Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!

Icon

Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia

Mlango wa Saba: Ali Muhsin na Nduguze

“Hawa watu hawatoyawacha makoloni yao bila ya kukusababishieni matatizo makubwa tena ya muda mrefu.” Wakati ule nikifikiri yule bibi masikini alikuwa hakijuwi anachokisema lakini kumbe nilikoseya. —Sheikh Ali Muhsin

 

Mzee Selemani ni mmoja kati ya wazee ambaye hakupendelea jina lake kutajwa ndani ya kitabu hichi.

Kabla ya kuendelea na suala la Manamba ni vema tukaizungumzia Mikindani ilioko Lindi kusini mwa Tanzania Bara. Kutoka sehemu ya Rasi ya Lamu, kwenda Tanga, Saadani hiyo, imekuja Bagamoyo, ukanda mzima huu, mpaka umefika Lindi, mpaka umefika Mikindani, hii jamii, ilikuwa koloni la Kiarabu kupita sehemu hiyo.1 Sasa katika koloni hizo zilikuwepo sehemu Waarabu walikuwa wameweka kama makao yao makuu. Mikindani, sababu ya kuingiliana Wamakonde, wale wa akina Ali Muhsin, MaBarwani kule ina maana walikuwa ni watu walioimarisha. Kuimarisha kwao, walichokifanya, wamemuoa mtoto wa Kimakonde. Kumuowa mtoto wa Kimakonde, sio Mmakonde machale, wa maraba wale, ni Waisilamu hao, wamesoma kweli kweli hao. Baada ya Waarabu kuwaowa wale Wamakonde, imekuja wamezaliwa watoto. Kuzaliwa watoto, kabila si wanafata upande wa baba, wanakuwa MaBarwani? Sasa utakuja kukuta Natepe yeye hakubahatika. Kaolewa baba Mmakonde, mama Mmakonde. Lakini ni ndugu. Ndo maana aliposikia Ali Muhsin amefariki akasema “lo, jamaa yangu keshakufa.” Kwa kujuwa yule Ali Muhsin ni Mmakonde mwenzangu mimi, kwa upande mmoja wa bibi zake wa upande wa mama. Sasa Ali Muhsin kwa kwetu kule sisi tunaweza kusema ndugu yetu.2

Mchanganyiko wa Kiarabu na Kimakonde, haujaweza kusaidia katika siasa za kuleta amani Zanzibar. Unajuwa, kitu kinachotufanya hivo ni ubinafsi. Ubinafsi umejenga ubinafsi. Na ubinafsi huu kukatika kwake ni muda mrefu sana. Kwa nini nikakwambia ubinafsi umetujenga? Mtu wa Chwaka si anasema “mimi si ndo kindakindaki Chwaka?” Sasa mtu wa Kidombo anasema “ebo! Itakuwaje? Tumbatu yote yangu mie. Asili ya kutoka huko na huko sie tumefikia Tumbatu. Sasa tukasambaa, ndo tumekuja Kidombo, tumefanya hivi, kwa hivo mpaka hivi sisi hasa watu wa Mkwajuni ndo kiboko yao!” Wa Kusini pia wanakuja kusema hivohivo. Mwarabu pia alikuwa haolewi na Muafrika au na Besar. Mwarabu akiweza kumuoa Muafrika, lakini Muafrika alikuwa hawezi kumuoa Mwarabu hata kama ni Musilamu.

Sasa hii haiwezi masuala kama haya jamii ikawa kitu kimoja, kutafuta maslahi ya nchi. Mshirazi hakubali kirahisi kuolewa na mtu wa bara. Unajuwa sasa hivi, Wapemba bara hawakuchukiza. Ni watu waliopendwa sana. Tizama Dar es Salaam mpaka kuendelea kufika huko Msumbiji, biashara zao kubwa sana. Kubwa sana. Kiasilimia Zanzibar, Mpemba ndo anayeongoza kibiashara. Mpaka leo. Kwa sababu Wapemba wana kitu kimoja. Huna kitu, nakuuliza “bwana we? Haya maisha unayoishi, vipi?” “Aa, mimi naishi mpaka sasa hivi hali yangu iko ovyo tu mpaka sasa hivi.” “Hapana. Sitaki uishi namna hiyo. Kamata hiki. Funguwa biashara hapo.” MuUnguja mpango huo hana. Ubinafsi zaidi. Nimsaidie fulani? Atanifanyia nini? Mwache akae hivohivo. Bora akucheke kuliko kule kumwambia, mimi nnakunyanyuwa. Sisi hapa hatuwezi kusonga mbele bila ya kwanza kuondosha ubinafsi wa mtu, wa kijamii, na wa kimajimbo.3 Tusijikatae, lakini tusijipe umbele wenye kulirudisha nyuma taifa. Pili, tuundoshe huu U-CUF na U-CCM na tuliweke mbele taifa la Zanzibar.4

Lakini hayo mengine. Tukirudi kwenye mada yetu [Manamba], kwa mfano, utakuta Amboni Matias ambaye ni Mmakonde kaandika Manamba kutoka Mtwara, kaja zake mpaka Tanga. Kufika Tanga, pahala pa kwanza alipofikia, alifikia shamba la Girigi. Kufikia shamba la Girigi, kakaa shamba la Girigi, ndo akahama, kuhama na akahamia shamba la Baniyani Mbezi. Mbezi ndipo walipokutana na Victor Mkello. Mkello akaja akawaeleza, skilizeni, kuna kazi yangu inataka kufanyika Zanzibar. Sasa kitu tunachotaka, yaani katika nyinyi Wamakonde, nyinyi Manamba nyinyi, mkutanike, mimi kazi yangu kukutana na nyie, nipate kiasi ya kiongozi mmoja au wawili wa kuweza kulizungumza hilo nnalolikusudia. Wakati huo wameshakutana na Abdalla Kassim Hanga, Musa Maisara, na Victor Mkello. Wamekaa pamoja kulijadili suala kama lile.

Mkello, akasema, mimi nnachotaka kufanya, ni kuwashawishi hawa Wamakonde waliekuja Manamba. Nnapowapata hawa, ntawarubuni, kusudi kuja kukusaidieni kazi yenu lakini nnachokuulizeni, mnajuwa wanakokuja kuna kifo, familia yao itatizamwa na nani? Au wao wakisha fanikisha, watatizamwa na nani? Wakakubaliana viongozi watatu tu kwanza. Hanga, Musa Maisara pamoja na Victor Mkello. Hili suala tunaweza kukatibiana kwamba sisi hawa maisha yao, na atakayekufa, kizazi chake maisha yake, kwa hiyo mkataba huo ukapita. Alichofanya Mkello kuwashawishi akina Amboni. Akina Amboni wamekaa kigengi chao pamoja. Jamani, kuna kazi hivi, hivi, hivi. Sasa vipi hili suala? Wakakubaliana wote kwa sauti moja.

Sasa siri ile sio alikuwa anapita akisema tu. Anachukuwa kigengi cha wakubwa. Sasa wenyewe kwa wenyewe wanajuwana. Ikabidi lilivokamilika lile suala kwamba wale kukubaliana, wakati wa kuondoka, hawakutumia kuchukuwa likizo. Hawakusema sisi tunakwenda likizo pahala, au tunataka likizo. Aa! Victor Mkello alichofanya, kuwatilia right [tiki] kuwa hawa wapo wakati wakiwa hawapo.

Wakubwa, matajiri wa yale mashamba siri hiyo hawakuijuwa. Kwa sababu na yeye alizungumza kwamba hii isijulikane. Kwa sababu ikija ikijulikana itabidi hawa wataulizwa tu kama wametoroka au wamekwenda wapi? Mkello itabidi aulizwe kwa sababu yeye ndo alokuwa mdhamini mkuu wa wale wafanyakazi. Kwa sababu kwanza alikuwa anatetea haki za wafanyakazi wa mkonge wote, yule, Mkello. Shamba fulani kadhulumiwa mtu yule anaingia, e bwana, e mbona hivi, mbona hivi, mbona hivi? Sasa uwezo huo ndo maana akawa all round [kahusika na kote] yeye. Mashamba. Akaweza akawafikia hawa Wamakonde hawa kuwaeleza suala, kama lile, manake wanajuwa kwamba huyu ni mtetezi wetu mkubwa huyu.

Wamakonde hawa walikuwa wa mwanzo. Kwanza, Wangoni wamo, mpaka Wanyasa waliokuwa walowezi wa Tanganyika, wapo walikuwemo. Wahyao, walikuwemo. WaMwera walikuwemo. Wamakonde wa Lindi, walikuwemo, pia walikuwemo.

Kina Amboni wao ni Wamakonde wa Msumbiji. Wamakonde wa Lindi mbali, Wamakonde wa Msumbiji mbali. Hii ni jamii imetiwa pamoja tu, kwamba jina ni Wamakonde. Kwa sababu bara hakukuchuliwa kwamba jamii ya Kimakonde peke yake ndo ilochukuliwa. Hapana. Yamechukuliwa makabila tafauti. Na waliochukuliwa zaidizaidi ni wale walokwenda vita vikuu vya pili va dunia. Ndo wale waliochukuliwa kwa sababu walijuwa kulenga risasi. Na usifikirie na hawa Wamakonde na hawa, kwamba wamechukuliwa bila ya fani za kivita walizokuwa nazo. Mkuki huu hapa, mpinde huu hapa, panga hili hapa. Mimi najuwa bunduki, bunduki.

Sasa ikawa kutokana na wale nnaokutajia kama Wangoni, Wahyao, Wamakuwa, wao wamechaguliwa kutokana na Mkello. Yeye aliwataka wale watu hasa waliekwenda vita vikuu kupigana, yaani wakati huo wakiita KAR [King African Rifles]. Aliwapata wale. Wakaingia. Kuingia, kilichofanyika, kuficha ile siri, kwenye mashamba, ondoka yao kutoka Kipumbwi kufikia Muwanda. Muwanda walivofika, hawakusambaa kwa kuja mjini. Wamepitia huko kwa huko, wanaefika Ndagaa, wanaefika Ghana, Dole, Ndunduke, hili Jimbo la Kati tu. Wao walikuwa wamo katika sehemu hizo. Kitu kikubwa walichokifanya, kufika kuchukuwa panga mahala wanalima. Huku shughuli zinaendelea. Mpaka kuna baadhi ya vikao misituni, hapa, kama va Masingini, shamba la Ndagaa lile, walikuwa wanashirikishwa, lakini nakumbuka kushirikishwa kwao katika sehemu ya Wamakonde, [Fundi] Tajiri peke yake ndo aliekuwa akishiriki vikao hivyo. Wengine hawajenda. Yeye akirudi anawaita wale kibusara. Kikao cha leo hivi hivi hivi…Kuchukuwa kigengi cha Wamakonde kuwapeleka sehemu za misituni kwenda kufanya mkutano siri itakuwa itatoka manake watu wataona “mbona hawa Wamakonde hawa wanaingia sana kwenye misitu. Kuna nini?”

Tajiri alikuwa Mmakonde wa Msumbiji. Tena machale hasa. Pwani hapo, custom [sehemu ya mizigo bandarini] nakumbuka kawahi kufanya kazi miaka mingi. Kwa hiyo utakuja kukuta alikuwa ni mtu mzowefu, mpaka Waarabu walimzowea, kuona kwamba huyu mfanyakazi mzuri, mtaratibu, kwa vile hawakuwa na shaka. Lakini kumbe ulikuwa moto wa kumbi. Unamungunya chini kwa chini. Baada ya kukamilika jamaa, Mkello kaja Unguja, akakutana pamoja na Kassim Hanga. Baada ya kukutana na Hanga, Hanga akasema, sasa hii kazi imeshakamilika. Sasa madam imekuwa imeshakamilika sasa tumwite Yusuf Himidi kwa sababu Yusuf Himidi ni mkubwa wa ukusanyaji silaha. Hili suala la Manamba na yeye alielewe. Alikuwa halijuwi. Alipoitwa Yusuf Himidi, Yusuf Himid na yeye akasema “hata!, nisiwe peke yangu.” Nendeni Mikunguni kamwiteni Mfaranyaki, alikuwa anachonga Mikunguni. Kamwiteni Mfaranyaki. Wakakutana Mkello, Twala, Hanga, Yusuf Himidi, na Mfaranyaki. Wakawa watu watano. Yusuf Himidi kumpenda Mfaranyaki ilikuwa kwa sababu Mfaranyaki kenda vita vikuu, na anajuwa nini vita.

Baada ya kufanikiwa yale mauwaji yalikuwa makubwa sana. Hii ilikuwa kutokana na Wamakonde [na makabila mengine kutoka bara] walikuwa wageni. Wanaona, mpaka sasa hivi huyu ndiye, huyu ndiye. Kumbe sio. Afro-Shirazi wangapi waliuliwa. Kuna Afro-Shirazi tulikuwa nao Waarabu, Washihiri, Wamanga. Wapo. Kwa vile Wamakonde waliingia kama ni wageni wasiejuwa kitu. Ndio Mzee Karume akasema “hapana, ho!” Anayekamatwa aletwe Raha Leo. Na wale [Wamakonde na makabila mingine] wakaambiwa, kilichobakia, wapi? Moja kwa moja Miti Ulaya. Wakaletwa Miti Ulaya, Miti Ulaya pale tena ikabidi wakapolea, walivoambiwa “kazi yetu tuliokusudia imekwisha! Sasa murudi kwanza majumbani mwenu, mtulie, tupange serikali, tupoze haya mapinduzi yetu, halafu tukae pamoja tulijadili suala lenu nyie na sie.”

Kila waziri wa wakati ule baada ya kuchaguliwa waliwekewa Wamakonde kuwalinda kama ni walinzi. Ilikuwa mwanzo tu. Manake na suala hilo halikufika hata mwezi. Lilifanyika mwanzomwanzo. Mwanzomwanzo tu. Baada ya kuchaguwa mawaziri wakasema, sasa hawa washirikiane na watu kulinda, kutafuta nini, kwamba wale mtu anavotokezea akimkuta Mmakonde machale kama yule anasema “huyu bwana, aa! Hana stahmali huyu.” Lakini mwezi haukufika ikaondoka ile halafu wakawekwa polisi tu. Mwanzo mwanzo ule. Joto joto lile.

Baina ya kufikiwa Manamba na mapinduzi hii bwana ilichukuwa chini ya miaka miwili. Chini ya miaka miwili ilitokea hiyo. Hii ilifika miaka miwili, inakwenda tu, inakwenda tu. Kwa sababu nini kufanya hivo? Lile suala halikuwa la vu! vu! vu! tu. Ni suala la kuwatongoza wale. Sasa Mkello alochukuwa dhamana akasema hii kazi niwachieni mimi. Ndipo alipofanya utaratibu.

Mkello kazi ile alipewa na Hanga. Na Hanga katoka hapa kampata yule baada ya kusema kwamba…Hanga alichotumia, Oscar Kambona kamwambia, weye kama unataka ufanikiwe uwapate watu wa Tanganyika. Kwa sababu watu wa visiwani wanajuwana, na halafu wamezaliana.5 Utamuona huyo Mswahili wa Tumbatu, lakini Mwarabu kamuoa dada yake au mama yake. Sasa kwa vyoyote utavofanya wewe, ukimpiga Mwarabu, yule pale aliyemzalia dada yake, basi ni lazima ataona uchungu, mtapigana. Sasa na siri hii, usiitumie kuisambaza kwanza Zanzibar. Hapana. Itumie kwanza kuisambaza kule bara.6 Hapo utapata mafanikio. Ndio ikabidi Oscar wakati ule Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje akija hapa, na alikuwa kuja kwake kama kupitia, anakwenda safari zake, ah! Ntateremka Zanzibar. Anateremka hapa, anaonana na Mzee Karume, lile suala sasa, Mzee Karume hamzungumzii, anamzungumzia Hanga. Siri yao. Ndo akamwambia, unataka Wamakonde machale, yuko mkuu wa Manamba, umpate huyu. Mimi ntampataje huyu, mbona simjui? Njoo Dar es Salaam. Akenda Dar es Salaam.

Kilichotendeka, Oscar akamwita Mkello. Wakakutana sasa watu watatu. Bwana nilokwitia huyu hapa, mimi nishazungumza yangu kwamba kuna mtu atakutana na weye. Bwana, yule mtu niliyekwambia ni huyu. Sasa tufanye nini? Akasema la kufanya bwana hivi sasa hivi tunataka hivi: tunataka Manamba wako. Tuna kazi yetu tunataka kuwatumilia. Je, bwana msaada huu utatusaidia? Mimi ntakuwa tayari lakini kutokana na utaratibu wa hao watu… Si kazi yako hiyo. Wewe utufanyie kazi hiyo tu. Kazi ya hao watu tunayo sie. Sawa! Unajuwa tena na yeye yule lazima kutoka pale, anaambiwa motisha yako hiyo hapo kwa hiyo kazi unotaka kuifanya. Mkello akashughulikia mpaka akafika kuhitimisha. Baada ya kuhitimisha, Oscar alipoona imekamilika, akamdokolea Mwalimu. “Mwalimu eh! Tunakaa, lakini Zanzibar Afro-Shirazi wakati wowote wanaweza kuipinduwa ile serikali.” Mwalimu akasema “eh, vipi?” Akamwambia “wanaweza kuipinduwa wale. Lakini siri hii, wewe na mimi, na Mkello, lakini Karume usimwambie.” “Nisimwambie vipi Karume?” “Hii siri anayeijuwa, mimi, Musa Maisara, Hanga, Yusuf Himidi, na Jimmy Ringo. Hii siri ndo wanayoijuwa pamoja na Mfaranyaki. Ndio waliokuja kunieleza mie kisiri. Lakini njia watakayoitumia, watawatumilia Manamba.”

Mwalimu alimwita Hanga. “Njoo. Kuna mnong’ono kidogo nimeupata.” “Umeupata vipi mnong’ono huo?” “Kuna mambo kidogo ya chinichini lakini hii ni siri kubwa. Kweli Unguja nyie mnaweza kupinduwa hii serikali, kweli?” Akamwambia “tunaweza.” “Sasa kwangu mnataka msaada gani?” Utusaidie, wakati utakaposikia nchi wameshaanza kupambana nao wale basi utuletee jeshi lako kwa siri. Pasi kujuwa. Kwa sababu wakijuwa watu, ile nchi tukishapinduwa itabidi sasa kabla hatujakaa miaka mitano, au miaka kumi, kwanza hapa itabidi wewe na sisi kwanza tuwe “benet, benet! [bega kwa bega]” Tukiwa sisi tu, wakati wowote tutaweza kupinduliwa. Mwalimu pale akaingia top [tele].

Akasema “sasa hii, Zanzibar ntaipata!” Hapo ndipo palipojengeka…lakini akasisitiza, akamwambia “Oscar njoo, na wewe Hanga, hebu njoo!” Bwana wewe sisi tunakusisitiza, kuna siri nyuma ilitendeka hii ikavuja. Jamali Nasibu aliivujisha. Karume kidogo tu auliwe. Sasa, sasa hivi tumegeuza mbinu. Sasa hii bwana, usije ukamwambia Karume kwa sababu Karume alisema “Wacheni kabisa! Wacheni!” Huyu sasa sisi itabidi tumwambie siku ya mwisho. Sawa sawa. Wakakubaliana. Mwalimu unajuwa tena mtu wenyewe, “mimi nimeshalizuwia hili, lakini nyie kuna Mfalme kule, na kuna Mngereza. Bwana mkija mkaanza vurugu hiyo msije mkampiga Mngereza! Hamfanikiwi. Mkija mkimgusa Mngereza bwana nchi mtaiona chungu kwa sababu yule Mfalme analindwa na Mngereza. Jamani msije mkafanya hivo?” Tumekubali. Sawa. Na kwa kweli yaleyale aliyeyazungumza Mwalimu ndo yalofatwa. Mngereza hakuguswa. Mngereza hapa nakumbuka yule wa jela aliuwa lakini jamaa wakasema “jamani msimdase huyo!”

Manamba walipomaliza mapinduzi wengi walikuwepo hapa, wengi walifanya kuselelea, wameselelea wengi tu. Wao na familia zao,7 walokufa wamekufa, waliobakia akina Amboni hao ndo wapo. Kama Tajiri alijiajiri kazi hapa. Alivotoka Manamba yeye kuja hapa, akajiajiri kazi, kwa sababu ukitazama utaona Tajiri alikuwa hadharani, na tizama basi Mwenye Enzi Mungu alivomjaalia, aliweka videvu, ndevu zake zilijaa zikawa nyeupee! Waarabu walimpenda sana. Kutokana na rangi yake ile na zile chale hazikuwa za kuonekana sana. Basi mjini utamkuta kakaa kitako barazani anazungumza na Waarabu. Wakisema “huyu Umakonde kapitia tu lakini huyu hasa baba yake huyu Mreno safi huyu.” Kachanganya yeye basi alikuwa ni mtu waliyempenda. Kustaafu kazi akenda zake Mfenesini. Khamisi Hemedi mbele ya Tajiri alikuwa hafui dafu hivo? Hasemi kitu. Hasemi chochote. Ndo mambo yalivokuwa yamekwenda.

Manamba waliokuja hapa viongozi wao walikuwepo hawa watatu. Baada ya Tajiri, alikuwepo mmoja Thomas, alikuwepo mmoja tukimwita “Kangaroo”. Walikuwa watatu hawa. Hawa ndo walokuwa mstari wa mbele wa kuwaongoza wale Wamakonde. Kwa sababu mara nyingi sana walikuwa wanatumia kilugha. Halafu wanasemeshana kilugha. Mpaka listi Mzee Karume anayo ya hawa watatu. Watu watatu hawa walikuwa watu madhubuti. Hawatetereki. Na kiapo chao waliapishana, wenyewe Wamakonde kwa Wamakonde. Bwana kama tutafeli, ukija ukikamatwa, bora ukatwe kichwa, usiseme.

Kazi ya Manamba ilikuwa zaidi katika kuyavamia maboma. Mtoni alikuwepo Tajiri. Hawa wawili, Thomas na “Kangaroo” walikuwa Bomani. Katika hawa watatu Tajiri tu peke yake ndo alokuwa Mtoni. Kwa sababu Mtoni Tajiri alisema “askari walioko Mtoni vitoto vidogo. Hawawezi kuhimili vishindo wale. Watakimbia wale. Lakini kambi kubwa Ziwani. Watu walokwenda mpakani wapo pale.” Akina Anthony Musa, wale wamekwenda vita vikuu na ndo walokuwa wakifundisha kule. Sasa operation ya mwisho wa kuwapanga wale, Anthony Kisasi ndo aliekuwa kapanga. Walikuweko na wengine. Weye uwende kule, nyie mushirikiane na hawa jamaa. Mwende Bomani, mwende Mtoni.

Bila ya Manamba mapinduzi ingekuwa si rahisi kufanyika. Si rahisi. Kwa sababu yenyewe, nnavokwambia. Moja tumelizungumza kwamba, sisi tunajuwana. Na mauwaji yalikuwa kwa wingi kwa sababu tulikuwa na wageni hawawajuwi wenyeji.8 Wamakonde, na makabila mengineyo kutoka bara, walikuwa wageni.9

Kutoka Bomani, boma limeshapinduliwa, pale pamebaki, askari wa Afro-Shirazi wapo pale, na wapinduzi wa Afro-Shirazi wapo pale, mchanganyiko pale wa Wamakonde…nakumbuka Ziwani watano, Mtoni watano, Malindi watano, wangapi hao? Kumi na tano. Waliobakia kumi na tano. Kumi na tano wanaingia kwenye magari ya patrol [kuranda doria]. Zilikuwepo gari za patrol kama sita hivi. Hizo gari zilikuwa zinafatana na mwenyewe John Okello.

Wana-round (wanazunguka) sasa, Unguja na mashamba. Unajuwa ndani ya kundi, kuna watu wana chuki binafsi. “Mwarabu huyu hapa!” Sasa unajuwa “Mwarabu huyu hapa” hapohapo Wamakonde watatu, wanne, watano. Nyote mnashuka pale. Sasa unajuwa, ukatili wa yule, yeye anakwenda tu anaingia tu mle ndani. Hamshauri mtu. Tena ikiwa panga, panga tu anaelekeza. Nyie sasa watu hapa mnaejuwa mnasema “aaa! Sivo hivyo.” Halafu yeye anarudi anakwambia “njomba, wewe mbona umekuwa una huruma, hawa wamekutawala, leo wewe unafanya huruma.” Sasa mtu kama yule sisi tulikuwa tunatahadhari sana nao wale. Ndo ikabidi ripoti sasa. Kwanza alielezwa Mfaranyaki, “Mfaranyaki eh! Sasa mauwaji yamekuwa makubwaa.” Sisi kazi yetu sasa hivi ni kuwachukuwa watu kuwapeleka Raha Leo, sio kufika leo ikawa mtu anauwa. Sivyo namna hii. Mfaranyaki alichofanya yeye, kamueleza Okello kwa Mzee Karume. Mzee Karume “zuwia sasa mambo ya mauwaji, kwa sababu sasa yamekuwa makubwa.” Sasa katika 10,000 aliowataja Okello, walouwa wengi wao wakiwa mchanganyiko, wengi wako wale wabara nlokutajia. Hili gurupu nnalokutajia mimi ni la Wamakonde tu. Makabila mengine waliuwa, na Wazanzibari pia, lakini hawakufika kiwango cha Wamakonde. Tuligutuka sisi, tukiwaogopa wenzetu. Ndo ikaamulika “hapana, na wakusanywe! Wapelekeni Miti Ulaya.” Wakaambiwa kaeni hapo. Kazi imekwisha, sasa kaeni hapo. Sisi tunabakia tukipita tukiwachukuwa watu tunawaleta Raha Leo.

Mimi nakumbuka nilikuwa 64 [jina la mtaa] hapo. Kuna Mwarabu alikuwa anatukana ile mbaya, lakini nyumba hii kwa hii. Sasa mimi nilivoona nikasema sasa huyu watamuuwa. Mbona nilichomoka na bunduki zangu mbili, nikaja zangu mpaka pale, nikamgongea mlango “pa, pa, pa, pa.” Akasema “ah, …anakuja kuniuwa.” Nkamwambia “funguwa wewe!” Namwambia “funguwaa!” Akafunguwa, nkamwambia toka huko ndani, njoo kwangu. Nikamtowa yeye, mkewe, watoto wake. Nikampeleka kwangu, nkamwambia, bwana nakukomelea, chakula hicho hapo, stover [jiko la mafuta ya taa] hio hapo, hakuna raha hapa. Pika ule, choo ndo hicho. Usije ukafunguwa mlango mpaka ukasikia mimi nnagonga. Sijaondoka mimi ile nyumba yake wamekwenda kuivamia watu ati. “Vunja, vunja! Vunja, vunja!” Kukukuu, kuingia ndani wanakuta hakuna mtu.

“Mwanaharamu, kakimbia huyu!” “Keshakimbia huyu mwanaharamu.” Mwarabu huyo nnakuhakikishia mpaka leo, Maskati aliko huko hukaa akasema “mimi namshukuru Selemani” Mimi nikaona “hmm!” Mimi yule sku moja alintukana matusi ya nguoni lakini mimi siyajali yale matusi. Mimi nijali roho yake. Nikenda nikamtowa bwana. Nikamtia mwangu ndani. Nikamueleza palepale Mzee Saidi Kibiriti nikamwambia “nyumba yangu ile pale asije akagonga mtu. Uwe mkali sana.” Kufika Maskati mwanawe mmoja huwa anakuja. Anapokuja anakuja mpaka nyumbani. Halafu hivi karibuni nlipata habari alikuwa ana safari ya kuja huku lakini bahati mbaya alipatwa na accident [ajali] ya gari.

Sasa tulivoona sasa Okello hili blanket [guo] anataka kulitumia vibaya, akaambiwa, hebu nenda ukakaguwe Pemba. Mimi nimeshuhudia yangu katika hizo safari za Okello na Wamakonde. Nakumbuka, najuwa, kutoka kwa Ali Natu [jina la mtaa]. Tumekwenda kwa miguu, moja kwa moja tumekuja zetu, tumekuja pinda Raha Leo, tumeingia kwa Haji Tumbo [jina la mtaa]. Kwa Haji Tumbo tulipofika, Mshihiri alikuwa hana habari kumbe serikali imepinduka. Kafunguwa hoteli yake, maharagwe yanapwaga, sasa, Okello akamuuliza “Mwarabu eh! Umefunguwa hoteli, usalama gani wewe uliokuwa nao.” “Ah, karibu bwana, karibu.” “Aa! Umefunguwa hoteli leo, usalama gani unao weye?” “Kwa nini basi jamani. Hebu nielezeni.” Wewe huna habari kama serikali imepinduka. Imepinduliwa serikali. Basi Mshihiri pale pale alipinduka “tu!” Sasa tizama Mmakonde hatari alokuwa akitaka kuifanya. Aipuwe maharagwe kwenye sufuriya amwagie! Akitaka kumwagia. Ikasukumiliwa mbali huko na Okello. Akamuuliza “we! Sasa huyu mateka unataka kumwagia maharagwe sufuria zima, unajuwa hii sufuria nzima unauwa? Unauwa!” Sasa Okello, alichofanya kutokana na yeye ilimjia hisia kwamba sasa mbona kunatumika ukatili. Pale pale, alimwambia “wewe utafatana na mie.” Mshihiri, sisi na familia yake akatwambia “mpelekeni Raha Leo.” Mimi nafsi yangu tukamchukuwa mpaka Raha Leo. Tukamuweka tukarudi tena.

Sasa Okello alichofanya yule Mmakonde kamchukuwa moja kwa moja mpaka kwa Yusuf Himidi. Anasema “huyu si mzuri kwa vile adabu yake huyu apelekwe moja kwa moja Kiinua Miguu, jela, afungiwe, mpaka tumalize haya mapinduzi hapa haya kwanza. Huyu damu imeshamlevya huyu.” Yusuf Himidi akamweka ndani kama hifadhi ya kumuweka atulie. Kweli wewe mtu leo, mie umenikuta umeniuliza kitu, sasa katika ile kuniuliza nimefanya msangao wangu, roho imenishtuka, nimeanguka, uchukuwe kisu tena unipige? Unguja hii Wamakonde wameshindwa kwa Sayyid Sudi [Sayyid Soud bin Ali bin Humud] peke yake. Kwa Seyyid Sudi peke yake ndo walokoshindwa Wamakonde.

Lakini kwa suala la kimapinduzi, madam wale tuliwachukuwa ni Manamba, lazima watumie uwezo wa aina namna hiyo. Manamba, walikuwepo viongozi. Viongozi hawa ndio waliokuwa wameshirikiana kwanza hapa. Mmoja akiwa Hanga, akina Juma Maneno hao, akina Jimmy Ringo hao. Mpaka yuko yule jamaa wa Tanga, Victor Mkello, ndio alipitia kwa sehemu ya Chama Cha Wafanyakazi. Katika kifungu cha wafanyakazi, wao wa bara ndo wakaweza kutowa ufumbuzi wa kujuwa kuwa sasa hivi bwana tufanye utaratibu wa kukutana na wenzetu bara, kule bara tutumie njia ya kupitia upande wa jamaa wa Chama Cha Wafanyakazi. Walimpata Victor Mkello wakakaa pamoja kulijadili suala hili. Hili kwanza ilikuwa kwa kuelezwa na mzee Abdalla Kassim Hanga, pamoja na Juma Maneno, halafu na huyu Jimmy Ringo, na huyu Musa Maisara, mpaka Natepe pia alikuwepo, akina Sefu Bakari hao, walikuwepo kulijadili hilo suala. Halafu, kinyume chake, Natepe na Sefu kwanza waliwekwa pembeni. Hanga ndo alokuwa hili suala alikuwa kalizamia mbizi. Kulifanyia utafiti, njia gani nipite kusudi hili suala isijulikane nnafanya nini. Hata nnafikiria hata baada ya kukutana na hawa, mkuu wa Wafanyakazi wa Tanganyika, Victor Mkello, ambaye kuona kwamba Manamba hawa ntawatumilia kwa kuwapeleka Zanzibar kwa kushirikiana na wale wenzi wao. Hapo baada ya kupata usahihi huu walifanya safari Hanga na Hasnu Makame wakenda bara kukutana na Mkello. Walipokutana na Mkello, wakapanga ushauri, kwamba sasa bwana utaratibu wa kuikombowa Zanzibar ni lazima tushirikiane baina ya nyinyi na sisi, nyinyi mutupe msaada. Tupate kujikombowa.

Kule walikotoka Tanga kwenye mashamba ya mkonge, Manamba walikuwa wakiishi ndani ya jamii za makabila yao. Jamii ya KiMakonde, ya Kingoni….Hapa Zanzibar Wahyao kiongozi wao Mohamed Kaujore. Yeye mwenyewe Mhyao. WaNgoni, Mfaranyaki. Wanyamwezi, hawakupewa siri. Wanyasa walikuwemo lakini Wanyasa walijiunga na Wangoni, kwa sababu hawakuwa na kiongozi wao hapa. Walikuwa na Mfaranyaki. Na jamii kuu ya kibara, baada ya Mohamed Kaujore na Mfaranyaki, hao ndio waliokwenda nao sambamba jamii ya kibara. Hao wawili hao. Ndo viungo vikubwa hivyo. Na hata katika utendaji wa mikutano ya siri, ya ndani kwa ndani, wao ndio waliokuwa wanahudhuria kwenye vikao vile, kwa niaba ya jamii zao. Sasa wanapotoka kule, wanakuja kuwatizama wafuasi wanaowajuwa, huyu anafaa kumueleza suala hili, huyu hafai. Wanaelezwa. Jamani tumekutana kwenye kikao, majadiliano tumefanya hivi hivi hivi. Sasa wale unakuwa mnongononongono kwa wale walioaminiana. Jamani, Kaujore leo na Mfaranyaki wamekutana mashimoni huko, kitu walichozungumza, suala linaendelea, hivi sasa hivi nakumbuka, mishale pamoja na mikuki inatengenezwa shamba kisirisiri. Halafu nani mchukuwaji? Mchukuwaji Yusuf Himidi, kwa sababu yeye alikuwa PWD [Public Works Department] akiendesha gari.

Viongozi wa Manamba waliokuja Zanzibar ni hao wawili, Kaujore na Mfaranyaki, lakini kiudokozi, kutokana na Victor Mkello, nakumbuka Mrangi alikuwemo, Warangi walishiriki, Wadigo walishiriki, mpaka hawa Waziguwa walishiriki. Ilikuwa si grupu, lakini ilikuwa wanachukuliwa watu kama watatu, wanne, watano, sita, kwa kila kambi, lakini wale walikuwa chini ya udhamini wa viongozi wawili hao. Hapa sio kama walikuja Wamakuwa tu, au Wahyao tu, au Wanyasa tu. Walichukuliwa makabila tafautitafauti waliokuwa wameshiriki. Fundi Tajiri yeye alikuwa mkubwa wa Wamakonde machale. Angelikuwa yuhai, yeye alikuwa ameweka ndevu. Wakimwita “Mwarab, Mwarab.” Manake ndevu zake zilikuwa nyeupeee, na halafu kutokana na ile rangi yake alikuwa mwekundu, sasa yeye ndo alokuwa kiungo cha Wamakonde. Na sehemu zake yeye alizokuwa akiwekea mikutano yake ya siri, Mfenesini. Kaujore yeye mikutano yake pamoja na Mfaranyaki, Shauri Moyo. Kutoka Shauri Moyo, Masingini, msitu wa serikali, kwamba hapa bwana kidogo pana dosari. Wakati huo Shauri Moyo ilikuwa ni pori lakini wakaona juu ya hivyo bora tuendelee tukazamie ndani huko Masingini. Watu wawili hao walikuwa wanashiriki sehemu kama hizo. Kwenda kwenda, sasa hapo ndipo walipokuja kuja kuchukuliwa akina Sefu Bakari, akina Abdalla Saidi Natepe hao, wakafikishwa mahali kama kule, jamani kinachoendelea, hiki hiki hiki hiki. Kwa kuarifiwa sasa. Kushirikishwa kwa sababu wao wako kwenye Umoja wa Vijana, ASPYL. Kwamba kama hatukuweza kuwashirikisha hawa, kidogo hapa mambo yanaweza kwenda kombo. Lakini hawa ni lazima tuwashirikishe na ushauri huu alitowa Hanga na Hasnu Makame.10 Jamani hili suala tukitaka tufanikiwe na hawa tuwaweke katika kundi hili, tuwavute kwetu, kwa sababu hawa ni Umoja wa Vijana. Hatuwezi kuwaacha mkono, Umoja wa Vijana utakuja kukuta utakuwa na nguvu.

Kina Sefu Bakari na Natepe kwanza walizibwa midomo. Wakaambiwa, bwana eh, kikao hiki hakielezwi kiongozi. Haelezwi kiongozi, alisema Kassim Hanga. Kikao hiki tunakutana sisi tu. Kiongozi anapewa top [siri] ya mwisho, lakini suala la huku linakuwa limekwisha malizika. Tunalimaliza sisi. Baada ya vikao vile vyote kumalizika, ndipo Kassim akenda kama kumdokolea Mzee Karume. Hapa pana mpango tunataka kufanya hivi. Japo aligutuka “vipi?” Sisi tunataka kufanya hivi. Jamani hili suala mtakuwa hamuwezi. Tutateketeza umma hapa. Akamwambia, hiyo si kazi yako. Sisi tunakueleza kama kukupa ushauri tu, lakini kazi hiyo sio yako. Na wewe Juni 1961 uliwahi kusema kwenye Baraza la Kutunga Sheria, kwamba vijana Tupendane walifanya fujo hapa, watu wakasema Karume anataka kupinduwa serikali. Wewe ndo ukakanusha kwamba, hakuna mu Afro-Shirazi wa kupinduwa serikali. Sasa tatizo hili sisi, hili sasa, hatukubambiki wewe.

Mkello aliwahi kufika Zanzibar. Yeye sio kuja mara kwa mara. Mimi kufahamu kwangu kaja hapa safari zake hizi mbili. Katika safari mbili hizi, Hasnu Makame ndiye aliyekuwa anakwenda naye bega kwa bega, kwenye mambo yao, kwa sababu inaonekana huyu yuko katika kazi na hapa pana chama cha wafanyakazi. Sasa inajulikana vyama va wafanyakazi ni lazima wanafanyiana ziara, kupeana utaratibu wa kikazi. Sasa kwa vile ikawa lile suala likafanya kufichika kidogo. Kurudi na kuja kwa Mkello kwa mara ya pili ndipo mpango sasa ulipokuwa umejengeka.

Hii nakumbuka ilichukuwa mwaka kabla. Alikuja Mkello kabla ya mapinduzi. Kwa sababu hili suala lilipangwa mipango muda. Nakumbuka mwaka mzima kabla ya 1963, tuseme 1962, miaka miwili kabla, alikuja akajitokeza Mkello.

Hata Hanga akawa anatoka hapa anakwenda kule, inakuwa yeye wanamuona yuko katika chama cha Afro-Shirazi, Afro-Shirazi na TANU ilikuwa ni moja. Na nnakumbuka baada ya kuja Mkello, Mwalimu alikuja akaja akafikia kwa Ali Natu, kuja, ilikuwa safari ile anakwenda zake Uingereza. Kupita, wakakutana na Mzee Karume, Thabit Kombo, na wazee wengine. Nyerere alikuwa yeye, John Rupia, na mtu mwengine nimemsahau. Nyerere akasema “hapa mpaka hivi mtapiga kura mpaka mnyonyoke mvi, mimi siwezi kukuambieni fanyeni hivi, kauli hiyo sitowi, lakini nnachosema mimi, nyinyi jisaidieni, msaada wa kichinichini mimi ntautowa.” Sasa msaada wa kichinichini alieutumia yeye kuwa address [kuwazungumza] Manamba na mkuu wao. Hiyo chamber [kikao cha siri] sasa kwa bara huko. Bwana wewe, hapa hakuna njia ya kufanya mpaka wasaidiwe Zanzibar. Kwa Wazanzibari tu peke yao hawatafanya kitu.11 Hawafanyi chochote. Kwa sababu kwa kukwambia hivo, ujuwe jamii ile imekuwa na mchanganyiko.12

Mwarabu kamuowa Mswahili, kamzaa Mwarabu. Mswahili ndie anayeshindwa kumuowa Mwarabu, lakini Waarabu wamewaowa Waswahili. Na jamii zaidi khasa ya Kimanyema imetokana huku bara, sasa utararatibu wa kufanya ni lazima wale, mara linapozungumzwa suala kama lile siri inatoka mara moja. Wamanyema wameingiliana na wamezaa na Waarabu.13

Lakufanya sasa hivi msaada utoke Tanganyika. Anaambiwa Victor Mkello kule na mwenyewe Nyerere. Mkello jawabu alilomjibu, kwa kauli ya Kassim Hanga hiyo, akasema, tumekutana na Hasnu Makame na Kassim Hanga, tumelizungumza hili suala, na hivi sasa hivi, kuendeleza kujuwa tutawapata vipi sisi hawa Manamba. Wakapewa muongozo. Hakuna njia ya kufanya, mchukuwe Wamakonde na tabaka za makabila. Isiwe mnawachaguwa Wamakonde tu. Siyo. Mnachukuwa kabila hili, hili, hili, hili. Muwachanganye. Na wanapofika Zanzibar wao muwatumbukize sehemu za mashamba. Wasilete mshtuko. Walitumia njia ya kutoroka. Wanatoroka kwenye mashamba ya mkonge. Kwenye shamba la mkonge Wahindi waliokuwemo mule, walikuwa wao wanajuwa tu “ah! Mbona fulani hayupo? Kila wakiita fulani hayupo. Kishashindwa kazi huyo. Kishatoroka huyo.” Sasa matoroshaji ya kule yalikuwa ya siri sana.

Sasa mkuu wa wafanyakazi, Mkello, ndiye aliefanya usajili wa kuwafanyia utaratibu wale watu wake aliewajuwa kwamba hawa sasa hivi walitoroka hapa, wamekwenda kule, wamefanikisha, sasa serikali ilipopatikana, Karume na Mwalimu iko fidia fulani walipewa wale.14 Walipewa wale fidia fulani, kutokana na tumekuvunjieni kazi yenu na mmekuja kutusadia. Tunakwiteni ni wakombozi mliekuja kuikombowa nchi. Lakini la kufanya, kwa kuficha hii siri, kumficha huyu…Mwalimu atakapojulikana na Waingereza kwamba kashiriki mapinduzi itakuwa makosa hiyo, ikijulikana. Sasa la kufanya wale, mkuu wa Manamba, bwana eh, wewe kwanza tunakufunika blangeti, sisi na huku tunajifunika blangeti. Hawa watu tumewatowa sisi hapa tumewapeleka kule, sasa lawama hatutaki na Waingereza, sio na Sultani. Hatutaki lawama na Mngereza.15

Na juu ya kulifunika blangeti huko lilijulikana. Kumfunika kwenyewe wale waliowachukuwa hesabu yao inaonekana kama hawa wametoroka, wameshindwa kazi. Kwa sababu unajuwa bara siku za nyuma Manamba walikuwa wanatoroka toroka sana. Na kule akitoroka mtu hafatiliwi tena. Anaetoroka hafatiliwi. Kwa sababu mimi nafsi yangu niliwahi kufanya kazi katika shamba la mkonge. Sasa nikaja nikaona hii! Hii kazi mbona ngumu. Ya mkonge. Kukata mkonge nikaona hapa bwana hapafanyiki kazi. Hii kazi itatuumiza sisi. Tukirudi kazini mikono imechanika chanika namna hii! Hii kazi ngumu hii. Tustahmili kwanza mwezi mmoja au miwili, tutapenya. Basi tuliondoka pale tukenda Dar es Salaam mafichoni. Hakuna alietufata. Manamba kwa kutoroka ni suala la kawaida. Na usajili wa Manamba wao walikuwa wanatoka wanakwenda Lindi, Mtwara huko ndo wanakwenda kuwasajili. Na sehemu nyengine tafauti. Baada ya kuwasajili na kukabidhiwa mwenyewe Muhindi, au Mgiriki, wakitoroka tena wao hawana jukumu tena. Wale wasajili wa kule hawana jukumu.

Wale matajiri wenyewe wa mashamba ya mkonge walikuwa hawalijuwi suala lile. Kwamba hawa wametoroka kwa sababu ya kwenda kupinduwa Zanzibar, hawalijuwi. Ila mkuu wa wafanyakazi analijuwa. Wale wanaotoroshwa kisirisiri kutoka Kipumbwi. Nendeni Zanzibar.

Wa kwanza nlokuwa nikimtambuwa ni huyu Mkello alokuwa akiungana na Hasnu Makame. Kwamba yeye ni fawahisha hapa. Tumemuona kwa macho yetu. Nakumbuka katika speech [khutba] yake ya mwisho alikuja kutueleza Shauri Moyo, jamani kuna ndugu zenu ntawaleta, Manamba, watakuja kukusaidieni kazi yenu, lakini muwe kitu hiki kimoja, kitu ubinafsi kiondoweni. Mkijenga ubinafsi hiki kitu hamfanikiwi. Alisema Mkello kauli hiyo. Alikuja alihutubia. Hasnu Makame yupo, Kaujore yupo, Juma Maneno yupo, Mfaranyaki yupo, Musa Maisara yupo, mpaka Kassim Hanga alikuwepo. Shauri Moyo. Likajadiliwa hilo suala kwa pamoja. Kumalizika suala lile Mkello akaondoka hakuja tena mpaka kumalizika kwa mapinduzi. Kufanyika mapinduzi alikuja kwa kifua kipana. Akaja hapa, nakumbuka alikumbatiana na Mzee Karume.

Hapa sasa ndo alipoanza kujuwa Mzee Karume. Mapinduzi yameshapinduliwa, serikali imeshaundwa, Mkello akafanya ziara ya kuja hapa Zanzibar. Alipofika, kampokea Kassim Hanga, Kassim Hanga akenda kumjuulisha na Mzee Karume, “huyu bwana kampeni zote tulizokuwa tukizifanya, Manamba katuleteya huyu hapa.” Mzee Karume aliinuka kwenye kiti akamkumbatia Mkello. Mambo hayo Ikulu. Nnakushukuru kwa msaada wako na sitokusahau maisha yangu, kwa sababu msaada ulionifanyia wewe, Kassim Hanga, Hasnu Makame, akina Mfaranyaki, nyote nnakushukuruni, lakini shukurani hiyo John Okello hakuwepo.

Wakati huo keshawekwa kwamba yeye ndo “Field Marshall” mwenyewe na anashughulika na mambo yale, lakini siri ya ndani hasa ya kujuwa kwamba huu U John Okello nimepewa, napewa vipi? John Okello hapo hapakuelewa. Yeye aliona tu kaebuka “mimi John Okello!”, anatamba.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: