Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!

Icon

Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia

Utangulizi

Utangulizi

Kutoka nusu ya pili ya karne ya ishirini mpaka kuingiya karne ya ishirini na moja, Zanzibar imekuwa ikisifika kwa mambo matatu yenye umuhimu mkubwa wa kijamii na wa kisiasa: kupatikana kwa uhuru wa Zanzibar tarehe 10 Disemba 1963, kupinduliwa dola huru ya Zanzibar tarehe 12 Januari 1964, na kuungana na Tanganyika tarehe 26 Aprili 1964.

Kitabu hichi kinasajili majadiliyano ambayo hayajapata kutolewa, kwa njia rasmi au zisizokuwa rasmi, na kikundi maalumu cha wazee waliyokuwa wanachama wa Afro-Shirazi Party (ASP) na wa Tanganyika African National Union (TANU) katika kuyafanikisha yale yenye kujulikana rasmi kama ni Mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari 1964. Kitabu piya kinatumiya marejeo ya daraja la kwanza ya kihistoria ambayo ni maandishi ya nyaraka za kitaifa za maofisa waliyoyashuhudiya mapinduzi au waliokuwa karibu sana na waliyoyashuhudiya. Kushuhudiya jambo kuna daraja.

Mchango wa wazee khasa waliyohusika na waliyokuwa mstari wa mbele kwenye Mapinduzi kunaziba pengo kubwa la kihistoria na ni dira na ramani mpya kwa wananchi wa Zanzibar na wa Tanganyika, kwa Wazanzibari waliyoko ughaibuni, na kwa wenye kufuatiliya masuala ya umoja na muungano wa nchi za Kiafrika. Piya ni mchango muhimu baina ya uhusiyano wa Waafrika na Waarabu ambao mwaka 1990 Profesa Ali A. Mazrui aliubatiza jina la Afrabia akimaanisha uhusiyano mkongwe na maalumu baina ya Waafrika na Waarabu na kubashiriya makundi mawili ambayo yamo katika safari ya mfungamano wa kuwa kitu kimoja.6

Zanzibar na Tanganyika, Tanzania, ziko kwenye njiya panda kuelekeya kunako mfungamano na zimekabiliwa na uamuzi mkubwa na wa haraka wa ya imma kuifuwata njiya ya amani na neema au kuifuata njiya ya ghadhabu na yenye kupoteza dira.

Usomaji wa maneno, udadisi wa maana, na uwelekezaji wake kwenye daraja za juu za ufahamu ndizo pekee zenye uwezo wa kutowa makusudiyo na maana ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa Zanzibar, kwa Tanganyika, na kwa mustakbal wa Zanzibar na Tanganyika—Muungano.

Tatizo la Zanzibar, Unguja na Pemba, au la Waafrika Waislam, ni tatizo ambalo lina picha ndogo na picha kubwa. Picha kubwa ni ustaarabu na khasa wa Dola ya Zanzibar ambao ni tishio kwa wale ambao bila ya kutambuwa wamefundishwa na kuamini kuwa wao wana haki zaidi Zanzibar kuliko hata Wazanzibari ambao hawana kwao kwengine isipokuwa Zanzibar.

Na kwanini tatizo likawa na Zanzibar, na si na Tanga, au Mafia, au Kilwa, au Lamu, lakini likawa na Zanzibar na Mwambao wa Kenya? Sababu ni Dola ya Zanzibar ndiyo dola pekee iliyo kongwe (mbali na Ethiopia) kuliko zote Afrika chini ya jangwa la Sahara ambayo iliupata uhuru wake tarehe 10 Disemba 1963. Kuukataa uhuru wa Zanzibar kutoka kwa Muingereza ni kukataa kuwepo kwa Dola ya Zanzibar na ustaarabu wa Waafrika Waislam wa karne juu ya karne. Na ni kuyakataa piya Mapinduzi ya 1964. Mapinduzi yangelikuja kama si uhuru wa Zanzibar wa tarehe 10 Disemba 1963?

Jan P van Bergen wa Uholanzi ameelezeya kwa ufasaha kuwa “Kutokeya ulipoanza, Ukristo umekuwepo kwenye bara la Afrika, Masri, Libya, na Afrika ya Kaskazini, na labda Ethiopia. Lakini hakuna kumbukumbu yoyote katika Zama za Giza (Dark Ages) ya kuingiya kwa Ukristo sehemu za kusini, si kwa kupitiya njiya ya baharini au ya barani. Kuingiya kwa Ukristo Tanzania ni jambo la miaka ya karibuni.”7

Ukifananisha na Afrika Magharibi, kufaulu kwa uenezaji wa Ukristo Afrika Mashariki kulisababishwa na “uhaba wa nguvu za Uislamu, uhaba wa Dola zenye nguvu na zilizojiandaa kuuzuwiya Ukristo, na rukhsa aliyoitowa Sayyid Said wa Zanzibar kwa mamishionari kuanza kufanya kazi zao, ambazo ni kinyume na imani yake ya Kiislamu, na upeo wa kipropaganda wa Livingstone Uingereza na nchi za Ulaya.” 8

Tukirudi nyuma zaidi na katika mwaka kama wa 975, anaelezeya mtafiti Bergen, “wakimbizi wa kidini na wa kisiasa kutokeya Persia na Arabia walianzisha miji midogo katika pwani ya Afrika Mashariki. Miji hiyo baadaye ilikuwa na kuwa miji mikubwa ya kibiashara, na dini kubwa ya ukanda wa pwani ikawa dini ya Kiislam…Kuowana kwa Waarabu, Wafarsi, Washirazi na Waafrika kukazaa kabila la mchanganyiko la Waswahili, na ustaarabu wa Kiafrika wa Kiislam.”9

Vipi udugu wa mtiririko wa zaidi ya karne kumi za ustaarabu, mila, na dini moja, utaweza kuvunjwa na miaka isiyozidi khamsini ya fitina zinazotokana na hadithi za kubuni za dhiki na dhuluma za utumwa? Juu ya yote yaliyotokeya na kufanyika ndani ya fitina za miaka michache, Wazanzibari wengi sana wamekuwa wakisononeshwa na kuwaombeya dua watu wa Zanzibar watuliye nafsi zao na Zanzibar ijirejeshee hishma na hadhi yake. Haya ya Zanzibar ni mfano wa yale aliyoyaelezeya msomi Eqbal Ahmad kuhusu mpasuko wa India:

Haiwezekani kukosa njia za kujiepusha na kufarikiyana kwa jamii mbili zinapoishi pamoja kwa miaka mia saba. Sifahamu kwa nini uongozi wa India, wa Kiislam na wa Kihindu, pamoja na Gandhi, wakashindwa kuhakikisha uendelezaji wa mtitiriko wa jamii mbili, moja ya Kihindu ya pili ya Kiislam, kuweza kuishi kwa pamoja. Kulikuwa na mivutano katika mahusiano yao kama kunavyokuwepo mivutano kwenye mahusiano yoyote yale. Muhimu zaidi ni makundi mawili haya yameishi kwa kutegemeyana na ndani yake kumezaliwa mambo mengi sana. Ustaarabu mpya umezaliwa. Lugha mpya ya Urdu imechomoza kutokana na mchanganyiko wa nini Waislam wameleta na walichokikuta Bara Hindi…Kutengana kungeliweza kuepukika kama alivyotabiri mshairi na mwandishi mkubwa Rabindranath Tagore ingelikuwa harakati za India zilizo dhidi ya ubeberu zingeliutambuwa umuhimu wa kujitenga na ideolojiya ya uzalendo (nationalism). Tuliupinga ubeberu wa Magharibi lakini katika kufanya hivyo tukaukumbatiya uzalendo wa Magharibi mzima mzima.10

Uongozi wa Zanzibar na wa Tanganyika, pamoja na Mwalimu Nyerere, ungeliweza kuhakikisha uendelezaji wa mtiririko wa makarne ya jamii mbili zilizouzaa ustaarabu wa Waafrika Waislam, lugha ya Kiswahili, na mengi mengineyo. Mtengano ulioletwa kwa makusudi na mapinduzi ya 1964 ulisababishwa na mrengo wa kisiasa wa kizalendo wa Pan-Africanism ambao chimbuko lake limetokana na Waafrika waliyosoma na kulelewa Ulaya. Matatizo pia yaliletwa na khofu ya mrengo wa kizalendo wa Pan-Africanism kuja kutawaliwa na mrengo wa Pan-Arabism ambao ulikuwa ndiyo mrengo wa Masri ya Rais Gamal Abdel Nasser, rafiki wa chama cha Zanzibar Nationalist Party kilichokuwa kikiongozwa na Zaim (kiongozi) Sheikh Ali Muhsin. Ni jambo la kushangaza vipi mirengo ya kizalendo ya viongozi wakubwa wa Afrika, Julius Kambarage Nyerere na Gamal Abdel Nasser imalizikiye na mauwaji ya halaiki na kuguswa na sumu ya fitina za utumwa.

Mara nyingi Zanzibar imejaribu kujipatiya utulivu na haikuweza kufaulu. Haya yalitokeya kabla ya Mapinduzi na yakajaribiwa tena baada ya Mapinduzi na zaidi kwenye Miafaka ya hivi karibuni. Wakati wa Mwenye Enzi Mungu kutaka ulikuwa bado haukufika na pia kwa sababu ya mashindano ya kisiasa baina ya Wazanzibari wenyewe kwa wenyewe yanayotokana na tabia ya kutoaminiyana.

Miaka arubaini na sita yameutiya umoja wa umma wa Kizanzibari wenye dini, mila, na kuingiliyana kwa kuowana, ndani ya mtego wa upotoshaji wa historia ya nchi ya Zanzibar. Kwa mujibu wa Bwana Abdulshakur:

Ukweli ni uvamizi ulikuwa ni tukio tu lakini yaliyofuata mavamizi hayo ulikuwa ni mlolongo maalum uliojengwa kiitikadi katika kumpotosha Mzanzibari na utambulisho (identity) wake. Mipango ya kumgeuza na kumpotosha Mzanzibari [mweusi na mweupe] ilianza kwa bahati tukiwa wadogo maskulini. Mengi yalitupata na mengi tukayashuhudia lakini kama watoto, mengi tuliyaona kwa jicho la kitoto pia.Tukitafakari leo kwa kutizama nyuma tulikotoka tunaweza kuona kuwa yote hiyo ilikuwa ni mipango yenye nia na madhumuni maalumu.11

Lililotoswa na kuzoweleka ndani ya akili za wengi ni kuwa mapinduzi ya Zanzibar yalikuja kuondowa dhiki na dhuluma za kikundi cha mabwanyenye wa Kiarabu wachache dhidi ya Waafrika walalahoi waliyo wengi. Kitabu hichi kinahoji kwa ushahidi kuwa mapinduzi ya Zanzibar yalikuwa na lengo la kuubomowa uhusiano mkongwe baina ya Waafrika na Waarabu na kuuweka uhusiano huo chini ya udhibiti wa nguvu za kiutawala za Tanganyika.

Kama alivyosema Eqbal Ahmad, hakuna uhusiano usiokuwa na matatizo yake na uhusiano wa zaidi ya miaka elfu mbili baina ya Waafrika na Waarabu uliyozaa ustaarabu, lugha, na dini ya Kiislam iliyozikaribisha na kuzihishimu dini nyengine Zanzibar, ushindwe kuundeleza mtiririko wa jamii hizo mbili kuweza kuishi kwa udugu na ujirani mwema.

Kwa mujibu wa mchoraji maarufu na bingwa wa lugha ya Kiswahili na habari za Waswahili, Profesa Ibrahim Noor Shariff:

Hakuna mgongano wowote wa mtu kuwa Mwarabu na wakati huohuo akawa Mwafrika kama vile hakuna mgongano wowote wa mtu kuwa Mbantu au Mmasai akawa pia ni Mwafrika.12

Wakati akizungumziya mapinduzi ya Zanzibar, Profesa Ali A. Mazrui aliandika:

Kwa maana ya uzalendo wa Kizanzibari, Jamshid bin Abdalla na Ali Muhsin walikuwa Wazanzibari zaidi kuliko John Okello lakini kwa maana ya uzalendo wa Kiafrika, John Okello alikuwa Muafrika zaidi kuliko Jamshid bin Abdalla na Ali Muhsin.13

Jambo lilokuwapo wakati ule wa nyuma ni kuwa Zanzibar si nchi ya Kiafrika kwa sababu ilikuwa na utawala wa Kisultani ambao ni wa asili ya Kiarabu na wa Kiislam. Na si hivyo tu ulikuwa utawala uliotanguliwa na tawala nyengine kongwe za Kiislam katika Pwani ya Afrika Mashariki na ushawishi mkubwa ndani ya bara la Afrika Mashariki na Kati ambazo pia zilikuwa zina asili ya mchanganyiko wa Kiarabu na wa Kiafrika. Hilo halikuwa jambo geni kwa Afrika Mashariki na Kati ziliyoko chini ya Jangwa la Sahara. Tatizo lilikuja pale wakoloni wa Kizungu walipoona wazi kuwa kuna mahusiyano mazuri na makubwa baina ya Zanzibar yenye ushawishi Afrika Mashariki na

Kati na nchi za Kiarabu za Kaskazini ya Afrika ambazo zilikuwa dhidi ya Wakoloni wa Kizungu.

Inafaa ikakumbukwa kuwa “nchi kumi (10) za Kiarabu ziko ndani ya bara la Afrika, na thuluthi moja ya umma wa Kiarabu inaishi Afrika, na aslimia 72% ya ardhi za nchi za Kiarabu ziko Afrika na kuwa dini ya Kiislam ni dini iliyotapakaa katika bara la Afrika kuliko dini yoyote nyengine.”14

Wapenzi wa matumizi ya neno “Muafrika” katika Afrika Mashariki hawana budi kuuzingatiya ushahidi wa kihistoria au ushahidi wa viini vya DNA vya miaka ya hivi karibuni wenye kuthibitisha kuwa Waafrika Wakristo na Waislam walikuwa kitu kimoja kwenye kuupendeleya mrengo wa uzalendo wa Kiafrika uliyotokana na Waafrika ambao waliishi nchi za Ulaya wakati Afrika ilipokuwa ikitawaliwa na Wakoloni wa Kizungu. Na hata baadhi ya Waarabu pia walitumbukiya ndani ya mrengo huo.

Lakini haina maana kuwa hisiya za kidini zilikuwa hazipo. Ukristo ambao ulikuwa ndiyo dini ya Wakoloni wa Kizungu ulikuja kufananishwa na sifa zote za Muafrika Mkristo aliyeonewa na aliyekosewa na dhuluma za kihistoria, na Waarabu Waislam wakapewa sifa zote mbovu kuwa wao ndiwo waliyoleta uovu wa biashara ya utumwa Afrika. Uchafu wote ukapelekwa Bagamoyo kwenye Uislam na usafi wote ukapelekwa Arusha kwenye Ukristo. Tanganyika ikageuzwa kuwa ndiyo msalaba wa kuisulubu Dola ya Zanzibar bila ya kujali hali ya mchanganyiko wa kidamu baina ya watu wa pande hizo mbili.

Yaleti siku ifike Katiba ya Zanzibar na ya Tanganyika zikapinga kwa maneno na kwa vitendo ubaguzi wa binaadamu yoyote yule kwa misingi ya kikabila, asili, au dini na kuwalinda na kuwapa zawadi watu binafsi au taasisi zitakazowaanika na kuwawajibisha bila ya kuwaoneya haya mafisadi wa kiasili, kidini na wa kiuchumi. Yasije yakawa yale ya Tom Mboya alipomuambiya Sheikh Abdillahi Nasser wa Kenya “rudi kwenu Oman!” na Sheikh Abdillahi akamjibu Mboya “na wewe rudi kwenu Sudan!” Mboya akajibu “angalau Sudan iko Afrika!” na Sheikh Abdillahi akamjibu “hata hivyo. Sudan bado ni memba wa Arab League! (Jumuiya ya Waarabu).” 15

Suala la ubaguzi Afrika limedharauliwa sana kutokana na imani kuwa mtu mweusi hawezi kuwa mbaguzi au kaburu kwa sababu ya historia ndefu ya kubaguliwa, kuuzwa, na kutumbikizwa ndani ya ukoloni. Chembelecho Mwalimu Nyerere, mbaguzi ni mbaguzi tu hata akiwa ni Muafrika mweusi.16 Muhimu binaadamu kujitambuwa na kushikiliya kutambuliwa kuwa ni binaadamu bila ya kuwaoneya haya wabaguzi wa Kiafrika kwa sababu ni weusi.

 

 

Nadhariya ya Kitunguu na Mlango Uliyofungwa

Nilifanya mahojiano mengi na kuzisajili sauti za wazee wa Mapinduzi ya Zanzibar lakini baadaye nikaamuwa nisizitumiye kwenye kitabu hichi kwa sababu niligunduwa kuwa nimekamata ganda kavu la kitunguu lililo karibu na nje. Nadhariya ya kitunguu imenisaidiya kufahamu kuwa kitunguu cha mapinduzi ya Zanzibar kina tabaka maalumu na chache mno. Mikono ya Mapinduzi huenda ikawa mingi lakini vichwa vya mapinduzi ni vichache sana. Hilo ni jambo la kawaida. Hakuna nafasi ya watu wengi kwenye jambo la siri kama la kupanga mapinduzi. Mapinduzi ya Zanzibar yana tabaka au vikundi tafauti vya kijamii na vya kisiasa ndani ya Zanzibar, Tanganyika, na nje ya Zanzibar na Tanganyika. Kuna maelezo ya dhahiri kukhusu Mapinduzi na piya yaliyojificha juu ya tukiyo hilo hilo. Maelezo ya dhahiri ni kuyaweka Mapinduzi ya Zanzibar ndani ya mabano ya visiwa na kutamka kuwa hakukuwa na mkono wa nje kwenye kuyafanikisha mapinduzi hayo. Maelezo yaliyojificha ambayo ni muhimu zaidi kwa mustakbal wa Zanzibar yanakubali kuwa Mapinduzi ya Zanzibar yalikuwa na wenyewe, na wenyewe hao walikuwa vichwa vya juu vya Mapinduzi na hawakuwa wanakindakindaki wa Kizanzibari. Wazanzibari wenyeji ambao hawakushirikiyana na vichwa vya mapinduzi kutoka nje hawakuaminiwa kupewa siri ya mipango ya mapinduzi na siri hiyo haikuwa kuingiya Bomani, au Ziwani kwenye vituo vya polisi na silaha.

Majiko ya Mapinduzi yalikuwa machache lakini nguvu zake ambazo ndizo zilokuja kuamuwa wapi Zanzibar ielekee hazikuwa nguvu za Wazanzibari wenyeji. Kwa vile majiko yalikuja kupinduwana msomaji anatakiwa awe makini kuelewa wapi kuna migongano ya maelezo na wapi kuna migongano ya majiko. Jiko asiliya la ndani la Mapinduzi ya Zanzibar lilipinduliwa siku tatu tu baada ya Mapinduzi kutokeya baada ya mikono ya mapinduzi ambayo kisiasa ilikuwa ikicheza mchezo baina ya jiko asiliya la Mapinduzi na baadaye kumkabidhi uongozi Mzee Karume.

Kitabu pia kinahoji kuwa hakukuwa na Kamati ya Watu 14 kabla ya tarehe 12 Januari 1964 iliyokaa kitako peke yao na Mzee Karume kupanga mipango ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kamati hiyo iliundwa na kupewa jina hilo baada ya kupinduliwa jiko la kwanza la akina marehemu Abdalla Kassim Hanga, Saleh Saadalla Akida, na Abdulaziz Twala. Waliyojiita baadaye kuwa ni Kamati ya Watu 14 walikuwa ni vijana wa Afro-Shirazi Party Youth League (ASPYL) ambao wakichukuwa miongozo yao kutoka kwa akina Saleh Saadalla. Lakini kwa sababu Hanga, Saadalla, na Twala walikuwa ni viongozi wasomi na wakiupinga uongozi wa Mzee Karume, vijana wa ASPYL ambao takriban wote hawakusoma walikuwa karibu zaidi na Mzee Karume. Mapinduzi yalipofaulu vijana wakamkabidhi uongozi Mzee Karume siku chache tu baada ya mapinduzi ya akina Hanga kufanikiwa.

Kuna sababu tafauti zilizowafanya wazee waamue kusimuliya kwa undani simulizi za Mapinduzi ya Zanzibar. Kuna waliyotaka kuisajili historia inayopoteya. Kuna waliyotanabahi kuwa Mapinduzi hayakuwaleteya faida walizo-kuwa wakizitarajiya. Wapo wenye hisia kuwa wakati umefika wa kubadilisha serikali kwa njia ya kura za wananchi badala ya kutumiya mtutu wa bunduki. Kuna wanaohisi wamedhulumiwa na wametupwa wao na kizazi chao baada ya kazi kubwa waliyoifanya katika Mapinduzi. Ni dalili ya msemo maarufu wa Mwalimu Nyerere kuwa upinzani [mabadiliko] khasa Tanzania yatatoka ndaniya chama hichihichi na uongozi huuhuu wa CCM na si nje yake kwa sababu hakuna njiya ya kuyafahamu Mapinduzi na Muungano nje ya ASP, TANU na CCM.

Na piya katika wazee wapo ambao wanataka kuiona Zanzibar na Tanganyika zinazoheshimu historia itakayomtowa binaadamu kutoka jela ya yaliopita na yasiyojulikana, na kuelekeya kunako Zanzibar na Tanganyika zenye mapenzi, umoja, na neema za maisha mazuri kwa kila mwananchi. Zaidi ya yote ni kugubikwa na kusahaulika kwa kumbukumbu za Mapinduzi ambazo kukosekana kwake kwa nusu karne kumezipotezeya Zanzibar na Tanganyika nafasi za kujikwamuwa.

 

Mfumo wa Kitabu

Muundo wa kitabu hichi ni wa simulizi kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964. Asilimiya kubwa sana ya kitabu ni simulizi za wazee waliyoshiriki au walioyashuhudiya Mapinduzi kwa undani wake. Kiwakati asilimiya kubwa ya mahojiano ya simulizi ziliyomo ndani ya kitabu yalifanyika kuanziya katikati ya mwaka 2004 na mwisho wa mwaka 2009.

Usajili wa mahojiyano ya muda mrefu ya awali ambayo hayamo ndani ya kitabu yalikuwa na akina marehemu Ali Omar (Lumumba), Othman “Bapa”, na wenginewo ambao hawakutaka majina yao kutajwa. Kutokana na nadhariya ya kitunguu nilikuja kuamuwa kuwa mahojiyano ya baada ya mwaka 2004 na kuendeleya yalikuwa yana umuhimu mkubwa zaidi katika kuisajili na kuiweka sawa historia ya mapinduzi ya Zanzibar kuliko ya kabla yake.

Ni vigumu kuyatoleya tarehe mahojiano niliyoyafanya ndani ya nyakati tafauti na ambayo nimeyapanga chini ya mtiririko wa maudhui na milango tafauti. Na kwa vile baadhi ya wazungumzaji hujitokeza kwenye mlango zaidi ya mmoja nimeona hakuna haja ya kumjuulisha tena msomaji ni nani anayezungumza endapo wasifu wake ulikwisha kutolewa huko nyuma. Kuna sehemu chache sana ambazo mahojiyano yalifanywa na zaidi ya mtu mmoja ndani ya wakati mmoja.

Kwa kifupi kitabu kinaanza na maelezo na simulizi ya vipi ndoto ya uhuru wa Zanzibar ilivyozimwa kwa siri nzito ya Mapinduzi na kinamalizikiya na tafsiri ya nyumba ya Afrabia ambayo inatowa picha ya mustakbal mwema wa Zanzibar na wa Tanganyika. Huenda msomaji kutoka Zanzibar, Tanganyika, na kokote kule duniani, aliyekuwa akisononeshwa na suala la Zanzibar akaweza kuuona mwangaza nje ya pango la upotoshaji wa historia. Msomaji wa aina hiyo ni sawa na yule mama aliyotoka ndani ya pango lenye giza huku amebeba ndoo ya maji ya hikma juu ya kichwa chake. Hapana shaka uamuzi wa mwisho na muhimu utakuwa ni wako msomaji.

Kitabu hichi kina mfumo wa binaadamu mwenye hamu na kiu ya kuisaidiya Zanzibar, ikiwa yuko ndani au nje ya Zanzibar, lakini hawezi kufanya hivyo bila ya kwanza kuandaliwa mazingira ya kikatiba na ya kimaisha ambayo yatamvutiya kuweza kufanya hivyo. Hichi si kitabu cha siasa ingawa kwa mtizamo wa kijuujuu kinaweza kuonekana kuwa ni kitabu cha kisiasa na cha wanasiasa. Ni kitabu cha wenye dira na ushujaa wa kumchaguwa kiongozi na uongozi ambao utakuwa na sifa na uwezo wa kuituliza Zanzibar na Tanganyika kwa kuufuta upotoshaji wa fitina ya historia ambayo ndiyo mzizi wa shari ya chini kwa chini ndani ya muungano. Muhimu zipatikane nguvu kazi za Wazanzibari na Watanganyika waliyozagaa duniani ili wasaidiye kuutekeleza mkakati wa kuuinuwa uchumi wa Zanzibar na Tanganyika na kuziweka nchi zao kwenye daraja bora zaidi.

Baina ya milango mitatu ya mwanzo na mitatu ya mwisho, katikati kuna milango kumi na tano iliyokusanya simulizi za wazee kuhusu mapinduzi ya Zanzibar. Asilimia kubwa sana ya simulizi hizo zinatoka kwa wazee waliyopinduwa na simulizi mbili kutoka kwa marehemu Sheikh Ali Muhsin juu ya Mapinduzi ya 1964 na Shirikisho la Afrika Mashariki.

Kivitendo, mchango wangu katika kazi hii ni kuandaa minhaji ya utafiti (methodology); kuwasaka na kuwapata wazee; kuisajili na kuiweka sawa historia ya Mapinduzi na kuwakumbusha wazee dhamana zao za kukisaidiya kizazi kipya kufahamu na kuyaondowa matatizo ya Zanzibar, baina ya Zanzibar na Tanganyika na baina ya Waafrika na Waarabu; kuandaa masuala yaliyomuongoza mtafiti ndani ya midani ya utafiti na nyaraka za kitaifa; kukaa na wazee kwa muda mrefu; kuwafanyiya mahojiyano na kuyasajili katika vilimbo vya kunasiya sauti; kuyaandaa majadiliyano katika milango na kwa lugha ya Kiswahili ambayo ndiyo iliyotumiwa na wazee wengi; kuwapiga picha baadhi ya wazee kwa rukhsa yao na kuzipiga picha sehemu muhimu za midani ya utafiti; pamoja na uchapishaji wa kitabu hichi.

Niliweza kuwachaguwa wazee niliyowahoji kwa kuzifuatiliya dalili tafauti kutoka midani ya utafiti na nyaraka za kitaifa za Kiingereza na za Kimarekani na muhimu zaidi kutoka kwa wazee wenyewe kunijuulisha na wanamapinduzi wenzao. Msomaji ataweza kuwatambuwa baadhi ya wazee wanaozungumza na wanaozungumzwa baina ya maelezo yao ya ndani ya kitabu. Kuna baadhi ya wazee nimewagubika wasijulikane kwa sababu hawakutaka kujulikana kwa hivi sasa. Wako wazee muhimu ambao wanayajuwa mengi zaidi kuliko yaliyomo ndani ya kitabu lakini sikuwafuatiliya kwa sababu nilifahamu kuwa walikuwa na uzito wa kuzungumza kwa sababu wanazozijuwa wao wenyewe.

 

Masuala ya Kujiuliza

Wazee wengi wenye kusimuliya simulizi za Mapinduzi ya Zanzibar ni wazee ambao wamebobea kwenye historia ya Mapinduzi. Ni wazee waliyokaa kitako mara nyingi na kukongeshwa kwenye viti vyao kwa fikra na mawazo ya muda mrefu ambayo hawajawahi kuwakabidhi watoto na wajukuu zao.

Kitabu kinauliza masuala matatu ya msingi. Jawabu za masuala hayo zilimezwa na nyangumi aliyeamuwa kuzamiya au aliyezamishwa kwa makusudi kwenye bahari ya historia kwa zaidi ya miaka 46. Masuala ambayo msomaji wa kitabu hichi anafaa kuyazingatiya kwa umakini mkubwa ni haya yafuatayo:

1) Ufunuo wa Mapinduzi ya Zanzibar ndani ya kipindi cha maridhiyano baina ya Wazanzibari utaweza kuisaidiya Tanganyika kuisitisha mivutano iliyojitokeza kwa kuukaribisha mfungamano ndani ya Zanzibar ambayo ni sehemu ya pili ya Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar?

2) Umoja wa maridhiyano baina ya Wazanzibari wenyewe kwa wenyewe, baina ya Wazanzibari na Watanganyika, na baina ya Waafrika Weusi na Waarabu Waafrika, utakuwa na faida gani kubwa za kisiasa na za kiuchumi kwa wananchi walio wengi wa Afrika Mashariki na Kati?

3) Madola makubwa ya Magharibi yalishiriki katika upangaji na utekelezaji wa Mapinduzi au waliyasaidiya kwa kuzidharau kwa makusudi taarifa za kiusalama walizokuwa nazo kwa sababu Mapinduzi na Muungano ilikuwa ni mihimili miwili yenye maslahi na wao zaidi kuliko maslahi ya Wazanzibari, ya Wazanzibari na Watanganyika, na ya Waafrika na Waarabu?

Yapo masuala mengi yaliyo muhimu ambayo hayakupewa haki yake na kitabu hichi. Kwa mfano, nini chanzo cha fedha zilizotumika kuyagharimiya Mapinduzi ya Zanzibar? Inatosha kumnukuu Bwana Godfrey Mwakikagile ambaye kwenye kitabu chake Nyerere and Africa: End of an Era anakiri kuwa katika mada alizozungumza kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza na mtoto mkubwa wa Mwalimu Nyerere, Andrew Nyerere, moja wapo ni “viongozi kama Mfalme Haile Selassie, Dk. Kwame Nkrumah waliyagharimiya kifedha Mapinduzi ya Zanzibar.”17

Ufuatiliyaji wa chanzo cha fedha zilizotumika katika kuyagharimiya mapinduzi ya Zanzibar unahitajiya kufanyika ikiwa chanzo chenyewe ni serikali ya Tanganyika, au Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) au vyanzo vyenginevyo. Iko haja ya kujiuliza kama kuna ushahidi wowote Msalaba Mwekundu kuwaondosha Waarabu ilikuwa kwa ajili ya kuyasaidiya Mapinduzi au la.

Kwa mujibu wa Frieder Ludwig, mwandishi wa kitabu Church & State in Tanzania: Aspects of a Changing Relationship, 1961–1994 “Mapinduzi ya Zanzibar yalipokelewa vizuri na Wakristo waliyokuwa wakiishi Zanzibar.” Ludwig amemnakili Mmishionari mmoja aliyemnakili mama mmoja mtu mzima akisema “Nilishindwa kujizuwiya kukumbuka vipi Bwana wetu alisema ‘Nimeyaona mateso ya watu wangu—na nikampeleka Musa kuwakombowa’—na sasa amemleta John Okello kutukombowa…Si Kamishna wa Polisi [Edington Kisasi] peke yake, bali Makamishna wa Gereza na Kazi ni wanachama wenye bidii katika kikundi cha dini yetu”.18

Suala la kujiuliza, ni jee, Kanisa lilimuunga mkono Mwalimu Nyerere katika kuipinduwa Zanzibar? Misikiti pia ilishiriki? Na viongozi wa Kiislamu wa TANU walikuwa na mchango gani katika kuipinduwa Zanzibar?19 Wazee wengi waliyohojiwa na mwandishi wa kitabu hichi ni Waislam, ingawa uongozi mkubwa ulikuwa kwa mwenyewe Nyerere na madola makubwa yaliyomuunga mkono. Lakini hata akina Oscar Kambona pia walikuja kuangushwa na Mwalimu Nyerere ingawa alikuwa Mkristo Muanglikani.

Kuna masuala ya msingi kuhusu mchango wa Mzee Abeid Amani Karume katika Mapinduzi ya 1964 na Muungano ambayo ni muhimu sana kuwekwa sawa kwa faida ya historia na zaidi kwa faida ya Zanzibar. Kwa mfano msomi maarufu Tanzania, Profesa Issa G. Shivji ameandika juu ya mahusiyano ya Mzee Karume na Muungano:

Maelezo rasmi yanarudia ….kuwa Karume alikuwa ni mwenye shauku kubwa juu ya Muungano. Hivyo ni mbali na ukweli ulivyo. Kama kuna kitu ambacho Wazanzibari wanamtukuza Karume nacho, mbali ya utawala wake wa kidikteta, ni Uzanzibari wake na upinzani usiyotetereka wa kukataa kuingizwa ndani ya Muungano na kuipoteza haki ya Zanzibar ya kujiamuliya mambo yake wenyewe. Kwa mfano, Smith, ambaye alikuwa hana kizuizi cha kumfikiya Nyerere na maofisa wengine wakati wa utafiti wake, anataja kuwa tishiyo la Nyerere la kuwaondowa askari wa polisi wa Tanganyika visiwani ndiyo lililomfanya Karume aukubali Muungano. Lakini alikuwa anasitasita mpaka dakika ya mwisho.20

Au angaliya namna R. K. Mwanjisi, ambaye aliwahi kuwa Seketeri wa Bunge, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tanganyika, kwenye kitabu chake kiitwacho Abeid Amani Karume anavyoelezeya matukio ya “Siri za Mapinduzi”. Kati ya nukta 46 za matukio ya Mapinduzi, Mwanjisi anaelezeya kunako nukta ya kwanza kuwa “Mwishoni mwa mwaka mwaka 1963 au mwanzoni mwa mwaka 1964 iliundwa ‘Kamati ya Mapinduzi ya watu 14’. Nukta 14 inaelezeya kwa ‘Sultani akaelea baharini siku nzima ya tarehe 12 na kesho yake. Meli yake ikakataliwa kutua Mombasa. Ndipo iliporuhusiwa kuingia Dar es Salaam na Serikali ya Tanganyika baada ya kuombwa na Mwingereza.’ Nukta ya 15 inasema: ‘Tarehe 12 Mwalimu Nyerere na Bwana Kambona waambiwa mambo yaliyotokea Unguja [Zanzibar].’ ”21

Kwa hiyo Mwalimu Nyerere na Oscar Kambona hawakujuwa kitu kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar mpaka pale yalipotokeya. Ina maana walikuwa hawana taarifa yoyote kabla ya siku hiyo. Piya hakuna popote pale ambapo Mwanjisi anaelezeya na kwa ushahidi kuwa Mzee Karume alihusika na upangaji wa Mapinduzi ya 1964. Maelezo rasmi juu ya wahusika wakuu wa Mapinduzi ni Kamati ya Watu 14 ambayo ni ya viongozi ambao hawaonekani kuwa walikuwa na kiongozi.

Jambo moja muhimu ambalo Mwanjisi aliligusiya ni pale alipoandika:

Madola ya Magharibi yanaamini kwamba ati Mapinduzi ya Unguja na Pemba yameendeshwa na Wakomunisti, hii ni dharau ile ile ya kusema kuwa Mwafrika hawezi kutenda kitu cho chote chenye maana! Pia ni kuwapa Wakoministi sifa wasiyostahili kupata.22

Wakati umefika wa kukaa na kujiuliza masuali mazito ya nafsi zetu na wapi tunataka kwenda. Hukumu ni ya wasomaji wenye kuyapima mambo kwa kutumiya vipaji vyao na uhuru wao wa kufikiri bila ya kupendeleya hata kama ukweli utakuwa unawagusa wale ambao wanawapenda. Bado kuna kuingiya ndani ya nyumba, vyumba na vipembe. Mwenzangu una akili na moyo wako mwenyewe. Jiulize mwenyewe. Jijibu mwenyewe. Wazee wameshatusaidiya mpaka hapa. Sasa tujisaidiye wenyewe palipobakiya kwa kujihami kidini, kihaki, kiakili, kukilinda kizazi kipya na kuilinda Zanzibar na Tanganyika (Tanzania) pamoja na kuutengeneza upya uhusiano mkongwe baina ya Waafrika na Waarabu kwa kuwaleteya maisha mazuri zaidi wananchi wa pande mbili za Muungano.

Lakini lengo muhimu na kubwa zaidi liwe lenye kutizama mbele. Hilo ndilo la muhimu zaidi. Lengo ni kuufuta ujinga wa kuidanganya dunia na kuinyang’anya Zanzibar sifa zake kama ni nchi. Kama tutakavyoona huko mbele, Mzee Karume hakushiriki katika mipango ya Mapinduzi na wala hakuupenda Muungano kama ukweli unavyopotoshwa na wenye kutaka kuupa uhalali kwa kumtumiliya kisiasa baada ya kufa kwake. Kama tutakavyokuja kuona baadae piya, alijaribu kuirudishiya Zanzibar sifa zake kama ni nchi na matokeo yake alijibiwa “wakati wake bado haujafika” na baada ya miezi michache akauliwa.

Mzee Jumbe na Maraisi waliyofuatiliya wa Zanzibar pamoja na aliyekuwa Waziri Kiongozi, Maalim Seif Sharif Hamad, piya walijaribu kwa njia zao kuirudishiya Zanzibar sifa zake kama ni nchi na wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuuzidisha muamko wa Wazanzibari katika kuiteteya nchi yao na katika kuiteteya na kuinusuru Zanzibar ndipo itakaponusurika Tanzania.

Tukitaka kurudishana nyuma hatutokosa la kulitafuta na kuwapata wa kuturudisha nyuma, na khasa kikundi kidogo cha wahafidhina wa Kizanzibari pamoja na wahafidhina wenziwao kutoka Tanganyika watakaotaka kumrudisha chui ndani ya zizi la ng’ombe badala ya kumtimuwa.

Upinzani mkubwa wa kitabu hichi utatoka kwenye jumuiya zisizo za kiserikali kama pale Zanzibar au Tanzania zinapotaka kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislam (OIC). Jumuiya hizo hazimo ndani ya mikono ya Waislam na zinamiliki zaidi ya asilimia 95% ya vyombo vya habari pamoja na bodi za wahariri wa magazeti, televisheni na vituo vya redio. Vyombo hivyo vya habari vitauelekeza umma na madola makubwa duniani kwenye khofu zisizo kuwa na msingi kwa kusema kuwa Zanzibar sasa inataka kugeuzwa kuwa Dola ya Kiislam. Niya na lengo litakuwa ni kuwatiya khofu za chini kwa chini na za wazi wazi wananchi na madola makubwa kuwa kuja juu kwa Zanzibar ni kuja juu kwa ugaidi. Au wataamuwa kukaa kimya na kuzipa kasi fitina za miaka 46 katika jamii na taifa na watapima muamko wa kijamii kabla kutekeleza mipango yao ya muda mrefu kwa Zanzibar na Tanganyika.

Tutarajiye kupaliliwa ngojera za “biashara ya utumwa wa Waarabu” na kuiunganisha fikra ya Afrabia na kuvunjika kwa Muungano wa Jamhuri ya Tanzania. Upande wa umma ambao ungelipendeleya kuiunga mkono fikra ya mfungamano wa Afrabia utakabiliwa na hatari mpya kwa sababu ungali dhaifu kiuchumi, kisiasa, na haumiliki vyombo vingi vya habari, au kupeyana khabari kwa njiya na mikakati mipya.23

Inatosha neno “Arabia” ndani ya neno “Afrabia” (Afrika na Arabia) likafyatuwa upinzani mkali kama ule uliyoonekana dhidi ya OIC. Inatosha pia kwa baadhi ya watu kuchagazwa na jina na asili ya mwandishi ambaye ana damu za makabila mengi tu yakiwemo makabila kadhaa ya Kiarabu, ya Kimanyema na ya Kimwera, nk. Inatosha pia kutowa mfano wa tukiyo liliyotokeya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2001 wakati mwanafunzi wa ilimu ya Sayansi ya Jamii alipokuwa anatowa hoja ndani ya semina ya darasa. Mwanafunzi huyo alikuwa akinukuu sentensi kutoka kipindi cha Profesa Ali Mazrui cha The Africans: A Triple Heritage. Wakati mwanafunzi huyo alipokuwa akimnukuu Profesa Mazrui, Profesa mmoja Mkristo wa ilimu ya sayansi ya jamii ambaye alikuwa mwalimu wa hiyo semina alikurupuka kwa hamaki na kusema “…kwa nini unamnukuu Ali Mazrui…yeye hata si Muafrika. Ni Mwarabu!”24

Kitabu hichi ni cha kuwailimisha wale ambao wamejazwa khofu dhidi ya Waarabu na Waislam au dhidi ya Waafrika na Wakristo. Lengo ni kuwa, hatimaye kitabu kituletee mapatano ya haraka na mashirikiyano baina ya Wazanzibari, baina ya Wazanzibari na Watanganyika, na baina ya Waafrika na Waarabu. Wenye kuogopa mfungamano wa Wazanzibari na wa Waafrika na Waarabu hawana uwezo wa kuuzuwiya kwa sababu kipindi cha uhusiano mkongwe wa zaidi ya miaka elfu mbili ni kirefu sana kuliko huu muda mfupi wa miaka arubaini na sita uliyogubikwa na guo la khadaa.

Kwa hakika kwa hali ya leo ya Zanzibar na ya Tanganyika, kitabu hichi ni bishara njema. Kwa mujibu wa mwandishi Bwana Mohamed Said “mazungumzo ya wazee yaliyomo ndani ya kitabu ni kama watu wanaotubu ili wapate msamaha. Jinsi wanavyozungumza utadhani wametiwa kitu waseme yote wautue mzigo.” Na wewe msomaji, popote ulipo, huenda ukautuwa mzigo wako pia na ukawa na moyo uliyotuliya na wenye matumaini makubwa katika mustakbal mzuri wa Zanzibar, Tanganyika, na wa Afrika Mashariki na Kati.

 

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: