Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!

Icon

Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia

Shukrani

Kwanza kabisa kuliko yote au yoyote, sina budi kumsujudiya na kumshukuru Mwenye Enzi Mungu kwa Rehma zake na kwa kunionyesha njia ndani ya midani ya utafiti ambayo haikuwa na alama rahisi za kupitwa na iliyokuwa imewekewa ngazi yenye kuelekeya kunako mlango wa jiwe uliyofungwa.

Baada ya Mwenye Enzi Mungu sina budi kuwashukuru kwa dhati kabisa wazee wote wa simulizi za Mapinduzi ya Zanzibar waliyomo ndani ya kitabu hichi. Bila ya Mungu kuwawezesha sio tu kitabu hichi kisingelikuwepo, bali mtazamo mpya wa wananchi wengi wa kawaida, wanasiasa, wasomi na watafiti wa pande zote mbili za Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, na hata waliyoko nje, ungelikosekana.

Kama Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 yalikuwa ni Mapinduzi ya mfarakano wa kijamii, basi nawashukuru wazee kwa kuuweka msingi wa mapinduzi ya mfungamano utakayoipa Zanzibar na Tanganyika mabega makubwa ya kusimamiya pamoja na kutambulikana na kuungwa mkono na madola yenye kupenda demokrasia na amani duniani.

Simulizi za wazee wa Mapinduzi ni mchango na changamoto muhimu sana kwa wasomi waliyobobeya wa nchi mbili za Muungano ambao wana jukumu la kuwafikishiya Wazanzibari na Watanganyika ujumbe utakaohifadhi utulivu wa kijamii na wa kisiasa ndani ya nchi mbili zilizoungana—Zanzibar na Tanganyika. Moja wapo wa ujumbe huo ni kuutambuwa na kuuhifadhi uhuru wa Zanzibar ulioupata tarehe 10 Disemba, 1963 na ndiwo uliyoipa Zanzibar nafasi ya kukubaliwa kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa (UNO). Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964, yasingeliweza kuja bila ya Uhuru wa tarehe 10 Disemba, 1963. Kwa hilo natowa shukurani zisizokuwa na mwisho kwa wazee wa simulizi za Mapinduzi.

Ni jambo la kumshukuru Mungu kuwa Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete umeweza kujenga utamaduni wa amani na utulivu kwa kutowa mvuto kwa kizazi kipya cha uongozi wa Tanzania. Ndani ya kipindi chake cha uongozi wa Urais wa Jamhuri ya Muungano Zanzibar imekuwa shwari kwa sababu yuko upande wa umoja na amani ya Wazanzibari.

Zanzibar piya imebahatika kuwapata viongozi wawili majasiri, Mheshimiwa Rais Amani Abeid Karume na Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad ambao wameamuwa kwa pamoja kutorudi nyuma katika kazi ya kujenga mazingira ya kuizaa Zanzibar Mpya. Yote hayo yanafaa kushukuriwa na ndiyo msingi utakaokuja kuujenga Muungano imara, ilimu bora na uchumi endelevu kwa tabaka kubwa la wananchi walio wengi.

Napenda kuwashukuru kwa dhati yangu marehemu wazazi wangu wawili ambao wamenileya na kunipa furaha ya utotoni ambayo ndiyo yenye kunipa utulivu na furaha ya moyo popote pale nilipo. Nilipokuwa bado niko Cairo masomoni, marehemu mama yangu, Bibi Asya Abdalla Jahadhmy, aliniandikiya barua na kunielezeya ndoto aliyoiyota na iliyoifananisha Zanzibar na mtu aliyekuwa ndani ya pango lenye giza totoro na nje limezungukwa na mwangaza mkubwa. Mapenzi yangu ya utotoni juu ya Zanzibar na Tanga pamoja na ndoto ya marehemu mama yangu ni moja kati ya motisha kubwa kwangu katika kuufanya na kuufanikisha utafiti huu.

Marehemu baba yangu, Bwana Mohamed Abdalla Ghassany, maarufu “Bingwa” wa kilimo na ufugaji, alikuwa na mapenzi makubwa juu ya Zanzibar na aliwahishimu sana watu wake. Baina ya ndoto ya marehemu mama yangu na mapenzi ya marehemu baba yangu juu ya Zanzibar, na sababu nyenginezo, ndipo nilipoingiwa na shauku ya kuutafuta ukweli wa Mapinduzi. Kabla ya hapo nilikuwa ni mmoja wa majeruhi ya upotoshaji wa historia na niliyaamini mengi ambaye leo najuwa kuwa hayakuwa na ukweli wowote.

Sina budi kuishukuru Dola ya Zanzibar chini ya uongozi wa Mzee Abeid Amani Karume, na khasa walimu wangu, kwa kunipa ilimu ya bure kutokeya ya msingi mpaka ya sekondari. Sio kuwa nilizaliwa tu na kulelewa Zanzibar bali tone la maji la Zanzibar ndilo lililonitiya kiu ya kutaka kuliangaza pango la saikolojiya ambalo limekuwa likiwanyima furaha ndugu zangu wengi kutoka Zanzibar. Hakuna ambaye hakuumiya Zanzibar na hakuna ambaye atashindwa kushukuru kwa fursa ambazo Zanzibar imetowa kwa watu wake. Msemo wa kheri imo ndani ya tumbo la shari ni msemo wenye kumgusa kila Mzanzibari na kila binaadamu aliyekuwa hai katika dunia hii.

Bado nakumbuka wakati nilipokuwa mtoto mdogo nimesimama mbele ya sinema ya Majestic iliyopo Zanzibar na kufadhaishwa na mgongano wa kiakili baina ya Wazanzibari wenye asili ya Kiarabu waliyokuwa wamevaa nguo za kuvutiya za kijeshi, bastola kiunoni na bunduki mikononi, na mimi kuikamata kalamu na kujibu masuali kuhusu somo la utumwa wa Waarabu darasani skuli ya Tumekuja. Suala langu lilikuwa, kama Waarabu wanachukiwa na wanachukiza mbona Makomred walikuwa mstari wa mbele Zanzibar?

Napenda kutowa shukurani zangu za dhati kwa Dola ya Oman chini ya uongozi wa busara wa Sultan Qaboos bin Said Al Said, kwa kukipokeya kizazi cha mashujaa wa KiOmani kilichotowa na kinachoendeleya kutowa mchango mkubwa katika kuikombowa, kuweka amani, na kuijenga Afrika Mashariki na Kati. Tumeweza chini ya uongozi wake kukutana na watu wetu na kufunguliwa milango ya kheri na fursa zisizokuwa na mwisho, na kwangu binafsi kwa kuipa familia yangu fursa zisizokuwa na idadi na watoto wenye kuinukiya ndani ya mazingira yaliyotuliya. Yote hayo yasingeliwezekana kufanyika bila ya hikma na mtazamo wenye kuona mbali wa Sultan Qaboos bin Said. Tunamuombeya dua Mwenye Enzi Mungu amzidishiye nguvu katika kuendeleya kuwaongoza watu wa Oman kwa ruu’ya yenye kuongozwa na umoja wa ndani wa nchi wa raia zake na urafiki na nchi jirani na za mbali—Amin.

Shukurani maalumu zinakwenda kwa Profesa Kelly M. Askew ambaye ni mshiriki mwenzangu katika kuandika kwa pamoja pendekezo la utafiti huu uliyoweza kutupatiya msaada wa kifedha wa awali uliyonidhihirishiya umuhimu wa kufanya utafiti mkubwa zaidi baada ya mwaka 2004. Kwa niaba ya Kelly na yangu, nalishukuru shirika la Kimarekani la Wenner-Gren Foundation for Anthropological Research liliyopo jijini New York, Marekani, kwa msaada wao muhimu na wa awali. Kelly, ahsante sana kwa urafiki na ushirikiyano wako kwenye utafiti huu na kwa kunijuulisha na mtandao wa mapinduzi ya uchapishaji wa Lulu.com. Ahsante sana sana Kelly.

Walimu wangu hayati Maprofesa Archie Mafeje na Cynthia Nelson wa Chuo Kikuu cha Kimarekani kiliyopo Cairo–Egypt, wamechangiya sehemu kubwa katika mafanikio ya masomo yangu. Hayati Profesa Roy Rappaport wa Chuo Kikuu cha Michigan, Ann Arbor, alikuwa mtu karimu na mwepesi wa kunikaribisha ofisini na nyumbani wake. Pia nilipokuwa masomoni Ann Arbor, nilibahatika kuhudhuriya mihadhara ya baba wa “theolojiya ya ukombozi ya Kikristo” Gustavo Guiterrez; na baba wa “Afrabia” Profesa Ali A. Mazrui.

Guiterrez alinifanya nimfahamu zaidi Yesu Kristo na khasa jinsi mchungaji Bartolome de Las Casas wa karne ya kumi na sita alivyopinga utesaji na mauwaji ya halaiki ya wenyeji Wahindi Wekundu uliyofanywa na wakoloni kutoka Spain. Niliwafahamu kutoka kwa Guiterrez na baadaye kutoka kwa Profesa Harvey Cox, Jr., akina Dietrich Bonhoeffer, Leonardo Boff, na wakombozi wengineo wa Kikristo kuwa ujumbe wa Kristo Yesu/Issa mtoto wa Bibi Maryam, ni ujumbe wa kiukombozi wenye lengo la kuleta amani duniani na haukubaliyani kabisa na vitendo vya utumiaji nguvu, mauwaji au ukandamizaji wa binaadamu wengine kwa jina la dini. Namshukuru sana Mzee Guiterrez kwa kunifunuwa macho na kunifanya niufahamu uwezo wa tafsiri ya kiukombozi ya Ukristo katika kumuinuwa binaadamu kutokana na ufakiri na kudumisha amani ulimwenguni.

Juu ya yote, milango ya utafiti huu kabisa isingeliweza kufunguka bila ya Dkt. Ramadhani Kitwana Dau kunijuulisha na wazee ambao majina yao wameomba yahifadhiwe, pamoja na kunijuulisha na mwandishi Bwana Mohamed Said.

Nilijuwana na Ramadhani tulipokuwa wanafunzi American University in Cairo (AUC) na sidhani kama tungeliweza kutambuwa kama kuna siku njiya zetu zitakutana na atanielekeza kwa wazee ambao ishara na mafumbo yao yalikuwa ni dira iliyoniongoza kunako njiya na matokeo ya utafiti huu.

Si Ramadhani, wala Mohamed, wala mimi mwenyewe, tungeliweza kutambuwa wakati ule kama ishara nilizopewa na wazee waliyonijuulisha nao zingeliweza kumalizikiya katika sura ya kitabu hichi. Mohamed ndiye aliyenijuulisha na Mzee Mkwawa na tulikwenda pamoja kuizuru mbuga ya Sakura na kijiji cha Kipumbwi kwa mara ya kwanza. Hiyo ilikuwa ni ishara ya pili iliyonifahamisha kuwa njiya ya Mapinduzi ya Zanzibar iko Tanganyika na kuyatafuta Mapinduzi ndani ya vichochoro vya Mji Mkongwe wa Zanzibar itakuwa ni kupotezana njia.

Ishara ya kwanza nilipewa na marehemu Mzee Hamza Azizi aliyekuwa Inspector General of Police (IGP) wa Tanganyika wakati wa mapinduzi ya Zanzibar. Mzee Aziz hakuwacha kuirudiya kauli yake ya kunipa moyo “Endelea kutafuta, usichoke; na hapa kwangu unakaribishwa tena na tena.” Piya alinidokoleya kuwa nitafaidika na ripoti ya Shirika la Ujasusi la Kimarekani (CIA) ambayo yeye alipata kuiona alipokuwa Balozi wa Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Canada. Bahati nzuri au mbaya niliipata ripoti hiyo mwishoni mwa utafiti wangu. Lakini mpaka kufariki kwake dunia, Mzee Hamza Aziz alifika kukubali kuzungumza na mimi lakini kwa ishara na mafumbo, tena nje ya nyumba yake! Khofu yake ilijieleza pale aliponiambiya kuwa “sisi tulikula kiapo kuhusu hili suala la Mapinduzi na ni kikundi cha watu wachache sana wanaoufahamu undani khasa wa Mapinduzi ya Zanzibar.”

Aliponielezeya Mzee Hamza Azizi kuwa mapinduzi ya Zanzibar yalizungumzwa katika nchi fulani ya Kiarabu wakati ujumbe wa Mwalimu Nyerere ulipoizuru nchi hiyo nilimuuliza “Ni Algeria?” Mzee Hamza alinijibu “umesema wewe!” Ishara kubwa aliyonipa Mzee Hamza ni pale aliponigutuwa kimafumbo kuwa itabidi kwanza niamuwe kama Mapinduzi ya Zanzibar yaliandaliwa Zanzibar au Tanganyika.

Napenda kumshukuru Mzee Abbas ambaye alinionesha anachokijuwa kwa kunitaka nikamate simu nyengine ya nyumbani kwake ili nisikilize simulizi za kiongozi na rafiki yake mpenzi huku yeye akizungumza kwenye simu iliyoko chini ukumbini kwake. Balozi Abdul Faraji ambaye alihusika na kuandaa chombo kilichowarudisha Zanzibar baadhi ya viongozi wa Afro-Shirazi kama Mzee Abeid Amani Karume na kiongozi wa chama cha Umma marehemu Abdulrahman Babu, aliamua kunihoji mimi kwanza kabla ya kumuuliza masuala yangu. Khofu zao zilikuwa ni ishara njema kwangu, kwa Zanzibar na kwa Tanganyika. Nilifahamu moja kwa moja kuwa wazee wa TANU wa Tanganyika walikuwa wana kitu wamekificha kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar kwa sababu walifahamu kuwa waliivamiya nchi ya watu na waliloifanyiya Zanzibar lilikuwa ni kosa la jinai la kimataifa. Nilikumbushwa na Profesa Ibrahim Noor Shariff, kuwa msomi mmoja maarufu duniani alipata kusema kuwa hayati Mwalimu Nyerere alikuwa tayari kuzipeleka nchi zote zilizoulisha raia wasiokuwa na makosa kwenye mahakama ya Arusha isipokuwa Tanganyika! Niliwahakikishiya wazee kuwa lengo langu ni kuiweka sawa historia na kuwa wana uhuru kamili wa kukubali au kukataa kuzungumza na mimi au kusajiliwa, au kuzungumza na kusajiliwa, kwa kuyataja au bila ya kuyataja majina yao ya kweli au kamili. Kwa waliyoniomba nisiyataje majina yao kwenye uhai wao nimeyahishimu matakwa yao na kwa hiyo sikuwataja. Waliyokubali nimeyataja majina yao kwa ukamilifu na wengine pamoja na picha zao.

Kuna kigogo kilosema wazi kuwa ana afadhali afe amenyooka na jeneza lake limevalishwa bendera na apigiwe wimbo wa taifa kuliko kunipa anayoyajuwa kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar na khasa kwa kujuwa kuwa anayetawala sasa Zanzibar ni mtoto wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Mzee Abeid Amani Karume. Kwa nini watu wa nchi nyingine waliogope jambo la ufakhari la kuiokombowa nchi jirani isipokuwa wanajuwa na wanaogopa kuwa hawakuitendeya haki nchi jirani?

Anaelezeya mzee mwengine ambaye jina nimelihifadhi: “Father K hakuweza kujidai kuwa anayajuwa mapinduzi na walokuwa wanayajuwa hawakuweza kujionyesha kuwa alikuwa hayajuwi. Karume alikuwa ni Mungu-mtu ambaye alifanya maamuzi yake kupitia Baraza la Mapinduzi (BLM). Alikuwa hawaheshimu hata mmoja katika BLM na aliwafanya wajue hivo. Karume alikuwa ni bingwa wa ‘bush politics’; tafauti baina ya kuwa na akili na kuwa na maarifa. Karume alikuwa ana kipaji cha kuzaliwa cha kujuwa hatari iko wapi na hisia kali ya kujilinda.”

Bwana Said Suleiman Al-Behlani ambaye aliishi sana Bagamoyo alinielezeya nilipomtembeleya nyumbani kwake Maskati jinsi siku moja manahodha wawili, Nakoma na Buguma walivyogombana pale Bagamoyo na Nakoma akamtukana Buguma na kumwambiya kuwa “wewe mnyama vipi unakula kwa Waarabu wakati wewe ulikuwa ukinijiya usiku nipeleke silaha Zanzibar? Mimi nilikuwa nikiogopa nisiuwawe tu lakini wewe si mtu”.

Kila alokuwa ana khofu alikuwa na khofu kuwa fulani yuhai na akisikiya nimeitobowa siri ya Mapinduzi nitakuwa nimejiweka pabaya. Kinyume na Shahrazade wa kitabu maarufu cha Alfu Lela U-Lela ambaye aliendeleya kumtoleya hadithi Sultan Shaharia mpaka saa za asubuhi kukimbiya kifo, wazee wa Mapinduzi wanaangaliya nani yuhai na nani kafa kabla ya kuamuwa kuyatowa walioyavumbika kwa miaka mingi. Kila anapokufa kiongozi wa Mapinduzi ndipo wazee walio hai hutokwa na khofu ya kuueleza ukweli wa Mapinduzi.

Wazee wengi walitokwa na khofu kwa kujuwa kuwa hayati Mwalimu Nyerere hayupo tena duniani lakini wengine bado wana khofu kwa kujuwa kuna viongozi wakongwe ambao bado wako hai. Baada ya kumuambiya Mzee Victor Mkello kuwa wanamapinduzi wengi wameshatanguliya kwenye haki, alinikumbusha kuwa Mzee Rashidi Kawawa bado yuhai na kwa nini sijazungumza naye? Sikutaka kumpa sababu zangu lakini niliyakumbuka maneno ya marehemu Mzee Hamza Aziz kuwa “atakachokuambia Kawawa take it with a spoon of salt.” Yaani juu ya kuwa ataelezeya na yasiokuwa sahihi pia.

Kwa upande wa Zanzibar napenda kumshukuru jamaa yangu Ali Saidi Al-Kittani kwa kunijuulisha na katibu wa Mapinduzi ya Zanzibar, Mzee Aboud “Mmasai.” Pia napenda kuwashukuru marehemu Ali Omar [Lumumba] wa Weles, Zanzibar, pamoja na marehemu Mzee Othman “Bapa”. Wazee wawili hawa walinisaidiya sana kwa kunijuulisha na wazee wengine ambao waliifahamu historia ya Mapinduzi ingawa kulikuwa na vipengee ambavyo hata wao walikuwa wanagenzi.

Mzee wangu na mwandishi Bwana Issa Nassor Al-Ismaili ametumiya wakati wake thamini na hikma zake za umri mrefu kunishauri nijaribu kadri nitakavyoweza niandike kwa kuungwa mkono na ushahidi na si kwa maneno yangu mwenyewe peke yake. Bwana Issa pia aliwahi kunihadithiya kuwa safari moja katika mazungumzo yeke na marehemu Abdulwahid Sykes, Bwana Abdu alipata kumuambiya kuwa “Bora tusiyazungumze mambo ya Zanzibar kwa sababu tukiyazungumza urafiki wetu utavunjika.” Kwa wengine kutoyazungumza Mapinduzi ya Zanzibar ilikuwa ni ishara ya kuyajuwa mengi ambayo yanatowa taswira mbaya kwao.

Namshukuru sana Profesa Ibrahim Noor Shariff kwa kuniruhusu kuitumiya picha iliyoko mbele ya gamba la kitabu aliyoichora mwaka 1960 wakati bado ni mwanafunzi wa shule ya sekondari. Kitabu chake Tungo Zetu kilizidi kunifunguwa macho kuhusu khabari kutoka Uswahilini na vita dhidi ya Waswahili, Waarabu, na baadaye Washirazi kwa kutumiliwa garasa la utumwa. Profesa Ibrahim aliwahi kunipa ushauri ambao zitoweza kuusahau pale aliponiambiya kuwa utaweza kuandika kwa lugha ya Kiswahili bila ya kutumiya maneno mengi ya Kiingereza ikiwa utakumbuka namna gani utasema Kiswahili na Bibi yako asiyejuwa Kiingereza!

Napenda kuwashukuru Susan Brandt kwa kulichora gamba la kitabu, Sherif Wahdan kwa kunisikiliza na kunishauri mengi ambayo sikuwa na hakika nayo. Huwayda, mtoto wa marehemu Bwana Nassor Abdalla Al-Shahimi, maarufu “Mlawwaz” ametowa mchango wa kifikra juu ya utangazaji wa kitabu, na Profesa Benjamin W. Fortson kwa kuuandaa muswada wa kitabu na kuuweka tayari kwa uchapishaji. Pia napenda kumshukuru Aziz Al Harrasi kwa kunisaidiya kulitengeneza jopo la kitabu katika facebook na mtandao wa kukipokeya kitabu.

Nimekuwa na mawasiliyano ya miaka mingi na Ismail Jussa na hivi karibuni amekuwa akisisitiza sana juu ya umuhimu wa kupatikana uongozi mpya Zanzibar ambao unatokana na viongozi wa CUF na CCM watakaosukumwa na umma uliyozindukana kuziongoza na kuzijenga Zanzibar na Tanganyika ambazo ni huru, zenye demokrasia ya kweli, ustahmilivu, na zenye amani na neema za kiuchumi kwa wote. Fikra zetu zimekuwa zikikutana kwenye imani kuwa kuusitisha mtikisiko wa nyumba ya Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar utategemeya sana kuunga mkono mpigo mpya wa moyo wa Zanzibar. Ahsante sana Al Habib.

Nimebahatika kukaa na kumsikiliza kwa muda marefu Muhammed Ahmed Sultan Mugheiry (Eddy Riamy). Eddy amekuwa akisisitiza tena na tena na kuchoka kunukuliwa kuwa Zanzibar inahitajiya chama kimoja tu cha kisiasa ambacho si CCM wala si CUF bali chama kimoja cha Uzanzibari na cha Wazanzibari wenye uaminifu na kuaminiyana. Amenitanabahisha juu ya umuhimu wa kujitenga na mirengo ya kisiasa ya Zanzibar na kuukamata mtitiriko wa historia ya uzalendo wa Kizanzibari. Ahsante sana Eddy kwa kuniongoza kwenye bahari ya uzalendo na matukiyo ambayo hayamo kwenye vitabu au hata katika maelezo yaliyoandikwa chini katika ukurasa.

Napenda pia kumshukuru Mohammed Khelef Ghassany, ambaye amechangiya sana katika kulijenga jukwaa la mawasiliyano kati ya Zanzibar na ulimwengu kupitiya mtazamo na msimamo wake usiyotetereka. Khalid Said Suleiman (Gwiji) maisha amekuwa akisisitiza juu ya umuhimu wa kizazi kipya kujiilimisha na kuuilimisha umma juu ya historia ya Zanzibar ambayo haikupotoshwa. Kizazi kipya cha Kizanzibari hakina kumbukumbu ya Mapinduzi na daima kimekuwa kikiomba wakati ufike wakifahamu kiini cha fitina zisizokwisha. Historia mliyokuwa mkiitafuta ndiyo hii hapa. Sasa kazi kwenu.

Undani wa Mapinduzi ya Zanzibar ulikuwa umefunikwa kwa muda mrefu na ikawa si rahisi kuufikiya kwa kukosekana utulivu na fursa za kufanya utafiti. Utulivu na fursa nilizozipata katika kufanikisha zisingelikuwepo bila ya wema mkubwa kutoka kwa upande wangu wa baba na khasa kutoka kwa marehemu Ami yangu Omar Abdalla Ghassany na mwanawe Rashid Omar Ghassany, marehemu Bwana Nassor Abdalla Nassor (maarufu “Mlawwaz”) na mke wake Anti Bishara Yahya, marehemu Ami Hamdan bin Ali Al-Abri, na ndugu zangu Abdullah Ahmed Abdullah Ghassany, Thurayya Mohammed Abdalla Ghassany, Dada Hinda Ahmed Ghassany, Ahmed Seif Msellem Al-Rawahi, Ami Harub Sheikhan Ghassany, na Shangazi langu Bibi Zayyana bint Ali Al-Abriyya na ukoo wangu wote kutoka Mwera Magayani, Zanzibar.

Kila Jumaapili jioni marehemu baba yangu alipokuwa akija kunichukuwa mimi na ndugu yangu wa kike kutoka Mwembetanga kurudi nyumbani mjini, marehemu bibi yangu mpenzi mzaa baba na mlezi wangu, Bibi Sarah bint Ahmed bin Muhammed Al Barwani Awlad Hijji alikuwa akituimbiya nyimbo ifuatayo ya kutuaga “Mbweyu mbweyu, indendi kuranga indendi mwanja, aruuu!” Sikuwa nikiifahamu maana ya nyimbo hiyo lakini nilifahamu kuwa nimezaliwa na kulelewa kuuhishimu ubora wa tamaduni za Kiarabu na za Kiafrika.

Daima nitamkumbuka marehemu bin ami yangu, Farid Ahmed Abdalla Ghassany ambaye tulifunga urafiki mkubwa kutokeya aliporudi kutoka msitu wa Ngezi, Pemba, alikokuwa akiishi na marehemu baba yake na ami yangu, Bwana Ahmed Abdullah Ghassany. Marahemu Farid alinifundisha kutembeya shingo juu na kutokubali kuonewa au kuanzisha ugomvi na mtu.

Sina shukurani za kutosha kwa Shangazi langu Bibi Khadija Abdalla Jahadhmy ambaye alikuwa mstari wa mbele katika maamuzi yote makubwa yaliyochangiya katika kunileteya mafanikiyo katika maisha yangu. Sina cha kuwalipa ndugu zangu Dr. Saadia Amour Sultan Al-Riyami na mumewe Sheikh Abdullah Hamoud Al-Riyami, Da Fatma Ali Jahadhmy/Trudeau, Dr. Abdullah Amour Al-Riyami, Mohammed Ali Al-Barwani, kwa kunipokeya, kunitazama, kuniongoza, na kwa kunipa msingi mzuri wa kimaisha.

Balozi Bwana Nassor Seif Al-Buali na mkewe Bibi Sharifa (Da Hobo) Mohammed Nassor Al-Lamki ni wazee ambao sitoweza kuusahau wema wao katika maisha yangu na katika uhai wangu hapa duniani. Ni Mwenye Enzi Mungu peke yake mwenye uwezo wa kuwalipa ihsani zao.

Na mwisho, napenda kumshukuru kwa dhati mke wangu, Asya Mohammed Suleiman Al-Lamki, nguzo madhubuti ya hikma na upole, kwa kusimama na mimi katika mambo yote muhimu katika maisha yangu. Asya ni shifaa na ni muongozo uliyotuliya na wenye kutuliza. Siwezi kumsahau shemegi na ndugu yangu, Fatma Mohammed Suleiman Al-Lamki kwa kusimama na familia yangu katika kila hali na kutuondoleya kila vikwazo katika maisha yetu, na mumewe, mwingi wa uungwana na ushauri wa busara, Sheikh Ali Mohammed Said Al-Busaidi.

Ni shauku na matamaniyo yangu kuwaona watoto wangu Aisha, Fatma, Ghassan, na Sarah, na kizazi kipya kilicho kama chao kwa jumla, wanayaendeleza mapenzi na wajibu wao kwa Zanzibar na Oman na kwa niya ya kudumisha amani na maendeleo, na kuzipenda lugha na turathi zao nzuri za Kiarabu na za Kiafrika, na za kutoka nchi za Magharibi. Wazee wangu, mke na watoto wangu na ndugu zangu niliyowataja hapo juu hawahusiki hata kidogo na utafiti au yaliyomo ndani ya kitabu hichi.

Piya napenda kuwashukuru wahafidhina wa Kizanzibari na wa Kitanganyika wasiopendeleya mashirikiano baina ya Wazanzibari na hata wale ambao wanataka milele Waarabu na khasa wakikusudiwa Waislam, wasisikilizane na waliyoko kusini ya Bara la Afrika, kwa kujitokeza kwa hoja na sera zao. Iwapo hoja zao ni za kitaalamu na hazina chuki basi watashukuriwa kwa kuuongoza mjadala utakaojenga usalama na mustakbal mwema kwa Wazanzibari.

La, wataendeleya kupinga kwa misingi ya khofu zinazotokana na chuki na fitina, piya wataonekana kwa niya na vitendo vyenye kupendeleya fitina na mitafaruku badala ya umoja baina ya Wazanzibari, baina ya Wazanzibari na Watanganyika, na baina ya Waafrika na Waarabu. Vyoyote itakavyokuwa, kheri hutoka ndani ya tumbo la shari na kheri na si shari ndiyo yenye kudumu na yenye uhakika wa kuwepo.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: