Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!

Icon

Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia

Mlango wa Kumi na Saba: Hayeshi Majuto Yao

Jambo la ajabu ni kuwa Kambarage akipenda sana kuwatolea Watanganyika wenziwe hadithi isemayo kama haya:

Miti midogo ilikuwa ikipiga kelele kuwaambia miti mikubwa:

Jamani wanakuja hao!

Miti mikubwa ilijibu: Vipi mwenzetu yumo?

Hayumo.

Basi hamna matatizo. Waachie, waachie waje.

Mara nyingine tena miti midogo ilinadi:

Jamani wanakuja tena haoo!

Nani?

Mashoka!

Mwenzetu yumo?

Wamo tele!

Ah, basi tumekwisha! —Ibrahim Noor Shariff

 

Mzee Aboud “Mmasai”

Khiyana imekuwa kubwa, kubwa sana. Na hii yote, kwa sababu mbili. Sababu ya kwanza, ni ujinga wa Karume. Yeye alikuwa na khofu na watu walokuwa na ilimu, hata mapinduzi bado. Aliwahi hata kuhutubia kusema “wakimbieni wenye ilimu.” Na sababu hizo ndo akenda kujiunga moja kwa moja na Nyerere bila ya kumshauri mtu kwamba asipinduliwe na hawa halafu wataleta Waarabu. Mimi nilikuwa sijui habari za muungano. Pia Babu alikuwa na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na yeye alikuwa hajuwi habari hio. Mimi nilikuwa nakwenda kazini, nafika kwa Sapriji, mbele si kuna duka la yule Muhindi anatengeneza radio anaitwa Dawud, nimesikia radio pale inasema juu, habari za muungano. Babu akasema yeye hajuwi habari hizo na yeye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje. Na Nyerere kakubali kwa makusudi kuitawala Zanzibar. Hichi ndicho ninachokiamini. Sababu moja ni hiyo ya Karume, ya pili ya Nyerere kukubali bila ya kuwashauri wananchi.

Halafu Karume Mawaziri wote walosoma kawapeleka bara. Kina Babu, kina Idris, Hasnu Makame. Wote wamepelekwa bara wakawa wanacheza ngoma huko. Na ndivo inavotawaliwa Zanzibar, manake mpaka leo hakuna Bunge la Muungano. Kuna Bunge la Tanganyika. Lina watu mia sita na ngapi, na watu wa Zanzibar wametiwa ndani watu khamsini, watafanya nini ndani yake?

Kinachotawaliwa kwenye muungano si idadi ya watu, bali ni mambo ya nchi za nje na ulinzi.1 Zanzibar ina nguvu yake kama Tanganyika hata kama Tanganyika ina mamilioni ya watu zaidi. Zanzibar ni nchi huru kama weye wa Tanganyika. Ningelikuwa mimi ni mtu wa kisiasa sitokubali. Namshukuru Mungu nalisema, mara tu baada ya kutangazwa muungano ikiwa kuwa hatuna Bunge la Muungano, tena mbele ya Bhoke Munanka, alikuwa ofisi yake Beitlajaibu, Waziri wa Mambo ya Muungano “ikiwa hatuna Union Parliament, Bunge la Muungano hatuwezi kulichukuwa Bunge la Tanganyia tukalifanya ni Bunge la Muungano.”

Udhaifu wa watu wetu wote hawaitetei hii Zanzibar. Nadhani kama Hanga alikuwa akiitetea ilikuwa ndo sababu ya kuuliwa. Mimi sikusikia kama aliwahi kuitetea Zanzibar. Hanga alitaka kufanyisha nishani kwa walioshiriki kwenye mapinduzi kwa sababu ni kujionyesha na kujiaminisha kwa watu. Na watu walopigana wawe na furaha. Mwalimu akamkubalia halafu akamuuwa.

 

Ubaguzi kwa Risasi: Karume “Afro”—Kombo “Shirazi”

Mzee Muhammed Baramia alikuwa memba wa Chama cha Umma na alihusika katika kesi ya mauwaji ya marehemu Mzee Abeid Amani Karume. Hivi sasa ni memba wa Chama cha Wananchi (CUF) na ni Imamu wa Msikiti.

Halikuwa jaribio la kwanza. La 1972 tulipanga tangu 1968. Madhumuni khasa ilikuwa kukamata serikali ya Zanzibar. 1968 tulijiona kidogo. Sababu ni tuliona kuna mabadiliko against [dhidi] yetu. Upepo ulikwisha anza kutugeukia. Karume kaifanyia hii nchi kama moja kwa moja yake, hasikilizi mtu, anafanya anavotaka. Mwisho wake ilikuwa baada ya wale kina Hanga, kina Twala, kina Saleh Saadalla, nani…, sasa alikuwa anamtaka Babu. Ndo akasema hasa, “lipo Hizbu kubwa huko Dar es Salaam, tunalitaka hapa.” Kwenye mkutano wa hadhara. Kweli Babu alikuwa Katibu Mkuu wa Hizbu na ndo maana Karume akasema “Hizbu kubwa.” Sasa anaanza kumtia hewani, kumuandama. Anamtaka yeye kwa kuwa aje au atavunja muungano. Alimwambia Nyerere hivo. Akiogopa kwa sababu wataalamu wote yeye hawataki. Kina Twala, kina Hanga…Yeye na Sefu Bakari kuwa waendeshe nchi wanavotaka, wafanye wanavotaka, hivo ndo ilivokuwa. Baada ya kutangaza hivo sisi tukaitana, hapa Zanzibar na Dar es Salaam, mikutano ilikuwa mingi. Hata mie nafsi yangu nilimwambia Sefu Bakari “mbona upepo unatubadilikia?” Akanyamaza kimya. Nilimkumbusha wakati wa interrogation [kuhojiwa]. Umesahau? Manake alinihujumu “hata wewe, wewe ulikuwa Afro-Shirazi na ghasia?” Nkamwambia “mmetugeukia.” Tukaendelea mpaka tuka-panga mipango. Kila nkiwatia kwenye line hawaingii, kina Natepe, kina nani, lakini Sefu Bakari sikuweza hata kujaribu kwa sababu alikuwa pro-Karume [akimuunga mkono] bila ya kiasi, Ali Mahfoudh alikuwa pro-Karume, akisikia chochote vilevile hatari. Wengi katika Baraza la Mapinduzi walikuwa pro-Karume. Hata Khamis Abdalla Ameir, Ali Sultani, tuliwaogopa. Badawi [Quallatein] baada ya kuhujumiwa Pemba, yeye alikuwa Waziri Mdogo, kahujumiwa na Karume, akageuka. Akabadilika akawa pamoja na sisi. Babu akitushtakia sisi kuhusu Khamis Abdalla Ameir. Ilikuwa linakuja jambo mbele ya Baraza la Mapinduzi dhidi ya Babu, basi Khamis akinyamaza kimya na wala hakuripoti kwa Babu kwa kuwa iko hivi hivi hivi. [Saidi] Bavuai ndo alokuwa anamwambia Babu, mambo yako hivi hivi hivi. Ukisemwa hivi hivi hivi.

Basi tukenda tukafanya mkutano mpaka karibu ya mwisho tena sasa tayari mambo lakini sasa sie watu wenyewe kidogo. Mimi nafsi yangu nimewaambia Hizbu, nimewaambia wale walokuwa Mobile Force wale, Afro-Shirazi nnowaweza wale, nimewaambia. Madhumuni ilikuwa tupinduwe kijeshi. Ikafeli kwa sababu walewale tulowaambia waje, kina [Amour] Dugheshi, kina nani, wote wamefanya woga. Ila yeye Babu ndo amesema kaja mpaka pwani hapo, akarudi. Kina Tahir Ali, wamepanda boti hasa waje. Walipopanda wakaona mambo yameshavuja wakarudi. Mambo hayo lini. Alkhamisi tuliwaambia watu wote waje, tuliagana Youth Tournament inakuja hiyo, kwa kuwa na nyie kabisa, Alkhamisi tuwe tayari. Lakini alokuja mmoja tu. Hashil Seif. Bas. Ndo baada ya kuona tumefeli ndo akapanda Cariboo bado hajajulikana, akarudi Dar es Salaam akakamatiwa hukohuko. Na wengine wengi wamekuja lakini tulikataa kuwataja majina.

Babu ilikuwa aongoze ile coup d’état [mapinduzi ya kijeshi]. Viongozi wangelikamatwa, akamatwe Karume akatangaze kwenye radio, aseme kuwa ameshindwa, na nini. Tulikuwa tuna wenzetu ndani ya jeshi. Walipoona tumefeli wakapinda wote. Sasa wakajifanya wao shrewd against [mahodari dhidi] yetu. Hao wanajeshi waliofanyiwa kampeni na Ahmada, Humudi, etc (na kadhalika)

Sisi tumepanga wiki moja ya kule store [ghala] ya silaha ni yetu sisi, na wiki moja yao wao, Afro-Shirazi. Wale walioko zamuni, wote wale wetu sisi. Kina Sindano, hao walokufa. Na wiki ya pili wanakuwa wao. Sasa sisi tulianza tangu Jumatatu kutowa silaha. Zikakaa kwa Humudi, kiasi mia, silaha mbalimbali, bastola, bunduki, machine gun. Aliziweka kwake. Humudi alimtowa mkewe akenda zake Dar es Salaam, ukumbi mzima zikawekwa silaha. Tungeweka kwa Ahmada ingelikuwa hatari. Niliwaambia tukiziweka kwa Ahmada na yeye Captain in charge wa mambo ya silaha atasachiwa. Na kweli, walishughulika juu ya Ahmada hawakumgusa Humudi. Mpaka saa tisa za jioni silaha hazijajulikana ziko wapi. Mpaka saa kumi. Mpaka magharibi sisi tunaripuwa hazijajulikana zile silaha ziko wapi. Siku ile walipokamata wale ma-ASP ilipojulikana silaha zimeshaibiwa siku ya Ijumaa, manake wiki nzima zimekaa, siku ya Ijumaa zilipohisabiwa hakuna, kina Ali Mahfoudh wakataka kutupiga curfew ile Ijumaa usiku, sisi tukasema hatuwahi.

Humudi ndo alipata ripoti hiyo saa nne asubuhi ndo akatuletea. Kuwa tukamatwe sote siku ileile ijumaa. Saa tisa tumekutana kwa Humudi ndo tukaamuwa. Hapo alikuweko Miraji, Chwaya, Harakati, Humudi, Ahmada, kina Falahy walikuwa chumba cha pili, hawajajuwa tunazungumza nini. Ishajulikana, hapana njia isipokuwa tumpige Karume na Sefu. Kwa sababu wale hawakuja, tutafeli, kina Amari Kuku, Ali Mshamgama, wogawoga, hawakuja kwenye mkutano saa tisa. Wote hawakuja. Potelea mbali. Wale wengine, khasa Saidi [Sindano] alokamata store silaha alikwishasema “tumeshakufa.” Kwa sababu Sindano keshakimbia tangu saa nne ilipojulikana, anatafutwa. Sasa watu wetu tena wakaanza khofu. Kupatikana gari ndo Harakati akenda kuazima kwa Khamis Abdalla Ameir, manake ndo dereva wake. Nna safari yangu nataka kwenda. Sasa Khamis hajuwi anataka gari kwa sababu gani. Hajui, kampa, haya nenda. Chwaya kachukuwa gari ya People’s Bank yeye ndo dhamana. Tena kina Ahmada wakaingia katika gari ya Chwaya, pamoja na…Gari ya Khamisi, Harakati, Saidi alouliwa Vuga. Na Rashid Falahy akaingia palepale Makao Makuu [ya Afro-Shirazi]. Sasa kumi na moja unusu tuseme wametoka, kumi na mbili wameshafika pale, wakaripuwa. Gari ya Chwaya, rangi ya bluu bluu ilitokea Malindi, ya manjano, ya Khamis, ina kipande cha MBM (Memba wa Baraza la Mapinduzi) kimeandikwa, ikapitia njia ya Majestic Cinema.

Iliamuliwa kuwa tumuuwe Karume, tusimuuwe Thabit Kombo. Tumtishe tu basi. Kwa sababu kuweka mgawanyiko, iweko ubaguzi, Karume na Kombo. Wote tungewaweza ati pale lakini tumefanya makusudi tuweze kubaguwa. Afro na Shirazi labda italeta mgongano. Manake Karume ndo “Afro”, yule Thabit Kombo “Shirazi.”

Alomuuwa Karume ni Ahmada. Lakini ile Humudi tumemtaja kwa kisiasa. Tangu mwanzo ndo alisema hasa kuwa yeye ndo atofanya.Tumehakikisha kwa sababu Falahy ndo alokuwepo pale, akaona. Hivo ndo ilivyo.Humudi alizubaa kule akawa anapiga ovyo. Watu wanaondoka wanakimbia, yeye kapiga tu lile hall zima juujuu kule, kutisha, watu washaondoka na gari. Sasa kutoka yeye, sasa hapa kuna kauli mbili. Moja kapigwa kwenye bustani na alikuwepo mtu akampiga, moja inasema alivoona vile hakuna mtu kajipiga mwenyewe.2

Nafikiri walikunywa kidogo. Walipofika Makao Makuu [ya ASP] mimi naona. Nipo pale ice cream club. Naona gari zinavoingia. Walipita pale Ahmada akaninyoshea mkono kuwa tunaingia. Nikawaambia haya kwa ishara ya kidole juu. Nikawaambia, haya! Manake kumpiga yule [Karume] faida itakuwepo. Asaa wale wenyewe wataweza kutanabahi…Iko siku karibu tena korti tunapelekwa, tushapigwa, tushafuswa sote, tukachukuliwa mpaka Migombani. Baada ya korti kwenda wamekubali watu tisa, walobaki wote wamekataa. Sasa wale tisa sote tulikuwa tupangwe tuseme vipi kule korti. Na Dourado alikuwepo, Mandera. Kama mtu kama Nourbhai alikuwa matusi sana kule korti mtajeni manake hakutajwa na mtu. Sasa akalazimishwa Miraji. Kwa sababu mlikuwa China pamoja basi sema wewe ninhi…hakumtaja. Mie nililazimishwa nimtaje Saidi “Tumbo.” Hakujuwa ati, sasa mimi nimtaje nini. Manake yeye hakutajwa vile vile. Lakini kapigwa wee basi kenda katowa statement wiki nzima anataja, mimi hivi nilikuwa hivi. Na hayumo.

[Kutoa amri Karume auliwe] mimi ndo ino ni haunt [inanipa jinamizi]. Inani haunt Naona nimefanya, kiama huko kuna dhambi, au vipi? Naona kama dhambi. Hiyo kusema, tumpige, tumuuwe. Japokuwa yeye kauwa watu wengi lakini. Mara nyengine nahisi, e bwana we, madam kauwa watu wengi na nini, nimesema auliwe, basi, potelea mbali. Lakini wakti mwengine Islamu mwenzio kumtia kwa kuwa auliwe si uzuri. Nna khofu ndani yake mbele ya kiyama. Khofu iko. Inanjia. Babangu alikuwa Hizbu. Ananambia tia tu hapo picha ya Ali Muhsin hata kama humpendi. Namwambia “sitii” na yeye akinfata mie kwa sababu mimi skuzile ndo nkiiendesha nyumba.

Basi sijuwi tuko wapi. Hata sijuwi. Ah, watu wanapinga sana. “Nyie ndo mlotutakia haya.” Hawajuwi madhumuni yake kwa nini tukaingia Afro-Shirazi. Kwa sababu chama chetu kilifungwa na Hizbu. Kulikuwa hakuna njia nyingine. Kilipigwa marufuku chama chetu tukaona sasa tunaninginia. Tena tukaingia Afro-Shirazi. Tukiwaponda Afro-Shirazi kwenye Hizbu tangu mwanzo. Kwa sababu tumefunguwa huku, huku hawatutaki. Tumefunguwa chetu hawataki. Twende wapi?

Haikuwa makosa Babu kutoka Hizbu. Makosa wao waloyafanya kumtowa. Manake kapeleka pendekezo wamelikataa. Basi kama mnalikataa mie natoka. Haya toka. Na wao wakitafuta hiyo. Wakitafuta atoke ili wapate uhuru. Kawaambia Mngereza, yule Koministi na ghasia, na ile wao ikawajaa tele. Mkimtowa sisi tutakupeni uhuru. Na yeye Babu hajajisema kama ni Mkominist. Hata sku moja. Lakini alikuwa na falsafa zake basi Mngereza akasema huyu ni mtu hatari. Sasa mkimtowa tutakupeni uhuru.

Siku hiyo ndo alokuja Sefu, watu tisa tulipokutana. Ndo anaulizwa mmojammoja. Wewe utafanya hivi, wewe hivi. Sasa nilipofika mie akanambia “hata wewe umeshiriki kwenye mambo haya?” Manake mimi kina Natepe wamenitetea kulekule kwenye Baraza la Mapinduzi, kwa kuwa hayumo haiwezi kuwa. Haiwezi kuwa yumo, mtu tunaye tunanhii… Ikasemwa imeamuliwa Makomred wote wakamatwe, tena ndo nkakamatwa. “Mimi si nlikwambia wewe kuwa mbona upepo unatubadilikia?” Kanyamaza kimya [Sefu Bakari]. Ndo Mandera nlipotoka tunarejeshwa gerezani tena, alinambia “unamjibu yule vile ufidhuli angelitwambia pale tukuuwe tungekuuwa tu.”

Sijaogopa chochote. Hata. Haijanijia hasa ile hisia kuwa niogope. Naona nimesema tu kama ilivo kwelikweli. Na ni kweli ati. Na nlikuwa naye kutwa Sefu ati. Aliponiuliza nikamwambia hivo ndivo ilivokuwa. Tena nifiche nini tena pale. Kufa na kupona. Bora mara kumi Natepe kwa fikra zake za kisiasa. Nikimsafiria sana Natepe kuliko Sefu. Tukizungumza manake. “Huyu Karume katuteka kila kitu anafikiri yeye tena, bora huo ufalme.” Tulikuwa tuna jina letu tunamwita Karume, “scandal bag.” Mie, Rajabu Kheri, Khatibu Hassan. Ukisema “scandal bag” manake Karume.

Nimewacha mambo ya dini na ghasia nimekwenda kwenye siasa. Hiyo ndo nnajilaumu. Akili inakujia ati. Wewe binaadamu ati. Na mimi Msikiti Baraza nilikuwa pamoja na huyu alokufa juzi, Zagar. Tumesoma pamoja. Kilochonifanya khasa kuingia siasa baada ya nilipomaliza skuli nilitafuta kazi kote lakini skupata. Tena Mr. Davis akanipeleka pwani, gatini. Naona kila nkenda kufanyiwa mahojiano naambiwa “wewe unaweza wapi kuchukuwa file huku ukaweka huku.” Rohoni mwangu nasema, siku hiyo nanyenyekea ati, lakini ngekuwa najibu ngemwambia “kwani skuli mabuku ukinchukulia weye?” Ingekuwa sasa, ah, ningemjibu hivo. Manake file tu yakhe kuweka huku na huku unanambia siwezi. Na kote nlipokwenda, ustawi wa jamii nlikwenda, afya nlikwenda, wapi, wote, wananijibu “tunasikitika kukuarifu…”

Babu naona ni mtu wa siasa tu. Mie kanivutia maneno yake, u-peasant na working class [wakulima na wafanyakazi]. Naona loh! Mimi tanguwapo nilikuwa trade unionist mwanzo, na nlikuwa 1956 nliingia Dock Workers na nlikuwa General Secretary wa Dock Workers, na Ismaili ndio President. Babu angeweza kuchukuwa serikali angelikuwa kiongozi mzuri. Mpaka leo naamini hivo, lakini hakubahatika, na kuna uwezekano wa Mwenyezi Mugu hapo tena, au vipi? Alikuwa mtu mfanyakazi wa kwelikweli, masaa ishirini na nne ukimwendea anafanya kazi.

Baada ya Natepe nnomjuwa mie basi. Kina Twala mimi sikuwa na uhusiano nao sana. Kassim Hanga na kina Babu, na Hassan Nassor Moyo.

 

Wasia wa Zanzibar wa Hayati Rais Samora Machel—J. J. Mchingama

Marehemu Samora Machel wakati alipokuwa karibu na kupata uhuru alitembelea Zanzibar mwaka 1972 kabla kidogo tu kabla ya kuuwawa Karume. Alikuja juulisha kwamba sisi karibu na ukombozi wetu, karibu tutapata uhuru, na kwamba ukoloni umeshaanza kufikia ngazi ya kushindwa. Tayari wanafanya mazungumzo ya kumaliza vita baina ya Mreno na wananchi wa Msumbiji. Pale alielezea, alikuwa anaongea na Makamanda wa kijeshi Migombani kwamba sisi Mozambique ukombozi tunaoufanya tunatafautiana na ukombozi mlioufanya nyinyi Zanzibar. Nyinyi mmekombowa Zanzibar kuondowa utawala lakini bado wananchi hamjawakombowa kifikra. Sisi Mozambique tunajikombowa kuondowa utawala na kumkombowa mwananchi kifikra bila ya kujali ukabila, rangi, dini, au asili ya mtu, au jinsia. Hapana. Tunasema wote ni watu wa Mozambique. Awe Mmakuwa, au Mmakonde, awe Mwarabu, awe Mreno. Mreno mwenyewe akikubali kwamba mimi ni mwana Mozambique na nakubaliana na matakwa ya FRELIMO, huyu ni mwenzetu. Hatumkatai kwa sababu alitawala.

Lakini nyinyi Zanzibar, bado watu wamekuwa na fikra finyu. Bado watu mnayo matabaka. Bado watu mnajaliana sana asili, kabila, rangi, jambo ambalo si ubinaadamu. Nitamleteeni matatizo siku za baadae. Wakati anazungumza Ali Mahfudh alikuwa amefatana nae. Ali Mahfudh huyu anajuwa ukombozi wa Mozambique ulivofanywa na anaona tunavofanya mpaka sasa. Kweli mnajitawala. Bendera mnayo, utawala mnao, lakini watu bado wana fikra zile zile za kumuangalia mtu huyu ni fulani, huyu ni fulani. Huo si ukombozi. Akaondoka Samora. Haikuchukuwa muda, kama wiki mbili tu, tukasikia kwamba Abedi Amani Karume ameshauwawa. [Wengine] wakasema bila shaka Samora alikuwa akisema vile kumbe alikuwa anajuwa huu mpango! Zile zikawa fikira finyu. Yeye alizungumza kama kiongozi jinsi alivoona upeo wake.

Mimi kukaa na wewe sasa hivi basi kama atapita mtu mwengine ataona, unajuwa bwana, tumemkuta Mchingama JJ amekaa sijui wanaongea nini na yule Mwarabu? Sijui niongee nini wakati wewe ni binaadamu mwenzangu? Na mtu mwengine atasema. Yule Mwarabu kimempeleka nini kwenye kituo cha FRELIMO? Vipi yule, kakaa na Wamakonde anazungumza nao. Hawawezi kufahamu. Hicho ndo kiliopo hapa Zanzibar. Bado ukombozi wa fikra.

 

Abdalla Kassim Hanga: Wasia wa Mwisho—Mzee Salum

Kwanza ningelipenda tuzungumze kutoka mwaka 1963 na 1964. Kwa sababu huo ndo wakti muhimu kwa mambo yale ya Unguja na haya tunayotafuta. Na vile vile muhimu kwangu mimi kuwa mimi nilikuwa nimeshaondoka Zanzibar 1963, niko Nairobi na nilivofika kule nikaombwa na umoja wa mapinduzi ya Ngazija kuwa niwe Katibu Mkuu wa MOLINACO. Nikaifufuwa MOLINACO Nairobi na nikabadilisha mikakati yake. Kabla ya hapo Katibu Mkuu wake alikuwa ni mwalimu Zanzibar na wengine wawili walikuwa wakitia vifungo kwa Bwana Ali Barwani.

Ni harakati ya kiukombozi ya Comoro ili kumtowa Mfaransa. Na nilikubali na katika watu ambao walikuwa mbele katika hiyo kamati ya ukombozi ya MOLINACO, Nairobi, alikuwa kijana mmoja Ahmed Abdalla Mbamba ambaye yeye ni mmoja katika walorejea Ngazija na wakawa wakubwa wa mapinduzi ya Ngazija na yeye aliuliwa pamoja na Rais Ali Saleh walivoingia hawa Wazungu kutoka South Africa. Mwengine kijana akiitwa Kenya, jina lake silikumbuki.

Sasa wakati mimi niko pale kama ni Secretary General nilikwenda mbele kufanya usajili wa kukubaliwa na Organisation of African Unity (OAU) kuwa MOLINACO ikubaliwe. Ilikuwa imeshakubalika kwa Dar es Salaam lakini hichi kipande cha Kenya na Uganda kilikuwa ni chengine. Uongozi ni wangu mimi na sio ule wa Dar es Salaam. Wakati ule nikaweza kujuwana na viongozi wengi wa serikali mpya ya Kenya, mfano, Mzee Mdiu Kaunange ambaye ndo alokuwa wa pili baada ya Kenyatta. Alikuwapo Tom Mboya ambaye ndo kila mtu akimjuwa, akimuelewa, alikuwa ni Waziri wa Mambo ya Biashara na Viwanda. Oginga Odinga alikuwa ndo Waziri wa Mambo ya Ndani na ni mtu mzito vilevile kwa pale, anakubalika Kenya na wengi nao ambao walikuwa pale, walinikubali mie kuwa huyu ni kijana ambaye anapigania uhuru wa Comoro.

Ama Oscar Kambona tumeweza kujuwana kwa yeye alivokuwa akija Nairobi. Nimejuwana naye kwa kujuulishwa na Tom Mboya na alipokwishajuwa kuwa mimi ndo nnaendesha MOLINACO pale, nasimamia MOLINACO, akafurahi kuwa ni Mzanzibari anoshughulikia mambo hayo. Kwa hivo jambo lile lilimfurahisha na akanambia kuwa hata nikihitajia msaada wowote, tangu wa pesa na venginevo yeye atakuwa nao uwezo wa kunisaidia kwa sababu yeye wakati ule ndo alokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ukombozi (ALC) ya OAU. Hapo ndiyo nilipojuwana naye Kambona.

Sasa wakati ule yeye ndo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanganyika, au Tanzania kwa sasa. Ilikuwa wakati ule bado 1963. Muungano haujakuwa bado. Kwa vile yeye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje akija sana Nairobi na kurudi, na kila akija ikiwa Tom Mboya kapata habari hunipigia simu na kuniuliza kama mzee yuko hapa ukiwa utataka kuonana naye basi kama kuna jambo lolote mie nlikuwa nakwenda kumuona. Niliwahi kuonana naye kama mara mbili tatu pale Nairobi. Sijaonana naye tena kwa sababu niliondoka Nairobi Septemba 1964 kwenda Ungereza kusoma. Na nlikuweko kule Ungereza kutoka 1964 mpaka 1969.

Kabla ya hapo mnamo mwezi wa October/November 1963, nilionana supermarket in Nairobi na Chief Clerk wa City Council of Nairobi ambaye alikuwa chini ya Meya wa Nairobi. Akanambia “Iko wapi wewe Mswahili? Nasikia iko matata Zanzibar. Sisi tunapata uhuru na jirani yetu anatawaliwa na Mwarabu, tena Muislamu.3 Hii Aibu kubwa! Unapata uhuru halafu unatawaliwa! Kweli itakuwa hii? Ipo karibu sana.” Nikampa barua mbili [jina nimelihifadhi]. Moja ampe mke wangu, ya pili ampelekee Zaim (Sheikh Ali Muhsin). Marehemu Sheikh Yahya Alawi aliwahi kuniambia “wameendesha serikali gani hawa (ZNP) hata ukawavulia kofia?”

Wakati ule Idhaa ya Zanzibar ilikuwa imetawaliwa na utamaduni wa Kiarabu dhidi ya Bara. Mimi niliiunga mkono ZNP kwa sababu mbili: moja ni shetani unayemjuwa, na pili, chama kilikuwa na ilani ambayo ilitayarishwa na Babu. Baada ya Mapinduzi Babu alimchaguwa jamaa yake Omar Zahran mwenye asili ya kutoka Yemen awe Rais wa Zanzibar chini ya utawala wa Chama cha Umma.

Jumaatatu tarehe 13 Januari Mboya akaniambia kuwa Oscar Kambona yupo Nairobi na anahitajiya msaada. Nyerere alimtuma amtake Mzee Kenyatta atumie ushawishi wake awazuwie Waingereza wasiingilie Zanzibar. Nyerere pia alimtaka Kambona aziombe Kenya, Uganda, na Tanganyika waitambuwe Serikali ya Zanzibar na pia kuziomba serikali za hizo nchi tatu wasaidie kijeshi au kwa njia yoyote ile nyengine. Akanambia Mboya kuwa ujumbe kutoka Uganda ulikuwa uwasili siku ya pili na mkutano ulifanyika kwenye uwanja wa ndege wa Nairobi tarehe 14 Januari. Hakukuwa na waandishi wa habari, hakuna ruhusa kupiga picha na wala kuweka rekodi zozote zile. Tanganyika iliwakilishwa na Oscar Kambona. Kutoka Uganda alikuja Milton Obote na Mawaziri wake wawili. Inawezekana ikawa nachanganya majina. Mmoja alikuwa Lulee aliyewahi kumuowa Mjapani, wa pili, ni Godfrey Binaisa ambaye ni bingwa wa sheria na aliwahi kusema kuwa Othman Sharif hatopumzika mpaka aupate Uraisi wa Zanzibar. Kutoka Kenya alikuwepo Tom Mboya na Joseph Murumbi. Obote alikuwa akipinga moja kwa moja mipango ya Tanganyika. Alisema “Hatuwezi kukubali kupeleka silaha kwa nchi jirani. Hawa ni watu wamoja. Tuwaachiye wayatatuwe matatizo yao wenyewe kwa wenyewe.” Abubakar Mayanja alikuwa Minister of Education ilikuwa aje kwenye mkutano wa uwanja wa ndege wa Nairobi lakini hakuweza kuja. Mboya aliniambia kaa kimya uyasikilize mambo ya kwenu [Zanzibar]. Kambona aliendelea kusisitiza kuwa serikali mpya ya Zanzibar inahitajiya kutambuliwa, silaha, na pesa.

Kwa upande wa Tanganyika msukuma gurudumu mkubwa alikuwa ni Katibu Mkuu na Mshauri wa Nyerere na Kawawa na rafiki wa karibu sana wa Nyerere, Bhoke Munanka. Paul Sozigwa, aliwahikuwa mtangazaji na mwenzake David Wakati, alikuwa ni Katibu Mwenezi wakati wa mapinduzi. Kulikuwa na Wazanzibari ambao walijiunga na TANU kama Shaaban Ame, Rajab Saleh na David Wakati ambaye alikuwa Katibu Ofisi ya Rais na mtangazi mkuu wa Idhaa ya Tanganyika. Rajab Saleh alikuwa Katibu Mkuu wa pili wa Baraza la Mapinduzi baada ya Salum Said Rashid. Unafikiri kwa nini?

Mwaka ule wa 1968 au 1969 ndo tukajuwa kwamba Oscar Kambona kaja [London] na nkawahi kuonana naye, ndo sku hiyo akatuletea habari kuwa anataka kuonana na sisi. Na alokuja kutupokea station [kituo] ya treni alikuwa ni huyu bwana, Kasembe. Na nilikuwa mimi na Ahmed Rajab. Ikawa Muhammed Nura maskini hajaja. Tukenda mpaka nyumbani kwake Oscar Kambona, tulipofika kupiga kengele alofunguwa mlango ni yeye. Ni fleti first floor [ghorofa ya kwanza]. Tumeingia akatuvuta upande.

Sasa tulivokuwa London yeye [Ahmed Rajab] kataja watu watatu tu. Kasema namtaka Ahmed Rajab wa BBC, na namtaka huyu kijana Muhammed Nura, ambaye ni kijana wa Kizanzibari ambaye alikuwa keshamaliza Masters yake pale na nnaskitika kusema Muhammed Nura hajaja katika mkutano huo na sasa amefariki, hayuko hai. Yeye si mtu wa BBC. Na yeye Oscar Kambona alimtuma kijana mmoja wa BBC, Kasembe anaitwa. Mtangazaji maarufu yeye tangu Tanganyika, Tanzania kwa sasa, na BBC katangaza sku nyingi sana. Baadae alirudi nilionana naye Arusha alifanya kazi East African Community na alikuweko katika ofisi of the agent wa public trustee [wakala wa amana ya umma] wa East African Community Arusha. Yeye ndo alokuwa in charge [mhusika] pale Arusha.

Nnavokumbuka mimi Oscar akatwambia sikilizeni bwana. Mimi nimekwiteni hapa mje mseme na ndugu yenu na mzee wenu huyu, Abdalla Kassim Hanga amekuja hapa na anataka kurudi nyumbani. Hajataja pahala. Na mimi nimemkataza. Nimemwambia huu si wakti mzuri ni bora yeye asiende. Ama angelibaki huko huko West Africa anokotoka kwa mkewe, au abaki hapa London lakini kakataa, anataka lazma arudi. Na mie na hofu maisha yake kuwa akifika kule hatoweza kupata salama. Kwanza kuwa yeye amefikia kwangu, anajulikana yeye na mimi ni rafiki, Nyerere atajuwa zaidi/uzuri hayo kuwa mimi tangu tuko kule tunasikilizana mimi na ndugu huyu Abdalla. Kwa hali hiyo mimi namwambia. Na yeye Abdalla anasema hana ugomvi na Nyerere.

Sasa mimi nimekwiteni mzungumze naye, mseme naye. Akatuchukuwa akatupeleka kwenye chumba akasema “Abdalla, hebu zungumza nao hawa jamaa wamekuja kukuamkia.” Tukaingia sie chumbani akatuacha mimi na Ahmed [Rajab] na Abdalla. Peke yetu watu watatu. Ndivo navokumbuka mie na ndivo anavokumbuka Ahmed [Rajab].

Mimi sikumbuki ile nilikwenda railway station. Kile mimi sijakumbuka. Kama ulivosema, mimi nyumba nilikuwa naijuwa, sina haja ya Kasembe kunpeleka. Lakini inaweza kuwa nimekwenda mimi na Kasembe kumpokea Ahmed Rajab. Yeye Ahmed kafkiri tu na mie ni mgeni. Hajajuwa kuwa mimi na Kambona tunajuwana na jirani, na nyumba yangu mie na yake si mbali.

Ahmed Rajab ndo anosema, tumefika alofunguwa mlango ni Oscar Kambona, na akatuonyesha chumba. Hajaeleza nini Kambona katwambia. Lakini mimi nakumbuka Kambona katwambia kwanza, “semeni naye.” Yeye kazungumza moja kwa moja, sisi tumekaribishwa tumekwenda kwa Abdalla. Yeye Ahmed amekumbuka mambo mimi sijayakumbuka. Kwa sababu, kasema tulipofika Abdalla Hanga katwambia skizeni: nyinyi ni vijana, watoto kwa sasa, lakini kesho nyie ndo mtakuwa viongozi. Nna maneno nnataka kukwambieni. Tukawa sasa tumekaa tunamsikiliza nini atasema.

Anasema nataka kukwambieni juu ya habari ya mapinduzi yetu ya Zanzibar. Kuna mabaya ambayo tuliyafanya na kabla sijasema lolote nnakutakeni jambo moja muhimu mlikumbuke. Msije mkakubali kufata siasa za ukabila.4 Siasa za ukabila ndizo zinotuletea matatizo na ndizo zitozidi kutuletea matatizo. Hilo ni jambo la mwanzo ambaye yeye Hanga katwambia. Akasema mimi (Hanga) nilivoondoka Zanzibar kupelekwa Dar es Salaam, kuwa Waziri wa kule, badili ya kuwa Vice-President [Makamo wa Rais] huku na Mzee Karume, alivopelekwa bara, anasema jambo moja katika mambo aloyafanya ni kuwasaidia Wazanzibari walokimbia kutoka Zanzibar wakakaa pale, wale ambao wataalamu, kuwatafutia kazi. Akataja majina. Akamtaja Maalim Salim Sanura, na akawataja wengine, mimi siwakumbuki. Kuwatafutia kazi na wakapewa kazi serkalini. Hata ikafika akaanza kusemwa, akalaumiwa, kuwa Abdalla, mbona unakwenda kinyume sasa? Hawa si ndo tuliowapinduwa, mbona wewe sasa hapa unawasaidia? Unawapokea? Akasema bwana, hapa mimi naona ni Mzanzibari tu hapa. Hawa wote ni Wazanzibari bwana. Na hawako nchi nyengine. Wako na sisi pamoja hapa. Kwa hali hiyo yeye anasema ule ndo uzi anataka sisi tuufate. Tusibaguwane.

Jambo la pili akasema, sisi Mungu atusamehe, tumefanya mambo mengi ambayo mabaya, tumedhulumu, tumechukuwa watoto na wake za watu, na Mwenye Enzi Mungu ndiye anojuwa. Basi mimi namuomba Mweye Enzi Mungu anisamehe na ninajuta kwa haya nlioyafanya. Ahmed Rajab akamuuliza suala. Akamwambia, mzee, lakini wewe na Janab [Babu] mnaskizana vipi kisiasa? Akamwambia, mimi na Babu sote wawili ni Marxists lakini Babu si tishio kwa Karume. Mimi ndo tishio. Mimi ndo ni tishio juu ya Karume, lakini Babu is not [si tishio]. Hiyo tafauti yangu mimi na Babu, anasema. Kwa Unguja. Sasa ndio tukamuuliza, Vipi ikawa wewe ndo tishio? Yeye Ahmed Rajab ndo anamuuliza.

Rome ilijaribu kuingia kati katika ugomvi wa Oscar na Nyerere na ilishindwa. Kambona alinieleza. Hata makanisa yamejaribu. Ugomvi ulikuwa mkubwa na hiyo akijuwa yeye zaidi Kambona ndo mana akahofu Abdalla asirudi. Ile imani yake ilikuwa kubwa kuwa Nyerere hatomdhuru. Na yeye akiona watu wangapi wamepotea lakini hajafikiria atakuja kuwa yeye.

Tukasema naye tukamwambia kweli hayo maneno anayoyasema Oscar inaonyesha ni bora usirudi kwa sasa. Akasema hapa kuna mambo mawili. Moja, kuna kutosikilizana baina ya Oscar Kambona na Mheshimiwa Nyerere, Raisi Nyerere. Sasa huyu bwana akisema mimi nisirudi anazungumzia kule kutosikilizana baina yake yeye na Raisi Nyerere. Sasa anahisi mie nikirudi labda kwa sababu mimi nimefikia kwake au ni rafki yake Nyerere anaweza akachukuwa hatuwa. Mimi nimeshafanya kazi na Nyerere na namjuwa uzuri mzee Nyerere, mimi na yeye hatuna ugomvi wowote. Abdalla Kassim Hanga anasema kuwa yeye na Nyerere hawana ugomvi. Na yeye ikiwa anarudi harejei kwa Zanzibar. Atarudi anakwenda zake akakae nyumbani Dar es Salaam. La pili alisema, kuna ukweli wa kuwa mimi na Mzee Abedi Amani Karume kuwa hatuskizani na kusema kweli si makosa yangu. Akasema Abdalla, jambo dogo sana limemfanya Mzee Abedi anichukie mimi hata ikawa mimi nikienda Zanzibar sasa siwezi kukaa nikalala Zanzibar. Lazima siku ileile nirudi Dar es Salaam.

Na hili jambo anasema, mimi nilivokuwa niko Tanzania Bara na Dar es Salaam ni mmoja katika Mawaziri, nilikuwa nnakwenda Zanzibar mara kwa mara. Na nikenda nikifia katika nyumba ilioko Migombani ambayo niliwahi kukaa nilivokuwa Makamo wa Raisi. Wakati mmoja nafikiri baada ya mapinduzi, President wa Zanzibar alikuwa ni Karume na Makamo alikuwa Hanga. Sasa ile nyumba ya Migombani ikawa yeye bado Hanga hajairejesha serikalini kila akienda Zanzibar anafikia pale. Siku katika siku alizokuweko pale anasema yeye kaja kafikia nyumbani pale Migombani na kila akenda watu wakipata habari kuwa Abdalla kaja, watu, jamaa, ndugu na marafiki, walikuwa wanakwenda kumuona na kuzungumza naye, na wengineo wanakuwa nayo mahitajio yao wanakwenda kumuomba awasaidie. Sasa sku moja hiyo Mzee Karume anatokea njia ya uwanja wa ndege kwenda zake mjini akapita pale Migombani akaona magari, akauliza. Kuna nini hapa, mbona magari mengi? Akaambiwa basi lazim Mzee Abdalla Kassim Hanga kaja. “Ala, sasa yeye kila akija lazma iwe namna hii?” Akaambiwa, yeye akija watu wanakuja hapa kumuamkia na kuonana naye. Basi jambo hilo anavosema Abdalla Kassim Hanga ndilo liloanzisha ugomvi baina yake na Mzee Karume. Karume akawa hataki tena na ikawa na yeye Abdalla akenda Zanzibar hafikii tena katika nyumba ile. Akakataa kabisa.5

Lakini inaskitisha kuwa tangu wakati ule yeye yupo pale London habari zishafika Cairo. Walioko Cairo maambassador wa pale wameshapeleka habari Tanzania kwa Mzee Nyerere. Ikawa serikali ninavosikia wamekaa wakimgojea arejee tu. Yeye Hanga hajajuwa, wala sisi hatujajuwa.

 

Tupendane na Vifo va Kina Hanga—Mzee Selemani

Tupendane wakawa wanaendelea na shughuli zao. Wameshahifadhika. Sasa kurupushani waliokuja kuifanya Tupendane, ndo tukasema, bwana hadithi zao kuzieleza hakika tishio, tunaogopa. Manake kuogopa kwenyewe kwa kwamba vipi? Unajuwa Tupendane baada ya kuja mapinduzi hapa, Tupendane wapo, lakini chini kabisa huko! Chini kabsaaa! Huwaoni. Wala zile suruwali hawavai tena. Lakini Tupendane ilikuwa iko pale pale baada ya mapinduzi. Karume alikuja kuwaita “njoni nyote.” Wakaja. Bwana we, mapinduzi haya tayari lakini kazi nnayokupeni, watatu nyinyi ntakupeni kazi. Wachunguzeni hawa. Kikosi hiki hiki, kichunguzeni. Kuja chunguzwa kile kikosi, matokeo yake, ikaonekana Othmani Sharifu kutoka Mrekani alikokuweko Ubalozi kufika hapa alimfata Twala, alimfata Hanga, alimfata nani huyu… Saadalla. Wakaambizana, huyu mtwana wa Mungu huyu katoka Nyasaland huko kaja hapa, leo sisi atutawale, lakini Hanga alisema. Jee, ikiwa huyu katoka Nyasaland, haya mimi Mzaramu niliotoka huku [Tanganyika] mnanihisabu kundi gani? Itakuwa ina maana kwamba hata huyu akafa leo mimi sina thamani. Othmani akamwambia hapana. Wewe ndie sisi tunayetaka kukuvisha kilemba cha nchi hii kwa sababu wewe msomi ati. Wewe Makamo unawawakilisha watu Uingereza, Marekani, wapi, nchi zote. Huyu [Karume] wapi alikokwenda? Hakupoo. Bwana yule kaingia tele. Kuingia tele, matokeo yake, hawakujuwa kwamba kikao kile walichokutana kilikuwa kama Mungu kawalani.

Alikuwepo Ramadhani Juma, Mzaramu huyo, halafu akawepo Mohamed tukimwita Mohamed “Mkunjeke” kafariki mwaka jana, huyu mtu wa Rufiji huyo, alikuwepo Ramadhani Asumani Bakari. Huyu ni mtu wa Masasi. Watu watatu hao.

Kikazi watu watatu hao walikuweko “Health Office.” Wote hao kazi yao ilikuwa “afya”—health office. Kuja mapinduzi Mohamed “Mkunjeke” kapelekwa kwa “Bwamkwe” [Hassan Mandera]. Usalama. Halafu mmoja, akapelekwa wapi? Pwani. Huyu Ramadhani huyu. Tupendane hao. Kumbe siku ile kunaamulia mambo kama yale, kumbe, huyu nani… Musa Maisara kakaa chonjo pale, anaskiliza tu. Hasemi wala hanyanyuwi mdomo wake. Akatoka. Akakutana na nani? Akakutana na Mohamed “Mkunjeke.” Mohamed, hebu njooo. Yaliopo unayajuwa? Siyajuwi. Bwana we, hawa wanakusudia wamuuwe huyu Mzee Karume lakini kilemba hichi, nafasi hii, wanataka kumpa Hanga. Hanga anasema ikiwa nyinyi mnamsema huyu leo Mnyasa, mimi Mzaramu, vipi, inaa maana hata mimi vilevile ntakuwa uhai wangu haupo. Huyo alosema Hanga atakuwa mtawala wa nchi hii kauli hiyo aliitamka nani? Akasema Othman Sharifu ndie aliezungumza maneno kama hayo. Ikachukuliwa ripoti ile moja kwa moja mpaka kwa mzee Karume akenda akaambiwa.

Kuambiwa, akasema hapana. Nimeshayasikia, lakini nnachotaka nipatafute pahala wanapokutana hawa. Wakikutana kina Othman Sharifu, akina Jaha Ubwa, Mdungi Usi hao, wanakutana. Hata siku hiyo akawaambia ngojea. Ikachukuliwa tepu ikenda kuwekwa chini ya meza. Ikafungiwa kule. Yoote yale, yalipomalizika kanda akapelekewa Mzee Karume. Akaisikilizaa, akawaambia, alaa, kumbe masuala yenyewe ndo kama hivi? Hapo nnakumbuka sasa, Mohamed “Mkunjeke” akiwa yeye ni Tupendane, akatoka akamwambia Mzee Karume, sasa wewe una utaratibu gani? Kwa sababu ajiziajizi matokeo yao huwa ndio. Sasa una mawazo gani. Aaa, wewe mfate Kisasi, na mfate Yusuf Himidi. Wakafatwa wale, kuja pale, likajadiliwa lile sualaa. Yusufu unajuwa alikuwa ni mtu mapresha. Anamwambia, bwana, unaweza kufilia mbali weye. Hawa watu hawa, ni wasomi hawa. Wana mipango ya kila aina hawa. Kwahivo watu kama hawa uwaondowe na mapema hawa. Hawa uwaachishe kazi na mapema hawa. Mzee Karume akamwita Kisasi. Kisasi njoo. Nnachokwambia, hawa watu hawa, wafanyie kazi, lakini usiwapeleke kwenye upelelezi uwemo u-CID ikajulikana. Wafanyie kazi. Nakukabidhi Tupendane hawa. Ikabidi ile kazi inakwenda chini kwa chini. Chini kwa chini.

Mzee kuja kuita mkutano People’s Palace, hapo sasa ndo palipokuwa pametoka kizaazaa cha Saadalla katowa bastola mfukoni kutaka kum shoot Mzee Karume. Siku ile ikabidi kamatakamata. Yeye, akina Jaha Ubwa hao, ndo mwanzo wa kuchukuliwa kundi la akina Othmani Sharifu, akina Hanga, akina nani, kuchukuliwachukuliwa. Kiinuwa Miguu. Kupelekwa kwa “Bwamkwe.” Matokeo yakee, akawaambia, kumbe fadhila ya punda mashuzi. Mimi nimewaweka mistari wa mbele vyeo vikubwavikubwa, leo matokeo yake wanataka kunigeuzia mimi, basi nawaanza wao mie hawa. Wakaitwa Tupendane wote wakaambiwa, wale kaburi lao likachimbwe Kama. Kachimbeni Kama.

Limechimbwa handaki na Tupendane bwana. Likachimbwa lile handaki. Moja tu. Hayakuchimbwa mawili bwana. Moja tu. Akawaambia, haya. Kuchukuliwa wale jamaa, walivopelekwa kule, kila mmoja, tupwa mle, tupwa mle, sasa kila anayetupwa, chuma! Kila anayetupwa, chuma! Haya. Mchezo ukamalizika, wakafukia jamaa pale. Kurudi. Mohammed “Mkunjeke” nafsi yake mwenyewe ananihadisia. “Selemani, mambo mazito sasa hapa nchini.” Vipi? Ananiambia, “bwana we, kina Othmani Sharifu wanaambiwa wamesafirishwa wamepelekwa bara, si kweli.” Nikamwambia ilio kweli ni ipi? Akasema tumekwenda kuwazika Kama. Nikamwambia “muwongo wewe.” Akanamibia alaa! Tafuta siku wewee, tafuta baskeli, mimi yangu nnayo.

Kweli, tukapanda baskeli mpaka Kama. Akanambia jitie kama unakwenda chooni. Hapa tulipofika hapa. Jitie kama unakwenda chooni. Utalikuta kaburi hapo chini ya midodo. Chini ya midodo. Nakwenda kweli nakuta kaburi moja, ah! Nikatazama. Pale pale, mimi nkatoka nkajifanya kama nachuchumaa pahala hivi. Kwasabu mimi isije ikawa kama mtu ananiona kama nimekuja kutazama tu pale. Unaona? Nikajitia kama kuchuchumaa pahala hivi halafu nikatoka pale, huyo nikamwambia “nimeona” akasema “basi hapo.” “Lakini wewe, wewe, wewe…” Kurudi kule ananiambia Hanga yuko pale, Othmani [Sharifu] yuko pale, Jaha Ubwa yuko pale, Mdungi Usi yuko pale. Anasema sisi tulikuwa ndani ya gari kama ni wachukuzi tumewafunga vitambaa veusi, sisi ndio tuliofukia.

Baraza la Mapinduzi ndilo lilouwa. Lakini sasa bunduki walikuwa nazo askari. Ni haohao wanajeshi hawa. Walitolewa watatu, na bunduki zao. Watatu tu. Haina haja ya kwenda mkururo kule ati. Watatu tu. Anaangushwa chuma kinapigwa. Anaangushwa chuma kinapigwa. Mpaka wamemalizika. Karume alikuwepo. Yumo uchungu kwa namna alivomfikiria yule mtu alivomuweka. Kassim, hata weye? Hata weye unathubutu weye? Alikuwepo mwenyewee, Karume. Ndo mwenye kichwa cha Tupendane ati. Wale majeshi waliambiwa ”tusikie hadithi tu basi na nyie mtakuja hapa!” Kimyaa! Sasa kimya kile kimekwenda sababu, imekuja vipi, kwamba kati ya hao wanajeshi mmoja akiwepo huyu Issa Kibwana!

Katika hao watatu, mmoja ni huyu Issa Kibwana. Ehee, wakati huo yuko jeshini yule ati. Kugeuka utakuja kukuta baada ya jeshi na huku Tupendane! Unasikia hapo sasa? Ndo ukaja ukamuona Issa anakwambia “leo nikajiseme, mimi ndie niliofanya tendo hili. Pagumu?” Yeye kachukuliwa jeshini kwa kazi ile. Kufika pale, hakuna cha kusaidiwa. Mzee Karume anasema “piga sasa. Piga!”

Kulikuwa na askari wengine wawili, mmoja alikuwa Mkamba, lakini Mkamba mwenyewe huyu, baadae, baada ya kustaafu kazi aliondoka akenda kwao Mombasa, Kenya. Mmoja huyu tukimwita Benedicto, kijana mmoja wa Kingoni. Benedicto baada ya kustaafu akakaa hapa akafikwa na maradhi, tumekwenda kumzika Kwerekwe. Kafia hapahapa. Watatu hao. Mkamba, Mzee Issa, Mruguru, na Benedicto. Mimi hayo nisingeyajuwa isipokuwa Mohamed “Mkunjeke.” Hii siri ni kubwa mno kwa sababu utakuja kukuta chairman [mwenyekiti] [Karume] mwenyewe kashiriki.

“Mkunjeke” alipelekwa kwa “Bwamkwe” ili wale wakorofi wakorofi wale watakutana na “Mkunjeke.” “Mkunjeke” hana mswalie. Hana msalie. Akikwambia bwana vua nguo, vua nguo. Tumbukia karo hili, weka! Mtumbukizeni huko kwenye karo, funga karo! Unataka kubughudhi hapa? “Mkunjeke” Mkunjeke kweli! Alikuwa Mkunjeke kweli. Namba kumi na moja huyo bwana.

Mdengereko so anachanja humu? Hataki masihara bwana. Hataki masihara huyo. Ukatili wake na wa Sefu [Bakari] sawasawa. Tupendane, historia zao, na kutokana na yale walioyafanya, ikaonekana, hawa bwana, Tupendane, hawasifikani tu lakini mambo walioyafanya Tupendane makubwa.

Mwalimu Nyerere na Visiwa va Ngazija—Mzee Salum

Mzee Nyerere, baada ya ule muungano na Zanzibar, fikra zangu ni kuwa alishindwa kuunganisha Uganda na Kenya wakawa kitu kimoja. Ile ndo ikawa ishavunjika. Basi akabadili mawazo yake. Akaona bora aendelee na ule ule mpango wake, kama alivofanya Zanzibar, aviunganishe vile visiwa. Visiwa va Komoro na visiwa va Seychelles vikaingia ndani ya plani. Ikawa yeye akapeleka majeshi Seychelles kumsaidia yule President alioko pale katika uchaguzi na nini, na akaleta na Komoro vilevile.

Kwa wakati huo alikuwa Ali Saleh, ndo huyo kishapinduwa kamuondowa Mfaransa. Kina Ali Saleh wakatowa maneno bora Mfaransa aondolewe moja kwa moja. Sasa kina Ali Saleh yeye alikuwa Waziri tu wa Ulinzi lakini alikuwa ana nguvu na Raisi alikuwa akiitwa Said Ibrahim wakati huo. Wakapasisha kunako Bunge lao la Ngazija kuwa Mfaransa hatumtaki hapa kabisa sasa. Hatutaki ulinzi wao, na wala hatutaki wakamate mambo yetu na nchi za nje. Hii ilikuwa 1975–76. Ilivokuwa wao kisharia wameshapasisha pale Wafaransa wakahamaki sana, basi wakatoa na wao kuwa masaa arubaini na nane wataondoka Ngazija. Masaa arubaini na nane. Kwa sababu walijuwa Ngazija haitoweza kusimama bila ya wao.6 Sisi tunatoka, hakuna mambo tunakubaliana mkataba wa miaka miwili au mitatu au nini. Hamtutaki sisi tunaondoka kesho! Madege yakaanza kuja, na nini. Serious! Na wakafanya sabotage nyingi. Magari yao walijuwa hawachukuwi basi wakayatia chumvi, na nini, kunako petroli. Hapati mtu kitu! Kwa sababu walihamaki sasa. Wakatangaza, Komoro ikatangaza, kama sasa wanahitaji msaada na nini. Hawawezi kuiendesha nchi. Hawana maengineer wa uwanja wa ndege, hawana maengineer wa kituo cha matangazo—redio.

Mimi nikajitolea. Nikaawaambia kazini kwangu kule East African Community nina ujuzi wa radio. Nilifanya kazi Radio Uganda, Radio Zanzibar kabla, na sasa niko na East African Community, nikisimamia Civil Aviation Engineering. Nilipata mafunzo kutoka Board of Trade in England kwa muda wa miaka mitano, ambayo nafikiri ilikuwa Wizara ya Ulinzi. Sasa mkinipa ruhusa nitakwenda kufanya uchunguzi Ngazija na wanahitajia kitu gani. Wakati huo niko Nairobi. Nilikuwa mkubwa engineer, mkubwa wa operations, wakati huohuo nilikuwa Chief Instructor wa East African School of Aviation. Wakakubali nende Ngazija. Na hii ilitoka juu kabisa kwa sababu tulipewa ruhusa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa kifupi niliruhusiwa kwenda Komoro. Nilikwenda na nikakaa wiki moja au mbili. Nilionana na Mawaziri wa pale, mmoja wao alikuwa Ali Saleh ambaye baadae akawa Raisi na tukazungumza kuhusu njia ya kuchukuwa katika kuisadia Ngazija. Jumuiya ya Afrika Mashariki inaweza kusaidia, nchi za Afrika ya Mashariki zitaweza kusaidia. Basi nilikwenda tukafanya vile. Mimi niliona kuwa hawana engineers na ndio kwanza wamemaliza kuujenga uwanja wa kutuwa ndege. Airport nzuri yenye vyombo vipya. Kuna transmitters na nini…ukiwa ni kisiwa na unataka kuwasiliana na ndege inayoondoka kuulekea Afrika ya Kusini kwa mfano,, au Dar es Salaam, kabla hujaondoka ni lazima uiarifu nchi unokwenda, sasa zile transmitters zilikuwa zina nguvu na ya imma hazikumalizika au ziliharibiwa kwa makusudi.

Nikarudi huku (Nairobi), mimi nikaambiwa na mabosi, wewe mwenyewe uko tayari kwenda? Nikawaambia, niko tayari. Unaona. Na wakati ule tangu wapo tulikuwa tuna problem Kilimanjaro na rada system, nilikuwa nakwenda kuwasaidia jamaa kuwa train, engineers wetu local, wakaniambia umeshakuwapo hapa kwa muda mrefu unaweza kwenda.

Ndo yeye Nyerere, hao ndo watu wake bwana! Lakini hatukujuwa wakati ule. Sisi hatujui. Sisi tunaona tunasaidia tu. Nimeanza kujuwa nshafika Ngazija. Nimeshafika kule. Mimi nilikaa mwaka na miezi mitatu sio? Ndo nikajuwa kwa sababu kaanzisha, kaleta jeshi la kuwafundisha wananchi wa Komoro wenyewe. Alikuja mmoja akiitwa Major Idi, baadae Kanal na nini, kijana wa Arusha, ndo alokuwa mkubwa wa Jeshi la Tanzania, Komoro. Wakawa tayari wao kufanya biashara ya kuleta ngombe. Ngazija ilikuwa haina pesa. Ilijitangaza muflis kwa kufuata ushauri wa Umoja wa Mataifa (UN), au kitu kama hivo. Iliwabidi ili wapate misaada yaani. Na hiyo ilikuwa tamu kwa Nyerere. Mwanya! (Anacheka). Yeye analeta ngombe, analeta michele, kutoka Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje akawa anakuja pale, wa Ulinzi, wanakuja Komoro wakiondoka.

Ali Saleh alisaidiwa na Nyerere kuja madarakani. Ile ilikuwa wakati wa biashara, sasa Ali Saleh yeye ana matatizo yake za kiserikali na Wafaransa na nini. Sasa hawajamuwacha sasa. Wamemsakama kwa sababu wameshaona kaingia Tanzania pale. Akitaka mashine, vitabu, kila kitu kwa Kifaransa. Kama sisi tulosoma kwa Kiingereza tulikua hatuwezi kusoma, tulikuwa hatuwezi kufanya kitu. Hatukuweza kusaidia. Wale watu wa biashara wakawa wao wameambiwa ziko cooperatives [vyama va ushirika] hapa. Sasa serikali ilipokuja ya Tanzania pale kutaka kufanya biashara, Ali Saleh kawaambia, sisi serikali, hatuhusiki na mambo ya biashara. Ziko cooperatives, nyinyi fanyeni mikataba yenu na wao. Sasa Tanzania wakawaalika wale Dar es Salaam, wakawachukuwa mabara, wakasain mkataba.

Ikawa kila meli inokuja inaleta ngombe, inaleta michele, inaleta nini. Sasa muda ukapita, miezi mitatu, sita, wale wanangojea pesa, huku bara. Pesa hazendi. Hawa jamaa washakula na hawalipi. Sasa ikalazim aje Waziri kutoka Dar es Salaam, akaja Waziri wa kwanza, akazungumzaa, akarudi. Baada ya muda akaja Malecela nafikiri, na babake Ahmed Rajab, Mzee “Makopo”. Basi yeye aliletwa, angalau Mngazija, atafahamiana. Akapata tabu yule Waziri peke yake kuonana na Raisi. Kila akitaka amuone anaambiwa azungumze na Waziri wa Mambo ya Nje, azungumze na nani, na nini, mzee kashughulika sana, hawezi. Na yeye hawezi kurudi sasa. Anataka lazim apate jawabu kwenda kumwambia Mzee Nyerere.

Sasa ule mpango wa biashara ndo Wangazija walopiga kelele kwa sababu wao Wangazija wanasema ikiwa umetupa sisi chakula, kama hiyo michele, unga, tumeshasain sisi tutakuwa tunawalipa. Lakini wao wanasisitiza kuwa sisi tuwalipe kwa karafuu, na nazi, cacao, langilangi, mali asili ya nchi. Wao wamezitaka hizo. Uwe mpango wa kubadilishana vitu kwa vitu na si vitu kwa pesa. Sasa hapo ndo ikawa ni mushkila. Wale Wangazija wakasema aaaa, hii haiwezekani. Mpango huo hakuna bwana. Vipi nyie mtatupa mavi sisi tukupeni dhahabu bwana! Anasema, wakawa wananishambulia mie sasa. Manake mimi ndo Mtanzania pale. Wananambia wewe ni mmoja katika hao. Wewe umeletwa hapa lakini sisi tunakwambia, kwanza sisi hatulewi, sisi Waislamu, vipi mnaleta nyinyi meli mmejaza ma whisky, manini, kutoka Tanzania. (Anacheka). Hatujaagizia sisi! Mnaleta sigireti, mmeleta masigara, hatuna watu wengi wa kuvuta sigara hapa. Wanovuta watu kidogo. Sasa hizi cooperatives haziwezi kuuza, zimejaa huko maghalani. Sasa wale jamaa walikuja kutoka Dar ikawa wamevunjika moyo sana. Wakafanyiwa mpango wakamuona Raisi, Ali Saleh, na Ali Saleh akawaambia, tizama skilizeni, e bwana, sisi kiserikali hatuwezi kuwaingilia hawa cooperatives kwa sababu hawa ni huru na nyie mmezungumza nao hawahawa, wamekuja Dar es Salaam, mmetia saini zenu, sisi hatumo! Lakini tunaweza kukusaidieni ili wakulipeni kidogokidogo, na hizi biashara ambazo wamelalamika kuwa wao hawataki, mchukuwe wenyewe mali yenu. Masigireti, ma whisky. (Anacheka).

Lakini sasa wao walikuwa wanaiuzia serikali vitu va jeshi. Wakileta matandiko, magodoro na vitanda va vyuma, vinaletwa kwa meli kutoka Dar es Salaam, bunduki, umeona? Jeshi ndo wao kina Major Idi. Major Idi ndo in charge [dhamana]. Anaagizia lakini yote ile inatozwa serkali ya Komoro. Nafikiri mimi Komoro ilitia wasiwasi, hii itatufunga sisi kibiashara. Wanatutia kamba hapa kibiashara, baade tutaingizwa kwenye siasa zao za Tanzania, ambazo hatuzitaki. Waligutuka! Nakwambia wasiwasi walokuwa nao pale, ni kuwa hiyo wanaona hii, sisi tumemtowa Mfaransa, sasa hawa Waafrika wanatufunga sisi kibiashara. Wanatufunga kibiashara na vilevile, jeshi wameshalichukuwa wao, sasa la pili litakuwa bendera tuambiwe basi. Na yeye Mzee Nyerere akiwasabilia Komoro na Seycheles kuwasaidia kwa hali na mali. Malecela tulimuonea huruma. Sisi tulokuwa Watanzania, manake hajafaulu. Wale cooperatives walikuwa wagumu na serkali ilikataa kuingilia kati. Ikawa ni makosa ya wao serkali ya Tanzania kwanini wao hawajawaachia watu wa biashara. Ingekuwa wamewaachia watu wa biashara wa Tanzania pale isingekuwa tatizo. Baina ya watu wenyewe kwa wenyewe bila ya mkono. Wao wamefanya vengine.

Yeye [Ali Saleh] hata siku moja hajawahi kumzuru [Nyeyere] lakini mashirikiano yalikuwepo. Ali Saleh alikuwa msoshalisti na aliuliwa walipoingia mamluki wa Kifaransa. Wakati fulani alifanya jambo ambalo alijuta. Alikwenda kunako radio akajiuzulu. Akasema tangu leo mimi nakuwachieni wenyewe Wangazija wa Komoro mchaguwe mtu wa kuiendesha hii nchi, na Major Idi atakamata jeshi mpaka mtakapochaguwa. Watu wote wa serikali, anatangaza kunako radio, watu wote wa serikali, kila mmoja arejee kwao kwa mamake akanyonye! Na nnakusikitikieni wenye mama vizee ambao maziwa yao yameshakauka.

Kafika kumuachia nchi Major Idi na akamuamini! Lakini baada ya siku tatu, nne, tano, ikafanywa ghasia kama vile Egypt vile [wakati wa Gamal Abdel Nasser], “tunamtaka Raisi wetu arejee”. Akarudi, akachukuwa tena. Na ile Major Idi ilikuwa ni jina tu, jeshi atakuwa yeye huku, lakini vijana wake Ali Saleh ndo walokuwa wamelimiliki jeshi la nchi. Ikiitwa Komanda Muwasi. Vijana wetu hawa kina Ahmed Abdalla Mbamba, ambao wamesoma Unguja hao wote, na yeye mmoja alikuwa memba katika hiyo MOLINACO, mimi nnaye, tulikuwa pamoja Nairobi.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Salim Himidi, anatoka Zanzibar. Yuko Paris sasa. Amin Ali Mvuani alikuwa United Nations [Umoja wa Mataifa]. Wote hao wamemaliza pamoja Cambridge Unguja. Amin kasoma Kuwait baadae, baadae kenda Sorbonne na akenda special courses za foreign affairs [kozi maalumu za mambo ya nchi za nje] Ufaransa. Yuhai, yeye yuko United Nations mpaka leo. Sasa mfanyaji kazi Congo. United Nations Representative. Anakuja hapa.

Si tunakwenda kwenye mikutano yetu ya ITU hii ya Telecoms ya United Nations, tunakuwa na jamaa hapa, mimi nime represent Kenya, au nime represent Komoro, in Geneva, tunawakuta jamaa kutoka Zanzibar au kutoka Oman, from Zanzibar, ni members wetu. Tunawakuta jamaa wengine kutoka nchi nyengine, wote walewale.

Abdurahman Babu hakuwa na mahusiano ya karibu hali kwao pale Ngazija. Hata ule wakati wa Ali Saleh utafikiria yeye kama ni Msoshalisti atajaribu kuja Ngazija. Hakufanya hivo. Lakini jina la “Comrades” lilikuwa baya Comoro. Kwa sababu ya Karume kuwarejesha Wangazija wa Zanzibar [waliokuwa raia wa Mfaransa], akawatangazia wafanye tajnisi, na wengine wale ambao hawajafanya wakarejeshwa, ilimfanya kila Mzanzibari pale anokuja mpya anaitwa “Comrade.” “Wewe Komred wewe, mtu mbaya wewe.” Sidhani kama Babu angeweza ku survive. Propaganda ilikuwa mbaya dhidi ya Makomred. Imeiharibu ile alaka [na Zanzibar] kabisa, nzuri ilokuweko, baina ya miaka na makarne. Ile kusema tu Karume hawa Wangazija si wananchi wa hapa, basi ile ilikoroga mambo yote. Mpaka wengine mimi niliwaona Ngazija ambao sijajuwa mie kama wale walikuwa nayo asli au hawana. Mmoja nimemkuta kule, Ali Sugu. Alitoka Unguja, yeye ni Muunguja, bila shaka. Lakini nimemkuta katika watu walorejeshwa. Yeye Ali Sugu, na wale wazee wa kiserikali walokuwa maofisa wa polisi na nini, wale wote walichukuliwa kumlinda Raisi wa Ngazija kule. Aliwafanya ndo aide-de-camp [msaidizi wa Rais], kama huyu Ahmed Darwesh, ambaye alikuweko Zanzibar lakini alikuwa yeye ni Inspekta wa Polisi Dar es Salaam. Bwana Aboud Said alikuwa Inspekta Aboud Said Zanzibar, katika watu waloondolewa. Bwana Hassan Muhammed Mshangama, Inspekta Hassan Mshangama. Kama Hassan Mshangama alikuwa ndo mkubwa wa uhamiaji pamoja na Darwesh, na wakati huohuo ni aide-de-camp wa Raisi, wanamtizama Raisi. Wakati huo alikuwa President 1970 ile, Said Muhammed bin Sheikh. Ndo alokuwa President. Sasa yeye alivofanya Said Mohammed bin Sheikh, yeye alihudhuria uhuru wa Zanzibar, ile Disemba 10, 1963. Kanambia mwenyewe kuwa mimi na Naibu wangu Prince Said Ibrahim, sote tulialikwa, tulikwenda tulikuweko Mnazi Moja.

Sasa kuna uzuri, jambo moja ambalo Wazanzibari Mwenye Enzi Mungu awabarik, wana umoja. Kuwa hata wakiwa wana ugomvi wao wa ndani kwa ndani Zanzibar lakini wakikutana nje yale yote yanasahauliwa. Utaona wanakuwa pamoja na nini. Sasa yale mambo yalivotokea Zanzibar, kama Wazanzibari wengine wakarejeshwa Komoro, serikali ya Komoro ikawapokea lakini hata na wananchi wa Komoro wao wenyewe wanazo alaka zile za miaka, wakawachukuwa watu, wakawapa viwanja, na serkali vilevile ya Komoro ikawa inawa interview [hoji]. Watu wanakuwa wanahojiwa na kamati. Walifanya kamati ya kuwapokea na kuwauliza vitu gani wanataka. Ikiwa wewe unataka kulima, mkulima, basi serikali ilikuwa imetenga ardhi kwa alotoka Zanzibar. Kama eka sijui ngapi wakipewa. Mmoja ni yeye Ali Sugu na jamaa wengine. Wamepewa ardhi. Walokuwa wamesoma, kapenta kama wajomba zetu na nini, au engineers, wakachukuliwa na Public Works Department au Vava Publik wenyewe wanaita, au hiyo polisi.

Lakini Nairobi, kulikuwa na watu, vijana ambao wamejitolea na wao. Watu wanokimbia, kwa sababu ilikuwa wasiwasi ukikimbia wewe kutoka Zanzibar, unakimbilia Dar es Salaam pale halafu ukipata njia unaingia Mombasa. Sasa mpaka Mombasa watu hawana salama. Kuna watu wengine, muhimu wale, wakawa wanakimbia wanakuja zao Nairobi. Kama kaja nakumbuka Salum Hakim Khuseibi, yeye nafikiri alipokimbia akenda Dar es Salaam, kutoka Dar es Salaam akenda upande wa Kongo, kutokea Kongo ndo akarejea kwa Nairobi. Sasa yeye Salim akachukuliwa. Kuna mwengine Nassor Muhammed Miskiri, huyu alokuwa Cairo sasa yuko hapa alikuwa akifanya kazi Gulf Air. Ahmed Nassor Riyami, huyu wa hapa wa msikiti hapa. Mara nyingine tukipigiwa simu mtu yuko Dar es Salaam bado, bwana mimi nakuja kwa basi fulani, nipokee bwana kwa hisani yako, mimi sina pakwenda bwana. Wengine walikuwa wapita njia, akina Daudi Muhammed huyu, anaitwa Babuchi. Anapita yeye tunakwenda kumpokea halafu siku ya pili yake au ya tatu anapanda ndege anakwenda zake Uingereza. Anakuwa keshafanya mipango yake. Yeye transit. Wengine wanakaa mpaka mezi sita. Wengine wanatafuta kazi tena palepale. Lakini ile mimi nasema kuwa bado ule utu wetu ule wa Kizanzibari Mwenye Enzi Mungu auendeleze, watu hawajatupana yaani. Na ndo nimeuona Ngazija, nimeuona huku Nairobi, Mombasa, wengine wakati tuko Uganda. Wanakuja Uganda jamaa, jee unakwenda wapi? Bwana mimi nataka kwenda Ulaya bwana. Sasa mbona umekuja Uganda? Ndo nnafanya kazi hapa kiasi mwaka mmoja miwili nkipata pesa ntakata tikti ntafika Sudani halafu Cairo, ntakwenda mpaka ntafika. Njia sku hizo ilikuwa tabu. Mimi mwenyewe nimewahi kupokea watu nkakaa nao miaka miwili Kampala. Wametafuta kazi, wafanye pesa, wakate tikiti, wende zao mbele. Wengine wamekwenda Europe, wengine wametafuta ma scholarship kwenda kusoma.

Bwana Amani Thani Fairoz alikuwa Katibu Mkuu wa pili wa Chama cha Zanzibar Nationalist Party baada ya Abdulrahman Mohammed Babu.

 

Bwana Amani Thani Fairoz

Oscar Kambona namna alivonihadithia mwenyewe mambo ya mapinduzi ya Zanzibar kwamba hili jambo walikuwa nalo baina ya, khasa, yeye Kambona, Nyerere na Kawawa kwa muda mrefu sana. Waliona wao kwamba kwa mwendo huu wa uchaguzi Afro-Shirazi haitoweza kushinda. Na ikiwa haitoweza kushinda wao hawatoweza kuwa na mamlaka yoyote juu ya Zanzibar. Kwa hivyo wao waliweka mipango hii zamani wafanye lazima waipinduwe serikali yoyote itayakuwa sio ya Afro-Shirazi. Haya ni maneno ya Kambona mwenyewe.

Sasa siku ile ya mapinduzi, yalipotokeya yale, ikawa mawaziri wanakwenda mbio kutaka msaada khasa kwa Balozi wa Kiingereza alokuwepo Zanzibar, anaitwa Crosswaith. Walikwenda kutaka msaada kwake. Sasa ilipofika habari kuwa msaada huu uko Kenya, askari wa Kiingereza wako Kenya, hapana shaka huyu Crosswaith alipeleka habari kwamba hawa mawaziri wanataka msaada kutoka Kenya.

Kwa hivo Nyerere alimtoa Kambona kwenda kuonana na Jomo Kenyatta ili kuzuwia lisije jeshi lolote la kutoka kule. Jeshi haliwezi kuondoka mpaka kwa rukhsa ya nchi ile. Kwa hivo Kambona alikwenda kule lakini Jomo Kenyatta alikuwa hayuko mjini akaonana na Odinga. Akamwambia kama kuna mpango wa kutakiwa jeshi la Kiingereza lende likazuwie mapinduzi, na haya mapinduzi ni Waafrika walofanya kwa hivo likipelekwa jeshi hili basi itakuwa linakwenda kuwauwa ndugu zao. Na nyie mna nguvu la kulizuwia kwa hiyo tunaomba, Mwalimu Nyerere anaomba kwamba msifanye kitendo hicho. Hayo maneno ya mwenyewe Kambona. Wakawa wamefunga njia kulizuwia jeshi la Kiingereza lisende Zanzibar. Kwa hakika jeshi lilikuwa limeshakuwepo uwanja wa ndege. Liko tayari kuondoka. Kambona kwa nafsi yake ndo alopelekwa na Nyerere. Kanambia mwenyewe hayo.

Pia alisema Kambona, kuwa, wacha mambo ya kupinduwa, tangu ilipokuwa mambo ya uchaguzi, anasema ilikuwepo kamati maalumu ya kupeleka watu Zanzibar, toka wakti wa uchaguzi mpaka katika masala ya mapinduzi. Kanielezea kuwa walipeleka watu wengi kutoka bara, kutoka Tanganyika. Aliniambia watu wametoka kwetu. Alitumia neno hilo. Alisema madam Zanzibar Serikali atakuwa yuko Mfalme ndani yake wanaona kwao wao hautokuwa mlingano mzuri baina ya jirani kwa jirani. Mimi nikamwambia kwamba, hilo tu au kuna suala la dini limo ndani yake? Hiyo khabari ya ufalme tu au na dini ilikuwa ndani yake Nyerere anayo? Akanambia Kambona kuwa Nyerere alisema tujaribu kama tutakavoweza kupunguza nguvu za Uislamu katika Zanzibar. Na ikiwa hatutokuwa na serikali Zanzibar hatutomudu kulifanya hilo. Yeye akanijibu, na dini ipo ndani yake. Hilo ndo jibu lake yeye. Hilo pia kanizungumzia. Katika hizo plan zao.

Kambona alinihadithia mengi. Alisema, Mwalimu unavomuona vile sivo alivo. Nikamuuliza nini khasa ugomvi wenu, wewe Kambona na Nyerere? Anavosema yeye tangu yalipotokea majaribio ya mapinduzi tarehe 20 Januari 1964. Wale majeshi wakamuendea yeye Kambona na kumtaka achukuwe nafasi ya Nyerere. Anasema mimi nilikataa na mimi ndo niliowabembeleza hao majeshi. Tangu pale alimuona Mwalimu kama ana wasiwasi na mimi. Na ilipotokea Hanga kutofahamiana na Karume na yeye Kambona anafahamiana na Hanga kwa mengi na wako pamoja kila mara ikawa Nyerere kaweka askari wa siri kuwatizama mwendo wao, nini wanafanya, nani wanaonana nao, wanakwenda wapi. Nyerere kafanya hayo. Akasema kwa bahati nzuri wale watu aliowaekea Nyerere walikuwemo ndani yake watu ambao walikuwa wasikilizana sana na Kambona. Wakamwambia tahadhar bwana, Mwalimu ana wasiwasi sana juu yako hasa kuhusu wewe na huyu rafiki yako Hanga kwa hiyo tumepewa kazi kulitizama kila jambo lako unalolifanya.

Na hilo ndilo lilomfanya Kambona awe na wasiwasi kwa vile anavomjuwa yeye Nyerere akishaanza mambo kama hayo mara hutumia njia zake za kumpoteza mtu. Amesema Nyerere kawapoteza watu wengi usione hivi. Na ndo sababu ya Kambona kuondoka katika nchi.

Tulipoonana naye sisi Kambona alikuwa kabadilika hali. Yeye alikuwa anasema kwamba Muungano umefanywa kwa njia si za barabara. Yeye akiwafika kuwepo Muungano. Si kwa sababu ya Zanzibar na Tanganyika tu, lakini yeye fikra zake Muungano uwepo Afrika Mashariki lakini kwa njia za matengenezo si za kwa njia hizo zilizokwenda ambazo Nyerere katumia kama kumzidi nguvu tu Karume. Lakini haukuwa mwendo barabara. Muungano haukufanywa kwa mujibu wa maadili ya kuungana. Kwa hivo yeye anasema kwamba hata ikiwa tutaigombowa Zanzibar itakuwa uzuri sana ikiwa tutakuwa sote pamoja na ndio maana akataka kushirikiana na sisi katika kuigomboa Tanzania.

Kitwana Kondo alikuwa katika watu ambao walikuwa karibu sana na Kambona. Saidi Tewa pia alikuwa yuko karibu naye sana. Kama Fundikira ameshafariki. Alikuwa akiwasiliana naye. Aliwahi kuwa karibu na Chipaka lakini naona kama waliwachana baadae. Khasa alikuwa amekamatana sana na Kitwana Kondo. Kondo alikuwa trade unionist huyu. Very powerful wakati wake. Na huyu [Kitwana Kondo] alikamatana naye mpaka kufa Kambona.

Kambona alikuwa na imani na alikuwa akitaassaf [akiona vibaya] sana juu yetu kwa mambo yaliopitikana kwetu Zanzibar. Alipokwenda kuonana na Sheikh Ali Muhsin Cairo alisema nilikuwa naona tabu kumkabil mtu kama yule kwa ubaya tuliokuwa tumeufanya sisi. Alikuwa na Bwana Ahmed Seif Kharusi [London] kabla ya Sheikh Ali kutoka jela. Alipotoka akamwambia Bwana Ahmed kwamba sasa midam mzee katoka nataka kwenda kuonana naye kwa hiyo nitengezee nikaonane naye. Bwana Ahmed akazungumza na Sheikh Ali na Sheikh Ali akasema yeye tayari na wakti wowote aje. Kambona akafanya safari kutoka Uingereza kwenda Cairo.

Yeye Kambona alinihadithia kwa urefu mambo ya Hanga tangu kuondoka, kukamatwa, mpaka alipokwenda Guinea akaonana na Rais Ahmed Sekou Toure, akenda kwake Uingereza akaonana naye, yeye akamshauri Hanga asirejee Tanzania. Akamwambia huu si wakati wa kurejea Tanzania. Wewe humjui Mwalimu kama ninavomjuwa mie. Mimi namjua zaidi. Hatojali ahadi yoyote atakapotaka kulifanya jambo lake. Usende sasa. Lakini Waswahili wanasema shikio la kufa halisikii dawa.

Leave a comment