Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!

Icon

Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia

Mlango wa Sita: Victor Mkello na Chama Cha Wafanyakazi

Victor Mkello wa Tanganyika Federation of Labour [Chama cha Wafanyakazi cha Tanganyika], akizungumza kwenye mkutano wa hadhara Pemba, aliushambulia ukoloni “chini ya bendera mbili—bendera ya Union Jack [ya Kiengereza] na bendera nyekundu (ya Usultani). Akaendelea kusema kuwa bendera zote mbili lazima ziondolewe…Kwa kuzingatia kuwa hakukuwa na tamko la ndani [kutoka upande wa Zanzibar] au juu ya uhusiano wa Mkello na Mawaziri wa Tanganyika, sishadidii sana ichukuliwe hatua yoyote, na nitakuwachiya wewe uamuwe kama kutapatikana faida yoyote kuifikisha taarifa hii kwa Serikali ya Tanganyika.” Barua kutoka kwa George Mooring (Balozi wa Uingereza Zanzibar) kwa F. S. Miles (Balozi wa Uingereza wa Tanganyika), tarehe 26 June 1963. CO 822/3204 116805

 

Mzee Victor Mkello

Kwa nini huku visiwani hakutulii kama tulivokusudia sisi? Inaonekana kuna maneno, maneno, maneno…Tulidhani sisi muungano huu umekubalika pande zote mbili bila ya tatizo lolote. Mimi hili suala tulitaka kujuwana wakati ule tuna msimamo wa namna gani ambao tungekubaliana nao. Mimi nikianzisha wangu nnaoujuwa na wewe wako unaoujuwa…Tulidhani kule kwenu Zanzibar juu ya vikundi vote vilokuwa mbali mbali hatimaye tutakuwa kikundi hiki “kimoja.” Bas! Tunajenga nchi yetu. Aliekufa, aliepona, bahati yetu, kazi ya Mungu. Lakini sasa tunachotaka sisi ni kitu kimoja. Asiingie mtu mwengine akasema mimi naleta Uarabu, mimi naleta…ah, ah! Hakuna. Tukae, tuzungumze, tukubaliane, kwamba sasa kama ikiwa kuna haja ya kujenga nchi yetu tukae basi tuijenge.

Palikuwa na vuruguvurugu nyingi. Kuwa kitu kimoja ingekuwa jambo rahisi na mimi nasema kilichovuruga, watu walidhani tukimtia yule Shekhe Karume atatupa uwezo zaidi wa kuongoza mambo yetu na tukafanikiwa. Lakini halafu yakatokwa manenomaneno ya akina Abdalla Kassim Hanga alienyongwa.

Maneno haya ya akina Hanga ndo yaloleta chuki. Wengine walisema Hanga ameonewa. Hata kama angekuja juu namna gani sisi kama tungesema tunasimama imara pamoja na Hanga asingeweza kutufanya kitu. Asingeweza. Sasa kikapita kipindi ikaonekana kama ni jambo la hatari kuwa naye huyu. Mojawapo ilikuwa ni kuwaogopa wasomi.

Sasa, kinachotakikana, labda, ni tutafute njia ya kuwaweka watu wetu hao katika hali ya kuelewa mambo. Kuelewa mambo katika line [mstari] hii tunayoitaka sisi, na ya line tuliokuwa nayo zamani. Jee, tukiziunganisha line zetu kutakuwa na mushkel kwa upande wetu? Labda kuna wengine hawatoridhika kama hawatopata ukubwa. Mimi nilifikiria tulipokuwa na skukuu ya miaka 43 ya mapinduzi, labda katika sikukuu hii, yatatobolewa mambo mengi, yakatupwa nje yasiotufaa, yanayotufaa tukawa tunayo.

Niliona dalili kwamba watu waliokuwa waogawaoga hivi…wakati wa kunyongana watu walinyongana. Sasa mambo yamekwisha. Ilobaki sasa ni kama unavosema, tusameh mambo yote na tutafute tusimame juu ya nini. Hili ni jambo la watu wote sasa. Dunia inavosema jambo kubwa kama hivi halitokufa tu hata kama tunataka sisi life.1 Litakwenda linachomokachomoka tu. Mwisho watu watakuja tambua mambo yalivyokwenda lakini hii Zanzibar mpaka hivi leo hawa waliokuwa wakubwa wenzetu pia hawajakubaliana kwamba uongozi wao ulikuwa ni thabiti kabisa.

Bado kuna wasiwasi. Hawa viongozi wa Zanzibar, ikiwa nia zao haziko pamoja na sisi [viongozi wa Tanganyika] na kama hatuwezi kuziunganisha tukawa sote pahali pamoja wanachotaka ni nini?

Manamba Zanzibar walikuwepo. Kuna mambo mengi tuliyafanya kwa kutumia Manamba. Kwenye Zanzibar. Watu walikuwa wanakutana bwana lakini kuna wengine hawataki lijulikane hilo kuwa fulani na fulani aliwaongoza.

Sasa hapo ndipo vurugu hiyo. Sasa hapo panakuja ukubwa na uongozi. Hapo panakuja ukubwa sasa na uongozi.2 Basi akitajika Mkello, ni mtu mkubwa huyu, lazma apate heshma huyu kwa sababu ameshiriki. Sasa kama hatukumtaja Mkello, hatukumtaja mtu mwengine, akina Kassim Hanga, tutaonekana hatuko pamoja.

Tukikataa tunanusurisha mgawanyiko. Tukikataa tunanusurisha mgawanyiko. Tukisema tuunganike pamoja wote itakuwa ni kitu kizuri kwa upande mmoja, lakini kuna watu wengine kwa ukubwa hasa hawa vijana wetu wa Unguja walopata Uraisi. Sasa watu wa namna hiyo wanataka mambo yao yaende katika msingi huo.

Ujulikane kama huo ndo msingi uliofanya mambo yote hayo. Ambapo kuna upande huu unaosema wewe hawataki, wanasema Manamba “si kweli.” Hawa walioko sasa wanataka wajulikane kwamba wao ndo wao! Wao ndio wao na ndo waliokuwa wakiyafanya baba zao. Sasa panapotakiwa kutobolewa ile siri kama haikuwa hivo. Mlikuwemo lakini sio katika uongozi mkubwa kiasi hivo. Hawajakuwepo katika shina.

Inategemea kule kutoboa kwenyewe kutatobelewa katika picha gani.3 Kuna wanaosema hamna faida yoyote. Sisi tulichotaka ni Mwarabu aondoke na ameshaondoka. Tunatakia nini kuingia mambo haya hayana faida yoyote. Tunataka kujenga nchi. Bas! Wengine wanasema, hapana, lazma tujenge nchi kwa kupenyeza uongozi mkubwa kwa watu flani flani.

Wakati huo Mwalimu Nyerere akijuwa na mengine akiyasogezasogeza yeye. Kwa mfano niliwahi kutumwa kwenda Moshi usiku wa manane. Nakwenda Moshi kwenda kupanga mipango hayohayo ya mapinduzi. Kushika chaji ya mambo yetu haya ya Zanzibar kuogopa kwamba kama tukichelewa watu wa Zanzibar…manake Zanzibar yenyewe nayo imekuwa headache [inaumisha kichwa]. Watu wawili Zanzibar. Kuna Waarabu na wasiokuwa Waarabu. Sasa kuna watu ambao wanataka, hawatakiwi wajitokeze katika unasaba wao na Uarabu. Hawatakiwi wajitokeze kwa ajili ya Uarabu wao. Hapana, hawa si watu wa upande wetu. Sasa tuwachujeje hawa mpaka wawe hawako upande wetu. Kazi kubwa! Maana watu tunao lakini hawa hawapendwi na kundi lingine. Kwa hiyo kazi hii ni kubwa sana.4

Moshi nilitumwa na Nyerere kwenda kuweka mambo sawa. Wakati huo Katibu Mkuu alikuwa ni Kambona na alikuwa katika kazi maalumu huko Moshi na ilikuwa lazma apatikane basi ikaonekana utoke ujumbe makao makuu umfate ndo nikachaguliwa mimi. Nyerere akilifahamu kwa sababu watu fulani akiwatuma katika jambo flani itakuwa hivi, itakua hivi, itakua hivi. Tena saa nane ya usiku natafutwa na magari ya polisi. Uingie ndani ya gari hii. Barua hii mpelekee Oscar. Nakwenda…nafika Morogoro nakutana na Kawawa naye ana kalendrova chake kadogo. Naye pia ametimuliwa. Sasa haya yote ulikuwa bado ujenzi, utafutaji wa kipi kinatafutwa. Wakati ule tulikuwa na wasiwasi. Tulitaka nchi yetu ya Zanzibar tuigomboe.5 Vilizuka vyama kule na walipozusha vyama hawakuzusha kwa amani na mapenzi. Wasiwasi wako mkubwa ni kwa nini jambo hili halishi. Hapo katikati hapo pakatoka vikundi venye kurusha maneno maneno hivi na kutupeleka mbali.

Makabila yote yalikwenda Zanzibar kushiriki katika mapinduzi. Wamakonde, Wabena, Warundi, Wanyamanga, wakina nani…Mahali mambo yakitaka kuharibika! Yanaharibika tu. Wote walikwenda. Sasa wao wanakataa tu huo ushahidi. Lakini watu wengi wamekuja. Wote ni woga tu. Unajuwa tulianza vibaya, kugongana kule, watu kuuwana kule. Sasa hao wenye kusema kuwa Manamba hawakwenda Zanzibar kwa kushiriki katika mapinduzi na watueleze ilikuwaje. Wakati wa Abedi Karume akina Kassim Hanga hao, ukizungusha nyuma hivi, bas, hurudi salama. Sasa kitu gani kinachoharibika hapa, kinachovurugika…ni kutaka Uarabu mbali, sijui unani sijui mbali. Ni nini kinachotuogopesha tusiungane pamoja tukafikia kwenye point unayoitaka weye?

Machano na Makame [Wazanzibari wenyeji] hawajakuwemo kwenye mapinduzi ya Zanzibar. Neno lenyewe hilo unalolisema si la uongo kwa sababu ya uhusiano wa kindowa, basi kabla ya hayo yakatokea mauwaji yale, sasa hapo wameingia woga. Wameowana hawa.6

Kielimu mimi sikwenda mbali. Sikwenda mbali. Tumesoma haya madarasa ya shule haya, shule za Anglican. Top kabisa wakati huo Anglican ilikuwa Kiwanda na Minaki. Hizo ndo shule ambazo mimi nilipata bahati ya kutafuta mitihani yao na nikakubalika. Baada ya shule ya Kiwanda kuvunjika ikapelekwa moja kwa moja yote Minaki. Kiwanda ilikuwepo hapo Muheza. Kutoka Muheza ikapelekwa Minaki. Baada ya hapo sasa ikasemwa watapunguzwa watu kwenda kusoma Minaki ambayo iko juu zaidi. Tukakubali. Sisi wengine tukasema turudi kwenye mkonge. Si kazi tunayo! Kwa hivyo hatukuendelea na masomo. Kurudi nyuma kwetu sisi ndo ikatokea uingiaji wa vyama va wafanyakazi. Hivi vyama va wafanyakazi, sisi Watanzania tulivipata kutoka Kenya kwa Tom Mboya. Tom Mboya yeye ndo alokuwa mwenzetu, halafu katika nafasi zao akapewa amri au order ya kuunganisha East Africa [Afrika Mashariki] kama ataweza kuipata katika vyama. Sasa katika kufanya hivyo ikaonekana kwamba tuanze kazi. Tukapatikana pale na baada ya kupatikana sisi pale tukafanya uchaguzi, baada ya kufanya uchaguzi na nini, mimi nikawa kiongozi mkubwa wa Tanganyika Federation of Labor (TFL). Kwanza walianza huyu Kawawa,7 Kamaliza, halafu mimi Mkello, katika huuhuu upresident wa TFL. Baada ya hapo tulizuwia, ngoma ilichezeka sasa hapo. Mimi sikulaza usingizi, bibi huyu hapa hakulala usingizi, kwa sababu sasa ni vita. Wazungu wa mkonge wamesimama imara kupinga movement [harakati] yetu ya haki za wafanyakazi na walinikuta mimi kama nilikozaliwa kwenye kupingana! (vicheko). Wamesikitika sana, na walijaribu hata kumuomba Mwalimu kama huyu kwa nini ukampa nafasi ile, Mwalimu [Nyerere] akawaambia “huyu si mtu wetu, huyu ni mtu wa labor [wafanyakazi] huyu. Mkimgonga huyo kesho watu wote asubuhi hakuna kazi.” Wakawa wananitizama kwa jicho baya lakini hawana la kufanya.

Basi sasa baada ya kuwa wameshindwa kunifanya lolote sasa wakatumia ujanja mmoja. Wakamtumia huyuhuyu Mwalimu, basi wakamtumia kumuambia, huyu matata huyu bwana, kidogo migomo, kidogo migomo, kama unaweza kumbanabana hivi. “Kumbana naweza kwa sababu ya u-President wa serikali naweza kumbana kwani kama sikuweza kumbana hii nchi si itaharibika? Sasa ngoja nitafute nafasi ya kumbana huyu ili isiwe mnagombana naye, ili naye akubali kama kuna mambo mengine si lazima sana maana yake hii nchi bado ni changa.” Basi, ikawa sisi tumekubali hilo na mimi wakanihishimu na security wao [watu wao wa usalama] wakajuwa habari zile Mzee amekubali kunibana na wao wakapata nguvu. Sasa kazi ikawaka moto ikawa na wao sasa wakashindwa kunitupa kando ikawa kila kitu kinachotokea katika mkonge nikawa mimi nilihusika. Mwalimu ana washauri privately [pembeni], na wakimuambia kuwa huyo alipokuwa shule alikuwa mkorofi. Kwa hakika hapo mtakuwa mmemvisha kofia ambayo alokuwa anaitaka yeye.

Basi, mimi nimekaa hapa na jamaa wa mkonge moja kwa moja, tuko pamoja. Na Central Sisal Council, hiki ni section [sehemu] ya cha chama cha mkonge, lakini kilikuwa na uzito wake kwa sababu chairman [mwenyekiti] wake alikuwa anatoka London! Eeeh! Mwenyekiti wetu alikuwa Mzee Fek yeye alikuwa ni interpreter [mtarjumani] na mimi chairman wa TFL. Basi mzee akija, ananipigia simu kutoka London kupanga tarehe ya kukutana. Huko Uiengereza yeye alikuwa ni ex-judge [kadhi aliyestaafu] na kwenye mkonge alikuwa ni chairman kabisa. Akaambiwa huyu mtu [Mkello] tunayekupa kidogo hana adabu lakini tunakuomba ujaribu u-create friendship [ujenge urafiki] naye. Usimuone hivyo huyo, akikasirika hata mbele za watu atakutukana huyo! Mzee akaona mmhhh! Nitapata kazi kubwa. Basi mzee yule ikawa hatwendi mbali. Kidogo ikawa “Mzee yule anakwita.” Mtu mzima, amenishinda mie. Basi, tukawa tumeshughulika wote pamoja na ikaleak [ikavuja] kuwa amepata warning [onyo] ya kuniheshimu. Basi hatukuhitalifiana sana isipokuwa mkonge wenyewe mambo yao kidunia yakawa si mazuri kwenye biashara ya mkonge.

Basi mimi nilikwenda nao hawa jamaa mpaka hapa katikati hapa ikatokea nikosane na President [Nyerere]. Sasa hapa ule mwiko unavunjika sasa. Nikakosana na President na nikapelekwa Sumbawanga. Lakini kule sikukaa sana. Tulikaa miezi mitatu pamoja na assistant [msaidizi] wangu [Shehe Amiri ambaye alikuwa Seketeri wa Oganizesheni wa Tanganyika Workers Union]. Ni kifungo ambacho ni cha ajabu manake, mimi sijapata kukiona. Tuko Sumbawanga, bwana mkubwa wetu wa Sumbawanga, afisa mkubwa yule wa kazi anaeshughulika na sisi, kila siku ya jumatatu tunapita kwake anatupa pesa, shilingi miamoja, mia moja. Kila jumaatatu. “Jamani ndo sheria!” Detention [kizuizini] unalipwa! Zingelinifika mpaka hii leo ingelikuwa ni vizuri. Mama Mkello atakuwa hana taabu ya mafuta ya taa tena.

Basi bwana, mambo yakenda tukarudi baada ya miezi mitatu. Mwalimu nae tukagombana tena. Nilikuwa na Regional Commissioner [Mkuu wa Mkoa] kule Sumbawanga na akanambia wewe kaa hapo nitazungumza na mzee kuhusu habari zako. Kaa hapo usikilize. Commissioner akanambia “unataka mke wako aje hapa?” Nikamwambia “ndio nataka mke wangu aje hapa kwa ndege, manake mimi nimekuja hapa kwa ndege.” Lo! Kumbe hilo limemuudhi Mwalimu. Kwa nini nimesema nimeletwa hapa kwa ndege na mke wangu aletwe kwa ndege. Baada ya Sumbawanga kikaja kifungo cha miaka miwili na nusu. Tulifungwa huko Kilwa Kivinje. Mapinduzi Zanzibar yameshatokea.

Sasa hapo tulikuja kusikilizana kwa masuali ya Zanzibar kwa sababu vijana ilionekana wana interest [hamu] sasa kwa Zanzibar hawa kuingia katika movement [harakati] yetu ya labor [chama cha wafanyakazi]. Wameona ina nguvu na ikitoa sauti inasikilizwa nchi nzima. Kama akina Adam Mwakanjuki hawa mara wakawa wenzetu, wanatuonea huruma na nini. Tukawa tuna solidarity [mshikamano]. Safari moja nilisafiri na mama Mkello hapa, kwa air [kwa ndege] lakini, nilipewa ndege na Raisi tukaruka hapa mpaka Zanzibar halafu tukenda Dar es Salaam. Hakunisahau Mwalimu. Baada ya kifungo cha Kilwa alinita ofisini kwake anipe kazi. Kwanza, alikuja Tanga kwenye ziara yake ya kawaida ya Mkoa wa Tanga na wakati ule Area Commissioner [Mkuu wa Wilaya] alikuwa Rajabu Kundya. Basi akamwambia Rajabu Kundya anitafute, nilikuwa nalima shamba baada ya kurudi Kilwa. Rajabu akanitumia salamu naitwa na Mzee. Nikashtuka. Mwalimu ni rafiki yangu lakini tulikaliana kiujanjaujanja. Nikasema nishavuruga nini tena?

Nikaonana na Mwalimu. Akanambia kwanza, mimi nafikiri mambo yamekwisha, “serikali ni serikali bwana, inawezekana tumekosea, au inawezekana imekwenda vizuri, lakini tumetekeleza kama tulivoelewa sisi. Sasa wewe huwezi kukaa hivihivi tuu, hapana. Sasa nitakupa kazi ambayo msimamizi wake nitakuwa mimi mwenyewe kwa sababu watu wengi ni maadui zako, sasa itabidi nikulinde. Sitaki watu wanatungatunga habari zao wananiletea mie. Akiniletea mtu habari na mimi nitakwita hapahapa. Watajuwa mmh…!” Nikamwambia mimi nakushukuru. Ilikuwa anipeleke Moshi kuwa Katibu wa chama wa Mkoa wa Moshi, halafu Kawawa akabadilisha, akaweka Dodoma. Kutoka Dodoma nikapata transfer [uhamisho] nikapelekwa Morogoro, lakini habari zangu zinajulikana wazi kabisa kwamba mbele ya Victor Mkello huwezi kuleta mchezo.

Kutoka Morogoro akanipa u Area Commissioner [Ukuu wa Wilaya] akanipeleka Njombe. Nikamwambia “sawa, lakini ninachokuomba mimi ni binaadamu, ukiniona nateterekatetereka unite unieleze, sio kuntumia asikari.” Basi akafurahi, akacheka kabisa! Akasema, “unaogopa askari eh?” Nikamwambia “askari si mchezo bwana, wale ukishawaambia neno basi.” Baada ya hapo nikahamishwa tena nikapelekwa Mkoa wa Tabora. U-Area Commissioner huohuo. Halafu nikapelekwa Area Commsioner Same, halafu Wilaya ya Bagamoyo ndipo nilipomalizia u-Area Commissioner wangu nikarudi Muheza nikawa Mwenyekiti wa Wilaya wa CCM. Ndo mwisho wangu na sasa niko kitandani. Ndo mwisho wangu wa u-Area Commissioner wangu huo. Lakini hakunisahau Mwalimu. Hakunisahau hata kidogo. Hakunisahau hata kidogo. Huo ndo mukhtasari wa elimu yangu na majukumu niliopewa. Wengi hapa wananifata kuniuliza kuhusu mashamba ya mkonge na Manamba waliingia kipivi, si kama ni wewe peke yako.

Suala la Mapinduzi ya Zanzibar hilo hawakulitaja. Hilo hawalijui na ni tafauti ya hayo mengine. Jambo la labor movement [harakati za wafanyakazi] ni kitu ambacho kilianza kwa undani sana. Ya Zanzibar na hata hii ya huku. Yaani, hawakuwa na uhusiano mzuri wa kushirikiana katika mambo…wenzetu Zanzibar kidogo walikuwa wakijitengatenga kwenye mambo ya labor movement. Wakijitengatenga. Hakujakuwa na mawasiliano mazuri.

Labor [chama cha wafanyakazi] ya Afro-Shirazi tulikuwa tumeshirikiana sana. Hata Nyerere mwenyewe alikuwa anapenda hiyo kuona kwamba sisi vijana tunashikana kuleta ile labor movement yetu na kusiwe na mtu wa kutuingilia. Manake walikwishaona vinenovineno va kutaka wenzetu hawa wa Kenya, hawa wa Zanzibar. Akasema hapana.

Nilitiwa kwenye suala hilo mara tu baada ya kutoka Pemba…hapana…wapi hapa?…tuliporudi mara ya pili…Kilwa…tukapata habari kwamba….tuliporudi kutoka Sumbawanga palitokea mgogoro ambao haukuwa na sababu yoyote ya maana sana ilionekana kana kwamba ni mgogoro wa kugawana, kwamba wenzetu wa Zanzibar na sie tuweke mambo yetu kando…hakuna atakayefuatilia la mwenzie katika mambo ya labor kwa sababu ile ni nchi kamili.8 Basi yalikwenda hivo. Vineno vidogovidogo, kina Adam Mwakanjuki hawa…tulikwenda nao vizuri. Mambo sasa yalikuja haribika lakini hivi vinenovineno vilipoungwa mkono na vyama va siasa hivi…jambo hili baya, jambo hili zuri, basi kidogo….

Sisi tulikuwa tukiitwa katika mambo mengi…Watu wetu, wao wenzetu walikuwa na nia hiyo ya kutaka kuungana. Sisi tuwe kitu kimoja lakini sasa kule kwetu, sio sisi sasa, kule Zanzibar huko, kule jamaa wakaanza kama kuwa na wasiwasi kwamba tunataka kunyang’anywa madaraka.

Tunataka kunyanganywa madaraka manake Tanganyika…tena hivi hivi hivi…Oh, sasa hapa kidogo ikawa ule urafiki wetu uliingia maji. Kumbe hawa wanaletwa wanakuja…wanataka kuwa wakubwa nao ndani ya nchi yetu.9 Lakini halikuwa jambo baya saana. Ah, ah. Ilikuwa maneno ya uvumi wa watu tu lakini hatukuwa na kitu ambacho kinashamiri kabisa kama kuna vita. Aa. Isipokuwa kuna arguments [mabishano]. Tukikutana katika vikao tu, imekuwaje tena akina Mkello kutuingilia…yalikuwa maneno kama hayo. Wenzetu wa Zanzibar walikuwa wakilalamika. Kulikuwa na vikundi va watu lakini havikutueffect [havikutuathiri] sisi na shughuli zetu. Hakukuwa na kitu cha kubishana mpaka ikawafanya watu…hakuna. Maneno maneno yalikuwepo.

Mchango wa mashirikiano baina yetu na wenzetu kule, huyo Kassim Hanga tulikuwa naye, na huyu kijana mwengine wa Songea…Hassan Nassor Moyo, tulikuwa naye, na mwengine, Mustafa Songambele kutoka Songea. Hawa ni wenzetu ambao kama kuna jambo kuweza kuleta umoja, tulizungumze kwa umoja basi mara moja tunakubaliana, kuitana na kuzungumza.

Mapinduzi [ya Zanzibar] yana chombo chake na chombo chake ni vyama va wafanyakazi. Mada ni nzito na uzito wenyewe ni vitu viwili vimekuja kama pamoja—serikali na vyama va wafanyakazi—labor. Sasa, mambo tulifunzana, kama mambo ya serikali tuiwachie serikali, yana sheria zake na nini na nini. Kama kuna mambo ya raia ya kiserikali kama yanataka yazungumzwe kwenye labor basi tuwe na vikao vingine.10 Tusichanganye mambo. Tutakuja zungumza vitu ambavyo havimo kwenye mandate [mamlaka] yetu.

Suala kama kuna watu walidokolewa mle kutoka kila shamba la mkonge kupelekwa Zanzibar kwa ajili ya mapinduzi mimi sidhani kama hili suala lilikuwa la wazi. Halikuwa suala la wazi. Hawajalijuwa. Hawajalijuwa kabisaa, kama watu wetu wanadokolewa. Katika kuwaorganize [kuwaandaa] wale watu sisi hatukushauriwa. Walishauriana wale watu na Mameneja. Kama wangelijuwa wao wasingelithubutu bila ya mimi. Lakini kuna wazungu wengine wana hamu, wakina David Leed, huyu wa hapa Mazimbe hapa. Mtoto yule kigego yule. Hashikiki kabisa.

Yeye anaweza kufahamu manake ni mpekepeke sana au anaweza kufanya kitokee kitu fulani. Kama hakikufanywa akishtukia tu kimefanywa au yeye anaweza kukipekenyuapekenyua. “Basi huyu Bwana Mkello anafanya hivi anafanya hivi.” Ndo kazi kubwa alokuwa anafanya yeye.

Ugumu wa Mwalimu, kuna mambo yanapoingia kwa Mwalimu, na yeye anakubali kuyatoa nje kwenye vikao vake vile. Anayazungumza. Lakini kuna mengine yakimwendea basi anachukuwa kitu kama kutokuwa na hamu ya kutowa kitu hiki, hiki, hiki, labda kijulikane na kina Mkello kitaweza kuleta maneno. Maneno hayo tumeyapata. Kama kuna mambo mengine Mwalimu amekuwa na wasiwasi kwamba tukiambiwa sisi tunaweza kuyatowa.

Mie nasema watu tulokuwa tukifuatana nao ni hao niliokutajia, Hanga, Adam Mwakanjuki. Moyo na mimi tukinongona sana. Mwalimu [Nyerere] alikuwa hapendelei sisi tuwe vianzo va matatizo ya Zanzibar.11 Khasa kama kuna jambo tunakaa kwenye ofisi yake anazungumza, “jamani, tumesikia nani hapa, kuna hivi, kuna hivi.” Sasa hapo kila mtu anajitetea lakini hilo mimi silikumbuki sana. Nataka ijulikane kama hatukuwahi kukaa na Mwalimu kuzungumza suala hilo la mapinduzi ya Zanzibar.

Kawawa tulionana Morogoro. Mimi nakwenda Dar es Salaam narudi, yeye anakwenda Moshi. Huko Moshi kuna Kambona huko. Mwalimu [Nyerere] ndo alokuwa akitoa miongozo (sauti ya chini). Mwalimu alikuwa muongozo wake mkubwa hataki itokee fujo ionekane kwamba hawa Wazungu walitaka ku create [kujenga] kama Tanganyika Federation of Labor, ndio wanaovuruga hii nchi. Mwalimu hakutaka mtu abuni maneno yasiokuwa na msingi halafu afanye labor movement [harakati za wafanyakazi] kuwa inahusika. Mimi nakataa kwa sababu mikutano yote nilioitisha mimi na wenzangu hamna tabu. Kama kuna kitu chengine chairman si lazima awepo pale all the time [kila wakati]. Chairman wa chama cha wafanyakazi anakuwa na majukumu mengi lakini nikirudi lazma niambiwe.

Mimi sikuhusika na ukusanyaji wa watu kwenda kufanya mapinduzi Zanzibar, lakini mimi nimehusika na mikutano yote ya wafanyakazi, karibu yote nimehudhuria mimi. Sasa ufahamu kama ni Zanzibar, mimi sikuwa kiongozi wa Zanzibar. Kama wenzangu wa Zanzibar wameitisha mikutano yao wakafanya bila ya mimi kuwepo hawawezi kunitaja kwamba na Mkello alikuwepo.

Manake vitu vengine mimi sikuwepo. Kama ni jambo hilo la Mkello, na Nyerere, na Kawawa, na kina Hanga, si mambo mageni hayo, wala si mambo yanayofichwa na mtu yoyote yule. Tunapokosana ni pale “Mkello ulikuwepo.” Mimi vema, mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyakazi, pengine mkutano unaitwa mimi siko Tanga, lakini nasikia kuna mkutano huko. “Haya fanyeni.” Hata Nyerere mwenyewe, vikao vengine alikuwa hayupo tunakaa na Kawawa.

Mimi ninavyokumbuka siku ya mapinduzi, wenzangu wa Zanzibar, au tuseme wenzetu, tunavosema sisi wengi kutoka Tanga, wenzetu wa Zanzibar kutoka Tanga kwenda kwenye hiyo siku kuu ya mapinduzi, hakuna anaweza kukataa, na wengi wanaweza kuona kama ni fahari. Lakini mimi kama nilikuweko wakati huo…

Unajuwa kama kuna siri moja inayotokana na suala lile la mapinduzi kwamba yasingetangazwa na mtu mwengine yoyote kwa sababu ni vitu va hatari. Hatukutaka vijulikane kabla. Iwe siri ya hali ya juu. Nilikuwepo Tanga. Kama hunioni Zanzibar niko Tanga. Watu Tanga walikuwa wanayasubiri. Hiyo, tena…nyinyi mnafanya mchezo. Tanga tulikuwa tunayasubiri kwamba leo ni mapinduzi. Leo tunapinduwa leo. Lakini mpaka nimekwambia hivo nimekutizama mara mbili mara tatu uso wako kama wewe ni mtu wa sawasawa au…Siku ile ya mapinduzi hakuna mtu alielala Tanga katika sisi. Hakunaaa! Sisi tuko huku tunawaunga wenzetu walioko Zanzibar kwenye muungano [mapinduzi ya kuiunganisha Zanzibar na Tanganyika]. Sisi tulikuwa tunataka Mwarabu aondoke. Hanga alikuwa anakuja Tanga lakini hakuwa na uhusiano wa karibu na mimi. Hanga alikuwa anakuja Tanga, alikuwa anakuja kwenye vikao va Tanga, lakini alikuwa haji kuniona mimi.

Mimi sikuwa na urafiki na mtu yoyote ambaye ni zaidi ya Adam Mwakanjuki. Huyu manake tunaelewana. Kiuongozi alikuwa mdogo lakini unajuwa katika mikutano watu wadogo huwa ndo wakubwa kwa sababu huwa wanaandika andika minutes [mukhtasari wa maneno yaliozungumzwa kwenye mkutano] kumpelekea huyu na yeye mlemle kimsimamo anakuwa anatia hivihivi. Hapa tulipo tunaozungumza wewe na mimi. Tunaisemaje Zanzibar? Iwe tumeshinda katika nia yetu ya kujenga Zanzibar mpya au hatukushinda? Hakuna kwamba tumefaulu Mwarabu hayupo na nini, na nini? Mbona yeye Mwarabu hakubali kuiacha Zanzibar? Na haitaki vipi na yeye ameshindwa?

Zanzibar sio nchi ya mwanzo duniani kupinduliwa. Nchi nyingi zimepinduliwa lakini nyingi zimeokoka vilevile. Zanzibar wasingeweza kupinduwa bila ya msaada wetu. Sasa hawa wanaolalamika Zanzibar kuhusu mapinduzi ni akina nani basi kumbe mambo yamekwenda vizuri namna hiyo na Mwarabu kaondoka?

Mtu ambaye anaweza kujulikana kama ni Victor Mkello ni huyu John Okello.

Mimi nakumbuka waliokuwepo pamoja na akina Mkello, ni mimi mwenyewe, na wengine nimeshakutajia. Na mimi nilikuwemo katika huo muungano wa tarehe 12 January 1964. Muungano [mapinduzi ya kuiunganisha Zanzibar na Tanganyika] waingia sisi tuko hapa Tanga tumeusubiri. Sisi tulikuwa tunasubiri katika ofisi yetu ya TANU. Tulikuwa watu wengi ambao tuna kazi mbalimbali.

 

Mzee Maulidi Sheni alikuwa kati ya viongozi wa Chama cha Wafanyakazi Tanganyika na msaidizi wa Mzee Victor Mkello

                                                              

Mzee Maulidi Sheni

Alikuwepo bwana mmoja alikuwa akiitwa Abdalla Mwinyi alikuwa ana chongo jicho lake moja. Yeye alikuwa ni kiungo baina ya TANU huku bara na Afro-Shirazi, Zanzibar. Kuna kitu kinakuja kutoka Dar es Salaam analeta mtu mpaka Mkwaja, kutoka Mkwaja mpaka Muwanda. Abdalla Mwinyi alikuwepo Dar es Salaam. Mimi nilikuwepo Tanga. Nikenda Zanzibar nikikaa siku moja mbili, nakula vitu pale halafu huyo nakwenda zangu. Najuwa mpango wote wa pale. Tulikuwa na kina Moyo, kina Mwakanjuki hawa, kina Khamis Masudi, kina Ahmed Diria, Shaabani Mloo, Twala. Juni 1961 tukijuwa kila kitu. Nikalipeleka gari la Land Rover Zanzibar likasaidiye. Itakuwa haina maana wafanyakazi wasiwasaidiye wafanyakazi wenzao walioko Zanzibar.

Watu tulikuwa tukiwapeleka sisi Waunguja. Tukiwachukuwa watu kimyakimya. Kama Tanga tuliiba. Wasambaa hawa, wadude gani. Bado wiki moja. Wiki moja kabla. Kwanza tulikuwa na yule kijana, “Jimmy Ringo”, Maulidi Juma. Aliuwawa yule. Yule alikuja mapema Tanga, alikimbia kukamatwa kule Unguja.

Siku ile ya mapinduzi niko Unguja. Nalikuja siku ile. Nikaambiwa mimi kazi yangu ku-patrol, kupiga doria. Kila mti unaoujuwa wewe uliokuwa pale Kiinua Miguu ulikuwa una watu. Mimi nilikuwa nikizunguka kwa baiskeli lakini. Unapita chini ya mti unasimama mtu anakutokelea. Nimetaka kujuwa tu kama upo. Sote tuko hapa. Nimezunguka nimezunguka mpaka juu kule Mwembe Matarumbeta.

Nyerere akamwambia Karume kuwa asikubali Hanga awe Waziri Mkuu na yeye asiwe na kitu. Lazima serikali ukaivunje, wewe uwe Rais na Hanga awe Makamo wa Rais. Kwa siku tatu serikali ilikuwa chini ya Hanga. Nyerere ana hadhar. Hakuitowa serikali kumpa mtu ovyoovyo. Alikuwa tayari akupe ukubwa wa majeshi lakini Nyerere alikuwa mgumu sana wa Ikulu. Ulipoundwa Muungano Hanga akaletwa huku [Tanganyika].

Mkello na Shehe Amiri walipopelekwa kizuwizini mimi tu nalibaki nje nikawa mimi naliongoza jahazi. Watu tuliowapeleka Zanzibar kwa ajili ya mapinduzi wengi walitoka Tanga na Dar es Salaam. Wengi. Watu wa Unguja walitutaka tuwapelekee watu wende wakapige kura kwa sababu baadhi ya majimbo yao yalikuwa na upungufu wa watu. Hao walikuwa kwa ajili ya kupiga kura kwenye uchaguzi. Hatukuwapeleka wote kwa pamoja. Tuliwapeleka kidogokidogo. Mohammed Mkwawa na Haruna ndiwo waliokuwa wakiwapeleka watu Unguja kutoka Tanga. Haruna kaka yake Abasi. Haruna amefariki.

Chama cha Wafanyakazi kilinipa magari kutumia kupeleka watu Kipumbwi, Mshongwe na Mkwaja. Na chakula cha kuwapa wale watu wenye kupiga kura.

Mkello alikuwa kucheza wazi hawezi. Alikuwa akinikubalia tu yangu. Ile active participation ilikuwa yangu mimi peke yangu. Si Muunguja! Waunguja wengine walikuwa pwani. Wengi walikuwa pwani. Wengi! Ndo kina Abasi hao, kina Haruna. Mtu na ndugu yake, baba mmoja mama mmoja. Wakifanya kazi Tanga.

Kutoka Unguja kuja Tanga, alikuja Natepe, alikuja kutaka Jimmy Ringo arudi Unguja. Natepe alikuja Tanga wiki mbili kabla ya mapinduzi. Akatwambia kuna shida ya mapanga na watu. Tukamwambia atakuja nao Jimmy Ringo. Ndo tukatia watu kupitia Kipumbwi watu ishirini na tano na mapanga mia mbili. Tukapeleka. Wakapelekwa wakatupwa Mkokotoni. Siku tatu kabla ya mapinduzi, mimi Abasi na Mohamed Mkwawa tukenda. Tukashukia Bumbwini. Wale kina Abasi kwao Bumbwini tukaja zetu mpaka mjini. Hatujuwani kila mmoja ana kwake. Mkutano Kijangwani.

Mimi nilijishirikisha mwenyewe huku bara. Nafanya mambo yangu, napeleka. Suala hili limegubikwa kwa sababu Serikali haitaki kujijuulisha na walikuja waandishi wengine wakaandikaandika maneno yao…Watu wengi wameandika ati na baadhi ya mambo yameoneka lakini yameonekana mengine ni uwongo. Mengi uwongo, maana yake sivo yalivokuwa. Kwanza wengi waliokuwa wakiulizwa sio wenye kuhusika! Unakwenda kumuuliza mtu wa Dar es Salaam katoka bara kaja hapa Dar es Salaam kwa kazi tu, kaletwa kwa kazi, unamuuliza mambo ya mapinduzi atajuwa? Yale sharti umpate mtu wa Unguja anacheza kati ya Unguja na huku. Yule ndo anajuwa.

Wanasema Wazanzibari upole wao hawawezi kufanya vitu kama vile [va mapinduzi], sasa hawa lazima watu wamekuwa imported from mainland, [wameletwa kutoka bara]. Maana yake hapakuwa na mtu aliyeletwa kutoka mainland isipokuwa wale watu kama mia mbili, mia tatu, sisi Tanga tumeleta kama mia mbili, hapa Dar es Salaam wameleta kama mia tatu, ambao wengi wao ni Waunguja wenyewe waliokuwemo humu wakifanya kazi. Na Waunguja wote waliokubali kwenda kufanya kazi ile ni wale waliokuwa pwani [bandarini], makuli. Wewe utamchukuwa Muunguja aliyokuwa ofisini karani ende akapigane? Atakubali?

Nyerere akijuwa na hata Mgereza alikuwa anajuwa na angetaka kuzuwia angezuwia. Mgereza aliiunga mkono ile na angetaka kuzuwia angezuwia. Babu alikuwemo kweli katika mipango lakini zile siri za ndani kabisa hakuwemo. Kuna mipango ile ya kwamba leo tutafanya, tena na kuna watu walijuwa toka mwanzo, na kuna watu walikuja kujuwa dakika ya mwisho. Tunapigana siku fulani. Makomred walijua, walijua hapa baadae tena kama sasa watu wanaeka na wanatafuta siku ya kupigana, sasa tutafuteni silaha na silaha kutafuta kazi. Kama Algeria ilileta silaha basi hiyo ilikuwa siri kali sana! Ambayo hata mimi sikuijua, ilikuwa siri kali sana hiyo.

Baada ya Mapinduzi tu mimi niliingia serikalini, nikakaa serikalini [Ikulu] pale Unguja. Hapana hata mmoja katika sisi tulotoka Tanga hasa aliyepata kazi nzuri. Labda mimi. Wengine hawakupata chochote…Baada ya mapinduzi kwisha ikabakia kazi ya kukamatana wenyewe kwa wenyewe. Nani alikuwa nini. Tukawa tunawaendea watu.

Majeshi yakagawanyika mapande mawili. Kuna jeshi likawa la kwenda kwa wanawake, kuwalala wanawake wa maadui zetu, kuna jeshi likawa linakwenda kwiba, mali zote unozojiuwa wewe za matajiri wa Unguja zilichukuliwa, na kuwakamata wale maadui zetu wale, kuwakamata na kuwapeleka vituoni. Mtu anaambiwa, “lala chini, lala!” Mama wa Kihindi anasema “baba, hii bado toto dogo, hii haiwezi baba, kuja hapa.” Mambo yalipotulia walihama wote wakaja zao Dar es Salaam. Wale wanawake walokuwa wakifanywa hivo ni wale Hizbu matusi. Wale walifanyiwa vurugu.

Mzanzibari nyama we! Kama yule alokuwa polisi Mwarabu wa Kimombasa yule. Sketty. Yeye alimpiga mtu risasi pale kwa Ali Msha na yeye alirushiwa shoka likamshinda kukwepa likamuingia. Shoka, mkuki? Alirushiwa mkuki…Watoto wa kwa Ali Msha. Tena pale Ngambo polisi pale. Watu wa Unguja nyama we. Upole wao, uungwana wao, ustahmilivu wao, uwongo mtupu! Kumbe upole ule wakati kuna usalama tu. Basi ikishakuwa kuna matatizo basi mbaya.

Kina Rashidi Kawawa wao wakijuwa tu, tena tunapokuja huku [bara] wanatupa hongera. Mimi nikikaa na Mkello na Regional Commissioner wetu, Jumaanne Abdalla. Area Commissioner wa Tanga mjini alikuwa Ali Mwinyi Tambwe. “Hongera, hongera, hongera!” Mimi sikwenda Dar es Salaam. Mimi nalikwenda special kwa Regional Commissioner wa Tanga, Jumaanne Abdalla. Tulikwenda watu watatu. Mimi, Abasi na Haruna. Wakati ule natoka kupigana. Akanambia, nieleze. Nikamueleza mapambano yalivokuwa na kila kitu. Akanambia, “hongera sana bwana.” Nikamuambia nitarudi tena Zanzibar, wamenita wale. Sisi sote tutarudi tena Unguja.

Jumaane akaniambia, haya, lakini mimi naona nyie msifanye haraka ya kwenda kule. Wale watu sku nyingi wamekaa wamebanwa wale. Hawakupata fursa ya kuitumikia serikali yao. Sasa waacheni wao wafanye nyinyi mbaki na kazi zenu. Sasa na sisi tukawa na hamu ya kukaa Zanzibar. Tuna hamu ya Zanzibar. Nilikaa kwangu Tanga. Baada ya kukaa Unguja siku kumi hali ishatulia nikenda kwangu Tanga. Wakanambia usikawie urudi. Nikarudi Tanga nikakaa kitako kazini kwangu kama kawaida, kama miezi mitatu.

Nikarudi Unguja. Niliporudi Unguja nkakaa nkahisi nahangaishwa. Nikawaambia kama mimi tabu kufanya kazi basi nitarudi Dar es Salaam. Hanga akanambia hapana bwana. Usiondoke bwana. Nisiondoke na mie sina kazi? Akatia mkono mfukoni akanipa pesa za kutumia, akanipa na barua kama huyu bwana hamna haja naye basi mwambieni arudi Tanga. Arudi kwake. Aboud Jumbe akaniambia usirudi, mimi kwangu nahitaji mtu. Akanambia, kwanza twende kwa Mzee. Karume akanambia nenda hukohuko ofisini kwa Hanga.

Hanga akanambia meza ile pale kakae. Haya meza hii inataka kufanywa nini? Akaniambia utakiona hapohapo juu ya meza. Nikenda nkakaa juu ya meza hiyo nikakuta ma file. E jamani, haya ma file niyaingilie? Wakanambia “ingia, yafanye.” Nikafanya. Anakuja huku [bara], Hanga, Aboud [Jumbe] na Babu. Wanakuja katika mambo ya Muungano sasa. Mara Oscar [Kambona] anakwenda Zanzibar, hawa wanakuja huku. Alimuradi ikawa fujo. Wakija huku mimi nakaa kule [Zanzibar] peke yangu, mimi na nani? Yule kijana yule, Ali Mohamed Ali Omar, yule jaji. Nikakaa pale. Na siri kubwa ya security yote iko pale. Huku kwangu mie kulikuwa hakuna kitu. Alipoondoka Ali Mohamed Ali akaja Rajab Saleh. Hakukaa hata miezi miwili akafukuzwa. Alitoa uamuzi mbaya. Badili ya kuiwachia serikali kutoa uamuzi alitoa uamuzi yeye. Wakamuhamisha.

Sasa mimi nikakaa pale, nikawa mimi na Makame Mzee. Makame Mzee hamna chochote. Hata kuandika hajui lakini Karume kataka basi. Akenda kule katika Baraza [la Mapinduzi] anaandika, minutes zikawa hazieleweki. Kina Badawi na Ali Sultani wakaleta fujo katika Baraza, Kwanini asipewe Maulidi “Mgazija” akaandika?

Nikaitwa horofa ya pili. Minutes zikitoka tu Barazani asizitowe mpaka kwanza zipite kwako. Thinian Mohamed Suleiman, kijana wa Kipemba pia alikuwemo mle na yeye pia alikuwa hazioni minutes. Yule Makame aliyachukuwa mambo ya Baraza kwa siri kubwa kwamba mtu yoyote asijuwe isipokuwa yeye. Kazi ikawa haifanyiki. Kaibana sana…Nikafukuzwa kazi.

Nikarudi hapa nikapata kazi TANCOT, Tanganyika Cotton Company. Sikukaa hata miezi mitatu, nikapata habari mamangu anaumwa Zanzibar. Nikaondoka nkenda. Na ilikuwa mwezi wa Ramadhani. Nimefika nimekaa sku moja pale, baada ya Magharibi kumalizika, tushafturu, nimekaa karibu na msikiti. Nimekaa tunazungumza zungumza na jamaa tunangoja sala ya Isha ifike tuingie, Mandera akanjia akanchukuwa palepale. Sikuibuka mpaka jela. Na skuibuka tena mpaka baada ya miaka mitano. Hata sikuambiwa sababu. Nimekaa miaka miwili detention [kizuwizini], miaka mitatu nkenda jela hasa.

Nilikuwa na mtoto mmoja wa Simba Makwega, ndugu yake huyu Sophia Makwega huyu. Sophia Simba Waziri huyu. Akanambia, mzee, wewe umefanya nini? Nikamwambia, shika adabu yako wewe mtoto. Unauliza unataka umbeya. Ma file unayo huko ndani, hebu soma hayo ma file. Akanambia, e bwana we, mie nshasoma hamna kitu. Nikamwambia, hata! Akanambia, basi kesho mimi nitayatizama halafu ntakiona, nkiiona ntakwita wewe uje uone hapo ilipoandikwa. Haya vyema. Kweli siku ya pili yake saa kumi akanifungulia huko chumbani kwangu nilikolala. We mzee twende ukanifagilie, ofisi chafu bwana watwana asubuhi wamekaa hawakuisafisha. Tukenda mpaka huko ndani.

Akanambia file hili soma. Maulidi Sheni mkaazi wa Mlandege kakamatwa siku fulani na kaekwa ndani, Sababu hamna. Akanambia, sasa unaona? Akanambia, wazee wenzio hawa. Haya basi. Nikamvizia Mandera. Kila nikimuona, bwana sina nafasi bwana, sina nafasi bwana. Huna nafasi nini wewe? Mimi nataka nikuulize. Sina nafasi bwana! Sina nafasi. Kwani unataka nini? Nataka kujuwa nimefanya nini? Sina nafasi bwana, kweli bwana, sina nafasi bwana. Nimekaa miaka miwili. Mandera alikuwa akipiga sana watu lakini mimi hajawahi kunipiga hata siku moja. Wala sikuulizwa. Nimekaa miaka miwili yote Wallahi Laadhim sijaulizwa, hata kutukaniwa mamangu sijapata. Mwisho nikaanza kunenepa. Nimeshaondosha hofu. Si nakula bure. Nalala tu. Nakula nikiamka, nakula nikiamka.

Kabla ya hapo, niko jela nshafungwa. Ile siku ya kwanza nimekwenda jela, sku ya pili, ya tatu, Hassan Ali, yule alokuwa Kamishna wa jela, yule Ithnaashir yule. Yule tulifanya kazi pamoja. Akanita. Aliwaambia, huyu msimpeleke shamba kwanza mpaka nionane naye. Siku ile nkaitwa. Maulidi, njoo bwana. Haya nkenda. Akanambia, umefanya nini wewe. Nikamwambia, hata sijui. Kama kujuwa wewe unajuwa.

File hili halina kitu. Hapa inasema umefungwa miaka kumi. Bas! Miaka kumi e? Haya. Sasa? Nakuuliza wewe mwenyewe, umefanya nini? Tunatafuta sote kujuwa sababu wewe kwanini umekamatwa, hatujui. Nikamwambia, hata msitafute, mimi nimeshafungwa basi, na nyie msije mkajifungisha ndugu zangu…Tukatolewa kwa kuwaambiwa kuwa sisi wezi wa karafuu, sasa kwa hivo tunaachiwa kwa sababu tunaowapelekea zile karafuu hawapatikani. Kwa hiyo sisi upande wa serikali inaona kama inatuonea kutufunga sisi wakati wezi wenzetu hawapatikani! Ndo tukafunguliwa. Nilipotoka jela nikamwendea Kawawa kumuomba kazi.

Zanzibar wame sign ile agreement [Articles of Union] unknowingly, bila ya kujijuwa. Alokuwa akiijuwa ile agreement ni Nyerere. Karume alifinyangwa na Nyerere. Hakumuachia kukaa na watu wake. Nyerere alikuwa ana akili zaidi. Hakumuachia Karume akae na watu wake kuijadili ile agreement. Imefanywa kati ya Karume na Nyerere na Nyerere alikuwa akimfahamisha Karume yale tu ambayo akitaka ayafahamu lakini mengine alikuwa hayajui.

Sasa kukwambia yote ndugu yangu siwezi lakini mustakbal wa Zanzibar na Tanganyika sioni bright future. Naona kama mwisho tutagombana tu. Naona tutagombana tu mwisho. Uwongo, hakuna mwisho mwema. Manake hawa [Tanganyika] kuregeza kamba hawatoregeza, na wale [Zanzibar] watakaza kamba zaidi. Na kila kinachokuja, hawa wanasema, hata, haiko hivi, na hawa wanasema…kwa sababu kile kitu kiko ndani ya maandishi na yamefinyangwa kiasi ya vile wanavotaka wenyewe. Patakuwa na usalama hapo?

Leo ikiwa Zanzibar CCM itashindwa atakamata Sefu, Sefu hatokubali hayo. Hii party ya Sefu [CUF] haitokubali hayo. Itataka lazma Articles of Union ibadilike, Hawa watakataa! Hapo pana usalama tena hapo? Kwa hiyo mimi sina tamaa ya…kwaherini jamani.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: