebu ya Kiunguja tunajuwana. Unamuangusha. Wengi wao watakaokuja ujuwa ukweli wataupenda, kwa sababu kuupenda kwenyewe kwa sababu nini, khasa kwa upande waliokuwa wamedhulumiwa wazee wao [wanamapinduzi]. Watasema nyinyi mnayetembea na mabenzi nyinyi bwana, baba zenu si waliofanya kazi hizo bwana! Waliofanya kazi hizo ni baba zetu sisi, lakini nyinyi mmevamia tu. Nyinyi virukia! Nyinyi bwana virukia. Sasa wale watachukia. Kwa sababu nini? Ureda. Wa bure.

Sasa hawa wenye uchungu ndio watakaofurahia. Hatukufikiria sisi yatakuja kufunguka haya. Bora yalivofunguka bwana. Wanatutambia hawa bwana! Ukweli wa mambo si huu bwana. Sasa utakuja kukuta wengi wao, khasa, khususan mashamba, wengi wao, basi watafurahia. Kwa sababu humo ndimo walikotoka watu ambao walioifanya kazi hii. Mashamba. Kwa sababu hata hao watu wa bara nnaokwambia wametoka mashamba ati. Hakuna mtu wa bara aliyekaa hapa mjini. Wote wameelekea sehemu za mashamba mashamba huko. Sasa, mule wamezaliana na watoto wao. Ndo mana Joseph Bhalo akasema “nchi hii mtihani.” Kwa nini Joseph? Anasema ehe! Mmakonde songa mbele, kumalizika mapinduzi, Mmakonde kaa pembeni. Hufai. Na leo utakuja kukuta Mmakunduchi hawezi leo kujitamba kama si Mzaramu. Si kweli. Wamakunduchi wote Wazaramu. Kunduchi hii ndo walikotokea. Hii mambo Shirazi haya, Shirazi Persia…Aliomo hatoki, na asiyekuwemo haingii.

Serikali watakipokea kitabu kwa mikono miwili. Watakisoma. Japo kidogo watakuja kusema “Mmhh! Hii sasaa funika kombe mwanaharamu apite, hii sasa imeshakuwa ngoma ndo hii.” Wataisoma ile historiaaa, watajuwa tu, hii ndio historia ya mapinduzi. Wanyonge kitabu kitawasaidia lakini iliokuwa mijoga na misomi watasema “mmh! Huyu sasa, bwana sasa, kula yetu sasa inafichuka sasa hapa. Hii kula sasa inafichuka hii. Tutakuja kuonekana sisi virukia sasa.” Sasa kitu kimeshatoka hakuna wa kukizuwia. Labda serikali iseme “hiki kitabu hivi kwanza bwana hapa, aa, ngojeni kwanza bwana.” Lakini sasa kikiziwiwa hapa, huko nje jee? Watu watataka kujuwa. Mbona hiki kitabu kinazuwiwa? Kwa nini? Kina nini ndani? Watakitafuta. Ikiwa watakipata Kenya, watakipata Uganda, watakipata bara. Sasa watakisoma wale. “Aaaa, serikali ya mapinduzi ndo maana ikazuwia kwa sababu kumbe haki za unyonyaji hizi kumbe hazikuanza leo bwana. Unaona watu walivowanyonya hawa? Kumbe huko nyuma kuna haki zao wameshindwa kuwapa.” Suala hilo usiwe na wasiwasi nalo. Tuliokuambia si wendawazimu. Watu na akili zetu timamu. Na hiki kitu tumekifanya. Mtu aliyefanya haogopi kusema. Anasema hivi hivi. Hiki nimefanya. Aa, hiki sikufanya. Sasa mimi ntakuficha wewe. Mwenyezi Mungu anafichika? Watu wanakufa midomo wazi. Wanasema “Ah! Mimi mpinduzi nakufa nawaacha watoto wangu maskini?” Huku walioikombowa nchi wanakula majani! Hawako radhi. Tukamate mavi kwa mkono na njia tunaiona?

Hakuna hiyo. Hamna, hamna. Madam njia wazi bwana, twende njia ilionyooka, sio tupinde pinde krosi. Hamna! Watu watajiweka sawa. Ndo watakapojuwa ‘Doo! Kweli ndo hii hapa.’ Sasa hivi jamani tujirekebisheni. Haya mambo yetu tujirekebishe. Waliokueleza si wendawazimu. Watu na akili zao! Wameishi na wakayaona yale mambo yaliotendwa. Wamefanya. Madhara yake, raha yake, tabu yake…Sisi tunapokufa Wallahi tunazikana wenyewe kwa wenyewe. Sisi wenyewe tunaingia vichochoroni “bwana we, fulani keshakufa.” Tunakamatana mashati. Tukope, tunyanganye tutalipa sisi lakini yule mtu tumzike. Wakati mwengine tunakwenda kuazima sanda msikitini! Halafu tunamzika mwenzetu, halafu tunarudi tunailipa ile sanda.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: