Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!

Icon

Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia

Mlango wa Tano: Sakura, Sadaka ya Tanganyika

Hayo ndio maumbile ya uhuru; lazima upiganiwe na ulindwe na wenye hamu nao. Uhuru wenye kupiganiwa na watu wa nje unakwenda kwa watu wa nje. —Mwalimu Julius Kambarage Nyerere

 

Mzee Mohammed Omar ambaye amehusiana na Chief Mkwawa pia anajulikana kwa jina la “Mzee Mkwawa”. Mzee Mkwawa alikuwa karibu sana na hayati Oscar Kambona na alikuwa mhusika mkuu wa kuwakusanya watu kutoka Mkoa wa Tanga kuwapeleka Zanzibar kupiga kura kabla ya mapinduzi ya 1964 na kuwapeleka wafanyakazi kutoka mashamba ya mkonge ya Tanga kushiriki katika Mapinduzi ya Zanzibar.

Madhumuni yetu ni kutafuta historia yetu ya Kiafrika matokeo yalotokea baina ya Visiwani [Zanzibar] na Tanganyika. Mwaka wa 1960 kwenye mwezi wa tisa [Septemba] kama hivi, walitolewa vijana wawili kati ya Zuberi Mtemvu na Chipaka, kuja eneo la Wete, Pemba, kuja kufanya kampeni. Hawa walichukuliwa na chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP) kuja kufanya kampeni ili kuonekana chama cha TANU kibaya. Zuberi Mtemvu alisema mnachokifata si chama cha haki, mnafikiri ule msikiti mkubwa ulojengwa Tanga msikiti, lakini si msikiti ule wanasali Waislamu na Wakristo. Kwa hivyo kama mnafuata TANU mmepotea ndugu zetuni, wa visiwani. Nyinyi ni Washirazi, waumini, leo mnaweza kuungana na chama dhaifu kama TANU ambapo kiongozi wao hana maadili ya Kiislamu. Kwa hivyo nyinyi ule sio msikiti na kama yupo ambaye anaweza kuhakikisha kuwa ule ni msikiti kwa hivyo ajitokeze. Kwa hivyo mimi nikaona nijitokeze. Nikasema mimi nauwelewa sana, nawaelewa watu walokuwa wameshuhudia kuwa ule ni msikiti wakaukubali. Wa kwanza ni Sultan mwenyewe Abdalla bin Khalifa ni mmoja aloalikwa kuufunguwa huo msikiti.

Msikiti mkuu wa Ijumaa wa Tanga. Kwa hivyo mimi nikaeleza Seyyid Abdalla alikuwepo, Sheikh Abdalla Saleh Farsi alikuwepo, Kabaka kutoka Uganda alikuwepo. Naskitika kusikia ati ule si msikiti. Kwa hivyo kama sku hiyo ndipo nliposema kama ni hivyo watu hawa watatu walitanassar wakafata dini ya Kikristo. Kwa sababu wamemfata kiongozi wa TANU wa Kikristo. Kwa hivyo hapo niliona uchungu. Nikakata kadi ya Afro-Shirazi sku hiyo nikawa mwanachama rasmi. Kwa hivyo hata shughuli zangu, mimi nilikuwa ni mjenzi…kama sub-contractor nikichukuwa majumba kujengesha, nilinyimwa. Nilinyanganywa kabisa shughuli zote. Nikafutiwa. Sasa kwa Zuberi kusema hivyo alikuwa kanunuliwa. Akaona awafurahishe mabwana lakini ana hakika kuwa yeye Zuberi ule ni msikiti. Lakini kwa sababu ya mambo ya kampeni ilibidi azungumze hivyo apate haja yake. Baada ya hapo mkutano ukafungwa, watu wakarudi, na mimi nikawekwa kituoni Wete, nikahojiwa umetuharibia kampeni yetu wewe, hufai. Nikaandikwa. Nikatiwa katika Tanganyika Standard ili nisafirishwe, wakati niliishi katika hapo mahala si chini ya miaka kumi na tano niko hapo. Hapo Pemba. Kwa hivyo nilipokuwa nimenyimwa kula kitu, hata nikenda dukani kutaka kitu japo kipo naambiwa hakipo. Nikawa nadhilika, nikatafuta mashuwa, nikapanda nikarejea Tanga. Ile kurejea Tanga nikafika ndani ya mikono ya serikali, nikahojiwa, nikakamatwa immigration paspoti sina, wakati ule mkubwa wa immigration wa kwanza alikuwa Alkabeza wa Mkoa wa Tanga. Myamwezi huyu. Kwa bahati asubuhi nikawachiwa nikaja zangu nyumbani. Kufika nyumbani si nikakaa kiasi ya wiki moja ya mapumziko, nikafatwa na Mkuu wa Mkoa pamoja na wazee wa TANU, nikachukuliwa ofisini, kwa Mkuu wa Mkoa, marehemu Bwana Jumanne Abdalla. Akanambia “tulikuwa tunataka mtu anaweza kuijuwa Unguja na Pemba vizuri kwa hivyo tumefurahi kukuona wewe.” Kwa hivyo mzazi wangu akanambia “utatumikia”. Kwa vile unaelewa utatumika kwenda, lolote la kule la kulielewa tukalipata sisi hapa.

Kwa hivyo alikuwa mzee wangu hasa alonizaa mwenyewe, Mzee Omari, na jamaa yangu Mwalimu Mlimhere, na wengineo, kina Abdalla Rashid Sembe, kina Kisenge, waziri huyu alikuwa. Kwa hivyo nilishughulika nikaambiwa nirejee Unguja. Kwa hivyo nikakubali kutumika. Nikaambiwa utakwenda Unguja pamoja na vitu vetu, kama barua hivi, security inaweza kujuwa hizi siri, kwa sababu security ina vyombo vya mivuke, barua inachanuka wenyewe, ikasomwa halafu ikarudishwa ikafika mahala.

Tunazungumzia mwaka 62. Kwa hivyo nikaanza kushughulika kwenda kule nikapeleka barua kule kama kutambulisha huyu kuwa ndiye atakayekuwa anawasiliana. Na nilifika ofisi Kijangwani. Na nikapokewa vizuri sana na waheshimiwa kina Aboud Jumbe, kina Saleh Saadalla, wengi tu.1

Barua zinatoka huku. Na mwenzetu, mkuu wetu wa safari alikuwa ni Master Oscar Kambona, ambaye alinichaguwa mimi na marehemu Issa Mtambo. Lakini ilikuwa lazma tukutane kule [Zanzibar]. Kwa hivyo mimi nikaambiwa nikutane na Issa na naweza mpa maelezo yangu niliyoyagunduwa mimi kule ayapeleke moja kwa moja kwa Oscar. Hata ndipo nliporudi tena ndo tukaanza kampeni ya kuona katika uchunguzi wetu kuiona hali ya Unguja na Pemba kwenye uchaguzi umeingiliana na Sultani kauvalia njuga. Kwa hivyo tulipata ari tukaona lazima tutetee Uafrika. Itabidi mimi nijitolee hali mali, kwa hivyo nikarudi Tanga nikawaambia hali ya huko ni ngumu kwa sababu Ufalme umeingilia kati. Hili suala ni gumu. Sasa lazma haya yetu tuchukuwe ziada. Kukaa kuendelea kiasi ya miezi miwili, uchaguzi karibu karibu, ZNP wakaanza kuchukuwa watu kujaza majimbo kutoka Kenya kuwatia Zanzibar. Kwa hivyo tukashtuka na sisi tukaanza kuomba misaada Tanganyika kupata watu wa kuweza kuwachukuwa na kuweza kupiga kura. Kwa hivyo tukaweza kuchukuwa watu kutoka Tanga, vijiji vyote vya Tanga, wanaojuwa lugha, lafidhi nzuri ya Kiswahili inofanana na Unguja. Kwa hivyo tukafanya hivyo. Tukachukuwa wake, waume, vijana, wavulana wanojiweza. Kwa hivyo tukapeleka Pemba na Unguja.

Vijiji vya Mkoa wa Pwani wote. Mikoa ya pwani na walokuwa lugha zao mbaya tulikuwa tukishawatia Unguja tunawatia chuoni mule ndani ya nyumba tunamowaweka. Na tulikuwa tunatumia kuwapa kila mtu mwana wa Afro-Shirazi kumpa watu watano alale nao, kumi, na wanafundishwa Kiswahili safi, na kijezo kilokuwa cha madhumuni, kilikuwa ni kijezo cha kuweza kutaja “halwa”, kutaja “binzari”, “tangawizi”. Kwa hivyo walikuwa wana uhakika hawa watu wa Unguja, kuwa watu wa bara hawawezi kutamka Kiswahili kama hicho. Kwa hivyo, tulifuzu katika watu tulokwenda nao wakaweza kutumia lugha vizuri, walipita.

Ilikuwa sentensi yako kabla hukiingia katika kuandika kutaka kwenda kupewa cheti, tiket ya kwenda kuvoti unaambiwa “taja suala hili, hii nini, inaitwa nini?”

Majina yameandikwa. Hii taja, hii ni halwa, tangawizi, binzari. Kwa hivyo walipita. Kwa sababu tuliwafundisha si chini ya miezi mitano, sita. Tumo ndani ya kuwafundisha lugha ile mpaka wakaelewa kuwaita watu kwa lafidhi za Kiunguja, japo wengine walikuwa wakijikwara, lakini ilikuwa si rahisi kumtambuwa. Kwa hivyo tulifuzu, tukaanza kuingia. Tukakaa kitako. Sasa kabla ya kura, tulipoona kuwa sasa vipi tutapata wanachama wengi katika upande wa Pemba, ikabidi tuwalishe yamini kwa sababu wote Pemba walijihisi ni Hizbul Watan (ZNP). Wote. Kwa hivyo pamoja na ZPPP, wakijifanya wao ni Washirazi, si Waafrika.2 Kwa hivyo sasa mtu alipokuwa akitaka aingie chama, tukifanya kampeni aingie cha Afro-Shirazi, tunampiga kampeni, tunampa msahafu, aape “Wallahi Billahi Tallahi mimi nitaipigia kura Afro-Shirazi hapo kama kuna sadaka ya kumhangaisha tunampatia. Na awe ana wazimu akiiunga mkono Hizbu. Awe akili zake si timamu.” Wengine walitupigia, wengine waliona haiwezekani. Kwa hivyo tulifaulu sana, hata vijiji vilokuwa vigumu, kijiji kimoja cha Ole na Kangagani, kilikuwa kigumu sana, kwa hivyo nilikwenda mimi pale nikaitwa “Tindo.”

Nikaipauwa, nikajenga shule ya pale. Pale nilifanya vituko vangu, pesa ya pale yote nikaiwacha pale. Nikawanunulia wanawake pale nguo. Nikaweza kupata wanachama pale na ilikuwa hakuna, kwa hivyo tukamwita Mzee hayati Karume, akaweza kuingia Kangagae na kufanya mkutano mkuu. Tukaipata Ole. Baada ya kufanya hivyo wakajuwa ni mimi nlofanya hivyo, hakuna alofanya isipokuwa yule fundi aloletwa. Kwa hivyo ikabidi mimi nitoke, nikaja kijiji cha Ole, Dodo. Pale usiku wa saa saba, nikatoka ili kufanya kampeni zangu, nikakamatwa kijiji cha Macho Mane, njia ya kwenda uwanja wa kutua ndege Vitongoji. Nikakamatwa hapo. Nikakamatwa na gari la Mohamed [Ahmed] Nassor Mazrui, ndo lilikuwa ni gari lake, na vijana kina Mtendeni, kina…wengi tu, kina Mkomi, kina Hatibu. Nikakamatwa, nikarudishwa Ole usiku huohuo. Nikatiwa kula rangi, nikapigiwa beni, nikaitwa “Kitimbakwiri cha Tanganyika”. Kwa hivyo nikakokotwa, nikapigwa sana, na nikatiwa pilipili lakini kwa bahati nzuri kulikuwa na Inspekta wa Kingazija, aitwa, kama Khamisi hivi, kile kifupi, pamoja na chini yake Master Benecto.

Pilipili nilipakwa mwilini. Kwa hivyo, kupelekwa Ole, nyumbani kwa candidate [mgombea] mwenyewe anayesimamia uchaguzi, yule ndiye atakayechaguliwa, Sheikh Rashid Hamadi. Wakaanza kupiga kelele wakamwita kwa jina lao la kichama “Ya Zaim!” Wakapiga kelele “Hayyen na Mkashkash!” Kwa hivyo tumekikamata hichi kitimbakwiri. Mimi nikatamka, nikamwambia “nakusikitia Sheikh Rashid hujapata kutawala unaanza kuuwa. Ukitawala utakuwaje? Wewe unaamrisha kikundi hiki kinikamate na kunitesa.” Kabla ya hapo, baada kumaliza hapo, wakaingia yule Inspekta pamoja na wa chini yake, Master Benecto, wakamwambia “unafahamu suala, kitendo kinopita kisheria unawezekana kuwa kesho usisimame kwenye uchaguzi? Kwa hivyo hichi kitendo kiondoke.” Kwa hivyo Sheikh Rashid akatowa amri palepale “mwachilieni! Mimi wala sikuwatuma nyie. Mmejifanyia kwa hamasa zenu na ari zenu za siasa tu, lakini mimi siwezi kuamrisha kitendo kama hicho cha haramu.”

Kwa hivyo nikaachiwa, nikarudi, nikapelekwa hospitali Chake Chake, nikahudumiwa na kijana, huyu alikuwa ni dresser msaidizi wa daktari, anaitwa Hassan Al Maardhi, wa Mtambwe kwao. Kwa bahati palikuwa na daktari mmoja wa Kiarabu, Dr Mahfudh, kwa hivyo alisaidia sana, nashkuru. Nikatiwa malhamu, nikatoka malengelenge, majimaji kwa lile joto la pilipili, na mpaka leo mbavu, hivi nnavozungumza hapa, mpaka leo mbavu huwa zanibana bana, kwa sababu zisizokuwa za kawaida—pilipili. Kwa hivyo nikaachiwa. Kuwachiwa, sasa mimi wakanitia moto zaidi. Hapo nikapamba moto. Nikachukuwa hatua kubwa sana ya kuigombania Afro-Shirazi kuliko hapo. Ndipo nilipoweza kuja huku, nikarudi Tanganyika, nikaanza kuchukuwa watu kwenda fanya kampeni, nawaorganise [nawapanga] watu…nikisha waorganise nawachukuwa nawapakia ndani ya magari, watu wa town [mjini] pale, na branch [tawi] yangu ilikuwa ni ile ya chama cha Wazungu, Magiriki, barabara ya kumi na nne.3

Kwa hivyo nikashirikiana na Chama cha Wafanyakazi [Tanganyika Federation of Labor] kiongozi, Bwana Victor Mkello. Kaweza kunikusanyia watu kufanya kampeni na kuweza kupata watu nikawa napakia hapa nenda nao kutoka [barabara ya] kumi na nne Head Quarters [makao makuu] nenda nao moja kwa moja napita njia ya Pangani, kijiji cha Kipumbwi.4 Nilikuwa nikipakia ndani ya mabasi yanoelekea njia ile ya Pangani na kutoka mashamba ya mkonge.

Mabasi kutoka Tanga yalikuwa ni gari ya Abdalla Saidi, marehemu sasa, magari yakina Hashu Sleman, mabasi ndo yalokuwa wakati huo yapo. Na magari mengini yoyote, yoyote yale, yanoelekea njia hiyo walikuwa watu wanarukia. Hata magari ya mizigo. Sio lazima basi. Kwa hivyo nikatia watu kwenda kuandikisha na kuwarudisha na kuwapeleka tena, kutegemea chaguzi. Tulifanikiwa, na kuwatia watu kama walivofanikiwa wao Hizbu. Kwa bahati tukafuzu. Tukapata viti va kutosha. Ikawa viti vilivotuangusha ni viti va Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP), viti sita. Tukasema, tutafanikisha. Tukamfata mwenzetu Mohamed Shamte, tukamvika buibui, tukaja naye YASU, mpaka kwa mkwewe Othman Sharifu. Akatujibu kuwa “hata mkinipa utume sitaweza kuwa pamoja na nyinyi.” Maneno hayo aliyasema nyumbani kwa mkwewe, Othman Sharifu. Na juhudi hizo zote alizifanya Othman Sharifu. Kumchukuwa mkwewe, akashirikana na wenzake kina Mdungi Usi, kina Saleh Saadalla. Karume akajitolea kuwa uongozi wote nitakupa wewe, mimi niwe chini yako, au niwache kamwe, niwe mtu wa kawaida lakini serikali iongozwe na Waafrika. Shamte akakataa. “Hata mkanipa utume,” nasema tena.5

Shamte alisema sitaki tu kuungana na watwana kama nyie. Sababu zake hatukuzielewa.6 Lakini mwanawe Baraka tulikuwa naye ndani ya chama. Katika watoto wa Shamte wote walokuwa mstari wa mbele ni Baraka Shamte. Ndipo ilipofanywa “coalition” [kuungana] ya kuunga chama chao, iwe siku hiyo ndo walete taarab kutoka Cairo, na wageni mbalimbali wa Kiarabu, na Waarabu wengine wa Pangani, na Ithnaasheri wengine wa Pangani. Walihudhuria. Mimi nlisema, hapa niliwaokoa hawa watu, nikawatetea kwa vile hawajitambuwi, nikawaona kama wapumbavu tu kujitia ndani ya mambo yale, kwa vile nawajuwa ni watu wa huku Tanga, niliwatowa Raha Leo. Nikalala nao kama wiki mbili tatu hivi nikawasafirisha wakarudi Tanga. Kwa hivyo niliwasaidia. Na niliporudi Tanga walinishukuru kwa kuwasaidia kuwatowa katika nakama kama hiyo. Na huku tulikwisha unda huku nyuma tukishindwa tufanye nini.

Kwa bahati mbaya walieka kuwa, tarehe kadha walipanga ndo waanze kusheherekea hivo vitu. Kwa hivyo Afro-Shirazi ikajiandaa. Lolote litakalotokea, lakini serikali tuchukuwe. Kwa hivyo ndo vijana wakajitolea, kuvamia serikali wakaingia Ziwani, wakaingia Mtoni, Magereza, Raha Leo. Tukakaa ndani ya muwafaka wetu tukafikiri, katika huo muafaka, tukafikiri nani atakoweza kuleta tishio, ndio tukamchaguwa John Okello, kwa sauti yake ya kibara mbaya, ya kutisha, hajuwi kusema vizuri, itawatisha Wazanzibari. Huyu John Okello akifanya kazi kwa Ahmed Nassor Mazrui. Na alikuwa ni mgeni kutoka Uganda.

Baada ya mapinduzi, kupinduwa, kufanikiwa kwa magongo yetu, tulipanga askari wa polisi, magereza, tulikuwa na vijana mule ndani, tuliwachomeka wajifanye ni ZPPP wapate kazi, ili tupate usiri wa ndani. Kwa hivyo walitusaidia sana. Wakati hawa wanakwenda kufurahikia furaha yao huku nyuma tulikuwa tuna mabaruti yetu, tukayatia katika mageti. Muafaka wetu ulikuwa ni usiku wa manane. Tukafyatuwa, tukawasha, boma la Mtoni, likaripuka, vijana maskini walokuwa wamewekwa na Hizbu, vijana wadogowadogo. Wakashtuka, vijana wa Afro-Shirazi wakaingia ndani wakavamia wakachukuwa silaha wakaanza kuteremka kwenye starehe. Tukateka.

Kwanza ilianguka Mtoni.7 Yale mabomu zilikuwa ni tambi za kuvunjia mawe majabali ndo zilochomwa katika mageti. Tambi zimechukuliwa kutoka Tanganyika. Tukazipeleka. Kisiri chetu, bila ya serikali kuelewa. Mkono ni Tanga, mapitio ni Tanga. Na wengine kutoka Bwagamoyo, akawa ni Abdalla Kheri, kijana wa Unguja.

Abdalla Kheri alikuwa akipeleka watu. Alikuwa mfanya kazi bandari Dar es Salaam. Lakini kwa hamasa ya uchungu wa kampeni kwa kuwa ni mwananchi alijitolea. Alikuwa anachukuwa watu kutoka bandarini, vijana wa Kiunguja, na vijana walio bandarini Dar es Salam, na vijana wa ki-Dareslam, wanaojuwa lafdhi nzuri. Akawapeleka Unguja na akawatafutia malazi pale mpaka siku za uchaguzi, mpaka mapinduzi. Basi kwa hivyo tukafanikiwa kupata serikali.

La ukweli, utaweza kuona kuwa wengine hawaelewi, wakaona ramda Waunguja ndio msaada wamejitegemea wao peke yao kwenye mapinduzi. Lakini utakuta si kweli kwa sababu kama ni WaUnguja wenyewe hawawezi kitu. Kwa sababu kwanza ni waoga. Hawakuzowea mambo ya harakati. Kwa hivyo ilikuwa kama ni wao ilikuwa haina maana kwenda kusaidiwa kuandikisha kura, wala kusaidiwa Wamakonde kujitia, vijana kupinduwa, wakashirikiana.8

Kuna Wamakonde walokuweko kule, kuna Wamakonde walotoka Tanganyika. Na walikuwa wanatoka sehemu za Sakura, wanatoka Ruwazi, Amboni, makabila mengi tu.9 Kulikuwa na Wamakonde, Wangindo, Wayao, Wamwera, Wahehe, na Wanyamwezi wengine, wengi tu. Kama akina Khamis Darweshi ni Myao, Mohamed Kaujore, Mohammed Mfaume, Mmakonde, watu wa Mtwara. Kwa hivyo hao wote Mungu aliwajaalia mapinduzi walipata nafasi ya kupata vyeo.

Technique [mbinu] za Afro-Shirazi ziliwafanya wote wapewe uwenyeji, uzalia, wawe ni wenyeji. Wanapewa mababu, wanafundishwa kupewa babu, na kumtambuwa Sheha wa zamani. Yule Sheha aliopo sasa, apewa Sheha wa zamanii asema “wewe ni mwenyeji.” Haya yalikuwa ni mahoji ya katika kupiga kura, kufanywa mtu mwenyeji. Unaambiwa “Sheha wako nani.” Fulani, Magaramwadi aliyemzaa fulani ndio babu yake fulani. Yule Sheha aliopo akitajiwa yule anaunganisha. Hawezi kuhoji. Katajiwa babu yake.

Kwa kuona Tanganyika, visiwani, wote wanodai uhuru ni Waafrika, kwa hivyo walikaa viongozi wakawa wanakutana. Tutashinda au tutashindwa. Tukishindwa tufanyeje. Ndipo wazee wakakaa kitako wakaziba macho yao, na mashikio, wakaweza kuwaachia vijana walio na ari kuingia. Wakati huo kulikuwa hakuna serikali ya Tanganyika. Kulikuwa na serikali ya kikoloni, haijahama. Mwaka 61 Tanganyika inapata uhuru wake, kwa hivyo ikafumba jicho, ikawaachia uhuru bahari ile, vinavyokwenda, madhali vinakwenda upande wa Afro-Shirazi watu wazibe macho wasione, wala nini. Ili kuwapisha Waafrika wapate hatuwa ya kujitawala. Kwa hivyo, vijana waliingia, na shauri walikaa kitako, tukishindwa walikaa pamoja kupeana mawazo. Tufanyeje mpaka tushinde? Hakuna. Wakaamua hakuna. Kama hakuna tukiwavamia WaUnguja wana kitu gani? Basi, kikatokea kikundi, kikakaa kitako, cha Makomred na Youth League. Vijana wa Youth League ni vijana wa Afro-Shirazi. Wakaamuwa twajitolea, hali, mali. Nafsi zetu. Kwa hivyo wakaanza, ndipo kilichopangwa, hapo tena, kikundi cha kuingia watakuwa hivi, hawa watakwenda Bomani, hawa watakaa boma hili.

Ikapangwa, ikaenea. Sasa ikawa watu wanakula doria katika sehemu zile kutizama utaratibu. Wakati huu vipi, kuna nani, kuna walinzi gani? Kwa hivyo wakapata fursa. Wakajuwa kumbe tukija hivi tufanye hivi, tutafanikiwa. Lakini humo ndani tuna watu pia, wanojuwa hilo litakalotokea, katika hiyo hiyo serikali ya Mfalme, kuwa kuna watu wetu.

Kina marehemu kina Sheikh Daud Mahmud, kwao Kilwa, ni katika hao. Watu wengi karibu Unguja wamechangia suala hilo. Vimezikwa vitu tu mpaka njia za panda. Katikati. Watu wamepiga makafara ya kuwashona paka macho. Nia kubwa Waarabu wapumbaye na serikali. Wasiwaze kabisa. Wadharau kila kitu. Hilo ndo lilofanikisha. Hakuna kitu kengine.

Kikao kikuu cha kuweza vijana kuchukuwa mazowezi, wa kibara na wa kisiwani [Zanzibar], pamoja, yalifanyika mbuga ya Sakura. Tukichukuwa askari waliowacha vita, walostaafu, tukawapa bunduki, nne, tano, huku na kule, kufundisha namna ya kufetuwa bunduki. Japo ilikuwa hatuna bunduki lakini ilikuwa hayo mazoezi yalifanyika, pamoja na kina Jimmy Ringo [Juma Maulidi Juma]10 wakishaona kuwa hatuna vitu va kuvipata, ndo tulipoamuwa, tutakapovamia, tunapopata bunduki, iwe wawili watatu, wanaweza kuzitumia. Walikuwapo watu kama watu mia na hamsini kwenye mbuga. Walikuwa wanakwenda kikundi cha watu kumi, wanarudi, wanakwenda wingine, wanarudi, sio wote kwa pamoja wanashughulika hizo habari. Waloonekana wameshajuwa wanakwenda zao. Wanavushwa wanakwenda zao. Walozowea wanavushwa wanakwenda zao. Hawana silaha, hawana chochote. Kitu kilichotumika kupinduwa serikali ni mapanga, shoka, misharee! Na pinde hizi. Na hivo vimetoka ndani ya Zanzibar na Tanganyika. Vimenunuliwa na wakapewa watu.

Walikuwepo kina Jimmy Ringo, akina Khamisi Hemedi, na vijana wengine. Viongozi wakubwa ni hao. Tulikuwa katika mwaka 1962, Jimmy Ringo alikuwa yuko Tanga barabara ya kumi na tatu kwa Fundi Kidere, halafu akarejea kisiwani Zanzibar. Ndani ya kufanya organisation [mipango] ya mapinduzi ikabidi yeye achaguliwe awe Sakura, yaani kuwashughulikia vijana watakaokwenda kupinduwa serikali ya Zanzibar, kwa hali na mali, wakiwa hawana silaha yoyote isipokuwa mapanga, marungu, mashoka, pamoja na wenzake kina Musa Maisara na Abdalla Kheri. Musa Maisara alikuwa ni kiongozi mkuu, wa pili ni Jimmy Ringo. Abdalla alikuwa akitokea katika safari zake Dar es Salaam anakuja Tanga, anafika Sakura, halafu yeye alikuwa ni msafirishaji pia vijana kutoka Bagamoyo kupitia Fumba, akaingiza mjini Zanzibar. Usaidizi wa kuweza kupinduwa serikali. Alipokuja Jimmy Ringo Tanga pale mwanzo mbuga ya Sakura ilikuwa haijaanza kufanya kazi ya maandalizi ya mapinduzi. YASU [Young African Social Union] ilikuja Tanga 1962 ili kuisadia Afro-Shirazi kupata pesa kwa ajili ya matumizi ya kampeni ya uchaguzi, badala kuwa kama tutashindwa ndio tukakaa kitako kikundi maalum, halafu ndipo tulipoamua tufanye hivo vitu.

Uamuzi wa kuijenga kambi ya Sakura tuliufanya kiwiziwizi tu kwanza bila ya kufahamika, baada ya kufahamika sawasawa ni kwenye 1962 mwishoni. Kufikia 1963 watu walikaa wako tayari. Palikuwa na historia. Ile historia ilihusikana na kina Jumaane Abdalla, Regional Commissioner wa hapa, kuamua kuweka Sakura kwa kuwa ni karibu na Kipumbwi, pa kuvukia kwenda Zanzibar. Watu wakitoka pale waingie mojamoja kwenda zao, bila ya kuingia mjini tena. Kuhusu Sakura nilikuwa nikifahamu, kwa sababu nimefahamu kutoka kwa Jimmy Ringo na Musa Maisara, na kujuwa pia kwa kamati nzima kuwa [mimi] ni mbebaji wa watu kuwapeleka na kuwarudisha Zanzibar. Uamuzi mkubwa ulikuwa na kina Jumaanne Abdalla, mimi pia mawazo ya kupatia pesa, nauli, na nini, nachukuwa kwake.

Hayo yalikuwa na watu wenyewe wa Jamhuri. Yako juu hayo. Vitu vote ni ngazi za juu kuanzia marehemu Nyerere, Kawawa, Kambona, Serkali nzima inajuwa hapo Sakura, na inajuwa, kwa sababu ilikuwa ni intelligence [usalama] ni siri kabisa. Kwa hivyo hivi vitu vinajulikana juu. Kwa sababu wasingeliweza kuwepo pale bila ya ngazi hizo hazielewi. Na sisi tunaelewa, mimi naelewa, kwa sababu ndizo ngazi zilikuwa lazima nizipitie.

Kambona ndo alokuwa kiongozi wangu. Kwa sibabu yeye alikuwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani. Ndo aloweza kutoa authority [amri] ya hii bahari kuitumia. Na nikapewa kiwango nikifika Chumbe pale mpakani basi huko litakalonikuta ni langu mwenyewe. Lakini huku nna hifadhi ya kupewa, wakati kule bado hakukuwa tayari na utawala.

Mara ya mwanzo kusikia habari ya kambi ya Sakura ilikuwa kutoka kwa Maulidi Sheni na yule Mzee, Victor Mkello. Kwa sababu pale ndo ilokuwa kambi kuu. Pale ndo wafanyakazi wa mashamba ya mkonge walikuwa wakipelekwa. Kwa sababu pale ndo ilikuwa kambi kuu.

Matajiri wa mashamba ya mkonge walikuwa ni Magirigi na Wahindi walikuwepo, akina Karimjee hawa. Kazi ya Chama cha Kazi kilikuwa kinakwenda kuchukuwa watu, watu wawili watatu, lakini wasikatwe mishahara yao.

Katika wafanyakazi wa mashamba ya mkonge walokwenda Zanzibar walitokea sehemu za Tanganyika zaidi ni Wamakonde, Wangoni, Wahehe, Muha, Wahyao, Wahaya, ni mchanganyiko wa makabila. Walikuwa wanachukuliwa hawa watu ikiwa wao wenyewe matajiri pia hawajuwi, walikuwa ni wasimamizi tu. [Matajiri] hawajuwi. Kwa sababu yeye achukuliwa mfanya kazi, yeye ajuwa mtu fulani hakuja kazini, ndani ya master roll [daftari la kuhudhuria kazi] wamejazwa. Tajiri yeye hawezi kujuwa. Hawajuwi matajiri. Lakini makarani wale wakubwa, kama mameneja, wakielewa. Kwa sababu msiwakate hawa, wanakwenda saidia umma.

Maulidi Sheni khasa yeye ni mtu wa Unguja. Kwao ni Mlandege na nyumbani kwao palepale. Huu mti, ule Mlandege wenyewe uko chini ya nyumba yao. Kwa upande wa mama, nafikiri ni mtu wa Uzini. Yeye msomi. Yeye kenda mpaka Ujerumani bwana. Huyu alikuwa kwenye utawala. Utawala ndo usomi wake. Si alikuwa ni katibu huyu, wa Victor Mkello.

Wenzake Maulidi Sheni mmoja ni bwana mmoja kwao Pongwe, ya hapa Tanga, lakini yuko Dar es Salaam. Alikuwa chini ya Maulidi Sheni. Huyu yuhai. Anakaa mtaa wa Magomeni pale. Tukimpata huyu atatwambia katika lile tawi lao. Wote ni wa Chama cha Wafanyakazi na wao ndio wakusanyaji.

Victor Mkello alikuwa na Kambona, na mwengine marehemu ameshakufa, ni Issa Mtambo, wa hapa huyu, kwao ni Korogwe. Na huyu ni mmoja alohusika hapo. Ndo alokuwa akigawa mambo ya pesa. Akichukuwa kwa Kambona. Nyerere ilikuwa si rahisi yeye kuja kwenye mambo kama haya.

Wengine waliowahi kufika Sakura ni akina [Mustafa] Songambele, kina Mzee Jangukire, John Rupia, walikuwa mstari wa mbele hao. Wao ndo walokuwa mstari wa mbele wanopanga. Songambele, alikuwa ni Area Commissioner wa Dar es Salaam. John Rupia ndo mwenyewe, ndo alokuwa tajiri kwa wakati ule, kifedha. Alokuwa IGP, Mzee Hamza Aziz, akijuwa.

[Kwa upande wa Zanzibar] Kinyasini kuna ithbati ya makabila. Wanyamwezi walikuwepo pale wengi, sasa na wale wanokuja ile siri itakuwa imefichika. Kwa sababu wote walikuwa ni vijana wa Afro-Shirazi. Kulikuwa hakuna tafauti. Ukiingia ulikuwa unajulikana kuwa huyu si wetu. Ndo walokokuwa akina Saidi Washoto, na nani, na nani.

Kifikra na kikubwa ilikuwa, kikambi pale [Sakura] watu walipokuwa wamekaa, tunapoingia, Mungu katusaidia tumeweza, tunapovamia, kwa sababu Waarabu wametuuwa, ili ndipo tulivoweza kupata kutawala pale, kwa sababu wametutia minyororo, wametupofowa macho, wametufanya ngombe kututoa khaswa, wanaake zetu kupasuliwa mimba kuonyeshwa watoto, kwa hivyo na sisi nasi tuwafanye hivyo, waone uchungu.11

Wakiona wale watoto wamepasuliwa, mke kapasuliwa na tunamwita mtoto wa Kiafrika, yamefanyika hayo, yamefanyika hayo Unguja, yamefanywa. Kuwa bibi njoo hapa uone mtoto anavokaa ndani ya tumbo. Nani asojuwa Unguja. Walofanya wamefanya. Kwenye vikao vyote walikuwa hisia hiyo wanayo. Ipo tayari. Hiyo ipo.

Kusimama [mapinduzi] lililetwa kundi kutoka Tanganyika, la Field Force. Likasimamisha vile vita. Matatizo kutuliza. Hilo ndilo lililotuliza na kuondoa wakabaki memba tu wa Baraza la Mapinduzi, kuna chuki sasa za moyo, wakiwaona watu wamekaa au wanasali kuwapiga risasi bure. Yaani ni uwehu tu. Ufahari wao wenyewe, mwenye akili chafu, kutumia vile vitendo.

John Okello ni mtu alochomozwa lakini hakuwa kiongozi. Ni jumla ya hiyo akili chafu. Kwa sababu mtu mmoja huwezi kupinduwa serikali. Pasipokuwa aliona katika yale mapenzi anopendwa, akajiamini, lolote anaweza kufanya na akaskizwa. Hatukutaraji kuwa atakuwa hivyo. Ni mtu aloletwa tu.

Okello hakufika Sakura. Alikuwa hajuwi. Kama aliambiwa aliambiwa tu watu walivokuwa wanakutana katika vikao. Hakufika hapa kwa sababu namuelewa alipokuwa Vitongoji, Pemba, kwa Ahmed Nassor Mazrui. Na kazi yake alikuwa akisonga matumbawe ya matofali, lile kulichonga likaelekea. Ukweli alikuwepo Vitongoji.

Yule Okello alikuwa ni fundi wa matofali wa Ahmed Mazrui. Nafikiri Ahmed Nassor kapata tabu sana. Kafungwafungwa sana mpaka ukiwa na imani yako unamuonea imani. Sasa sijui alikuwa naye ana siri gani baina ya Afro-Shirazi na Hizbu. Kwa sababu baada ya serikali kawekwa mstari wa mbele kapewa contracts za Zanzibar yote. Mashule yote anajenga yeye. Toka ukoloni ajenga hayo na hii kapewa, bila ya bughdha. Lakini ikitokea struggle [mapambano] atiwa ndani. Kapata tabu sana yule.

Kama ni mchoraji unaichora ile kambi ya Sakura, watu walikutana hapa kisirisiri, wakawa wanakaa sirisiri, sehemu ya mazoezi kwenye msitu huu, kulikokuwa wazi, hapa ndo walikuwa wanapata chai (mkahawa), wanachomoka mmojammoja wanaingia baharini, mpaka wamalizika, waingia ndani ya vyombo hivyo, wanakwenda. Usiku mnalala kujifichaficha, kuziba siri zenu zisitangae. Lakini fununufununu, serikali yenyewe ilikuwa haijatimia hivyo. Je, Muengereza keshatoweka kabisa? Lawama, kuwa hawa wanakwenda ingia nchi ya watu.12 Nafkiri nlikwambia unapopewa barua hapa kupeleka Zanzibar, waambiwa, ukikamatwa wewe ukubali kufa, hii izamishe, isipatikane.

Barua zilikuwa ni za mazungumzo na mipangilio. Zinatoka serikalini huku. Kutoka kwa Oscar na yeye inatoka kwa mwenyewe kinara, inakwenda kwa kinara cha kule. Hizi si za chama. Ukifika moja kwa moja unampa Aboud Jumbe au Hasnu Makame. Mipangilio ile ya huku na huku. Mimi nilikuwa sielewi ndani mna nini. Mimi kazi yangu kufikisha mzigo. Nyengine ni fedha. Kuwasaidia wale viongozi wanapotaka kusimamia kura. Zamani pesa zilikuwa zikitiwa kwenye ile mifuko ya kuvuta ya nguo. Barua za Abdalla Kheri zinatoka Dar es Salaam. Na yeye alikuweko katika Chama cha Kazi, pia huyo.

Chama cha Kazi ndo kimefanya kazi kubwa! Chama cha Wafanyakazi ndo mstari wa mbele. Mkubwa wao yule pale Victor Mkello. Na yule kapata cheo cha kuwa Regional Commissioner, kama si Regional Commissioner…kwa sababu ya chama, kwa sababu ya wale wafanyakazi wa mkonge walokwenda pinduwa Zanzibar, akapewa uwezo na madaraka. Akazidi kupanda hadhi. Uongozi wote unatoka kwenye Chama cha Wafanyakazi, pande zote mbili. Si ndo walokuwa wakichanga pesa wakikamuliwa. Mkello akafungwa. Inasemekana alihusika. Ndo maana akafungwa ati. Sasa tumpate kijana wa Pongwe, mimi nimuone Makalo nimuulize, alochaguliwa katika Bunge wa kuteuliwa na Nyerere wakati ule. Sasa nimuulize yule bwana alokuwa katika chama cha kazi, Abdulrahman nafikiria hivi, yuko Dar es Salaam au yuko Mazazara, Pongwe? Wako wengi tu walokuwa kwenye chama cha kazi wenye kumbukumbu ya mapinduzi ya Zanzibar.13 Wafanyaji kazi wa mashamba ya mkonge hawakupelekwa Zanzibar kama ni Manamba. Wamenyokolewa tu kwenye mashamba ya mikonge tafauti, wawili watatu, wamekubaliana, nikawatia katika chombo mpaka Zanzibar. Ndivo ilivokuwa. Baadhi yao ni hao hao Wamakonde wanaokataa. Mwisho wengine waliozwa watoto wa kike wa Kiarabu wakaja nao ndani ya meli hapa katika kile kipindi kilichovusha Waarabu wengine wakarudi Oman, wengine katika hao Manamba wakateremka hapa wakenda mwakwao. Sasa unakuta wale walipokwenda, sasa wale wengine walibaki wakaoa. Mmoja tulikuja nae mpaka hapa na mkewe, Mmakonde, wakenda zao. Baadhi ya hao Wamakonde na makabila mengine yalokwenda wapo hapa Tanga.

Wamakonde waliokuwa wakiishi Zanzibar nawajuwa na kweli walikuwepo. Wale walikuja zamani. Walikuweko. Walokwenda walikamatwa kwenye mashamba ya Mkonge. Hawakwenda kwa ajili ya kufanya kazi za Manamba Zanzibar. Walikuwa Manamba huku. Zanzibar walichukuliwa kwa kwenda kusaidia mapinduzi tu. Hakukuwa na utaratibu wa Manamba Zanzibar. Ukenda ukawauliza watu wa Mwera ya hapa Tanga utapata habari zao na utawapata. Hapa ukimpata yule Mmakonde alotiwa upande wa jeshi akaowa mke wa Kiarabu na marafiki zetu wa Kimakonde, na makabila mengine, walioko huku wanayafahamu haya. Walioko Unguja wanaweza kukataa kwa sababu hakuna alochukuliwa pale. Lazma wakatae. Kwanza walikuwa woga. Walishiriki wengine lakini ki organization [kimipango] walikuwa hawamo. Kwa sababu walikuwa walinzi katika mashamba ya Waarabu. Wataunga vipi?

Victor Mkello ni mzuri sana kwa habari hizi lakini na yeye ndo vile, sijui ana woga gani. Alitiwa ndani yule ndo mana. Ana woga yule. Ukenda kuwauliza wenyeji wa pale pale Kipumbwi karibu na shamba la mkonge la Sakura, wangesema kweli watu waliondokea hapa. Pale pale. Leo mwana TANU wa hapa hawezi kusema hajui suala hilo. Wanaweza wengine wakawa woga lakini wapo wanaosema. Ningekueleza Unguja au Dar es Salaam mbele ya [Shaaban] Mloo basi Mloo angekuambia kuwa ni kweli. Angelikuambia kuwa huyu ndie alokuwa akiwasafirisha. Manake walikuwa wanapigwa kampeni, ewe bwana tuna kazi yetu twende Unguja ukatusaidie. Kulisha na mpaka kula na gharama kila kitu zilikuwa zinatowa TANU. Marehemu Jumaane Abdalla alokuwa Regional Commissioner [Mkuu wa Mkoa] hapa ndo alokuwa anotukusanyia hapa halafu tunakwenda. Na yule alokuwa Area Commissioner, Issa Mtambo, naye amekufa. Yule alitolewa kama security [usalama] akakaa mtaa wa Malindi, akawa anasali msikiti wa Malindi, kuchunguza wanazungumza nini. Alikuwa karibu na Sheikh Abdalla Saleh Farsy, kasoma vizuri, kajitia imamu kuchunguza. Ukweli ni huo.

 

Wafungwa wa Siri Nzito ya Historia

Nyerere ndie alokuwa akifanya organisation [mipango] yote na kuweza kuwafanya watu wapinduwe serikali ya Zanzibar. Yeye Nyerere. Sasa yeye akaona akifanya historia, kumbukumbu, anaogopa Umoja wa Mataifa wa ulimwengu wakamuelewa kuwa yeye ni kitimbakwiri…Ile ni siri yake. Hakutaka siri itoke. Ingekuwa aibu kwake. Anasikia lawama litamfika kubwa.

Kwa sababu halafu si unamuona ataka utawala uje kwake. Yeye ndo awe leader [kiongozi]. Yeye si ndo alotaka Regional Commissioner [Mkuu wa Mkoa] wa Zanzibar aje Tanzania, Regional Commissioner [Mkuu wa Mkoa] wa Pemba aje mkoa wa Tanga. Yaani aichukuwe Zanzibar kimaarifa. Alikuwa keshaanza zamani sana, baada ya mapinduzi tu. Akakataa marehemu Karume. Akatia guu. Akasema, “mimi nikiingia Zanzibar, ni Rais kamili,” ka-announce [akatangaza] hasa mwenyewe kwenye mkutano: “Nikishafika Chumbe, nikipita ninakuwa ni Makamo wa Raisi. Na yeye Nyerere akiingia Zanzibar lazma aniskize mimi huku kwa sababu mimi ndo Rais wa Zanzibar. Na sina haja ya uchaguzi kama anavotaka Nyerere. Au mnasema nini wananchi? Muangalieni yule mtoto Nyerere, anataka uchaguzi ati, Zanzibar. Mimi nimeshachaguwa Januari. Mnakubali wananchi au mnakataa?” “Ndiooo!”

Sasa alikuwa ana maana gani? Mie hasa usinikumbushe mambo ya Nyerere. Akaingilia Uganda. Uganda rafiki yake Obote kwa kuwa ni Mroma mwenzake na yule Idi Amini ni Islamu, akaona ampe uwezo na awauwe watoto wetu hapa kuwapeleka Uganda, hakuna maana yoyote aloyafanya. Wale pale wako. Hawana macho, masura mabaya, wazazi hawakupewa single penny [hata pesa moja] kwa mchango wao walioutowa. Hawa wasojuwa ndo wanamuona Nyerere ni binaadamu.

Sasa watu wamepata maradhi yale, wote wanakuwa waoga. Wanaiona serikali hii ya Tanzania tukifanya historia tutaingizwa ndani, tutapoteza maisha yetu. Ndo woga wote wa kina Mkello. Kwani watu hawajuwi? Hakuna hata kimoja kisichojulikana. Sasa ile kutishwa. Unajuwa unapopelekwa ndani ya nakama, ukitolewa, una hofu. Sasa ukitupwa namna ile alivotupwa Mkello, ukirudi, unakuwa umefungwa. Yeye yule hayuko huru pale.

Anamuogopa huyu alorithi [Benjamin Mkapa] mwanawe Nyerere. Akili zao si moja tu. Nini maana ya kumchaguwa lazima achaguliwe Mkapa? Si kampigia kampeni yeye? Njia yao moja. So Mroma mwenzake? Nakwambia, kamlea mwenyewe. Watu wengi wanasema. Huko uliko hujajuwa kuwa Nyerere anaikwamisha hii nchi?

Nyerere alichukia baada ya kuokolewa na Kambona nchi ilipochukuliwa na jeshi. Alikuwa amekwisha Nyerere. Alikwisha! Yule akalituliza lile jeshi. Sasa Nyerere akaona doo! Hivi mimi si lolote, si chochote, mbele ya huyu? Wakati wowote, mimi nimeshindwa kulisimamisha. Huyu kasimamisha kama kunusa? Akapata nafasi ya kukimbia akenda akakaa kando! 14

Nyerere akaona huyu, bila ya kumtia query [kumdhania dhana mbovu], bila shaka walikuwa pamoja. Kambona akaona anusuru roho yake akapotoka. Na wengine wale waliotaka kumpinduwa Nyerere 1964 wajomba zangu. Mpaka leo mjomba wangu yuko. Huyo alotaka kupinduwa. Utapata tabu sana kuyapata yaliyotokea. Yataka kula mmoja umtekenye, atowe kidogo.

Wengi walioshiriki katika mapinduzi si Wazanzibari. Kwa mfano, Khamisi Hemedi Nyuni kwao hapo Kivumbitini [Tanga]. Si ndo mana nikakuuliza wepi? Yusuf Himidi yule ni mbara lakini kazaliwa kule. Ni mtu wa Pemba. Wengi wao ni wabara. Mbona unajuwa ulimwengu mzima, mapinduzi ya Zanzibar headquarter [makao makuu] ni Tanga? Wengi wanajuwa Unguja. Si unawaona viongozi wa CUF? Juma Ngwali, anajuwa. Mzee [Shaaban] Mloo, anajuwa. Ni mmoja katika chama cha kazi huyo. Kwanza Mloo mimi nikimpata aweza kuntosha. Nitamwambia “komredi wewe umeshakuwa mzee, ukifa kufa, na mimi ndo hivo hivo. Kwa nini tunaitupa historia?” Katika CUF wako wengi tu. Yuko yule bwana wa Donge yule alokuwa polisi [Machano Khamis Ali], yule alokuwa mwanasheria, Ali Haji Pandu, anajuwa. Na ni wenzangu hao.15

Serikali yenyewe ndo ilogoma kuweza kupata lawama. Kuambiwa ni chanzo cha vita, uchochezi.16 Linoogopwa hilo tu. Hakuna jingine. Sasa imewabana watu kuwa ukiitowa siri hii basi mawili yatakukuta: kifungo cha maisha au kunyongwa. Sasa hivi haidhuru. Ilikuwa ikitisha kwa Nyerere tu alikuwa haitaki. Wote wasomi sasa hivi. Sasa hivi watu wote wasomi. Ni kumbukumbu za hawa wanosoma. Hawa watoto wanosoma hawa.

Jimmy Ringo alikuwa mtundu bwana. Alikuwa ni mtu matata. Katili. Kulikuwa na bwana mmoja, Abdi Tarazo, alikuwa akitia tarazo. Huyu aliwahi kusafirishwa. Badala ya kupatikana serikali alitiliwatiliwa maneno kwenda kinyume na serikali, Zanzibar, hiihii Afro-Shirazi, wakamsafirisha, wakamrudisha kwao Morogoro. Alikuwa ni kijana wa mapinduzi. Alishiriki kwenye mapinduzi vizuri tu. Alikuwepo Sakura.

[Kama nilivoelezea kabla] mimi niliporudi kuchukia kisiwani, nirudi niondoke kisiwani Pemba, nikaja zangu Tanga, nilipofika Tanga, nikakaa, ndipo nilipopewa uwezo wa kuweza kuwapeleka watu Unguja na Pemba, halafu, nilipowapeleka huko, nikapewa, kuwa unapokutwa ndani ya chombo hichi, basi kama una barua ya kuipeleka huko, basi bora ufe kuliko kukamatwa na hii. Kwa hivyo utakubaliana na kifo? Wewe uwe kama sadaka ya Tanganyika. Kwa hivyo nikajitolea nikawa kweli ni sadaka ya Tanganyika. Nikakubali kifo, nikakubali kusalimika, na nikapewa gharama ya kuwa uwezo nlopewa ni kutoka bahari yetu ya Hindi hii mwisho ni Chumbe, mpaka wa bahari ya Tanzania Bara,Tanganyika, na Zanzibar.

Lakini hii ya Tanganyika nimeitawala. Nikiingia tu, naingia bahari ya Zanzibar litakalonikuta, nimeuliwa, nimepona, basi yote yawe ni sawa. Lakini isiwe nije nimeshikwa nijieleze. Ah! Mimi nimetolewa Tanganyika. Hapana. Niwe niko serious [madhubuti] na kuokoa Zanzibar.

Kwa vile nikakubali kwa moyo mmoja wa kufanya hayo kwa sibabu tunataka kuukomboa Uafrika. Kwa hivyo na mie ni Muafrika, na ni asili yangu pia.

Na Zanzibar, mimi nilikuwa nalala chugachuga. Leo nikilala nyumba hii, nikae sku mbili, nikishaona hawa watu wameshaanza kunitambua naondoka, nakwenda mahala kwengine. Ni mtu wa kushtukiza. Sku nyingine kwa Mdungi Usi, sku nyingine Mosi Jecha Pili, sku nyingine YASU na sana nililala YASU pamoja na Swanzi.

Ilikuwa wakati nikifika na watu Kipumbwi, ninagawa mashuwa. Napeleka watano, kumi. Hawa nawapeleka waingie pale saa nane, wengine waingia alfajiri, wengine saa kumi, mashuwa mbalimbali. Kusudi nisishtuwe kuingiza kwa kikundi moja kwa moja. Wakifika pale Muwanda, kituo cha Muwanda, Zanzibar, wanapata mtu anawashindikiza mpaka barabara kubwa. Kwanza wanakwenda kwa chairman [mwenyekiti] wa Afro-Shirazi, nyumba yake iko ufukweni, unaiona bahari ile pale. Na ilikuwa nkitia watu, wakati wavuvi wanatoka baharini na wale nawatia waonekane ni wavuvi. Na tunavua tunateremka na mashazi yetu ya samaki.

Baharini kunaweza kuwa na vyombo kama kumi na tano, kumi. Manake vinakwenda mbalimbali tafauti. Kula mmoja na mivuvi yake. Mwengine enda mbali zaidi, mwengine enda karibu. Kwa hivyo sisi tunaanzia Tanga kuvuwa, Kipumbwi. Tunavuwa tukenda, huku tunakwenda tunavuwa mishipi. Tunachukuwa samaki tunatia tunatunga ndani ya mashazi. Na nguo zetu safi tumevuwa tuna nguo za kivuvi. Suruali kipande au mashuka machafuchafu. Kofia tunavaa za makindu.

Tukifika pale twatoa begi zetu zatangulizwa barabarani. Kijangwani ilikuwa tunaingia saa mbili usiku. Hatujapanda gari mchana, ila mimi peke yangu. Wanajulikana wageni kadhaa wameingia. Tukifika Kijangwani tunasajili watu wangapi wameingia. Hasnu Makame ndo alokuwa akiwasajili, ndo bwana fedha ati. Hatoi fedha. Anajuwa wakati wa asubuhi posho itahitajika ya watu wangapi. Kula mtu na wageni wake atakaekuwa nao apewa hela awapikie huko.

Pale Kipumbwi wanalala usiku majumbani, pale nje kwenye branch ile hoteli nlokuonesha. Ile ilikuwa ikilala watu. Chai, mbaazi, mikate, kila kitu hapo. Halafu kisha pale mmeshiba tena, kula unakwenda kula Unguja huko.

Tunatoka alfajiri wakati wa umande tunaingia mapema kule, saa nne, tano. Twateremka, Ya Allah! Sasa tutafute mahala watu wanapumzika, mpaka wakati utakapofika. Walikuwa wanalala chumba watu watano, watu kumi, kumi na tano. Hawatoki. Watakuwa wanasoma Kiswahili humo. Watoto wa kike wanawasomesha, wa Kiunguja. Manake ukitaka lafdhi nzuri ni mtoto wa kike.

Sasa wale watu walikuwa hawana cha mafao. Pesa walikuwa wakipewa kama pocket money [pesa kidogo za kutumia] za sigara. Bas. Baada ya mapinduzi wamerudi wenyewe. Wote. Wamerudi. Walotaka kukaa wapo, wamekaa. Wako wengine walibaki. Wale walokuwa hawana kazi huku. Wengi wao waliokuwepo walirudi wote.

Baada ya mapinduzi wakaanza kuwakataa watu wa Tanganyika, Kenya. Fitna. Wakaingiwa na moyo wa choyo. Vijana wa Kizanzibari. Kutakuwa hawawapendi watu wa Tanganyika. Wakawa wanawafitinifitini. Maneno ya uongo yasofaa na Mzee [Karume] akawa anayakubali, mengine hayakubali, manake wanatisha. Na mtu ukipinduwa ukitishwa watishika. Japo lisiwe la ukweli lakini ukiambiwa kuwa wale wataka pinduwa, wamekaa tumewakuta, kumbe hawana lolote, wewe utatishika kwa sababu unafahamu ukidharau itakuwa umejidharau. Sasa lazima ulibane, halafu ulichunguze. Ni kweli? Wako watu waliwekwa namna hiyo halafu walitolewa jela. Ikaonekana si kweli.

Matarajio ya muungano ulivokuwa, ilikuwa muungano ni wa misaada inavotokea harakati mbaya wasaidiane, lakini kula mmoja na mambo yake ya nchi, ya ndani. Na ilikuwa ni ten years [miaka kumi], tulivofahamu wote Wazanzibar ni ten years [miaka kumi], na kwa bahati Mzee [Karume] hakufika miaka kumi, amechelea kwenye miaka minane.

Mazungumzo ukweli ya mwenyewe marehemu Mzee Karume ilikuwa “tukiona muungano wetu wahitajika kuwa tuuendeleze tutakaa kitako tuuendeleze. Tukiona tutauwacha utabaki urafiki mwema.” Na kuitengeza Zanzibar iwe ni huru ni nchi ilokuwa haitaki ghasia, iwe kama Paris. Hizo ndo fikra nilizokuwa nikizipata kwake. Na ndivyo, kwa sababu alikuwa keshaanza kujenga mambo ya starehe. Majumba, mtu huwa hachajiwi [halipishwi] achajiwa umeme tu. Hata kisiwani kule alitaka kufanya kiwe kisiwa cha starehe. Na dalili ni ile alojenga Bwawani. Alikuwa akiendelea. Kwa hivyo alikuwa hana lengo baya Mzee Karume. Akizijuwa hizi habari lakini jemedari wa mambo bwana [Abdalla Kassim] Hanga.

Nyerere aliyasema maneno kwenye radio kuwa leo Wazanzibari mnajuwa hakiii? Sasa sisi tunofahamu tulibaki kucheka. Tukafasiri kama leo Wazanzibari mwataka haki, mwaijuwa haki, ni kusema, wakati ule mbona mlikataa msiungane mkawa wamoja, ikawa hawa ZPPP, hawa ZNP, hawa nini, leo badala ya sisi kuwasaidia mwaidai haki kwetu. Vipi? Kwa sisi tunojuwa namna gani Tanganyika ilivoisaidia Zanzibar, mimi haikunipa tabu. Nilifikiri haraka sana. Na nikacheka sana. Kwa hivyo aliwatukana.

Hawa watu kwa kuwa utawala kwao ni mgeni, utawala ni mgeni kwao wote, basi ilikuwa wajuwa nikifanya historia labda ntateswa, eh, rabda nikisema hivi ntatengwa, ntaonekana sifai, na hususan hasa ntafichwa, ntafungwa, au ntauliwa kwa mateso. Mara nyingi ukweli Tanganyika na Tanzania nzima, ukweli ndo hawautaki. Kula unaposema ukweli, wewe ni mbaya sana. Ndo mana hawathaminiani. Ukiwa na wazo lako zuri basi Mtanganyika halitaki. Kwa sababu Mtanzania anajitaka yeye mwenyewe manfaa yeye mwenyewe tu. Ashapata mahala pazuri basi yuko tayari kukukandamiza wewe usende.

Historia si hiyo imeshapotea! Hii ya Zanzibar ni filam kali sana. Hata ya Uganda ni historia kali sana. Wameipoteza pia. Iko wapi? Mimi nimekwisha andika historia na kitabu cha babu yangu marehemu Mzee Mkwawa. Nnayo historia yetu ya Wahehe. Tumeanza kutoka mlimani kule mpaka tukaja makaburi ya Nyondo, Ibamba, Ikwatwiru. Chifu Adam Sapi ni mjomba wangu. Mkono wa Nazi ni mjomba wangu. Gaugen Marangarira ni kakangu.

Kamati ya Ukombozi ilikuwepo. Msaada wa kuweza kuzikombowa nchi zilizokuwa na matatizo kuzisaidia kisiasa. Ndani ya TANU. Mpaka sasa zinaendelea. Baada ya Zanzibar ikaja Uganda. Kabaka halafu Amin. Ikaja Sychelles, Komoro. Kamati ya Ukombozi ilikuwa ikiongozwa na Oscar pamoja na Mzee, kina Kawawa hao. Hao ndo wenyewe.

[Na kama nilivokwishaeleza] Issa Mtambo alikuwa anatumwa na Oscar Kambona, ndo alokuwa moja kwa moja na upande wa Kambona na Usalama wa Taifa. Sasa Issa alikwenda upande ule kuweza kujuwa mazungumzo ya Waarabu wanasema nini katika nchi. Ni rafki zake, aswali nao, kawa shekhe mkubwa, alikuwa kasoma uzuri, na anafaham dini. Sasa akawa yuko kule. Akiyapata yale, na nafkiri alikuwa ana chombo cha kurikodia maneno, sasa unakuta Issa, yaani yeye alikuwa akikutana na viongozi hao. Na halafu akajikubalisha kama yuko upande wao. Wanamuona ni mwenzao. Sasa akawa anapata sehemu mbalimbali. Akitoka pale sasa ndo anakwenda kukutana na akina Mzee Karume, pale pale Zanzibar. Si anapachuka. Ana safari zake. Anaonana na wale, anaeleza, anazungumza.

Rafiki zake wakubwa zaidi mimi nilikuwa siwezi kujuwa kwa sababu yeye alikuwa akifatilizia kule moja kwa moja. Akitoka huku, Tanzania Bara, alikuwa anakwenda moja kwa moja kule Zanzibar. Mwenyeji wake alikuwa yule Kadhi, Sheikh Abdalla Saleh Farsy, ndo alokuwa mwenyeji wake. Alikuwa anajitia kama anasoma ilimu. Alikuwa yuko mjini Zanzibar. Anapiga kanzu yake, akaa kule, taratibu, dini na yeye na mkeka, bas. Hata mimi nikiwa nimeishiwa na pesa Zanzibar nikiambiwa nionane na yeye Issa Mtambo. Akaja YASU pale tukakutana, akanipatia hela ya matumizi, mimi nikarudi huku. Kwa hivyo yeye alikuwa kule, mimi nilikuwa katika Uafrika, na yeye alikuwa upande wa Waarabu.

Abdalla Kheri yeye kazi zake kama za Issa lakini anapeleka watu kule, na wakati ule wa organisation [mipango] ya mapinduzi, yeye alishiriki pia, kuwaleta watu kwa kupitia Bweleo. Ni ndo njia mbili tu hizo, Bweleo na Muwanda. Hakuna njia nyengine ilokuwa ikitumika. Hii ya Pemba hii sio sana. Ilitumika, lakini ilitumika wakati wa kura tu. Halafu huyu Abdalla Kheri alikuwa ni mstari wa mbele. Kwa sababu alikuwa ni mkakamavu sana. Ndivo alivokuwa.

Mimi ni grupu la akina Maulidi Sheni. Sikuwa na wasaidizi. Mimi nlichaguliwa peke yangu kwa sababu nilikuwa kama ni amiri jeshi kuwakuta wale kwenda nao, na kuwahifadhi na kuwarudisha. Usalama wao wote upitie kwangu. Na alonchaguwa mimi ni Kambona mwenyewe pamoja na Jumaanne Abdalla hapa, marehemu.

Tulikaa pamoja. Hadithi ni ukombozi. 62 hiyo mwishoni mpaka 63. Na ndio tumo kwenye kazi sasa hiyo 63. Tulikuwa hatujuwani isipokuwa tulikuwa tukikutana Kijangwani, Zanzibar. Lazim kule tutakutana. Huku kula mmoja ana njia yake. Kula mmoja alikuwa akikutana na Kambona kivyake. Haijapata kutokea kukutana kwa pamoja na Kambona. Haijatokea. Hata mara moja. Kiunganisho kilikuwa ni Ungujaa! Kule ndo twafahamiana sasa.

Mimi nilikuwa nakutana…tulokuwa tunakutana tulikuwa ni Jumaanne Abdalla pamoja na Kambona hapa, Ikulu hapa Tanga, si Dar es Salaam. Yeye alikuwa akija hapa. Kawawa alikuwa akija hapahapa Tanga. Kwa hivyo ilikuwa haina haja mimi kwenda kule, kwa sababu hapa naweza kutoa ripoti zote kwa Regional Commissioner [Mkuu wa Mkoa]. Anaweza kuzitekeleza OK, hawezi anampigia simu Kambona.

Sijapata kukaa na Nyerere hata mara moja. Yeye akikaa na Kambona, Jumaanne Abdalla. Pale juu. Na halafu yeye alikuwa anajuwa yote, si kwa sababu alikuwa akielezwa. Kuonana naye lazma utaonana naye. Kusudi si atambue. Alikuwa hawezi kujitambulisha kwa sababu alikuwa si mtendaji.17 Si katika sheria mtendaji ni Katibu Mkuu [wa TANU], Kambona na wenzake?

Nyerere alikuwa ana wasiwasi kwa kwamba hili suala halitofaulu kwa sababu walikuwa hawana silaha. Sasa wewe uwe utakwenda kichwa kichwa itakuwa vipi? Na sasa yale nlokwambia walitiwa bumbuwazi wadharau.

Habari za silaha kutoka Algeria mimi sina. Si angelinambia Issa kwa sababu alikuwa karibu sana na mie kwa sababu tunatoka mji mmoja. Yeye si Mzigua anatoka hapo Korogwe. Kwa sababu mengi tukiambizana sisi.

Tulijuwa kuwa tungefeli tungelitawaliwa vibaya. Sasa hilo tuwe nalo. Tusilie. Lakini tulipima tuliona hawa lazima tutawaweza. Kwa sababu, kwanza walikuwa na jeshi la kipumbavu, la kitoto. Watoto watupu. Uimara wa moyo walikuwa hawana. Mie pia nlikaa nikawa najiuliza “hizi silaha walizonazo kweli watawezekana watu kama hawa?” Haya tuyitazame.

Mimi bwana nilikuwa mtu nikiishi kule toka 1949. Ofisini mwake Jumanne Abdalla akanambia “tunashukuru kukuona kwa sababu tulikuwa na shida na mtu anayeijuwa Unguja na Pemba vizuri.” Mzee wangu alikuwa mstari wa mbele katika TANU. Yeye Jumanne Abdalla akanijuulisha kwa Kambona. Walichaguliwa vijana watatu wakakataa. Ukikamatwa itakuwa wewe umeshiriki kutia vita kule kwa sababu si nchi yako.18 Akampigia simu Kambona akaja tukakaa watatu. Tulipokaa ndipo waliponambia kuwa wewe utashughulika kupeleka barua zetu kwa sababu zinafunguliwa kwa posta.

Pia nilikuwa napewa maagizo ya mdomo na kikaratasi cha idadi ya watu. Basi imekwisha. Nikiwasilisha tu, zinasomwa, zinapigwa moto. Huwezi kuweka kitu kama hicho. Mambo yote Kijangwani ndo headquarter [makao makuu]. Pesa za kampeni pia ndo nlokuwa nikipita nazo.

Walikuwa hawana lolote. Afro-Shirazi ilikuwa haina hela bwana. Haina kabisa. Pesa zikitoka Tanzania Bara, Tanganyika. Hapa hapa tu. Ndo maana sku ile, Sefu [Sharifu] adai serikali tatu, Nyerere akamwambia “leo hii. Mnaweza kufika mkajuwa haki yenu? Nawashangaa sana.” Mimi nkacheka sana. Nyerere awatukana hawa. Kwa Kiswahili unawatukana. Awafanya hawa walikuwa hawajuwi, msingetaka msaada mgelijikombowa wenyewe. Manake ni hiyo. Wasingeliweza kujikombowa wenyewe bila ya msaada wetu. Hawawezi. Iangalie Pemba na Unguja ilivyo. Bila ya hapa ilikuwa hawawezi. Kwa sababu angalia wakati wa uchaguzi wa Julai 1963.

Umma Party usiwatowe.19 Wao ndo walokuwa na harakati zote za kupinduwa. Uongozi na kitendo mambo mbalimbali. Uongozi wa kujuwa namna mambo ya mapinduzi yakoje, na kujuwa kutumia silaha ni Umma Party. Huku imeshirikiana kiwatu na kipesa. Lakini watendaji, tukiingia, tukifanya hivi, hapa patabomolewa hivi, Umma Party. Na kamando si anopiga. Ni mwekelezaji. Wao ndo waloelekeza. Badala ya kushika serikali wao ndo wakawa wasimamizi wakuu. Fanyeni hivi, wakatiwa utomvu wa mafenesi, ukangandishwa, imetokana na wao, sio hawa. Majani unaona kama yanapepea, yamo kwenye migongo ya watu. Kazi yao.

Si Babu huyo? Alikuwa keshaweka watu wake sawasawa halafu huyo akaondoka zake. Akajiweka Dar es Salaam. Na Ali Mahfudh ndo mwanajeshi mkuu khasa wa Umma Party ndo alotowa vitu kwenye mapinduzi. Halafu anakataa nani? Ali Nyau aweza juwa kwa sababu ni mmoja mstari wa mbele. Wale ndo walokuwa wameshika mstari mbele. Tanganyika walikwenda kupeleka watu, kama jeshi, na wote alama zao wavae mapakacha, ili wajulikane kuwa ni wenzetu.

Hata bila ya Umma Party mapinduzi Zanzibar yangelitokea. Yangelitokea. Kama ndo wamekwisha funguka. Kwa sababu, hata hiyo Afro-Shirazi haikuandaa kuwa ati wasaidiwe na Umma Party. Pasipokuwa, baada ya kukaa, kuwa wanachama walojiunga pamoja, ndo wakafanya kikao cha pamoja tutashirikiana juu ya hili suala, na sisi kulielewa na kivita, na kutoka hapo uelewe, kuwa Abrahman Babu anaelewa muongozo wa kivita, kwa sababu ni Mkoministi. Na ni kweli kutoka siasa yeye alikuwa na Ma China, wakatia silaha, magari, sijui nini. Makomred usiwatowe kabisa. Kwa sababu ni watu wanojulikana…

Kabla ya yote ni kuweza kukaa kukusudia kwenda Zanzibar kwa kufanya mapinduzi ilibidi tufanye mambo ya jadi ya kuweza kula amini kiapo kikubwa ambapo ukiweza kukikosea kiweze kukudhuru. Kwa hivyo tulifanya kiapo kwa kukubaliana atakayevujisha siri basi ina maana aone nyungu impige, kiapo cha nyungu, cha jadi ya mila ya Kidigo, ya Kisambaa, ya Kiziguwa.

Kwa hivyo tukafanya kiapo hicho kwa pamoja na kikundi chote kiliopo pale mstari wa mbele kwenye mbuga ya Sakura. Kwa hivyo hakuthubutu mtu yoyote kuweza kujuwa.

Nyungu inakuwa hichi chungu cha kupikia, lakini kinakuwa bado hakijapikiwa, safi, hakina kitu ndani, pasipokuwa ni kunuwia, kinakamatwa na watu wawili, watatu, wane, kwa sauti moja, kwa yule mwenzake huyu amkamata huyu amkamata huyu, basi inakuwa kashiriki pale, kwa hivyo hiyo siri imefanyika bila kutangaa. Halafu kinaangushwa chini. Kikivunjika bas, kinaokotwa vigae vile kinatupwa.

Ukivujisha, ukiumwa, safari tu unakwenda. Ukiumwa kidole unakwenda, ukiumwa kichwa unakwenda, ukiumwa tumbo unakwenda. Ilimradi kitakachokuuma ndio mauti yako. Nyungu kazi yake. Nayo inaeleweka.

Watu sita pamoja na wengine kushika mashati na nini, ili wote ni kama wamekishika. Wote jumla kama ni ishirini.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: