Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!

Icon

Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia

Mlango wa Nane: Musa bin Bek (Mozambique) na Zanzibar

Mzee Jonas Joseph Mchingama ni katika vijana waliopelekwa Shimo la Mungu na Chama cha Afro-Shirazi na kusomea masomo ya siasa na mafunzo ya kijeshi. Baada ya mapinduzi alijiunga na Jeshi la Watu wa Zanzibar na kufundisha somo la siasa. Hivi sasa anajishughulisha na shughuli za Chama cha Urafiki baina ya Tanzania na Msumbiji—Tanzania-Mozambique Friendship Association (TAMOFA).

 

Asili ya Wamakonde—J. J. Mchingama

Mimi kwa jina naitwa Jonas Joseph Mchingama. Sasa hivi nasema ni mzee wa Kimakonde kulingana na umri wangu nilizaliwa tarehe 6 Julai 1944. Katika kisiwa cha Unguja nlifika kwanza mapema mwaka 1953. Nimefika hapa kukiweko utawala wa kikoloni wa KiSultani na Mngereza. Mwaka 1956 nilichukuliwa na hayati Mtoro Rehani Kingo ambaye baadae alikuwa Meya wa Zanzibar. Yeye huko nyuma alikuwa na mashine yake ya kuchapisha magazeti. Gazeti lake likiitwa Afrika Kwetu.1 Basi yeye akawa ananilea. Alikuwa hana mke na mara zote nilikuwa nakula nyumbani kwa hayati Abeid Amani Karume. Mpaka mwaka 1957 ndipo ulipotokea muungano wa African Association na Shirazi Association. Huo ni mukhtasari wangu wa kwanza.

Pili, Mmakonde, asili yake ni Msumbiji, Mkoa wa Kaskazini kabisa wa Msumbiji unaitwa Cape Delgado. Ndiko walokotokea Wamakonde. Katika kuzaliana wengine wakavuka wakaja Mtwara. Hawa wakaitwa “Wamakonde wa maraba.” Kwa nini wakaitwa Wamakonde wa maraba? Kwa kuwa huku Tanzania wanatumia sana “shikamoo, marahaba, shikamoo marahaba.” Sasa wa kule na wa huku wamekuwa wajukuu na vitukuu wamezaliana basi wale wa kule Msumbiji wanasema “Wamakonde wale Wamakonde wa maraba wale.” Hata sasa hivi ukenda Mtwara sehemu za Newala mpaka Mtwara mjini kuna watu wanalima Msumbiji. Ni kwao wanadhani hii ni koo imetoka kule Msumbiji lakini yeye kazaliwa huku Tanzania. Na mimi nimezaliwa Tanzania [Morogoro] lakini asili yangu nimetoka Msumbiji. Kwa hivo hiyo ndo ikawa wale Wamakonde wa Mtwara wanaitwa wa “maraba” na wale kwa kuwatania wale wanasema “Wamahiwa hao” kwa sababu mara nyingi walifikia hapo kwenye kijiji cha Mahiwa. Lakini wote ni watu wamoja.

Na hii kuita “Wamakonde machale” ni kwa sababu ile ya kuchanja. Na sio wote wenye kuchanja. Lakini zamani ilikuwa ni utamaduni wa kabila lenyewe la Wamakonde. Pengine unaweza ukamkosa mchumba kama hukuchanja. Ni kama sifa fulani ya ushujaa. Kwamba mtu anaweza kustahmili maumivu yale ya kuchanjwa.

Kuna Wamakonde waliletwa hapa Zanzibar mwaka 1953 kulima na kuchuma karafuu. Shida iliokuwa ikiwakuta wanyonge wa Afrika wa nchi hii ilikuwa ikiwakumba na wao. Na hasa ilipokuja harakati ya kisiasa za kudai uhuru wa nchi hii.2 Chama kikubwa kilokuwa kinawatenga watu hasa wanyonge wakulima na wafanyakazi ni chama cha Hizbu. Hiki kilikuwa kabisa hakitaki kuwaona Waafrika wanatawala. Kama ndo sera yao. Na kulikuwa na mfumo maalum mtu mweusi kuonekana majumba ya mawe labda awe na kazi maalum, boi au katumwa mchukuzi kupeleka mizigo. Lakini si mtu wa kutembea kule. Anaweza kutangazwa akaambiwa mwizi au akasingiziwa jambo lolote. Huo ni mfumo. Kwa hivyo tayari ukatokea ubaguzi, wale wanyonge wakaonekana kwamba wananyanyasika, na wao wakajenga chuki kwa wale ambao wanajifanya waungwana.

Zanzibar Nationalist Party (ZNP) walikuwa wamegunduwa kuwa watu wa kutoka bara wana support [wanaunga mkono] zaidi Afro-Shirazi Party (ASP). Kwa hivyo tufanye njia ya kuwaondosha watu wa bara. Ukiacha jeshi la polisi, lakini hata raia walianza kufukuzwa kwenye mashamba, wengine zikatolewa meli bure, kama tripu nne au tano zilitolewa hapa na utawala huo kwamba watu wa bara warudi kwao. Hapa si kwao.3 Tendo hili iliifanya ASP iitumie nafasi hiyo nayo kuwachukuwa vijana wake kuwapeleka nje kujifunza mambo ya kisiasa. Mimi mmoja wapo nilokuwa nimetumiwa nafasi hiyo nikaelekea Mtwara kwenda kujifunza mambo ya siasa na mambo ya kivitavita. Lakini niliondoka hapa kama kwenda kujifunza mambo ya siasa tu. Ilikuwa ni siri ya mwenyewe Mzee Karume. “Nyinyi mnakwenda kwa sababu nyinyi mnategemewa kuwa viongozi wa kesho.” Sasa nafasi ya meli ya bure ya kuwarudisha watu wa bara kwao, na sisi tukaingia pale. Tukenda zetu kule tukawa tumechukuwa mafunzo ya siasa kweli pamoja na mafunzo mengine.

 

Shimo la Mungu

Safari yetu ya kwenda kusoma sisi tulikuwa watu kama 58. Lakini baadae 1963 tukarudi lakini huku mambo yalikwisha kuanza kuwiva mno. Mambo ya mapinduzi. Yamewiva mno. Siri zake hatuzielewi vizuri lakini nataka kusema kwamba Mzee Abedi Amani Karume alikuwa anajuwa viini vote.4 Na tishio kubwa lilikuwa ni kwa Mngereza kwa sababu ndo alokuwa mdhamini wa nchi hii katika utawala wa Sultani. Ndipo baada alipokwenda kufunga mkataba wa kuondoka Mngereza hapa, kule Lancaster House [Uingereza], wakenda kufunga mkataba Muingereza aiwachie Zanzibar. Yaliyobakia tutamalizana wenyewe.

Kwa lugha hii nataka kusema kuwa Mzee Karume alikuwa anajuwa habari za mapinduzi. Inakuja automatic kama kumalizana huku kama watakuwa wakaidi tutafanya mapinduzi. Na jengine ni baada ya kupatikana kwa uhuru 1963 mimi nilikuwepo pale Coopers pale bendera ya Muingereza inashushwa na ya Zanzibar inapanda, ya nyekundu na karafuu. Niko pale. Wengi walimlaumu sana Karume kaiuza nchi na katika kundi hilo tuloliongelea hapa la wasomi. Walimlaumu. Karume kauza nchi, kenda huko katia saini mkataba kwamba nchi ile basi tupate uhuru basi sisi tuendelee kutawaliwa tu. Walimlaumu sana Karume. Kauza nchi huyu. Hapa si kwao.5 Yeye [Karume] Mnyasa. Anajuwaje mambo ya hapa. Wakamlaumu lakini uhuru ukapitakana. Ikaandaliwa fete lakini maandalizi ya fete hii yanajulikana, tunafanya fete hii kwa madhumuni gani. Mkutano ukafanyika mkubwa, nakumbuka mpaka leo maneno ya Karume akasema “Wananchi tunatakiwa sisi WaAfro-Shirazi tusherehekee uhuru huu uliopatikana Zanzibar. Lazma tuusherehekee huu uhuru. Nchi yetu sasa iko huru. Yaliobakia tutasawazisha.” Bado anasisitiza lugha ile ile ya mapinduzi. Yaliobakia tutasawazisha wenyewe lakini Muingereza akishaondoka kwa sababu kizingiti kikubwa Muingereza. Hatumtaki Muingereza. Watu wakashangiria. Fete ikaandaliwa usiku kwamba sherehe za kusherehekea uhuru wa Zanzibar. Lakini uhuru huo huo ndo utakaopinduliwa siku hiyo hiyo! Ulisheherekewa kwanza.6

Na taarifa hizo za kwamba alikwenda kuzungumzwa yule Kamishina wa Polisi, yule Mzungu, ilikuwa moja ya mbinu za kivita. Nafikiri Mzee Karume si msomi lakini alikuwa ana akili ya mbinu za kivita. Ile ilikuwa ni triki ya kuwavuta askari kutoka makambini wakati mnahitaji kambi kuvamiwa. Wakiwepo wengi kutakuwa na upinzani mkali. Ni kuwavuta wawe nje. Yule Mzungu akaona Karume amefanya jambo la busara. Anataka nchi iwe na amani. Kumbe kambi tayari zilikuwa ziko wazi. Wanamapinduzi usiku ulipofika ilikuwa si ngumu kwao kuingia katika kambi na kuteka kwa haraka.

Na siku ile nakumbuka tulikwishaambiwa, kwamba vijana wote turudi sehemu zetu za majumbani kwa wazee. Kusiweko mtoto yoyote anafanya kazi kwa Wahindi na nani. Wote warudi majumbani. Lakini hatujui ile siri yenyewe iko vipi. Tulikuwa hatujui. Hapana. Na kweli wakatokea wazee wa kabila langu la Kimakonde, na wao wakati ule kulikuwa na viongozi wao. Chama cha FRELIMO kilikuwa tayari kishakuweko. Kulikuwa na branch [tawi] hapa Zanzibar, Dar es Salaam, Tanga, na Mtwara. Sasa wale viongozi wa FRELIMO tayari walikwishakuwa wamepata hizo habari. Kwa hivyo wakusanywe vijana watakaoshiriki katika mapinduzi lakini iwe ni siri.

Asitiwe mtu yoyote. Na wakakabidhiwa watu maalum. Mfano watu wa Kitope kiongozi wao ni fulani. Watu wa Mfenesini kiongozi wao ni fulani. Watu wa wapi, mtu fulani. Lakini silaha zao zote zilipakiwa mapema kwenye magari kuletwa mjini. Mjini zikapelekwa porini Mtoni pale, nyengine zikafichwa hapa. Kwa hivyo zilipofika time za usiku wazee wale waliondoka tu kuingia katika kambi. Na silaha wakazikuta huko huko. Baadhi ya viongozi wenzake, kwa sababu ya hitilafu zilokuwa zimejitokeza baina yao wakati huo walikuwa si rahisi kuzipata habari za Karume moja kwa moja. Na huu utata wa kwamba walikuwa wamekusudia kumuuwa ni kweli, walikusudia kumuuwa, lakini kwa sababu yeye ni kamanda alikuwa ana kitu kinaitwa RV, sehemu yake ya kutolea amri ya maficho.7 Badala mnamjuwa kuwa Kamanda wetu yuko mahala fulani lakini yeye yuko sehemu flani. Wanajuwa watu wachache tu. Pindi ikitokea mkinihitaji nitakuwa niko wapi. Ndani ya kundi hilo hilo la mapinduzi wako walokuwa wakimsaka. Wale walikuwa wanamtafuta Karume si kwa nia njema, kwa nia wamuuwe.

Wamakonde kutoka Msumbiji wameshiriki mapinduzi kikamilifu. Walikuwa watu wa kwanza kweli kuunga mkono mapinduzi. Na waliambizana, na wakapanga mission zao kwa Kimakondemakonde, wakaweka ngoma zao na wao. Moja ilikuweko Jumbi, moja ilikuweko Dunga, kwa niaba ya kuwakusanya wanawake na watoto tu kwenye kundi lakini wanaume wote wakaja kushiriki katika mapinduzi.8 Hizo mbinu walizifanya, waliunga mkono vizuri, na hapo Ziwani, Mzee Joseph Balo alokwenda vunja kwa shoka ghala ya silaha. Na wengine ni akina Mzee Ngamia, Tajiri Fundi, Mzee Tomeo, Namina. Katika nnaowatambua hao. Walikuwepo hapahapa. Kwa hivo Wamakonde mapinduzi ya Unguja walishiriki vizuri kwa kuwaunga mkono wenzao ambao wote walinyanyaswa pamoja katika serikali hiyo ya mkoloni.

Zanzibar FRELIMO iliundwa baada ya kutoka katika chama cha Mozambique African National Union (MANU). Na kulikuweko na chama chingine kikiitwa ODENAMO. Vyama hivi kwa pamoja vilikuwa vikidai uhuru Msumbiji lakini vikawa vinabaguana. MANU ilikuwa inataka uhuru wa Msumbiji upatikane kwa mkoa mmoja tu wa Msumbiji, yaani Cape Delgado. Wanokoishi Wamakonde na Wamakua. Na RENAMO yenyewe ilikuwa ni ya wasomi. Wao walikuwa wanataka wale wasomi na wana maarifa tu wajitawale wao wapate hadhi katika serikali ya ukoloni wa Kireno. Lakini Dr. Eduardo Chiwambo Mondlane yeye kwa kuombwa na hayati Mwalimu Nyerere, wakati yuko Amerika, kuna wananchi wenzako wa Mozambique wako kule Tanganyika, wanataka chombo lakini wamefarakana katika mfumo wa vyama vingi. Unaonaje ukenda wasaidia? Ndipo akaja Dar es Salaam akaunganisha vyama hivi kikawa chama kimoja cha FRELIMO, mwaka 1962 tarehe 25 June. Ikaundwa hiyo FRELIMO (Front Liberation Le Mozambique).

Sasa kuunganika huko, wana Msumbiji walioko Zanzibar wakawa na makao makuu yao pale Makadara baada ya kuvunjwa hiyo MANU ambayo ilikuwa makao makuu yake pale Msikiti wa Bi Zeredi. Wakiita “klabu ya Wamakonde, klabu ya Wamakonde.” Kama unaelekea kwa Haji Tumbo. Kiongozi wa kwanza alikuwa Mzee Mtalama Likolo, halafu baada ya yeye akafatia Mzee Jabir Mpinyeke, sasa hivi ni marehemu, amezikwa hapo Dunga. Hawa ndo walokuwa waanzilishi na wazee wengine wapo hapa Zanzibar. Wakawa wanahamasisha vijana lakini pia walikuwa chini ya msaada wa Afro-Shirazi Party. ASP ikawa inawaunga mkono katika harakati hizi za ukombozi wa Msumbiji.

1964 ulipopatikana ukombozi wa Zanzibar FRELIMO nayo ikawa ina vijana wanahitaji kwenda ikombowa Msumbiji. Lakini vijana hao ikumbukwe kwamba pia walishiriki katika mapinduzi ya Zanzibar. Sasa wale FRELIMO wakahitaji msaada wa Afro-Shirazi kwa sababu wameshajikombowa, kuwasafirisha vijana wake waende Algeria kwenye mafunzo ya kijeshi baadae waende Msumbiji. Hayati Abedi Amani Karume akasema “Hapana. Ni gharama kubwa mwanafunzi mmoja kumlipia katika nchi katika mambo ya masomo ya kijeshi. Lakini kwa kuwa sie hapa tushafanya mapinduzi, vijana wote wataingia katika jeshi la Zanzibar, watapata mafunzo hapa, baadae tutawasafirisha kuwapeleka nyumbani.” Ndipo likatengwa hilo eneo la Dunga, jumba la mawe, kuwakushanya vijana wote walokuwa tayari kwa ajili ya ukombozi. Pale ikawa wanapata mafunzo ya kwanza ya kijeshi kupitia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Zanzibar. Nakumbuka wanafunzi wake mmoja alikuwa Muharam Mohamed Dosi na Musa Maisara hao. Muharam alikuwa sana akishughulikia mambo ya afya. Maana alikuwa ni daktari. Lakini kina Musa Maisara, kina mzee Issa Kibwana, wao ndo walokuwa wakienda kutoa mafunzo ya awali na ili kuwaandaa hao vijana.

Wanapokuwa tayari wanasafirishwa pale, wanapelekwa Nachingwea ndo kwenye kambi kubwa ya wapigania uhuru wote. Wanachukuwa mafunzo tena pale ya mwisho, baadaye wanapelekwa nyumbani.

Wakati wanafunzi 58 tulipopelekwa Shimo la Mungu kiongozi wa FRELIMO Zanzibar alikuwa Mzee Mueba Mfaume. Viongozi wa FRELIMO walikuwa wakikutana na viongozi wa Afro-Shirazi hasa na Mzee Karume. Wanaporudi wanatuhamasisha sisi kwamba lazima tuwe kitu kimoja na Afro-Shirazi na hawa ni ndugu zetu, kwa hivo lazma kitu chetu kiwe hiki: kimoja.9 Lolote mtakalokuwa mmetumwa na Afro-Shirazi Party lazima mulitumikie. Na kutoka hapo vijana wengi ndo tukaingia katika Afro-Shirazi Youth League, huku tukiwa ni wanachama wa FRELIMO lakini wakati huohuo ni Afro-Shirazi Youth League. Lakini kwenye mapinduzi sisi 58 hatukuingia. Viongozi wa zamani wanaijuwa historia ya FRELIMO na Afro-Shirazi Party inafahamika hapa Zanzibar lakini hawa wa sasa hivi hawaijui.

Unajuwa mpaka sasa hivi nchi hii kama walivofanya Msumbiji na nchi nyengine kwamba kuna sehemu ya mashujaa. Zanzibar hakuna sehemu ya mashujaa. Hakuna! Na sisi tunawaambia kwamba Mzee Ali Hassan Mwinyi (Rais Mstaafu] kenda kujenga mwahala kwenye kaburi la mkusanyiko wa wanamapinduzi!10 Sasa tizama basi. Pana nini pale? Palifaa pawekwe nini? Pawekwe mnara wa kumbukumbu kuwa mashujaa wako hapa! Mimi siku moja nilimwambia ati Mzee Ali Hassan Mwinyi. Nikamwambia “Mheshimiwa, unakuja kutujengea juu ya migongo? Au ndo kwa sababu hatuna maana tena kwa sababu tumekufa?” Basi aliinama chini hivi akasema “Ah!”

 

Mzee Issa Kibwana

Pale napafahamu uzuri saana. Huwenda katika hao wanozungumza kwa ajili ya mahala pale mimi mmoja wapo, lakini hakuna anonisikiliza. Kisa, sijui kwa nini hawanisikilizi, lakini napigia ngoma saana. Nadhani mtu mmoja angelikuwa huyu yuhai pale mahala pangelifanikishwa. Mzee Kaujore, au Idi Bavuai. Kwa sababu wale wana idili ya mambo ya kumbukumbu.11

 

J. J. Mchingama

Walikwenda Shimo la Mungu na walikutana na vijana kutoka Msumbiji akiwemo marehemu Samora Moses Machel, alokuwa Raisi wa Msumbiji. Wakati huo hajawa kiongozi, hajawa chochote. Na yeye safari yake ya mwanzo anaenda kuchukuwa mafunzo ya kijeshi. Mpigania uhuru tu wa kawaida. Wanakwenda Algeria kusomea mambo ya kijeshi lakini itabidi wapitie hapo Shimo la Mungu kwa kuchukuwa hayo mafunzo. Na vijana hao waliotoka Zanzibar wakenda wakachanganywa pamoja pale. Sasa wakati wa kuondoka pale wale wanakwenda Algeria kuchukuwa mafunzo ya awali ya kijeshi, hawa wakarudi Unguja. Wale wa Msumbiji hawakuja Unguja. Wa Msumbiji walikwenda zao Algeria kwa ajili ya kuchukuwa mafunzo zaidi na Samora Moses Machel na wale wa Unguja wakafaulu wakarudi huku.

Tulokwenda pamoja Shimo la Mungu kuna George Jua Kali. Yuhai sasa hivi anaishi Mwakaje hapa hapa Zanzibar. Nnaye ndugu yangu mwengine Lucas Anthony, yuko Koani, yuhai. Nnaye mwenzangu mwengine anaitwa John Mango, yupo hapa Unguja, yuko Ziwani. Kwa bahati mbaya kuna wenzangu wengine wamefariki. Michael Sakoma amefariki. Kafia Uganda katika vita va Uganda. Kuna mwengine Mohamed Ali Mzee, naye bahati mbaya amefariki alikuwa akiishi hapa hapa Bububu ninapoishi. Lakini hao watu wapo ni wazima na afya. Kama utawafatilia hao watu ukawapata basi ni rahisi sana wakakueleza kwamba kweli tulikuwepo. Kama si wewe basi hao watakaohoji au kutaka kufuatilia. Kwa sababu ni muda mrefu wengine watakuwa hatujawasiliana hadi sasa na wengine wamekufakufa.

Sisi tulipoondoka hapa kwanza tulikusanya vijana kutoka sehemu mbalimbali. Tukakutanika Miti Ulaya ndo palipokuwa Afro-Shirazi Youth League [ASPYL]. Tukaambiwa kama wako wenye kutaka kwenda kusoma masomo ya siasa nje wajitokeze. Tukajitokeza sisi. Wengine walikuwa waoga pale. Ah! Huko tutapelekwa sisi, nchi za watu, tutakwenda kuchinjwa, na nini. Lakini watu wengine tukawa kama tumekufa wadudu. Tukanyosha vidole. Huo ulikuwa mwaka 1962. Tukajiandikisha pale nendeni, basi siku fulani muje mtakutana na wazee mpangiwe safari yenu. Kweli ikafika siku hiyo tukenda pale tukakutana na Mzee Karume, Sefu Bakari, Khamisi Hemedi, Hafidh Suleman. “Nyinyi vijana mmejikubalisha safari sio?” Msemo wake [Mzee Karume] ulikuwa wa kutishatisha. “Mmekubali safari? Mnajuwa mnakokwenda? Basi mtakutana na wenzenu kwenda hiyo safari huko. Mkajifunze siasa ya nchi. Namna gani kujitawala. Nyinyi. Kwa hiyo hapana kufanya mchezo mnakokwenda. Watengezee safari.” Kina Rajabu Kheri walikuweko pale.

Mtu wa bara anaetaka kwenda kwao meli bure! Mpaka Dar es Salaam. Tulipofika kule tukapokelewa na TANU Youth League. Tukafikia kwenye kambi ya TANUYL, tukaondoshwa pale Dar es Salaam moja kwa moja mpaka Mtwara. Tuliondoka kwa magari ya malori. Tukenda zetu mpaka Mtwara tukafikia kambi sasa hivi ni makao makuu ya Tanzania-Mozambique Friendship Association (TAMOFA). Chama cha urafiki. Ndo tukafikia pale. Tukafika pale tukalala, asubuhi yake tukapelekwa huko kwenye kambi yetu Shimo la Mungu. Tukaanza kupangiwa pale kwa section [kikundi] na tena tukagawanywa. Hatukuwa Wazanzibari watupu pahala pamoja.12 Tukachanganywa katika vikundi. Wabara na wa visiwani [Zanzibar] tukachanganywa kando. Hii platoon number 1,2, hii namba 3…Tunakutana kwenye madarasa kwenye masomo na wakati wa chakula, na wakati wa michezo. Kwa bahati wenzetu bara walikuwako na wasichana.

Kwanza kulikuwa na vijana wa TANU Youth League baadae kulikuwa na wataalamu hawa wa Kichina na baadae kutoka Kanada. Walikuwepo pale wakifunza lakini kwa siri kabisa. Na nafikiri harakati hizi alokuwa akizijuwa ni Mwalimu Nyerere na Karume. Pia kulikuwa na kambi ya Bagamoyo ya wapigania uhuru wa Msumbiji, FRELIMO. Kukawa na kambi ya Mazimbo, ni jirani ya Ngerengere. Kwanza ilikuwa ya FRELIMO halafu wakaachiwa hawa ZIPA, nafikiri wa Afrika ya Kusini. Kuna kambi ya FRELIMO ilokuwepo Kongwa, Dodoma kule. Kambi ya Nachingwea ya wapigania uhuru wa Msumbiji ilikuja baadae. Lakini hiyo ninayoinzungumzia ya Shimo la Mungu ni ya TANU Youth League na Afro-Shiraz. Ya Mtwara.

Njia za kurudia [Zanzibar] walizozitumia zilikuwa njia za ngarawa. Wengine walikuwa wakivukia Mtoni hapo, au Mangapwani, au Bweleo, na moja ya Kizimkazi. Kulikuwa na nahodha mmoja sana ndo alokuwa akiwachukuwa akiitwa Mzee Kopa. Huyu ndo alokuwa akitumiwa sana kuvusha watu kwa njia ya magendo. Alikuwa akikaa Makadara hapo, Msikiti Zabibu. Walikuwa manahodha kama watatu lakini mimi namkumbuka huyo. Ilikuwa si rahisi wakati wao wameshawaondowa watu wa bara kurudi kule halafu wapite tena njia za meli kurudi huku. Ilibidi warudi njia za panya. Wakifika Dar es Salaam wanatawanisha. Nyie mtaondoka leo, wengine mtaondoka kesho, lakini pengine siku ile ile mtaondoka makundi mawili. Lakini hamuwezi kujuwa. Nyinyi mnaondoka kwa njia ya Kunduchi, wengine wanaondoshwa kwa njia nyingine. Mnakutana mshafika huku.

 

Manamba Hakuna

Kwa uzushi wa watu wanaweza kusema kuwa wameletwa watu kutoka mashamba ya mkonge ya Tanga kuja kupinduwa Zanzibar. Hio si kweli. Mfano John Okello, wanasema John Okello ni Mau Mau alieletwa makusudi kwa ajili ya revolution [mapinduzi] ya Zanzibar. Si kweli. Kwa kuona ile lugha alokuwa akitumia. Lafidhi yake. Wameona, kweli Mau Mau wameingia hapa. Unajuwa kwenye vita kuna vita va kipropaganda. Wanaweza kusema watu hivo lakini kuletwa watu kwa ajili ya mapinduzi hakuna. Hakuna kabisa nakataa…Kwa sababu kama itatokea Manamba watakuwa Wamakonde, Warundi, ndo watu walokuwa wakiishi kwenye mashamba ya mikonge. Wanyamwezi kiasi tu, si wengi sana. Wanyachusa. Na hao hakuna Unguja waliokuja kwa njia hiyo. Hakuna. Walikuwa hakuna Wajaluo wengi ambao walikuwa wakishiriki kwenye mambo hayo ya mikonge. Wajaluo walikuwa wachache. Torozima Luich, na Thomas Pet alikuwa jeshi la polisi. Kwa hiyo suala hilo kabisa mimi naona, sio naona, nakuhakikishia kuwa hakuna mtu alieletwa kwa njia hiyo.

Si kweli kabisa! Ni uzushi na propaganda. Lakini ukinambia mkataba wa kuchuma karafuu, au watu waliokuja wenyewe binafsi, hiyo nakubali. Ndo mana pale Kinazini. Unajuwa mfumo wa Unguja wakati ule, mtu yoyote akionekana akionekana Mnyamwezi tu. Akiwa Mgogo, Mnyamwezi. Kwa hivo pale Kinazini unasikia “Banda la Wanyamwezi.” Pale inapojengwa ile benki mpya, palikuwa na banda la Wanyamwezi. Wakitoka huko wanafikia pale, Waarabu wanawachukuwa watu pale kuwapeleka mashambani mwao. Mkubwa wao alikuwa nani? Abdalla Kututu. Ndo akipokea jamaa pale yeye anawauza. Kwa upande mmoja mimi naipongeza sana serikali kujenga benki pale. Badala ya kuwa benki ya watu sasa wameweka benki ya kuhifadhi fedha. Mimi nimefurahia sana kile kitendo na amefikiri sana Raisi. Kwa sababu ilikuwa ni benki ya watu. “Wanyamwezi” walikuwa wanakuja kuchukuliwa pale na matajiri. Sasa imekuwa benki ya kisasa. Mimi napongeza sana kitendo hichi. Vijana wa kisaivi wanajuwa Kinazini lakini mtu mzima yoyote mwambie “banda la Wanyamwezi.” Na mimi mwaka 1953 nilifikia pale nikiwa na umri wa miaka minane, na babangu na mamangu. Tulifikia pale. Akaja Mwarabu, Yahya wa Pongwe. Akaja kutuchukuwa pale!

Baada ya kufika pale siku mbili kuna jamaa yetu, ndo huyo wa Tunguu kapata habari tumefika pale akaona “Lo! Pabaya hapa.” Akaja akatuhamisha usiku kwa kututorosha! Tukendahamia Tunguu nyumbani kwake. Ukenda Pongwe huvuki.

Si kweli. Si kweli kabisa. Musa Maisara ni mtu wa Kitundu. Hayati babake akiitwa Maisara Kapungu, ana rungu lina meno saba! Akijiita “Mungu mtu.” Ule utundu wote alokuwa nao Musa Maisara kampeleka [kaupata kutoka kwa] babake. “Jimmy Ringo” [Juma Maulidi Juma] namfahamu wakati wa siasa yeye kwenye mkutano alikuwa anahutubia, neno lake la kwanza anasema “chama kimeniruhusu niseme ninachokitaka. Nikichelea nitachelea mimi lakini chama changu imara.” Ndo anaanza kufunguwa mkutano “Jimmy Ringo.” Kuwa yeye na Musa Maisara wakisimamia kambi kwenye mashamba ya mkonge hizo ni propaganda. Au mtu alikuwa anataka kufurahisha hizi taarifa zinoge zaidi lakini sio kweli.

Omari Kopa ndo alokuwa nahodha mkubwa wa kuvusha watu kutoka Tanga kuja hapa. Magendo. Kwa hiari zao wenyewe watu. Yeye anasema “ukitaka kutajirika nenda Unguja. Pesa mara moja. Unachuma karafuu ukimaliza wewe una pesa.” “Njia gani? Omari Kopa yupo. Anavusha watu.” Anakwenda mtu binafsi anakwenda pale anapatana na Omari Kopa.

Ningepata ushahidi kwanza huyo mtu anaejuwa hivo akatueleza hao watu alokuwa akiwakusanya walikuwa kambi fulani. Akatupatia japo mmoja wawili wakatwambia kuwa wao walikuja kwa njia hiyo.13 Akiri yeye mwenyewe kuwa mimi nilikuja kwa njia hiyo ya Manamba. Na kambi yako ilikuwepo pale. Nafikiri ingetusaidia zaidi. Mtu atafikiri mwenyewe. Mimi mmoja wapo nilishiriki. Ndo mmoja nilikuwepo kambi hiyo. Lakini kama atazungumza mtu akasema mimi ni mmoja wapo nilikuwa kiongozi nilikuwa nikiwasimamia, anaweza kuwa anajipamba ili na yeye apate sifa fulani. Nijipambie sifa. Anaweza kufanya hivyo. Kama tutampata mwenyewe muhusika…basi sio wote wamekufa, watakuwa wapo watu. Watakuwa wapo na yeye atakuwa anawajuwa. Katika kukaa nao katika kambi hakosi mtu mmoja wawili walokuwa wa karibu.

Suala la Manamba linawezekana lakini mimi siwezi kulijibu hili suala lakini nnachokifahamu mimi ni kweli watu wengi kutoka Msumbiji walikwenda kuchukuliwa Manamba. Wanakuja Mtwara wanasafirishwa wanapelekwa Tanga, Morogoro, wapi, kabla wakati huo Chama cha Wafanyakazi hakijaundwa wala TANU. Nyuma kabisa huko! Ambapo mimi babangu alichukuliwa Manamba na mjomba wake kutoka Msumbiji. Mjomba twende huku kuna kazi, na nini, na nini. Akamchukuwa mpaka Mtwara, Mtwara akamsafirisha mpaka Morogoro. Morogoro yapo mashamba ya mkonge. Kuna shamba la Mazimbo, Kilosa, Kinguruwira, Ngerengere. Yote mashamba ya mkonge. Si Tanga peke yake. Mashamba ya mkonge yapo Tanga na Morogoro. Babangu alipofika Morogoro kwa bahati yuleyule mjomba wake akamkabidhi cheo cha unyapara kwa kuwasimamia Manamba wenziwe. Mimi nikazaliwa mwaka 1944 kwenye shamba la mkonge. 1953 ndo tukaondoka Morogoro kuja Dar es Salaam babangu kuja fuata karafuu. Kwamba Unguja wakati ule karafuu ilikuwa ni mali sana. Pishi unachuma kidogo tu una mapesa mengi sana. Ukenda kulima kibarua hapa na pale ushapata pesa nyingi sana. Kweli anakwenda mtu mwezi mmoja miwili anarudi nyumbani. Babangu akashawishika akaja hapa Zanzibar.

Sasa kama Chama cha Wafanyakazi kilifanya organization [mipango] hizo kwa sehemu ya Tanga, kwa sababu ya urahisi, karibu na Zanzibar, kwa hiyo inawezekana kama kulikuwa na organization hizo za kuwashirikisha watu kutoka huko. Itakuwa hiyo ni high level [daraja ya juu kiongozi] ambako pengine sisi hatujuwi kama walikuja watu wa aina hiyo.

Lakini suala la vijana waliokuwa wamekuja au wamekwenda huko Shimo la Mungu…njia zake walikuwa wanaandaliwa kiuongozi, kisiasa na hata kijeshi kidogo. Walikuwa wanaandaliwa hivo. Karume alikuwa ameipata mapema kwamba lazima niwe na vijana niliowaandaa katika misingi ya Afro-Shirazi Party kuliko hawa wasomi ambao tumekutana katika chombo cha Afro-Shirazi Party. Ndo hao akina Abdalla Kassim Hanga, na Twala, na yeye mwenyewe akawagunduwa kama hawa watakuwa kidogo si wenzangu hawa. Sasa lazma mimi niandae kikosi changu. Vijana wangu ambao wataondokea katika migongo ya chama cha Afro-Shirazi Party. Kwa hivo tukapelekwa kule Shimo la Mungu. Zaidi tukawa tunafanya siasa. Namna gani kuutumikia umma wa watu. Namna gani kuijenga nchi. Namna gani kulinda nchi. Hiyo kweli tulikuwa tumefanya.

Nilikaa na Mzee Karume tukazungumza haya masuala kuhusu kupelekwa mafunzoni. Nilikuwa mimi, Kali Haji, Juma Haji, tulikuwa tunakwenda sana kula pale kwake. Tunakula, yeye anatwambia “nyinyi vijana fanyeni hiyo kazi lakini pia nyinyi mnatakiwa msome mjifundishe, hali ya nchi yenu muijuwe, kwa sababu nyinyi kesho mtatakiwa kuwa viongozi wa nchi hii. Sisi tunafanya kazi kumsaidiyeni nyinyi ili muweze kukaa vizuri ndani ya nchi yenu.”

Katika mwezi wa Aprili au Mei hivi 1963 tulirudi Zanzibar kutoka Shimo la Mungu. Kwa sababu ule uhuru ulipatikana mwisho wa mwaka 1963 sote tuko. Tuko pamoja. Tunakutana Youth League pale Miti Ulaya. Tunaonana wote. Mzee mwenyewe anakuja pale anasema “nyie tulieni tu. Msiwe na wasiwasi. Haya mambo yamekwisha haya.”

 

Mapinduzi Si Kuuwa

Tuliporudi Zanzibar tulitakiwa na Mzee Sefu Bakari tuwafunze wenzetu masomo ya siasa na baada ya mapinduzi nikawa mwalimu wa siasa katika kikosi nilichopewa. Katika somo fulani la kisiasa wakati ule Sefu Bakari alitusomesha, kwamba katika Baraza la Mapinduzi la Zanzibar Kenya inatakiwa ilete mjumbe mmoja katika kikao kinapokutana. Lakini Kenya hawashiriki kwa vile kila wakati kiti kile kinakuwa kiko wazi.14 Kwa sababu gani? Kenya ilichangia mapinduzi ya Zanzibar baada ya kumkataa Sultani kushuka katika bandari ya Mombasa. Kwa sababu kama angeshuka bandari ya Mombasa, Mombasa kihistoria ni sehemu ya Zanzibar. Kwa vile alikuwa na haki kuomba msaada pale wakati wowote ulimwenguni. Kwa sababu bado yumo ndani ya nchi. Lakini kitendo cha Jomo Kenyata kusema “aa, huku mimi staki fujo” ikabaki aelee baharini. Kitendo hicho tayari alikwisha shiriki kuyaunga mkono mapinduzi. Kwa hivo [Kenya] ikapewa heshma iwe na kiti chake kwenye Baraza. Lakini kwa bahati mjumbe wa kule akawa haji na hakufahamu maana zake kile kiti kikawa kiko wazi kila Baraza linavokutana.

Na hivi sasa Baraza la Mapinduzi linakufa taratibu na nafasi yake inachukuliwa na Baraza la Wawakilishi ambalo kikatiba halina nguvu mbele ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.15 Neno hili “Baraza la Mapinduzi” na kwa sababu lilokotokea, limefanya mambo makubwa. Limetaifisha mali, mashamba, majumba, limefunga watu, pengine limenyonga watu. Leo ukilizungumza watu wanatishika. Wanaona “Lo! Unakuja mfumo ule ule.” Lakini ndani ya Baraza la Mapinduzi kulikuwa na vipengele ambavo walivipanga.

Tunataka mapinduzi ya kilimo, mapinduzi ya elimu, mapinduzi ya afya. Ni neno “mapinduzi.” Mapinduzi si kuuwa. Si kutisha. Si kunyonga. Hapana. Mapinduzi ni kukigeuza kitu fulani kukifanya kitu fulani. Mapinduzi ni ya maendeleo. Kama ni hivo basi, lile Baraza la Mapinduzi, na still [bado] wangetafuta vipengele fulani, vitakavoungana baina ya Baraza la Mapinduzi na Baraza la Wawakilishi katika miswada pengine inayopitishwa au vikao fulani wanavokaa. Wakajadili kitu fulani na Baraza la Mapinduzi. Kinyume cha hivo, kuwepo basi Baraza la Mapinduzi hakuna maana kwake. Na hao vijana wetu ambao tayari wameshakuwa memba wa Baraza la Mapinduzi wakati hawayajuwi hayo mapinduzi yenyewe, wakati pengine hawakuona kumbukumbu yoyote kwenye maandishi nini na nini, wataendelea kubaki tu, mimi nina nafasi ya rank [cheo] cha memba wa Baraza la Mapinduzi. Lakini mapinduzi yenyewe siyajui. Sasa vipi mimi nitakuwa memba wa Baraza la Mapinduzi wakati mapinduzi yenyewe siyajui? Kwa hivyo huu utata huu nafikiri upo.

Kuna watu wengine wanafurahi kwa kutokuwepo kwa jina hili la “Baraza la Mapinduzi” kwa sababu wameathirika wakati wa mapinduzi yenyewe. Hata katika sherehe zenyewe hizi unapowakumbusha kuna watu wanaathirika. Kuna watu muungano [na Tanganyika] hawaupendi. Kwa sababu zao tu na malengo yao. Hawapendi kwa sababu labda wengine wamehusika kwa kupinduliwa. Hawapendi kwa sababu pamoja na kwamba ni kupinduliwa ingelikuwa ni rahisi wangeomba msaada kurudisha tena (counterrevolution), lakini wanashindwa kwa sababu wakiigusa Zanzibar tayari wameigusa Tanzania nzima.

Kwa hivo muungano hapo hapo unalinda mapinduzi.16 Kwa sababu sasa hivi ukiichokoza Zanzibar umeichokoza Tanzania nzima. Ukiichokoza Tanzania nzima watakuuliza sababu wewe kwanini unaivamia Tanzania. Hawasemi unaivamia Zanzibar. Kwa hivo hapo kuna mtu anasema mimi staki muungano. Tukae wenyewe hivi hivi. Wengine wanasema mimi staki mapinduzi kwa sababu wameathirika na mapinduzi. Hataki kusahau yale yaliopita kwamba yale yamepita sasa tuendelee na kujenga nchi yetu. Ni wachache wanaofikiria hivo. Lakini hii kama itatoka kwa vovote vile itakuwa inatuletea usahihi hata kama umeupata kasorobo, sio kamili, kasorobo sio kamili, itakuwa imesaidia pakubwa sana.17 Kwa mtu mwenye akili ataanza kufikiri hapa panazungumwa ukweli ulikuwa huu, huu. Hivo sasa mimi nakwenda wapi? Kwanini tusikae pamoja tukajenga hii nchi?

 

Mauwaji ya Mashamba

Kwanza walianza Hizbu kuwafukuza wanachama wa Afro-Shirazi Party kwenye mashamba yao. Kama hutaki kuwa Hizbu ondoka. Na wakati ule mashamba mengi yalikuwa yamemilikiwa na matajiri wao. Mimi nafsi yangu nilikuwa Cheju tuliondokea pale kuja mjini. Kulikuwa na bwana mmoja Mwarabu akiitwa Sleman bin Hemedi. Mjomba wake yuko mpaka sasa. Yeye nilimlipiza kisasi kwa mambo mawili. Jambo la kwanza lilokuwa limeniuma ni nilipokuja hapo 1953 niliwakuta wazee wawili wa Kinyasa. Ni watu wazima. Na mmoja ana mshipa. Walikuwa watumwa wa baba yake huyo Mwarabu. Lakini wameshakuwa wazee sana. Wazee wale wakawa wanapewa kazi ya kila siku, hiyo ni daily routine [utaratibu wa kila siku]. Ajaze makalbi mawili yule bwana maji. Kisha apasuwe kuni vigogo va mkarafuu. Akangowe muhogo au akate ndizi, aweke pale. Hizo ni kazi za asubuhi. Afue nazi, aweke pale. Yule mwanamke, kazi yake ya kwanza amenye ndizi na muhogo, akune nazi lakini lile tuwi asilikamue yeye. Tui atakujakamua bibie. Wakati wa kula wao hawaruhusiwi kupewa kula. Watakaa wangojee, wao wakishamaliza halafu yale makombo wapewe. Sasa mzee yule sku moja akawa amepindwa na ule mshipa wa ngiri, usiku. Akawa anapiga kelele babangu akatoka kwenda kumsikiliza akamwambia wewe umepindwa na ngiri. Sasa hawana la kufanya. Ikabidi walale mpaka asubuhi.

Asubuhi yule bwana Mwarabu anamwambia kwa nini hukwenda kuchota maji? “Mimi nnaumwa.” “Ebo, unaumwa? Sisi hatuna maji unatwambia wewe unaumwa?” Babangu akamwambia yule Mwarabu “huyu mtu mgonjwa atachotaje maji?” “Wewe inakuhusu nini? Wewe umekuja hapa kufata kazi si kuulizia mambo ya watu.” Hakujibu kitu. Ikabidi yule bibi afanye kazi mbili, yake na yule bwana yule. Zote mbili. Mimi nna miaka kama kumi mpaka kumi na mbili. Hilo kidogo mimi nikahisi unyonge na baba alivokuwa akinungunika na mamangu nikajuwa hili jambo limewauma sana.

Halafu jengine, huyu bwana Mwarabu huyu, alichonikera ni kuwa tunatozwa kodi tunalima katika bonde la mpunga lile, lile shamba anasema ni ardhi yake.

Kila mwaka ukilima mpunga utowe pishi tano, kama umepata kama hukupata, lakini umlipe pishi tano za ardhi yake. Sasa mwaka ule hatukuvuna mpunga, hatukupata. Akasema mimi sijui habari hizo. Mimi nataka unletee pishi zangu tano. Ikabidi babangu na mamangu wende wakaombe kwa jirani ambaye amelima pishi tano akakope kule aje amlipe huyu bwana.

Kwa hivo siku ile ya mapinduzi baada ya kutulizana mmoja katika mlipa kisasi nlikuwa mie. Nilikwenda hukohuko kwake. Kwa bahati walikuwa hawajakamatwa bado…Kitendo kile nilichofanya wale wenzangu wengine walosikia vile wakasema “ala! Kwanini mmemuacha.” Wao wakenda mchukuwa wakamleta Raha Leo. Imekuwa kama mimi nimechangia sasa kisasi kile. Kwa sababu kama sio mimi kuelezea na kufanya vile pengine angenusurika yule. Nimewatia mori wale. Hivo kisasi kitapanda zaidi. Kwa hivo inawezekana kuwa na wenzangu wamefanya zaidi ya hivo kulingana na jinsi walivyo. Lakini mimi nimeshiriki kwa sababu ya kuona uchungu wa yale nilokuwa nimeyaona.

Halafu siku moja yuko mjomba wake Saidi mpaka leo tunakwenda kuwinda usiku paa. Mimi nabeba bunduki, napiga paa, wawili watatu. Tukirudi anakata ile miguu ndo ananipa mimi nikafanye kitoweo. Paa yule, matumbo, kila kitu anachukuwa yeye, mimi nikale ile miguu. Babangu anasema “wewe mwanangu umemuendesha usiku kucha halafu unakwenda kumpa miguu. Kuanzia leo sitaki tena umchukuwe mwana wangu. Na wewe nikikuona unafuatana na yule hapa pangu uhame.”

Kuna watu walifanya chaka la watu wa bara. Yule kanifanyia hiki na hiki lakini nikijitokeza mimi ni jirani atakuja kunilaumu. Nitamtizama vipi. Kwa hivo anamtumia mtu wa bara. “Unamuwacha yule vipi bwana?” Yule hivi na hivi na hivi. Sasa mtu wa bara anajitokeza anafanya kitendo kile. Anapata lawama yeye. Yule anakwenda kulekule. “Binaadamu hawa hawasikii.” Kumbe yeye ndo aliyemtuma. Aliyetomeza. Imetokezea mifano mingi sana ya namna hiyo.

Wazanzibari walishiriki kwenye Mapinduzi ya Zanzibar. Wamo. Si Pili Khamisi, Hafidh Suleman “Sancho”, Ramadhani Haji? Wapo lakini wengi inawezekana kwamba katika ku advance [kusonga mbele] wakawa nyuma. Hawakuwa mstari wa mbele. Baada ya kufanikisha ndie anakuwa mstari wa mbele. Sasa kapata nguvu. Imekua hivi eh! “Sasa tufanye hivi, tufanye hivi, njoo hapa.” Sasa wewe ndo umekuwa leader [kiongozi]. Lakini wakati ule wa kukitafuta kitendo chenyewe anakuwa nyuma nyuma. Ni wachache walokuwa wamesonga mbele.

Kabla ya Mapinduzi ilipotea bunduki Ziwani. Bunduki hii ilikuwa ikichukuwa mafunzo sehemu zote nyingi. Kwa Hani imekaa hapo watu wanachukuwa mafunzo. Lakini walikuwa wanachukuliwa watu maalumu. Ilipogunduliwa kwamba iko Kwa Hani ikahama. Ikenda mpaka Kiwengwa huko. Bunduki hiyohiyo moja. Watu wanachukulia mafunzo. Huku inatafutwa huku watu wanajifundisha. Mpaka ilipofikia tarehe watu wakagawiwa. Sasa Wamakonde hawa. Wamakonde tabia yao mara zote watakuwa ni wapole lakini ukimchokoza akishasema “see!” basi hapo hakuna utakachomfanya. Anakuwa mbogombogo. Chinja! Chinja! Hiyo tabia wanayo. Lakini kwa kawaida utawaona kimya. Ushahidi huo ntakupa kuwa hata ukiangalia ukombozi wa Msumbiji wenye asili ya Wamakonde ndio walioikombowa hiyo nchi. Kutoka Cape Delgado kuelekea huko, hawa wana jadi ya vita. Mbali ukimuongezea mafunzo.

Na Wamakonde hapa walikuwa hawachanganyiki. Shamba wanokaa, maalum kwa sehemu ya kwetu hii, Kitope. Walikuwa Kitope pale watupu! Sasa wenyeji wa pale Kitope wazaliwa wa hapo wakisema “hapo wako Wamakonde ukenda unaliwa! Wamakonde wanakula watu!” Sasa ile khofu imewapa wale jamaa msisimko. Tunaogopwa, bora tuzidishe! Ndo wakazidi kuwa wakali. Kitu hicho tuliwapa sie. Kwa kilimo huwagusi! Kumbe sivo. Wapole sana. Na wasafi sana. Ukenda kondeni utamkuta yuko kazini lakini ukirudi nyumbani tafauti. Nyumba ya nyasi lakini safii! Ukiambiwa sufuria hii inapikiwa utakataa. Inasuguliwa safi. Sahani inaanikwa kwenye jua ikauke! Hata alokuwa mkubwa wa Hizbu, Ali Muhsin, wazee wake kwa upande wa bibi zake wana asili ya Kimakonde kutoka Lindi.

 

Waafrika wa Zanzibar na wa Msumbiji

Kihistoria sisi binaadamu wananchi ni wamoja. Pemba Kaskazini sana wametokea Tanga. Wadigo na sehemu za Lamu, huku Mombasa huku. Ukija kusini yake wengi wametokea Msumbiji. Ukenda kisiwa Panza pale ukiwakuta wazee wenye umri mkubwa ukimuuliza asili ya kabila yake atakwambia Mmakonde, Mmakua. Waliletwa na Mreno. Unguja hii Matemwe ni watu wenye asili ya Pemba Bay. Kuna kisiwa pale kinaitwa “Matemo” ndiko walikotokea. Ukifika Pemba Bay mjini pale ukiuliza “Matemo” utaambiwa kisiwa kile pale wanatoka hapa na ni Wamakua. Kivazi, tabia zao zote, vyakula wanavyotumia Matemwe ndivo wanavotumia wale kule. Uwele, mtama, mhogo mkavu ule.

Chaani. Asili yake ni Wamakonde wa Mtwara. “Chaani mwepo.” Wawili wale walikuwa wanagombana. Sasa yule watatu akauliza “Chaani mwepo. Simgombana?” Nini nyinyi mnachogombana? Ndo neno “Chaani.” “Chaani mwepo champatana.” Akiwauliza wale hawataki kujibizana wanagombana tu “e, nipamuwanda.” Ndo ikawepo Donge Muwanda sijui na Chaani. “Muwanda” maana yake “mimi nenda zangu” hamnisikii, hamnijibu, mimi naondoka. Asili yao Wamakonde. Na ukienda pale Chaani masingini uliza maana ya “Chaani” kwa wazee watakwambia. Asili yao ni Wamakonde. Sasa wote sisi ni ndugu. Leo tuwe katika mfumo huo wa mapinduzi yalotokea, tunatafuta historia ya mapinduzi, tujenge tujijuwe kwamba wote tuwa moja.

Halafu mwengine awe anabeza aone kuwa historia hii si nzuri. Ni historia nzuri. Kwa sababu kwa vizazi vijavo tutakuwa na historia ya changamoto kubwa ya kuwafundisha vizazi vyetu “Ah! Kumbe mapinduzi yalitokea hivi na hivi na hivi.” Unajitowa muhanga, unawacha shughuli zako muhimu. Sasa hiyo si kazi rahisi. Historia itakuwa ya vizazi vijavo wa pande zote, ziwe za Kiarabu, ziwe za Kiswahili, wote wanaingia. Utakapotoa historia hii itakuwa “Ah! Kumbe makosa yalikuwa upande huu. Kumbe makosa yalikuwa yetu sisi.” Na sasa hivi kinachotakiwa tufanyeje sote tujenge nchi [ya Zanzibar] kwa pamoja. Lakini hatuwezi kujenga nchi kama tunakotoka hatukujuwi.

Tukirudi kwenye mapinduzi yenyewe sisi hatukupangwa na wala hatukuingia mabomani. Aloingia bomani aliingia kwa mpango wake. Na wengi sisi vijana hatukuingia mule. Ilikuwa siri ya wenyewe watu wa mapinduzi. Kwa kwenda kuiba na kuvunja maduka huko tulishiriki. Hiyo ukweli wa mambo. Wengine tulikuwa tunakutana “Vipi? Nimeshachukuwa vitambaa. Nimeshachukuwa baiskeli.” Wengi wetu tulitokea mashamba. Mimi branch yangu ilikuwa Chuini. Mwengine Mwakaje. Mjini walikuweko wachache tu. Mapinduzi Jumapili. Alkhamisi watu wakaitwa kujiandikishi jeshi. Sisi tulipelekwa makambini. Mimi nilipelekwa Mtoni. Wengine walipelekwa makamisaa. Kilimo sijui. Vitu kama hivo. Basi, nikabaki mie jeshini. Nilipostaafu nikarudi kwenye mambo ya FRELIMO ya ukombozi wa Msumbiji. Mmoja alikuwa Mchunga Mitama, yeye aliondoka akenda nyumbani kwenye ukombozi. Huyo mmoja tu. Suala la nguvu za ukombozi wa Msumbiji kutoka kwa Mreno hilo ni suala la jeshi la Tanzania lote kwa jumla limeshiriki. Pamoja na huyu Ali Mahfoudhi alikuwa akiongoza mkanda mzima wa kusini. Vikosi vote vile vilokuwa kusini yeye ndo akivishughulikia.

 

Ali Mahfudhi na Msumbiji

Kwa kweli aliisaidia Msumbiji kwa kiasi kikubwa sana. Kutoa ushauri kuhusu ulinzi wa kijeshi. Wakati wa ukombozi wa Msumbiji yeye ndo alokuwa mtu wa kwanza kusaidia suala la ukombozi. Na alikuwa ni mpelelezi mkali sana wakupeleleza kambi za Msumbiji, hasa zilioko mipakani mwa Tanzania na Msumbiji. Moja wapo ikiwa kambi ya Nangade. Albarto Sipande na Raymundu Pasinuwapa, hao ni majemedari wa Msumbiji. Hawa ndo majemedari wakuu wa Mkoa huu wa Cape Delgado. Wote wahai. Na ndo walokuwa wanakwenda sambamba kabisa na Ali Mahfudh.

Hiyo, yeye alikuwa amekwenda kule kwa mda wa siku tatu nzima akiifanyia upelelezi na alipokamilisha upelelezi wake ndipo sasa akatowa ushauri wake wa kuvamiwa kambi ile na kuipiga kambi ile ya Wareno ilioko Nangade. Ikawaka moto muda wa siku saba! Wakati huo yeye akifanya tena upelelezi wa kambi nyengine, Shaishai. Iko mbele zaidi. Nayo pia ikashambuliwa. Kwa hivo Wareno wakaona huku ni kwahala hakukaliki tena. Mipakani. Ikawa Wareno sasa wanatumia kuleta ndege za kivita, kupiga mabomu, wanaondoka. Wakawa ndugu zetu wengi wa Mtwara wakaathirika kwa makombora ya ndege za Kireno, mabomu ya kutegwa, walikuwa wanakuja wanatega huku kusudi kuona watu wa Mtwara wanawakaribisha watu wa Msumbiji kuja kujihifadhi huku. Lakini Ali Mahfudhi alijitahid sana kufanya kazi hiyo na walikuwa sambamba kabisa na Rais Samora Machel. Hasa juzijuzi tu katika kumbukumbu ya miaka 20 ya kifo cha Samora, pia na yeye Ali Mahfudh ametajwa katika mdahalo wake kwamba ni mmoja alisaidia sana ukombozi wa Msumbiji. Mpaka Msumbiji kupatikana kwa uhuru yeye bado alikuwa anaendelea kusaidia.

Ali Mahfudhi akifahamu Kireno. Wareno na Kispaniola wanaelewana. Na habari nyingi tulikuwa tunazipata, zilikuwa zinapatikana Msumbiji kwa yeye baada ya kuwakamata na kuwatesa na kuwahoji, ndo zikawa zinapatikana habari kwa wingi. Alikuwa hodari wa kufanya interrogation [mahojiano ya nguvu yenye lengo la kupata habari]. Sana, sana! Mwisho alichukuwa uraia wa Msumbiji. Ndo maana maiti yake imezikwa kule. Alipokufa ililetewa taarifa kwa family na serikali hapa [Zanzibar] ikaomba mwili wake uje uzikwe hapa. Lakini serikali ya Msumbiji ikasema, hapana. Tutamzika sisi kwa sababu huyu alikuwa tayari ni raia wetu. Lakini tunaruhusu family yote ije kwa mazishi. Na kwa bahati yuko kakaake kule. Ni Dokta na ndo alokuwa akishughulika kumtibu wakati wote alipokuwa anaumwa. Kaka yake anafanya kazi hospitali ya Beira, Msumbiji. Kwa hivo family hapa ikaondoka ikenda kule. Kazikwa kwa heshma zote kwa kweli. Amepewa heshima zote za kitaifa.

Sijui, mambo ya tamaa tamaa haya. Alikuwa mtu amependeza sana katika jeshi la Tanzania. Majeshi wakimpenda sana. Lakini kumbe mambo yao, alikuwa against [dhidi] na matakwa. Akaingia kesi ya uhaini. Lakini sasa kuna ushahidi ambao ulionekana katika kifo cha Karume. Yeye ndo aliefanya movement [harakati] ya kwanza, ya kuzunguka jumba lile kama kufanya inspection [uchunguzi]. Wakati Mzee Karume anaingia pale kwenye jumba yeye kapita kaangalia alivokaa, karudi, kapita tena. Ndipo kikaja kile kikundi kuja kumuuwa. Halafu la pili, wakati Karume keshapigwa risasi, yeye akawa wa kwanza kutokea katika tukio. Na baada ya kutokea, kufika pale kwenye tukio, badala ya kumhami Mzee Karume kumpeleka hospitali, alimkimbilia muuwaji wa Karume kwamba akimbizwe hospitali. Yaani kamuona yule Karume sio muhimu kuliko huyu Humudi ambaye amemuuwa Karume.

Inasadikika kwamba Ali Mahfudhi anahusika. Kwanza, yeye alikuwa Chief of Staff, Makao Makuu ya Jeshi, Dar es Salaam. Baadae akapata uhamisho wa kuja Zanzibar kuwa Operations Commander, Mkuu wa Mafunzo na Utendaji Kivita, Chief of Operations wanaita wenyewe au kitu kama hicho. Wakati huo kukawa na fununufununu ya upotevu wa silaha katika kambi za jeshi hasa kambi ya Idi Bavuai pale Migombani. Pakawa na upotevupotevu wa silaha. Palikuwa na vikosi vingi. Ahmada alikuweko pale. Humudi alikuweko pale. Ahmada alikuwa akishughulikia mambo ya michezo (sports) katika jeshi. Alikuwa na kikosi chake pale lakini wakati huohuo akawa anashughulikia michezo. Kwa hivo mara nyingi alikuwa kwenye sports lakini kwenye kikosi chake kukawa na huyu Humudi, ambacho kikosi hicho kilikuwa kikenda mara kwa mara Mtwara kufanya ulinzi wa mipaka kati ya Msumbiji na Tanzania.

[Kikosi] hicho cha Humudi mara nyingi kilikuwa kinakwenda huko. Na yeye Humudi alikuwa akienda. Lakini mwezi wa Aprili 1972 kikosi kikapewa likizo askari wake wote.18 Akabakishwa askari mmoja tu wa kutunza silaha pale, ghala ya silaha. Ni huyo Saidi Sindano. Wengine wote likizo. Ila yeye Saidi Sindano akaendelea kubaki pale kutunza ghala ya silaha mpaka watakaporudi wenzake ndipo yeye atatoka ataenda likizo. Lakini ile ilikuwa pia ni ujanja wa kumfanya, kwa sababu yeye alikuwa ni mtu wao [Makomred], kuwa yeye atakapobaki pale kikosi kimekwenda likizo hakuna atakayeshughulika pale, yeye itakuwa ni urahisi kutowa silaha kuzipeleka nje. Alipangiwa hivo. Na akafanya kazi hiyo. Ikawa kila siku anapotoka kidogo kwenda nje anaondoka na silaha moja. Anaifunguwa, anaitia kwenye mfuko, anatoka nayo. Na kulikuwa hakuna mtu wa kumsachi [kumpekuwa], wa kumuuliza anatoka na nini.

Lakini zikapatikana fununu hizo kwanza kuna upotevu huo wa silaha. Ikaenda fununu hiyo mpaka ikabainika kwamba kuna kitendo cha uhaini kinataka kufanyika kwa kupinduwa serikali. Kukawa kuna habari hizo, kuna mpango unafanywa nje ya kambi za jeshi kwa kutaka kupinduwa serikali. Kwa sababu ripoti ilikuwa inapatikana huko nje. Na mikutano ilokuwa ikifanywa huko nje ilikuwa ikiwataja kina Ali Mahfoudh, Babu, wako katika mpango huu wa kutaka kupinduwa serikali. Sasa wakawa wanafatiliwa katika nyendo zao, taratibu na vikosi va usalama, kutaka kujuwa. Hata mwisho ndo inafika tarehe hiyo, 7 Aprili 1972, wakajikuta wale kumbe siri zetu zimeshajulikana. Sasa tufanye mpango gani? Mpango hakuna, japokuwa tumejulikana, na sisi tulipe kisasi japo kidogo. Ndipo njama za kumuuwa Karume zikabainika.

Na siku ile Karume anauliwa, tayari habari zishamfika yeye mwenyewe. Kwamba leo wewe usiondoke, usitoke nyumbani kwako. Aliambiwa hivyo na Kanali Sefu Bakari na Yusuf Himidi, na huyo kijana ambaye alizipokea hizo habari. Kijana mmoja wa Kiarabu. Jina lake simjui lakini najuwa alikuwa kijana wa Kiarabu alopeleka habari hizo kwa Sefu Bakari. Bwana, kuna hiki, na hiki, na hiki, kitafanyika. Mimi kwa uchungu naona zitateketea roho za watu bure. Hakuna maana. Na kijana huyo alikuwa anaripotiwa tokea nyuma kwamba anazipokea hizo habari, nafikiri alikuwa akiwasiliana na watu wa Usalama wa Taifa. Akizipeleka huko. Wanasema alikuwa akiuza kahawa sehemu za Raha Leo pale. Alikuwa muuzauza kahawa hivi.

Sasa siku ile anaripotiwa Karume habari hizi kachukuliwa na yule kijana wa Kiarabu. Msikilize mwenyewe huyu kijana anachokizingumza. Nyumbani kwake pale Maisara. Siku ile ndo atakuja kuuliwa. Akaambiwa, Mheshimiwa masuala kama umeyasikia ni kweli leo usitoke. Wana njama za kutaka kukuuwa. Habari ziko hivi na hivi na hivi, wakahadithia picha yote, lakini mwisho wameshindwa, njama yao ni kukuuwa wewe. Usitoke. Jibu alolijibu pale Karume ni kwamba nimekusikia, fiamanillah! Nendeni. Wakaondoka.19 Sasa kitendo cha kutoka yeye ni ule ukaidi wake, au ndo wito umeshamfika wa kifo, akaondoka. Akaanza kutembea, na yeye alikuwa na tabia lazima akitoka jioni atembee mpaka sehemu za Kianga hapo kwa rafki yake mmoja wazungumze. Akirudi lazima afike Sebleni majumba ya wazee awasalimie wazee pale, japo kwa kuzunguka na gari, halafu ndo anaongoza anakwenda zake Makao Makuu [ya ASP] Kisiwandui, anacheza pale dhumna. Ulikuwa mchezo wake akiupenda sana.

Basi akafanya hivo. Ali Mahfoudh alikuwa kwa Khamis Machungwa. Alipoona msururu wa magari unaingia, ndipo yeye mtu wa kwanza kupita kwenda kuangalia. Lakini wale walinzi pale hawakuwa na khofu naye kwa sababu wanamjuwa huyu ni mkubwa katika jeshi, anapita njia zake. Punde kidogo akapita na huyu Humudi na yeye akapita. Wakati huo alikuwa na cheo cha Kepteni. Na wale walinzi wa usalama hawakumtilia mashaka kwa sababu ni kiongozi wa jeshi. Kapita akarudi. Halafu Ali Mahfoudh alipita, akarudi.

Ikaja gari pale ikapiga risasi za harassing [za kuudhi mazingira], wale walinzi walipolala chini ndipo Humudi akatoka akamshoot [akampiga risasi] Karume na yeye alikuwa amepiga goti, akapigwa risasi pale pale na wale walinzi na amekufa akiwa na bunduki yake. Ahmada ndio waliotoroka. Kuna ripoti za Humudi tangu yuko Urusi kuwa atalipa kisasi cha babake na ripoti hizo zilikuwa zikiripotiwa wakati yuko na wanafunzi wenzake hukohuko. Inasemekana kabla hajashoot [hajapiga risasi], sauti ilitoka kwa Karume “Humudi unafanya nini?” Sauti ilisikika “Humudi unafanya nini?” Ilisikika hiyo. Kwa sababu pale waliokuweko kina Thabiti Kombo hao walikuweko, na mmoja katika waliojeruhiwa. Kabla hajapiga risasi, keshashuka ndani ya gari, kapinda goti, ndipo Karume akasema “Humudi unafanya nini?” Unafanya nini, risasi zikatoka. Zikampiga yeye na kuwajeruhi wengine. Isipokuwa Mtoro Rehani Kingo tu, alikuwa hayuko, yuko chooni. Kwa hiyo aliposikia mlio wa risasi na yeye akabana huku huko! (anacheka). Akangojea mpaka mambo yametulia, akaja kugongewa ndo akatoka.

Siku ile jioni nilikuwa uwanja wa Mao Tse Tung tukifundisha hawa Valantia mambo ya gwaridegwaride. Tunaanza kufundisha tu, ndo ikatoka amri, akaja Sefu Bakari, akasema leo zoezi vunjeni askari wote warudi makambini. Hatujaambiwa sababu. Kwa vile mimi nilikuwa nimetoka nyumbani kwangu, siko kwenye zamu kambini, ilikuwa niende nikafundishe nirudi nyumbani kwangu Sebleni.

Lakini si dakika kumi, kumi na tano, ndo nikasikia mayoo yanapigwa sasa, “vita, vita!” Magari, watu wananinginia kwenye magari wanakimbilia mashamba. Mwenye kwao anarudi kwao. “Kuna nini?” “Kuna vita mjini.” Wengine wanasema kumesikika risasi Kisiwandui. Nikaona hali hii mimi kama ni askari nikimbilie kambini. Kwa hivo nikapita kwa njia za ndani kwa ndani mpaka nikatokezea kiwanda cha viatu cha Mwendo, Maruhubi. Pale nikakutana na Yusuf Himidi anafanya mazoezi kwa sababu wakati ule karibu amerudi Ujerumani kufanyiwa operation fulani na akaambiwa moja wapo afanye mazoezi. Anatroti kwa miguu. Nkamsimamisha nafsi yangu, nikamwambia “Mheshimiwa, kuna suala limetokea huko mjini.” Akasimama “Suala gani?” “Kuna mayowe mingi kuna vita Kisiwandui.” Kwa hivo pale pale aligeuza na nnafikiri kina Ahmada hawakumtambuwa Yusuf Himidi pale. Kuna gari ilitupita pale na wangelimjuwa kama ni yeye wangelimshoot. Lakini hawakumjuwa kutokana na zile nguo alizovaa za kisports, za kiraia tu. Yusuf Himidi akasimamisha gari akarudi kwake Sharifu Msa. Palepale akarudi moja kwa moja kuelekea makao makuu [ya jeshi].

Tayari Ali Mahfudhi keshafika makao makuu. Yeye keshaanza kutangaza katika vyombo va habari va kijeshi, hali ya hatari kwa sababu yeye ndo Kamanda wa Mafunzo na Utendaji wa Kivita. Keshatangaza vikosi vote hali ya hatari, standby, na wakati huo kutaka serikali nzima ya Zanzibar iwepo makao makuu ya jeshi. Na wakati huohuo katika opereshen yake yeye akatangaza kwamba popote mtakapomkuta Ahmada na Saidi Sindano, wapigwe risasi. Wauliwe moja kwa moja! Sio wakamatwe. Hapana. Popote atakapopatikana Ahmada na Saidi Sindano wauliwe na tayari akaandaa kikosi cha kumsaka Ahmada na Saidi Sindano. Kina Chwaya hatujawajuwa hawa. Hao wawili. Timu haijajulikana hapo. Kwa hivo kikosi kilipoondoka kumsaka Saidi Sindano na yeye Ali Mahfudhi akawa yumo ndani ya gari. Wakaelekea, sijui, Unguja Ukuu, akawa hayupo, lakini ndani anazungumza kwenye army radio [redio ya jeshi] huku anakwenda, “popote pale mtakapomkuta Ahmada auliwe.”20

Huku viongozi wote wa serikali, viongozi wote wa kijeshi wako makao makuu ya jeshi, Migombani except [isipokuwa] yeye tu kajitia yuko nje katika harakati! Ndo walipoulizana ndani. Mimi nimetolewa kwenye kikosi changu Mtoni kwenda makao makuu kuwalinda viongozi wote wa serikali walioko pale. Ndo tukawa tuko mlangoni. Anayeingia hana ruksa kuingia na silaha. Haidhuru ni viongozi. Kwa sababu pale haijulikani nani ni nani! Suala hilo tunaambiwa na Sefu Bakari kwamba viongozi wote watakaoingia silaha zote waziweke nje kwa sababu hatujuwani katika sisi ni nani mkweli nani nini. Ni suala kubwa. Yasije yakatokea mengine ndani. Mimi nayasikia hayo. “Itakuwaje huyu Operations Kamanda ndiyo, lakini vikosi vyote vina makamanda. Yeye hawaamini hao kwamba wanaweza kumpata.” Anazungumza Khamisi Hemedi kwa sababu ndo alokuwa mkubwa wa usalama wa jeshi. Sasa nafikiri yeye anachambuwa katika mambo yake ya kisecurity [kiusalama]. Itakuwaje huyu mtu mzima, kamanda mkubwa asiwaamini makamanda wake wadogo aende yeye? Na wakati katika ripoti zake za mikutano ya nje huyu yumo! Leo inatokea anajitowa yeye hapa anakwenda nje kwenye operation na ananganganiza lazma hawa watu wauliwe. Kwa nini? Kuna maana gani? Aitwe!

Akaitwa. Huko nje aliko huko. Akaambiwa, wewe bwana, hupaswi sasa hivi kuwa nje kufata kikosi kumfata askari mmoja au wawili. Kama itatokea vurumai kubwa zaidi, nani ataongoza operation ya vikosi vote? Wewe unapaswa ubaki hapa makao makuu ili likitokea kubwa wewe uweze kuongoza vikosi vote! Anaelezwa na Khamisi Hemedi, Yusuf Himidi na Sefu Bakari. Ndipo akabaki yeye pale, Migombani. Sasa hapo ndo ikabidi wakamatwe watu walokuwa wakituhumiwa katika ripoti za usalama za nyuma. Huku watu wanaendelea kusakwa. Ikenda hali hiyo mpaka Ahmada akakamatwa, akajeruhiwa sehemu za Mangapwani. Hajafa bado. Lakini baada ya kuripoti wale vikosi kwamba tumeshawapata hawa watu, tumepambana nao, tumeshawajeruhi, yeye, nafkiri kama skosei na huyu Chwaya. Tunawaleta. “Mnawapeleka wapi?” Anajibu kwenye radio. “Nimesema kwamba Ahmada mkimuona popote auliwe! Kwanini mnamleta. Mpige risasi. Askari akapokea amri, akapigwa risasi.” Wameuliwa Mtoni. Huko wametoka wakiwa hai. Basi, maiti zao zikapelekwa hospitali.

Lakini ripoti huku za usalama zinaripoti Ali Mahfudhi anahusika, lakini nani atayemkamata pale ufike kumtia ndani? Kwa sababu the most senior [mwenye cheo kikubwa] alikuwa ni yeye katika rank zote [vyeo vyote] zilioko pale. Wote pale. Yeye alikuwa full Kanali. Sefu Bakari ni Luteni Kanali. Ni mdogo mbele yake. Anaweza akamwambia tu “mguu sawa! Geuka!” na yeye akafata amri. Sasa ifanyike triki gani? Ndipo ripoti zile zikaripotiwa Dar es Salaam, kwamba kati ya watuhumiwa yumo na fulani lakini tunashindwa kumkamata. Ndipo ikatoka ndege na message [ujumbe] ikatumwa. Sefu Bakari, Natepe, na Ali Mahfudhi, mnatakiwa muje katika Kikao Maalum cha Ulinzi (KMU). Na ndege inakuja kumchukuweni. Kwa hivo wakaondoka hapa kama wao wanafuata kwenda kwenye Kikao Maalumu cha Ulinzi. Watatu hao. Natepe alikuwa vilevile Luteni Kanali, kama Sefu Bakari.

Wakaingia ndani ya ndege mpaka Dar es Salaam. Kufika Dar es Salaam, pale tena, kuna wakubwa mbalimbali, wenye vyeo vikubwa, wamefika pale, ndipo alipokuja mkuu wa majeshi, akasema, “kikao cha leo sio kikubwa sana. Wewe na wewe na wewe, mko chini ya ulinzi kuanzia sasa hivi.” Vua viatu, vua mkanda, vua rank! Na ma MP [Military Police] wameshazunguka. Ikabidi Ali Mahfudhi akatoa kitabu chake cha check (check book) aka sign cheki zake kwa familia yake. Jambo ambalo ni la ujasiri. Na akaona sasa nimeshanaswa. Nimeshaingia kwenye mtego. Anatengeneza mipango sasa. Kaandika cheki zake za miezi sita kwa ajili ya familia yake nyumbani. Hizi nipelekeeni nyumbani. Twendeni. Katulia, hata wasiwasi hana. Wakachukuliwa wote watatu wakapelekwa mpaka Ukonga. Kufika Ukonga, wakaingizwa ndani, wakagawiwa vyumba, wale wengine wakatolewa mlango wa pili wakatoka.

Alokusudiwa ndo keshapatikana. Wale wakapanda ndege jioni wakarudi Zanzibar. Lakini bado katika kesi ilipokuwa ikiendeshwa, Ali Mahfudhi alikuwa anatakiwa, Babu alikuwa anatakiwa. Waje Zanzibar lakini Mwalimu Nyerere akawa mgumu kuwatowa kwa sababu alijuwa kwamba wakifika huku hakuna chengine kitakachotokea isipokuwa ni kuuliwa. Na nafikiri labda Mwalimu Nyerere alikuwa hapendi sana masuala haya ya kuuwauwa. Ikawa wanazuwiliwa mpaka ikabidi mahakama iwahukumu wale kifo lakini wakiwa nje ya Zanzibar.

Sasa iwe mfano kama wameshaondoka nchini, Tanzania kwa jumla, akienda Umarekani pengine, kama iko tuhuma hio, au akenda nchi nyengine, anaweza kufanya vurugu kubwa zaidi dhidi ya Zanzibar.

Kwa hivo ikafanyika triki tena ya Samora Moses Machel wa Msumbiji amfanye Ali Mahfudh awe mshauri wa kijeshi lakini tayari wakati huo atakuwa katika detention [kifungo]. Anaangaliwa. Anachunguzwa. Na yeye alikuwa anajuwa. Anajuwa kuwa mimi nimeletwa nchi hii nikiwa chini ya ulinzi. Lakini yeye haijamshughulisha. Hicho kitu naweza kusifu alijitahidi. Na amekaa kule mpaka vilipotokea vita va Uganda. Ali Mahfudh aliomba akiwa Msumbiji, kwamba mimi nataka kwenda Uganda nikapigane kwa sababu nchi yangu imeingia mapiganoni. Kwa hivo mimi popote nlipo lazima niende. Akakataliwa. Msumbiji ilitowa ushauri, Mwalimu Nyerere akasema “hapana. Huyu asije hapa. Abakie hukohuko.” Wao walikuwa tayari wamtowe lakini Tanzania ikakataa kwa sababu vikosi vinavopigana ni pamoja na va Zanzibar. Pengine watakuwa bado wana uchungu wa kuuliwa kwa Karume, wanaweza wakamlipa kisasi huyu vitani.

Akabakia Ali Mahfudh Msumbiji mpaka kifo chake. Lakini kule aliunda shirika la ujasusi la upelelezi wa nchi za Kiafrika. Kama nchi fulani inataka kuvamiwa, kijeshi au kisiasa, yeye akipokea anazipelekea nchi hizo. Bwana, nchi yako inataka kufanyiwa kadhaa, kadhaa, kadhaa. Alikuwa analipwa na ile nchi pengine. Makaburu Afrika Kusini, wakagunduwa habari zetu za Msumbiji zinavuja kutokana na huyu Ali Mahfudhi. Wakamtumia majasusi kutaka kumshambulia kwenye nyumba yake alokuwa akilala. Lakini kwa sababu na yeye watu wake alikuwa nao, walikuwa very sharp [wako macho]. Wakazipata zile habari. Leo nyumbani kwako utakuja kushambuliwa. Kwa hivo siku ile Ali Mahfudhi hakulala nyumbani kwake. Kenda kulala hoteli. Wale wakaishambulia nyumba yake kwa mabomu. Yeye kumbe hayumo. Na wakatangaza Afrika ya Kusini, yule jasusi mkubwa anayepeleleza basi ameshauliwa—Ali Mahfudhi. Wanatangaza radio ya Afrika ya Kusini. Tushampata tayari. Asubuhi Ali Mahfudhi amekutikana mitaani Maputo anatembea. Na yeye akasema, bado. Ali Mahfudhi huyo sie! Mie bado nipo. Basi akaendelea kubaki kule na mwisho akaamua kuchukuwa uraia wa Msumbiji.

Na yeye wakati wote yuko full uniform. Hata siku moja humkuti amevaa kiraia Ali Mahfudhi. Yeye yuko katika combat. Kama amepumzika avue viatu. Na mkewe ilikuwa hivohivo. Alikuwa amechukuwa mafunzo. Hata haya mambo ya Judo, Karate, yule mama usimchezee. Kabisa, kabisa. Ali Mahfudhi akijuwa mambo haya ya Judo. Amejiandaa vizuri sana. Cuba ndo alikosoma sana. Siku moja nakumbuka katika mambo ya kawaida, mkewe alikuja sokoni pale, akawa amechukuwa pesa mkononi, sasa kuna jamaa fulani anamfahamu akamwambia. “Wewe mama utanyanganywa pesa zako.” Akasema “kwa vijana hawa walioko hapa wote hakuna hata mmoja. Waje kumi hawazichukuwi hizi pesa. Na kama husadiki atokee mmoja ajaribu. Nitaondoka nazo hivihivi.” Ni kweli.

Leave a comment