Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!

Icon

Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia

Tanbihi

Kutanabahisha

Fikra na maelezo yaliyomo ndani ya kitabu hichi hazina uhusiano wa aina yoyote ile na Serikali, misimamo au sera za vyama vya siasa. Ni kitabu chenye kukusanya simulizi za wazee zenye kuungwa mkono na ushahidi kutoka nyaraka za kimataifa wenye kuufunuwa upotoshaji na kuukombowa utumwa wa kiakili ambao umekuwa ukitumika kwa nusu karne nzima kuipumbazisha na kuinyima usingizi na utulivu Zanzibar na Tanganyika—Tanzania.

Kudhihirika kwa ilimu iliyofichwa huenda ikawa sababu ya kuwaingiza wengi kati ya wasomaji katika harakati mpya na kubwa zaidi kutoka historia na siasa kuelekeya kunako ilimu ya maadili (ethics) na kutoka kwenye nafsi iliyotupwa gizani kuelekeya kunako nafsi iliyo huru, itakayoongeza nuru na utulivu Afrika Mashariki na Kati. Si lengo la kitabu kukusanya yote yenye kujulikana au yasiyojulikana kuhusu mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 na kuusimamisha “ukweli halisi” wa tukio hilo. Kufanya hivyo itakuwa ni sawa na kuusimamisha “ukweli” mpaka atakapotokeya mtafiti mwengine atakayekusanya taarifa nyingi zaidi na kutunga “ukweli halisi mpya” mwengine wa mapinduzi.1

Yaliyomo ndani ya kitabu hichi ni asilimia ndogo sana ya yale ambayo yanaweza kutolewa kuhusu mapinduzi ya Zanzibar na muungano na Tanganyika ndani ya wakati tulionawo. Lengo la kitabu ni kukusanya maelezo na tafsiri mbalimbali za mapinduzi ya Zanzibar na vipi yanavyotumika hii leo, kwa kufahamu au kwa kutokufahamu, katika kuinyima Zanzibar na Tanganyika milango na madirisha ya kutoka ndani ya mnaso ambao unaonekana kuhatarisha mustakbal wa nyumba ya Tanzania.

Kwa hiyo na kwa upande muhimu, maudhui ya kitabu si upotoshaji wa historia ya mapinduzi ya 64 bali vipi upotoshaji wa historia hiyo unavyotumika ndani ya mkwamo wa wakati tuliyonao hivi sasa na vipi maelezo na tafsiri mpya ya tukio hilo itaweza kutusaidiya kutuongoza nje ya matatizo ya Muungano baina ya Zanzibar na Tanganyika.

Mtizamo wa kitabu ni tafauti na mitizamo ya maandishi mingi sana yaliyoandikwa kabla kuhusu mapinduzi ya Zanzibar. Msomaji hatojikuta amenasishwa kutokeya mwanzo ndani ya mtego wa gurudumu la historia lenye kuiweka mbele na kuisukuma biashara ya utumwa kama ndiyo sababu kuu ya mapinduzi ya Zanzibar.

Lengo ni kuyapiga tochi mapinduzi ya Zanzibar ndani ya pango la upotoshaji kwa kuizingatiya mipango na sababu halisi za mapinduzi badala ya kuzidhoofisha nguvu za akili za wasomaji kwa kuwapumbaza kwa visingiziyo na ubunifu wa sababu za mapinduzi. Ni vyema msomaji akayaweka kando mifuniko ya macho ya historia kabla ya mapinduzi na kujaribu kuyafahamu mapinduzi kwa mujibu wa mazingira na vikomo vyake wenyewe. Ni kweli kuwa historia ya kabla ya mapinduzi itakuwa ina mchango fulani lakini tathmini hiyo ni ya kuja baada ya kukusanya maalumati na tafsiri sahihi kutoka kwa wahusika sahihi wa mapinduzi hayo.

Kwa kifupi na kwa kukariri, msomaji anatakiwa auweke kando uzowefu wenye kuihusisha biashara ovu ya utumwa na matabaka ya kiuchumi kama ni bashraf ya taarab ya mapinduzi ya Zanzibar. Maelezo yasiyokuwa na uthibitisho wa kiutafiti na yenye kuongozwa na chuki dhidi ya watu fulani na wenye kufuata dini fulani, huwa yamesimama juu ya msingi wa nadhariya ya uchokozi (provocation thesis) ambayo lengo na udhaifu wake mkubwa ni kuvidharau vitendo vya wahusika halisi wa mapinduzi ambao wanatoka kunako dini zote.

Lengo la kitabu ni ushindi dhidi ya ukataaji wa kuyafahamu mapinduzi kwa mujibu wa vitendo na sababu halisi za tukio lenyewe. Kila taifa lina fitina yake na fitina ya Dola ya Zanzibar ni utumwa. Fitina hizo ambazo wahubiri wake wa Kanisa la Anglikan la Mkunazini, wanasiasa wa Kiisilamu wa jeshi na vikosi vya Zanzibar, au majumba ya makumbusho ya kitaifa yaliyopo Dar es Salaam, au Bagamoyo, huwa haziichafulii tu jina zuri la Zanzibar peke yake bali zaidi huichafuliya jina la dini aliyokuja nayo Kristo Issa (Yesu) mtoto wa Bibi Maryam, na Mtume Muhammad, sala na salamu za Mwenye Enzi Mungu ziwashukiye. Wahubiri hao wanakunywa maji kutoka kisima cha fitina na ufisadi ambacho hakikaukwi na sauti isiyosita yenye kusema kuwa Waarabu wameleta vitu viwili vibaya Afrika: Uislam na utumwa.

Chimbuko la fitina hizo kwanza lilitoka nchi za Ulaya na zinatokana na mrengo maalumu wenye chuki dhidi ya Uislamu na sio ule ambao unaoitambuwa na kuihishimu dini hiyo ambao upo lakini si wenye kujulikana na kupendwa na vyombo vya habari na wasomi.2 Mfano mzuri ni ule wenye kuupa utumwa wa Afrika Magharibi jina la bahari ya Atlantic na ukajulikana duniani kote kwa jina la Atlantic Slave Trade (Utumwa wa Bahari ya Atlantic), na si utumwa wa Wazungu Wakristo. Kinyume chake, utumwa wa Afrika Mashariki haukupewa jina la Indian Ocean Slave Trade (Utumwa wa Bahari ya Hindi) na badala yake na mara nyingi hubatizwa jina la “Utumwa wa Waarabu/Waislam.”

Fitina ya utumwa juu ya nchi ya Zanzibar si jambo ambalo linahusishwa na Dola ya Zanzibar iliyopinduliwa tarehe 12 Januari 1964 peke yake. Fitina ya utumwa ni moja kati ya visingiziyo vya ukoloni wa mtawala mweusi kutoka Tanganyika kuiondoleya Zanzibar kiti chake Umoja wa Mataifa na bega la kuliliya duniani. Na si kweli kuwa kiundani suala la “utumwa wa Uislam au wa Waarabu” ni suala linalotokana na dini ya Ukristo au ujumbe wa Mtume Issa, mtoto wa Bibi Maryam. Ukristo na Uislam wa Mabwana Issa na Muhammad unasingizwa na unatupiwa lawama chafu kutokana na vitendo vya watu wenye chuki binafsi na wenye kuupenda utukufu wa kidunia.

Suala la utumwa wa Waarabu Waislam limebuniwa na kuvikwa guo la Ukristo na watu ambao lengo lao khasa ni kulinda maslahi yao ya kiuchumi na ya kisiasa kwa kuwafitinisha Waafrika Waislam na Waafrika Wakristo. Lengo lao jengine ni kuhalalisha unyama waliowafanyiya Waafrika kwa kujifanya kuwa wao ndio wakombozi wa Waafrika na wapingaji wakubwa wa utumwa ambao wao au mabwana zao walikuwa ndiyo washiriki wakuu na makatili wakubwa.

Kwa wale ambao wako tayari kujihangaisha na kulifahamu suala la utumwa watafahamu kuwa kuingiya kwa mapinduzi ya viwanda au Industrial Revolution utumwa ulikuwa hauna tena faida duniani kwa sababu ya mfumo mpya wa kibepari ambao ukitegemeya malipo bila ya kuwalisha na kuwahudumiya watumwa. Wazungu hawakuusitisha utumwa duniani kwa sababu waliwapenda Waafrika. Katika kuusitiri ubaya wao na kuyaendeleza maslahi yao ya kiuchumi wakaufanya utumwa wa Afrika Mashariki kuwa ni suala la kurusha nambari yoyote ile ya idadi ya Waafrika waliyotiwa utumwani almuradi ipatikane idadi kubwa ya “biashara ya utumwa wa Uislam”, waufunike ubaya wao, na waendelee na maslahi mapya ya kiuchumi.3

Ilikuwa ni njia ya kuwaondoleya wahusika khasa wa biashara hiyo hisiya ya uovu wa waliowafanyiya mamilioni ya Waafrika ambao ushahidi wa kizazi chao na maovu waliyowafanyia ni jambo ambalo lina ushahidi mzito na wala si wa kubuni. Ili kuugubika uovu wao wamejifanya kuwa wao ndiyo watetezi wakubwa wa Kristo na kuwatupiya Waislam zigo la lawama na fitina za chuki ambazo athari zake ni mauwaji ya halaiki na mateso makubwa na maovu zaidi hata kuliko yale waliyokusudiya kumtendeya Kristo. Kwa nini ikawa hivyo wakati Ukristo ulianza miaka mia sita kabla ya Uislamu na wakati Qur’an ina aya nyingi sana ambazo zinawaamrisha waumini wa Uislam kuwakombowa watumwa? Kwa nini wafuasi wa dini ya Mitume Issa na Muhammad wafitinishwe wakati ujumbe wao ni kutoka kwa Mungu mmoja na si ujumbe wa wafuasi wa dini fulani dhidi ya wafuasi wa dini nyngine?

Hili wasomaji wa Kiislam na wa Kikristo wanatakiwa walizingatiye sana wasije wakaingizwa na wakaingiya ndani ya mtego wa kuendeleya kuchukiyana. Mapinduzi ya Zanzibar yalipangwa na kufanywa na Wakristo na Waislam waliyotekwa akili na propaganda chafu iliyokilenga Chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP) kuwa ni chama cha Waarabu wenye kutaka kuurudisha utumwa Zanzibar. Chama cha ZNP kilichukiwa na kuwatisha Waingereza kwa sababu kilikuwa kikisema wazi kuwa mkoloni Afrika Mashariki aliingiya kupitiya Zanzibar na atatoka kupitiya Zanzibar na Uislam utaruka kuingiya Afrika Mashariki na Kati kupitiya Zanzibar.4

Kitabu hichi hakina niya ya kukisaidiya au kukiharibiya chama chochote kile cha kisiasa kwa sababu mwandishi haungi mkono chama chochote cha kisiasa au wanasiasa wasiotaka kuutizama na kuongozwa na ukweli. Hichi ni kitabu cha wenye kuomba kuongozwa na ukweli utakaoilinda hishma ya Zanzibar na ya Tanganyika (Tanzania) bila ya lengo la kupata mavuno binafsi ya kisiasa. Kwa hiyo si lengo la kitabu hichi kuwaharibiya wazalendo waaminifu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) au wa Chama cha Wananchi (CUF), au vyama vyengine vya kisiasa, ambao wameshatambuwa kuwa Zanzibar imeingizwa ndani ya makucha ya vyama vingi na chui yuleyule ambaye aliingizwa ndani ya zizi la ngombe la Tanganyika kwanza na baadaye la Zanzibar. Ni moja wapo wa fitina na mkakati mkubwa na wa zamani wa kuwatenganisha Wazanzibari walio wengi.

Hapana shaka wapo wanasiasa wahafidhina ndani ya vyama vikubwa vya kisiasa wenye kufaidika na hali ilivyo Zanzibar na wako tayari kuendeleya na hali hiyo midam matakwa na mapato yao yataendeleya kuhifadhiwa. Kwa mujibu wa hali inavyokwenda Zanzibar na duniani, wanasiasa wenye kuyalinda maslaha yao ya kibinafsi na kuizuwiya Zanzibar kufikiya umoja, huenda wakajajikuta wameondolewa ngazi na kuanguka ndani ya pango la ujanja, ugonganishaji vichwa, na upotoshaji wa maadili ya ukweli na kuaminiyana.

Kutofahamika kwa Mapinduzi ya 1964 na kubomolewa kwa Dola ya Zanzibar kumesababisha Zanzibar kukosa kuungwa mkono na vyombo vya habari pamoja na mataifa yenye kuunga mkono demokrasia ya kweli duniani. Hii ni sababu moja kubwa Zanzibar kukosa bega la kuliliya duniani kutokea 1964 mpaka hii leo. Kukosa kuilimika kwa vyombo vya habari, walimu na wanafunzi, na mataifa jirani na mataifa makubwa na madogo duniani, kumeendeleza kwa muda mrefu sana kukosa kuifahamu Zanzibar na kuisababisha kusota kwa muda mrefu.

Kukosekana kwa ilimu iliyofichwa kunaleta hatari ya kuwapa uwanja wanasiasa waliokata tamaa kusababisha vurugu za makusudi ambazo huenda zikatowa kisingiziyo chengine cha kuvamiwa upya Zanzibar kwa kutangaziwa hali ya hatari, almuradi ubinafsi wao uendelee kunenepa. Kwa upande wa lugha, kitabu hichi kimeandikwa kwa lugha ya Kiswahili ili watumiaji wa lugha hiyo waweze kufahamu namna gani historia ya Zanzibar ilivyopotoshwa na wachangiye kujenga harakati mpya itakayounawirisha umoja baina ya Wazanzibari, baina ya Wazanzibari na Watanganyika, na baina ya Waafrika na Waarabu kwa ujumla.

Tafsiri ya maandishi ambayo marejeo yake ni ya lugha ya Kiingereza au ya Kiarabu imefanywa na mwandishi wa kitabu hichi isipokuwa hotuba ya marehemu Mzee Abeid Amani Karume ya kuukaribisha uhuru wa Zanzibar (kiambatanisho A).

Maandishi ya baadhi ya maneno yaliyomo ndani ya kitabu yameandikwa kufuatana na matamshi ya wazungumzaji waliyonukuliwa. Kwa mfano neno “ndio” limeandikwa “ndo” kama lilivotamkwa na mzungumzaji aliyenukuliwa, lakini alipoliandika mwandishi mwenyewe ametumia neno “ndiyo.” Neno “siku” limeandikwa “sku” kwa mujibu wa matamshi ya mzungumzaji, na kadhalika.

Neno “mapinduzi” limetumika namna mbili tafauti. Namna ya kwanza ni ile inayotumiwa na wanamapinduzi wenyewe, yaani washiriki wakuu wa mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari 1964. Wanamapinduzi wamelitumiya neno “mapinduzi” kumahanisha kuanguka kwa serikali ambayo kwa ufahamu wao haikuwa ikisimamiya haki za Waafrika wa Zanzibar. Mapinduzi hayo yalikuwa mapinduzi ya kutumiya nguvu na ya kumwaga damu—kuuwa. Wengi waliyomo ndani ya kundi hili, na ni kundi ambalo wamo viongozi na wafuasi wa vyama tafauti vya kisiasa, wanaona kuwa muungano ndio wenye kuwafarikisha na kuwafukarisha Wazanzibari na si mapinduzi yaliyouzaa muungano. Wengi pia wanasononeshwa zaidi na dhiki za muungano kuliko upotoshaji wa mapinduzi.

Wako watakaojitiya wenyewe kunako mtego ya ima kwa kujaribu kuyapinga maelezo ya wazee wa mapinduzi yaliyomo kwenye kitabu hichi au kuyanyamaziya kimya na kuyatumiya kuyaonyesha maovu ya muungano. Na wako watakaokuwa kama dagaa kwenye ubavu wa papa. Hata hivyo, baadhi ya waliyomo ndani ya kundi hili wanaamini kuwa muungano ndiwo wenye kuyalinda mapinduzi ya 1964 na si upotoshaji wa mapinduzi wenye kuulinda muungano wenye kutawaliwa na Tanganyika. Kundi hili la kwanza ni kundi muhimu ingawa duara lenye kuyaunganisha matukiyo mawili ya Mapinduzi na Muungano bado halijafunga ndani ya akili zao.

Matumizi ya pili ya neno “mapinduzi” yanatokana na ufahamu mwengine wa tukio la tarehe 12 Januari 1964. Kwa kundi hili, mapinduzi ni tukio la kuvamiwa Zanzibar kutoka nje na kumezwa na Tanganyika tarehe 26 Aprili 1964. Maana ya mapinduzi kwa kundi hili la pili ni namna wanavyotafautisha baina ya Uzanzibari wa waliopinduwa na Uzanzibari wa waliyopinduliwa. Suala kubwa linalolifarikisha kundi hili na lile kundi la mwanzo ni suala la uhalali wa mapinduzi katika kuipinduwa dola halali ya Zanzibar tarehe 12 Januari 1964. Kundi hili halina uwelewa kuwa hata viongozi waliyoitawala Zanzibar baada ya mapinduzi ya 1964 mpaka hii leo wamekuwa wakikabiliwa na suala la kuiteteya Zanzibar na walilikabili bila ya kutetereka na liliwagharimu kwa hata kupoteza maisha yao, uongozi, au afya zao.

Kwa ujumla, Wazanzibari waliyo wengi bado neno “mapinduzi” halina utata kama ulivyo mfumo wa muungano. Hii inatokana na kukosekana kwa ilimu iliyofichwa ambayo ndiyo yenye kukiweka kiungo baina ya mapinduzi na muungano. Kutangaziwa Zanzibar si nchi na kuibuka kwa suala la mafuta kumewaamsha Wazanzibari wengi hata kuliko huko kunyimwa ilimu juu ya historia ya mapinduzi na mahusiyano yake na mapinduzi, na hata kuliko machachari yote ya vyama vya upinzani.

Tanganyika iliupata uhuru wake kutoka kwa Mngereza mwaka 1961 kwa njia ya salama kabisa, na kwa hiyo lazima iweko sababu ya chama cha siasa chenye chimbuko Tanzania Bara kubeba jina la “mapinduzi”. Jee, ingelikuwa si Tanganyika mapinduzi yangelipatikana Zanzibar na baadaye kupatikana Chama cha Mapinduzi Tanzania? Nguvu za mapinduzi ya Zanzibar zilizotokana na mrengo uliyoasi ndani ya ASP na TANU kwa kupitiya Chama cha Wafanyakazi na ndipo kilipokuja kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).5

Inavyoaminika ni kuwa kuundwa kwa CCM kulitokana na niya ya kuzifuta tafauti zilokuwepo huko nyuma baina ya ASP na TANU na kuanzisha mapinduzi yatakayowafanya watu wasimame juu ya kitu kimoja. Ilikuwa ni fikra yenye lengo zuri ingawa lengo lilificha mapinduzi ambayo usiri wake uliwanyima walengwa mapinduzi yaliokusudiwa kufanyika. Mwalimu Julius Nyerere piya alikuwa na fikra ya mapinduzi dhidi ya uhafidhina ndani ya Ukristo na alikuwa akiufuata mrengo wa kiukombozi wa Kikristo ambao una chimbuko lake Marekani ya Kusini wenye kujulikana kwa jina la “liberation theology” (theolojia ya kikristo ya ukombozi).

Kwa hiyo neno “mapinduzi” linaongeza maana zaidi kuliko zile mbili zilizotajwa hapo juu. Na kitabu hichi piya ni aina ya chimbuko jipya la mapinduzi na ni kazi ya mtafiti mwenye niya ya kuusimamisha baadhi ya ukweli ili Zanzibar na Tanganyika, Waafrika na Waarabu, Waislam na Wakristo, wapate kupiga hatuwa zitakazowazidishiya masikilizano, amani na neema kwao na kwa vizazi vya mustakbal wa mbali. Haikuwa jambo rahisi kuyakusanya, kuyaandika, na zaidi, kuyatowa hadharani maelezo ya kitabu hichi bila ya kuzingatiya kwa kina kikubwa faida na khasara zake. Kuna sababu kadhaa zilizonifanya nikiandike kitabu hichi. Moja wapo ni hamu ya muda mrefu ya Wazanzibari wengi wenye kuipenda Zanzibar na wenye kuitakiya umoja na mema. Kuna mengi zaidi ambayo watakuja watu baadaye kuyaeleza na kwa ufasaha mkubwa zaidi.

La msingi ni kutambuwa vipi tafsiri tafauti za mapinduzi za miaka arubaini na sita nyuma zimeweza kutumika kuwaweka Wazanzibari katika hali ya kushindwa kukaa kwa kusafiyana niya kunako meza moja ya umoja na kutambuwa kuwa adui yao mkubwa ni fitina. Adui mkubwa wa Wazanzibari si Tanganyika, wala si Muafrika au Mwarabu, bali ni adui aliyeweza kujificha nyuma ya akili na nafsi za Wazanzibari, Watanganyika, Waafrika na Waarabu. Adui hayuko nje na adui mbaya zaidi ni yule aliyejificha au kufichwa ndani ya nafsi ya binaadamu bila ya mwenyewe kutambuwa na kukubali. La mwisho na la muhimu la kumtanabahisha msomaji ni kuwa kitabu hichi si cha Wazanzibari dhidi ya Watanganyika bali ni cha Wazanzibari na Watanganyika ambao kwa pamoja waliwekwa ndani ya pango la upotoshaji wa historia ya mapinduzi ya Zanzibar.

Hili linafaa likafahamika kwa lengo la kuzidhibiti tuhuma za watakaotaka kujenga chuki binafsi dhidi ya Watanganyika wananchi au hata wanasiasa wasiokuwa na hatiya. Ni muhimu kutafautisha baina ya mtawala na watawala wa Zanzibar na wa Tanganyika waliohusika na maafa ya Zanzibar na ya Tanganyika na wananchi na wanasiasa ambao hawana ilimu au mafunzo kutokana na historia ambayo wengi wao hawaijuwi. Kitabu kitasomwa na kuchipuwa kaumu za aina mbili.

Moja itakuwa ni sawa na ile kaumu ya zama za Nabii Musa na kisa cha ngombe. Watauliza masuala na watapewa jawabu na watauliza masuala zaidi na watajiweka mbali na kila ushahidi utakaowadhihirikiya mbele ya macho yao hata kama baadhi yao pembeni watakiri kuwa yanayozungumzwa yana ukweli ndani yake. Kihistoria kundi hili ni la zamani sana na likiamuwa kuendeleya na fitina na vitendo vya kuwagawa Wazanzibari na kuwagawa Wazanzibari na Watanganyika, watajijengeya mazingira ya kuwajibika na kuwajibishwa na sheria za Zanzibar na/au za Tanganyika au za Mahakama ya Jinai ya Kimataifa, International Criminal Court (ICC).

Kaumu ya pili itakuwa ni ndogo kwa idadi ya watu kuliko ile ya kwanza, na haitopendeleya kuuona Muungano unavunjika na piya haitopendeleya kuuona ukitawaliwa kwa hoja na vitendo vya kikoloni ikiwa ni kutoka kwa wahafidhina wa upande wa Zanzibar, wa Tanganyika, au wa nje ya Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.

Ni matumaini yangu kuwa baada ya kukisoma kitabu hichi Wazanzibari na Watanganyika watachukuwa hatuwa ya kujenga maridhiyano mapya ya kisheriya na ya kikatiba yatakayoujenga msingi mpya na kuuimarisha mustakbal mwema baina ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Harith Ghassany

Washington DC

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: